Je Inafaa Kusoma Surah Katika Rakaa Ya Tatu Na Ya Nne?

 

SWALI:

Asalaam Aleykum

 suala langu  ni kuuliza wakati mwengine unaposali tuseme unasali salaa ya maghrib rakaa ya kwanza na ya pili unasoma Alhamdu na sura,na rakaa  ya tatu unasoma Alhamdu peke yake sasa mara nyengine unasahau unataka kusoma tena sura na ushaanza kusema bismi lahi jee sasa inafaa kusoma sura au undelee kurukuu tu na kuna chochote unasema baada ya salam.Shukran


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Kuna ikhtilaaf katika rai za Maulamaa kuhusu kusoma Surah baada ya Raka'ah mbili za mwanzo yaani baada ya kusimama kutoka katika Tashahhud ya mwanzo kama inapendekezeka au la. Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) ameona kuwa ni makruuh (inachukiza). Ama Imaam Ash-Shaafi'iy (Rahimahu Allaah) ameona kuwa ni mustahabb (inapendekezeka) katika rai yake ya mwisho, na sio rai yake ya mwanzo. Na rai ya Imaam Shaafi'iy ya mwisho inaonekana sahihi zaidi na kutiliwa nguvu na hadiyth na maelezo yatakayofuatia mbele.

Ilivyo kawaida tunavyojua wengi kusoma Surah baada ya Suratul-Faatiha ni katika Raka'ah mbili za mwanzo. Na Katika Raka'a ya tatu au ya nne ni kusoma Suratul Faatiha pekee kutokana na Hadiyth ifuatayo:

عن أَبِي قَتَادَةَ رضي الله عنه " أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ   كَانَ يَقْرَأُ فِي الرَّكْعَتَيْنِ الأُولَيَيْنِ مِنْ الظُّهْرِ وَالْعَصْرِ بِفَاتِحَةِ الْكِتَابِ وَسُورَةٍ , وَيُسْمِعُنَا الآيَةَ أَحْيَانًا , وَيَقْرَأُ فِي الرَّكْعَتَيْنِ الأُخْرَيَيْنِ بِفَاتِحَةِ الْكِتَابِ "  مسلم 

Imetoka kwa Abu Qataadah رضي الله عنه kwamba "Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akisoma Surah ya kufungulia kitabu (Suratul-Faatiha) katika Raka'ah mbili za mwanzo kwenye Swalah ya Adhuhuri na Alasiri na wakati mwingine akitusikilizisha ayah, na katika Raka'ah mbili za mwisho alikuwa akisoma Suratul-Faatiha" (pekee)   [Muslim]

Hivi ndivyo msimamo wa asili. Lakini inaruhusiwa kusoma Surah au ayah baada ya Suratul Faatiha katika Raka'a mbili za mwisho wakati mwingine,  kutokana na usimulizi ufuatao:

عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رضي الله عنه "َنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ   كَانَ يَقْرَأُ فِي صَلَاةِ الظُّهْرِ فِي الرَّكْعَتَيْنِ الأُولَيَيْنِ فِي كُلِّ رَكْعَةٍ قَدْرَ ثَلاثِينَ آيَةً , وَفِي الأُخْرَيَيْنِ قَدْرَ خَمْسَ عَشْرَةَ آيَةً , أَوْ قَالَ نِصْفَ ذَلِكَ , وَفِي الْعَصْرِ فِي الرَّكْعَتَيْنِ الأُولَيَيْنِ فِي كُلِّ رَكْعَةٍ قَدْرَ قِرَاءَةِ خَمْسَ عَشْرَةَ آيَةً , وَفِي الأُخْرَيَيْنِ قَدْرَ نِصْفِ ذَلِكَ"  مسلم

Imetoka kwa Abu Sa'iydil-Khudhriy رضي الله عنه kwamba "Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akisoma katika Raka'a mbili za mwanzo kwenye Swalah ya Adhuhuri takriban aya thelathini katika kila Raka'ah, na katika Raka'ah mbili za mwisho takriban aya kumi na tano, au kasema nusu yake. Katika Raka'ah mbili za mwanzo za Swalah ya Alasiri alikuwa akisoma katika Raka'ah takriban aya kumi na tano, na Raka'ah mbili za mwisho karibu nusu yake" [Muslim]

Shaykh Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema: "Hadiyth hii inaonyesha kwamba kusoma zaidi ya Suratul-Faatiha katika Raka'ah mbili za mwisho ni Sunnah na ni rai ya Maswahaba wengi pamoja na Abu Bakar As-Swiddiyq (Radhiya Allaahu 'anhu). Hii ni rai ya Imaam Ash-Shaafi'iy ikiwa ni katika Swalah ya Adhuhuri au Swalah yoyote nyingine. Na miongoni mwa Maulamaa wa karibuni ni rai ya Abul-Hasanaat Al-Laknawi" [Sifatus-Swalah]

Na hiyo ni aidha akiwa mtu anaswali pekee yake au katika Swalah ya Jamaa.

Shaykh ibn 'Uthaymiyn aliulizwa akasema: "Ikiwa mwenye kuswali amemaliza kusoma Suratul-Faatiha na Surah nyingine katika Swalah ambazo Qur'aan inasomwa kimya kimya, na Imaam bado hakurukuu, je, anyamaze kimya?"

Akajibu: "Mwenye kuswali asinyamaze kimya anapomaliza kusoma Al-Faatiha na Surah nyingine kabla ya Imaam kurukuu, bali aendelee kusoma hadi atakaporukuu Imaam. Kwa hiyo ikiwa katika Raka'ah mbili baada ya Tashahhud na amemaliza kusoma Suratul-Faatiha lakini Imaam hakurukuu, basi asome Surah nyingine hadi Imaam arukuu, ili kusikuweko ukimya katika Swalah isipokuwa ikiwa mwenye kuswali anasikiliza kisomo cha Imaam wake"  [Majmuu' Fataawa ibn 'Uthaymiyn 15/108]

Na Kusoma Surah baada ya Suratul-Faatiha ni miongoni mwa vitendo vya Sunnah katika Swalah, kwa hiyo hata kama mtu amesahau kusoma Surah baada ya Faatiha, ikiwa ni katika Raka'ah mbili za mwanzo au Raka'ah za baada ya Tashahhud ya mwanzo, basi  hana haja kurudia kusoma Surah na Swalah yake ni sahihi, atafanya tu Sajdatus-Sahw mbili  (Sajda ya kusahau) kabla ya kutoa salaam.

Kwani katika Swalah kuna vitendo vya Sunnah na fardhi. Anaposahau mtu kutenda vitendo vya fardhi ndipo inapombidi arudie kile kitendo kwani Swalah haisihi ikipunguka kitendo cha fardhi. Ama anaposahau mwenye kuswali vitendo vya Sunnah, haimpasi kuvirudia na Swalah yake ni sahihi.   

Na katika hali yako muulizaji, hakuna ubaya kama ungeliendelea kusoma Surah katika Raka'ah ya tatu, na hata kama umeacha hali kadhalika hakuna ubaya na Swalah yako sahihi.

Ama kuhusu cha kusoma kabla au  baada ya salaam imethibitika katika Sunnah kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akisoma du'aa mbali mbali na zote utazipata katika viungu vifuatavyo:

Du'aa Baada ya Tashahhud  Kabla ya Salaam

Du'aa Baada Ya Salaam

 

Na Allah Anajua zaidi.

 

Share