003-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AR-RABB

 

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

الرَّبّ

 003-AR-RABB

 

 

 

Ar-RABB: Rabb: Al-Maalik (Mfalme), Ar-Razzaaq (Mwenye kuruzuku), Al-Murabbi (Mlezi), Al-Khaaliq (Muumbaji), Al-Mudabbir (Mwendeshaji na Mpangaji).

 

Ni Rabb wa walimwengu na Anaundesha ulimwengu wote. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 الْحَمْدُ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٢﴾

Himidi zote Anastahiki Allaah Rabb wa walimwengu.  [Al-Faatihah (1: 2)]

 

Na pia Ar-Rabb inamaanisha kama alivyosema Ibn Al-Mandhdwur: “Ar-Rabb katika lugha ni Al-Maalik (Mfalme), As-Sayyid (Bwana), Al-Mudabbir (Mwendeshaji na Mpangaji), Al-Murabbi (Mlezi), Al-Qayyim (Msimamiaji), Al-Mun’im (Mwenye kuneemesha).” [Lisaan Al-‘Arab (1/399)]

 

Ar-Rabb inajumuisha pia Mwenye kuabudiwa kwa dalili ya kuwa swali mojawapo la kaburini ni “Man Rabbuka” (Nani Rabb wako)” yaani; nani Muabudiwa wako”.

 

Na Ar-Rabb katika asili ni katika ulezi: yaani Yule anayelea na kukuza kidogo kidogo hadi anakamilika, wala haisemwi kwa yeyote Ar-Rabb isipokuwa kwa Allaah Pekee na huongezwa kwa kusema: “Rabbul ‘Aalamiyn”. Au kwa asiyekuwa Allaah kwa kuongezewa kitu mbele yake kama vile kusema: Rabb Ad-Daar (bwana au mwenye nyumba), Rabb Al-Faras (bwana au mwenye farasi) au ngamia kwa anayemiliki hivyo [Angalia ‘An-Nihaayah fiy Gharyib al-Hadiyth (338) na Mufradaat Alfaadhw Qur-an (336) na Al-Asmaa (1/394)]

 

Jina hili tukufu linakusanya sifa nyingi za kimatendo, “Bali linaweza kuunganishwa na majina mengine matukufu ya kiutendaji na sifa zake tukufu. [Fiqh Al-Asmaa Al-Husnaa Dr. Abdur-Razzzaq Al-Badr (79)]  Hivyo Ar-Rabb kuingia katika: Al-Qaadir, Al-Khaaliq, Al-Baariu, Al-Muswawwir, Al-Hayyu, Al-Qayyuwm, Ar-Rahmaan na mengineyo. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 سَلَامٌ قَوْلًا مِّن رَّبٍّ رَّحِيمٍ ﴿٥٨﴾

Salaamun”; kauli kutoka kwa Rabb Mwenye kurehemu) [Yaasiyn (36: 58)]

 

Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ambaye ni Rabb wa viumbe wote, kila kilichoko mbinguni na ardhini ni mja Kwake na katika udhibiti Wake. Yeye ndiye Aliyelea viumbe vyote kwa neema Zake, kisha Akakipa kila kitu umbo lake linalolaiki, kisha Akakiongoza kama ilivyothibiti katika Qur-aan:

قَالَ فَمَن رَّبُّكُمَا يَا مُوسَىٰ ﴿٤٩﴾

 (Fir’awn) Akasema: “Basi nani (huyo) Rabb wenu ewe Muwsaa?”

 

قَالَ رَبُّنَا الَّذِي أَعْطَىٰ كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَىٰ ﴿٥٠﴾

 (Muwsaa) Akasema: “Rabb wetu ni Yule Aliyekipa kila kitu umbo lake, kisha Akakiongoza.” [Twaahaa (20: 49-50)]

 

Akawaenezea viumbe Vyake neema kubwa kubwa ambazo lau watazikosa hawatoweza kuishi. Akawakuza, Akawapa malisho, Akawalea kwa malezi kamilifu. Basi hakuna neema isipokuwa neema Yake. Ndipo Jina hili likawa tukufu, lenye umuhimu mkubwa na azizi katika nafsi na nyoyo za Manabii, na vipenzi vya Allaah, na ndipo ikawa aghlabu ya du’aa za Qur-aan na Sunnah ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Salaf zinaanzia na “Rabbanaa” au “Rabbi” kama du’aa ya Nabiy Aadam ('Alayhis-Salaam):

 

 قَالَا رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٢٣﴾

“Rabb wetu! Tumedhulumu nafsi zetu, na basi Usipotughufuria na Ukaturehemu; bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” [Al-A’raaf (7: 23)]

 

Na du’aa ya Khaliylur-Rahmaan Nabiy Ibraahiym ('Alayhis-Salaam):

 

رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ ﴿٤١﴾

“Rabb wetu! Nighufurie na wazazi wangu wawili na Waumini Siku itakayosimama hesabu.[Ibraahiym (14: 41)]

 

Na Du’aa ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

وَقُل رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ ﴿٩٧﴾ وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُونِ ﴿٩٨﴾

Na sema: “Rabb wangu! Najikinga Kwako kutokana na uchochezi (na wasiwasi) wa mashaytwaan.” “Na najikinga Kwako Rabb wasinihudhurie.” [Al-Muuminuwn (23: 97-98)]

 

 

Na du’aa za wenye ‘ilmu:

 

رَبَّنَا لَا تُزِغْ قُلُوبَنَا بَعْدَ إِذْ هَدَيْتَنَا وَهَبْ لَنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً ۚ إِنَّكَ أَنتَ الْوَهَّابُ ﴿٨﴾

“Rabb wetu, Usizipotoe nyoyo zetu baada ya kutuongoza na Tutunukie kutoka kwako rahmah. Hakika Wewe ni Mwingi wa kutunuku na kuneemesha.” [Aal-‘Imraan (3: 8)]

 

 

Na du’aa za ‘Ibaadur-Rahmaan (waja wa Mwingi wa Rahmah):

 

  رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا ﴿٧٤﴾

“Rabb wetu! Tutunukie katika wake zetu na dhuria wetu viburudisho vya macho yetu, na Tujaalie kuwa waongozi kwa wenye taqwa [Al-Furqaan (25: 74)]

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kuhusu Rabb kuwa mja anakuwa karibu Naye wakati wa kusujudu na ndipo ikawa kusujudu ni sababu moja wapo ya wasiylah (kujikurubisha) kwa Ar-Rabb katika kuomba du’aa:

 

أقربُ ما يكُونُ الرَّبُّ مِنَ العبدِ في جوفِ اللَّيلِ الآخِرِ،  فإنِ استطعتَ أن تكونَ ممّن يذكُرُ اللهَ في تِلكَ الساعةِ ،  فكُن

“Wakati Rabb Anakuwa karibu kabisa na mja, ni wakati wa mwisho wa usiku, kwa hiyo ukiweza kuwa miongoni mwa wanaomdhukuru Allaah katika saa hiyo basi uwe.” [Swahiyh At-Tirmidhiy (3578)]

 

 

 

 

Share