25-Wewe Pekee Tunakuabudu: Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah: Kutawassal Kwa 'Ahlul-Badr' Watu wa Badr

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada

 

Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah

 

25-Kutawassal Kwa Ahlul-Badr  Watu wa Badr

 

 

 

 Ahlul-Badr -   اهل البدر

 

Baadhi ya watu hutawassal kwa uradi unaojulikana katika jamii kama "albadiri" au "halalbadri" kama wanavyotamka watu wengi wa kawaida.

 

Jina lenyewe la tawassul hiyo laonesha wazi jinsi gani watu hawakufahamu maana yake halisi kama ilivyokusudiwa katika lugha ya Kiarabu kwamba maana yake ni: ‘Ahlul-Badr’ (Watu wa Badr).

 

Hao "Ahlul-Badr" ni Maswahaba waliopigana jihaad katika vita vya Badr Na Badr ni jina la mji ulio kiasi cha kilomita mia na khamsini mbali na mji wa Madiynah ambako Waislamu walipopigana vita vya kwanza na washirikina wa Makkah. Vita hivyo viliongozwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Baadhi ya mapokezi yanaeleza kuwa walikuwa Waislamu mia tatu na kumi na tatu au kumi na nne na riwaya zingine zinasema kuwa walikuwa mia tatu na kumi na saba.

 

Themanini na sita kati yao ni Muhaajiriyn (watu wa Makkah waliohamia Madiynah) na mia mbili thelathini na moja ni watu wa pale pale Madiynah.

 

Juu ya kuwa idadi ya Waislamu ni ndogo kulingana na jeshi la makafiri wa Makkah iliyofika takriban mara sita yao, Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliwajaalia ushindi katika vita hivyo.

 

Baadhi ya Waislamu waliuawa katika vita hivyo wakafa wakiwa ni mashuhadaa.

 

Wazushi wakaandaa katika kijitabu kidogo, majina ya mashuhadaa na kufanya ni uradi wa kutawassal  ili mtu apate kukubaliwa du’aa yake.

 

Wengine hukusudia kwa kupitia du'aa hizo walizotunga, kumuombea laana au maangamizi mtu. Hutajwa majina yao mmoja baada ya mwengine. Na kila mmoja hutajwa kwa kumtambulisha kabila lake au asli ya eneo alilotokea; mfano ni ‘fulani Al-Answaariy’ au ‘fulani Al-Muhaajiriy’ au ‘fulani Al-Khazrajiyy’ au ‘fulani Al-Awsiy’ n.k.

 

‘Ulamaa wa Al-Lajnah Ad-Daaimah wamesema: “Akishafariki mwana Aadam, masikio yake hayafanyi kazi wala hadiriki kusikia sauti za duniani wala kusikia mongezi yao kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

وَمَا أَنتَ بِمُسْمِعٍ مَّن فِي الْقُبُورِ ﴿٢٢﴾

nawe huwezi kuwasikilizisha walioko kaburini. [Faatwir: 22] 

[Fataawaa Al-Lajnah Ad-Daaimah (1/478-479)]

 

 

Na Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Na wanayoyafanya katika kuomba viumbe kama vile Malaika au Manabii na waja wema waliofariki mfano wa du’aa zao kwa Maryam na wengineo na kuwaomba shafaa'ah (uombezi) waliofariki kwa Allaah, hakutumwa Nabiy yeyote kuleta hilo (kufundisha hilo)."  [Al-Jawaab Asw-Swahiyh (5/187)]

 

 

Tawassul  kama hii ni baatwil; haijuzu kabisa kwa sababu ni shirki ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na Rasuli Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wameiharamisha kwa dalili kadhaa zilizokwishatangulia; na  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ مَا يَمْلِكُونَ مِن قِطْمِيرٍ ﴿١٣﴾

Na wale mnaowaomba badala Yake hawamiliki hata kijiwavu cha kokwa ya tende.

 

إِن تَدْعُوهُمْ لَا يَسْمَعُوا دُعَاءَكُمْ وَلَوْ سَمِعُوا مَا اسْتَجَابُوا لَكُمْ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكْفُرُونَ بِشِرْكِكُمْ ۚ وَلَا يُنَبِّئُكَ مِثْلُ خَبِيرٍ ﴿١٤﴾

Mkiwaomba, hawasikii maombi yenu, na hata wakisikia, hawatakuitikieni.  Na Siku ya Qiyaamah watakanusha ushirikina wenu, na wala hakuna atakayekujulisha vilivyo kamaMwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [Faatwir: 13-14]

 

 

 

 

Share