10-Wewe Pekee Tunakuabudu: Wanaotakabaliwa Du’aa Zao

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada

 

10 - Wanaotakabaliwa Du’aa Zao

 

 

 

Baadhi ya waliotajwa kuwa du’aa zako zinatakabalilwa na dalili zake:

 

 

1-Du’aa Za Imaam Muadilifu, Mwenye Swawm Na Aliyedhulumiwa

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((ثَلاَثَةٌ لاَ تُرَدُّ دَعْوَتُهُمْ، الإِمَامُ الْعَادِلُ، وَالصَّائِمُ حَتَّى يُفْطِرَ، وَدَعْوَةُ الْمَظْلُومِ يَرْفَعُهَا اللَّهُ دُونَ الْغَمَامِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَتُفْتَحُ لَهَا أَبْوَابُ السَّمَاء،وَيَقُولُ بِعِزَّتِي لأَنْصُرَنَّكِ وَلَوْ بَعْدَ حِينٍ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (([Watu] Watatu hazirudishwi du'aa zao; Imaam muadilifu, mwenye Swawm mpaka afuturu, na du'aa ya aliyedhulumiwa, Anainyanyua Allaah bila ya mawingu Siku ya Qiyaamah na inafunguliwa milango ya mbingu na Anasema: Kwa Utukufu Wangu, Nitakunusuru japo baada ya muda.))[Swahiyh At-Tirmidhiy (2526) Ibn Maajah, Ahmad]

 

Kuhusu mwenye Swawm ni kwamba ana fursa pana mno ya kuomba du'aa nyingi wakati wote tokea anapoanza kufunga Swawm asubuhi hadi Magharibi anapofuturu.  

 

Na kuhusu aliyedhulumiwa naye amepewa fadhila ya kukubaliwa du'aa zake dhidi ya aliyemdhulumu kwa aina yeyote ya dhulma; kudhulumiwa mali yake, kukandamizwa, kuteswa, kusengenywa, kuvunjiwa heshima yake na uovu wowote ule atakaofanyiwa. Hivyo basi ni khatari kwa anayedhulumu pindi mdhulumiwa akinyanyua mikono yake kumuombea mabaya kwani du’aa yake huitikiwa moja kwa moja bila ya kizuizi:

 

عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا) أَنَّ النَّبِيَّ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) بَعَثَ مُعَاذًا إِلَى الْيَمَنِ فَقَالَ:  ((اتَّقِ دَعْوَةَ الْمَظْلُومِ فَإِنَّهَا لَيْسَ بَيْنَهَا وَبَيْنَ اللَّهِ حِجَابٌ))

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpeleka Mu’aadh Yemen akasema: ((Iogope du’aa ya aliyedhulumiwa, kwani haina pazia baina yake na baina ya Allaah.)) [Al-Bukhaariy (2448), Swahiyh At-Tirmidhiy(2014), Swahiyh Al-Jaami’ (1037)]

 

Na pia Hadiyth ya ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

   اتَّقوا دعوةَ المظلومِ، فإنها تَصعدُ إلى السماءِ كأنها شرارةٌ

((Ogopeni du’aa ya aliyedhulumiwa kwani inapanda mbinguni kama cheche za moto.)) [Al-Haakim katika Al-Mustadrak ameisahihisha Al-Albaaniy; Swahiyh Al-Jaami’ (118), Swahiyh At-Targhiyb (2228)]

 

Hakuna tofauti ya aliyedhulumiwa akiwa ni Muislamu mwenye taqwa au muovu au hata Kafiri kama ilivyothibiti:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((دَعْوَةُ الْمَظْلُومِ مُسْتَجَابَةٌ وَإِنْ كَانَ فَاجِرًا فَفُجُورُهُ عَلَى نَفْسِهِ))

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Du’aa ya aliyedhulumiwa (dhidi ya aliyemdhulumu) ni yenye kuitikiwa japo akiwa ni mtendaji dhambi kwani dhambi zake ni dhidi ya nafsi yake.)) [Ahmad, Swahiyh At-Targhiyb (2229), Swahiyh Al-Jaami’ (3382)]

 

عَنْ أنس رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: اتَّقُوا دَعْوَةَ الْمَظْلُومِ وَإِنْ كَانَ كَافِرًا فَإِنَّهُ لَيْسَ دُونَهَا حِجَابٌ

 

Imepokelewa kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ogopeni du’aa ya aliyedhulumiwa hata akiwa ni Kafiri, kwani haina baina yake kizuizi.)) [Ameisahihisha Al-Albaaniyn katika Swahiyh At-Targhiyb (2231)

 

 

 

2- Du’aa Ya Mzazi Kwa Mwanawe

 

Du’aa ya mzazi kwa mwanawe hairudi:

 

عّنْ أَنسْ بِنْ ماَلِكْ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ): ((ثَلاَثُ دَعْواتِ لاَ تُرَدُّ: دَعْوَةُ الْوَالِدِ لِوَلَدِهِ، وَدَعْوَةُ الصَّائِم،  وَدَعْوَةُ الْمُسَافَرَ))

Kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu): ((Du’aa za watatu hazirudishwi; du’aa ya mzazi kwa mwanawe, na du’aa ya mwenye kufunga Swawm, na du’aa ya msafiri.))[Al-Bayhaqiy katika Swahiyh Al-Jaami’ (3032) na katika Asw-Swahiyhah (1797)]

 

Mzazi ana haki zaidi kutendewa wema na kutiiwa na mwanawe. Na ndipo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalih wa sallam) ameonya wazazi wasiwaombee watoto wao du’aa mbaya, kwani ni yenye kutakabaliwa:

 

عَنْ جَابِرِ بْنِ عَبْدِ اللَّهِ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((لاَ تَدْعُوا عَلَى أَنْفُسِكُمْ ولاَ تَدْعُوا عَلَى أَولاَدِكُمْ))

Kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msijiombee dhidi ya nafsi zenu wala msiombe dhidi ya watoto wenu.)) [Muslim (3009), Abuu Daawuwd, taz. Swahiyh Abiy Daawuwd (1532) na Swahiyh Al-Jaami’ (7267)]

 

Hadiyth nyingine pia inayothibitisha kukubaliwa du’aa ya mzazi kwa mwanawe ni iliyotajwa pamoja na aliyedhulumiwa na msafiri.

 

 

 

3- Du’aa Ya Mtoto Mwema Kwa Wazazi Wake

 

Du’aa ya mtoto mwema kwa mzazi wake aliyefariki ni miongoni mwa ‘amali tatu ambazo aliyefariki anaendelea kunufaika nayo:

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) قَالَ: ((إِذَا مَاتَ الإِنْسَانُ انْقَطَعَ عَنْهُ عَمَلُهُ إلاَّ مِنْ ثلاَثَةٍ: صَدَقَةٍ جَارِيَةٍ، أَوْ عِلْمٍ يُنْتَفَعُ بِهِ، أَوْ وَلَدٍ صَالِحٍ يَدْعُو لَهُ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Anapofariki mtu hukatika 'amali zake ila mambo matatu; swadaqah inayoendelea au elimu inayonufaisha au mtoto mwema anayemuombea.)) [Muslim, Abu Daawuud, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Ahmad]

 

Na pia

 

عن أبي هريرة عن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((إنَّ الرجل لتُرفع درجتُه في الجنَّة فيقول: أنَّى هذا فيقال: باستغفار ولدك لك ))  

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwama Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika mtu hupandishwa daraja yake Jannah  basi husema: “Kutokana na nini?” Husemwa: “Kutokana na mwanao kukuombea maghfirah.”)) [Ibn Maajah (3660) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (1617)]

 

 

 

4- Du’aa Ya Msafiri

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ): ((ثلاثُ دَعَوَاتٍ مُسْتَجَابَاتٌ لاَ شَكَّ فِيهِنَّ، دَعْوَةُ الْمَظْلُومِ، وَدَعْوَةُ الْمُسَافِرِ، وَدَعْوَةُ الْوَالِدِ عَلَى وَلَدِهِ))

Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Du’aa tatu ni zenye kuitikiwa, hazina shaka ndani yake; du’aa ya aliyedhulumiwa, du’aa ya msafiri, na du’aa ya mzazi kwa mwanawe.)) [Swahiyh At-Tirmidhiy (1905), Swahiyh Ibn Maajah (3129) Swahiyh Al-Jaami’ (3033)

 

 

 

5- Du’aa Ya Mwenye Kumuombea Muislamu Mwenzake Kwa Siri

 

عَنْ أَبِي الدَّرْدَاءِ رضي الله عنه، قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم: مَا مِنْ عَبْدٍ مُسْلِمٍ يَدْعُو لأَخِيهِ بِظَهْرِ الْغَيْبِ، إِلاَّ قَالَ الْمَلَكُ: وَلَكَ بِمِثْلٍ

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Ad-Dardaai (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakuna mja Muislamu anayemuombea nduguye kwa ghayb (kwa siri) isipokuwa, Malaika husema: Nawe pia upate mfano wake.)) [Muslim (2732) na pia (2733)]

 

Na riwaayah nyingine pia katika Muslim:

 

 مَنْ دَعَا لأَخِيهِ بِظَهْرِ الْغَيْبِ، قَالَ الْمَلَكُ الْمُوَكَّلُ بِهِ: آمِينَ، وَلَكَ بِمِثْلٍ

((Atakayemuombea nduguye kwa ghayb (kwa siri), Malaika aliyewakilishwa kwake husema: “Aamiyn nawe upate kama hivyo.")) [Taz pia: Swahiyh Al-Jaami’ (6235), (5737), (3380), (3381), (3379), Swahiyh Ibn Maajah (2358) Abuu Daawuwd (1534)

 

 

 

6- Du’aa Ya Mwenye Dhiki

 

Muislamu aliye katika dhiki, shida, au kufikwa na janga, balaa amkabili Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kumuomba huku akiwa na matumaini na kutegemea Rahmah Yake. Anasema Allaah ('Azza wa Jalla):   

 

أَمَّن يُجِيبُ الْمُضْطَرَّ إِذَا دَعَاهُ وَيَكْشِفُ السُّوءَ وَيَجْعَلُكُمْ خُلَفَاءَ الْأَرْضِ ۗ أَإِلَـٰهٌ مَّعَ اللَّـهِ ۚ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ ﴿٦٢﴾

Au nani Anayemuitika mwenye dhiki mno anapomwomba, na Akamuondoshea ouvu na Akakufanyeni makhalifa wa ardhi? Je, yuko mwabudiwa pamoja na Allaah? Ni machache mno mnayokumbuka. [An-Naml: 62]

 

 

 

7- Du’aa Ya Mwenye Kufikwa Na Msiba

 

Muislamu anapopatwa na msiba, atambue kwamba amepewa fadhila badala yake ya kuomba du’aa, ili arudishiwe alichopoteza na ambacho kitakuwa cha khayr zaidi kuliko kilichomuondokea au kumsibu. Inapasa asichelewe kuomba du’aa yake bali hapo hapo akumbuke na aombe du’aa iliyothibiti katika Sunnah. Alifanya hivyo Mama wa Waumini Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) alipofiwa na mumewe Abuu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kama ilivyoelezwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ أُمِّ سَلَمَةَ (رَضِيَ الله عَنْهَا) قَالَتْ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) يَقُولُ: ((مَا مِنْ مُسْلِمٍ تُصِيبُهُ مُصِيبَةٌ فَيَقُولُ مَا أَمَرَهُ اللَّهُ, إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ, اللَّهُمَّ أْجُرْنِي فِي مُصِيبَتِي وَأَخْلِفْ لِي خَيْرًا مِنْهَا, إلاَّ أَخْلَفَ اللَّهُ لَهُ خَيْرًا مِنْهَا)) قَالَتْ: فَلَمَّا مَاتَ أَبُو سَلَمَةَ قُلْتُ أَيُّ الْمُسْلِمِينَ خَيْرٌ مِنْ أَبِي سَلَمَة أَوَّلُ بَيْتٍ هَاجَرَ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم). ثُمَّ إِنِّي قُلْتُهَا فَأَخْلَفَ اللَّهُ لِي رَسُولَ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ). قَالَتْ: أَرْسَلَ إِلَيَّ رَسُولُ اللَّهِ (صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ) حَاطِبَ بْنَ أَبِي بَلْتَعَةَ يَخْطُبُنِي لَهُ. فَقُلْتُ: إِنَّ لِي بِنْتًا وَأَنَا غَيُورٌ فَقَالَ: ((أَمَّا ابْنَتُهَا فَنَدْعُو اللَّهَ أَنْ يُغْنِيَهَا عَنْهَا وَأَدْعُو اللَّهَ أَنْ يَذْهَبَ بِالْغَيْرَةِ))

Imepokelewa kutoka kwa Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Hakuna Muislamu anayefikwa na msiba akasema Alivyoamrishwa na Allaah: "Hakika sisi ni wa Allaah, na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea. Ee Allaah, nilipe kwa msiba wangu na nipe badala yake kilicho bora kuliko huo (msiba)", basi hapana isipokuwa Allaah Atampa kilicho bora kuliko [msiba] huo)). Alipofariki Abuu Salamah, alisema: “Muislamu gani ni bora kuliko Abuu Salamah ambaye familia yake ilikuwa ya kwanza kuhajiri kwa  Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kisha nikaisoma [du’aa hiyo] na Allaah Akanipa badala yake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akaendelea kusema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamtuma Haatwib bin Abiy Balta’ah anipose kwake nikasema: “Mimi nina binti [anayenitegemea] nami nina tabia ya wivu. Akasema: ((Ama kuhusu binti yake tutamwomba Allaah Amtoshelezee [asiwe na jukumu naye], na namuomba Allaah Amuondoshee tabia ya wivu na hamaki.)) [Muslim]

 

 

 

Share