05-Al-Lajnah Ad-Daaimah: Mwanamke Asiye Na Mahram Hawajibiki Kufanya Hajj

 

Mwanamke Asiye Na Mahram Hawajibiki Kufanya Hajj

 

Al-Lajnah Ad-Daaimah

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Mwanamke ambaye anajulikana sana kwa taqwa yake, akiwa katika umri wa wastani au kukaribia uzee anataka kufanya Hajj. Lakini hana Mahram. Nchi anayoishi kuna mwanamume ambaye anajulikana kwa kuwa ni mwenye taqwa ambaye anataka kufanya Hajj, naye anasafiri na jamaa yake mwanamke. Je inafaa mwanamke huyo kwenda Hajj na mwanamume huyo ambaye atakuwa ni mlinzi wao?  Je, anawajibika kufanya Hajj au hawajabiki kwa vile hana Mahram, ingawa anao uwezo kifedha? Tupeni jibu, Allah Awalipe. 

 

JIBU:

 

Mwanamke huyo ambaye hana Mahram hawajibiki kufanya Hajj kwa sababu kuwa na Mahram ni katika kipengele cha uwezo wa kufanya Hajj. Kuwa na uwezo ni moja wa sharti halisi ya kuwajibika kufanya Hajj kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ

Na kwa ajili ya Allaah ni wajibu kwa watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo.   [Al-'Imraan: 97]

 

Hairuhusiwi kwake kusafiri kwenda Hajj au safari nyingine bila ya mume au Mahram. Hii ni kutokana na Imaam Al-Bukhaariy alivyohifadhi kuwa Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((لا يحل لامرأة مسلمة تسافر مسيرة اليوم وليلة إلا مع ذي حرمة منها))

((Haimpasi mwanamke Muislamu kusafiri msafara wa mchana na usiku ila awe na Mahram)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Vile vile imerekodiwa na ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba kamsikia Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 

((لا تسافر المرأة إلا مع ذي محرم ، ولا يدخل عليها رجل إلا ومعها محرم))

((Mwanamke asisafiri ila akiwa na Mahram na mwanamke asiwe peke yake ila akiwa na Mahram wake))

 

Mtu mmoja alisema: "Ee Rasuli wa Allah, mke wangu amesafiri kwenda kufanya Hajj na nimemuwakilisha na kundi fulani." Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Nenda kafanye Hajj na mke wako))

 

Hii ni rai ya Al-Hasan, Al-Nukhaaiy, Ahmad, Is-haaq, ibn Al-Mundhir na ‘Ulamaa wanasheria wa Asw-haab Ar-raaiy. Ni rai iliyo sahihi kwa sababu imekubalika kutokana na kukubalika na wote Hadiyth ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo inakataza mwanamke kusafiri bila ya mume au Mahram.

 

Maalik, Ash-Shaafiy na Al-Awzaaiy wametoa rai tofauti. Wote wametoa sharti ambayo haina dalili. Ibn Al-Mundhir amesema: "Wote wameacha yaliyo dhahiri, maana ya Hadiyth iliyo wazi na wameweka sharti ambayo hawana dalili."

 

Wa biLLaahi At-Tawfiyq wa Swalla Allaahu ‘alaa Nabiyyina Muhammad wa aalihi wa Swahbihi wa sallam.

 

[Al-Lajnah Ad-Daaimah - Fataawa al-Mar-ah]

 

Share