04-Du'aa Za Ruqyah: Kuomba Uthibiti Wa Moyo Juu Ya Uislamu

 

 

Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake

 

04-Kuomba Uthibiti Wa Moyo Juu Ya Uislamu

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

عن انس قال: كان النبي صلى الله عليه وسلم  يكثر أن يقول: ((اللَّهُمَّ يَا مُقَلِّبَ الْقُلُوبِ ثَبِّتْ قَلْبِي عَلَى دِينِك))   قال أنس فقلنا: يا رسول الله آمنا بك، وبما جئت به، فهل تخاف علينا؟  فقال: ((نعم، إن القلوب بين أصبعين من أصابع الله عز وجل يقلبها))

Imepokelewa na Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akisema: "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa akikithirisha kusema:

 

((Ee Mwenye Kuzigeuza nyoyo, Uthibitishe moyo wangu juu ya Dini Yako)). Anas anasema: Tukasema: Ee Rasuli wa Allaah! Tumekuamini na yale uliyokuja nayo. Je watuogopea?" Akasema: ((Naam. Hakika nyoyo ziko baina ya Vidole viwili kati ya Vidole vya Allaah  ‘Azza wa Jalla,  Huzigeuza)). [Imepokelewa na Anas (Radhwiya Allaahu ‘snhu). Imesimuliwa na At-Tirmidhiy 2140 na Ahmad 12128. Al-Albaaniy kasema Hadiyth Swahiyh kwenye Mishkaat Al-Maswaabiyh 102].

 

 

 

Faida Na Sharh:

 

Sisi ni lazima tuviogope Vitendo vya Allaah ('Azza wa Jalla). Kati ya vitendo hivyo ni kuzigeuza nyoyo zetu. Na hii ndiyo sababu iliyomfanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kutuhofia sisi kuhusiana na suala hili.

 

Ugeuzaji huu wa nyoyo unaweza kuwa ni wa kheri kwa mja. Moyo wake unaweza kugeuzwa toka kwenye ubatili kwenda kwenye haki, kutoka kwenye upotofu kwenda  kwenye hidaayah, kutoka kwenye maasia kwenda kwenye utiifu, kutoka kwenye bid'ah kwenda kwenye Sunnah, kutoka kwenye shirki kwenda kwenye Tawhiyd na kutoka kwenye ukafiri kwenda kwenye Uislamu.

 

Aidha, ugeuzaji huu unaweza kuwa wa shari kama kugeuzwa kinyume ya hayo yaliyotangulia.

 

 

Ugeuzaji huu wa nyoyo unaonyesha Uadhama wa Allaah ('Azza wa Jalla). Ni Yeye tu Peke Yake Mwenye Uwezo huu. Ni Yeye Aliyezipindua nyoyo za wachawi wa Fir‘awn katika muda mfupi mno toka kwenye ukafiri na kuingia kwenye iymaan thabiti iliyowafanya kuuawa wakiwa mashuhadaa. Hawakutishika kamwe na vitisho vya Fir’awn vya kuwakata miguu na mikono na kuwasulubu, bali walishikamana na iymaan yao na wakafa nayo kama yalivyosimuliwa hayo katika Surah Ash-Shu’araa.

 

 

Kisa cha kusilimu ‘Umar bin Al-Khattwaab pia ni mfano hai wa hili.

 

 

Suala hili la kuzipindua nyoyo Allaah Peke Yake Ndiye Mwenye kulisimamia. Hata Malaika hawakupewa kazi hiyo, na wala hawajui lolote kuhusiana na siri iliyoko ndani ya nyoyo za watu. Kuna mambo mengi wanayoyafanyia kazi, lakini hili hawawezi kulikurubia kabisa.

 

Du’aa hii kila mmoja wetu anahitajika aikithirishe kiasi awezavyo kama alivyokuwa akifanya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye Allaah Anamwambia.

 

وَلَوْلَا أَن ثَبَّتْنَاكَ لَقَدْ كِدتَّ تَرْكَنُ إِلَيْهِمْ شَيْئًا قَلِيلً

Na lau kama Hatukukuthibitisha; kwa yakini ungelikaribia kuelemea kwao kidogo. [Al-Israa 17:74]

 

Ni du’aa wanayoiomba ‘Ulamaa waliozama na kubobea katika 'ilmu kutokana na kuijua hatari iliyopo. Na ndiyo sababu ya Anas kumuuliza Rasuli: "Je, unatuhofia?"

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anataja du’aa ya kuthibitisha nyoyo zetu Anaposema:

 

(( رَبَّنَا لاَ تُزِغْ قُلُوبَنَا بَعْدَ إِذْ هَدَيْتَنَا وَهَبْ لَنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً))

Rabb wetu! Usizipotoe nyoyo zetu baada ya kuwa Umetuhidi, na Tutunukie kutoka kwako rahmah. Hakika Wewe ni Mwingi wa kutunuku na kuneemesha.  [Aal-Ímraan 3:8]

 

Na ili du’aa hii ipate uimara na kinga zaidi, Muislamu anatakiwa awe na pupa ya kuwajibika na yote aliyoamrishwa na kuyaepuka yote aliyokatazwa. Akiwa katika hali hii pamoja na kuweka dhana njema kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  basi ugeuzaji utakuwa daima salama kwake wa kumtoa katika hali na kumwingiza katika hali bora zaidi kuliko ya nyuma. Allaah (‘Azza wa Jalla) Hampotoi asiyetaka kupotoka.  Anatuambia:

 

وَالَّذِينَ جَاهَدُوا فِينَا لَنَهْدِيَنَّهُمْ سُبُلَنَا

Na wale waliofanya juhudi kwa ajili Yetu, bila shaka Tutawaongoza njia Zetu. Na hakika Allaah Yu Pamoja na watendao ihsaan. [Al-‘Ankabuwt 29:69].

 

Ama wenye kukataa Maamrisho ya Allaah ('Azza wa Jalla)  kwa inadi na kibri na kutaka wenyewe kupotoka, basi hawa ugeuzaji huo utazidi kuwadidimiza pabaya zaidi kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَلَمَّا زَاغُوا أَزَاغَ اللَّهُ قُلُوبَهُم

Basi walipopotoka, Allaah Akapotosha nyoyo zao; na Allaah Haongoi watu mafasiki. [Asw-Swaff 61:5]

 

Na Anasema pia:

 

وَأَمَّا ثَمُودُ فَهَدَيْنَاهُمْ  فَاسْتَحَبُّوا الْعَمَى عَلَى الْهُدَى))

Na ama kina Thamuwd, Tuliwaongoza, lakini walistahabu upofu kuliko Uongofu.)). [Fusw-swilat 41:17].

 

Share