Kusema Assalam Alaykum Kwa Mkristo Inajuzu?

 

SWALI:

Asalam alikum, mie nina suali

niliwahi kutolewa asala alaikum na mkristo mmoja na mie nikamuitikia walaikum salam, jee inakubaliwa kumuitikia  salam yake? inshallah nategemea  mtanipa jibu halisi.shukran

 

 







JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukran kwa swali hili zuri.

Kwa hakika Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametukataza mwanzo kuanza kuwasalimia makafiri pale aliposema: “Musianze kuwasalimia Mayahudi na Manasara” (Muslim, Abu Dawud na at-Tirmidhy kutoka kwa Abu Hurayrah [(Radhiya Allaahu 'anhu)]).

 Na ni katika mwenendo wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam.) kuwa alipokuwa anasalimia na asiyekuwa Muislamu basi akimjibu wa ‘Alaykum. Anahadithia Anas (Radhiya Allaahu 'anhu) kuwa Mtume wa Allah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam.) amesema: “Anapowasalimia mtu miongoni mwa Ahlul Kitaab, jibuni wa ‘alaykum (al-Bukhari, Muslim, Abu Dawud na Ibn Maajah).

Na yeye mwenyewe anatuonyesha mfano pale walipomjia Mayahudi nyumbani kwake na wakamsalimia kwa kumwambia as-Saam ‘alaykum (yaani mauti yawe juu yako) akawajibu wa ‘alaykum. Bi ‘Aishah (Radhiya Allaahu 'anha) aliyesikia salamu hizo alikasirika sana na kuhamaki kwa kuwaambia as-Saam ‘alaykum wal la‘na (mauti yawe juu yenu na laana). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam.) akamwambia ‘Aishah (Radhiya Allaahu 'anhu) mimi nishawajibu na haina haja ya yote hayo kwani hukunisikia nikisema as-Saam ‘alaykum (na juu yenu) {al-Bukhari na Muslim).

Hii ni hivyo kwani wasiokuwa Waislamu huwa hawawapendelei mema Waislamu na huenda wakawa wanatoa maneno yanayokaribiana nay a salamu lakini yenye maana nyengine kama Mayahudi wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo, inavyotakiwa ni kuwajibu as-Saam ‘alaykum  (siyo as-salaam) na juu yenu yale munayotutakia sisi.

Na Allah Anajua zaidi.

 

 

 

 

Share