Anaweza Kutumia Pesa Za Watoto Akizihitaji?

SWALI:

ASALAM ALYKUM, SAMAHANI MIMI NAULIZA NNA WATOTO WANGU NA IMEFIKA  SIKUKUU  AU SIKU ZA KAWAIDA NA NIKAENDA KUSALIMIA PAHALI PAMOJA NA WATOTO WANGU NA MTU AKATOA PESA KUMPA YULE MTOTO AU WATOTO NA BAADAE MIMI NIKAZICHUKUA KWA   MAHITAJI YANGU  NIKAZITUMIA INAFAA KUTUMIA ILE PESA HAINA MATATIZO  NAOMBA  JIBU ILI NIWE KATIKA WACHA MUNGU ZAID INSAALLAH

 

 


JIBU:

BismiLLaah wa AlhamduliLLaah was-Swalaatu wa Salaamu ‘alaa Muhammad wa ‘alaa  aalihi wa Aswhaabihil Kiraam, wa Ba’ad:

Inafaa kutumia pesa za mtoto wako pindi kukiweko haja ya kufanya hivyo, na hii ni kutokana na dalili ya usimulizi wa Hadiyth ifuatayo:

عن عبد الله   بن عمرو رضي الله عنه أَنَّ رَجُلا قَالَ : يَا رَسُولَ اللَّهِ ، إِنَّ لِي مَالا وَوَلَدًا وَإِنَّ أَبِي يُرِيدُ أَنْ يَجْتَاحَ مَالِي ، فَقَالَ : (( أَنْتَ وَمَالُكَ لأَبِيكَ ))  . والحديث صححه الألباني في صحيح ابن ماجه

Imetoka kwa 'Abdullahi ibn 'Amr رضي الله عنه kwamba mtu mmoja alisema: "Ewe Mjumbe wa Allaah, mimi nina mali na mtoto, na  baba yangu anataka kuchukua mali yangu yote: Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema: ((Wewe na mali yako ni vya baba yako)) [Ibn Maajah katika sahiyh yake,  na ameipa daraja ya sahiyh Sheykh Al-Al-Baaaniy]

Lakini kuchukua huko pesa za mtoto kumewekewa sharti zifuatazo na wataalamu. Ibn Qudaamah رضي الله عنه amesema: Baba anaweza kuchukua mali yoyote anayotaka ya mwanae na ikawa ni yake, ikiwa baba anaihitaji au haihitaji, ikiwa mtoto ni mdogo au mkubwa lakini kwa sharti mbili:

1.  Kwamba hamuonei mtoto au kumdhuru na hachukui chochote katika kile anachokihitaji mtoto wake.

2.  Kwamba hachukui mali ya mtoto wake na kumpa mtoto mwingine. Hii imetajwa na Imaam Ahmad, kwa sababu hairuhusiwi kupendelea mtoto mmoja kwa kumpa hata mali yake mwenyewe, kwa hiyo bila shaka kuchukua mali ya mtoto mwingine na kumpa mtoto mwingine ina makatazo zaidi ya hayo.  

Abu Haniyfah, Maalik and Shaafi'iy wamesema: Haimpasi kuchukua  katika mali ya mwanawe isipokuwa kiasi cha mahitaji yake kwa sababu Mtume صلى الله عليه وآله وسلم amesema :

(( إن دماءكم وأموالكم عليكم حرام , كحرمة يومكم هذا , في شهركم هذا))   متفق عليه    

 ((Damu zenu na mali zenu ni tukufu  juu yenu, kama ilivyo tukufu siku hii yenu na mwezi huu wenu)) [Al Bukhaariy na Muslim]  

Kuna mapokezi ya hadiyth yanayotilia nguvu rai ya wengi wao kwamba kuna sharti ya baba kuchukua ikiwa anahitaji tu, nayo ni Hadiyth kutoka kwa Bibi 'Aishah رضي الله عنها :

 قال رسول الله صلى الله عليه وسلم : ( إن أولادكم هبة الله لكم  (( يهب لمن يشاء إناثاً ويهب لمن يشاء الذكور)) فهم وأموالهم لكم إذا احتجتم إليها))  والحديث صححه الشيخ الألباني في  السلسلة الصحيحة

Amesema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم: ((Watoto wenu ni zawadi kwenu kutoka kwa Allah, ((Anamtunukia Amtakaye watoto wa kike, na Anamtunukia Amtakaye watoto wa kiume [Ash-Shuuraa:49])) Wao na mali zao ni zenu mkizihitaji)) [Imesahihishwa na Sheykh Al-Albaaniy katika kitabu chake cha 'Silsilat Ahadiyth Swahiyha']  

Kwa hiyo baba akihitaji pesa, anaweza kuchukua pesa za mwanae, na kutumia kwa nafsi yake au kwa mahitaji ya wanaomtegemea, maadam hatamtia katika tabu mwanawe kuchukua mali hiyo, yaani hatomkalifisha, na asichukue chochote kutoka kwa mtoto wake kile anachokihitaji mwenyewe mtoto.

Na Allah Anajua zaidi.

 

 

Share