001-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Ikhlaasw Na Kutia Niyyah Katika ‘Amali, Maneno, Hali Zilizodhihirika Na Zilizofichika

Riyaadhw Asw-Swaalihiyn

 

باب الإخلاص وإحضار النية في جميع الأعمال والأقوال البارزة والخفية­

  001-Mlango Wa Ikhlaasw Na Kutia Niyyah Katika ‘Amali Zote,

Maneno, Hali Zilizodhihirika Na Zilizofichika.

 

Alhidaaya.com

 

 

قَالَ اللهُ تَعَالَى

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ حُنَفَاءَ وَيُقِيمُوا الصَّلَاةَ وَيُؤْتُوا الزَّكَاةَۚ وَذَٰلِكَ دِينُ الْقَيِّمَةِ

Na hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Allaah wenye kumtakasia niyyah Dini, wenye kujiengua na upotofu kuelemea Dini ya haki na wasimamishe Swalaah na watoe Zakaah; na hiyo ndiyo Dini iliyosimama imara.[Al-Bayyinah: 5]

 

لَن يَنَالَ اللَّـهَ لُحُومُهَا وَلَا دِمَاؤُهَا وَلَـٰكِن يَنَالُهُ التَّقْوَىٰ مِنكُمْ ۚ كَذَٰلِكَ سَخَّرَهَا لَكُمْ لِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ ۗ وَبَشِّرِ الْمُحْسِنِينَ

Haimfikii Allaah nyama zake wala damu yake, lakini inamfikia taqwa kutoka kwenu. Hivyo ndivyo Tulivyowatiisha (hao wanyama) kwenu ili mpate kumtukuza Allaah (kusema: Allaahu Akbar) kwa yale Aliyokuongozeni; na wabashirie wafanyao ihsaan. [Al-Hajj: 37]

 

 قُلْ إِن تُخْفُوا مَا فِي صُدُورِكُمْ أَوْ تُبْدُوهُ يَعْلَمْهُ اللَّـهُ ۗ وَيَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

Sema: “Mkificha yale yaliyomo katika vifua vyenu au mkiyafichua, Allaah Anayajua. Na Anajua yale yaliyomo katika mbingu na yale yaliyomo katika ardhi. Na Allaah juu ya kila kitu ni Muweza.”  [Aal-‘Imraan: 29]

 

 

Hadiyth - 1

وعن أمير المؤمِنين أبي حَفْصٍ عمرَ بنِ الخطابِ بنِ نُفَيْلِ بنِ عبدِ العُزّى بن رياحِ بنِ عبدِ اللهِ بن قُرْطِ بن رَزاحِ بنِ عدِي بنِ كعب بنِ لُؤَيِّ بنِ غالبٍ القُرشِيِّ العَدويِّ رضي الله عنه قالَ: سَمِعتُ رَسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم يقُولُ: ((إنّمَا الأَعْمَالُ بالنِّيّاتِ، وَإِنَّمَا لِكُلِّ امرِئٍ مَا نَوَى، فَمَنْ كَانَتْ هجرته إلى الله ورسوله، فهجرته إلى الله ورسوله، ومن كانت هِجْرَتُهُ لِدُنْيَا يُصيبُهَا، أَوْ امْرَأَةٍ يَنْكَحُهَا، فَهِجْرَتُهُ إِلى مَا هَاجَرَ إِلَيْه)). مُتَّفَقٌ عَلَى صِحَّتِهِ. رَوَاهُ إمَامَا الْمُحَدّثِينَ، أبُو عَبْدِ الله مُحَمَّدُ بْنُ إسْمَاعيلَ بْن إبراهِيمَ بْن المُغيرَةِ بنِ بَرْدِزْبهْ الجُعْفِيُّ البُخَارِيُّ، وَأَبُو الحُسَيْنِ مُسْلمُ بْنُ الحَجَّاجِ بْنِ مُسْلمٍ الْقُشَيريُّ النَّيْسَابُورِيُّ رضي اللهُ عنهما فِي صحيحيهما اللَّذَيْنِ هما أَصَحُّ الكُتبِ المصنفةِ.

Kutoka kwa Amiri wa Waumini, Abu Hafsw ‘Umar bin Al-Khatwaab bin Nufayl bin ‘Abdil ‘Uzza bin Riyaah bin ‘Abdillaah bin Qurt bin Razaah bin ‘Adiyyi bin Ka’ab bin Lua-yyi bin Ghaalib Al-Qurashiyyi Al-‘Adawiyyi (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesimulia: “Nilimsikia Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa   aalihi wa sallam) akisema: “Hakika kusihi kwa ‘amali huzingatiwa na niyyah. Na hakika kila mtu atalipwa kwa kile alichokinuia. Ambaye hijrah yake itakuwa ni kwa ajili ya Allaah na Rasuli Wake, basi hijrah yake itakuwa ni kwa ajili ya Allaah na Rasuli Wake. Na ambaye hijrah yake ni kuiendea dunia ili aihodhi, au kumuendea mwanamke ili amuoe; basi hijrah yake itakuwa ni kwa aliloliendea.”  [Hadiyth hii imepokelewa na Maimaam wawili ‘Ulamaa wa Hadiyth, Abuu ‘Abdillaah Muhammad bin Ismaa’iyl bin Ibraahiym bin Al-Mughiyrah bin Bar-dizbah Al-Ju’fiyy Al-Bukhaariy, na Abul-Husayn Muslim bin Al-Hajjaaj bin Muslim Al-Qushayriyy An-Naysaaburiyy (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) Wameipokea katika vitabu vyao ambavyo ndio Swahiyh katika vitabu vya Hadiyth vilivyosanifiwa]

 

 

                                                                              Hadiyth - 2                  

وعن أمِّ المؤمِنينَ أمِّ عبدِ اللهِ عائشةَ رضي الله عنها قالت: قالَ رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((يَغْزُو جَيْشٌ الْكَعْبَةَ فإِذَا كَانُوا بِبَيْدَاءَ مِنَ الأَرضِ يُخْسَفُ بِأَوَّلِهِمْ وآخِرِهِمْ)). قَالَتْ: قلتُ: يَا رَسُولَ اللهِ، كَيْفَ يُخْسَفُ بأوَّلِهِمْ وَآخِرِهِمْ وَفِيهمْ أسْوَاقُهُمْ وَمَنْ لَيْسَ مِنْهُمْ؟! قَالَ: ((يُخْسَفُ بِأَوَّلِهِمْ وَآخِرِهِمْ ثُمَّ يُبْعَثُونَ عَلَى نِيّاتِهمْ)). مُتَّفَقٌ عَلَيهِ. هذَا لَفْظُ الْبُخَارِيِّ 

Mama wa Waumini, Ummu ‘Abdillaah, ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa), amesimulia: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kuna jeshi litakalotaka kuivamia Al-Ka’bah, litakapofika katika ardhi ya jangwa, wote watadidimizwa.” Nikauliza: Eee Rasuli wa Allaah, vipi wote wadidimizwe na miongoni mwao kuna raia wa kawaida na hawakuwa miongoni mwao? Akajibu: “Wote watadidimizwa kisha watafufuliwa kulingana na niyyah zao.” [Hadiyth hii ni lafdh ya Al-Bukhaariy]

 

 

Hadiyth – 3

وعن عائِشةَ رضيَ اللهُ عنها قَالَتْ: قَالَ النبي صلى الله عليه وسلم: ((لا هِجْرَةَ بَعْدَ الفَتْحِ، وَلَكِنْ جِهَادٌ وَنِيَّةٌ، وَإِذَا اسْتُنْفِرْتُمْ فانْفِرُوا)). مُتَّفَقٌ عَلَيْه

‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) amesema: Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna hijrah baada ya Fat-hi (ukombozi wa Makkah), lakini kuna jihaad na niyyah. Na mnapohimizwa kutoka katika jihaad basi nendeni haraka.”  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 4

وعن أبي عبدِ اللهِ جابر بن عبدِ اللهِ الأنصاريِّ رَضي اللهُ عنهما قَالَ: كُنَّا مَعَ النَّبيِّ صلى الله عليه وسلم في غَزَاةٍ، فَقالَ: ((إِنَّ بالمدِينَةِ لَرِجَالًا ما سِرْتُمْ مَسِيرًا، وَلا قَطَعْتُمْ وَادِيًا، إلا كَانُوا مَعَكمْ حَبَسَهُمُ الْمَرَضُ)). وَفي روَايَة: ((إلا شَرَكُوكُمْ في الأجْرِ)). رواهُ مسلمٌ.
ورواهُ البخاريُّ عن أنسٍ رضي الله عنه قَالَ: رَجَعْنَا مِنْ غَزْوَةِ تَبُوكَ مَعَ النَّبيِّ صلى الله عليه وسلم فقال: ((إنَّ أقْوامًا خَلْفَنَا بالْمَدِينَةِ مَا سَلَكْنَا شِعْبًا وَلا وَاديًا، إلا وَهُمْ مَعَنَا؛ حَبَسَهُمُ العُذْرُ))

Abu ‘Abdillaah, Jaabir bin ‘Abdillaah Al-Answaary (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: Tulikuwa pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika vita fulani. Akasema: “Hakika Madiynah kuna watu ambao nyinyi hamkwenda mwendo wowote wala hamkupita jangwa lolote isipokuwa wao walikuwa nanyi, wamezuiliwa na ugonjwa.” Na katika simulizi nyingine imesema: “Isipokuwa wameshirikiana nanyi katika ujira.” [Muslim].

 

 

Hadiyth – 5

وعن أبي يَزيدَ مَعْنِ بنِ يَزيدَ بنِ الأخنسِ رضي الله عنهم وهو وأبوه وَجَدُّه صحابيُّون قَالَ: كَانَ أبي يَزيدُ أخْرَجَ دَنَانِيرَ يَتَصَدَّقُ بِهَا، فَوَضعَهَا عِنْدَ رَجُلٍ في الْمَسْجِدِ، فَجِئْتُ فأَخذْتُها فَأَتَيْتُهُ بِهَا. فقالَ: واللهِ، مَا إيَّاكَ أرَدْتُ، فَخَاصَمْتُهُ إِلى رسولِ اللهِ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ: ((لكَ مَا نَوَيْتَ يَا يزيدُ، ولَكَ ما أخَذْتَ يَا مَعْنُ)). رواهُ البخاريُّ.

Abu Yaziyd Ma’ni bin Yaziyd bin Al-Akhnas (Radhwiya Allaahu ‘anhum), yeye na baba yake na babu yake wote ni Maswahaba, amesema: Baba yangu Yaziyd alikuwa amezitoa dinaar akizitolea swadaqah. Akaziweka kwa mtu Msikitini. Nikaja nikazichukua na nikaja nazo. Akaniambia: Wa-Allaahi sikuwa nimekukusudia wewe!  Nikashtakiana naye kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akasema: “Ee Yaziyd, utapata ulilolinuia, na ee Ma’ni! Ulichokichukua ni chako”. [Al-Bukhaariy]

 

 

Hadiyth – 6

وعن أبي إسحاقَ سَعدِ بنِ أبي وَقَّاصٍ مالِكِ بنِ أُهَيْب بنِ عبدِ منافِ ابنِ زُهرَةَ بنِ كلابِ بنِ مُرَّةَ بنِ كعبِ بنِ لُؤيٍّ القُرشِيِّ الزُّهريِّ رضي الله عنه أَحَدِ العَشَرَةِ المشهودِ لهم بالجنةِ رضي الله عنهم قَالَ: جاءنِي رسولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم يَعُودُنِي عَامَ حَجَّةِ الوَدَاعِ مِنْ وَجَعٍ اشْتَدَّ بي، فقُلْتُ: يَا رَسُولَ اللهِ! إنِّي قَدْ بَلَغَ بي مِنَ الوَجَعِ مَا تَرَى، وَأَنَا ذُو مالٍ وَلا يَرِثُني إلا ابْنَةٌ لي، أفأَتَصَدَّقُ بِثُلُثَيْ مَالِي؟ قَالَ: ((لا))، قُلْتُ: فالشَّطْرُ يَا رَسُولَ اللهِ؟ فقَالَ: ((لا))، قُلْتُ: فالثُّلُثُ يَا رَسُولَ اللهِ؟ قَالَ: ((الثُّلُثُ، والثُّلُثُ كَثيرٌ- أَوْ كبيرٌ- إنَّكَ إنْ تَذَرْ وَرَثَتَكَ أغنِيَاءَ خيرٌ مِنْ أنْ تَذَرَهُمْ عَالَةً يتكفَّفُونَ النَّاسَ، وَإنَّكَ لَنْ تُنفِقَ نَفَقَةً تَبْتَغي بِهَا وَجهَ اللهِ إلا أُجِرْتَ عَلَيْهَا حَتَّى مَا تَجْعَلُ في فِيِّ امْرَأَتِكَ))، قَالَ: فَقُلتُ: يَا رسولَ اللهِ، أُخلَّفُ بعدَ أصْحَابي؟ قَالَ: ((إِنَّكَ لَنْ تُخَلَّفَ فَتَعملَ عَمَلًا تَبتَغي بِهِ وَجْهَ اللهِ إلا ازْدَدتَ بِهِ دَرَجةً ورِفعَةً، وَلَعلَّكَ أنْ تُخَلَّفَ حَتّى يَنتَفِعَ بِكَ أقْوَامٌ وَيُضَرَّ بِكَ آخرونَ. اللَّهُمَّ أَمْضِ لأصْحَابي هِجْرَتَهُمْ ولا تَرُدَّهُمْ عَلَى أعقَابهمْ، لكنِ البَائِسُ سَعدُ بْنُ خَوْلَةَ)). يَرْثي لَهُ رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم أنْ ماتَ بمَكَّة. مُتَّفَقٌ عليهِ.

Abu Is-haaq Sa’d bin Abi Waqqaas Maalik bin Uhayb bin ‘Abdi-Manaaf bin Zuhrah bin Kilaab bin Murrah bin Ka’b bin Lu-ayyi Al-Qurashiyy Az-Zuhriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu), ambaye ni mmojawapo kati ya waliobashiriwa Jannah, amesimulia: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinitembelea mwaka wa Hajjatul-Wadaa’i kutokana na ugonjwa ambao uliokuwa umenishitadi. Nikamwambia: Ee Rasuli wa Allaah, ugonjwa umenifikisha kama unionavyo, nami ni mwenye mali nyingi, wala hakuna atakayenirithi isipokuwa bint yangu (mmoja tu). Je, nizitoe swadaqah thuluthi mbili za mali yangu? Akasema: “Hapana.” Nikasema: Basi nitoe nusu yake ee Rasuli wa Allaah? Akasema: “Hapana”. Nikasema: Je, thuluthi (moja)? Akasema: “Thuluthi (unaweza kutoa). Na hiyo thuluthi ni nyingi – kwa hakika uwaache wenye kukurithi ni wenye kujiweza, ni bora kulikoni kuwaacha wawe mafukara wakiomba watu. Na hakika hutatoa gharama ya matumizi ukawa unataka radhi za Allaah kwa matumizi hayo, isipokuwa utapewa ujira kwayo; hata unachokitia katika kinywa cha mkeo.” Nikamwambia: Eee Rasuli wa Allaah, nitaachwa (niishi muda mrefu) baada ya wenzangu?” Akasema: “Hakika hutoachwa ukafanya 'amali kwa ajili ya kutafuta radhi ya Allaah kwa 'amali hiyo, ispokuwa utazidi daraja na utukufu kwa 'amali hiyo. Na (huenda) ukaachwa (uishi) mpaka watu wanufaike kwa sababu yako, na wengine wadhuriwe kwa sababu yako. Ee Rabb! Wakamilishie Maswahaba wangu hijrah yao, wala usiwarejeshe nyuma kwa visigino vyao. Lakini masikini ni Sa’d bin Khawlah!” Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamsikitikia kwa kuwa amekufa Makkah.  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 7

وعنْ أبي هريرةَ عبدِ الرحمنِ بنِ صخرٍ رضي الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ الله صلى الله عليه وسلم: ((إنَّ الله لا ينْظُرُ إِلَى أَجْسَامِكُمْ، ولا إِلى صُوَرِكمْ، وَلَكن ينْظُرُ إلى قُلُوبِكمْ)). رواه مسلم

Abuu Hurayrah, ‘Abdir-Rahmaan bin Swakhr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Kwa hakika Allaah hatazami viwiliwili vyenu wala sura zenu, lakini Anatazama nyoyo zenu na matendo yenu.” [Muslim]

 

 

Hadiyth – 8

وعن أبي موسى عبدِ اللهِ بنِ قيسٍ الأشعريِّ رضي الله عنه قَالَ: سُئِلَ رسولُ الله صلى الله عليه وسلم عَنِ الرَّجُلِ يُقاتلُ شَجَاعَةً، ويُقَاتِلُ حَمِيَّةً، ويُقَاتِلُ رِيَاءً، أَيُّ ذلِكَ في سبيلِ الله؟ فقال رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ قَاتَلَ لِتَكونَ كَلِمَةُ اللهِ هي العُلْيَا، فَهوَ في سبيلِ اللهِ)). مُتَّفَقٌ عَلَيهِ

Abuu Muwsaa, Abdillaah bin Qays Al-Ash’ariyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa mtu aliyepigana kwa ajili ya kuambiwa shujaa, na anayepigana kwa taasubi (ukabila), na anayepigana kwa riyaa (kujionesha), ni yupo katika hao yupo katika njia ya Allaah? Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu: “Anayepigana ili Dini ya Allaah iwe juu, basi huyo yupo katika njia ya Allaah.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 9

 

وعن أبي بَكرَةَ نُفيع بنِ الحارثِ الثقفيِّ رضي الله عنه أَنَّ النَّبيَّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((إِذَا التَقَى المُسلِمَان بسَيْفَيهِمَا فالقَاتِلُ وَالمَقْتُولُ في النّارِ)). قُلتُ: يا رَسُولَ اللهِ، هذا القَاتِلُ فَمَا بَالُ المقْتُولِ؟ قَالَ: ((إنَّهُ كَانَ حَريصًا عَلَى قتلِ صَاحِبهِ)). مُتَّفَقٌ عليهِ

Abu Bakrah, Nufay’i bin Al-Haarith At-Thaqafiy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesimulia kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema: “Waislamu wawili wakipigana kwa panga zao, basi muuaji na aliyeuliwa wataingia motoni.” Nikauliza: Ee Rasuli wa Allaah, huyu aliyeua (ni sawa kuingia motoni)! Je, aliyeuliwa? Akajibu: “Yeye aliyeuliwa alikuwa na hamu ya kumuua mwenzie.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 10

 

وعن أبي هريرةَ رضي الله عنه قَالَ: قالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: ((صَلاةُ الرَّجلِ في جمَاعَةٍ تَزيدُ عَلَى صَلاتهِ في بيتهِ وصلاته فِي سُوقِهِ بضْعًا وعِشرِينَ دَرَجَةً، وَذَلِكَ أنَّ أَحدَهُمْ إِذَا تَوَضَّأَ فَأَحْسَنَ الوُضوءَ، ثُمَّ أَتَى المَسْجِدَ، لا يَنْهَزُهُ إِلا الصَلاةُ، لا يُرِيدُ إلا الصَّلاةَ: لَمْ يَخْطُ خُطْوَةً إِلا رُفِعَ لَهُ بِهَا دَرجَةٌ، وَحُطَّ عَنْهُ بها خَطِيئَةٌ حَتَّى يَدْخُلَ المَسْجِدَ، فإِذا دَخَلَ المَسْجِدَ كَانَ في الصَّلاةِ مَا كَانَتِ الصَّلاةُ هِي تَحْبِسُهُ، وَالمَلائِكَةُ يُصَلُّونَ عَلَى أَحَدِكُمْ مَا دَامَ في مَجْلِسِهِ الَّذِي صَلَّى فِيهِ، يَقُولُونَ: اللَّهُمَّ ارْحَمْهُ، اللَّهُمَّ اغْفِرْ لَهُ، اللَّهُمَّ تُبْ عَلَيهِ، مَا لَم يُؤْذِ فيه، مَا لَمْ يُحْدِثْ فِيهِ)). مُتَّفَقٌ عليهِ

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mtu kuswali kwa jamaa’ah (ujira wake) huzidi kuswali sokoni kwake na nyumbani kwake kwa daraja zaidi ya ishirini. Nako ni kuwa, mmoja wao anapotawadha vizuri kisha akaenda Msikitini, hakusudii isipokuwa Swalaah, hakuna lililomuinua isipokuwa ni Swalaah tu, basi (atakuwa) hakuinua hatua isipokuwa atainuliwa daraja kwa hatua hiyo na ataondolewa dhambi kwa hatua hiyo mpaka aingie Msikitini, atakuwa angali yupo katika Swalaah maadamu Swalaah ndiyo iliyomzuia. Na Malaika humuombea rahmah mmoja kati yenu maadamu yupo katika kikao chake alichoswalia, wanaomba: “Ee Rabb Mrehemu, Ee Rabb Mghufurie! Ee Rabb Mpokelee tawbah yake!” (Hali inaendelea namna hiyi) maadamu hajaudhi au kupatwa na hadathi.” [Al-Bukhaary na Muslim]

 

 

Hadiyth – 11

 

وعن أبي العبَّاسِ عبدِ اللهِ بنِ عباسِ بنِ عبد المطلب رضِيَ اللهُ عنهما، عن رَسُول الله صلى الله عليه وسلم فيما يروي عن ربهِ تباركَ وتعالى قَالَ: ((إنَّ اللهَ كَتَبَ الحَسَنَاتِ والسَّيِّئَاتِ ثُمَّ بَيَّنَ ذلِكَ، فَمَنْ هَمَّ بحَسَنَةٍ فَلَمْ يَعْمَلْهَا كَتَبَها اللهُ تَبَارَكَ وتَعَالى عِنْدَهُ حَسَنَةً كامِلَةً، وَإنْ هَمَّ بهَا فَعَمِلَهَا كَتَبَهَا اللهُ عَشْرَ حَسَناتٍ إِلى سَبْعمائةِ ضِعْفٍ إِلى ضعَافٍ كَثيرةٍ، وإنْ هَمَّ بِسَيِّئَةٍ فَلَمْ يَعْمَلْهَا كَتَبَهَا اللهُ عِنْدَهُ حَسَنَةً كَامِلةً، وَإنْ هَمَّ بِهَا فَعَمِلَهَا كَتَبَهَا اللهُ سَيِّئَةً وَاحِدَةً)). مُتَّفَقٌ عليهِ.

‘Abul-‘Abbaas, ‘Abdillaah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amepokea kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika aliyopokea kutoka kwa Rabb wake Mtukufu. Amesema: “Kwa hakika Allaah Ameandika mema na mabaya, kisha akabainisha hayo: Atakayefanya hamu ya kutenda jema kisha asitende, Allaah Aliyetukuka Atamuandikia Kwake jema moja kamili. Na akilifanyia hamu na akalitenda, Allaah Atamuandikia mema kumi hadi nyongeza mia saba, hadi nyongeza nyingi zaidi (zaidi ya hizo). Na akifanya hamu ya kutenda jambo baya kisha asilitende, Allaah Atamuandikia Kwake jema kamili. Na akifanya hamu ya kulitenda na akalitenda, Allaah Atamuandikia baya moja.” [Al-Bukhaary na Muslim]

 

 

Hadiyth – 12

 وعن أبي عبد الرحمن عبدِ الله بنِ عمرَ بن الخطابِ رضيَ اللهُ عنهما، قَالَ: سمعتُ رسولَ الله صلى الله عليه وسلم، يقول: ((انطَلَقَ ثَلاثَةُ نَفَرٍ مِمَّنْ كَانَ قَبْلَكُمْ حَتَّى آوَاهُمُ المَبيتُ إِلى غَارٍ فَدَخلُوهُ، فانْحَدرَتْ صَخْرَةٌ مِنَ الجَبَلِ فَسَدَّتْ عَلَيْهِمُ الغَارَ، فَقالُوا: إِنَّهُ لا يُنْجِيكُمْ مِنْ هذِهِ الصَّخْرَةِ إِلا أنْ تَدْعُوا اللهَ بصَالِحِ أعْمَالِكُمْ. قَالَ رجلٌ مِنْهُمْ: اللَّهُمَّ كَانَ لِي أَبَوانِ شَيْخَانِ كبيرانِ، وكُنْتُ لا أغْبِقُ قَبْلَهُمَا أهْلًا ولا مالًا، فَنَأَى بِي طَلَب الشَّجَرِ يَوْمًا فلم أَرِحْ عَلَيْهمَا حَتَّى نَامَا، فَحَلَبْتُ لَهُمَا غَبُوقَهُمَا فَوَجَدْتُهُما نَائِمَينِ، فَكَرِهْتُ أنْ أُوقِظَهُمَا وَأَنْ أغْبِقَ قَبْلَهُمَا أهْلًا أو مالًا، فَلَبَثْتُ- والْقَدَحُ عَلَى يَدِي- أنتَظِرُ اسْتِيقَاظَهُما حَتَّى بَرِقَ الفَجْرُ والصِّبْيَةُ يَتَضَاغَوْنَ عِنْدَ قَدَميَّ، فاسْتَيْقَظَا فَشَرِبا غَبُوقَهُما. اللَّهُمَّ إنْ كُنْتُ فَعَلْتُ ذلِكَ ابِتِغَاء وَجْهِكَ فَفَرِّجْ عَنّا مَا نَحْنُ فِيهِ مِنْ هذِهِ الصَّخْرَةِ، فانْفَرَجَتْ شَيْئًا لا يَسْتَطيعُونَ الخُروجَ مِنْهُ. 

قَالَ الآخر: اللَّهُمَّ إنَّهُ كانَتْ لِيَ ابْنَةُ عَمّ، كَانَتْ أَحَبَّ النّاسِ إليَّ- وفي رواية: كُنْتُ أُحِبُّها كأَشَدِّ مَا يُحِبُّ الرِّجَالُ النساءَ- فأَرَدْتُهَا عَلَى نَفْسِهَا فامْتَنَعَتْ منِّي حَتَّى أَلَمَّتْ بها سَنَةٌ مِنَ السِّنِينَ فَجَاءتْنِي فَأَعْطَيْتُهَا عِشْرِينَ وَمائةَ دينَارٍ عَلَى أنْ تُخَلِّيَ بَيْني وَبَيْنَ نَفْسِهَا فَفعَلَتْ، حَتَّى إِذَا قَدَرْتُ عَلَيْهَا- وفي رواية: فَلَمَّا قَعَدْتُ بَينَ رِجْلَيْهَا، قالتْ: اتَّقِ اللهَ وَلا تَفُضَّ الخَاتَمَ إلا بِحَقِّهِ، فَانصَرَفْتُ عَنْهَا وَهيَ أَحَبُّ النَّاسِ إليَّ وَتَرَكْتُ الذَّهَبَ الَّذِي أعْطَيتُها. اللَّهُمَّ إنْ كُنْتُ فَعَلْتُ ذلِكَ ابْتِغاءَ وَجْهِكَ فافْرُجْ عَنَّا مَا نَحْنُ فيهِ، فانْفَرَجَتِ الصَّخْرَةُ، غَيْرَ أَنَّهُمْ لا يَسْتَطِيعُونَ الخُرُوجَ مِنْهَا. 
وَقَالَ الثَّالِثُ: اللَّهُمَّ اسْتَأْجَرْتُ أُجَرَاءَ وأَعْطَيْتُهُمْ أجْرَهُمْ غيرَ رَجُل واحدٍ تَرَكَ الَّذِي لَهُ وَذَهبَ، فَثمَّرْتُ أجْرَهُ حَتَّى كَثُرَتْ مِنهُ الأمْوَالُ، فَجَاءنِي بَعدَ حِينٍ، فَقالَ: يَا عبدَ اللهِ، أَدِّ إِلَيَّ أجْرِي، فَقُلْتُ: كُلُّ مَا تَرَى مِنْ أجْرِكَ: مِنَ الإبلِ وَالبَقَرِ والْغَنَمِ والرَّقيقِ، فقالَ: يَا عبدَ اللهِ، لا تَسْتَهْزِئْ بي! فَقُلْتُ: لا أسْتَهْزِئ بِكَ، فَأَخَذَهُ كُلَّهُ فاسْتَاقَهُ فَلَمْ يتْرُكْ مِنهُ شَيئًا. الَّلهُمَّ إنْ كُنتُ فَعَلْتُ ذلِكَ ابِتِغَاءَ وَجْهِكَ فافْرُجْ عَنَّا مَا نَحنُ فِيهِ، فانْفَرَجَتِ الصَّخْرَةُ فَخَرَجُوا يَمْشُونَ)). مُتَّفَقٌ عليهِ.

Abu ‘Abdir-Rahmaan, ‘Abdillaah bin ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: Nilimsikia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Waliondoka watu watatu, miongoni mwa watu waliokuwa kabla yenu waliosafiri hadi wakaingia pangoni ili walale. Likaviringika jiwe kutoka juu ya jabali likawafungia pango. Wakasemezana: Hakuna kitakachowaokoa kutokana na jiwe hili isipokuwa mumuombe Allaah kwa ‘amali zenu njema. Mmoja miongoni mwao akaanza kuomba: Ee Rabb, nilikuwa nina wazazi wawili wazee wakongwe, nilikuwa sitangulizi (kabla yao kunywa maziwa) familia wala watumwa. Siku moja haja ya kutafuta kuni ikanipeleka mbali, sikuweza kuwarudia (mapema) mpaka wakalala. Nikawakamulia maziwa yao, nikawakuta wameshalala. Nikachukia kuwaamsha na (nikachukia pia) kuwapa maziwa familia na watumwa kabla yao. Nikawa na (bilauri) imo mikononi mwangu mpaka waamke, hadi alfajiri ikatokeza huku watoto wakipiga kelele kwa njaa miguuni mwangu; wakaamka na wakanywa maziwa yao. Ee Rabb, ikiwa nilifanya hivyo kwa kutaka radhi Zako, basi tufariji katika dhiki tuliyonayo ya jiwe hili. Kukafunguka kidogo kidogo kwa namna ambayo hawawezi kutoka. Mwengine akasema: Ee Rabb, nilikuwa nina bint wa ‘ammi yangu, nilikuwa nikimpenda mno, (Riwaayah nyingine imesema): Nilikuwa nikimpenda kama vile wanaume wanavyopenda mno wanawake. Nikamtaka (kuzini nae), akanikatalia. Mpaka alipokuja mwaka wa ukame, akanijia nikampa dinaar 120 ili niwe nae faragha. Akakubali. Nilipokuwa nimeshamuweza, (Riwaayah nyingine inasema): Nilipoketi baina ya miguu yake akanambia: Mche Allaah, usiivunje pete ila kwa haki yake. Nikamuondokea nikiwa nampenda mno (wala sikumfanya chochote), na nikamuachia dhahabu niliyompa. Ee Rabb, ikiwa nilifanya hivyo kwa ajili ya kupata radhi Zako, basi tufariji katika dhiki tuliyonayo. Jiwe likafunguka, lakini walikuwa hawawezi kutoka. Mtu wa tatu akasema: Ee Rabb, mimi niliwaajiri wafanyakazi, nikawapa ujira wao isipokuwa mtu mmoja, aliuacha ujira wake na akaenda. Nikauzalisha ujira wake mpaka ukawa ni mali nyingi. Baada ya muda akanijia na kuniambia: Ee mja wa Allaah, nipe ujira wangu! Nikamwambia: Kila unachokiona katika ngamia, ng’ombe, mbuzi na watumwa ni ujira wako! Akaniambia: Ee mja wa Allaah, usinifanyie istihzai (usinikebehi)!  Nikamwambia: Sikufanyii istihzai. Akachukua mali yote na akayachunga na wala hakubakisha mali yoyote. Ee Rabb, ikiwa nilifanya hivyo kwa kutaka radhi Zako, basi tufariji katika dhiki tuliyonayo. Jiwe likafunguka wakatoka zao.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Share