03-Buluwgh Al-Maraam: Kitabu Cha Swalaah: Mlango Wa Masharti Ya Swalaah

بُلُوغُ الْمَرام

Buluwgh Al-Maraam

 

كِتَابُ اَلصَّلَاةِ

Kitabu Cha Swalaah

 

بَـــابُ شُــرُوطِ اَلصَّلَاةِ

03-Mlango Wa Masharti Ya Swalaah

 

 

 

 

 

161.

عَنْ عَلِيِّ بْنِ طَلْقٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم {إِذَا فَسَا أَحَدُكُمْ فِي اَلصَّلَاةِ فَلْيَنْصَرِفْ ، وَلْيَتَوَضَّأْ ، وَلْيُعِدْ اَلصَّلَاةَ}  رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ

Kutoka kwa ‘Aliy bin Twalq[1] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mmoja wenu akitoa upepo katika Swalaah aondoke akatawadhe, na arudie kuswali[2].” [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) na akaisahihisha Ibn Hibbaan]

 

 

 

162.

وَعَنْ عَائِشَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا عَنْ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم  قَالَ : {لَا يَقْبَلُ اَللَّهُ صَلَاةَ حَائِضٍ إِلَّا بِخِمَارٍ}  رَوَاهُ اَلْخَمْسَةُ إِلَّا النَّسَائِيُّ ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ

Kutoka kwa ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Allaah haikubali Swalaah ya mwanamke aliyebaleghe mpaka avae khimaar[3] (shungi la kufunika kichwa na mwili).” [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad) isipokuwa An-Nasaaiy, na akaisahihisha Ibn Khuzaymah]

 

 

 

163.

وَعَنْ جَابِرٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  أَنَّ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم  قَالَ لَهُ : {إِنْ كَانَ اَلثَّوْبُ وَاسِعًا فَالْتَحِفْ بِهِ}   يَعْنِي : فِي اَلصَّلَاةِ  وَلِمُسْلِمٍ : {"فَخَالِفْ بَيْنَ طَرَفَيْهِ  وَإِنْ كَانَ ضَيِّقًا فَاتَّزِرْ بِهِ "}  . مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ .

وَلَهُمَا مِنْ حَدِيثِ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  {لَا يُصَلِّي أَحَدُكُمْ فِي اَلثَّوْبِ اَلْوَاحِدِ لَيْسَ عَلَى عَاتِقِهِ مِنْهُ شَيْء}

Kutoka kwa Jaabir (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Iwapo nguo ni pana, jizungushie mwili wote (yaani wakati wa kuswali)

Na katika tamshi la Muslim: “Kutanisha ncha mbili, na ikiwa inabana, izungushie kiunoni.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Nao wawili (Al-Bukhaariy na Muslim) wamenukuu Hadiyth ya Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ): “Asiswali mmoja wenu na vazi moja tu lisilofunika mabega.”

 

 

 

164.

وَعَنْ أُمِّ سَلَمَةَ  رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهَا ; أَنَّهَا سَأَلَتْ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم   {أَتُصَلِّي اَلْمَرْأَةُ فِي دِرْعٍ وَخِمَارٍ ، بِغَيْرِ إِزَارٍ  ؟ قَالَ : "إِذَا كَانَ اَلدِّرْعُ سَابِغًا يُغَطِّي ظُهُورَ قَدَمَيْهَا}  أَخْرَجَهُ أَبُو دَاوُدَ وَصَحَّحَ اَلْأَئِمَّةُ وَقْفَهُ

Kutoka kwa Ummu Salamah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) amesema kuwa alimuuliza Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): “Je, mwanamke anaweza kuswali na vazi refu na ushungi bila kuvaa nguo ya chini? Akasema: “Ikiwa hilo vazi ni refu linalofunika miguu yake.[4][Imetolewa na Abuu Daawuwd, na wakaisahihisha Maimaam kuwa ni Mawquwf]

 

 

 

165.

وَعَنْ عَامِرِ بْنِ رَبِيعَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : {كُنَّا مَعَ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم  فِي لَيْلَةٍ مَظْلَمَةٍ ، فَأَشْكَلَتْ عَلَيْنَا اَلْقِبْلَةُ ، فَصَلَّيْنَا . فَلَمَّا طَلَعَتِ اَلشَّمْسُ إِذَا نَحْنُ صَلَّيْنَا إِلَى غَيْرِ اَلْقِبْلَةِ ، فَنَزَلَتْ : (فَأَيْنَمَا تُوَلُّوا فَثَمَّ وَجْهُ اللَّـهِ)}  أَخْرَجَهُ اَلتِّرْمِذِيُّ وَضَعَّفَهُ

Kutoka kwa ‘Aamir bin Rabiy’ah[5] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Tulikwa na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) katika usiku wa giza na hatukuwa na hakika ya Qiblah, tukaswali, jua lilipochomoza tukagundua tulielekea upande usiokuwa Qiblah, ikateremka Aayah: (basi popote mnapogeuka kuna Wajihi wa Allaah) [Al-Baqarah: 115].” [Imetolewa na At-Tirmidhiy, na akaidhoofisha]

 

 

 

166.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم   {مَا بَيْنَ اَلْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ قِبْلَةٌ}  رَوَاهُ اَلتِّرْمِذِيُّ ، وَقَوَّاهُ اَلْبُخَارِيُّ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Baina ya Mashariki na Magharibi ni Qiblah[6].” [Imetolewana At-Tirmidhiy, na akaipa daraja la Qawiy Al-Bukhaariy]

 

 

 

167.

وَعَنْ عَامِرِ بْنِ رَبِيعَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : {رَأَيْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  يُصَلِّي عَلَى رَاحِلَتِهِ حَيْثُ تَوَجَّهَتْ بِهِ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

زَادَ اَلْبُخَارِيُّ : {يُومِئُ بِرَأْسِهِ ، وَلَمْ يَكُنْ يَصْنَعُهُ فِي اَلْمَكْتُوبَةِ}

وَلِأَبِي دَاوُدَ : مِنْ حَدِيثِ أَنَسٍ : {كَانَ إِذَا سَافَرَ فَأَرَادَ أَنْ يَتَطَوَّعَ اِسْتَقْبَلَ بِنَاقَتِهِ اَلْقِبْلَةِ ، فَكَبَّرَ ، ثُمَّ صَلَّى حَيْثُ كَانَ وَجْهَ رِكَابِهِ}  وَإِسْنَادُهُ حَسَنٌ

Kutoka kwa ‘Aamir bin Rabiy’ah[7] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nimemuona Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akiswali huku kapanda mnyama wake akielekea kokote alikoelekea mnyama wake.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Al-Bukhaariy akaongeza: “Huku akiashiria kwa kichwa, hakufanya hivyo (kuswali huku kapanda mnyama) kwa Swalaah za faradhi.”

 

 

Na Abuu Daawuwd amepokea Hadiyth ya Anas (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) kuwa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): “Aliposafiri na akataka kuswali Swalaah ya Sunnah, alikuwa akimuelekeza ngamia wake Qiblah[8], akapiga takbiyra na kuendelea kuswali huku akielekea kokote ngamia wake alikoelekea.” [Isnaad yake ni Hasan]

 

 

 

168.

 وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  عَنْ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم  {اَلْأَرْضُ كُلُّهَا مَسْجِدٌ إِلَّا اَلْمَقْبَرَةَ وَالْحَمَّامَ} رَوَاهُ اَلتِّرْمِذِيُّ، وَلَهُ عِلَّةٌ

Kutoka kwa Abuu Sa’iyd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Ardhi yote ni Msikiti, isipokuwa makaburini na msalani.” [Imetolewa na At-Tirmidhiy, na ina dosari]

 

 

 

169.

وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ  رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: {نَهَى اَلنَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم  أَنْ يُصَلَّى فِي سَبْعِ مَوَاطِنَ : اَلْمَزْبَلَةِ، وَالْمَجْزَرَةِ ، وَالْمَقْبَرَةِ، وَقَارِعَةِ اَلطَّرِيقِ، وَالْحَمَّامِ، وَمَعَاطِنِ اَلْإِبِلِ، وَفَوْقَ ظَهْرِ بَيْتِ اَللَّهِ}  رَوَاهُ اَلتِّرْمِذِيُّ وَضَعَّفَهُ 

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema kuwa: “Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikataza kuswali katika sehemu saba[9]: (a) jalalani (b) machinjioni (c) makaburini (d) katikati ya njia (e) msalani (bafuni, chooni) (f) wanapokaa ngamia, katika sehemu ya kunywea maji, na (g) juu ya paa la Ka’bah.” [Imetolewa na At-Tirmidhiy, na akaidhoofisha]

 

 

 

170.

وَعَنْ أَبِي مَرْثَدٍ اَلْغَنَوِيِّ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : سَمِعْتَ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  يَقُولُ: {لَا تُصَلُّوا إِلَى اَلْقُبُورِ ، وَلَا تَجْلِسُوا عَلَيْهَا}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ

Kutoka kwa Abuu Marthad Al-Ghanawiyy[10] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akisema: “Msiswali kuelekea makaburi[11], wala msiyakalie[12].” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

171.

وَعَنْ أَبِي سَعِيدٍ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  {إِذَا جَاءَ أَحَدُكُمْ اَلْمَسْجِدَ ، فَلْيَنْظُرْ، فَإِنْ رَأَى فِي نَعْلَيْهِ أَذًى أَوْ قَذَرًا فَلْيَمْسَحْهُ ، وَلْيُصَلِّ فِيهِمَا}  أَخْرَجَهُ أَبُو دَاوُدَ ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ خُزَيْمَةَ

Kutoka kwa Abuu Sa’iyd (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ): “Mmoja wenu anapokuja Msikitini na atazame, na akiona uchafu katika viatu vyake, basi avipanguse na kisha aswali navyo.” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na akaisahihisha Ibn Khuzaymah]

 

 

 

172.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم   {إِذَا وَطِئَ أَحَدُكُمْ اَلْأَذَى بِخُفَّيْهِ فَطَهُورُهُمَا اَلتُّرَابُ}  أَخْرَجَهُ أَبُو دَاوُدَ وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ 

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Mmoja wenu akikanyaga uchafu kwa khofu yake (soksi zake za ngozi), basi kitakaso chake ni mchanga[13].” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na akaisahihisha Ibn Hibbaan]

 

 

 

173.

وَعَنْ مُعَاوِيَةَ بْنِ اَلْحَكَمِ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ  صلى الله عليه وسلم { إِنَّ هَذِهِ اَلصَّلَاةَ لَا يَصْلُحُ فِيهَا شَيْءٌ مِنْ كَلَامِ اَلنَّاسِ ، إِنَّمَا هُوَ اَلتَّسْبِيحُ ، وَالتَّكْبِيرُ ، وَقِرَاءَةُ اَلْقُرْآنِ}  رَوَاهُ مُسْلِمٌ 

Kutoka kwa Mu’aawiyah bin Al-Hakam[14] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hakika hii Swalaah ndani yake haifai chochote katika maneno ya watu, kwa kuwa hiyo ni Tasbiyh, Takbiyra na kusoma Qur-aan.” [Imetolewa na Muslim]

 

 

 

174.

وَعَنْ زَيْدِ بْنِ أَرْقَمَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : {إِنْ كُنَّا لَنَتَكَلَّمُ فِي اَلصَّلَاةِ عَلَى عَهْدِ اَلنَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم  يُكَلِّمُ أَحَدُنَا صَاحِبَهُ بِحَاجَتِهِ، حَتَّى نَزَلَتْ : (حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ) ]اَلْبَقَرَة : 238] ، فَأُمِرْنَا بِالسُّكُوتِ، وَنُهِينَا عَنْ اَلْكَلَامِ}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ، وَاللَّفْظُ لِمُسْلِمٍ 

Kutoka kwa Zayd bin Arqama[15] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Sisi tulikuwa tukiongea ndani ya Swalaah zama za uhai wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), na mtu alikuwa akiongea na mwenzake kuhusu mahitaji yake, ilipoteremka Aayah:

(حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ وَقُومُوا لِلَّـهِ قَانِتِينَ)

(Shikamaneni na Swalaah na khaswa Swalaah ya katikati (Alasiri), na simameni mbele ya Allaah katika hali ya utiifu) [Al-Baqarah: 238] tukaamrishwa kunyamaza na tukakatazwa kuongea[16].” [Al-Bukhaariy, Muslim na tamshi hili ni la Muslim]

 

 

 

175.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  {اَلتَّسْبِيحُ لِلرِّجَالِ، وَالتَّصْفِيقُ لِلنِّسَاءِ} مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

زَادَ مُسْلِمٌ {فِي اَلصَّلَاةِ}

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Tasbiyh (Kusema Subhaana-Allaah) ni kwa mwanamume, na kupiga makofi[17] ni kwa wanawake.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Muslim akaongezea: “Ndani ya Swalaah[18].”

 

 

 

176.

وَعَنْ مُطَرِّفِ بْنِ عَبْدِ اَللَّهِ بْنِ الشِّخِّيرِ ، عَنْ أَبِيهِ قَالَ : {رَأَيْتُ رَسُولَ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  يُصَلِّي، وَفِي صَدْرِهِ أَزِيزٌ كَأَزِيزِ اَلْمِرْجَلِ، مِنْ اَلْبُكَاءِ}

أَخْرَجَهُ اَلْخَمْسَةُ ، إِلَّا اِبْنَ مَاجَهْ ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ

Kutoka kwa Mutwarrif bin ‘Abdillaah bin Shikh-khiyr[19] (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema kutoka kwa baba yake[20] amesema: “Nimemuona Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) akiswali, na nikasikia sauti kifuani mwake kama kuchemka kwa chungu, kwa sababu ya kulia[21].” [Imetolewa na Al-Khamsah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ahmad) isipokuwa Ibn Maajah, na akaisahihisha Ibn Hibbaan]

 

 

 

177.

وَعَنْ عَلَيٍّ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : {كَانَ لِي مَعَ رَسُولِ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  مَدْخَلَانِ ، فَكُنْتُ إِذَا أَتَيْتُهُ وَهُوَ يُصَلِّي تَنَحْنَحَ لِي}  رَوَاهُ النَّسَائِيُّ ، وَابْنُ مَاجَهْ

Kutoka kwa ‘Aliy (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Nilipata ruhusa ya Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) kumwona nyumbani kwake mara mbili, na kila nilipokwenda na kumkuta anaswali, alikuwa anajikohoza kwa ajili yangu[22] (kuwa anaswali).” [Imetolewa na An-Nasaaiy na Ibn Maajah]

 

 

 

178.

وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ  رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ : {قُلْتُ لِبِلَالٍ : كَيْفَ رَأَيْتُ اَلنَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم  يَرُدَّ عَلَيْهِمْ حِينَ يُسَلِّمُونَ عَلَيْهِ ، وَهُوَ يُصَلِّي  ؟ قَالَ : يَقُولُ هَكَذَا ، وَبَسَطَ كَفَّهُ}  أَخْرَجَهُ أَبُو دَاوُدَ ، وَاَلتِّرْمِذِيُّ وَصَحَّحَهُ 

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُمَا) amesema Nilimuuliza Bilaal hivi: “Ulimuona Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) anawajibu vipi Mswahaba zake pindi wanapomsalimia akiwa anaswali? Bilaal akasema: alikuwa akifanya hivi, naye Bilaal akaonyesha kwa kupanua kiganja chake[23].” [Imetolewa na Abuu Daawuwd na At-Tirmidhiy naye aliisahihisha]

 

 

 

179.

 

وَعَنْ أَبِي قَتَادَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ : {كَانَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم  يُصَلِّي وَهُوَ حَامِلٌ أُمَامَةَ بِنْتِ زَيْنَبَ، فَإِذَا سَجَدَ وَضَعَهَا ، وَإِذَا قَامَ حَمَلَهَا}  مُتَّفَقٌ عَلَيْهِ

وَلِمُسْلِمٍ : {وَهُوَ يَؤُمُّ اَلنَّاسَ فِي اَلْمَسْجِدِ}

Kutoka kwa Abuu Qataadah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: “Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alikuwa anaswali huku kambeba Umaamah bint Zaynab[24], na aliposujudu[25] alimweka chini, na aliposimama alimnyanyua.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

Na katika Muslim amesema: “Na yeye (Nabiy) anaswalisha watu.”

 

 

 

180.

وَعَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُ  قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم   {اُقْتُلُوا اَلْأَسْوَدَيْنِ فِي اَلصَّلَاةِ : اَلْحَيَّةَ، وَالْعَقْرَبَ}  أَخْرَجَهُ اَلْأَرْبَعَةُ ، وَصَحَّحَهُ اِبْنُ حِبَّانَ

Kutoka kwa Abuu Hurayrah (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Ueni vyeusi viwili mkiwa ndani ya Swalaah: nyoka na nge[26].” [Imetolewa na Al-Arba’ah (At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, Abuu Daawuwd, Ibn Maajah) na akaisahihisha Ibn Hibbaan]

 

 

 

[1] Aliy bin Twalq bin Al-Mundhir bin Qays Al-Hanafiy ni ambaye kutoka kwa Banu Hanifa, As-Sahimi, na Al-Yamami. Alikuwa ni Swahaba, na inasemekana kuwa ndiye aliyekuwa baba wa Twalq bin ‘Aliy, lakini ilisemekana kuwa majina hayo mawil ni ya mtu mmoja huyo huyo.

 

[2] Hii maana yake ni kwamba, ikiwa wudhuu umetanguka wakati wa Swalaah, lazima kuchukua wudhuu upya na Swalaah hiyo irudiwe. Hii ndiyo bora zaidi.

 

[3] Khimaar ni mtandio au kipande cha nguo ambacho kwacho mwanamke hujifunikia eneo la kichwa na la shingo lake. Hiyo inamaanisha kuwa mwili mzima wa mwanamke sharti ufunikwe pamoja na kichwa na nywele zake.

[4] Hii iko pamoja na masharti ya Swalaah kuwa, mwanamke sharti pia afunike miguu yake mpaka kwenye visigino, vinginevyo Swalaah yake haitokubaliwa.

 

[5] ‘Aamir bin Rabiy’ah bin Maalik Al-‘Inzy, na inasemekana ni Al-‘Adawy. Alisilimu na akafanya Hijrah mara mbili. Alihudhuria Vita vyote. Alifariki wakati alipokufa ‘Uthmaan (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ).

 

[6] Kwa maneno hayo, Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) ameelezea upande iliko Qiblah (Ka’bah) kwa ulimwengu mzima. Watu wanaoishi Mashariki au Magharibi ya Qiblah, wachukue maana ya Hadiyth hii kwamba Qiblah iko kati ya kunakochomozea jua na kunakochwea jua mnamo majira ya baridi na joto. Na wale wanaoishi kaskazini na kusini ya Qiblah, wachukue maaana ya kuwa, wakisimama huku Mashariki na Magharibi iko upande wao wa kuume na kushoto, basi Qiblah yao iko katikati ya pande hizi mbili.

 

[7] ‘Aamir bin Rabiy’a alikuwa mmoja wa wana wa ‘Anz bin Wa’il, ambaye alikuwa ndugu ya Bakr na Taghlib, wana wa Wa’il. Alikuwa Swahaba aliyesilimu mapema sana na akafanya Hijrah (kuhama) zote mbili. Alishiriki katika Badr na vita zote nyingine, na akafariki mnamo mwaka 32 au 35 A.H

 

[8] Hii maana yake ni kwamba, Swalaah ya Sunnah (Nafl) ndiyo inayoweza kuswaliwa huku mtu kapanda mnyama au chombo, kwa sharti kuwa pale anapoanza kuswali, mnyama yule au chombo kile akielekeze Qiblah, na baada ya hapo badiliko lolote la mwelekeo haliathiri kitu. Lakini Swalaah za faradhi zisiswaliwe mtu akiwa kampanda mnyama, lakini meli, majahazi, mitumbwi, na ndege, vinaruhusiwa.

 

[9] Hadiyth hii ni ushahidi kuwa kuswali makaburini hairuhusiwi, uwe unaswali juu ya makaburi au katikati ya makaburi, na si hoja ikiwa makaburi hayo ni ya Waislaamu au wasiokuwa Waislaamu. Kuswalia makaburini kunatoa picha ya kuabudu asiyekuwa Allaah, ambalo ni kosa kubwa la ushirikina. Imekatazwa kuswali msalani kwa sababu ya najisi na uchafu uliyoko huko; na isitoshe Hadiyth zinasema kuwa msalani ni mahala pa shaytwaan.

 

[10] Jina la Abuu Marthad Al-Ghanawiyy ni Kannaz bin Hussayn bin Yarbu’ Al-Ghanawiyy kizazi cha Ghani bin Ya’sur, kabila la Ghatafan. Alikuwa ni Swahaba ambaye alishuhudia Badr na alikuwa sahibu wa Hamza bin ‘Abdil-Muttwalib, na alikuwa sawa naye ki umri. Alishiriki katika Vita vyote, na akafa mnamo mwaka 12 A.H. akiwa na umri wa miaka 66.

 

[11] Ina maana kuwa, imekatazwa kuswali huku ukielekea makaburi. Watu wengine wanajenga Misikiti karibu na makaburi ya watakatifu ili kupata fadhila za roho zilizokufa. Hii pia imekatazwa. Katika Hadiyth ya ‘Aaishah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) imesemwa waziwazi kuwa: “Allaah (عز وجل) Awalaani Mayahudi na Wakristo, kwani walifanya makaburi ya Manabii wao kuwa mahali pa kusalia.” Inaweza kumaanisha pia kwamba matendo yatakiwayo kuyafanya mbele ya Allaah (عز وجل) Misikitini kamwe yasitendwe katika makaburi. Au pia yaweza kumaanisha kuwa kamwe mtu asiswali mahala ambapo kuna makaburi mbele yake.

 

[12] Kukalia juu ya makaburi kuna maana mbili: moja ni kupumzika au kuegemea makaburi; na pili ni kuyamiliki makaburi kama Mujawwir (mwangalizi wa makaburi ambaye pia hukusanya pesa na vitu vingine kutoka kwa watu wanaozuru makaburi ili kupata radhi za roho zilizozikwa). Aina zote hizo mbili zimekatazwa, inaweza kuwa na maana nyingine kwamba mtu yoyote asikae juu ya kaburi au asijisaidie haja kubwa au ndogo. Hii pia imekatazwa.

 

[13] Hadiyth hizi mbili zinaonyesha kuwa kuswali huku mtu amevaa soksi na au viatu inaruhusiwa. Zinasema pia kuwa endapo viatu hivyo vitachafuliwa na uchafu wowote, vinyesi vya wanyama au bin Aadam, inatosha kusugua kwa vumbi na hakuna haja ya kuosha kwa maji.

 

[14] Huyu Mu’aawiyah bin Al-Hakam alikuwa Swahaba aliyehesabika miongoni mwa wakazi wa Hijaaz. Alikuwa akizuru Madiynah na akawa anakaa kwa akina Banu Sulaym. Alifariki mnamo mwaka 117 A.H.

 

[15] Zayd bin Arqam alipewa jina la utani la Abuu ‘Amr, na alikuwa Answaar Mkhazraj. Kwanza alishiriki katika Vita vya Al-Khandaq, na akaongozana na Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) katika misafara 17. Alihudhuria Vita vya Siffin pamoja na ‘Aliy kwa kuwa alikuwa mmoja wa wafuasi wake. Alilowea kule Kuwfah, na akafia huko mnamo mwaka 66 A.H.

 

[16] Inamaanisha kuwa kuongea wakati wa Swalaah kumekatazwa. Mnamo siku za mwanzo mwanzo za Uislaam, watu walikuwa wakiongea tu ndani ya Swalaah, kisha likaja katazo.

 

[17] Inamaanisha kwamba, iwapo Imaam akitenda kosa kwa bahati mbaya ndani ya Swalaah, wanaume maamuma wake (wanaokuwa nyuma ya huyo Imaam) hutakiwa waseme hivi:

سبحان الله

(kumkumbusha Imaam alisahihishe kosa lake hilo), na wanawake wanatakiwa wapige makofi kidogo (kwa maana hiyo hiyo ya kumkumbusha Imaam), ili sauti (ya mwanamke) isisikike na wanaume.

 

[18] Yaani ikiwa mtu anataka kumkumbusha Imaam jambo alilolisahau, ndani ya Swalaah, sharti aseme:

 سبحان الله

Lakini ikiwa ni mwanamke anayetaka kumkumbusha Imaam, basi sharti mwanamke huyo apige makofi kwa kuvipiga pamoja na vidole vya kiganja chake cha kuume kwa cha kushoto.

 

[19] Huyu Mutwarrif ndiye Mutwarrif bin ‘Abdillaah bin Ash-Shikhkhir Al-Harashi Al-‘Aamir Al-Basr, miongoni mwa Taabi’iyna wa zamani. Aliaminika sana, alikua muadilifu, na alifanya matendo mengi ya sifa nzuri nzuri. Alikufa mnamo mwaka 95 A.H

 

[20] Baba yake Mutwarrif alikuwa ni ‘Abdullaah bin Ash-Shikhkhir bin ‘Awf bin Ka’b Al-Harashi Al-‘Aamir, huyo wa mwisho ni Swahaba. Alikuwa ni mjumbe wa ujumbe wa Banu ‘Aamir na anaaminiwa kuwa alilowea Basra.

 

[21] Kwa mujibu wa Hadiyth, kulia ndani ya Swalaah kwa kumuogopa Allaah kunaruhusiwa; lakini kulia kwa sababu ya ugonjwa au adha yoyote kunabatilisha Swalaah.

 

[22] Inamaanisha kuwa kutoa dalili ya kukohoa hasa mara moja moja au mbili, hakutangui Swalaah. Kitabu cha Musaffa cha ufafanuzi wa Mu’atta kinaelezea kuwa, kukohoa, kulia, au kucheka kwa mfululizo, ingawa huko siyo kusema, kunatangua Swalaah.

 

[23] Inamaanisha kuwa matendo madogo madogo hayabatilishi Swalaah.

 

[24] Umaamah ni mjukuu wa Nabiy (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ), binti wa Zaynab kwa Abdul-‘Aass bin Ar-Rabi’. Aliolewa na ‘Aliy baada ya kifo cha Faatwimah (رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا) kwa mujibu wa mapendekezo ya Faatwimah. Na ‘Aliy alipouliwa, aliolewa na Al-Mughiyrah bin Nawfal, na akafariki wakati akiwa kwa mume huyu.

 

[25] Shah Waliyu-Allaah wa Delhi aliandika katika kitabu chake  حجة الله البالغة kuwa, Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) alifanya vitendo vidogo vidogo kwa maksudi ili kuonyesha kuwa vitendo vidogo vidogo havitengui Swalaah. Hadiyth zinasema kuwa, kukiwa na dharura, yafuatayo hayaathiri wala kutangua Swalaah: (a) Tamko dogo, (b) Kuhama kidogo mahali ulipo, vitendo vidogo, (c) Badiliko dogo la mahala uliko kuenda mbele au nyuma, (d) Kutoa ishara au kuashiria kitu kwa mguu, (e) Kufungua mlango kwa kuhama kidogo tu, (f) Kusogea nyuma wakati mtu (wa tatu) anajiunga nanyi (kuswali jamaa), (g) Kulia kwa kumuogopa Allaah, (h) Kutoa ishara ili kuelewesha kitu fulani, (i) Kuua nge au nyoka, (j) Kutazama pembeni bila kugeuza shingo.

 

[26] Hadiyth hii inathibitisha vitu viwili: (a) Swalaah haitanguki kwa kuua nge na nyoka, (b) Mtu asiwaonee huruma. Sharti wauawe na wasiachwe kwani wao wana madhara.

 

Share