Anapozini Mmoja Katika Wanandoa, Je, Ndoa Inavunjika?

SWALI:

 

Assalamu alaykum, naomba kuelimishwa watu waliopokwenye ndoa mmoja wapo akizini na ushahidi ukapatikana, je ndoa itakuwepo au imeshavunjika

 


JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Ndoa haivunjiki kwa mmoja wa wanandoa kuzini. Lakini hata hivyo, haifai kuishi na mwanandoa anayezini ikiwa anaendelea na tabia hiyo kama hajaacha na kutubia.

 

Anasema Mwanachuoni Ibn Qudaamah (Rahimahu Allaah):

“Ikiwa mwanamke amezini na mwanamme, au mume wake kazini, ndoa haivunjiki, ikiwa imetokea kabla au baada ya kuingiliana, kwa mujibu wa Wanachuoni wengi.

Huu ndio mtazamo wa Mujaahid, ‘Atwaa, An-Nakha’iy, Ath-Thawriy, Ash-Shaafi’iy, Is-haaq na Asw-haab Ar-Ra-y.”

 

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) yeye anaona ni Mustahab kwa mwanamme kumuacha mkewe ikiwa amezini, na akasema kuwa, “Sidhani kama anapaswa kuendelea kuishi na mke kama huyo, kwani hakuna dhamana kuwa atabaki kuwa mwaminifu kwake na ataweza kumhusisha na mtoto asiye wake.” …

 

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema: “Hapaswi kulala naye hadi ithibitike kuwa hana mimba, kwa kusubiri kwa vipindi vitatu vya hedhi.”

 

(Ibn Qudaamah anaendelea kueleza) Lakini, inawezekana zaidi kujulikana kama ana mimba kwa kukaa kipindi kimoja cha hedhi.

Mwisho wa kunukuu.

 

[Al-Mughniy (9/565)]

 

Ni muhimu mmoja wa wanandoa anapoona tabia hiyo chafu kwa mwenzake, amnasihi aache haraka sana, na ikiwa ataendelea na tabia hiyo, basi anaweza kutengana naye.

 

Kuishi na mwanandoa mwenye kuzini, ni khatari kwa kizazi, familia na mmonyoko wa maadili na malezi mabaya. Haifai kuishi na mwanandoa wa aina hiyo.

 

Ikiwa ni mwanammke ndiye anayefanya kitendo hicho, basi mume ana nafasi ya kutoa talaka ikiwa hatotaka kuendelea kuishi na mwanamke huyo, au ikiwa alikuwa bado anataka kuishi naye lakini kamnasihi na kumkanya na bado akawa anaendeleza tabia hiyo.

 

Ama ikiwa mume ndiye anayefanya kitendo hivyo, basi mke anaweza kudai talaka na ikiwa mume hataki kutoa talaka, basi mke ana haki ya kujivua kwenye ndoa (khul’u).

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share