10 - Baadhi Ya Watu Wanaojinasibisha Na Uongozi Wa Dini Wanachangia Sana Kudumisha Mitihani Hiyo Kwa Kuwakumbatia Vinyozi Wafanyao Maasi Na Hata Kuwashirikisha Kwenye Uongozi Wa Mambo Ya Dini

 

 

10. Baadhi Ya Watu Wanaojinasibisha Na Uongozi Wa Dini Wanachangia Sana Kudumisha Mitihani Hiyo Kwa Kuwakumbatia Vinyozi Wafanyao Maasi Na Hata Kuwashirikisha Kwenye Uongozi Wa Mambo Ya Dini

 

Matatizo haya ya hizi kazi na uharamu wake, unatiliwa nguvu na baadhi ya watu wanaojipa majukumu ya dini au kujinasibisha na uongozi wa dini kwa kuwakumbatia hao vinyozi na kushirikiana nao katika mambo mbalimbali ya baatwil na kutowapa nasaha wala kuwasaidia katika kuwaongoza na kuwaonya na haramu wanazozifanya.

Viongozi kama hao wa taasisi na jumuiya za dini kama ilivyo baadhi ya maeneo katika nchi za Ulaya, wanaweka maslahi mbele kuliko shariy’ah ya dini. Dini kwao itatumika tu pale katika kuvuta yale maslahi yao au kuzuia maslahi yao yasiharibike.

Mitihani na khasara inapatikana zaidi kwa kuwa hao wanaojinasibisha na dini na uongozi wake, ni watu dhaifu kielimu na kimaadili, ndio maana ni vigumu wao kuwa mfano katika yale ya kuamrisha mema na kukataza maovu.

Inasikitisha utawakuta hao viongozi ndio wenye kuwatumia hao vinyozi na watu wanaokiuka maadili na shariy’ah za dini, kuwatumia kwa maslahi yao, au kuwasaidia katika maovu. Kumetokea qadhiyyah nyingi katika jamii kama hao viongozi kuwatumia vinyozi na watu mfano wao, katika kutoa ushahidi wa uongo au kujipa mahusiano baatwil ili kutwaa wasiyostahiki au kuchukua majukumu ambayo hawakuwa na haki nayo.

Hili –la viongozi wa dini kuwakumbatia watu waovu na wasio na maadili- limechangia sana kuharibu jamii na kuleta ufisadi mwingi.

Baya zaidi, ni hao viongozi wakishirikiana na vinyozi waovu wasio na maadili na watu wengine waovu katika jamii kupambana na watu wanaosimamia dini na kuamrisha mema na kukataza maovu. Matokeo ni kukithiri jamii ya watu wenye uadui na mafunzo sahihi ya Uislamu.

Lakini, tunatarajia nini ikiwa viongozi sampuli hiyo wao wenyewe hawajawa tayari kufuata dini ingawa wanapenda uongozi na kuung’ang’ania kwa ajili ya maslahi yao ya kidunia, ilhali nao wenyewe wanafanya kazi za haramu na hawafanyii kazi nasaha wanazopewa?

Viongozi hao ukiwatazama walivyo kuanzia madhahiri yao kidini ni mtihani na maadili na mwenendo wa kimaisha vilevile msiba. Kwa wenye kupenda dini na ufahamu dini wameshajaribu sana kuwapa nasaha lakini hawako tayari kwani hima yao kubwa si dini bali ni dunia. Lakini khasara kubwa ni kwa wale watu wengi wa kawaida wasiojua dini yao, wao ni wenye kuhadaiwa na kuzolewa na watu sampuli hiyo na mwisho kupotezwa!

 

Na wanawatumia watu wasiojua dini wenye matatizo mengi ya kimaadili na kuwapa nafasi za uongozi na majukumu kwenye jumuiya zao za dini ili wafunikiane yale maovu yao. Ndio si ajabu kuwaona kila mara hao viongozi kuwatembelea hao vinyozi kwenye masaluni yao na kucheka nao na kusengenya na kupiga porojo. Hakuna kunasihiana, wala kuamrishana mema, wala kukatazana maovu! 

Allaah Anatuamrisha tuwe ni wenye kuamrishana mema na kukatazana maovu, Aliposema:

“Na uweko (watokeze) kutoka kwenu Ummah unaolingania kheri na unaoamrisha mema na unaokataza munkari. Na hao ndio waliofaulu.” [Aal-‘Imraan: 104]

Vilevile Allaah Anatuhadharisha na kutoamrisha mema, Anapotupa mfano wa Banuu Israaiyl:

“Wamelaaniwa wale waliokufuru miongoni mwa wana wa Israaiyl kwa lisani ya Daawuwd na ‘Iysaa mwana wa Maryam. Hivyo ni kwa sababu ya kuasi kwao na walikuwa wakitaadi.

“Walikuwa hawakatazani munkari waliyofanya. Uovu ulioje waliyokuwa wakiyafanya.” [Al-Maaidah: 78-79]

Kadhaalika Allaah Anatoa makemeo ya kusaidiana katika maovu, madhambi, uadui, Anaposema:

“Na saidianeni katika wema na uchaji Allaah. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui.” [Al-Maaidah : 02]

Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

“Atakayeona munkari [uovu] basi aubadilishe kwa mkono wake, na asipoweza basi kwa ulimi wake, na asipoweza basi kwa moyo wake [achukizwe] na huo ni udhaifu wa Iymaan.” [Muslim]

Muumin ni yule anayekataza maovu na asipoweza achukie kwa moyo wake au sivyo atakuwa katika khatari ya kupotoka, kupata adhabu na kutokukubaliwa du’aa yake. Anasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

“Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake, hakika mtaamrishana ma’aruwf [wema] na mtakatazana munkari [maovu], au Allaah Atakuleteeni adhabu, kisha mtamuomba wala Hatokuitikieni.” [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan]

Tunatahadharisha na viongozi wa dini sampuli hiyo ambayo wanapigania matumbo yao na umaarufu na madaraka katika jamii, hawasaidii jamii isipokuwa maslahi yao, na wakisaidia ni katika maovu na kueneza uozo katika jamii. Inafika hadi wale watu wa Sunnah “Ghurabaa” wanaotengeneza yale yaliyofisidiwa na watu, jamii inawaona hao ndio maadui na wale wanaoozesha jamii ndio wazuri!! Ni yale aliyotukhabarisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  kuwa mwisho wa zama mambo yatageuka ndio sio na sio ndio, pale aliposema:

“Zitakuja kwa watu zama za udanganyifu, atasadikishwa yule muongo na atakadhibishwa yule mkweli, ataaminiwa yule khaini na atakhiniwa yule mwaminifu, na atazungumza yule “Ruwaybidhwah.” Itasemwa: ‘Ni nani “Ruwaybidhwah”? Atajibu: ‘Ni yule mjinga asiye na kima anayezungumzia mambo ya watu’.” [Ibn Maajah, na Al-Albaaniy kasema Swahiyh katika Swahiyh Ibn Maajah]

Watu wanapaswa wakae mbali sana na wajiepushe na viongozi kama hao waovu wanaojinasibisha na dini ilhali dini iko mbali nao kwa maadili yao mabovu, maadui wa Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wenye ulafi wa madaraka, tamaa za dunia na ukosefu wa maadili na wenye kula chumo la haramu.

 

 

 

Share