03-Du'aa Za Ruqya: Kuomba Kinga Dhidi Ya Shari Ya Masikio, Macho, Ulimi, Moyo Na Utupu

 

 

Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake

 

03-Kuomba Kinga Dhidi Ya Shari Ya Masikio, Macho, Ulimi, Moyo Na Utupu

 

www.alhidaaya.com 

 

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa anajilinda kwa Allaah ('Azza wa Jalla)  akisema:

 

((اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ سَمْعِي، وَمِنْ شَرِّ بَصَرِي، وَمِنْ شَرِّ لِسَانِي، وَمِنْ شَرِّ قَلْبِي، وَمِنْ شَرِّ مَنِيِّي))

((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako na shari ya masikio yangu, na shari ya macho yangu, na shari ya ulimi wangu, na shari ya moyo wangu, na shari ya manii yangu)). [Abuu Daawuwd 1551, At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy 5470].

 

 

Faida Na Sharh:

 

Katika Hadiyth hii, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  anajilinda na shari ya masikio yake. Shari hii ni ya kusikiliza kila lililoharamishwa na ambalo Allaah (‘Azza wa Jalla) Haliridhii kama shirki, kufr, masengenyo, uongo, uzushi, ala za muziki na kadhalika. Anaomba masikio yake yasisikilize ila lile la haki kama dhikr, nasaha njema, mawaidha mema na kadhalika.

 

 

Anajilinda na shari ya macho yake. Anaomba asiangalie chochote ila kile tu ambacho Allaah (‘Azza wa Jalla) Anakiridhia. Asiangalie wanawake walioharamishwa, asiwaangalie watu kwa jicho la dharau au viumbe vinginevyo vya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na pia asisahau kuviangalia viumbe vya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kwa mazingatio na utaamuli ili kuzidi kupata iymaan na kujuua zaidi Uwezo wa Allaah (Tabaaraka wa Ta’alaa).

 

Kadhalika, anajilinda na shari ya ulimi wake kama kusengenya, kufitini, kusema uongo, kuyazungumzia yasiyomhusu mtu au kuyanyamazia yanayomhusu na kadhalika, kwa kuwa wengi wataingia motoni kutokana na ndimi zao. Anaomba asitamke ila lililo la haki kama kumdhukuru Allaah ('Azza wa Jalla) na kumshukuru, kuamrisha mema na kukataza munkari, kusoma Qur-aan na mengineyo ya faida na kadhalika. Atambue kwamba viungo vyake vya mwili vitakuja kumshuhudia matendo yake mazuri na maovu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَوْمَ تَشْهَدُ عَلَيْهِمْ أَلْسِنَتُهُمْ وَأَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢٤﴾

Siku zitakaposhuhudia dhidi yao ndimi zao, na mikono yao, na miguu yao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.  [An-Nuwr: 241]

 

Na Anasema pia Allaah ('Azza wa Jalla):

 

الْيَوْمَ نَخْتِمُ عَلَىٰ أَفْوَاهِهِمْ وَتُكَلِّمُنَا أَيْدِيهِمْ وَتَشْهَدُ أَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٦٥﴾

 Leo Tunatia vizibo juu ya vinywa vyao, na itatusemesha mikono yao, na itashuhudia miguu yao kwa yale waliyokuwa wakiyachuma. [Yaasiyn: 65]

 

Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ﴿١٦﴾

Na kwa yakini Tumemuumba insani na Tunajua yale yanayowaza nafsi yake, na Sisi Tuko karibu naye kuliko mshipa wa koo.

 

إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنِ الْيَمِينِ وَعَنِ الشِّمَالِ قَعِيدٌ﴿١٧﴾

Pale wanapopokea wapokeaji wawili (Malaika) wanaokaa kuliani na kushotoni. 

 

مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ﴿١٨﴾

Hatamki kauli yeyote isipokuwa anaye mchungaji aliyejitayarisha (kurekodi). [Qaaf (50: 16-18)]

 

Pia, anajilinda na shari ya moyo wake. Shari hii inatokana na unafiki, hasadi, hikdi, riyaa, kibr, dhana mbaya, itikadi potofu, kuipenda dunia na kufuata hawaa ya nafsi.  Na nyoyo zenye kuepukana na shari hizo ni nyoyo zitakazokuwa salama na katika amani Aakhirah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾

 “Siku hayatofaa mali wa watoto.

 

إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾

 “Isipokuwa yule atakayemfikia Allaah na moyo uliosalimika. [Ash-Shu’araa: 88-89]

 

Mwisho anaomba Allaah (‘Azza wa Jalla) Amlinde kutokana na shari ya manii yake. Hapa anakusudia utupu wake, yaani kuuweka mahala pasipo pake kwa kuzini, kulawiti, kupiga punyeto na mengineyo ya haramu. Matamanio ya tupu ni moja kati ya mitihani migumu inayomkabili mwana Aadam, na inahitaji subira imara ya kuepukana na shari zake na maharamisho yake na hususan katika zama zetu za leo.

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amejilinda na shari ya viungo hivi, kwa kuwa ndivyo kiini cha matamanio ya mtu na mchemko wa ladha yake, na ndiyo asili na chimbuko la shari zote. Allaah (‘Azza wa Jalla) Amemtunuku mwana Aadam viungo hivi ili anufaike navyo kwa kutenda kheri za kumnufaisha katika dunia yake na Aakhirah yake, na si kuvitumia kwa mambo yenye kumkasirisha Yeye, na kisha mwanadamu huyu kukhasirika duniani na aakhirah.

 

 

Share