011-Riyaadhw Asw-Swaalihiyn: Mlango Wa Kufanya Juhudi

Riyaadhw Asw-Swaalihiyn

 

باب المجاهدة

011 – Mlango Wa Kufanya Juhudi

 

Alhidaaya.com

 

 

قَالَ الله تَعَالَى:

 

وَالَّذِينَ جَاهَدُوا فِينَا لَنَهْدِيَنَّهُمْ سُبُلَنَا ۚ وَإِنَّ اللَّـهَ لَمَعَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٦٩﴾

Na wale waliofanya juhudi kwa ajili Yetu, bila shaka Tutawaongoza njia Zetu. Na hakika Allaah Yu Pamoja na watendao ihsaan. [Al-‘Ankabuwt: 69]

 

وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ ﴿٩٩﴾

Na mwabudu Rabb wako mpaka ikufikie yakini (mauti). [Al-Hijr: 99]

 

وَاذْكُرِ اسْمَ رَبِّكَ وَتَبَتَّلْ إِلَيْهِ تَبْتِيلًا ﴿٨﴾

Na dhukuru Jina la Rabb wako, na jitolee Kwake kwa kujitolea (kikamilifu). [Al-Muzzammil: 8]

 

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ ﴿٧﴾

Basi yule atakayetenda kheri (hata kama) uzito wa chembe ya atomu (au mdudu chungu) ataiona. [Zalzalah: 7]

 

وَمَا تُقَدِّمُوا لِأَنفُسِكُم مِّنْ خَيْرٍ تَجِدُوهُ عِندَ اللَّـهِ هُوَ خَيْرًا وَأَعْظَمَ أَجْرًا ۚ وَاسْتَغْفِرُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٠﴾

Na chochote kile cha kheri mnachokadimisha kwa ajili ya nafsi zenu, mtakikuta kwa Allaah. Ni bora, na ujira mkubwa zaidi. Na muombeni Allaah maghfirah, hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu). [Al-Muzzammil: 20]

 

وَمَا تُنفِقُوا مِنْ خَيْرٍ فَإِنَّ اللَّـهَ بِهِ عَلِيمٌ ﴿٢٧٣﴾

Na chochote mtoacho katika khayr basi Allaah kwacho ni Mjuzi. [Al-Baqarah: 273]

 

 

Hadiyth – 1

عن أبي هريرة رضي الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: ((إنَّ الله تَعَالَى قَالَ: مَنْ عادى لي وَلِيًّا فَقَدْ آذَنْتُهُ بالحَرْبِ، وَمَا تَقَرَّبَ إِلَيَّ عَبْدي بشَيءٍ أَحَبَّ إلَيَّ مِمَّا افْتَرَضْتُ عَلَيهِ، وَمَا يَزَالُ عَبْدِي يَتَقرَّبُ إلَيَّ بالنَّوافِلِ حَتَّى أحِبَّهُ، فَإذَا أَحبَبتُهُ كُنْتُ سَمعَهُ الَّذِي يَسْمَعُ بِهِ، وَبَصَرَهُ الَّذِي يُبْصِرُ بِهِ، ويَدَهُ الَّتي يَبْطِشُ بِهَا، وَرِجْلَهُ الَّتِي يَمْشي بِهَا، وَإنْ سَأَلَني لأُعْطِيَنَّهُ، وَلَئِنِ اسْتَعَاذَنِي لأُعِيذَنَّهُ)). رواه البخاري

Imetoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiyah Allaahu ‘anhu) kwamba: Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Allaah (Ta’aalaa) Anasema: “Mwenye kumfanyia uadui kipenzi Changu, basi Nimeshamtangazia vita. Mja Wangu hajikurubishi Kwangu ila kwa jambo linalonipendeza mno kulikoni kutenda fardhi nilizomfaradhishia; mja Wangu ataendelea kujikurubisha Kwangu kwa kujitolea mpaka Nimpende. Nitakapompenda, Nitakuwa ni masikilizio yake anayosikilizia, na ni macho yake anayoonea, na ni mkono wake anaoshikia, na ni mguu wake anaotembelea. Akiniomba Nitampa, na akiomba kinga Kwangu Nitamkinga.” [Al-Bukhaariy]

 

 

Hadiyth – 2

عن أنس رضي الله عنه عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم فيما يرويه عن ربّه عز وجل قَالَ: ((إِذَا تَقَربَ العَبْدُ إلَيَّ شِبْرًا تَقَربْتُ إِلَيْه ذِرَاعًا، وَإِذَا تَقَرَّبَ إلَيَّ ذِرَاعًا تَقَربْتُ مِنهُ بَاعًا، وِإذَا أتَانِي يَمشي أتَيْتُهُ هَرْوَلَةً)). رواه البخاري

Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amepokea kutoka kwa Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu aliyopokea kutoka kwa Rabb Wake (‘Azza wa Jalla) Anasema: “Mja Wangu atakaponikaribia kwa shubiri, Nitamkaribia kwa dhiraa. Akinikaribia kwa dhiraa, Nitamkaribia kwa pima, na akinijia kwa kutembea nami Nitamkimbilia.” [Al-Bukhaariy]

 

 

Hadiyth – 3

عن ابن عباس رضي الله عنهما قَالَ: قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: ((نِعْمَتَانِ مَغبونٌ فيهما كَثيرٌ مِنَ النَّاسِ: الصِّحَّةُ، وَالفَرَاغُ)). رواه البخاري

‘Abdullaah bin ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Watu wengi wamepoteza neema mbili: afya na faragha [wakati].” [Al-Bukhaariy]

 

 

Hadiyth – 4

عن عائشة رَضي الله عنها: أنَّ النَّبيّ صلى الله عليه وسلم كَانَ يقُومُ مِنَ اللَّيلِ حَتَّى تَتَفَطَّرَ قَدَمَاهُ فَقُلْتُ لَهُ: لِمَ تَصنَعُ هَذَا يَا رسولَ الله، وَقدْ غَفَرَ الله لَكَ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِكَ وَمَا تَأَخَّرَ؟ قَالَ: ((أَفَلا أُحِبُّ أنْ أكُونَ عَبْدًا شَكُورًا)). مُتَّفَقٌ عَلَيه

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa): Kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisimama usiku (kuswali) mpaka miguu yake ikivimba. Nikamuuliza: mbona unafanya hivi yaa Rasula-Allaah na hali ya kuwa Allaah Ameshakughufuria dhambi zako zilizotangulia na zitakazokuja? Akajibu: “Kwani sipendelei niwe ni mja mwenye kushukuru?” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 5

عن عائشة رضي الله عنها، أنَّها قَالَتْ: كَانَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم إِذَا دَخَلَ العَشْرُ أَحْيَا اللَّيلَ، وَأيْقَظَ أهْلَهُ، وَجَدَّ وَشَدَّ المِئْزَر. مُتَّفَقٌ عَلَيه

Kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa): Alikuwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inapoingia kumi la mwisho (katika mwezi wa Ramadhwaan) hukesha usiku, akiwaamsha watu wa nyumbani kwake akijipinda na kukaza kikoi chake.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 6

عن أبي هريرة رضي الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: ((المُؤْمِنُ القَوِيُّ خَيرٌ وَأَحَبُّ إِلَى اللهِ مِنَ المُؤْمِنِ الضَّعيفِ، وَفي كُلٍّ خَيرٌ. احْرِصْ عَلَى مَا يَنْفَعُكَ، واسْتَعِنْ بِاللهِ وَلا تَعْجَزْ. وَإنْ أَصَابَكَ شَيءٌ فَلا تَقُلْ لَوْ أنّي فَعَلْتُ كَانَ كَذَا وَكَذَا، وَلَكِنْ قُلْ: قَدرُ اللهِ، وَمَا شَاءَ فَعلَ؛ فإنَّ لَوْ تَفْتَحُ عَمَلَ الشَّيطَانِ)). رواه مسلم

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Amesema Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Muumin mwenye nguvu ni bora na anapendeza mno mbele ya Allaah kulikoni Muumin dhaifu, na katika wote (hao) kuna khayr, fanya bidii katika jambo linalokunufaisha, na uombe msaada kwa Allaah na wala usifanye uvivu. Utakaposibiwa na jambo usiseme; Lau ningalifanya kadhaa na kadhaa, lakini sema: "Qadaru Allaahi wa maa Shaa Fa'ala - Allaah Amejaaliya, na Atakalo Yeye huwa." Kwani kusema; lau, hufungua ‘amali ya shaytwaan.” [Muslim]

 

 

Hadiyth – 7

عن أبي هريرة رضي الله عنه أنَّ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((حُجِبَتِ النَّارُ بالشَّهَواتِ، وَحُجِبَتِ الجَنَّةُ بِالمَكَارِهِ)). مُتَّفَقٌ عَلَيه

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Moto umezunguka kwa matamanio, na Jannah imezungukwa kwa machukivu.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 8

عن أبي عبد الله حُذَيفَةَ بنِ اليمانِ رضي الله عنهما، قَالَ: صَلَّيْتُ مَعَ النَّبيّ صلى الله عليه وسلم ذَاتَ لَيلَةٍ فَافْتَتَحَ البقَرَةَ، فَقُلْتُ: يَرْكَعُ عِنْدَ المائَةِ، ثُمَّ مَضَى. فَقُلْتُ: يُصَلِّي بِهَا في ركعَة فَمَضَى، فقُلْتُ: يَرْكَعُ بِهَا، ثُمَّ افْتَتَحَ النِّسَاءَ فَقَرَأَهَا، ثُمَّ افْتَتَحَ آلَ عِمْرَانَ فَقَرَأَهَا، يَقرَأُ مُتَرَسِّلًا: إِذَا مَرَّ بآية فِيهَا تَسبيحٌ سَبَّحَ، وَإذَا مَرَّ بسُؤَالٍ سَأَلَ، وَإذَا مَرَّ بتَعَوُّذٍ تَعَوَّذَ، ثُمَّ رَكَعَ، فَجَعَلَ يَقُولُ: ((سُبْحَانَ رَبِّيَ العَظِيمِ)) فَكَانَ رُكُوعُهُ نَحوًا مِنْ قِيَامِهِ، ثُمَّ قَالَ: ((سَمِعَ اللهُ لِمَنْ حَمِدَهُ ربَّنا ولك الحمد)) ثُمَّ قَامَ قِيامًا طَويلًا قَريبًا مِمَّا رَكَعَ، ثُمَّ سَجَدَ، فَقَالَ: ((سُبْحَانَ رَبِّيَ الأَعْلَى)) فَكَانَ سُجُودُهُ قَريبًا مِنْ قِيَامِهِ. رواه مسلم

Abuu ‘Abdillaah, Hudhayfah bin Al-Yamaani (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: Usiku mmoja niliswali na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaanza kusoma Suwratu Al-Baqarah. Nikasema (moyoni) atarukuu katika Aayah ya mia. Lakini akaendelea, nikasema atamaliza Suwrah yote katika rakaah moja. Akaendelea. Nikasema: Atarukuu akimaliza Suwrah hii, halafu akaianza Suwratu An-Nisaa. Akaisoma yote, kisha akaianza Suwratu Aal-‘Imraan, akaisoma yote. Alikuwa akisoma taratibu, anapoisoma Aayah yenye kumsabih Allaah, yeye humsabbih, na anaposoma Aayah ya kuomba yeye huomba, na anaposoma Aayah ya kujikinga yeye hujikinda. Kisha akarukuu na akawa anasema: “Subhaana Rabbiyal-‘Adhwiym - Ametakasika Rabb wangu Adhimu.” Rukuu yake ikawa inafanana na kisimamo chake, kisha akasema: “Sami’a Allaahu liman Hamidah Rabbanaa walakal Hamd - Allaah Amemsikia mwenye kumuhimidi, Ee Rabb wetu, ni Zako Wewe tu sifa njema.” Kisha akasimama kisimamo kirefu kinachokaribiana na rukuu, kisha akasujudu, akasema: “Subhaana Rabbiyal-A’laa - Ametakasima Rabb Aliye juu.” Sijdah yake yake ikakaribiana na kisimamo chake. [Muslim]

 

 

Hadiyth – 9

عن ابن مسعود رضي الله عنه قَالَ: صَلَّيْتُ مَعَ النَّبيّ صلى الله عليه وسلم لَيلَةً، فَأَطَالَ القِيامَ حَتَّى هَمَمْتُ بأمْرِ سُوءٍ! قيل: وَمَا هَمَمْتَ بِهِ؟ قَالَ: هَمَمْتُ أنْ أجْلِسَ وَأَدَعَهُ. مُتَّفَقٌ عَلَيه

‘Abdullaah bin Mas’uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesimulia: “Usiku mmoja niliswali na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akarefusha kisimamo hata nikafikiria kutenda jambo baya. Akaulizwa: kwani ulifikiri kufanya nini? Akajibu: Nilifikiria nikae chini na nimuache Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 10

عن أنس رضي الله عنه عن رَسُول الله صلى الله عليه وسلم، قَالَ: ((يَتْبَعُ المَيتَ ثَلاَثَةٌ: أهْلُهُ وَمَالُهُ وَعَملُهُ، فَيَرجِعُ اثنَانِ وَيَبْقَى وَاحِدٌ: يَرجِعُ أهْلُهُ وَمَالُهُ، وَيَبقَى عَملُهُ)). مُتَّفَقٌ عَلَيه

Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amepokea Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Mambo matatu humfuata maiti: Familia yake, mali yake na ‘amali zake. Mawili kati ya hayo hurejea nayo na kubakia na moja; familia na mali hurejea na ikabakia ‘amali yake.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hadiyth – 11

 عن ابن مسعود رضي الله عنه قَالَ: قَالَ النَّبيّ صلى الله عليه وسلم: ((الجَنَّةُ أَقْرَبُ إِلَى أَحَدِكُمْ مِنْ شِرَاكِ نَعْلِهِ، وَالنَّارُ مِثلُ ذلِكَ)). رواه البخاري

‘Abdullaa bin Mas’uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Jannah ipo karibu zaidi kwa mmoja wenu kulikoni mkanda wa kiatu chake, na moto ni hivyo hivyo.” [Al-Bukhaariy]

 

 

Hadiyth – 12

عن أبي فِراسٍ ربيعةَ بنِ كعبٍ الأسلميِّ خادِمِ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم، ومن أهلِ الصُّفَّةِ رضي الله عنه، قَالَ: كُنْتُ أبِيتُ مَعَ رسولِ الله صلى الله عليه وسلم فآتِيهِ بِوَضُوئِهِ وَحَاجَتِهِ، فَقَالَ: ((سَلْنِي)) فقُلْتُ: اسْأَلُكَ مُرَافَقَتَكَ في الجَنَّةِ. فَقَالَ: ((أَوَ غَيرَ ذلِكَ؟)) قُلْتُ: هُوَ ذَاكَ، قَالَ: ((فأَعِنِّي عَلَى نَفْسِكَ بِكَثْرَةِ السُّجُودِ)). رواه مسلم

Abuu Firaas, Rabi’ bin Ka’b Al-Aslamiy mtumishi wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ni katika watu wa suffah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Nilikuwa nikilala kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nikimpelekea maji ya kutawadhia na mahitajio yake mengineo. Akaniambia: “Niombe.” Nikamwambia: Nakuomba kuwa na wewe Jannah. Akaniuliza: “Una lingine?” Nikamjibu: Ni hilo tu. Akaniambia: “Nisaidie juu nafsi yako kusujudu kwa wingi.” [Muslim]

 

 

Hadiyth – 13

عن أبي عبد الله، ويقال: أَبُو عبد الرحمن ثوبان - مولى رَسُول الله صلى الله عليه وسلم رضي الله عنه، قَالَ: سَمِعْتُ رسولَ الله صلى الله عليه وسلم يَقُولُ: ((عَلَيْكَ بِكَثْرَةِ السُّجُودِ؛ فَإِنَّكَ لَنْ تَسْجُدَ للهِ سَجْدَةً إلا رَفَعَكَ اللهُ بِهَا دَرجَةً، وَحَطَّ عَنكَ بِهَا خَطِيئةً)). رواه مسلم

Abuu ‘Abdillaah, pia huitwa Abuu ‘Abdir-Rahmaan, Thawbaan muachwa huru wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Nilimsikia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Kithirisha kusujudu kwa wingi, kwani wewe hutosujudu sijdah (moja) isipokuwa Allaah Atakupandisha daraja kwa sijdah hiyo, na Atakuondoshea dhambi kwa sijdah hiyo.” [Muslim]

 

 

Hadiyth – 14

عن أَبي صَفوان عبد الله بنِ بُسْرٍ الأسلمي رضي الله عنه، قَالَ: قَالَ رَسُول الله صلى الله عليه وسلم: ((خَيرُ النَّاسِ مَنْ طَالَ عُمُرهُ، وَحَسُنَ عَمَلُهُ)). رواه الترمذي، وَقالَ: ((حديث حسن))

Abuu Swafwaan, ‘Abdullaah bin Busri Al-Aslamiy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mbora katika watu ni yule ambaye umri wake umerefuka na ‘amali zake zikatangamaa.” [At-Tirmidhiy, na amsema: Hadiyth hii ni Hasan]

 

 

Hadiyth -15

عن أنس رضي الله عنه، قَالَ: غَابَ عَمِّي أَنَسُ بْنُ النَّضْرِ رضي الله عنه عن قِتالِ بدرٍ، فَقَالَ: يَا رسولَ الله، غِبْتُ عَنْ أوّل قِتال قَاتَلْتَ المُشْرِكِينَ، لَئِن اللهُ أشْهَدَنِي قِتَالَ المُشركِينَ لَيُرِيَنَّ اللهُ مَا أصْنَعُ.

فَلَمَّا كَانَ يَومُ أُحُدٍ انْكَشَفَ المُسْلِمونَ، فَقَالَ: اللَّهُمَّ أعْتَذِرُ إلَيْكَ مِمَّا صَنَعَ هؤُلاءِ- يعني: أصْحَابهُ- وأبْرَأُ إلَيْكَ مِمَّا صَنَعَ هؤُلاءِ- يَعني: المُشركِينَ- ثُمَّ تَقَدَّمَ فَاسْتَقْبَلهُ سَعدُ بْنُ مُعاذٍ، فَقَالَ: يَا سعدَ بنَ معاذٍ، الجَنَّةُ وربِّ الكعْبَةِ إنِّي أجِدُ ريحَهَا منْ دُونِ أُحُدٍ. قَالَ سعدٌ: فَمَا اسْتَطَعتُ يَا رسولَ الله مَا صَنَعَ!

قَالَ أنسٌ: فَوَجَدْنَا بِهِ بِضْعًا وَثَمانينَ ضَربَةً بالسَّيفِ، أَوْ طَعْنةً بِرمْحٍ، أَوْ رَمْيَةً بسَهْمٍ، وَوَجَدْنَاهُ قَدْ قُتِلَ وَمَثَّلَ بِهِ المُشْرِكونَ فما عَرَفهُ أَحَدٌ إلا أُخْتُهُ بِبَنَانِهِ.

قَالَ أنس: كُنَّا نَرَى أَوْ نَظُنُّ أن هذِهِ الآية نزلت فِيهِ وفي أشباهه: {مِنَ الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللهَ عَلَيْهِ} [الأحزاب: 23] إِلَى آخِرها. مُتَّفَقٌ عَلَيه

Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesimulia: Ammiy yangu Anas bin Nadhwr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) hakuwepo katika Vita vya Badr. Akasema: Yaa Rasula-Allaah, nilighibu katika vita vya kwanza ulivyopigana na washirikina. Wa-Allaahi! Allaah Akinijaalia kuhudhuria katika kupigana na washirikina, Atawadhihirishia (washirikina) kile nitakachofanya. Siku ya Vita vya Uhud, Waislamu walikimbia akaomba: Ee Rabb, nakuomba msamaha kwa yale waliyoyafanya hawa (watu wake), na najitenga kwa yale waliyoyafanya washirikina. Halafu akaenda mbele, akakabiliwa na Sa’d bin Mu’aadh, akamwambia: Ee Sa’d bin Mu’aadh, Jannah! Naapa kwa Rabb wa Al-Ka’bah, naisikia harufu yake chini ya jabali la Uhud. Sa’d akasema: Sina uwezo wa kukueleza namna alivyofanya Anas bin An-Nadhwr yaa Rasula-Allaah. Anas bin Maalik anaelezea: Tukamkuta amepigwa zaidi ya mapigo themanini ya mapanga, au kudungwa mkuki au kurushia mshale. Tulimkuta ameshauliwa na washirikina na wamemkata pua na masikio yake. Basi hakuna aliyeweza kumtambua isipokuwa dada yake, alimtambua kwa ncha ya vidole vyake. Anas bin Maalik anaeleza: Tulikuwa tukiona au tukidhani Aayah hii Suwratu Al-Ahzaab: 23. Ilikuwa imeshuka kwa sababu yake na mfano wake. [Al-Bukhaariy na Muslim]

مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ رِجَالٌ صَدَقُوا مَا عَاهَدُوا اللَّـهَ عَلَيْهِ ۖ

Miongoni mwa Waumini, wapo wanaume wamesadikisha yale waliyomuahidi Allaah. [Al-Ahzaab: 23]  

 

 

Hadiyth – 16

عن أبي مسعود عقبة بن عمرو الأنصاري البدري رضي الله عنه قَالَ: لَمَّا نَزَلَتْ آيةُ الصَّدَقَةِ كُنَّا نُحَامِلُ عَلَى ظُهُورِنَا، فَجَاءَ رَجُلٌ فَتَصَدَّقَ بِشَيءٍ كَثيرٍ، فقالوا: مُراءٍ، وَجَاءَ رَجُلٌ آخَرُ فَتَصَدَّقَ بِصَاعٍ، فقالُوا: إنَّ اللهَ لَغَنيٌّ عَنْ صَاعِ هَذَا! فَنَزَلَتْ: {الَّذِينَ يَلْمِزُونَ الْمُطَّوِّعِينَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ فِي الصَّدَقَاتِ وَالَّذِينَ لا يَجِدُونَ إِلا جُهْدَهُمْ} [التوبة: 79]. مُتَّفَقٌ عَلَي

Kutoka kwa Abuu Mas'uwd ‘Uqbah bin ‘Amruw bin Al-Answaariy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Ilipoteremka Aayah ya swadaqah tulikuwa tukibeba mizigo kwa migongo yetu (pato lake tukitolea swadaqah). Akaja mtu, akatoa swadaqah mali nyingi. Wanafiki wakasema: Anajionyesha. Akaja mtu mwingine akatoa swadaqah kiasi cha pishi. Wanafiki wakasema: Allaah hana haja ya pishi la huyu! Ikashuka Aayah hii katika Suwrat At-Tawbah: 79. [Al-Bukhaariy na Muslim]

الَّذِينَ يَلْمِزُونَ الْمُطَّوِّعِينَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ فِي الصَّدَقَاتِ وَالَّذِينَ لَا يَجِدُونَ إِلَّا جُهْدَهُمْ

Wale wanaowafedhehesha wenye kujitolea kwa hiari katika kutoa swadaqah miongoni mwa Waumini, na (pia) wale wasiopata (kitu cha kutoa) isipokuwa juhudi zao. [At-Tawbah: 79]

 

 

Hadiyth – 17

عن أبي ذر جندب بن جُنادة رضي الله عنه، عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم فيما يروي عن اللهِ تَبَاركَ وتعالى، أنَّهُ قَالَ: ((يَا عِبَادي، إنِّي حَرَّمْتُ الظُلْمَ عَلَى نَفْسي وَجَعَلْتُهُ بيْنَكم مُحَرَّمًا فَلا تَظَالَمُوا.

يَا عِبَادي، كُلُّكُمْ ضَالّ إلا مَنْ هَدَيْتُهُ فَاستَهدُوني أهْدِكُمْ.

يَا عِبَادي، كُلُّكُمْ جَائِعٌ إلا مَنْ أطْعَمْتُهُ فَاستَطعِمُوني أُطْعِمْكُمْ.

يَا عِبَادي، كُلُّكُمْ عَارٍ إلا مَنْ كَسَوْتُهُ فاسْتَكْسُونِي أكْسُكُمْ.

يَا عِبَادي، إنَّكُمْ تُخْطِئُونَ باللَّيلِ وَالنَّهارِ وَأَنَا أغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا، فَاسْتَغْفِرُوني أغْفِرْ لَكُمْ.

يَا عِبَادي، إنَّكُمْ لَنْ تَبْلُغوا ضُرِّي فَتَضُرُّوني، وَلَنْ تَبْلُغُوا نَفعِي فَتَنْفَعُوني.

يَا عِبَادي، لَوْ أنَّ أوَّلَكُمْ وَآخِرَكُمْ وَإِنْسَكُمْ وَجنَّكُمْ كَانُوا عَلَى أتْقَى قَلْبِ رَجُلٍ وَاحِدٍ مِنْكُمْ مَا زَادَ ذلِكَ في مُلكي شيئًا.

يَا عِبَادي، لَوْ أنَّ أوَّلَكُمْ وَآخِرَكُمْ وَإِنْسَكُمْ وَجنَّكُمْ كَانُوا عَلَى أفْجَرِ قَلْبِ رَجُلٍ وَاحِدٍ مَا نَقَصَ ذلِكَ من مُلكي شيئًا.

يَا عِبَادي، لَوْ أنَّ أوَّلَكُمْ وَآخِرَكُمْ وَإِنْسَكُمْ وَجنَّكُمْ قَامُوا في صَعِيدٍ وَاحِدٍ فَسَألُوني فَأعْطَيتُ كُلَّ إنْسَانٍ مَسْألَتَهُ مَا نَقَصَ ذلِكَ مِمَّا عِنْدِي إلا كما يَنْقصُ المِخْيَطُ إِذَا أُدْخِلَ البَحْرَ.

يَا عِبَادي، إِنَّمَا هِيَ أعْمَالُكُمْ أُحْصِيهَا لَكُمْ ثُمَّ أوَفِّيكُمْ إِيَّاهَا، فَمَنْ وَجَدَ خَيرًا فَلْيَحْمَدِ الله وَمَنْ وَجَدَ غَيْرَ ذلِكَ فَلا يَلُومَنَّ إلا نَفْسَهُ)).

قَالَ سعيد: كَانَ أَبُو إدريس إِذَا حَدَّثَ بهذا الحديث جَثا عَلَى رُكبتيه. رواه مسلم

Abuu Dharr, Jundub bin Junaadah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amepokea kutoka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika aliyopokea kutoka kwa Rabb wake (Ta’aalaa) Anasema: “Enyi waja Wangu, hakika Nimeharamisha dhulma, na Nimeijaalia ni haramu miongoni mwenu; kwa hivyo msidhulumiane. Enyi waja Wangu, nyote mmepotea isipokuwa Niliyemuongoza, kwa hivyo Niombeni uongofu Nami Nitawaongoa. Enyi waja Wangu, nyote mna njaa isipokuwa niliyemlisha, kwa hivyo niombeni chakula Nami Nitawalisha. Enyi waja Wangu, nyote mpo uchi isipokuwa Niliyemvisha, kwa hivyo niombeni Niwavishe, Nami Nitawavisha. Enyi waja Wangu, nyinyi mnakosea usiku na mchana, Nami Naghufuria dhambi zote; kwa hivyo niombeni maghfirah Nami Nitawaghufuria. Enyi waja Wangu, nyinyi hamuwezi kunidhuru wala hamuwezi kuninufaisha. Enyi waja Wangu, lau wa mwanzo wenu na wa mwisho wenu, wana Aadam wenu na majini wenu wangalikuwa sawa na moyo wa mchaji Allaah mno miongoni mwenu, basi hilo lisingalipunguza chochote katika Ufalme Wangu. Enyi waja Wangu, lau wa mwanzo wenu na wa mwisho wenu, wana Aadam wenu na majini wenu wangalikuwa sawa na moyo wa mtu muovu mno miongoni mwenu, basi hilo lisingalipunguza chochote katika Ufalme Wangu. Enyi waja Wangu, lau wa mwanzo wenu na wa mwisho wenu, wana Aadam wenu na majini wenu wangesimama katika uwanja mmoja, wakaniomba; Nami Nikampa kila mmoja ombi lake, isingalipungua chochote katika Nilichowapa isipokuwa ni kama vile sindano iliyochovywa baharini inavyopunguza maji. Enyi waja Wangu, hakika Nimezidhibiti ‘amali zenu, kisha Nitawalipa; atakayekuta khayr amuhimidi Allaah, na atakayekuta kinyume chake basi asilaumu isipokuwa ailaumu nafsi yake.” Sa’d (ambaye ni mpokezi wa Hadiyth hii) amesema: Abuu Idriys alikuwa, anapohadithia Hadiyth hii, akikaa kwa kupiga magoti. [Muslim]

 

 

Share