03-Zawadi Kwa Wanandoa: Mahari

 

 Zawadi Kwa Wanandoa

 

03- Mahari

 

المهر

 

 

 

Ulipaji wa Mahari huwa unategemea jamii waliyopo waoaji na huwa haina kiwango maalum. Na huitwa hayo mahari صداقا kwa maana ya kuwa ni dalili ya ukweli wa mtu kutaka kuoa, na huitwa wakati mwingine kuwa ni نحلة kwa maana ya kipewacho mtu kisichokuwa na mbadala, na huitwa wakati mwingine kuwa ni حباء kwa maana ya anachopewa mtu katika mali ili kumkirimu sahibu yake, au huitwa kuwa ni علاقة yaani chenye kuunganisha baina ya wanandoa wawili.

 

 

Ndoa katika Uislam haiwi ila kwa Mahari, kwa dalili ya neno Lake Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) :

وآ توا النساء صدقاتهن نحلة

“Na wapeni wanawake mahari yao…” (An-Nisaa: 4)

 

Na Akasema tena Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  katika Surat Al-Ahzaab:

 

يا أيها النبي إنا أحللنا لك أزواجك اللاتي آتيت أجورهن

“Ewe Nabii! Tumekuhalalishia wake zako uliowapa mahari yao…” (Al-Ahzaab: 50)

 

Na Akasema vile vile katika Surat An-Nisaa:

فما استمتعتم به منهن فآتوهن أجورهن فريضة

“ … basi wale mnaowaoa miongoni mwao wapeni mahari yao yaliyolazimishwa…” (An-Nisaa: 24)

 

Uislam haukupanga malipo maalum ya mahari, cha kuzingatia hapa katika mahari ni maridhiano ya pande mbili husika, lakini kinachopendeza ni kuwa iwe hafifu na kinachowezekana bila ya taklifa kwa yule muoaji.

 

Imepokewa kutoka kwa Aamir bin Rabia kuwa mwanamke wa kabila la Banii fazara aliolewa kwa Ndara mbili, akasema Mtume (Swalla AAllaahu 'alayhi wa sallam):

 

أرضيت عن نفسك  ومالك بنعلين؟  فقالت : نعم , فأجازه

“Je, kwa Nafsi yako na kwa mali yako umeridhika kwa ndara mbili? yule mwanamke akajibu: ‘ndio’, akamkubalia.” (At-Tirmidhiy)

 

Kutoka kwa Sahl bin Saad kuwa Mtume (Swalla AAllaahu 'alayhi wa sallam)  alimjia mwanamke akamwambia:

Ee, Mtume wa Allaah mimi nimeitoa Nafsi yangu kwako, baada ya kusema hivyo ikawa taabu kubwa (kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ), akasimama mtu akasema, ‘Ee, Mtume wa Allah niozeshe mimi kama wewe huna haja nae’, akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ,  ‘Je, una chochote cha kutoa sadaka?’ akajibu mtu yule: ‘Sina isipokuwa ni hili shuka langu ninalojifungia,’ akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) , ‘Ukimpa hii shuka yako utakaa bila kuwa na shuka ya kutumia, tafuta kitu kingine,’ akasema mtu yule, ‘Sina kitu kingine.’ Akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  kumwambia mtu yule, ‘Tafuta walau pete ya chuma’, mtu yule akatafuta na hakupata kitu, akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  kumwambia mtu yule, ‘Je, umehifadhi chochote katika Qur’an?’ Akasema mtu yule, ‘ndio, sura kadha na kadha, na akataja sura hizo.’ Hapo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  akasema, ‘Nimekuozesha kwa hicho ulichokuwa nacho katika Qur-aan.’”

(Al-Bukhaariy na Muslim)

 

Imepokewa kutoka kwa Anas, kuwa Aba Twalhah alimposa Umu Sulaym, akasema Umu Sulaym kumwambia Aba Twalhah, Wa-Allaahi! mfano wako harejeshwi, lakini wewe ni kafiri na mimi ni Muislamu, na haiwi halali kwangu kuolewa nawe, ukisilimu hiyo ndio mahari yangu, na sitotaka kingine zaidi ya hilo. Na hiyo ndio ikawa mahari yake (baada ya kusilimu Aba Twalhah).

 

Hadithi zote hizi za Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam)  zilizotangulia zinakubali mahari hata ikiwa ni ndogo kiasi gani.

 

 

Share