05-Du'aa Za Ruqyah: Kuomba Yaqiyn, ‘Afwa na ‘Aafiyah Duniani na Aakhirah

 

Du’aa Za Ruqyah (Kinga): Faida Na Sharh Zake

 

05-Kuomba Yaqiyn, ‘Afwa na ‘Aafiyah Duniani na Aakhirah

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa anajilinda kwa Allaah ('Azza wa Jalla)   akisema:

 

((اللَّهُمَّ إنِّي أسْألُكَ اليقين والعفو و الْعَافِيَةَ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ))

((Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba Al Yaqiyn, Al-‘Afw  na Al-‘Aafiyah duniani na Aakhirah)). [Imesimuliwa na At-Tirmidhiy katika Kitabu cha Ad-Da’awaat Hadiyth nambari 3514].

 

 

 

Faida Na Sharh:

 

 

 اليقين Al-Yaqiyn,  ni jambo lililothibiti bila shaka yoyote ndani yake.

 

 العفو  Al-‘Afw, ni msamaha wa madhambi na kuacha kutoa adhabu juu yake.

 

 

 العافية Al-‘Aafiyah, ni neno jumuishi lenye maana ya Allaah ('Azza wa Jalla)  kumpa salama na amani  Mja Wake, kumlinda na majanga, shari na misukosuko, na kusalimika na magonjwa, na mabalaa na pia kubakia salama katika Dini yake. Pia ni afya mbali na maradhi.

 

 

Du’aa hii ya barkah, imekusanya maombi mazito ambayo kila mtu anayatamani katika Dini yake, dunia yake na Aakhirah yake. Mja anamwomba Allaah ('Azza wa Jalla)  amani, na kinga ya shari zote za dhahiri na zisizo dhahiri, zinazoonekana na zisizoonekana. Amani na usalama ni lengo la viumbe wote katika ulimwengu huu; wanadamu, wanyama, ndege, wadudu na kadhalika.

 

 

Kati ya magonjwa ya kindani na kimaanawi ni magonjwa ya moyo. Kati ya magonjwa hayo, ni shakashaka kuhusiana na baadhi ya masuala ya kidini. Na kwa ajili hiyo, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amemwomba Allaah ('Azza wa Jalla) Ampe yaqiyn ya moyo, kwani yaqiyn ya moyo ndiyo daraja ya juu kabisa ya iymaan itakayomfaulisha Muislamu duniani na Aakhirah. Haya ni magonjwa mabaya kabisa ya moyo, na kwa ajili hiyo, alikuwa akiomba akisema:

 

((اللَّهم زدنا إيماناً ويقيناً وفهماً ))

((Ee Allaah! Tuzidishie iymaan, yaqiyn na fahmu)). [Imekharijiwa na Ahmad 14/278].

 

Hivyo yaqiyn ikijikita ndani ya moyo, Muislamu huisusa dunia na kushikamana na Aakhirah.

 

Du’aa hii kiujumla ni muhimu sana kwa Muislamu kuiomba kila wakati.

 

 

Dalili ya hilo ni kuwa mtu mmoja alikwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na kumwambia: “Ee Rasuli wa Allaah! Ni du’aa ipi bora zaidi?" Akasema: ((Unamwomba Rabb wako Al-‘Afwa na Al-‘Aafiyah duniani na Aakhirah)). Kisha akamwendea tena kesho yake akamuuliza: "Ee Rasuli wa Allaah! Ni du’aa ipi bora zaidi?" Akasema: ((Unamwomba Rabb wako Al-‘Afwa na Al-‘Aafiyah duniani na Aakhirah)). Kisha akamwendea siku ya tatu akasema: "Ee Rasuli wa Allaah! Ni du’aa ipi bora zaidi?" Akasema:

 

((تَسْأَلُ رَبَّكَ الْعَفْوَ وَالْعَافِيَةَ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ، فَإِنَّكَ إِذَا أُعْطِيتَهُمَا فِي الدُّنْيَا، ثُمَّ أُعْطِيتَهُمَا فِي الْآخِرَةِ فَقَدْ أَفْلَحْتَ))

((Unamwomba Rabb wako Al-‘Afwa na Al-‘Aafiyah duniani na Aakhirah. Kwani wewe kama utapewa mawili hayo duniani, kisha ukapewa mawili hayo Aakhirah, basi umefuzu bila shaka)). [Imesimuliwa na Ahmad 19/304 Hadiyth nambari 12291 na At-Tirmidhiy Hadiyth nambari 3512].

 

 

Hivi ndivyo walivyokuwa Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na hima ya juu kabisa ya kutaka kujua du’aa bora zaidi ya kuomba.

 

 

Na ndivyo alivyokuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akiomba asubuhi na jioni.

 

 Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) akisema: "Hakuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akiacha kuomba du’aa hizi inapomfikia jioni, na anapopambaukiwa:

 

((اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْعَافِيَةَ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ، اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْعَفْوَ وَالْعَافِيَةَ فِي دِينِي وَدُنْيَايَ وَأَهْلِي وَمَالِي، اللَّهُمَّ استُرْ عَوْرَاتي، وآمِنْ رَوْعَاتي، اللَّهمَّ احْفَظْنِي مِنْ بَينِ يَدَيَّ، ومِنْ خَلْفي، وَعن يَميني، وعن شِمالي، ومِن فَوْقِي، وأعُوذُ بِعَظَمَتِكَ أنْ أُغْتَالَ مِنْ تَحتي )).

((Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba Al-‘Aafiyah duniani na Aakhirah. Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba Al-‘Afwa na Al-‘Aafiyah katika Dini yangu, dunia yangu, watu wangu na mali yangu. Ee Allaah! Nisitiri aibu zangu, na Nipe amani na usalama kwa ninavyoviogopa. Ee Allaah! Nihifadhi toka mbele yangu, toka nyuma yangu, toka kulia kwangu, toka kushoto kwangu na kutoa juu yangu. Na ninajilinda kwa Uadhama Wako kushambuliwa toka chini yangu)).

 

 

Na imepokelewa toka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akisema: Nilikuwa namtumikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kila anaposhuka. Nami nilikuwa nikimsikia akikithirisha kusema:

 

((اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنَ الْهَمِّ وَالْحَزَنِ، وَالْعَجْزِ وَالْكَسَلِ، وَالْبُخْلِ وَالْجُبْنِ ، وَضَلَعِ الدَّيْنِ، وَغَلَبَةِ الرِّجَالِ))

((Ee Allaah! Hakika mimi najilinda kwako na hamu na huzuni, na ajizi na uvivu, na ubakhili na woga, na kulemewa na madeni na kudhalilishwa na watu)). [Al Bukhaariy Hadiyth nambari 6363].

 

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amejilinda na mambo haya yote kwa kuwa yanachafua raha ya maisha ya mtu kwa pande zake zote kisaikolojia, kimwili, kiakili na kwenye moyo.

 

 

Hamu na huzuni zina madhara makubwa kwa mwili. Zinanyong'onyeza nguvu za mtu, zinachafua fikra na akili, zinamkosesha mtu mambo mengi ya kheri na kumfanya asitekeleze mawajibiko yanayompasa kwa ufanisi unaotakiwa. Hii ni hamu ya dunia.

 

 

Ama ikiwa ni hamu ya Aakhirah, hii inatakiwa kwa kuwa inamfanya Muislamu azidishe kasi ya kuyafanya kheri na mema na kumchunga Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  katika nyenendo zake zote. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  anasema:

 

((مَنْ جَعَلَ الْهُمُومَ هَمًّا وَاحِدًا: هَمَّ الْمَعَادِ، كَفَاهُ اللَّهُ هَمَّ دُنْيَاهُ، وَمَنْ تَشَعَّبَتْ بِهِ الْهُمُومُ في أَحْوَالِ الدُّنْيَا، لَمْ يُبَالِ اللَّهُ فِي أَيِّ أَوْدِيَتِهِ هَلَكَ))

((Mwenye kuzifanya humuum (dhiki, wahka) kuwa hamu moja; hamu ya siku ya miadi, Allaah Atamtosheleza na hamu ya dunia. Na ambaye humuum zitamchukua huku na kule katika hali za dunia, Allaah Hatojali ni katika bonde gani kati ya mabonde Yake atahiliki)). [Ibn Maajah 4106, Al-Haakim 2/443, Ibn Abiy Shaybah 13/220 na Al-Bazzaaz 5/68. Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahiyh Ibn Maajah  207].

 

 

Ama madeni mazito anayodaiwa mtu, hili pia ni tatizo linalomfanya mtu asilingamane na kuwa sawa. Wakati wote anakuwa akiandamwa na jinamizi la wadai wake kumuulizia madeni yao, kumsumbua na hata wakati mwingine kumtishia kuchukua hatua kali dhidi yake ya kumshitaki, na hivyo kuishia jela. Na hata wakati mwingine inabidi ageuze njia akiwaona kwa mbali, au afunge mawasiliano nao ili kupata nafasi ya kupumua, na pia kuwaahidi ahadi za uongo. Hayo yote humkosesha raha na hata uimara wa kumtii Allaah hudhoofika kutokana na msongo wa mawazo.

 

 

Jingine alilojilinda nalo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ni kudhalilishwa na watu kwa njia ya dhulma, kunyanyaswa na kunyanyapaliwa. Hii ni kama polisi wanavyowafanyia watu kwa kuwapiga bila makosa, kuwavua nguo, kuwatesa kimwili na kisaikolojia, kuwanajisi, kuwabaka na mengineyo mengi. Mtu akifanyiwa haya, hunyong'onyea kabisa kisaikolojia na kujiona si mtu tena mwenye thamani, na hali hii hudhoofisha ari yake ya uzalishaji, utendaji mambo ya kheri na mengineyo mazuri.

 

 

Inatakikana kwa kila Muislamu akithirishe du’aa hii tukufu. Tunaihitajia sana du’aa hii na hususan katika zama zetu za leo zilizojaa humumu, ghumumu na uadui kutoka pande zote. Tunamwomba Allaah salama katika Dini yetu na dunia yetu.

 

 

Share