Kumtaja Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم) Katika Swalaah Kwa Kusema "Sayyidinaa"

 

 

 

SWALI:

Kuna ndugu zetu wakiwa katika sala hasa wakati wa kuleta kunuti imma iwe ile ya uzushi au ya kisheria ya maafa humtaja Mtume saw kwa sifa ya Seyyidina na pia kumtaja Mtume saw kuwa ni awwarina wal'akhirina {Wa mwanzo na wa mwisho} ina dalili  na nini maana yake. Allah awalipe kwa kushughulikia mambo matukufu.

 


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

 

Shukran kwa swali lako zuri kuhusu mas-ala ya ‘Ibadah ambao ndiyo msingi mkubwa wa Dini yetu na hasa ‘Ibadah ya Swalah ambayo ndiyo itakaokuwa ya mwanzo kukaguliwa Siku ya Kiyama. Katika mas-ala ya Swalah, Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Swalini kama mlivyoniona mimi nikiswali” (al-Bukhaariy).

 

Na katika mas-ala ya Hijjah, akasema: “Chukueni kutoka kwangu amali hiyo (manaasik) ya Hija” (Muslim).

 

Ikiwa hivyo ndivyo inavyotakiwa kuwa itabidi tuangalie alivyofundisha Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu mas-ala ya kumswalia. Jambo hili lipo wazi kabisa katika Dini yetu. Allah Anasema wazi katika Suratul-Ahzaab:

((إِنَّ اللَّهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا))

“Hakika Allah na Malaika Wake wanamswalia Nabii. Enyi mlioamini! Mswalieni na mumsalimu kwa salamu” (33: 56).

 

 

Imaam Al-Bukhaariy anatueleza tafsiri ya Aayah hiyo ni kuwa Maswahaba walimuuliza Mtume kuwa washajua namna ya kumtakia amani (salaam) juu yake, lakini hawakujua namna gani wamswalie. Mtume akawaambia waseme, 'Allahumma Swalli 'alaa Muhammad wa 'alaa aali Muhammad.....’ hadi mwisho kama ilivyo kwenye tashahhud. Katika huku kumswalia alikotufundisha hakutia Sayyidna katika jina lake wala jina la Nabii Ibraahiym (Alayhis Salaam).

 

 

Na ukitazama katika vitabu vya Fiqhi vyote vinapotaja kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) havitii Sayyidna, la katika tamko la Nabii Muhammad wala Nabii Ibraahiym. Anasema Shaykh ‘Abdallah Saleh Farsy: "Kitabu pekee ambacho kimeongeza tamko hilo ni kile kinachoitwa Babu. Nacho kimetungwa pande hizi za Afrika Mashariki wala hakijulikani huyo aliyekitunga. Hivyo, nyongeza hiyo ya Sayyidna haifai ndani ya Swalah ikiwa ni katika Qunuti au Tashahhud na pia nje ya Swalah. Zipo Hadithi ambazo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametumia neno hilo kama pale aliposema mimi ni Sayyid katika watoto wa Adam, lakini hizo hazihusiani na ‘Ibadah. Kwa kawaida katika mazungumzo unaweza kumuita Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au hata Swahaba mwengine kwa tamko hili. Hii inapatikana katika athar pale ‘Umar ibn al-Khatwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliposema: “Abu Bakr ni (Sayyiduna) bwana wetu, naye alimuacha huru (Sayyiduna) bwana wetu (yaani Bilaal ibn Rabaah)”.

 

Na kuhusu sifa hii ya Awwaalina wa Akhirina (wa mwanzo na wa mwisho) ni sifa ambayo haifai kupewa mtu yeyote kwani sifa hizo ni za Allah (Subhaanahu wa Ta'ala). Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:

((هُوَ الْأَوَّلُ وَالْآخِرُ وَالظَّاهِرُ وَالْبَاطِنُ وَهُوَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ))

 “Yeye ndiye wa Mwanzo na ndiye wa Mwisho, naye ndiye wa Dhaahiri na wa Siri, naye ndiye Mjuzi wa kila kitu” (57: 3).

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share