103-Aayah Na Mafunzo: Amri Ya Kuswali Kwa Wakati Wake Na Baadhi Ya Fadhila

 

Aayah Na Mafunzo

An-Nisaa

Amri Ya Kuswali Kwa Wakati Wake Na Baadhi Ya Fadhila

Alhidaaya.com

 

Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

فَإِذَا قَضَيْتُمُ الصَّلَاةَ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِكُمْ ۚ فَإِذَا اطْمَأْنَنتُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ ۚ إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا ﴿١٠٣﴾

Mtakapomaliza Swalaah, basi mdhukuruni Allaah mkiwa wima, mmeketi, au mmejinyoosha. Na mtakapopata utulivu, basi simamisheni Swalaah (kama desturi), hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekewa nyakati maalumu. (4:103).

 

Mafunzo:

 

Maamrisho ya kutimiza Swalaah kwa wakati wake, na makemeo ya kuipuuza yamesisitizwa katika Qur-aan ana Sunnah na miongoni mwa Hadiyth za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ni:

 

عن عَبْدِ اللَّهِ  ابن مسعود قَالَ سَأَلْتُ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم أَىُّ الْعَمَلِ أَحَبُّ إِلَى اللَّهِ قَالَ ‏"‏ الصَّلاَةُ عَلَى وَقْتِهَا ‏"‏‏.‏ قَالَ ثُمَّ أَىُّ قَالَ ‏"‏ ثُمَّ بِرُّ الْوَالِدَيْنِ ‏"‏‏.‏ قَالَ ثُمَّ أَىُّ قَالَ ‏"‏ الْجِهَادُ فِي سَبِيلِ اللَّهِ ‏"‏‏.‏

 

‘Abdullaah bin Mas'uwd  (رضي الله عنه)  amehadithia kwamba: Nilimuuliza Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Ni ‘amali gani inayopendeza kwa Allaah? Akajibu: “Ni kuswali kwa wakati wake.” Nikamuuliza tena: Kisha ni ‘amali gani? Akajibu: “Ni kuwafanyia wema wazazi.” Nikamuuliza tena: Kisha ni ‘amali gani? Akajibu: “Ni kupigana jihaad katika njia ya Allaah.” [Al-Bukhaariy Na Muslim].

 

Amesema pia: “Kitu cha kwanza atakachohesabiwa nacho mja Siku ya Qiyaamah katika ‘amali zake ni Swalaah, ikitengenea atakuwa amefuzu na amefanikiwa, na ikiharibika atakuwa ameshapita patupu na amekhasirika…” [At-Tirmidhy na amesema Hadiyth hii ni Hasan Swahiyh].

 

'Abdullaah bin 'Amru bin Al-‘Aasw (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)   siku moja alitaja kuhusu Swalaah akasema: “Atakayeihifadhi atakuwa na Nuru na burhaan, na ataokoka Siku ya Qiyaamah, na asiyeihifadhi hatokuwa na Nuru wala burhaan wala hatookoka na Siku ya Qiyaamah atakuwa pamoja na Qaaruwn, Fir'awn, Haamaan na ‘Ubayy bin Khalaf)) [Musnad Ahmad ikiwa na isnaad Swahiyh na amesema Al-Albaaniy Isnaad yake Hasan (Ath-Thamar Al-Mustatwaab (uk. 53)].

 

Buraydah bin Al-Haswiyb  (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  akisema: “Mafungamano baina yetu na baina yao (wasio Waislamu) ni Swalaah, atakayeiacha atakuwa amekufuru.” [Ahmad, Abuu Daawuwd, An-Nasaaiy na Ibn Maajah].

 

Imaam ibn Baaz (رحمه الله) amesema: “Yeyote atakayeweka kengele ya saa makusudi imuamshe baada ya kutoka jua akakosa Swalaah ya Alfajiri, basi mtu huyo amepuuza kuswali kwa wakati wake na hivyo ni kufru kubwa kama walivyokubaliana ‘Ulamaa wengi kwa sababu amekusudia kuswali baada ya jua kutoka. Ni sawa na mtu ambaye anachelewesha kuswali Alfajiri akaiswali karibu na Adhuhuri. [Fataawa Ibn Baaz, Kitaab As-Swalaah 10/374].

 

Kwa faida ziyada bonyeza kiungo kifuatacho:

 

Swalaah - Kuwajibika Na Fadhila Zake

 

 

 

 

 

 

Share