059-Aayah Na Mafunzo: Amri Na Masisitizo Ya Kuwatii Watawala Na Viongozi

 

Aayah Na Mafunzo

An-Nisaa

 

Amri Na Masisitizo Ya Kuwatii Watawala Na Viongozi

 

Alhidaaya.com

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ ۖ فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٥٩﴾

Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Rasuli na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Rasuli mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri zaidi. [An-Nisaa: 59]

 

Mafunzo:

 

Amri Na Masisitizo Ya Kuwatii Watawala Na Viongozi

 

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ameamrisha na kusisitiza katika Hadiyth kadhaa suala la kutii watawala na viongozi; miongoni mwanzo ni: “Muislamu anapaswa kusikia na kutii kwa anayoyapenda na anayoyachukia, madhali hakuamrishwa kuasi. Na pindi akiamrishwa katika maasi, basi hakuna kusikia wala kutii.” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Na amesema pia: “Sikieni na tiini (watawala na viongozi wenu) hata kama ni mtumwa wa Habash ambaye kichwa chake ni kama zabibu.” [Al-Bukhaariy].

 

Amri ya kuwatii kwa wema watawala na viongozi wa mambo ya Waislamu, ni jambo ambalo limenukuliwa na Ijmaa’ juu yake, bali ndiyo ‘Aqiydah iliyokuwa sahihi ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah. Lakini kwa masikitiko makubwa jambo hili wamelipuuza wengi katika Waislamu na wale wasiofahamu mafunzo ya Dini yao. Na matokeo ya kwenda kinyume na jambo hilo na ‘Aqiydah hiyo ni kuleta munkari mkubwa katika Ummah na ufisadi mpana. Kuna wanaofanya maandamano kupinga viongozi, kuna wanaojilipua kwa mabomu na kuua watu, kuna wanaoua watu kwa njia mbali mbali na kadhalika kumwaga damu za wanaadamu bure! Na wametumia njia hiyo maadui wa Uislamu ili kuuchafua Uislamu na kuudidimiza.

 

 

Sababun-Nuzuwl: Aayah hii imeteremka kuhusu ‘Abdullaah Ibn Hudhaafah (رضي الله عنه) pale alipotumwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwenye msafara wa Jihaad. [Amehadithia Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) ameipokea Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Pia Imeteremshwa pale Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alipotuma jeshi chini ya uongozi wa mtu mmoja wa Answaar. Walipoondoka, aliwaghadhibikia kwa sababu fulani akawaambia: Kwani Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hakukuamrisheni mnitii? Wakasema: Ndio! Akasema: Okoteni kuni. Kisha akawasha moto akasema: Nakuamrisheni muingie motoni humu. Wakakaribia watu kuuingia lakini kijana mmoja miongoni mwao akasema: Nyinyi mmekimbia moto kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hivyo msikimbilie mpaka mrudi kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kisha akikuamrisheni kuingia hapo muuingie. Waliporudi kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) wakamwelezea yaliyojiri, kisha yeye akasema: “Mngeliuingia, msingetoka kamwe humo. Hakika utiifu ni katika mema.” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

 

 

Share