19-Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno! - Istighaathah Kwa Asiyekuwa Allaah

 

إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيم

 

Hakika Shirki Ni Dhulma Kubwa Mno!

 

19 - Istighaathah (Kuomba Uokozi) Kwa Asiyekuwa Allaah

Alhidaaya.com

 

 

 

 

 

Maana Ya Istighaathah na dalili zake:

 

Istighaathah maana yake ni kuomba uokozi kwa ambaye ataweza kuokoa kutokana na hali ya shida, dhiki na kukaribia kudhurika au kuangamia. Na istighaathah kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) inajumuisha kujidhalilisha Kwake na kuitakidi kwamba hakuna mwengine atakayeweza kuokoa isipokuwa Yeye, kama vile hali ilivyokuwa katika vita vya Badr, Ibn Kathiyr amesema:

 

 

"Ilipokuwa siku ya Badr na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaona uchache wa Maswahaba wake na wingi wa adui zake, wakawa katika shida na khofu, akaelekea Qiblah na kuomba uokovu na akaendelea kumuomba Mola wake mpaka joho lake likamuanguka begani mwake, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Akateremsha:

 

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ

Na pindi mlipomuomba uokovu Rabb wenu Naye Akakuitikieni  [Al-Anfaal: 9] [mpaka mwisho wa Aayah 13 Suwrat Al-Anfaal]

 

 

Kuomba uokovu kwa bin-Aadam kwa jambo ambalo limo katika uwezo wake inafaa kwa dalili kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuhusu kisa cha Nabiy Muwsaa (‘Alayhis-Salaam):

 

وَدَخَلَ الْمَدِينَةَ عَلَىٰ حِينِ غَفْلَةٍ مِّنْ أَهْلِهَا فَوَجَدَ فِيهَا رَجُلَيْنِ يَقْتَتِلَانِ هَـٰذَا مِن شِيعَتِهِ وَهَـٰذَا مِنْ عَدُوِّهِ ۖ فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ

Na akaingia mjini wakati watu wake wako katika mighafiliko, akakuta humo watu wawili wanapigana; mmoja ni miongoni mwa kundi lake, na mwengine miongoni mwa adui wake. Akamsaidia kumuokoa yule ambaye katika kundi lake dhidi ya yule ambaye ni katika adui wake… [Al-Qaswasw: 15]

 

Pia, mtu anaweza kuomba uokovu kwa mwenziwe amuokoe kutokana na adui zake katika hali ya vita n.k. Au mfano mtu anapokuwa katika hali ya kukaribia kuzama baharini akaita: “Ee ndugu! Nazama niokoe!”

 

Ama kuomba uokovu kwa jambo ambalo halimo katika uwezo wa bin-Aadam, hapo huwa ni shirki. Mfano mtu kumuomba mwenziwe:

 

“Ee fulani! Nisaidie kuniokoa na Moto wa Jahannam na niingize Jannah!”

 

“Ee Fulani! Nisaidie kuniokoa katika upotofu unijaalie hidaaya!”

 

Au kuomba walio kaburini:

 

“Ee walii wangu, au shekhe wangu!

 

Au sharifu fulani! Nisaidie kuniokoka na adhabu za kaburi! Nisaidie kuniokoa katika maradhi niliyo nayo!”

 

Kadhaalika, kuomba uokovu kwa mazimwi, mashaytwaan n.k. kuitakidi kuwa wao wana uwezo wa kuokoa katika hali ambazo hakuna mwenye uwezo isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). 

 

Vilevile kuomba uokovu kwa kumchanganya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihu wa sallam) kwa mfano: kusema  "Ee Allaah  niokoe mie katika hizi dhiki kwa baraka Zako na baraka za Rasuli Wako."

 

Hivyo ni shirki kubwa na inamtoa mtu nje ya Uislamu.

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwamba hao wanaoombwa uokovu n.k. hawawezi wenyewe kujinusuru nafsi zao humo walimo makaburini wala Siku ya Qiyaamah hawatokuwa na uwezo wowote ule!

يَوْمَ لَا يُغْنِي مَوْلًى عَن مَّوْلًى شَيْئًا وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ﴿٤١﴾

Siku ambayo jamaa wa karibu hatomfaa jamaa wa karibu chochote, na wala wao hawatonusuriwa. [Ad-Dukhaan: 41]

  

Hata Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa na uwezo wa kumuokoa mtu kwa dalili kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema katika Aayah kadhaa kwamba yule Ambaye Ameshamhukumu kuwa ni mpotofu, basi hakuna wa kumhidi:

 

مَن يَهْدِ اللَّـهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِ ۖ وَمَن يُضْلِلْ فَلَن تَجِدَ لَهُ وَلِيًّا مُّرْشِدًا ﴿١٧﴾

Ambaye Allaah Amemwongoza, basi yeye ndiye aliyehidika. Na Anayemwacha kupotoka basi hutompatia mlinzi wa kumuongoza. [Al-Kahf: 17]

 

Au ambaye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amemhukumu kuwa ni mtu wa Motoni, basi hakuna wa kumuokoka, Akamwambia Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

أَفَمَنْ حَقَّ عَلَيْهِ كَلِمَةُ الْعَذَابِ أَفَأَنتَ تُنقِذُ مَن فِي النَّارِ ﴿١٩﴾

Je, yule iliyemthibitikia neno la adhabu je, basi wewe utaweza kumuokoa aliyemo katika moto? [Az-Zumar: 19]

 

 

Alikuweko mnafiki mmoja akiwaudhi Waumini ikahadithiwa:

 

عن عُبَادَةَ بْنَ الصَّامِتِ (رضي الله عنه) قال: خَرَجَ عَلَيْنَا رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) فَقَالَ أَبُو بَكْرٍ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ): قُومُوا نَسْتَغِيثُ بِرَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) مِنْ هَذَا الْمُنَافِقِ. فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم)َ:  ((أنه لاَ يُسْتَغَاث بِي، وَإِنَّمَا يُسْتَغَاثُ باِلله))

Kutoka kwa ‘Ubaadah bin Asw-Swaamit (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitujia kisha Abu Bakr akasema: Simameni tutake msaada kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) atuokoe na mnafiki huyu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Hakika haipasi kuombwa uokovu kwangu, bali inapaswa kuombwa uokovu kwa Allaah)) [At-Twabaraaniy fiy Mu’jamil–Kabiyr]  

 

Pia Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amehadithia kwamba ilipoteremshwa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ ﴿٢١٤﴾

Na onya (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) jamaa zako wa karibu. [Ash-Shu’araa: 214]

 

 

دَعَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قُرَيْشًا فَاجْتَمَعُوا فَعَمَّ وَخَصَّ فَقَالَ: ((يَا بَنِي كَعْبِ بْنِ لُؤَيٍّ، أَنْقِذُوا أَنْفُسَكُمْ مِنْ النَّارِ، يَا بَنِي مُرَّةَ بنِ كَعْبٍ أَنْقِذُوا أَنْفُسَكُمْ مِنْ النَّارِ، يَا بَنِي عَبْدِ شَمْسٍ أَنْقِذُوا أَنْفُسَكُمْ مِنْ النَّارِ،يَا بَنِي عَبْدِ مَنَافٍ أَنْقِذُوا أَنْفُسَكُمْ مِنْ النَّارِ، يَا بَنِي هَاشِمٍ أَنْقِذُوا أَنْفُسَكُمْ مِنْ النَّارِ ، يَا بَنِي عَبْدِ الْمُطَّلِبِ أَنْقِذُوا أَنْفُسَكُمْ مِنْ النَّارِ، يَا فَاطِمَةُ أَنْقِذِي نَفْسَكِ مِنْ النَّارِ، فَإِنِّي لَا أَمْلِكُ لَكُمْ مِنْ اللَّهِ شَيْئًا غَيْرَ أَنَّ لَكُمْ رَحِمًا سَأَبُلُّهَا بِبَلَالِهَا))

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaita Maquraysh akawaonya kwa ujumla kisha makhsusi (kwa kabila fulani) akasema:  ((Ee Baniy Ka’ab bin Luayy, okoeni nafsi zenu kutokana na Moto!  Ee Baniy Murrah bin Ka’b, okoeni nafsi zenu kutokana na Moto! Ee Baniy ‘Abdi Shams, okoeni nafsi zenu kutokana na Moto. Ee Baniy ‘Abdi Manaaf, okoeni nafsi zenu kutokana na Moto.” Ee Baniy Haashim, okoeni nafsi zenu kutokana na Moto.” Ee Baniy ‘Abdil-Muttwalib, okoeni nafsi zenu kutokana na Moto.” Yaa Faatwimah, okoa nafsi yako kutokana na Moto! Kwani hakika mimi similiki uwezo wowote kwenu isipokuwa nitaendelea kuweka uhusiano wetu wa damu.)) [Muslim]

 

Anatahadharisha pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika kauli Zake mbali mbali:

 

وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ لَا يَسْتَطِيعُونَ نَصْرَكُمْ وَلَا أَنفُسَهُمْ يَنصُرُونَ﴿١٩٧﴾

Na wale mnaowaomba (na kuwaabudu) badala ya Allaah hawawezi kuwanusuru na wala hawawezi kujinusuru nafsi zao. [Al-A’raaf: 197]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 أَمْ لَهُمْ آلِهَةٌ تَمْنَعُهُم مِّن دُونِنَا ۚ لَا يَسْتَطِيعُونَ نَصْرَ أَنفُسِهِمْ وَلَا هُم مِّنَّا يُصْحَبُونَ ﴿٤٣﴾

Je, kwani wana waabudiwa wanaoweza kuwakinga Nasi?  Hawawezi kujinusuru nafsi zao na wala hawatolindwa Nasi. [Al-Anbiyaa: 43]

 

Na pia Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 وَاتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ آلِهَةً لَّعَلَّهُمْ يُنصَرُونَ ﴿٧٤﴾

Na wamejichukulia badala ya Allaah waabudiwa ili wakitumaini kuwa watawanusuru!

 

لَا يَسْتَطِيعُونَ نَصْرَهُمْ وَهُمْ لَهُمْ جُندٌ مُّحْضَرُونَ ﴿٧٥﴾

Hawawezi kuwanusuru, na watahudhurishwa (adhabuni) kama askari dhidi ya hao (waliowaabudu). [Yaasiyn: 74-75]

 

 

 

Share