03-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo:Umahasusi Wa Swawm Kwa Allaah ‘Azza wa Jalla

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

03-Umahasusi Wa Swawm Kwa Allaah ‘Azza wa Jalla

 

 

 

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال ((قال الله عزوجل: كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ لَهُ إِلَّا الصِّيَامَ فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)    kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah ‘Azza wa Jalla Kasema: Kila ‘amali ya mwana Aadam inamhusu Yeye isipokuwa Swiyaam kwani hakika hiyo inanihusu Mimi, Nami Ndiye Ninayeilipia)) [Al-Bukhaariy, Muslim]

 

 

Mafunzo:

 

 

Hadiyth hii adhimu imethibiti toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), inaonyesha fadhila na hadhi kubwa ya ‘amali ya Swawm kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kulinganisha na ‘amali nyinginezo za mja pale Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alipotujulisha kwamba ‘amali hii Ameinasibishia Kwake Pekee kimalipo.

 

‘Ulamaa wamejaribu kufafanua maana ya Neno Lake:

 

إِلَّا الصِّيَامَ فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ

 

((Isipokuwa Swiyaam kwani hakika hiyo inanihusu Mimi, Nami Ndiye Ninayeilipia))

 

Wakisema: “’Amali zote anazozifanya mja hapa duniani, basi thawabu za ‘amali zake zitatumika Siku ya Qiyaamah kulipiwa makosa na haki za watu alizodhulumu hapa duniani.  Aliowadhulumu watalipwa mema yake yatokanayo na ‘amali zake njema zitokanazo na Swalaah, Zakaah, swadaqah, na kadhalika kama anavyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((أَتَدْرُونَ مَا الْمُفْلِسُ؟))‏ قَالُوا: الْمُفْلِسُ فِينَا مَنْ لاَ دِرْهَمَ لَهُ وَلاَ مَتَاعَ .‏ فَقَالَ: ((إِنَّ الْمُفْلِسَ مِنْ أُمَّتِي يَأْتِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ بِصَلاَةٍ وَصِيَامٍ وَزَكَاةٍ وَيَأْتِي قَدْ شَتَمَ هَذَا وَقَذَفَ هَذَا وَأَكَلَ مَالَ هَذَا وَسَفَكَ دَمَ هَذَا وَضَرَبَ هَذَا فَيُعْطَى هَذَا مِنْ حَسَنَاتِهِ وَهَذَا مِنْ حَسَنَاتِهِ فَإِنْ فَنِيَتْ حَسَنَاتُهُ قَبْلَ أَنْ يُقْضَى مَا عَلَيْهِ أُخِذَ مِنْ خَطَايَاهُمْ فَطُرِحَتْ عَلَيْهِ ثُمَّ طُرِحَ فِي النَّارِ))  مسلم‏

 ((Je, Mnamjua muflis?)) Wakasema [watu]: “Muflis kwetu sisi ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na dirhamu [pesa] wala vyenye kumnufaisha yeye hapa duniani”. Akasema (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Hakika muflis katika Ummah wangu ni yule atakayekuja Siku ya Qiyaamah na Swalaah, Swiyaam, na Zakaah, lakini amemtusi huyu, kumsingizia huyu mwingine kuwa amezini, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya mwingine na kumpiga mwengine. Thawabu zake zitapatiwa huyu na yule mpaka zimalizike. Na zinapokwisha basi madhambi ya hao [aliowadhulumu] atabandikwa nayo, hivyo kuingizwa Motoni))].  [Muslim]

 

 

Lakini Swawm yake haitoguswa kabisa, bali Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Atamhifadhia na kumbakishia.

 

Maneno haya yanathibitishwa na Hadiyth nyingine isemayo:

 

 

(( كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ لَهُ كَفَّارَة إِلَّا الصّوْم فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ))

((Kila ‘amali ya mwana Aadam ina kafara isipokuwa Swawm, kwani hakika Swawm kwani hakika hiyo inanihusu Mimi, Nami Ndiye Ninayeilipia)) [Musnad Ahmad]

 

Wengine wakasema:

 

“Maana yake ni kuwa Swawm ni ‘amali ya kindani isiyoonekana, na kwa hivyo hakuna ajuaye undani wake isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Peke Yake. Ni niyyah ya kimoyo kinyume na ‘amali nyinginezo zinazoonekana na watu. Lakini Swawm, ni ‘amali ya siri kati ya mja na Mola wake.  Na kwa ajili hiyo, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

 

((انه ترك شهوته وطعامه وشرابه من اجلي))

((Ameacha matamanio yake, chakula chake na kinywaji chake kwa ajili Yangu)).

 

Swadaqah, Swalaah, Zakaah, Hijjah ni ‘amali za kuonekana, lakini Swawm hakuna aionaye”.

 

‘Ulamaa wengine wanasema: “Swawm haiingiliwi na shirki kabisa kinyume na ‘amali nyinginezo. Wapagani na washirikina tunawaona wakitoa kafara kwa viabudiwa vyao kama wanyama na kadhalika. Wanasujudia masanamu yao na kuyabusu. Lakini hakuna mshirikina yeyote au mpagani yeyote anayefunga Swawm kwa ajili ya masanamu hayo. Hivyo, Swawm inakuwa kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Peke Yake pasina mwengine. Na hii ndio maana ya Neno Lake:

 

(( الصوم لي وانا اجزبي به))

((Swawm ni kwa ajili Yangu, Nami Ndiye Ninayeilipia))

 

 

Hadiyth nyengineyo kuhusu fadhila za Swawm:

 

 

عن أبي هريرة  رضي الله عنه  قال: قال رسول اللَّه  صلى الله عليه وسلم: (( قالَ اللَّهُ:  كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ لَهُ إِلاَّ الصِّيَامَ، فَإِنَّهُ لِي، وَأَنَا أَجْزِي بِهِ‏.‏ وَالصِّيَامُ جُنَّةٌ، وَإِذَا كَانَ يَوْمُ صَوْمِ أَحَدِكُمْ، فَلاَ يَرْفُثْ وَلاَ يَصْخَبْ، فَإِنْ سَابَّهُ أَحَدٌ، أَوْ قَاتَلَهُ فَلْيَقُلْ إِنِّي امْرُؤٌ صَائِمٌ‏.‏ وَالَّذِي نَفْسُ مُحَمَّدٍ بِيَدِهِ لَخُلُوفُ فَمِ الصَّائِمِ أَطْيَبُ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ رِيحِ الْمِسْكِ، لِلصَّائِمِ فَرْحَتَانِ يَفْرَحُهُمَا إِذَا أَفْطَرَ فَرِحَ، وَإِذَا لَقِيَ رَبَّهُ فَرِحَ بِصَوْمِهِ ‏)) رواه البخاري.

 

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema:

((Allaah ‘Azza wa Jalla Amesema: “Kila ‘amali ya bin Aadam inamhusu yeye isipokuwa Swiyaam, kwani hakika hiyo inanihusu Mimi, Nami Ndiye Ninayeilipia.  Na Swawm ni ngao, na itakapokuwa siku ya Swawm ya mmoja wenu, basi asitamke maneno yasiyolaiki, wala asifanye maasia, wala asipayuke ovyo. Ikiwa mtu atamvuta watukanane au wapigane, basi aseme: “Hakika mimi nimefunga”. Naapa kwa Ambaye Nafsi ya Muhammad iko Mkononi Mwake, hakika kutaghayari harufu ya kinywa cha mwenye Swawm kunanukia mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski. Mwenye Swawm ana furaha mbili anazozifurahikia; anapofungua hufurahika kwa Swawm yake, na atakapokutana na Mola wake atafurahi kwa Swawm yake)) [Al-Bukhaariy]

 

 

 

Swawm ni nguzo ya nne kati ya nguzo za Uislamu. Mwislamu huupokea mwezi wa Ramadhwaan kwa kifua kilichofunguka, nafsi nzuri na moyo uliotulia kwa kuwa anajua fika kwamba huu ni mwezi wa  kheri na barkah zisizopatikana katika mwezi mwingine.

 

Mwislamu kama huyu, utamwona anafanya hima ya juu ya kujichunga na kila lile ambalo linaweza kuivuruga Swawm yake, na anakuwa na shime ya kweli ya kufanya kila tendo jema ili apate jaza iliyoahidiwa na Allaah (‘Azza wa Jalla)  isiyokuwa na mipaka maalumu.

 

Swawm hii ni ngao na kinga kwa Mwislamu wa kweli, kwani humzuia na mambo yote yatakayomghadhibisha Allaah (‘Azza wa Jalla) hapa dunaini, na Aakhirah itakuwa kinga dhidi ya moto.

 

Hadiyth hii tukufu imetupa mwongozo kamili juu ya namna ya kuitumia kinga hii:

 

Kwanza, mwenye Swawm anatakiwa auzuie ulimi wake usije kutamka mambo ya ovyo yasiyolaikiana na mwezi huu. Ni kama kutaja mambo ya ngono ambayo yanaweza kuchemsha matamanio ya mtu.

 

Pili, asifanye vitendo vyovyote vya maasia na ufasiki, kwani haviendani kabisa na uadhama wa mwezi huu.

 

Tatu, asinyanyue sauti yake kama inavyofanyika kwenye mazingira ya sokoni. Upazaji huu unamkosesha mtu haiba yake na hasa kama kinachopaziwa sauti ni kitu kisicho na maana.

 

Nne, ikiwa mtu atajaribu kumtukana au kumporomoshea maneno ya kumuudhi, basi asirudishe wala kujibu, bali ajiondokee zake taratibu bila kumjibisha wala kumjali. Madereva wengi sana huwa na tabia ya kutukana kwa kosa dogo la barabarani. Hawa inabidi kuwapuuza, na Mwislamu inabidi ajiweke mbali kabisa na tabia hii. Hali kadhalika, ikiwa yeyote atamkabili na kumkunja shati, basi apoe na kuondokana naye kwa amani na salama ila kama atashambuliwa, basi hapo itabidi kujitetea kwa mujibu wa hali.

 

 

Kisha Hadiyth inatugusia kuwa harufu mbaya ya kutaghayari kinywa cha mfungaji kutokana na kutokula, inanukia kuliko mafuta ya miski mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).    Na haya ni makarimio makubwa ya Allaah (‘Azza wa Jalla) kwa mwenye Swawm na nafasi kubwa aliyonayo mwenye Swawm mbele ya Mola wake kutokana na kuitii amri Yake na kutekeleza ili kuzipata Radhi Zake.

 

 

 

Share