018-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-MUHAYMIN

 

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

الْمُهَيْمِن

AL-MUHAYMIN

 

 

 

 

Al-Muhaymin: Mwenye kudhibiti, kushuhudia, kuchunga na kuhifadhi, Mwenye kudabiri mambo.

 

Jina hili Tukufu limetajwa mara moja katika Qur-aan Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

هُوَ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْمَلِكُ الْقُدُّوسُ السَّلَامُ الْمُؤْمِنُ الْمُهَيْمِنُ ا

Yeye Ndiye Allaah Ambaye hakuna Muabudiwa wa haki ila Yeye, Mfalme, Mtakatifu Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye kusalimisha, Amesalimika na kasoro zote, Mwenye kusadikisha ahadi, Mwenye kuaminisha, Mwenye kutawalia, kuchunga na kuhifadhi [Al-Hashr 59: 23]

 

Kisha sifa hiyo Akaihusisha na Qur-aan kuwa ni Muhaymin kwa maana ni Kitabu kinachodhibiti vitabu vyote vinginevyo vya mbinguni na inachunga na inahifadhi upotofu wowote ule kama potofu zilizopachikwa katika vitabu vya mbinguni. Na hata yeyote anayedai kama wanavyodai baadhi ya watu kutunga Qur-aan au kuipotosha basi Qur-aan hii Adhimu inadhibiti na kubatilisha hizo zinazotungwa. Na Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ الْكِتَابِ وَمُهَيْمِنًا عَلَيْهِ ۖ   

Na Tumekuteremshia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Kitabu kwa haki kinachosadikisha Vitabu vilivyokuwa kabla yake na chenye kudhibiti, kushuhudia na kuhukumu juu yake (hivo Vitabu).  [Al-Maaidah 5: 48]

 

Hivyo basi, Allaah (‘Azza wa Jalla) Ndiye Al-Muhaymin wa kila kitu:

Allaah (‘Azza wa Jalla) Mwenye kushuhudia matendo ya waja Wake, Mwenye kuwachunga na kuyatazama mambo yao; katika kauli zao, matendo yao wala hakipotei katika matendo yao chochote. Mwenye kuangalia mambo yao ya ndani yaliyojificha na yaliyo ndani ya nyoyo zao, kila kitu kimeenea katika ujuzi wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

وَمَا تَكُونُ فِي شَأْنٍ وَمَا تَتْلُو مِنْهُ مِن قُرْآنٍ وَلَا تَعْمَلُونَ مِنْ عَمَلٍ إِلَّا كُنَّا عَلَيْكُمْ شُهُودًا إِذْ تُفِيضُونَ فِيهِ ۚ وَمَا يَعْزُبُ عَن رَّبِّكَ مِن مِّثْقَالِ ذَرَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي السَّمَاءِ وَلَا أَصْغَرَ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْبَرَ إِلَّا فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ﴿٦١﴾

61. Na hushughuliki katika jambo lolote, na wala husomi humo katika Qur-aan, na wala hamtendi ‘amali yoyote isipokuwa Tunakuwa Mashahidi juu yenu mnaposhughulika nayo. Na hakifichiki kwa Rabb wako hata cha uzito wa chembe (au sisimizi) katika ardhi wala mbinguni na wala kidogo kuliko hicho na wala kikubwa zaidi ya hicho isipokuwa kimo katika Kitabu kilicho bayana. [Yuwnus 10: 61]

 

Allaah (‘Azza wa Jalla)  Ndiye  Anayewachunga waja Wake, Anayewahifadhi na kuwalinda Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

لَهُ مُعَقِّبَاتٌ مِّن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ يَحْفَظُونَهُ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ ۗ  

Ana Malaika wanaofuatana kwa zamu mbele yake na nyuma yake wanamhifadhi kwa amri ya Allaah.  [Ar-Ra’d 13: 11]

 

Allaah (‘Azza wa Jalla) Mwenye kufanya islahi ya hali zao, mambo yao, mwenye kutawalia wao kwa uwezo Wake, Naye istawaa juu ya ‘Arshi Yake Adhimu.

 

Imaam As-Sa’dy (Rahimahu Allaah) amesema: “Al-Muhaymin ni Ambaye Anayeangalia mambo yaliyojificha kwa kuwa Kwake Yeye Mjuzi. Yeye Anajua siri zako na unayoyadhihirisha. Anajua yaliyo na maslahi nawe na ambayo yenye kukufisidi kama Alivyosema:

وَاللَّـهُ يَعْلَمُ الْمُفْسِدَ مِنَ الْمُصْلِحِ ۚ

 Na Allaah Anamjua fisadi na mtengenezaji. [Al-Baqarah 2: 220]

 

Hivyo basi Yeye Huangalia mambo yaliyojificha na ambayo vifua vinayaficha. (kama Anavyosema Allaah):

يَوْمَ تُبْلَى السَّرَائِرُ ﴿٩﴾

Siku siri zitakapopekuliwa. [Atw-Twaariq 86:9]

 

Allaah (‘Azza wa Jalla) Mwenye kusadikisha, Ambaye Anawasadikisha Manabii Wake kwa uchaguzi wa Rabb wao Adhimu, kwa kuwa wao ni wakweli, na kilichodhihiri katika miujiza juu ya mikono yao. [Jaami’ Al-Bayaan (28/36) Tafsiyr Ibn Kathiyr (8/105) Fat-hul Baariy (6/366), Tafsiyr As-Sa’dy (5/488), Al-Minhaaj (1/202) Ar-Raaziy (202) Fat-hur-Rahiym Al-Malik Al-'Alaam...  (21-22)]     

 

 

 

Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Muhaymin:

 

1-Tahadhari Allaah Anakuchunga na Anashuhudia

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ﴿٦﴾

...na Allaah ni Shahidi juu ya kila kitu. [Al-Mujaadilah 58: 6]

 

Na Anasema:

وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴿٨٥﴾

...na Allaah si Mwenye kughafilika kuhusu myatendayo. [Al-Baqarah 2: 85]

 

Kuwa na khofu daima kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anashuhudia matendo yetu katika hali zote kwani Yeye ni Mwenye kushuhudia ya siri na dhahiri duniani na Aakhirah. Yampasa Muumini kuwa na hisia katika hilo, katika utawala wake binafsi, kwa familia yake, katika kuchunga 'amali zake, katika majukumu yake na kutambua kwamba atakuja kusimamishwa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuulizwa. 

Hadiyth ifuatayo ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inathibitisha hayo:

عَبْد اللَّهِ بْنِ عُمَرَ يَقُولُ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((كُلُّكُمْ رَاعٍ وَكُلُّكُمْ مَسْؤول عَنْ رَعِيَّتِهِ، الإِمَامُ رَاعٍ وَمَسْؤولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ، وَالرَّجُلُ رَاعٍ فِي أَهْلِهِ وَهُوَ مَسْؤولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ، وَالْمَرْأَةُ رَاعِيَةٌ فِي بَيْتِ زَوْجِهَا وَمَسْؤولَةٌ عَنْ رَعِيَّتِهَا، وَالْخَادِمُ رَاعٍ فِي مَالِ سَيِّدِهِ ومَسْؤولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ)) قَالَ: وَحَسِبْتُ أَنْ قَدْ قَالَ((وَالرَّجُلُ رَاعٍ فِي مَالِ أَبِيهِ وَمَسْؤولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ- وَكُلُّكُمْ رَاعٍ وَمَسْؤولٌ عَنْ رَعِيَّتِهِ)).

((Nyinyi nyote ni wachunga na kila mmoja ataulizwa alichokichunga, kiongozi wa watu ni mchunga na ataulizwa kwa alichokichunga, na mwanamme ni mchunga wa familia yake na ataulizwa kwa alichokichunga, mwanamke ni mchunga wa nyumba ya mume wake na watoto wake naye ataulizwa alichokichunga, na mtumwa ni mchunga wa mali ya bwana wake naye ataulizwa kuhusu uchungaji wake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

2. Soma na ifanyie kazi Qur-aan kwa kuwa ni Muhaymin

Qur-aan itakuja kushuhudia ima juu yako kwa kuisoma na kufanya matendo mema au dhidi yako kwa kufanya matendo mabaya.

عَنْ أَبِى مَالِكٍ الأَشْعَرِىِّ  رضي الله عنه  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ  صلى الله عليه وسلم: ((الْقُرْآنُ حُجَّةٌ لَكَ أَوْ عَلَيْكَ)) رواه مسلم

Imepokelewa kutoka kutoka kwa Abuu Maalik Al-Ash’ariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Qur-aan itakuwa ni hoja kwako au dhidi yako)) [Muslim]

 

Kwa hiyo, inakupasa uhalalishe yale ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameyahalalisha na uharamishe yale ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameyaharamisha na ubakie katika mipaka ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

3. Endesha utawala wako kwa kufauta shariy’ah za Qur-aan

Qur-aan ni Muhaymin kwa hiyo mwenye utawala wa aina yoyote ule atumie shariy’ah za Qur-aan kuhukumu baina ya walio katika ulinzi wake katika kesi zao, kupatansisha magomvi yao, kwani baada ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kutaja sifa ya Qur-aan kuwa ni Muhaymin, Akaamuru kuwa Qur-aan Aliyoiteremsha, itumiliwe kwa ajili ya kuhukumu baina ya watu kama Anavyosema:

وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ مُصَدِّقًا لِّمَا بَيْنَ يَدَيْهِ مِنَ الْكِتَابِ وَمُهَيْمِنًا عَلَيْهِ ۖ فَاحْكُم بَيْنَهُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ ۖ  

  Na Tumekuteremshia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Kitabu kwa haki kinachosadikisha Vitabu vilivyokuwa kabla yake na chenye kudhibiti, kushuhudia na kuhukumu juu yake (hivyo Vitabu). Basi hukumu baina yao kwa yale Aliyoyateremsha Allaah.  [Al-Maaidah 5: 48]

 

 

4. Chunga moyo wako kwa kuwa ni kiungo kinachodhibiti na kuchunga viungo vinginevyo

Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

عَن النُّعْمَانَ بْنَ بَشِيرٍ (رضي الله عنهما) قَال: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ:  ((الْحَلاَلُ بَيِّنٌ وَالْحَرَامُ بَيِّنٌ، وَبَيْنَهُمَا مُتَشَابِهَاتٌ لاَ يَعْلَمُهَا كَثِيرٌ مِنَ النَّاسِ، فَمَنْ اتَّقَى الشُّبُهَاتِ اسْتَبْرَأَ  لِدِينِهِ وَعِرْضِهِ، وَمَنْ وَقَعَ فِي الشُّبُهَاتِ وَقَعَ فِي الْحَرَامِ، كَالرَّاعِي يَرْعَى حَوْلَ الْحِمَى َيُوشِكُ أَنْ يَرْتَعْ فِيهِ، أَلاَ وَإِنَّ لِكُلِّ مَلِكٍ حِمًى، أَلاَ وَإِنَّ حِمَى اللَّهِ مَحَارِمُهُ، أَلاَ وَإِنَّ فِي الْجَسَدِ مُضْغَةً إِذَا صَلَحَتْ صَلَحَ الْجَسَدُ كُلُّه, وَإِذَا فَسَدَتْ فَسَدَ الْجَسَدُ كُلُّهُ أَلاَ وَهِيَ الْقَلْبُ)) متفق عليه

Imepokelewa kutoka kwa An-Nu’maan bin Bashiyr (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kwamba: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Hakika halali imebainika na haramu imebainika.  Baina ya mawili hayo mna yenye kutia shaka. Wengi miongoni mwa watu hawayajui. Basi atakayejiepusha na yenye kutia shaka, atakuwa amejiepushia shaka katika Dini yake na heshima yake. Na Atakayetumbukia katika yenye kutia shaka, ataingia kwenye haramu. Kama mchunga anayechunga kando ya mipaka, ni haraka kulisha humo [mpaka mwingine wa watu]. Zindukeni!  Kila mfalme ana mipaka. Zindukeni! Kwa yakini mipaka ya Allaah ni haramu Alizoziharamisha. Zindukeni! Kwa yakini katika mwili mna kinofu [cha nyama], kinapokuwa kimesalimika, mwili wote unakuwa umesalimika. Kinapoharibika, mwili wote unaharibika. Zindukeni! Kinofu hicho ni moyo)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

5. Ridhika na Qadhwaa na Qadar: (Yaliyohukumiwa na Yaliyokadiriwa) na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)

 

Kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

  يَعْلَمُ الْمُفْسِدَ مِنَ الْمُصْلِحِ ۚ

Anamjua fisadi na mtengenezaji. [Al-Baqarah 2: 220]

 

 

6. Muombe Al-Muhaymin Akuchunge, Akuhifadhi, Akuendeshee Mambo yako

Unapofikwa na shida, khofu ya uadui na kadhaalika, mambo yako yanapokuwa hayaendi vizuri, maadui na shari zimekuandama, vikwazo vimekuelekea mbele yako, muombe Al-Muhaymin; Atakusaidia, Atakunusuru, Atakulinda, Atakupa tawfiyq, Atakutengeneza mambo yako. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiomba:

يا حَـيُّ يا قَيّـومُ بِـرَحْمَـتِكِ أَسْتَـغـيث، أَصْلِـحْ لي شَـأْنـي كُلَّـه، وَلا تَكِلـني إِلى نَفْـسي طَـرْفَةَ عَـين

Yaa Hayyu Yaa Qayyuwm bi-Rahmatika astaghiythu, Aswlihliy sha-ani kullahu walaa takilniy ilaa nafsiy twarfata ‘aynin

Ee Uliye hai daima, Msimamizi wa kila kitu, kwa Rahmah Zako ninakuomba uniokoe, nitengenezee mambo yangu  yote, wala usiniachie  mambo yangu mwenyewe (pasina kunisaidia) hata kwa muda (mdogo kama muda) wa kupepesa jicho. [Hadiyth ya Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ’anhu) - Abuu Daawuwd (4/3180), At-Tirmidhiy (5/465), Al-Haakim. Taz. Swahiyh At-Targhiyb (1/273), Swahiyh Al-Jaami’ [5820].

 

Share