135-Aayah Na Mafunzo: Amrisho La Kutoa Ushahidi Bila Kupendelea Jamaa Tajiri Au Maskini

Aayah Na Mafunzo

An-Nisaa

Amrisho La Kutoa Ushahidi Bila Kupendelea Jamaa Tajiri Au Maskini  

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاءَ لِلَّـهِ وَلَوْ عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَوِ الْوَالِدَيْنِ وَالْأَقْرَبِينَ ۚ إِن يَكُنْ غَنِيًّا أَوْ فَقِيرًا فَاللَّـهُ أَوْلَىٰ بِهِمَا ۖ فَلَا تَتَّبِعُوا الْهَوَىٰ أَن تَعْدِلُوا ۚ وَإِن تَلْوُوا أَوْ تُعْرِضُوا فَإِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا ﴿١٣٥﴾

135. Enyi walioamini! Kuweni wenye kusimamisha uadilifu mtoapo ushahidi kwa ajili ya Allaah japokuwa ni dhidi ya nafsi zenu au wazazi wawili, au jamaa wa karibu. Akiwa tajiri au maskini Allaah Anawastahikia zaidi. Basi msifuate hawaa mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa au mkikanusha basi hakika Allaah daima kwa myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika.

 

Mafunzo:

 

Amrisho la kusimamia na kutoa ushahidi bila ya kupendelea wenye uhusiano wa damu, wala tajiri wala maskini. Imaam As-Sa’diy katika Tafsiyr yake amesema: Allaah (سبحانه وتعالى) Anaamrisha waja Wake Waumini wawe: “Wenye kusimamisha uadilifu mtoapo ushahidi.” Na Al-Qawwwaam ni neno lenye kuzidisha ile sifa ya usimamizi yaani kuweni katika kila hali zenu wenye kusimamia uadilifu ambao ni uadilifu katika haki za Allaah na haki za waja Wake. Hivyo, uadilifu katika haki ya Allaah ni kutotumia neema zake katika maasi yake, bali atumie kwa utii Wake.  Na Al-Qistw (uadilifu) katika haki za bin-Aadam ni kutimiza haki zote ambazo ziko juu yako kama ambavyo unavyozitaka haki zako (upatiwe au utekelezewe). Utatoa matumizi ya wajibu, (utalipia) madeni, na utaamiliana na watu kama ambavyo unavyopenda waamiliane na wewe, kwa akhlaaq na malipo na mengine yasiyo hayo.

 

 

 

Share