003-Aayah Na Mafunzo: Kauli Za ‘Ulamaa Kuhusu Kuabudiwa Allaah Mbinguni Na Ardhini Naye Anajua Siri Na Dhahiri Na Wanayochuma Waja

 

Aayah Na Mafunzo

 

Al-An’aam

 

Kauli Za ‘Ulamaa Kuhusu Kuabudiwa Allaah (سبحانه وتعالى) Mbinguni Na Ardhini Naye Anajua  Siri Na Dhahiri Na Wanayochuma Waja

 

 

003-Al-An’aam:   Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

 

وَهُوَ اللَّـهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَفِي الْأَرْضِ ۖ يَعْلَمُ سِرَّكُمْ وَجَهْرَكُمْ وَيَعْلَمُ مَا تَكْسِبُونَ ﴿٣﴾

Na Yeye Ndiye Allaah mbinguni na ardhini, Anajua ya siri yenu na ya dhahiri yenu, na Anajua yale mnayoyachuma. [Al-An’aam (6: 3)]

 

Mafunzo:

 

Wafasiri wa Qur-aan wamekhitilafiana katika kauli nne kuhusu Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):

وَهُوَ اللَّـهُ فِي السَّمَاوَاتِ وَفِي الْأَرْضِ ۖ يَعْلَمُ سِرَّكُمْ وَجَهْرَكُمْ وَيَعْلَمُ مَا تَكْسِبُونَ ﴿٣﴾

Na Yeye Ndiye Allaah mbinguni na ardhini, Anajua ya siri yenu na ya dhahiri yenu, na Anajua yale mnayoyachuma. (6:3).

 

 

Kauli ya kwanza:

 

Maana yake ni: Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) ni Ilaah (Apasaye kuabudiwa kwa haki) Anayeabudiwa mbinguni na ardhini kwa sababu Yeye Pekee Ndiye Mwabudiwa wa haki katika ardhi na mbingu, kwa ushahidi wa Kauli Yake (تعالى):

وَهُوَ الَّذِي فِي السَّمَاءِ إِلَـٰهٌ وَفِي الْأَرْضِ إِلَـٰهٌ ۚ  

Na Yeye Ndiye Mwabudiwa wa haki mbinguni na ardhini pia (Ndiye Huyo Huyo) Ilaah. [Az-Zukhruf (43:84)]

 

[Al-Qurtwubiy, Ibn Kathiyr, Ash-Shanqiytwiy, Ibn Al-Anbaariy na wengineo. Taz. Al-Jaami’u li-Ahkaamil-Qur-aan (6/390), Tafsiyr Al-Qur-aan Al-‘Adhwiym (3/240), Adhwaau Al-Bayaan (7/4)]  

 

 

Kauli Ya Pili: 

 

Kwamba maana yake ni: Yeye Allaah Anajua siri zenu mbinguni na ardhini, na ushahidi ni Kauli Yake:

(تعالى)  

 

قُلْ أَنزَلَهُ الَّذِي يَعْلَمُ السِّرَّ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ  

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Ameiteremsha Ambaye Anajua siri katika mbingu na ardhi. [Al-Furqaan (25:6)]

 

Kwa kuzingatia kwamba Kauli Yake: 

 

mbinguni na ardhini[Al-An’aam (6:3)] inahusiana na: Anajua siri zenu.”

 

Na amesema Imaam Ad-Daaniyy: Na imesemwa kuwa maana yake ni: Yeye Ndiye Mwabudiwa mbinguni na ardhini.

 

Na kadhaalika, Al-Ashmuwniyy kaunga mkono ufafanuzi huo.

 

Na amesema An-Nahhaas kuwa kauli hiyo ni bora katika yaliyoelezwa juu ya Aayah hiyo.

 

[Al-Muktafaa Fiy Al-Waqf Wal-Ibtidaa Fiy KitaabiLLaah ‘Azza Wa Jalla (273), Manaaru Al-Hudaa Fiy Bayaan Al-Waqf Wal-Ibtidaa (265). Adhwaau Al-Bayaan Fiy Iydhwaah Al-Qur-aan bil-Qur-aan (4/7)]   

 

 

Kauli Ya Tatu:

 

Kwamba maana yake ni:  Yeye Allaah, Ambaye Yeye Yuko mbinguni na katika ardhi, Anajua siri zenu na ya dhahiri yenu katika ardhi.  Naye Yuko juu ya ‘Arsh Yake Akiwa juu ya Viumbe Vyake wote, Akiwa Anajua siri za watu wa ardhini na ya dhahiri yao, hakuna kinachofichika Kwake katika hayo. Na ushahidi ni Kauli Yake (تعالى):

 

أَأَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يَخْسِفَ بِكُمُ الْأَرْضَ فَإِذَا هِيَ تَمُورُ﴿١٦﴾

Je, mnadhani mko katika amani na (Allaah) Aliyeko mbinguni kwamba Hatokudidimizeni ardhini, tahamaki hiyo inatikisika?

 

 

أَمْ أَمِنتُم مَّن فِي السَّمَاءِ أَن يُرْسِلَ عَلَيْكُمْ حَاصِبًا ۖ فَسَتَعْلَمُونَ كَيْفَ نَذِيرِ﴿١٧﴾

Au mnadhani mko katika amani na (Allaah) Aliyeko mbinguni kwamba Hatokutumieni tufani ya mawe? Basi mtajua vipi Maonyo Yangu!

 

[Al-Mulk (67:16-17)]

 

 

Na Kauli Yake (تعالى):

 

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴿٥﴾

Ar-Rahmaan (Mwingi wa Rahmah), Yuko juu (Istawaa) ya ‘Arsh. [Twaahaa (20:5)]

 

 

Kauli Ya Nne: 

 

Ina maana kutangulizwa na kuakhirishwa, yaani: Yeye Allaah Anajua siri zenu na ya dhahiri yenu mbinguni na ardhini. Na hii ni kauli ya Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما) .

 

Kauli iliyo na nguvu kabisa katika kauli hizo nne ni:

 

Kauli ya kwanza ambayo ni kauli ya wengi katika Mufassariyn, pamoja na kwamba kuna uwezekano wa kauli nyingine katika hizo kwa sababu kila kauli ina ushahidi wake katika Qur-aan.

 

Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah (رحمه الله) amesema: “Maimaam wakubwa kama Imaam Ahmad na wengineo wameifasiri kwamba: “Kuwa Yeye ni Mwabudiwa mbinguni na ardhini.” [Al-Furqaan Bayna Awliyaair-Rahmaan Wa-Awliyaa Ash-Shaytwaan (244)]

 

Ibn Kathiyr (رحمه الله)  amesema “Kauli iliyo sahihi kabisa ni kwamba: “Allaah Anaombwa mbinguni na ardhini, yaani Anaabudiwa,   Anapwekeshwa, Anakiriwa kwa Uabudiwa na Anaitwa Allaah. Naye Anaombwa na wote kwa utashi na khofu isipokuwa wakanushaji katika majini na wanaadamu.”  [Tafsiyr Al-Qur-aan Al-‘Adhwiym, (3/240)]  

 

 

Share