16-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Kuweka Nadhiri Kwa Asiyekuwa Allaah

 

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!

 

16- Kuweka Nadhiri Kwa Asiyekuwa Allaah

 

Alhidaaya.com

 

 

Kuweka nadhiri ni mtu kuilazimisha nafsi yake kwa kitu ambacho hajalazimishwa na Shariy’ah.  Amesema Al-Isfhaan (Rahimahu Allaah) katika Mufradaat Alfaadhw Al-Qur-aan (uk. 797): “Nadhiri ni unapojishurutisha kutenda jambo lisilokuwa wajibu kwa sababu ya kutaka jambo fulani likutokee. Anasema Allaah:

 

إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَـٰنِ صَوْمًا 

Hakika mimi nimeweka nadhiri ya swawm kwa Ar-Rahmaan [Maryam: 26]

 

Baadhi ya ‘Ulamaa wameharamisha kwa dalili ya Hadiyth ifuatayo:

 

عن النبيَّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّمَ ؛ أنه نهى عن النذر  وقال:  إنه لا يأتي بخير. وإنما يستخرج من البخيل

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza nadhiri akasema: ((Haileti khayr bali inatolewa kutoka kwa bakhili)) [Muslim (1639)]

 

Na katika riwaayah nyingine:

 

  نَهَى النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنْ النَّذْرِ وَقَالَ:  إِنَّهُ لَا يَرُدُّ شَيْئًا وَلَكِنَّهُ يُسْتَخْرَجُ بِهِ مِنْ الْبَخِيلِ

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza nadhiri akasema: ((Hakika hairudishi chochote, bali inatolewa kutoka kwa bakhili)) [Al-Bukhaariy (6693)]   

 

Na Hadiyth ya Mama wa Waumini ‘Aaishah  (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba  amesema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 من نذر أن يُطِيعَ اللهَ فلْيُطِعْهُ ، ومن نذرَ أن يعصِيَه فلا يَعْصِه

((Aliyeweka nadhiri kumtii Allaah amtii, na aliyeweka nadhiri kumuasi Allaah, basi asimuasi))[Al-Bukhaariy (6696)]

 

 

Kutokana na Hadiyth hii, inadhihirisha kukubaliwa kwake nadhiri pindi mtu akiazimia, kwa dalili pia za Qur-aan:

وَمَا أَنفَقْتُم مِّن نَّفَقَةٍ أَوْ نَذَرْتُم مِّن نَّذْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُهُ

Na chochote mtoacho au mkiwekacho nadhiri, basi Allaah Anakijua. [Al-Baqarah: 270]

 

Na pia kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 يُوفُونَ بِالنَّذْرِ وَيَخَافُونَ يَوْمًا كَانَ شَرُّهُ مُسْتَطِيرًا﴿٧﴾

Wanatimiza nadhiri na wanaiogopa siku ambayo shari yake ni yenye kuenea kwa upana. [Al-Insaan: 7]

 

Na pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُمْ وَلْيُوفُوا نُذُورَهُمْ

Kisha wamalize ‘ibaadah zao; wajisafishe taka zao na watimize nadhiri zao, [Al-Hajj: 29]  

 

 

Na kwa vile nadhiri ni aina ya ‘Ibaadah, haifai kuielekeza kwa asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) mfano kuifanya kwa ajili ya Nabiy, au Walii, au Shaykh, au kaburi na kadhaalika. Kufanya hivyo ni shirki kubwa inayomtoa mtu nje ya Uislamu.

 

Fataawa za ‘Ulaama kuhusu kuweka nadhiri kwa asiyekuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

 

Shaykh Fawzaan (Hafidhwahu Allaah)

 

Swali: 

 

Je, ikiwa mtu ameweka nadhiri mfano akasema: “Allaah Akinipa shifaa kwa magonjwa yangu, nitachinja kwa ajili ya Allaah katika kaburi la fulani ili kujikurubisha kwa Allaah. Je, inajuzu mfano wa ‘amali kama hii? Na je, kuna sehemu zilizoharamishwa kuchinja?

 

Jibu: 

 

Ikiwa ameweka nadhiri kuchinja kwa ajili ya Allaah katika kaburi, basi nadhiri hii ni ya maasi, haijuzu kuitimiza. Na kuchinja katika kaburi ikiwa imekusudiwa kujikurubisha kwa mwenye kaburi, hiyo ni shirki kubwa inayomtoa mtu katika Dini hata kama ataja Jina la Allaah wakati anachinja.

 

Na ikiwa kujikurubisha kwa Allaah basi hayo ni maasi makubwa na wasiylah (njia ya kujikurubisha) za shirki kwa sababu haijuzu kuswali kaburini wala kuomba wala kuchinja kaburini hata kama tunakusudia Allaah kwani hivyo ni kujifananisha na washirikina na wasiyla za shirki. 

 

Abuu Daawuwd amepokea kutoka kwa Thaabit bin Adhw-Dhwahaak (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba mtu mmoja aliweka nadhiri kuchinja ngamia katika Buwaanah. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza: ((Je, kuliweko masanamu ya kijaahiliyyah (kabla Uislamu) yakiabudiwa?”

Wakasema: “Hapana” Akasema: ((Je, kuliweko sherehe za kijaahiliyyah zikifanywa hapo?)) Wakasema: “Hapana” Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Timiza nadhiri yako, kwani hakuna kutimiza nadhiri katika kumuasi Allaah, wala katika ambayo hayamiliki bin Aadam)). [Abuu Daawuwd na ameisahihisha Al-Albaaniy]

 

 

 

Imaam bin Baaz (Rahimahu Allaah)

 

Swali:

 

Imenitokea mushkila nikaweka nadhiri kwa ajili ya mmojawapo wa ma-Imaam, kisha nikaja kutambua kuwa haifai kuweka nadhiri kwa asiyekuwa Allaah. Tambua kuwa sehemu aliyoko huyo Imaam iko mbali, je, inajuzu nilipize nadhiri hii kwa mafakiri au niifanyie kafara?

 

Jibu: 

 

Nadhiri hiyo ni baatwil, kwa sababu ni ‘ibaadah kwa asiyekuwa Allaah.  Inakupasa utubie kwa Allaah kwayo na urudi Kwake kwa kutubia na kuomba maghfirah na kujuta kwani nadhiri ni ‘ibaadah, Anasema Allaah Ta’aalaa:  

 

وَمَا أَنفَقْتُم مِّن نَّفَقَةٍ أَوْ نَذَرْتُم مِّن نَّذْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُهُ

Na chochote mtoacho au mkiwekacho nadhiri, basi Allaah Anakijua. [Al-Baqarah: 270]

 

Yaani: Atakulipeni kwayo. Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

من نذر أن يُطِيعَ اللهَ فلْيُطِعْهُ، ومن نذرَ أن يعصِيَه فلا يَعْصِه

((Aliyeweka nadhiri kumtii Allaah amtii, na aliyeweka nadhiri kumuasi Allaah, basi asimuasi))  

 

Kwa hiyo nadhiri hiyo ni baatwil, na ni kumshirikisha Allaah (‘Azza wa Jalla) kama vile nadhiri kwa ajili ya ma-Imaam na waliokufa ni nadhiri baatwil na ni kumshirkisha Allaah, basi nadhiri haijuzu isipokuwa kwa ajili ya Allaah Pekee, kwa sababu ni ‘ibaadah kama vile Swalaah, na kuchinja na nadhiri, na kufunga Swiyaam na du’aa zote ni kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kama Anavyosema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ ﴿٥﴾

Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada. [Al-Faatihah: 5]

 

 

Na Anasema (Subhaanahu):

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

Na Rabb wako Amehukumu kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee [Al-Israa: 23]

 

 

Na Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَادْعُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ﴿١٤﴾

Basi mwombeni Allaah wenye kumtakasia Dini japokuwa wanachukia makafiri. [Ghaafir: 14]

 

 

 

Na Anasema (‘Azza wa Jalla):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا﴿١٨﴾

Na kwamba Misikiti ni kwa ajili ya Allaah, basi msiombe yeyote pamoja na Allaah. [Al-Jinn: 18]

 

 

Basi ‘ibaadah ni haki ya Allaah, na nadhiri ni ‘ibaadah, na Swawmi ni ‘ibaadah, na Swalaah ni ‘ibaadah, na du’aa ni ‘ibaadah basi inawajibika kuisafisha kwa ajili ya Allaah Pekee. Kwa hiyo nadhiri hiyo ni baatwil, na haikupasi kufanya chochote, si kwa mafukara wala wengineo, bali inakupasa utubie tu na huna haja ya kuilipizia nadhiri hiyo kwa vile ni baatwil na ni shirki, ila tu utubie tawbah ya kikweli na kufanya matendo mema, Allaah Akuwafikie na Akuongoze katika yanayomridhisha na Akujalie ufanye tawbah ya kikweli.

 

 

 

 

Share