Shaykh Fawzaan: Kuweka Nadhiri Kuchinja Kwa Ajili Ya Allaah Lakini Kuchinja Makaburini

 

 Hukmu Ya Kuweka Nadhiri Kuchinja Kwa Ajili Ya Allaah Lakini Kuchinja Makaburini

 

Shaykh Swaalih bin Fawzaan Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

SWALI:

 

Je, ikiwa mtu ameweka nadhiri mfano akasema: “Allaah Akinipa shifaa kwa magonjwa yangu, nitachinja kwa ajili ya Allaah katika kaburi la fulani ili kujikurubisha kwa Allaah. Je, inajuzu mfano wa ‘amali kama hii? Na je, kuna sehemu zilizoharamishwa kuchinja?

 

JIBU:

 

 

Ikiwa ameweka nadhiri kuchinja kwa ajili ya Allaah katika kaburi, basi nadhiri hii ni ya maasi, haijuzu kuitimiza. Na kuchinja katika kaburi ikiwa imekusudiwa kujikurubisha kwa mwenye kaburi, hiyo ni shirki kubwa inayomtoa mtu katika Dini hata kama ataja Jina la Allaah wakati anachinja.

 

Na ikiwa kujikurubisha kwa Allaah basi hayo ni maasi makubwa na wasiylah (njia ya kujikurubisha) za shirki kwa sababu haijuzu kuswali kaburini wala kuomba wala kuchinja kaburini hata kama tunakusudia Allaah kwani hivyo ni kujifananisha na washirikina na wasiyla za shirki. 

Abuu Daawuwd amepokea kutoka kwa Thaabit bin Adhw-Dhwahaak (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba mtu mmoja aliweka nadhiri kuchinja ngamia katika Buwaanah. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza: ((Je, kuliweko masanamu ya kijaahiliyyah (kabla Uislamu) yakiabudiwa?”

Wakasema: “Hapana” Akasema: ((Je, kuliweko sherehe za kijaahiliyyah zikifanywa hapo?)) Wakasema: “Hapana” Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Timiza nadhiri yako, kwani hakuna kutimiza nadhiri katika kumuasi Allaah, wala katika ambayo hayamiliki bin Aadam)). [Abuu Daawuwd na ameisahihisha Al-Albaaniy]

 

 

[Mawqi' Ar-Rasmiy li-Ma'aaliy  Shaykh Swaalih Al-Fawzaan]

 

 

 

 

 

Share