33-Wewe Pekee Tunakuabudu: Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah: Kutwassal Kwa Majini Na Mazimwi

 

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

Wewe Pekee Tunakuabudu Na Wewe Pekee Tunakuomba Msaada

 

Tawassul Za Shirki Kufru Na Bid’ah

 

33-Kutwassal Kwa Majini Na Mazimwi

 

 

 

Baadhi ya Waislamu wanatafuta kujikinga na shari au kutaka poza ya maradhi na haja nyinginezo mbali mbali kwa kupitia majini, mazimwi au mashaytwaan.

 

Haumwi mtu au hahamii nyumba mpya au hafikiwi na dhara au mtihani wowote ila hukimbilia kwa wenye kupandisha mashaytwaan wamsikilize shaytwaan huyo anatabiria nini na anadai nini. 

 

Ada hiyo ya kutawassal kwa majini ilianza tokea zama za ujaahiliyyah, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

وَأَنَّهُ كَانَ رِجَالٌ مِّنَ الْإِنسِ يَعُوذُونَ بِرِجَالٍ مِّنَ الْجِنِّ فَزَادُوهُمْ رَهَقًا﴿٦﴾

 “Na kwamba walikuwa wanaume miongoni mwa wana Aadam wanajikinga na wanaume miongoni mwa majini, basi wakawazidishia madhambi, uvukaji mipaka ya kuasi na khofu.” [Al-Jinn: 6]

 

 

Amesema Shaykh Swaalih bin ‘Abdil-‘Aziyz Aal Ash-Shaykh (Hafidhwahu Allaah): “Maana ya ‘rahaqa’ ni khofu na mpigo wa moyo. Wakawajaza khofu moyoni na mwilini na katika roho zao, na hivyo majini wakajitukuza na wakazidisha shari…. na washirikina walikuwa wanapotua katika bonde au mahali penye kutisha, waliitikadi kwamba kila mahali kuna jini au mkuu wa majini anahudumia sehemu hiyo na anatawala, ikawa wanapofikia bonde au mahali husema: ‘tunajikinga na bwana wa bonde hili kutokana na wajinga wa kaumu yao’ wakimaanisha majini. Hivyo wakajikinga kwa majini ili wawaepushe na shari ya muda wa makazi yao.” [Sharh Kitabit-Tawhiyd li ibn ‘Abdil-Wahhaab]

 

Wanaotawassal kwa viumbe hivyo watambue kwamba ni makhaini wenye kuhadaa wana Aadam, na Siku ya Qiyaamah watakanushana ushirikiano wao wa duniani: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَقَالَ الشَّيْطَانُ لَمَّا قُضِيَ الْأَمْرُ إِنَّ اللَّـهَ وَعَدَكُمْ وَعْدَ الْحَقِّ وَوَعَدتُّكُمْ فَأَخْلَفْتُكُمْ ۖ وَمَا كَانَ لِيَ عَلَيْكُم مِّن سُلْطَانٍ إِلَّا أَن دَعَوْتُكُمْ فَاسْتَجَبْتُمْ لِي ۖ فَلَا تَلُومُونِي وَلُومُوا أَنفُسَكُم ۖ مَّا أَنَا بِمُصْرِخِكُمْ وَمَا أَنتُم بِمُصْرِخِيَّ ۖ إِنِّي كَفَرْتُ بِمَا أَشْرَكْتُمُونِ مِن قَبْلُ ۗ إِنَّ الظَّالِمِينَ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٢٢﴾

Na shaytwaan atasema itakapokidhiwa jambo: “Hakika Allaah Alikuahidini ahadi ya haki (na Ameitimiza); nami nilikuahidini kisha nikakukhalifuni. Na sikuwa na mamlaka juu yenu isipokuwa nilikuiteni mkaniitikia. Basi msinilaumu, bali laumuni nafsi zenu. Mimi siwezi kukusaidieni kukuokeeni wala nyinyi hamuwezi kunisaidia kuniokoa. Hakika mimi nilikanusha yale mliyonishirikisha zamani. Hakika madhalimu watapa adhabu iumizayo.” [Ibraahiym: 22]

 

 Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ جَمِيعًا يَا مَعْشَرَ الْجِنِّ قَدِ اسْتَكْثَرْتُم مِّنَ الْإِنسِ ۖ وَقَالَ أَوْلِيَاؤُهُم مِّنَ الْإِنسِ رَبَّنَا اسْتَمْتَعَ بَعْضُنَا بِبَعْضٍ وَبَلَغْنَا أَجَلَنَا الَّذِي أَجَّلْتَ لَنَا ۚ قَالَ النَّارُ مَثْوَاكُمْ خَالِدِينَ فِيهَا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ۗ إِنَّ رَبَّكَ حَكِيمٌ عَلِيمٌ﴿١٢٨﴾

Na Siku Atakapowakusanya wote (Allaah Atasema):  Enyi hadhara ya majini! Kwa yakini mmetafuta kwa wingi (kuwapotoa) katika wana Aadam. Na watasema marafiki wao wandani katika wana Aadam: “Rabb wetu! Tulinufaishana baadhi yetu na wengineo, na tumefikia muda wetu ambao Umetupangia.” (Allaah) Atasema: Moto ndio makazi yenu, ni wenye kudumu humo, isipokuwa Atakavyo Allaah. Hakika Rabb wako ni Mwenye hikmah wa yote, Mjuzi wa yote. [Al-An’aam: 128]

 

Maana ya “tulinufaishana” ni kwamba watu wamewatukuza majini na wakawanyenyekea na wakaomba, na majini wakawahudumia waliyoyataka, na wakawapatia wanayotaka. [Fataawa Al-Lajnah ad-Daaimah lil-Buhuwth  Al-‘Ilmiyyah wal-Iftaa]

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametahadharisha kuwa mashaytwaan ni waongo:

 

هَلْ أُنَبِّئُكُمْ عَلَىٰ مَن تَنَزَّلُ الشَّيَاطِينُ ﴿٢٢١﴾

Je, nikujulisheni wanaowateremkia mashaytwaan?

 

تَنَزَّلُ عَلَىٰ كُلِّ أَفَّاكٍ أَثِيمٍ ﴿٢٢٢﴾

Wanateremka juu ya kila mzushi mkubwa mwingi wa kutenda dhambi. 

 

يُلْقُونَ السَّمْعَ وَأَكْثَرُهُمْ كَاذِبُونَ ﴿٢٢٣﴾

Wanaotega sikio na wengi wao ni waongo. [Ash-Shu’araa 26: 221-223]

 

 WabiLLaahi At-Tawfiyq

 

 

 

  

 

 

 

Share