Itikadi Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah Kuhusiana Na Qur-aan – 01

 

Itikadi Ya Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah Kuhusiana Na Qur-aan – 01

 

Je, Qur-aan Ni Kiumbe?

 

Abuu Rabiy’

 

 

 

 

الحمد لله رب العالمين ثم الصلاة والسلام على رسولنا محمد صلى الله عليه وعلى آله وسلم أما بعد:

 

Baada ya kumshukuru Allaah Tabaaraka Wa Ta’aalaa na kumtakia Swalah na Salaam Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Anasema Allaah katika Kitabu Chake Kitukufu:

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ ﴿٦٢﴾

“Hivyo ni kwa kuwa Allaah Ndiye wa Haki na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batili…” [Al-Hajj: 62]

 

Na anasema tena Jalla Jalaaluhu:

وَتَمَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ صِدْقًا وَعَدْلًا ۚ لَّا مُبَدِّلَ لِكَلِمَاتِهِ ۚ وَهُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿١١٥﴾

“Na limetimia neno la Rabb wako kwa kweli na uadilifu. Hakuna mwenye kuyabadilisha maneno Yake. Naye ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.” [Al-An’aam: 115]

 

Na anasema Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

"أعوذ بكلمات الله التامات التى لا يجاوزهن بر ولا فاجر"

"Nataka hifadhi kwa maneno ya Allaah yaliyotimia ambayo hayamvuki mwema wala muovu"

 

Hadiyth ameipokea Imaam Ahmad na Ibn Abiy Shaybah na Abuu Ya'laa kutoka kwa Abdur-Rahmaan ibn Khambash (Radhi za Allaah ziwe juu yake).

 

Ndugu msomaji, kutokana na Maibadhi kupenda kujitapa na kueneza kuwa Qur-aan imeumbwa, nilipenda sana na Mimi nishiriki japo kidogo kubainisha itikadi ya Masalafi kuhusiana na Qur-aan na ubatili wa madhehebu ya Maibadhi pamoja na ndugu zao Mu'tazilah na Jahmiyyah na Mashia na mapote mengine ambayo yamepinda katika mlango huu.

 

Tunasema wabiLLaahi nasta'iyn:

Katika mojawapo ya itikadi ya Ahlus-Sunnah ni kuamini kuwa Allaah Anasifika na kila sifa iliyokuwa nzuri na kutakasika kuepukikana na kila sifa ya mapungufu.

 

Na tunaweza kusema kuwa kila sifa iliyokuwa kamili kwa mwanaadamu basi sifa hiyo kuithibitisha kwa Allaah ni katika mlango uliokuwa bora zaidi.

 

Na hii si katika kila sifa kwani kuna baadhi ya sifa zinaweza kuwa kamili kwa binaadamu lakini kwa Allaah zinakuwa ni pungufu na wala Hastahiki Allaah kusifika nazo.

 

Mfano:

  1. Sifa ya njaa na kushiba:

Sifa hizi mbili ni kamilifu kabisa kwa mwanaadamu kwani mwanaadamu ambae hasikii njaa na wala akila hashibi ipasavyo huwa ana mapungufu, lakini sifa hizi haijuzu kumthibitishia Allaah (Tabaaraka Wa Ta’aalaa).

 

B) Sifa ya kuoa na kulala:

Hizi ni sifa thabiti na kamilifu kwa mwanaadamu lakini kwa Allaah zinakuwa na mapungufu kwa hiyo hatuwezi kumthibitishia Allaah.

 

Lakini kuna sifa zingine zimekuja moja kwa moja na zinathibitisha ukamilifu wa mwanaadamu kama vile kuzungumza, kucheka, kughadhibika, kusikia n.k.

 

Sifa hizi kumthibitishia Allaah inakuwa ni katika mlango uliokuwa bora zaidi na zaidi. Na ndio maana utaona usluubu wa Qur-aan katika kujadiliana na washirikina na kubatilisha wale waabudiwa wao kuwa  hawana haki wala sifa ya kuwa waabudiwa. Allaah alikuwa Anawadhihirisha wale waabudiwa wao kwa kutokukamilika kwao kwa baadhi ya sifa. Anasema Allaah Mtukufu Akisimulia mjadala uliopita kati ya Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) na baba yake:

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنكَ شَيْئًا ﴿٤٢﴾

“Pale alipomwambia baba yake: “Ee baba yangu! Kwa nini unaabudu vile visivyosikia na visivyoona na visivyokufaa kitu chochote?” [Maryam: 42]

 

Angalia hapo ndugu yangu, Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) anajadiliana na baba yake kuhusiana na huyo muabudiwa wake ambae ni sanamu, sasa amuuliza baba yake; Vipi umuabudu walhaal hasikii wala haoni na wala hakunufaishi na chochote??

 

Kwa sababu ikiwa kiumbe kinaona na kusikia na kinamnufaisha mwenzake katika baadhi ya mambo sifa hizi kusifika nazo muumba ni bora zaidi na kwa umakini zaidi!!

 

Kwanini?

Hata isifikie kiumbe kuwa amekamilika kuliko yule aliyemuumba. Na ndio maana Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) akabatilisha ibaadah ya baba yake kwa yale masanamu kwa kukosa kwao kusifika na hizi sifa.

 

Hebu angalia tena namna gani Allaah alivyowaaibisha watu wa Muusaa (‘Alayhis Salaam) pale ambapo walipoamua kumuamudu yule ndama ilikuwaje? Allaah Anasema:

أَلَمْ يَرَوْا أَنَّهُ لَا يُكَلِّمُهُمْ وَلَا يَهْدِيهِمْ سَبِيلًا ۘ اتَّخَذُوهُ وَكَانُوا ظَالِمِينَ ﴿١٤٨﴾

“…Je, hawakuona kwamba huyo (ndama) hawasemeshi na wala hawaongozi njia? Walimfanya (muabudiwa) na wakawa madhalimu.” [Al-A’raaf: 148]

 

Kwa mujibu wa Aayah hizi muabudiwa anatakikana awe na sifa zilizokuwa kamili na ziwe juu kuliko sifa za yule anayemuabudu.

Hata isiweze kuwa muabudu yupo juu kisifa na kiuwezo kuliko muabudiwa!

Ikiwa kiumbe atasifika na sifa ya kusikia basi muabudiwa asifike zaidi na sifa hiyo, na ikiwa kiumbe anasifika na sifa ya kuzungumza basi muabudiwa anatakikana kusifika zaidi na sifa hiyo; hakadhaa.

 

 

Tanbihi:

 

Kuna kufanana kwa majina ya sifa kati ya muumba na viumbe vyake na wala hii haimaanishi kuwa wamefanana kwa kila kitu; laa hashaa!!

 

Mfano Allaah Anasifika kwa sifa ya kuzungumza na pia mwanaadamu anasifika kwa sifa hiyo! Sasa hatuwezi kusema kuwa kumthibitishia Allaah sifa ya kuzungumza ni kumfananisha na viumbe Wake!!

 

Hii haipo sawa sawa kwa sababu wewe wazizungumzia dhati mbili tofauti, wamzungumzia Allaah na wamzungumzia mwanaadamu sasa vipi umfananishe Allaah na kiumbe wake? Na wakati wafahamu fika kuwa Allaah hafanani na kitu chochote?

 

Na ndio hapa utaona kuwa Ahlus-Sunah wameweka msingi madhubuti sana katika mlango huu kwa kusema:

“Kila sifa iliyokuwa thaabit kwa Allaah sisi tunamthibitishia sifa hiyo kama Alivyoithibitisha Allaah Mwenyewe na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pasina kufanya namna wala kufananisha wala kukanusha wala kubadilisha.

 

Na kama Allaah alivyokuwa mmoja katika dhati yake kadhalika ni mmoja katika sifa Zake (Subhaanahu wa Ta’aalaa) hafanani na yeyote katika sifa Zake, na mwenye kumfananisha Allaah na yeyote katika sifa Zake basi huyo ni mushabbiha.

 

Na kama alivyokuwa Allaah bila ya mwanzo kadhalika sifa zake Alikuwa nazo kwani zimefungamana na dhati Yake.

 

Sasa hatuwezi kusema kuwa Allaah Ameumba sifa zake na yeye yupo pasina kuwa na sifa!!

Hili haliingii katika akili kuwepo kitu pasina kuwa na sifa!

 

Maana yake hicho kitu hakipo kwa sababu hata wewe Muibadhi tukikuambia tusifie kitu ambacho kipo lakini hakina Hata sifa hutaweza!

 

Kwa hiyo, kila kilichopo lazima kiwe na sifa.  Na kwa Allaah ni katika mlango uliokuwa bora zaidi.”

 

 

Sifa Ya Kuzungumza:

 

Sifa hii ni thaabit kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) pasina ubishi wowote wala khilafu kwa yule ambaye Allaah Amemruzuku maarifa yaliyokuwa sahihi.

 

Anasema Allaah Mtukufu:

وَكَلَّمَ اللَّـهُ مُوسَىٰ تَكْلِيمًا ﴿١٦٤﴾

“Na bila shaka Allaah Alimsemesha Muwsaa maneno moja kwa moja.” [An-Nisaa: 164]

Aayah hii ipo wazi sana juu kuthibitisha sifa ya kuzungumza kwa Allaah (Tabaaraka Wa Ta’aalaa).

 

Na watu wa lugha wanasemaje kuhusiana na kitendo kitakapokuja kisha kikasisitizwa kwa maswdar?

 ﻗﺎﻝ ﺍﻟﻨﺤﺎﺱ: "ﻭﺃﺟﻤﻊ ﺍﻟﻨﺤﻮﻳﻮﻥ ﻋﻠﻰ ﺃﻧﻚ ﺇﺫﺍ ﺃﻛﺪﺕ ﺍﻟﻔﻌﻞ ﺑﺎﻟﻤﺼﺪﺭ ﻟﻢ ﻳﻜﻦ ﻣﺠﺎﺯﺍ"

Anasema Imaam Nahhaas (Allaah Amrehemu):

"Wamekubaliana watu wa Nahw kwamba wewe ukikisisitiza kitendo kwa maswdar haiwi majazi"

Yaani amenukuu Ijmaa’ kutoka kwao.

 

Kwa hiyo, hapo hata kwa wale wanaoona usahihi wa majazi katika Aayah hiyo haingii kwa sababu hicho kitendo ambacho ni "Kallama" Kimekokotezwa kwa maswdar ambayo ni "Takliymaa" Sasa hapo hauwezi kufasiri ila tafsiri ya uhakika kuwa Allaah Alimzungumzusha Muusaa (‘Alayhis Salaam). Na mas-alah ya majazi, si mada yetu.

Bali majazi ni ngazi wanayopandia watu waliopinda ili wafikie kwenye kukanusha sifa za Allaah ambazo ni thaabit. Allaahul Musta'aan.

 

Na wala hakuna swali hapo ila kwa wale wenye maradhi kwamba je, Allaah Ana mdomo na je, ana maneno na ulimi?

 

Swali hili halina faida kwa sababu Allaah Amethibitisha kuwa Anazungumza na neno "Kuzungumza" ni neno lenye kuakilika, na wala hajatubainishia Anazungumzaje. Kwa hiyo, sisi tunaamini maana ya "Kuzungumza" na tunathibitisha sifa ya kuzungumza na tunaamini kuwa Allaah Anazungumza lakini hatujui Anazungumzaje na tunaamini kuwa Anayo kayfiyyah ya kuzungumza lakini sisi hatuijui.

 

Aayah ya pili yenye kujulisha kuwa Allaah Anazungumza ni kauli Yake:

وَلَمَّا جَاءَ مُوسَىٰ لِمِيقَاتِنَا وَكَلَّمَهُ رَبُّهُ ﴿١٤٣﴾

“ Na alipokuja Muwsaa katika muda na pahala pa miadi Yetu, na Rabb wake Akamsemesha…” [Al-A’raaf: 143]

 

 Hapo pia papo wazi kabisa kuwa Allaah ndio mzungumzaji na Muusaa (‘Alayhis Salaam) ndiye mzungumzishwa.

 

Na ukisoma tafsiri za ‘Ulamaa kama vile Ibn Kathiyr, Atw-Twabariy, Al-Qurtwubiy na wengineo, wameeleza wazi kuwa Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa Alimzungumzisha Muusaa (‘Alayhis Salaam). 

 

Na pia zimekuja Hadiyth nyingi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuthibitisha kuwa Allaah Anazungumza.

 

Kama ilivyokuja katika Swahiyh Al-Bukhaariy, Hadiyth ya Abuu Sa’iyd Al-Khudriy (Radhi za Allaah ziwe juu yake) kuwa amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

ﻗﺎﻝ ﺭﺳﻮﻝ ﺍﻟﻠﻪ ﺻﻠﻰ ﺍﻟﻠﻪ ﻋﻠﻴﻪ ﻭﺳﻠﻢ: "ﻳﻘﻮﻝ ﺍﻟﻠﻪ ﺗﻌﺎﻟﻰ: ﻳﺎ ﺁﺩﻡ، ﻓﻴﻘﻮﻝ: ﻟﺒﻴﻚ ﻭﺳﻌﺪﻳﻚ، ﻓﻴﻨﺎﺩﻱ ﺑﺼﻮﺕ: ﺇﻥ ﺍﻟﻠﻪ ﻳﺄﻣﺮﻙ ﺃﻥ ﺗُﺨﺮِﺝ ﻣﻦ ﺃﻣﺘﻚ ﺑﻌﺜًﺎ ﺇﻟﻰ ﺍﻟﻨﺎﺭ"

"Atasema Allaah Aliyekuwa juu, Ee Aadam! Ataitikia, Labbayka Wasa'dayk, na ataita kwa sauti, Hakika Allaah Anakuamrisha utoe kundi la watu katika ummah wako motoni"

 

Pia Hadiyth hii ipo wazi kuwa Allaah Anazungumza.

 

Wa-Allaahi, dalili juu ya sifa hii ni nyingi sana na wala Mimi sizitaji zote bali naashiria kwa mwenye kuzitaka basi arejee vitabu vya ‘Aqiydah vya Ahlus-Sunnah atatosheka.

 

Na katika yale ambayo Allaah Ameyazungumza ni hii Qur-aan ambayo ipo mikononi mwetu ambayo imeandikwa kwa wino na kuhifadhiwa kifuani na kusomwa na wasomaji.

 

Hii Qur-aan ni maneno yake Ar-Rahmaan ambayo Yeye Ameyazungumza na amesikia Jibriyl (‘Alayhis Salaam) kutoka kwa Allaah na akamfikishia Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Hii Qur-aan ni maneno Yake Allaah kwa sauti na herufi na wala haikuumbwa kama wanavyosema Mu'tazilah na Jahmiyyah na Ibaadhwiyyah (Maibadhi) na Shia na wengineo.

 

Bali ni maneno Yake Allaah, Kwake yametoka na Kwake yatarudi.

 

 

Fuatana na Mimi katika makala namba mbili in Shaa Allaah.

 

 

Share