01-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swalaah: Mlango Nyakati Za Swalaah

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلصَّلَاةِ

Kitabu cha Swalaah

 

بَابُ اَلْمَوَاقِيتِ

Mlango Nyakati Za Swalaah

 

 

 

127.

عَنْ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ عَمْرِوٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا‏ ، أَنَّ نَبِيَّ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم  قَالَ: {وَقْتُ اَلظُّهْرِ إِذَا زَالَتْ اَلشَّمْسُ‏،  وَكَانَ ظِلُّ اَلرَّجُلِ كَطُولِهِ  مَا لَمْ يَحْضُرْ اَلْعَصْرُ‏،  وَوَقْتُ اَلْعَصْرِ مَا لَمْ تَصْفَرَّ اَلشَّمْسُ‏،  وَوَقْتُ صَلَاةِ اَلْمَغْرِبِ مَا لَمْ يَغِبْ اَلشَّفَقُ‏،  وَوَقْتُ صَلَاةِ اَلْعِشَاءِ إِلَى نِصْفِ اَللَّيْلِ اَلْأَوْسَطِ‏،  وَوَقْتُ صَلَاةِ اَلصُّبْحِ مِنْ طُلُوعِ اَلْفَجْرِ مَا لَمْ تَطْلُعْ اَلشَّمْسُ}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ

وَلَهُ مِنْ حَدِيثِ بُرَيْدَةَ فِي اَلْعَصْرِ: {وَالشَّمْسُ بَيْضَاءُ نَقِيَّةٌ}

وَمِنْ حَدِيثِ أَبِي مُوسَى: {وَالشَّمْسُ مُرْتَفِعَةٌ}

Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema: Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Wakati wa Swalaah ya Adhuhuri[1] ni jua linapopinduka (meridani) na kivuli cha mtu kuwa kama urefu wake, madamu haujaingia wakati wa Swalaah ya Alasiri. Wakati wa Swalaah ya Alasiri ni muda jua halijawa njano (machweo). Wakati wa Swalaah ya Magharibi (machweo)[2] ni katika wakati wa mawingu hayajapotea[3]. Wakati wa Swalaah ya ‘Ishaa hadi nusu ya usiku. Wakati wa Swalaah ya Alfajiri ni tangu kuchomoza Alfajiri mpaka wakati wa kuchomoza jua.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

Buraydah[4] amesema katika Hadiyth nyengine kuhusu Alasiri   kuwa: “Jua likiwa jeupe angavu[5].” [Imetolewa na Muslim]

 

 

Na Hadiyth ya Abuu Muwsaa[6] amesema kuhusu wakati wa Swalaah ya Alasiri: “Wakati jua liko juu.”[7] [Imetolewa na Muslim katika Hadiyth ndefu inayosema: “Kisha akamuamrisha akakimu Alasiri”]

 

 

 

128.

وَعَنْ أَبِي بَرْزَةَ الْأَسْلَمِيِّ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم  يُصَلِّيَ اَلْعَصْرَ‏، ثُمَّ يَرْجِعُ أَحَدُنَا إِلَى رَحْلِهِ  فِي أَقْصَى اَلْمَدِينَةِ  وَالشَّمْسُ حَيَّةٌ‏،  وَكَانَ يَسْتَحِبُّ أَنْ يُؤَخِّرَ مِنْ اَلْعِشَاءِ‏،  وَكَانَ يَكْرَهُ اَلنَّوْمَ قَبْلَهَا  وَالْحَدِيثَ بَعْدَهَا‏،  وَكَانَ يَنْفَتِلُ مِنْ صَلَاةِ اَلْغَدَاةِ حِينَ يَعْرِفُ اَلرَّجُلُ جَلِيسَهُ‏،  وَيَقْرَأُ بِالسِّتِّينَ إِلَى اَلْمِائَةِ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ 

وَعِنْدَهُمَا مِنْ حَدِيثِ جَابِرٍ: {وَالْعِشَاءَ أَحْيَانًا وَأَحْيَانًا: إِذَا رَآهُمْ اِجْتَمَعُوا عَجَّلَ‏، وَإِذَا رَآهُمْ أَبْطَئُوا أَخَّرَ‏،  وَالصُّبْحَ: كَانَ اَلنَّبِيَّ ‏ صلى الله عليه وسلم  يُصَلِّيهَا بِغَلَسٍ}  

وَلِمُسْلِمٍ مِنْ حَدِيثِ أَبِي مُوسَى: {فَأَقَامَ اَلْفَجْرَ حِينَ اِنْشَقَّ اَلْفَجْرُ‏، وَالنَّاسُ لَا يَكَادُ يَعْرِفُ بَعْضُهُمْ بَعْضًا}

Kutoka kwa Abuu Barzah Al-Aslamiy[8] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akiswali Swalaah ya Alasiri na baada ya Swalaah, mmoja wetu alirejea nyumbani kwake mwisho kabisa wa Madiynah na kufika wakati jua bado linang’aa, na alipenda kuichelewesha Swalaah ya ‘Ishaa, na hakupenda kulala usingizi kabla yake na kuzungumza baada yake.[9] Na baada ya Swalaah ya Fajr alikuwa akitoka wakati mtu aliweza kumtambua mwenzie aliyekaa karibu naye, na alikuwa akisoma Aayah sitini hadi mia za Qur-aan katika Swalaah ya Fajr.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Kwao wawili (Al-Bukhaariy na Muslim) wamepokea Hadiyth ya Jaabir kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akiiwahisha Swalaah ya ‘Ishaa na mara nyingine akiichelewesha, kila alipowaona watu wamekusanyika ili kuswali ‘Ishaa, aliiswali mapema, na watu wakiwa wamechelewa, naye aliichelewesha. Swalaah ya Fajr aliiswali wakati bado kungali kiza.”[10]

 

Muslim alimnukuu Abuu Muwsaa (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ): “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akiswali Fajr wakati wa kupambazuka ambapo watu hawakutambuana.”

 

 

 

129.

وَعَنْ رَافِعِ بْنِ خَدِيجٍ  رَضِيَ اللهُ عَنْهُ قَالَ: {كُنَّا نُصَلِّي اَلْمَغْرِبَ مَعَ اَلنَّبِيِّ ‏ صلى الله عليه وسلم  فَيَنْصَرِفُ أَحَدُنَا وَإِنَّهُ لَيُبْصِرُ مَوَاقِعَ نَبْلِهِ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ 

Kutoka kwa Raafi’ bin Khadiyj[11] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Tulikuwa tukiswali Magharibi na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) halafu mmoja wetu alitoka nje ya Msikiti akaweza kuona mahali mshale ulipoangukia.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

130.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {أَعْتَمَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم  ذَاتَ لَيْلَةٍ بِالْعَشَاءِ‏،  حَتَّى ذَهَبَ عَامَّةُ اَللَّيْلِ‏،  ثُمَّ خَرَجَ‏، فَصَلَّى‏، وَقَالَ: "إِنَّهُ لَوَقْتُهَا لَوْلَا أَنْ أَشُقَّ عَلَى أُمَّتِي"}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alichelewesha Swalaah ya ‘Ishaa hadi sehemu kubwa ya usiku ilipopita, halafu akenda nje akaswali Swalaah ya ‘Ishaa akasema: “Huu ndio wakati wake[12] ingekuwa siyo kuogopea mashaka kwa Ummah wangu.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

131.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ  رَضِيَ اللهُ عَنْهُ  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم   {إِذَا اِشْتَدَّ اَلْحَرُّ فَأَبْرِدُوا بِالصَّلَاةِ‏، فَإِنَّ شِدَّةَ اَلْحَرِّ مِنْ فَيْحِ جَهَنَّمَ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Joto likiwa kali lipoze kwa Swalaah[13] kwani ukali wa joto hutoka kwenye pumzi ya Jahannam.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

 

132.

وَعَنْ رَافِعِ بْنِ خَدِيجٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم   {أَصْبِحُوا بِالصُّبْحِ فَإِنَّهُ أَعْظَمُ لِأُجُورِكُمْ}  رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ‏، وَصَحَّحَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ‏، وَابْنُ حِبَّانَ

 

Kutoka kwa Raafi’ bin Khadiyj (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Pambazukeni kwa Swalaah ya Alfajiri[14] kwani hiyo ndio kubwa zaidi kwa ujira wenu.” [Imetolewa na Al-Khamsah na wakaipa daraja la Swahiyh At-Tirmidhiy na Ibn Hibbaan] 

 

 

 

133.

‏ وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم قَالَ: {مَنْ أَدْرَكَ مِنْ اَلصُّبْحِ رَكْعَةً قَبْلِ أَنْ تَطْلُعَ اَلشَّمْسُ فَقَدْ أَدْرَكَ اَلصُّبْحَ‏، وَمَنْ أَدْرَكَ رَكْعَةً مِنْ اَلْعَصْرِ قَبْلَ أَنْ تَغْرُبَ اَلشَّمْسُ فَقَدْ أَدْرَكَ اَلْعَصْرَ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ 

وَلِمُسْلِمٍ عَنْ عَائِشَةَ نَحْوَهُ‏، وَقَالَ: "سَجْدَةً" بَدَلَ "رَكْعَةً". ثُمَّ قَالَ: وَالسَّجْدَةُ إِنَّمَا هِيَ اَلرَّكْعَةُ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mwenye kuipata Rakaa moja ya Swalaah ya Alfajiri kabla jua halijachomoza, anakuwa ameipata Swalaah ya Alfajiri kwa wakati wake, na mtu anayeswali Rakaa ya Alasiri kabla ya jua halijatua anakuwa ameipata Swalaah ya Alasiri.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Na katika Muslim alipokea masimulizi kama hayo kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) na amesema: “Sajdah badala ya Rakaa.” Kisha amesema: “Sajdah inaashiria Rakaa.”

 

 

 

134.

وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ اَلْخُدْرِيِّ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ  قَالَ: سَمِعْتَ رَسُولَ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم  يَقُولُ: {لَا صَلَاةَ بَعْدَ اَلصُّبْحِ حَتَّى تَطْلُعَ اَلشَّمْسُ وَلَا صَلَاةَ بَعْدَ اَلْعَصْرِ حَتَّى تَغِيبَ اَلشَّمْسُ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

وَلَفْظُ مُسْلِمٍ: {لَا صَلَاةَ بَعْدَ صَلَاةِ اَلْفَجْرِ}  

وَلَهُ عَنْ عُقْبَةَ بْنِ عَامِرٍ: {ثَلَاثُ سَاعَاتٍ كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم  يَنْهَانَا أَنْ نُصَلِّي فِيهِنَّ‏، وَأَنْ  نَقْبُرَ فِيهِنَّ مَوْتَانَا: حِينَ تَطْلُعُ اَلشَّمْسُ بَازِغَةً حَتَّى تَرْتَفِعَ‏، وَحِينَ يَقُومُ قَائِمُ اَلظَّهِيرَةِ حَتَّى تَزُولَ   اَلشَّمْسُ‏، وَحِينَ تَتَضَيَّفُ  اَلشَّمْسُ لِلْغُرُوبِ}  

وَالْحُكْمُ اَلثَّانِي عِنْدَ "اَلشَّافِعِيِّ" مِنْ:

حَدِيثِ أَبِي هُرَيْرَةَ بِسَنَدٍ ضَعِيفٍ. وَزَادَ: {إِلَّا يَوْمَ اَلْجُمْعَةِ} 

وَكَذَا لِأَبِي دَاوُدَ: عَنْ أَبِي قَتَادَةَ نَحْوُهُ 

Kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al Khudriyy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema nimemsikia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akisema: “Hakuna Swalaah baada ya Swalaah ya Alfajiri hadi jua kuchomoza[15], wala hakuna Swalaah baada ya Swalaah ya Alasiri hadi jua lizame.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Na tamshi la Muslim amesema: “Hakuna Swalaah baada ya Swalaah ya Alfajiri.”

 

Na Muslim amenukuu Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir[16] kuwa: “Nyakati tatu ambazo Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alitukataza kuswali wala kuzika[17] wafu wetu: (a) Wakati wa kuchomoza jua mpaka lipae. (b) Wakati jua liko juu kati kati hadi lipinduke. (c) Wakati jua linakaribia kuzama (kuingia Magharibi).”

 

Hukmu ya pili kwa Ash-Shaafi’y[18] inatokana na Hadiyth ya Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) kwa Isnaad dhaifu, akaongezea: “Isipokuwa siku ya Ijumaa.” Kadhalika Abuu Daawuwd alisimulia hivyo kutoka kwa Abuu Qataadah.

 

 

 

135.

وَعَنْ جُبَيْرِ بْنِ مُطْعِمٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم   {يَا بَنِي عَبْدِ مَنَافٍ‏، لَا تَمْنَعُوا أَحَدًا طَافَ بِهَذَا اَلْبَيْتِ وَصَلَّى أَيَّةَ سَاعَةٍ شَاءَ مِنْ لَيْلٍ أَوْ نَهَارٍ}  رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ‏، وَصَحَّحَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ‏، وَابْنُ حِبَّانَ 

Kutoka kwa Jubayr bin Mutw’im[19] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Enyi Baniy ‘Abdil-Manaaf, msimzuie yeyote kutufu Nyumba (Al-Ka’bah) hii na akaswali saa yoyote anayotaka, usiku au mchana.” [Imetolewa na Al-Khamsah, na wakaisahihisha At-Tirmidhiy na Ibn Hibbaan]

 

 

 

136.

وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا‏، عَنْ اَلنَّبِيِّ ‏ صلى الله عليه وسلم  قَالَ: {اَلشَّفَقُ اَلْحُمْرَةُ}  رَوَاهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ وَصَحَّحَ اِبْنُ خُزَيْمَةَ وَغَيْرُهُ وَقْفَهُ 

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mawingu (ya machweo ya jua) ni wekundu.” [Imetolewa na Ad-Daaruqutwniy, na akaisahihisha Ibn Khuzaymah, na wengine waliipa daraja la Mawquwf]

 

 

 

137.

وَعَنْ اِبْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم  {اَلْفَجْرُ فَجْرَانِ: فَجْرٌ يُحَرِّمُ اَلطَّعَامَ وَتَحِلُّ فِيهِ اَلصَّلَاةُ‏، وَفَجْرٌ تَحْرُمُ فِيهِ اَلصَّلَاةُ ‏ أَيْ: صَلَاةُ اَلصُّبْحِ ‏ وَيَحِلَّ فِيهِ اَلطَّعَامُ}  رَوَاهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ‏، وَالْحَاكِمُ‏، وَصَحَّحَاهُ 

وَلِلْحَاكِمِ فِي حَدِيثِ جَابِرٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ  نَحْوُهُ‏، وَزَادَ فِي اَلَّذِي يُحَرِّمُ اَلطَّعَامَ: {إِنَّهُ يَذْهَبُ مُسْتَطِيلاً فِي اَلْأُفُقِ}  وَفِي اَلْآخَرِ: {إِنَّهُ كَذَنَبِ اَلسِّرْحَان}

Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Alfajiri ni Alfajiri mbili: Alfajiri moja inaharamisha chakula na inahalalisha Swalaah, na Alfajiri nyingine inaharamisha kuswali ndani yake: yaani Swalaah ya Alfajiri wakati huo chakula kinakuwa halali.” [Imetolewa na Ibn Khuzaymah na Al-Haakim aliyeisahihisha]

 

Na Al-Haakim alipokea Hadiyth ya Jaabir mfano wake, na ikaongeza katika ambayo inaharamisha kula: “Kumesambaa sana katika pambizo upeo.”

 

Na katika nyingine amesema: “Ni kama mkia wa mbwa.”

 

 

 

138.

وَعَنْ اِبْنِ مَسْعُودٍ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم   {أَفْضَلُ اَلْأَعْمَالِ اَلصَّلَاةُ فِي أَوَّلِ وَقْتِهَا}  رَوَاهُ اَلتِّرْمِذِيُّ‏، وَالْحَاكِمُ. وَصَحَّحَاهُ   .

وَأَصْلُهُ فِي "اَلصَّحِيحَيْنِ" 

Kutoka kwa Ibn Mas’uwd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Amali bora kabisa ni Swalaah mwanzo wa wakati wake[20].” [Imetolewa na At-Tirmidhiy na Al-Haakim aliyeisahihisha] na chanzo chake ni katika Swahiyh mbili.

 

 

 

139.

وَعَنْ أَبِي مَحْذُورَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ  أَنَّ اَلنَّبِيَّ ‏ صلى الله عليه وسلم  قَالَ: {أَوَّلُ اَلْوَقْتِ رِضْوَانُ اَللَّهُ‏، وَأَوْسَطُهُ رَحْمَةُ اَللَّهِ‏ ، وَآخِرُهُ عَفْوُ اَللَّهِ}  أَخْرَجَهُ اَلدَّارَقُطْنِيُّ بِسَنَدٍ ضَعِيفٍ جِدًّا 

وَلِلتِّرْمِذِيِّ مِنْ حَدِيثِ اِبْنِ عُمَرَ نَحْوُهُ‏، دُونَ اَلْأَوْسَطِ‏، وَهُوَ ضَعِيفٌ أَيْضًا 

Kutoka kwa Abuu Mahdhuwrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Wakati wa mwanzo ni radhi ya Allaah, wa katikati yake ni wa Rahmah za Allaah, na wa mwisho wake ni msamaha wa Allaah.” [Imetolewa na Ad-Daaruqutwniy kwa Isnaad dhaifu sana]

 

Na At-Tirmidhiy alisimulia hivyo hivyo, na kutokana na Hadiyth ya Ibn ‘Umar, bila kutaja wakati wa kati na kati. [Hii Hadiyth pia ni dhaifu]

 

 

 

140.

وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا أَنَّ رَسُولَ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم  قَالَ: {لَا صَلَاةَ بَعْدَ اَلْفَجْرِ إِلَّا سَجْدَتَيْنِ}  أَخْرَجَهُ اَلْخَمْسَةُ‏، إِلَّا النَّسَائِيُّ 

وَفِي رِوَايَةِ عَبْدِ اَلرَّزَّاقِ: {لَا صَلَاةَ بَعْدَ طُلُوعِ اَلْفَجْرِ إِلَّا رَكْعَتَيْ اَلْفَجْرِ}

وَمِثْلُهُ لِلدَّارَقُطْنِيّ عَنْ اِبْنِ عَمْرِوِ بْنِ اَلْعَاصِ 

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hakuna Swalaah baada ya Alfajiri isipokuwa sajdah mbili (Rakaa mbili za Alfajr)[21].” [Imetolewa na Al-Khamsah isipokuwa An-Nasaaiy]

 

 

Katika Riwaayah nyingine ‘Abdur-Razzaaq pia alisimulia: “Hakuna Swalaah baada ya kupambazuka Alfajiri isipokuwa Rakaa mbili za Sunnah ya Alfajir[22]i.”

 

Mfano wa Hadiyth hiyo imepokewa na Ad-Daaruqutwniy kutoka kwa ‘Amr bin Al-‘Aasw.

 

 

 

141.

وَعَنْ أَمْ سَلَمَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا قَالَتْ: {صَلَّى رَسُولُ اَللَّهِ ‏ صلى الله عليه وسلم اَلْعَصْرَ‏، ثُمَّ دَخَلَ بَيْتِي‏، فَصَلَّى رَكْعَتَيْنِ‏، فَسَأَلْتُهُ‏، فَقَالَ: "شُغِلْتُ عَنْ رَكْعَتَيْنِ بَعْدَ اَلظُّهْرِ‏، فَصَلَّيْتُهُمَا اَلْآنَ"‏، قُلْتُ: أَفَنَقْضِيهِمَا إِذَا فَاتَتْنَا‏ ؟ قَالَ: "لَا"} أَخْرَجَهُ أَحْمَدُ 

وَلِأَبِي دَاوُدَ عَنْ عَائِشَةَ بِمَعْنَاهُ

Kutoka kwa Ummu Salamah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema, Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliswali Alasiri, kisha akaja nyumbani kwangu, akaswali Rakaa mbili, halafu nikamuuliza juu ya hizo, naye akasema: “Nilishughulishwa na Rakaa mbili za Sunnah baada ya Swalaah ya Adhuhuri, kwa hivyo nimeziswali sasa.” Nikasema: Tuzilipe tukizikosa? Akasema: “Hapana[23].” [metolewa na Ahmad]

Naye Abuu Daawuwd amepokea Hadiyth ya ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) yenye maana sawa na hiyo.

 

 

 

[1] Inamaanisha kuwa wakati wa Swalaah ya Adhuhuri ni hadi kivuli kiwe na ukubwa sawa (kutoka wakati jua linapanda mpaka wakati ukubwa wa mtu na wa kivuli chake viwe sawa), na baada ya pale, wakati wa Swalaah ya ‘Aswr huanza. Baadhi ya ‘Ulamaa wanahesabu wakati wa Swalaah ya Adhuhuri ni mpaka kivuli kiwe na ukubwa mara mbili, lakini hii haijathibitishwa na Hadiyth yoyote sahihi.

 

 

[2] Hadiyth hii inasema kuwa, Swalaah ya Maghrib pia ina nyakati mbili, mwanzo na mwisho. Katika Hadiyth ya Jibriyl wakati mmoja tu umetajwa kwa ajili ya Swalaah ya Maghribi mara zote mbili, lakini hii ilikuwa ni wakati wa mwanzo wa Uislaam. Baadaye kule Al-Madiynah, wakati wa Swalaah ya Maghribi ulirefushwa.

 

[3] اَلشَّفَقُ‏ Wakati wa mwanga wa jua unapofifia yaani ni ule wekundu katika upeo wa Maghribi wakati wa jioni jua linapotua, kama maelezo yanavyosimuliwa na Ad-Daaraqutniy.

 

[4] Huyu Buraydah ndiye Abuu ‘Abdillaah Buraydah bin Al-Husayb Al-Aslami. Alisilimu yeye pamoja na wenziwe themanini pale Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alipompita yeye wakati akihama kwenda Al-Madiynah. Baadaye alikuja kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) baada ya Vita vya Uhud, na akashiriki katika Vita zingine. Na pia alihudhuria Al-Hudaybiyyah na pia Bay’atu Ar-Ridhwaan. Alilowea Basra, kisha akaenda na msafara hadi Khurasaan na akalowea Marwa alikofia na akazikwa mnamo mwaka 62 au 63 A.H.

 

 

[5] Inamaanisha kuwa Swalaah ya ‘Aswr ni sharti iswaliwe mapema. Baada ya kivuli chenye ukubwa sawa, wakati unatosheleza kuswali rakaah nne tu ambayo ndiyo kawaida kati ya Swalaah ya Dhuhuri na ya ‘Aswr. Baada ya hapo, wakati wa Swalaah ya ‘Aswr huanza.

 

[6] Abuu Muwsaa ndiye ‘Abdullaah bin Qays Al-Ash’ariyy aliyekuwa mmoja wa Swahaba maarufu kabisa. Alihamia Habasha (Abyssinia) na baadaye akaja kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kule Khaybar. Aliteuliwa kutawala Zabid na ‘Aden, na kisha akawa Gavana wa ‘Umar kule Kuwfah na Basra. Alisaidia kuikomboa Tastar na miji mingine kadhaa. Huenda alifariki mnamo mwaka 42 A.H

 

[7] Simulizi zote zilizotajwa zimethibitisha kuwa kila Swalaah ina “Wakati wa mwanzo” na “Wakati wa mwisho” kuiswali Swalaah ile; lakini kila Swalaah sharti iswaliwe katika wakati wake wa mwanzo.

 

[8] Abuu Barzah Al-Aslamiyy ndiye Nadla bin ‘Ubayd. Alisilimu mapema sana na akashuhudia kutekwa kwa Makkah na Vita zingine muhimu. Alilowea Basra, na baadaye Khurasaan, na akafia Marwa au Basra mnamo mwaka 60 au 64 A.H.

 

[9] Baada ya Swalaah ya ‘Ishaa imekatazwa kuongea. Sababu ya katazo hili ni kwamba dhambi za Muumini zimesamehewa baada ya kuswali, na bora kuenda kitandani kuliko kuongea na kushiriki katika mambo ya kidunia. Baada ya kuswali ‘Ishaa, mtu kuenda zake kulala kunampa faida maradufu; kwanza ni kujiepusha na dhambi, na pili ubora Swalaah ndiyo ihesabiwe kuwa ni tendo lake la mwisho kabla hajalala.

 

 

[10] Kuhusu wakati wa Swalaah ya Fajr, yapo maoni tofauti ya Swahaba wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Katika Hadiyth hii, hilo neno la Kiarabu la   غَلَسٍ inamaanisha wakati ambao kupambazuka kunaonekana katika giza la usiku.

 

[11] Raafi’ bin Khadiyj ndiye Answari aliyeitwa Abuu ‘Abdillaah. Alikosa Vita ya Badr kwa sababu ya umri wake kuwa mdogo, lakini akashiriki katika Vita ya Uhud na Vita vilivyofuata. Alifariki mnamo mwaka wa 73 au 74 A.H akiwa na umri wa miaka 86.

 

[12] Ni ubora kuiswali Swalaah ya ‘Ishaa wakati wa mwisho kadiri iwezekanavyo. Amri hii ni maalumu kwa Swalaah ya ‘Ishaa tu, na siyo kwa Swalaah nyingine yoyote. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akingoja na kuichelewesha Swalaah hii.

 

 

[13] Kuna maoni tofauti kuhusu kuswali Dhuhuri mapema au mwishoni wakati wa majira ya joto. Lakini ni sawa kuichelewesha kidogo hadi mtu aweze kutembea katika vivuli vya kuta. Kwa mujibu wa Abuu Daawuwd na An-Nasaaiy: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa akiichelewesha Swalaah ya Dhuhuri hadi kivuli kilipokuwa na urefu wa hatua tatu au tano.”

 

[14] Hii inamaanisha kuwa mwanga wa Alfajiri sharti uonekane waziwazi na kusiweko shaka yoyote juu yake. Kwa hivyo Hadiyth hii haipingani na hiyo Hadiyth ya “Giza” hapo nyuma. Kipengele kingine ni kuwa Swalaah sharti ianze kuswaliwa wakati ikiwa giza, na visomo virefushwe mpaka mwanga wa Alfajiri uonekane waziwazi.

 

[15] . Maana yake hii ni kuwa, tangu kunapopambazuka mpaka kuchomoza jua, na tangu ‘Aswr hadi jua linapokuchwa, Swalaah za khiari (Nawaafil) zozote haziruhusiwi. Rakaah mbili kabla ya Swalaah ya faradhi ya Fajr hazimo katika amri hii, kama ilivyothibitishwa kutoka kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ). Ingawa Rakaah hizi mbili huswaliwa kabla ya Swalaah ya faradhi (Fajr), ukizikosa hizi unaweza kuziswali baada ya Swalaah ya fardhi kama ilivyoripotiwa katika At-Tirmidhiy.

 

 

[16] ‘Uqbah bin ‘Aamir alikuwa ni Junani aliyepewa jina la utani Abuu Hammad au Abu ‘Aamir. Alisilimu, akahama na kuandamana na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) mwanzoni kabisa. Aliisoma sana Qur-aan na alikuwa mtaalamu wa Kanuni za Shariy’ah na mirathi, na alikuwa msomi na mshairi. Alipewa ardhi Basra, na alishiriki katika Siffin pamoja na Mu’aawiyah. Baadaye aliitawala Misri kwa niaba ya Mu’aawiyah kwa miaka mitatu, na akawa mkuu wa misafara ya baharini. Alifariki mwaka 58 A.H. kule Misri, na akazikwa Al-Muqtam.

 

[17] Hapa, “Kuzika” maana yake ni “Swalaah za maiti”. Swalaah za maiti zisiswaliwe katika nyakati hizo, lakini kumzika maiti inaruhusiwa. Lakini kwa mujibu wa Wanazuoni wengine, hata kuzika hakuruhusiwi. Kwa hivyo, katika hali hizo, inamaanisha kuwa hata maziko yasifanyike katika nyakati hizo. Lakini iwapo nyakati hizi zimewadia katikati ya shughuli za maziko, au hakuna njia nyingine, basi kuzika kunaruhusiwa.

 

[18] Amri ya pili maana yake wakati wa katikati ya siku, ambapo hakuna Swalaah inayoruhusiwa kuswaliwa wakati huu. Lakini Ijumaa haimo katika amri hii. Siku za Ijumaa inaruhusiwa kuswali wakati jua liko juu kabisa, kama inavyodhihirisha Hadiyth iliyoripotiwa na Abuu Hurayrah.

 

[19] Jubayr bin Mutw’im ndiye Abuu Muhammad au Abuu ‘Umayyah Jubayr bin Mutw’im bin ‘Aad bin Nawfal Al-Quraysh. Alikuwa mstahamilivu sana, mjuzi wa ukoo wa Maquraysh. Alisilimu kabla ya Fat-h (kutekwa kwa Makkah) na alilowea Al-Madiynah, na akafia huko mnamo mwaka 54 au 57 au 59 A.H.

 

[20] Katika Hadiyth hii, Swalaah inayoswaliwa katika nyakati zake za mwanzo huhesabika kuwa ni tendo bora sana. Katika Hadiyth zingine, Iymaan, Swadaqah na Jihaad huhesabika kuwa matendo bora sana. Hizi Hadiyth zinaonyesha Iymaan ni tendo la sifa, Swalaah ni tendo la mwili, Swadaqah ni tendo la mali, na Jihaad ni tendo la ujana na afya. Kwa hivyo haya yote ni matendo makubwa na bora kwa namna zake na mahala pake; na hakuna mapingano.

 

[21] Maana yake ni kwamba, baada ya kupambazuka, Swalaah za khiari (Nawaafil) haziruhusiwi, lakini Rakaa mbili za Sunnah zinakubaliwa, na zinaweza kuswaliwa baada ya Swalaah ya Fajr, kama rejeo la At-Tirmidhiy lilivyotaja hapo nyuma

 

[22] Hizo Rakaa mbili ni zile za Sunnah kabla ya Swalaah ya faradhi ya Fajr, ambayo Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kamwe hakuwa anaikosa hata iwe baada ya kupambazuka, kama ilivyoonyeshwa na Hadiyth hii na Hadiyth zingine.

 

[23] Hadiyth hii inatuarifu kwamba, baada ya Swalaah ya ‘Aswr, kuswali Swalaah za ziada au za khiari tulizozikosa ni kwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) tu, watu wengine hawaruhusiwi kulipa Swalaah za khiari. Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) aliiswali Swalaah ile kwa sababu watu fulani wa kabila la Abdul-Qays walimzuru na walileta vitu vya Swadaqah, kwa hivyo ziara yao ile na ugawanyaji wa vitu walivyoleta ulimchelewesha.

 

 

Share