Kisa Cha Nabiy Ibraahiym (عليه السلام) - 1

 

 

 

Kisa Cha Nabii Ibraahiym (‘Alayhis-Salaam) - 1

 

Alhidaaya.com

 

بسم الله الرحمن الرحيم

 الحمد لله رب العالمين والصلاة والسلام على اشرف الانبياء والمرسلين نبينا محمد وعلى اله وصحبه اجمعين و بعد

 

Utangulizi:

 

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alizaliwa Iraq, inavyosemekana Babylonia. Baba yake akiitwa Aazar na kauli nyingine inasema kuwa huyu ni ami yake aliyemlea tokea mdogo baada ya kufa baba yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ni Mjuzi zaid. Na huyu Aazar alikuwa akichonga masanamu.

 

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) ni Khaliylul-Allaah. yaani kipenzi wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amemchagua kumpa Risala Yake na Akamfadhilisha zaidi ya viumbe Vyake vingine. 

 

Alikuwa akiishi na watu waliokuwa wakiabudu sayari (nyota, mwezi, jua na kadhalika), na wengine wakiabudu masanamu na wengine wakiabudu wafalme wao.  Hakuridhika na ibaada hizo zao, bali alihisi kuwa yupo Aliyeanzisha uumbaji wa yote na kwamba Muumba Huyo Ndiye Anayestahiki kuabudiwa. Akawa anawaza na kutafuta uhakika hadi Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamwongoza na kumchagua kumpa Unabii na Urasuli.

 

Akaanza Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kuwalingania watu wake katika Tawhiyd ya Allaah (Kumpwekesha), lakini watu wake hawakumuamini bali walimkanusha na wakajaribu kutaka kumwangamiza kwa kumtia katika moto waliouasha kwa kuni nyingi, lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alimuokoa mbele ya macho yao. Kisha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamjaalia kupata watoto wawili ambao ni Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) na Is-haaq (‘alayhis-salaam) ambao Manabii wote waliobakia, wametokana nao kama ifuatavyo:   

 

Is-haaq (‘alayhis-salaam) alimzaa Ya'quub ambaye ndiye aliyejaaliwa kutoa kizazi cha Manabii wote waliobakia hadi Nabii 'Iysa (‘alayhis-salaam). Baada ya hapo ikapita miaka takriban mia sita bila ya kutokea Nabii yeyote yule mpaka tena akazaliwa Nabii Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ametokana na kizazi cha Nabii Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) aliyeachwa Makkah na baba yake Nabii Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akiwa pamoja na mama yake Haajar. 

 

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) na mwanamwe Ismaa'iyl (‘alayhis-salaam) ndio waliojenga Al-Ka'bah Makkah, mji mtukufu kabisa  ambao  Waislamu wote  wanafika kutimiza Hajj.

 

Fadhila Na Sifa Za Nabii Ibraahiym (‘Alayhis-salaam)

 

Fadhila na Sifa za Nabii Ibraahiym (‘alayhis-salaam) ni nyingi mno kutokana na mafundisho tunayopata katika Qur-aan na Hadiyth, na katika Qur-aan ametajwa mara nyingi katika Suwrah kadhaa na katika Hadiyth mbalimbali. Miongoni mwazo ni zifuatazo:   

 

Miongoni Mwa Fadhila Za Nabii Ibraahiym (عليه السّلام):

 

(i) Allaah (سبحانه وتعالى) Amemteua yeye Nabii Ibraahiym na mwanawe Nabii Ismaa’iyl (عليهما السّلام) waijenge Al-Ka’bah. Kisha Allaah (سبحانه وتعالى) Akamteua Nabii Ibraahiym (عليه السّلام) awatangazie watu kwenda kutekeleza Hajj. Hivyo basi, akawa yeye (عليه السّلام)  na ahli wake ni mwongozo kwa watu katika utekelezaji wa manaasik (ibaada na taratibu) za Hajj na ‘Umrah. Rejea Al-Hajj (22:26-37). Na miongoni mwa manaasik hizo, ni kuswali katika Maqaam Ibraahiym baada ya kutufu Al-Ka’bah. Rejea Al-Baqarah (2:125). Pia, kusai baina ya  Swafaa na Marwah, rejea Al-Baqarah (2:158)  kama ni kigezo cha mkewe Haajar alipokuwa akihangaika kumtafutia maji mwanawe Ismaa’iyl (عليه السّلام). Na huko ndiko palipotokea mbubujiko wa maji ya Zamzam  ambayo watu wanakunywa kwa niya tofauti kama alivyogusia hilo Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Pia kuchinja mnyama baada ya yeye kupewa mtihani au majaribio makubwa, pindi alipoona njozini kuwa anamchinja mwanawe, naye kutokana na utiifu wake, akataka kutekeleza njozi hiyo akiamini kuwa ni Amri ya Allaah (سبحانه وتعالى). Lakini kumbe ilikuwa ni mtihani na jaribio, hivyo akafaulu katika hili, na hapo Allaah (سبحانه وتعالى) Akambadilishia kwa kumteremshia kondoo  kutoka mbinguni ili amchinje badala ya mwanawe.  Rejea Asw-Swaaffaat (37:101-107). Pia kutupia vijiwe Jamaraat ambayo ni katika waajibaat za Hajji na Sunnah zake nyenginezo.

 

(ii) Ni kipenzi cha Allaah. Rejea An-Nisaa (4:125).

 

(iii) Ameitwa Baba wa Manabii:  Kama ilivyokuwa hali ya  Nabii Nuwh (عليه السّلام): Al-‘Ankabuwt (29:27). Na katika Al-Hadiyd (57:26), ametajwa yeye Nabii Ibraahiym (عليه السّلام) pekee kuwa amejaaliwa kuwa na Unabii na kupewa Kitabu.

 

Imaam Ibn Kathiyr amesema kuhusu Aayah ya Suwrah Al-‘Ankabuwt: “Hii ni fadhila na baraka kubwa sana. Sio tu kwamba Allaah Alimfanya (Nabii Ibraahiym) kuwa ni kipenzi Chake na kumfanya Imaam wa watu, bali pia Alijaalia Unabii na Kitabu kuwa katika dhuriya zake. Baada ya zama za Ibraahiym, hapakuwa na Nabii ambaye hakutokana na kizazi chake. Manabii wote wa Wana wa Israaiyl (Ya’quwb) walikuwa katika kizazi chake, kuanzia Ya’quwb bin Is-haaq bin Ibraahiym hadi wa mwisho wao, `Iysa bin Maryam, ambaye alisimama kuwatangazia kaumu yake, bishara ya kuja kwa Nabii Mwarabu, Al-Qurashiy, Al-Haashimiy, Nabii wa mwisho wa Manabii wote, bwana wa wana wa Aadam katika dunia hii na Aakhirah, ambaye Allaah Alimteua kutoka kwa Waarabu safi wa asili  kutoka kwa kizazi  cha Ismaa’iyl bin Ibraahiym (عليهما السلام).  Hakuna Nabii yeyote katika ukoo wa Ismaa’iyl isipokuwa yeye Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم). [Tafsiyr Ibn Kathiyr] 

 

(iv) Ameomba duaa  kizazi chake kitoe Nabii wa mwisho; Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) baada ya kujenga Al-Ka’bah. Rejea (2:129).

 

(v) Ibraahiym (عليه السّلام)  ni Imaam wa Tawhiyd:

 

Allaah (سبحانه وتعالى) Amemfanya kuwa ni Imaam wa watu wa kufuatwa katika Tawhiyd. Rejea Al-Baqarah (2:124). Na pia Ummah umeusiwa kufuata mila yake. Rejea Al-Baqarah (2:135), Aal-‘Imraan (3:95), An-Nisaa (4:125), Al-An’aam (6:161), na An-Nahl (16:123). Na pia, Amewausia wanawe na kizazi chake Uislamu. Rejea Al-Baqarah (2:130-132). Na pia Amefanya neno la Tawhiyd (laa ilaaha illa-Allaah) lenye kubakia katika kizazi chake. Rejea Az-Zukhruf (43:28). Ingawa Rusuli wengineo wote wamekuja pia katika kulingania Tawhiyd, ila Nabii Ibraahiym (عليه السّلام)  amekuwa ni makhsusi kwa Tawhiyd. Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (رحمه الله)  amesema alipoulizwa:

 

Kwa nini Nabii Ibraahiym (عليه السّلام) amehusishwa zaidi na Tawhiyd, ilhali Manabii wote wengineo wamelingania Tawhiyd?

Akajibu:  Manabii wote wamekuja na (kulingania) Tawhiyd. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ ﴿٢٥﴾

“Na Hatukutuma kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Rasuli yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: Hakika hapana mwabudiwa wa haki ila Mimi, basi Niabuduni.” [Al-Anbiyaa (21:25)]

 

Lakini Ibraahiym ni baba wa Waarabu, na baba wa Waisrael, naye amelingania Tawhiyd khalisi, na Mayahudi na Manaswara wamedai kuwa ni wafuasi wake, na Waislamu ndio wafuasi wake. Kwa hiyo yeye (عليه السّلام) akahusishwa kuwa ni baba wa Manabii, na kwamba yeye ndiye mwenye Haniyfiyyah (sifa ya kuelemea haki na kujiweka kando na shirki). Na sisi tumeamrishwa kumfuata, kwa sababu sisi ndio tulio karibu zaidi Ibraahiym kama Anavyosema Allaah (عزّ وجلّ):

 

إِنَّ أَوْلَى النَّاسِ بِإِبْرَاهِيمَ لَلَّذِينَ اتَّبَعُوهُ وَهَـٰذَا النَّبِيُّ وَالَّذِينَ آمَنُوا ۗ وَاللَّـهُ وَلِيُّ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٦٨﴾

“Hakika watu walio karibu zaidi kwa Ibraahiym ni wale waliomfuata na huyu Nabii (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) na wale walioamini. Na Allaah Ni Mlinzi wa Waumini.” [Aal-‘Imraan (3:68)]

 

Na Akasema kuwaradi Mayahudi na Manaswaara:

 

مَا كَانَ إِبْرَاهِيمُ يَهُودِيًّا وَلَا نَصْرَانِيًّا وَلَـٰكِن كَانَ حَنِيفًا مُّسْلِمًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٦٧﴾

“Ibraahiym hakuwa Yahudi wala Naswara, lakini alikuwa mwenye kujiengua na upotofu akaelemea Dini ya haki, Muislamu na hakuwa miongoni mwa washirikina.” [Aal-‘Imraan (3:67)]

 [Liqaa-a Al-Baab Al-Maftuwh Swali namba (7/189).  

 

 

(vi) Anatajwa katika kila Swalaah, kwenye Tashahhud, kwa Swalaah inayojulikana kama Swalaatul-Ibraahiymiyyah.

 

Na fadhila hii tukufu ni kutokana na sababu zilizotangulia kutajwa juu na Imaam Ibn ‘Uthaymiyn.  Pia kutokana na sababu zifuatazo kama walivyosema ‘Ulamaa: Kwamba (عليه السّلام) Ibraahiym  ni babu (kizazi kilichoanzia kwa Ismaaiyl) wa Nabii Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم). 

 

Na ‘Allaamah Badr Ad-Diyn Al-Hanafiy (رحمه الله) ana maelezo mengineyo katika kubainisha sababu ya hili. Amesema: “Ikiwa mtu atauliza: Kwa nini Ibraahiym (عليه السّلام)  ameteuliwa yeye pekee kutajwa katika Swalaah badala ya Manabii wengine (عليهم السّلام)?

 

Nitajibu: Kwa sababu Nabii (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwaona katika usiku wa Mi’iraaj, Manabii na Rusuli wote, na akamtolea Salaam kila Nabii, na hakuna hata mmoja wao aliyesalimia ummah wake isipokuwa Ibraahiym (عليه السّلام) . Hivyo basi, Nabii (صلى الله عليه وآله وسلم) ametuamrisha tumswalie kila mwisho wa Swalaah mpaka Siku ya Qiyaamah, kama malipo ya wema wake. Na imesemwa: Ibraahiym (عليه السّلام)   alipomaliza kuijenga Al-Ka’bah, aliuombea Ummah wa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم)  akisema:  Ee Allaah! Atakayehiji Nyumba hii miongoni mwa Ummah wa Muhammad, basi Mpe amani kutoka kwangu. Pia akawaombea ahli zake na watoto wake kwa duaa hii. Hivyo basi tukaamrishwa tuwakumbuke katika Swalaah kama malipo ya wema wao.” Mwisho. Ufafanuzi wa Sunan Abi Daawuwd cha Al-‘Ayniy (4/260). Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

 

(vii) Kizazi chake kimepewa ufalme mkubwa: An-Nisaa (4:54). 

 

(viii) Nabii (صلى الله عليه وآله وسلم) alimkuta mbingu ya saba  akielemea Bayt Al-Ma’muwr inayozungukwa na Malaika elfu sabiini.  (Haya yapo katika Hadiyth ndefu iliyopokelewa na Imaam Muslim katika Kitaab Al-Iymaan,  na wengineo). 

 

(ix) Alijaaliwa Ar-Rushd (Uongofu) na Allaah (سبحانه وتعالى)  Alimjua vyema: Al-Anbiyaa (21:51).

 

(x) Ni Nabii ambaye amemshabihi Nabii Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم): Hadiyth ya Abu Hurayrah (رضي الله عنه)  [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

(xi) Ni miongoni mwa Rusuli watano wa Ulul-‘Azmi: Al-Ahzaab (33:7).

 

(xii) Amewaombea Waislamu wawe wenye kuelekeza nyoyo zao kuipenda Makkah na Al-Ka’bah. Ibraahiym (14:37).

 

(xiii) Amewaombea duaa kizazi chake wasimamishe Swalaah, na Amewaombea Waumini maghfirah Siku ya Hesabu. Ibraahiym (14:40-41).

 

(xiv) Atakuwa wa kwanza kuvalishwa nguo baada ya kufufuliwa kutokana na vile washirikina katika kaumu yake  walivyomuingiza motoni akiwa  uchi   baada ya kuvunja masanamu yao. Yapo haya kwenye Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما):

 

Nabii (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Enyi watu, hakika mtafufuliwa na Allaah hali ya kuwa hamna viatu, mpo uchi na bila kutahiriwa  (na magovi). ”Kisha akasoma: 

 

كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ ۚ

“Kama Tulivyoanza umbo la awali Tutalirudisha tena.” [Al-Anbiyaa (21:104)]

 

Tanabahini! Hakika mtu wa kwanza atakayevishwa nguo ni Nabii Ibraahiym (عليه السّلام).   [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Na ‘Ulamaa wameeleza pia kuwa sababu ya kutangulizwa Ibraahiym kuvishwa nguo Siku ya Qiyaamah kabla ya wengine ni kuwa hapakuweko miongoni mwa watu wa mwanzo na wa baadae, waliomkhofu zaidi Allaah kuliko yeye. Hivyo basi, nguo zitamharakia ili kumhifadhi, na moyo wake upate kutulia.

 

Na sababu nyingine -kama ilivyoeleza Hadiyth- ni kuwa, inawezekana kwamba yeye alikuwa ni wa kwanza kuvaa suruali wakati anaposwali ili kupata sitara ya ziada isiyo na shaka na kulinda tupu yake isigusane na sehemu yake ya kuswalia, naye akafanya kama alivyoamrishwa, na akalipwa hilo kuwa wa kwanza kusitiriwa Siku ya Qiyaamah.

 

Kadhalika, inawezekana kuwa wale waliomtupa motoni, walimwacha uchi na wakamvua nguo zote mbele ya watu kama anavyofanywa mtu anayetekelezewa adhabu ya kifo. Hivyo atalipwa nguo zake Siku ya Qiyaamah, na atakuwa mtu wa kwanza kuvaa mbele ya halaiki, na haya ni malipo mazuri zaidi. [Al-Qurtwubiy katika At-Tadhkirah]

 

(xv) Nabii (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema kwamba yeye ni kiumbe bora kabisa:  Amesimulia Anas bin Maalik (رضي الله عنه):  Alikuja mtu mmoja kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwambia: “Ee kiumbe bora kabisa!”  Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akamjibu: “Huyo ni Ibraahiym (عليه السّلام). [Muslim]

 

Sifa Za Nabii Ibraahiym (عليه السّلام):

 

(i) Hakuwa mshirikina kabisa. Ametajwa kwa sifa hii katika Suwrah kadhaa kwenye Qur-aan ikiwemo Suwrah hii An-Nahl (16:120). Pia, kisa chake katika Al-An’aam (6:74-81) cha kutokuabudu nyota wala mwezi wala jua kinathibitisha sifa hii. Kadhalika, alimuomba Allaah Amuepusha yeye na  wanawe wasiwe washirikina: Ibraahiym (14:35). Isitoshe, alimnasihi baba yake pia asiwe mshirikina lakini hakumsikiliza bali alimfukuzilia mbali: Maryam (19:41-48) na Ash-Shu’araa (26:69-89).

 

(ii) Alikuwa ni mtimizaji ahadi: An-Najm (53:37).

 

(iii) Ni mwenye huruma mno na mvumilivu: At-Tawbah (9:114).

 

(iv) Ni mvumilivu sana, mnyenyekevu mno kwa Allaah, na mwingi wa kurejea Kwake. Huwd (11:75).

 

(v) Mkarimu mno: Huwd (11:69), na Adh-Dhaariyaat (51:24-26).

 

(vi) Mwenye utukufu: Rejea Tanbihi namba 1 ya Aayah namba (4) katika Suwrah Yuwsuf.

 

(vii) Mnyeyekevu, kwani aliomba duaa baada ya kujenga Al-Ka’bah: Al-Baqarah (2:128). Al-Ka’bah ni Nyumba Tukufu kabisa katika Vitukufu vya Allaah katika Mji Mtukufu kabisa. Lakini juu ya utukufu huu, alikuwa na wasiwasi juu ya kutaqabaliwa kitendo hiki, kwa maana hakuwa na kibri kuwa madamu amejenga kitu kitukufu kabisa cha Allaah, basi awe amesifika au ni mtu bora kabisa.

 

(viii) Ana kisa muhimu cha uthibitisho wa Tawhiyd iliyojikita moyoni mwake wakati alipoingizwa motoni na watu wake kwa sababu aliyavunja masanamu waliyokuwa wakiyaabudu: Al-Anbiyaa (21:51-70),  na Asw-Swaaffaat (37:83-99).

 

(ix) Mwenye moyo uliosalimika: Asw-Swaaffaat (37:84).

 

(x) Swiddiyq (mkweli wa kidhati): Maryam (19:41).

 

(xi) Mwenye akhlaaq na mfano wa maadili mema: Al-Mumtahinah (60:4).

 

(xii) Amekhitariwa duniani, na Aakhirah ni miongoni mwa Swalihina: Al-Baqarah (2:130).

 

(xiii) Mwenye nguvu na busara: Swaad (38:45). Na katika busara zake, alimwambia mwanawe Ismaa’iyl abadilishe kizingiti chake badala ya kumwambia moja kwa moja “mwache mkeo.” Hii ni kutokana na malalamiko ya mke huyo kuhusu maisha yao na shida zao. Kisha akamtaka athibitishe kizingiti chake, akimaanisha aendeleze ndoa yake na mkewe mwengine (asimtaliki), mke wa pili ambaye hakulalamika shida zao za kimaisha. Maelezo ya hili yapo katika Hadiyth ndefu ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما)  iliyopokelewa na Al-Bukhaariy, Kitaab Ahaadiyth Al-Anbiyaa.

 

Pia katika busara zake ni kumtaka mfalme Namruwd aliyejifanya kuwa yeye ni Mola na mwabudiwa, alichomoze jua kutoka Magharibi badala ya Mashariki, lakini mfalme huyo akabakia kinywa wazi ameduwaa. Rejea Al-Baqarah (2:258) kwenye maelezo bayana katika faida ya Aayah hiyo.

 

Pia katika busara yake nyengineyo ni vile alivyovunja masanamu kisha akatundika shoka ya sanamu lilokuwa kubwa lao. Kaumu yake walipomuuliza nani aliyevunja masanamu yetu, alijibu: “Waulizeni wakiwa wanaweza kunena!” Akikusudia pia kama kweli  wanastahiki kuabudiwa ikiwa hawawezi kujihami wenyewe kusingiziwa uvunjaji wa masanamu yao. Rejea Al-Anbiyaa (21:57-63), na Asw-Swaafaat (37:88-96)

 

(xiv) Alikhofia familia yake wasije kuabudu masanamu. Naye mwenyewe tokea utotoni alichukia ibaada ya shirki na masanamu. Na alikhiari Dini kuliko dunia, napo ni pale alipowaacha familia yake katika bonde la Makkah ambako hapakuwa na chochote, na alitaja sababu yake kuwa ili wasimamishe Swalaah: Ibraahiym (14:35-37).

 

Utoto Wake Na Da'wah Kwa Watu Wake:

 

Tokea utoto wake Ibraahiym (‘alayhis-salaam), alikuwa akiyachukia masanamu kwani alishangaa kuwa vipi wanaabudu masanamu wanayachonga wenyewe na ambayo hayakuweza kumdhuru au kumfaa chochote mtu? Ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema kuwa Alimjua vizuri na Akampa uongofu tokea mdogo:

 

وَلَقَدْ آتَيْنَا إِبْرَاهِيمَ رُشْدَهُ مِن قَبْلُ وَكُنَّا بِهِ عَالِمِينَ ﴿٥١﴾

Na kwa yakini Tulimpa Ibraahiym uongofu wake kabla, na Tulikuwa Wenye kumjua vizuri. [Al-Anbiyaa:51]

 

Akawa anajadiliana na watu wake ili awatoe kutoka katika upotofu: 

 

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَا هَـٰذِهِ التَّمَاثِيلُ الَّتِي أَنتُمْ لَهَا عَاكِفُونَ ﴿٥٢﴾

Alipomwambia baba yake na watu wake: Nini haya masanamu ambayo nyinyi mnayakalia kuyaabudu. [Al-Anbiyaa: 52]  

 

Lakini kila walivyokuwa wakiitwa katika Tawhyid, jibu lilikuwa wamekuta wazazi wao wanafanya hivyo. Lakini Ibraahiym (‘alayhis-salaam) hakuacha kuendelea kujadiliana nao:

 

 وَلَقَدْ آتَيْنَا إِبْرَاهِيمَ رُشْدَهُ مِن قَبْلُ وَكُنَّا بِهِ عَالِمِينَ ﴿٥١﴾

Na kwa yakini Tulimpa Ibraahiym uongofu wake kabla, na Tulikuwa Wenye kumjua vizuri.

 

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَا هَـٰذِهِ التَّمَاثِيلُ الَّتِي أَنتُمْ لَهَا عَاكِفُونَ ﴿٥٢﴾

Alipomwambia baba yake na watu wake: Nini haya masanamu ambayo nyinyi mnayakalia kuyaabudu?

 

قَالُوا وَجَدْنَا آبَاءَنَا لَهَا عَابِدِينَ ﴿٥٣﴾

Wakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu.

 

قَالَ لَقَدْ كُنتُمْ أَنتُمْ وَآبَاؤُكُمْ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٥٤﴾

Akasema: Kwa yakini mmekuwa nyinyi na baba zenu katika upotofu bayana.

 

قَالُوا أَجِئْتَنَا بِالْحَقِّ أَمْ أَنتَ مِنَ اللَّاعِبِينَ ﴿٥٥﴾

Wakasema: Je, umetujia kwa haki, au wewe ni miongoni mwa wafanyao mchezo?

 

قَالَ بَل رَّبُّكُمْ رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الَّذِي فَطَرَهُنَّ وَأَنَا عَلَىٰ ذَٰلِكُم مِّنَ الشَّاهِدِينَ ﴿٥٦﴾

Akasema: Bali Rabb wenu ni Rabb wa mbingu na ardhi, Ambaye Amezianzisha, nami ni katika wenye kushuhudia hayo. 

 [Al-Anbiyaa: 51-56]  

 

Akaendelea kuwalingania kwa kuwauliza vipi wanaabudu vitu visivyoona au kusikia wala kuwafaa au kuwadhuru? Na majibu yao yakawa ni hayo hayo tu:

 

وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ إِبْرَاهِيمَ ﴿٦٩﴾

Na wasomee (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) khabari za Ibraahiym.

 

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَا تَعْبُدُونَ ﴿٧٠﴾

Alipomwambia baba yake na watu wake: Mnaabudu nini?

 

قَالُوا نَعْبُدُ أَصْنَامًا فَنَظَلُّ لَهَا عَاكِفِينَ ﴿٧١﴾

Wakasema: Tunaabudu masanamu, na tutaendelea kuyakalia kwa kuyaabudu.

 

قَالَ هَلْ يَسْمَعُونَكُمْ إِذْ تَدْعُونَ ﴿٧٢﴾

Akasema: Je, yanakusikieni mnapoyaomba?

 

أَوْ يَنفَعُونَكُمْ أَوْ يَضُرُّونَ ﴿٧٣﴾

Au yanakunufaisheni au yanakudhuruni?

 

قَالُوا بَلْ وَجَدْنَا آبَاءَنَا كَذَٰلِكَ يَفْعَلُونَ ﴿٧٤﴾

Wakasema: Bali tumewakuta baba zetu wakifanya hivyo.

 

قَالَ أَفَرَأَيْتُم مَّا كُنتُمْ تَعْبُدُونَ ﴿٧٥﴾

Akasema: Je, mnaona hivyo mlivyokuwa mkiviabudu?

 

أَنتُمْ وَآبَاؤُكُمُ الْأَقْدَمُونَ ﴿٧٦﴾

Nyinyi na baba zenu waliotangulia?

 

 [Ash-Shu'araa: 69-76] 

 

 

Tawhiyd Inamdhihirikia Nabii Ibraahiym (‘Alayhis-salaam)

 

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) aliendelea kuhojiana na watu wake kuhusu ibaada zao za kuabudu masanamu, waliodai kuwa wanawakurubisha kwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), ilhali Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hahitaji kuombwa kwa kupitia mtu au kitu chochote, bali linalopasa ni kumuomba Yeye moja kwa moja bila ya kuweko yeyote kati Yake.

 

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akawa anawaza vitu wanavyoabudu zaidi ya masanamu, kama vile nyota, jua na mwezi. Ikawa haimuingiia akilini kabisa kuwa vitu hivyo vinapasa kuabudiwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akataka kumdhihirishia hayo. Ikawa kila usiku na mchana unapoingia, Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alikuwa anatoka na kuangaza mbinguni. Akatafakari na akatambua kuwa vyote hivyo ni vitu vyenye kutoweka na kwamba Yuko Muumba wa vitu hivyo Anayestahiki kuabudiwa kwa haki. Yametajwa hayo katika Kauli za Allaah (Subhaanahuu wa Ta’aalaa):

 

 وَكَذَٰلِكَ نُرِي إِبْرَاهِيمَ مَلَكُوتَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلِيَكُونَ مِنَ الْمُوقِنِينَ ﴿٧٥﴾

Na hivyo ndivyo Tunavyomwonyesha Ibraahiym ufalme mkubwa wa mbingu na ardhi na ili awe miongoni mwa wenye yakini.

 

فَلَمَّا جَنَّ عَلَيْهِ اللَّيْلُ رَأَىٰ كَوْكَبًا ۖ قَالَ هَـٰذَا رَبِّي ۖ فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَا أُحِبُّ

Na ulipomwingilia usiku akaona nyota. Akasema: Huyu ni Rabb wangu. Ilipotoweka akasema: Hakika mimi sipendi wanaotoweka. 

 

فَلَمَّا رَأَى الْقَمَرَ بَازِغًا قَالَ هَـٰذَا رَبِّي ۖ فَلَمَّا أَفَلَ قَالَ لَئِن لَّمْ يَهْدِنِي رَبِّي لَأَكُونَنَّ مِنَ الْقَوْمِ الضَّالِّينَ ﴿٧٧﴾

Kisha alipoona mwezi umechomoza akasema: Huyu ni Rabb wangu. Ulipotoweka akasema: Asiponiongoza Rabb wangu bila shaka nitakuwa miongoni mwa watu waliopotea.

 

فَلَمَّا رَأَى الشَّمْسَ بَازِغَةً قَالَ هَـٰذَا رَبِّي هَـٰذَا أَكْبَرُ ۖ فَلَمَّا أَفَلَتْ قَالَ يَا قَوْمِ إِنِّي بَرِيءٌ مِّمَّا تُشْرِكُونَ ﴿٧٨﴾

Kisha alipoliona jua limechomoza akasema: Huyu ni Rabb wangu, huyu ni mkubwa zaidi. Lilipotoweka akasema: Enyi watu wangu! Hakika mimi simo katika yale mnayoyashirikisha (na Allaah). [Al-An'aam: 75-78]

 

Akahojiana na watu wake:

 

إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ حَنِيفًا ۖ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٧٩﴾

Hakika mimi nimeelekeza uso wangu kwa Ambaye Ameanzisha mbingu na ardhi, nikijitenga na itikadi potofu na kuelemea haki, nami si katika washirikina.

 

وَحَاجَّهُ قَوْمُهُ ۚ قَالَ أَتُحَاجُّونِّي فِي اللَّـهِ وَقَدْ هَدَانِ ۚ وَلَا أَخَافُ مَا تُشْرِكُونَ بِهِ إِلَّا أَن يَشَاءَ رَبِّي شَيْئًا ۗ وَسِعَ رَبِّي كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا ۗ أَفَلَا تَتَذَكَّرُونَ ﴿٨٠﴾

Na watu wake wakamhoji. Akasema: Je, mnahojiana nami kuhusu Allaah na hali Amenihidi?  Na wala sikhofu hayo mnayomshirikisha Naye (kwani sitodhurika) isipokuwa Rabb wangu Akitaka jambo. Rabb wangu Amezunguka kila kitu (kwa Ujuzi).  Je, basi hamkumbuki?

 

 

وَكَيْفَ أَخَافُ مَا أَشْرَكْتُمْ وَلَا تَخَافُونَ أَنَّكُمْ أَشْرَكْتُم بِاللَّـهِ مَا لَمْ يُنَزِّلْ بِهِ عَلَيْكُمْ سُلْطَانًا ۚ فَأَيُّ الْفَرِيقَيْنِ أَحَقُّ بِالْأَمْنِ ۖ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٨١﴾

Na vipi nikhofu yale mnayoyashirikisha, nanyi hamkhofu kwamba mnamshirikisha Allaah na ambayo Hakuyateremshia kwenu hoja. Je, basi kundi gani kati ya mawili linastahiki zaidi kuwa katika amani kama nyinyi mnajua? [Al-An'aam: 79-81

 

Nabii Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akazidi kuwachukia washirikina wa kaumu yake na akathibitisha Tawhiyd yake kwa Allaah:

 

فَإِنَّهُمْ عَدُوٌّ لِّي إِلَّا رَبَّ الْعَالَمِينَ ﴿٧٧﴾

Basi hakika hao ni adui zangu isipokuwa Rabb wa walimwengu.

 

الَّذِي خَلَقَنِي فَهُوَ يَهْدِينِ ﴿٧٨﴾

Ambaye Ameniumba, Naye Ananiongoza.

 

وَالَّذِي هُوَ يُطْعِمُنِي وَيَسْقِينِ ﴿٧٩﴾

Na Ambaye Ndiye Anayenilisha na Ananinywesha.

 

وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ ﴿٨٠﴾

Na ninapokuwa mgonjwa, basi Yeye Ananiponyesha.

 

وَالَّذِي يُمِيتُنِي ثُمَّ يُحْيِينِ ﴿٨١﴾

Na Ambaye Atanifisha kisha Atanihuisha.

 

وَالَّذِي أَطْمَعُ أَن يَغْفِرَ لِي خَطِيئَتِي يَوْمَ الدِّينِ ﴿٨٢﴾

Na Ambaye natumai Atanighufuria makosa yangu Siku ya Malipo.

[As-Shu'araa: 77-82]

 

 

Mjadala Baina Ya Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) Na Mfalme Kafiri Nimruwdh Bin Kuwsh:

 

 

Nimruwdh alikuwa mfalme na alitoka katika kizazi cha Nuwh (‘alayhis-salaam) Jina lake ni Nimruwdh bin Kanaan, bin Kuwsh, bin Saam bin Nuwh.   [Amenukuu Mujaahid - Tafsyir Ibn Kathiyr 2:35]. 

 

Mujaahid vile vile amesema: "Wafalme waliotawala pande za Mashariki na Magharibi za dunia walikuwa wanne, wawili walioamini; Sulaymaan bin Daawuud na Dhul-Qarnayn. Ama waliokuwa makafiri ni; Nimruwdh na Nebuchadnezzar" [At-Twabariy 5:433] Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ni Mjuzi zaidi.

 

Mfalme huyo alikanusha kuweko kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), akajiona kuwa yeye ndiye anayepasa kuabudiwa.  Na kilichomfanya Nimruwd ajifanye ni muabudiwa ni kutokana na kibri yake kwa kuwa alitawala kwa muda mrefu. Na kibri hiyo ni kama ya Firawni.

 

Aliposikia kuwa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) Anasema kuwa kuna Yuko Anayepasa kuabudiwa kwa haki, na Mwenye kumiliki nafsi za wanaadam na Mwenye Kuhuisha na Kufisha, akahojiana na Ibraahiym (‘alayhis-salaam):

 

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِي حَاجَّ إِبْرَاهِيمَ فِي رَبِّهِ أَنْ آتَاهُ اللَّـهُ الْمُلْكَ إِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّيَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ قَالَ أَنَا أُحْيِي وَأُمِيتُ ۖ قَالَ إِبْرَاهِيمُ فَإِنَّ اللَّـهَ يَأْتِي بِالشَّمْسِ مِنَ الْمَشْرِقِ فَأْتِ بِهَا مِنَ الْمَغْرِبِ فَبُهِتَ الَّذِي كَفَرَ ۗ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿٢٥٨﴾

Je, hukumzingatia yule ambaye alimuhoji Ibraahiym kuhusu Rabb wake kwa vile Allaah Alimpa ufalme aliposema Ibraahiym: Rabb wangu ni Yule Ambaye Anahuisha na Kufisha. Akasema: Mimi (pia) nahuisha na kufisha. Ibraahiym akasema: Hakika Allaah Analileta jua kutoka Mashariki basi wewe lilete kutoka Magharibi. Aliyekufuru akabaki kinywa wazi bila jibu, akataghayuri rangi. Na Allaah Haongoi watu madhalimu. [Al-Baqarah: 258]

 

Kudai kwa Nimruwdh kuwa yeye ana uwezo wa kuhuisha na kufisha, ni kumwachia huru mmoja kati ya watu waliohukumiwa kufa, na kumuua mwengine. [At-Twabariy (5:433-437), imepokelewa na Qataadah, Muhammad bin Is-haaq na As-Suddi]

 

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akamhoji kuwa, ikiwa yeye anadai ana uwezo huo wa kuhuisha na kufisha, basi na aonyesha uwezo wa wa kulichomoza jua kutoka Magharibi, kwani Muumba wa wanaadamu Analichomoza kutoka Mashariki, basi yeye ageuze mwenendo huo alifanye litokeze upande wa Magharibi.  Akapigwa na mshangao na hakuweza kujibu lolote bali alitahayarika.

 

Allaah Akamuangamiza Nimruwdh kwa mbu ambaye ni kiumbe dhaifu kabisa. Kisa chake kimesimuliwa katika Hadiyth za Israaiyliyyaat na hakuna kosa kusimulia ili tupate kupata mafunzo yake. Allaah   Alimfisha mfalme aliyejidai kuwa yeye ndiye anayepasa kuabudiwa, kwa kidudu dhalili na kidogo mno! [Hadiyth ya ‘Amr bin Al-Aasw (Radhwiya-Allaahu ‘anhu) ameipokea Al-Bukhaariy]  

 

Imaam Atw-Twabariy ameitoa katika Jaami’u Al-Bayaan (14/204) kutoka kwa Zayd bin Aslam kwamba: “Nimruwdh hakika alikuwa dhalimu wa kwanza duniani. Allaah Akampelekea mbu, wakaingia masikioni na puani mwake.  Alibaki kujipiga kichwa chake kwa nyundo kwa miaka mia nne! Watu waliokuwa na huruma zaidi walikuwa ni wale waliounganisha mikono wakawa wanampiga kichwani (kutuliza mbu).  Alijifanya jabari na alikuwa dhalimu kwa muda wa miaka mia nne, basi Allaah Akamuadhibu miaka mia nne sawa na muda wa utawala wake. Kisha Allaah Akamfisha.”

 

 

Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) Anamuomba Allaah Amuonyeshe Vipi Anahuisha Wafu:

 

‘Ulamaa wamesema kwamba kuna sababu ya ombi hili la Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kutaka kuonyeshwa vipi Allaah (Subhanaahu wa Ta’aalaa) Anahuisha aliyekufa. Mfano Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alipomuambia Nimruwd:

 

  رَبِّيَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ  

Rabb wangu ni Yule Ambaye Anahuisha na Kufisha. [Al-Baqarah: 258]

 

Nabii Ibraahiym alitaka kuyanika na Uwezo wa Allaah wa Kuhuisha na Kufisha akamuomba Allaah Amwonyeshea vipi Anahuisha wafu. Na Hadiyth ya Nabii (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ifuatayo inasema kwamba sisi tuna uwezekano mkubwa zaidi wa kutia shaka kuliko Ibraahiym. Yeye Ibraahiym alimwomba Rabb wake amwonyeshe jinsi ya kuwahuisha wafu ili ashuhudie na atulize moyo wake:

 

عن أبي هريرة، رضي الله عنه، قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم  ((نحن أحق بالشك من إبراهيم، إذ قال: (رَبِّ أَرِنِي كَيْفَ تُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۖ قَالَ: أَوَلَمْ تُؤْمِن ۖ قَالَ بَلَىٰ وَلَـٰكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِي ۖ ) البخاري

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya-Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Sisi tuna uwezekano mkubwa wa kuonyesha shaka kuliko Ibraahiym aliposema: 

 

رَبِّ أَرِنِي كَيْفَ تُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۖ قَالَ أَوَلَمْ تُؤْمِن ۖ قَالَ بَلَىٰ وَلَـٰكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِي   

Rabb wangu! Nionyeshe vipi Unahuisha wafu? (Allaah) Akasema: Je, kwani huamini? Akasema: Sivyo hivyo! Bali Naam (naamini)! Lakini ili moyo wangu utumainike.

[Hadiyth ameipokea Imaam Al-Bukhaariy]  

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamtakabalia Ibraahiym (‘alayhis- salaam) ombi lake na Akamtaka achukue ndege wanne.  (‘Ulamaa wa Tasfiyr wamekhtilafiana kuhusu aina ya ndege waliotajwa kwani haikuelezwa ndege aina gani.)  Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamtaka Ibraahiym (‘alayhis-salaam) awazoeshe kwanza ndege kwake, kisha awakate vipande vipande. [Ibn 'Abbaas, Ikrimah, Sa'iyd bin Jubayr, Abu Maalik, Abu Al-Aswad, Ad-Dili, Wahb bin Munabbih, Al Hassan na As-Sudi kutoka Ibn Haatim (3:109), (1040)]

 

Ibraahiym (‘alayhis-salaam) akawazoesha kwake, kisha akawachinja na kuwatoa manyoa na kuwakata vipande vipande, kisha akavichanganya vipande hivyo pamoja.  Kisha akagawa vipande na kuviweka katika vilima vinne au saba.  Ibn 'Abbaas amesema, "Ibraahiym (‘alayhis- salaam) aliweka vichwa vya ndege hao katika mikono yake." Kisha akafanya kama Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Alivyomuamrisha kuwaita hao ndege kwake.  Akashuhudia kwa macho yake manyoya yao, damu na viungo vya kila ndege, vikiruka kujikusanya pamoja katika umbile lake, wakawa wanafika   mbele ya Ibraahiym (‘alayhis- salaam) wakitembea haraka kuelekea kwake. Ikawa kila ndege alikwenda kwa Ibraahiym (‘alayhis-salaam) kuchukua kichwa chake kutoka mikononi mwa Ibraahiym (‘alayhis-salaam), na alipojaribu kumpa ndege mmoja kichwa cha ndege mwengine, ndege alikataa kupokea na kujiunga. Subhana Allaah! Kwa hiyo kila kichwa cha ndege kilijunga na kiungo chake kile kile cha asili yake, kwa Uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). [Al-Qurtubi 3:300].

 

Allaah Alifanya hivyo ili Ibraahiym (‘alayhis-salaam) ashuhudie kwa dhahiri kuhuishwa kwa ndege hao na apate na kutuliza moyo wake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

وَإِذْ قَالَ إِبْرَاهِيمُ رَبِّ أَرِنِي كَيْفَ تُحْيِي الْمَوْتَىٰ ۖ قَالَ أَوَلَمْ تُؤْمِن ۖ قَالَ بَلَىٰ وَلَـٰكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِي ۖ قَالَ فَخُذْ أَرْبَعَةً مِّنَ الطَّيْرِ فَصُرْهُنَّ إِلَيْكَ ثُمَّ اجْعَلْ عَلَىٰ كُلِّ جَبَلٍ مِّنْهُنَّ جُزْءًا ثُمَّ ادْعُهُنَّ يَأْتِينَكَ سَعْيًا ۚ وَاعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٢٦٠﴾ 

Na pindi aliposema Ibraahiym: Rabb wangu! Nionyeshe vipi Unahuisha wafu? (Allaah) Akasema: Je, kwani huamini? Akasema: Sivyo hivyo! Bali Naam (naamini)! Lakini ili moyo wangu utumainike. (Allaah) Akasema: Basi chukua ndege wanne wazoeshe kwako, (uwachinje), kisha weka juu ya kila jabali sehemu ya hao (ndege), kisha waite watakujia mbio (wakiumbika upya), na jua kwamba hakika Allaah Ni Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Baqarah 2:260]

 

.../2

Share