017-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-MUUMIN

 

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

الْمُؤمِن

AL-MUUMIN

 

 

 

 

Al-Muumin: Mwenye Kusadikisha Ahadi, Mwenye Kuaminisha, Mwenye kuweka amani na usalama.

 

Jina hili Tukufu limetajwa mara moja katika Qur-aan:

اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ  

Ndiye Allaah Ambaye hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye, Mfalme, Mtakatifu Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye kusalimisha, Amesalimika na kasoro zote, Mwenye kusadikisha ahadi, Mwenye kuaminisha,  [Al-Hashr 59: 23]

 

Maana za Jina hili Tukufu zimetumika kama zilivyokuja katika Aayah zifuatazo:

 

Maana ya kusadikisha na kuaminisha (amani):

Allaah Anasema kuhusu kisa cha nduguze Yuwsuf kwa baba yao:

قَالُوا يَا أَبَانَا إِنَّا ذَهَبْنَا نَسْتَبِقُ وَتَرَكْنَا يُوسُفَ عِندَ مَتَاعِنَا فَأَكَلَهُ الذِّئْبُ ۖ وَمَا أَنتَ بِمُؤْمِنٍ لَّنَا وَلَوْ كُنَّا صَادِقِينَ﴿١٧﴾

Wakasema: “Ee baba yetu! Hakika sisi tulikwenda tukishindana mbio na tulimwacha Yuwsuf kwenye vitu vyetu; basi mbwa mwitu akamla. Nawe hutotuamini japo tukiwa ni wakweli.” [Yuwsuf 12: 17]

 

Maana ya amani na salama: Ni kinyume na  khofu na kuogopa [Mu’ujam Maqayiys Al-Lughah (1/133) na Tafsiyr Asmaai Allaah (Uk 31)].

Allaah Ta’ala Anasema:

الَّذِي أَطْعَمَهُم مِّن جُوعٍ وَآمَنَهُم مِّنْ خَوْفٍ ﴿٤﴾

Ambaye Anawalisha kuwaokoa na njaa, na Akawapa amani kutokana na khofu. [Qurayish 106:4]

 

Jina hili Tukufu lina maana nyingi za ukamilifu na Utukufu:

 

1. Allaah (‘Azza wa Jalla) Ambaye Amewaaminisha (Amewapa amani) watu na dhulma (Hatowadhulumu). Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ النَّاسَ شَيْئًا وَلَـٰكِنَّ النَّاسَ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿٤٤﴾

Hakika Allaah Hadhulumu watu chochote, lakini watu nafsi zao wenyewe   ni wenye kujidhulumu. [Yuwnus 10:44]

 

Na Atawaaminisha wanaostahiki kuaminishwa na dhulma Siku ya Qiyaamah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

فَالْيَوْمَ لَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا وَلَا تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٥٤﴾

Basi leo nafsi yoyote haitodhulumiwa kitu chochote, na wala hamtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyatenda. [Yaasiyn 36: 54]

 

2. Yeye Allaah (‘Azza wa Jalla) Ambaye Anasadikisha ahadi Zake kwa waja Wake. Kila Anachowabashiria katika mambo ya ghayb kwa njia ya Wahy. Ahadi za mazuri na maonyo Anayowaonya, hapa duniani na  huko Aakhirah:  

a. Anawasadikisha waja Wake Waumini kwa iymaan zao kwa kile Alichowaahidi katika thawabu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

جَزَاؤُهُمْ عِندَ رَبِّهِمْ جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًاۖ

Jazaa yao iko kwa Rabb wao; Jannaat za milele zipitazo chini yake mito ni wenye kudumu humo abadi.  [Al-Bayyinah 98: 8]

 

b. Anawasadikisha makafiri katika Alichowaahidi ya adhabu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَعَدَ اللَّـهُ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْكُفَّارَ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ هِيَ حَسْبُهُمْ ۚ وَلَعَنَهُمُ اللَّـهُ ۖ وَلَهُمْ عَذَابٌ مُّقِيمٌ﴿٦٨﴾

Allaah Amewaahidi wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na makafiri moto wa Jahannam, ni wenye kudumu humo; unawatosheleza (kuwaadhibu vilivyo)! Na Allaah Amewalaani, na watapata adhabu ya kudumu. [At-Tawbah 9: 68]

 

3. Yeye Allaah (‘Azza wa Jalla) Anawaaminisha waliomuamini ambao wanampwekesha, kwamba watakuwa katika amani na hawatopata adhabu Zake kwa kuwa wamejiepusha na dhulma ya kumshirikisha.

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٨٢﴾

Wale walioamini na hawakuchanganya iymaan zao na dhulma; hao ndio watakaopata amani nao ndio walioongoka. [Al-An’aam 6: 82]

 

4. Wanaopewa amani zaidi na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni waja wema. Huwapa tumaini katika nyoyo zao hapa duniani na Siku ya mwisho.

 

-Duniani:

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا ۚ  

Allaah Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema kwamba bila shaka Atawafanya makhalifa katika ardhi kama Alivyowafanya makhalifa wale waliokuwa kabla yao, na bila shaka Atawamakinishia Dini yao Aliyowaridhia, na bila shaka Atawabadilishia amani badala ya khofu yao... [An-Nuwr 24: 55]

 

Na katika jihaad na katika mitihani, zitateremka sababu za kuwapa amani. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

إِذْ يُغَشِّيكُمُ النُّعَاسَ أَمَنَةً مِّنْهُ  

(Kumbukeni) Pale Alipokufunikeni kwa usingizi (kuwa ni) amani kutoka Kwake… [Al-Anfaal 8: 11]

 

Na Akawatia utulivu nyoyo za Waumini:

هُوَ الَّذِي أَنزَلَ السَّكِينَةَ فِي قُلُوبِ الْمُؤْمِنِينَ لِيَزْدَادُوا إِيمَانًا مَّعَ إِيمَانِهِمْ ۗ  

Yeye Ndiye Aliyeteremsha utulivu katika nyoyo za Waumini ili Awazidishie iymaan pamoja na iymaan zao.  [Al-Fat-h]

 

Na Akawapa Rusuli Wake ushindi dhidi ya maadui Zake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

ثُمَّ صَدَقْنَاهُمُ الْوَعْدَ فَأَنجَيْنَاهُمْ وَمَن نَّشَاءُ وَأَهْلَكْنَا الْمُسْرِفِينَ ﴿٩﴾

Kisha Tukawasadikishia ahadi Tukawaokoa wao na wale Tuliowataka; na Tukaangamiza wapindukiaji mipaka. [Al-Anbiyaa 21;9]

 

Na Anasema tena (Subahaanu wa Ta’aalaa):

إِذْ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى الْمَلَائِكَةِ أَنِّي مَعَكُمْ فَثَبِّتُوا الَّذِينَ آمَنُوا ۚ  

(Kumbuka) Pale Rabb wako Alipowatia ilhamu Malaika (kuwaambia): “Hakika Mimi Niko pamoja nanyi; basi wathibitisheni wale walioamini."  [Al-Anfaal 8:12]

 

-Wakati wa mauti:

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anawaaminisha Waumini pale Malakul-Mawt anapoteremka kuwatoa roho zao. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ ﴿٣٠﴾

Hakika wale waliosema: “Rabb wetu ni Allaah.” Kisha wakathibitika imara; Malaika huwateremkia: (kuwaambia): “Msikhofu, na wala msihuzunike, na pokeeni bishara njema ya Jannah ambayo mlikuwa mkiahidiwa.”

نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ ﴿٣١﴾

“Sisi ni rafiki zenu walinzi katika uhai wa dunia na katika Aakhirah. Na mtapata humo yale yanayotamani nafsi zenu, na mtapata humo yale mtakayoomba.

نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ ﴿٣٢﴾

“Ni mapokezi ya takrima kutoka kwa Mwenye kughufuria, Mwenye kurehemu.” [Fusw-Swilat 41;30]

 

-Katika Al-Barzakh (Maisha baina ya kufariki mpaka kufufuliwa)

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anawaaminsha waja Wake Waumini wanaojitolea katika jihaad, kwa kuwahifadhi na  fitna za kaburi:

عن فَضَالَةَ بْنُ عُبَيْدٍ رضي الله عنه عَنْ رَسُولِ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنَّهُ قَالَ: ((كُلُّ مَيِّتٍ يُخْتَمُ عَلَى عَمَلِهِ، إِلاَّ الَّذِي مَاتَ مُرَابِطًا فِي سَبِيلِ اللهِ، فَإِنَّهُ يُنْمَى لَهُ عَمَلُهُ إِلَى يَوْمِ القِيَامَةِ، وَيَأْمَنُ مِنْ فِتْنَةِ القَبْرِ))

Imepokelewa kutoka kwa Fadhwaalah bin ‘Ubayd  (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((‘Amali za kila anayefariki zinamalizika isipokuwa ambaye amefariki akiwa analinda mipaka ya adui katika njia ya Allaah, kwani yeye huzidishiwa ‘amali zake mpaka siku ya Qiyaamah na huaminishwa na fitna za kaburi)) [At-Tirmidhiy na amesema ni Hadiyth Hasan Swahiyh na ameisahihisha Al-Albaaniy: Swahiyh At-Tirmidhiy  (1621), Swahiyh Al-Jaami’ (4562)]

 

-Aakhirah:

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anawaaminisha Waumini katika mfazaiko mkubwa ya Siku ya Qiyaamah. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

إِنَّ الَّذِينَ سَبَقَتْ لَهُم مِّنَّا الْحُسْنَىٰ أُولَـٰئِكَ عَنْهَا مُبْعَدُونَ ﴿١٠١﴾

Hakika wale ambao umewatangulia wema Wetu, hao watabaidishwa nao (moto).

 

لَا يَسْمَعُونَ حَسِيسَهَا ۖ وَهُمْ فِي مَا اشْتَهَتْ أَنفُسُهُمْ خَالِدُونَ ﴿١٠٢﴾

Hawatosikia mvumo wake. Nao watadumu katika ambayo zimetamani  nafsi zao.

 

لَا يَحْزُنُهُمُ الْفَزَعُ الْأَكْبَرُ وَتَتَلَقَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ هَـٰذَا يَوْمُكُمُ الَّذِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ ﴿١٠٣﴾

Haitowahuzunisha mfazaiko mkubwa kabisa; na Malaika watawapokea (wakiwaambia): “Hii ni ile Siku yenu mliyokuwa mkiahidiwa.” [Al-Anbiyaa 21; 101-103]

 

Na Anawaaminisha na adhabu za Jahannam:

أَفَمَن يُلْقَىٰ فِي النَّارِ خَيْرٌ أَم مَّن يَأْتِي آمِنًا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ

Hakika wale wanaozipotosha Aayaat Zetu hawawezi kujificha kwetu. Je, basi yule atakayetupwa katika moto ni bora au yule atakayekuja akiwa katika amani Siku ya Qiyaamah? [Fusw-swilat 41: 40]

 

-Jannah:

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anawasadikisha ahadi Yake na Anawaaminisha katika maisha ya furaha za milele: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي صَدَقَنَا وَعْدَهُ وَأَوْرَثَنَا الْأَرْضَ نَتَبَوَّأُ مِنَ الْجَنَّةِ حَيْثُ نَشَاءُ ۖ فَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ﴿٧٤﴾

“AlhamduliLLaahi, Himidi Anastahiki Allaah Ambaye Ametuhakikishia kweli ahadi Yake, na Ameturithisha ardhi tunakaa popote katika Jannah tutakapo.” Basi uzuri ulioje ujira wa watendao.  [Az-Zumar 39: 74]

 

 

Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah: Al-Muumin:

 

1. Muumini anapaswa kuzingatia na kufahamu maana ya Al-Muumin na makusudio yake. Kisha atende kwa mujibu wake. Na asiwe na shaka kuamini ahadi za Allaah (Ta'aalaa) na kuaminisha Kwake na kila khofu. Kwa hiyo, marejeo yake yote katika hali ya khofu na kupungukiwa iymaan, yawe ni kwa Rabb wake (‘Azza wa Jalla):

 

2. Muumini anapaswa kuwaaminisha Waumini wenzake kutokana na shari za kila aina. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

((المؤمنُ مَنْ أَمِنَهُ الناسُ، والمسلمُ مَنْ سَلِمَ المسلمُونَ من لسانِهِ ويَدِه، والمُهاجِرُ مَنْ هجرَ السُّوءَ، والذي نَفسي بيدِهِ لا يدخلُ الجنةَ عَبْدٌ لا يَأْمَنُ جارُهُ بَوَائِقَهُ))

Muumini ni yule anayeaminisha watu. Na Muislamu ni ambaye anayewaekea amani Waislamu kwa ulimi wake na mkono wake, na   Muhaajir ni ambaye anahama maovu. Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake., haingi Jannah mja ambaye jirani yake hana amani kwa uovu wake)) [Hadiyth ya Anas bin Maalik - Swahiyh At-Targhiyb (2555)]

 

Riwaaya nyingine:

 

((Je, niwajulisheni ni nani Muumini! Ni Yule ambaye anawaaminisha watu katika mali zao na nafsi zao, na Muislamu ni Yule mwenye kuwasalimisha Waislamu kutokana na ulimi wake na mkono wake)) [Swahiyh Ibn Maajah (3934), Swahiyh An-Nasaaiy (4622)]

 

Mifano ya shari za ulimi ni: ghiybah (kusengenya), An-Namiymah (kufitinisha), kuwatusi watu, kukashifu, kukaripia n.k.

 

Mifano ya shari za mikono ni: kuwaumiza watu, kuwaibia au kuwapunjia mali zao, kushika ya haraam, n.k.

 

3. Muumini anapaswa asadikishe katika kauli zake na ‘amali zake. Awe mkweli daima katika kila hali hadi aandikiwe na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuwa ni mkweli na mwenye kusadikisha.  Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((عَلَيْكُمْ بِالصِّدْقِ فَإِنَّ الصِّدْقَ يَهْدِي إِلَى الْبِرِّ وَإِنَّ الْبِرَّ يَهْدِي إِلَى الْجَنَّةِ وَمَا يَزَالُ الرَّجُلُ يَصْدُقُ وَيَتَحَرَّى الصِّدْقَ حَتَّى يُكْتَبَ عِنْدَ اللَّهِ صِدِّيقًا))

((Ni juu yenu kuwa wakweli, kwani ukweli unapeleka kwenye wema, na wema unapeleka kwenye Jannah. Mtu huendelea kuwa mkweli  na kujitahidi katika ukweli mpaka huandikiwa mbele ya Allaah kuwa ni mkweli….)) [Muslim Kitaab Al-Birr wasw-Swillah Wal-Adaab]

 

4. Muumini atende 'amali njema na aamini yaliyoahidiwa Siku ya Qiyaamah yaliyo mazuri huko Jannah na aamini ambayo ya kutishiwa na adhabu zake na mifazaiko ya Siku hiyo. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

مَن جَاءَ بِالْحَسَنَةِ فَلَهُ خَيْرٌ مِّنْهَا وَهُم مِّن فَزَعٍ يَوْمَئِذٍ آمِنُونَ ﴿٨٩﴾ ﴾

Atakayekuja na jema, basi atapata bora zaidi kuliko hilo; nao watakuwa katika amani na mafazaiko ya Siku hiyo. [An-Naml 27: 89]

 

5. Aminika kwa watu, wanapokupa amana zao uzitunze, wanapozitaka amana zao uwakabidhi. Tunza siri za watu. Mwili wako pia ni amana, basi utunze na uhifadhi na maasi.

 

6. Muombe Al-Muumin:

 

a. Akuthibitishe katika iymaan; uwe katika hali na sifa hiyo mpaka yatakapokufikia mauti.

 

b. Unapokuwa na khofu, muelekee Al-Muumin umuombe amani.

 

c. Akujaalie uwe mkweli kwa watu, uwe mwenye kuaminisha wenzako na shari.

 

d. Akuhifadhi shari ya viungo vyako kama alivyokuwa akiomba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

أللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ سَمْعِي وَمِنْ شَرِّ بَصَرِي وَمِنْ شَرِّ لِسَانِي وَمِنْ شَرِّ قَلْبِي وَمِنْ شَرِّ مَنِيِّي   

Allaahumma inniy a’uwdhu bika min sharri sam-’iy wamin sharri baswariy, wamin sharri lisaaniy wamin sharri qalbiy, wamin sharri maniyyi

 

Ee Allaah, hakika mimi najikinga Kwako shari ya kusikia kwangu [masikio yangu], na shari ya kuona kwangu [macho yangu], na shari ya ulimi wangu, na shari ya moyo wangu, na shari ya manii yangu. [Abuu Daawuwd , At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy – Taz. Swahiyh At-Tirmidhiy (3/166) na Swahiyh An-Nasaaiy (3/1108)]

 

7. Mdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa wingi pale iymaan yako inapopungua, pale unapokosa utulivu, unapokosa raha, unapokuwa katika dhiki kwani kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kunatuliza nyoyo na unabakia kuwa katika amani. Na hii ni mojawapo ya sifa ya Muumini!  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

الَّذِينَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِكْرِ اللَّـهِ ۗ أَلَا بِذِكْرِ اللَّـهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ ﴿٢٨﴾

Wale walioamini na zikatua nyoyo zao kwa kumdhukuru Allaah. Tanabahi!  Kwa kumdhukuru Allaah nyoyo hutulia! [Ar-Ra’d 13: 28]

 

 

 

 

Share