20-Hadiyth Za Ramadhwaan Na Mafunzo: Zakaatul-Fitwr Hikma Yake Kiwango Chake Na Kuwajibika Kwake

 

 

Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo

 

20- Zakaatul-Fitwr  Hikma Yake Kiwango Chake Na Kuwajibika Kwake

 

 

 

عَن ْابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: " فَرَضَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ الْفِطْرِ صَاعًا مِنْتَمْرٍ أَوْ صَاعًا مِنْ شَعِيرٍ عَلَى الْعَبْدِ وَالْحُرِّ وَالذَّكَرِ وَالأنْثَى وَالصَّغِيرِ وَالْكَبِيرِ مِنْ الْمُسْلِمِينَ". البخاري

Kutoka kwa bin 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhuma): "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameifanya Zakaatul-Fitwr ni fardhi kwa mtumwa na aliye huru, mwanamume na mwanamke, mdogo na mkubwa miongoni mwa Waislamu kwa kutoa swaa' moja ya tende kavu au swaa’ moja ya shayiri." [Al-Bukhaariy] 

 

 

Mafunzo:

 

Kuwajibika kwa Zakaatul-Fitwr:

 

Hadiyth hiyo tukufu ni dalili kuwa Zakaatul-Fitwr ni fardhi kwa Waislamu.   Na pia katika Hadiyth nyengine ifuatayo:   

 

عنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رضى الله عنه قَالَ: "كُنَّا نُخْرِجُ فِي عَهْدِ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَوْمَ الْفِطْرِ صَاعًا مِنْ طَعَامٍ‏".‏ وَقَالَ أَبُو سَعِيدٍ "وَكَانَ طَعَامَنَا الشَّعِيرُ وَالزَّبِيبُ وَالأَقِطُ وَالتَّمْرُ"‏.‏

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) akisema: “Tulikuwa tukitoa zama za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Siku ya ‘Iydul-Fitwr pishi ya chakula.” Na Akasema Abuu Sa’iyd: “Na chakula chetu kilikuwa ni shayiri zabibu, jibini na tende”. [Al-Bukhaariy]

 

 

Zakaatul-Fitwr ni wajibu kwa kila Mwislamu mwenye chakula cha kutosha na ziada kwake yeye na wale wote ambao anawalisha kwa usiku wa kuamkia ‘Iyd na mchana wake. Zakaatul-Fitwr hii imewekwa kwa hikmah iliyoelezewa kwenye Hadiyth hii tukufu kuwa ni kitwaharisho kwa mfungaji Swawm kutokana na matelezo madogo madogo ambayo anaweza kuwa aliyafanya wakati wa Swawm yake, au makosa mengineyo ambayo pengine yalitia madoa kwenye Swawm yake kama kauli chafu, kukebehi na kadhalika. Zakaatul-Fitwr hii inasafisha madoa doa hayo na kukarabati popote pale palipoharibika katika Swawm ya mtu.

 

Ni wajibu kuwatolea watoto wadogo na wakubwa, mke, mtumishi na kila yule ambaye mtu anamkimu kimaisha. Ama mtoto ambaye bado hajazaliwa yumo tumboni mwa mama yake, basi hawajibiki kutolewa Zakaatul-Fitwr, lakini kama mtoto kazaliwa baada ya kuzama jua usiku wa mwisho wa Ramadhwaan basi inapendekezeka kumtolea kwa sababu Swahaba Mtukufu ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) alifanya hivyo japokuwa si fardhi.

 

Aina ya chakula:

 

Wengi katika ya ‘Ulamaa wanasema kuwa chakula kinachokusudiwa kwenye Hadiyth hii ni “burri” yaani ngano. Lakini ‘Ulamaa wengine wanaona kuwa chakula chochote kinacholiwa zaidi na wenyeji wa mji wowote vyovyote kiwavyo ikiwa ni ngano, mahindi, mtama na kadhalika basi chafaa kutolewa Zakaatul-Fitwr.

 

 

Lengo na hikma yake:

 

Hadiyth imetaja hikma yake.

 

عَن ابنِ عَبَّاسٍ رضي الله عنهما  قَالَ: "فَرَضَ رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم  زَكَاةَ الفِطرِ طُهرَةً لِلصَّائِمِ مِنَ اللَّغوِ وَالرَّفَثِ، وَطُعمَةً لِلمَسَاكِينِ، مَنْ أدَّاهَا قَبلَ الصَّلَاةِ فَهِيَ زَكَاةٌ مَقبُولَةٌ، وَمَن أدَّاهَا بَعدَ الصَّلَاةِ فَهِيَ صَدَقَةٌ مِنَ الصَّدَقَاتِ"

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amefaradhisha Zakaatul-Fitwr kwa ajili ya kumtwaharisha mfungaji (Swawm) kutokana na maneno yasiyolaikiana, na kauli au matendo machafu, na kwa ajili ya chakula kwa masikini. Mwenye kuitoa kabla ya Swalaah, basi hiyo ni Zakaa yenye kukubaliwa. Ama mwenye kuitoa baada ya Swalaah, basi hiyo ni swadaqah katika swadaqah nyinginezo.” [Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Abiy Daawuwd (1609), Swahiyh Ibn Maajah (1492), Swahiyh Al-Jaami’ (3570)]

 

Na pia hikmah nyingine ni  kuwawezesha masikini kupata mlo katika siku hiyo ya furaha ambapo chakula kinakuwa ni sehemu muhimu ya kukamilisha furaha hiyo. Kuwapatia chakula, kunakuwa ni kinga kwao na sitara ya kunyoosha mikono ya ombaomba, na hivyo kuifanya furaha ienee kwa Waislam wote matajiri na masikini.

 

 

Chakula gani kutoa:

 

Zakatul-Fitwr ni kutoa chakula kinachopendwa zaidi na nchi nyingi za Kiislamu kama mchele na hususan kwenye nchi za ghuba. Hivyo hakuna ubaya kutoa mchele kama Zakaatul-Fitwr kuliko kutoa ngano ingawa pia inatumika sana lakini si kulinganisha na mchele. Lakini ikiwa mtu hakupata mchele, anaweza kutoa mtama, shayiri na kadhalika ikiwa vyakula hivyo vinatumika zaidi sehemu alipo.

 

Kiasi cha kutoa Zakaatul-Fitwr:

 

Ni kama ilivyotajwa katika Hadiyth zilizotangulia kwamba ni swaa' ya chakula.

 

swaa’: Ni kiasi cha chakula  cha ujazo kamili wa viganja viwili vya mikono vya ukubwa wa wastani.. Hiyo ndio tafsiyr ya صاع kwa mujibu wa kamusi. Na ujazo huo ni sawa na takriban kilo mbili na nusu.

 

 

Wakati wa kutoa Zakaatul-Fitwr:

 

La wajibu jingine, ni kutoa Zakaatul-Fitwr kabla ya kwenda kuswali Swalaah ya ‘Iyd, na haijuzu kuichelewesha baada ya Swalaah, kwani itahesabiwa kuwa ni swadaqah ya kawaida, na si Zakaatul-Fitwr. Baadhi ya ‘Ulamaa wanasema kuwa inajuzu kuitoa kabla ya ‘Iyd kwa siku moja au mbili kwa kuwa Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wakiitoa kabla ya ‘Iyd kwa siku moja au mbili.

 

Wanaopewa Zakaatul-Fitwr

 

Wanaostahiki kupewa Zakaatul-Fitwr ni masikini na mafukara, kwani hao ndio walengwa wakuu.

 

 

Je, Zakaatul-Fitwr inafaa kutolewa mali badala ya chakula?

 

 

Kwa  mujibu wa Jamhuri ya ‘Ulamaa, haifai kutoa Zakaatul-Fitwr kwa thamani ya pesa, bali la wajibu ni kutoa chakula kama alivyoamuru Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambapo yeye mwenyewe alifanya hivyo na Maswahaba wake pia wakafanya hivyo. Mwenye kutoa thamani ya chakula, basi kaenda kinyume na alivyofanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Jamhuri ya ‘Ulamaa wanasema kuwa haijuzu kabisa kutoa fedha badala ya chakula. Kwa kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amefaradhisha kitolewe chakula na kuainisha aina ya vyakula hivyo, na Maswahaba wake walitoa pia vile vile chakula huku wakiwa pia na fedha. Na sisi bila shaka ni lazima tuwafuate.

 

Halafu utoaji Zakaatul-Fitwr wa chakula, kipimo chake kisha ainishwa cha pishi moja. Lakini kwa fedha kipimo hiki hakidhibitiki ingawa baadhi ya ‘Ulamaa wamesema kinaweza kwa thamani ya kilo mbili na nusu ya chakula kinachotolewa ambazo ni sawa na pishi moja.

 

Na mtu anaweza kusema: “Pesa zinamfaa zaidi masikini kwa kuwa anaweza kununulia kitu kingine chochote anachokihitajia kwa mapishi kama chumvi, mafuta na kadhalika.”

 

Lakini tunasema: “Kuna vyanzo vingine vya maduhuli ya pesa kwa masikini kama Zakaatul-Maal (Zakaah ya mali) swadaqah nyinginezo kiujumla, tunukio na kadhalika. Hivyo basi, haifai kutoa pesa kama Zakaatul-Fitwr kwa masikini, bali chakula kama alivyoamuru Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kulifanya hilo Maswahaba wake (Radhwiya Allaahu ‘anhum).

 

 

Share