011-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Kustanji (Kuchamba)

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

011-Kustanji (Kuchamba)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Maana Ya Kustanji Na Hukmu Yake

 

Kustanji ni (neno la Kiarabu katika wazn wa) "Istif'-aal" kutokana na neno: (نجوت الشجرة) yaani: "Nimeukata mti". Ni kana kwamba amejiondoshea adha.

Na katika istilahi, ni kusafisha athari ya kilichotoka kwenye njia mbili (ya mbele na nyuma) kwa jiwe au karatasi na mfano wake.

Pia huitwa "Al-Istijmaar" kwa vile mtu hutumia vijiwe vidogo katika kustanji, na na huitwa pia Al-Istitwaabah", kwa vile mtu huutakasa mwili wake kwa kuuondoshea uchafu. [Al-Mughniy (1/205)].

 

 

Hukmu Yake:

 

Kustanji ni lazima kwa kila kilichozoeleka kutoka katika njia mbili kama mkojo, madhii na kinyesi (kwa mujibu wa Jamhuri ya Maulamaa kinyume na Abuu Haniyfah).  [Mahanafi wamesema: Kustanji ni Sunnah iliyokokotezwa madhali najsi haijavuka sehemu yake ya kutokea. Wanatolea dalili Hadiyth isemayo: ((Mwenye kustanji kwa vijiwe, basi afanye kwa idadi ya witri. Mwenye kufanya, basi kafanya vizuri, na ambaye hakufanya, basi hapana ubaya kwake)). Na hii ni Hadiyth Dhwa’iyf.  Angalia Kitabu cha Dhwa’iyf Al Jaami’i (5468)].

 

 Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 ((إذا ذهب احدكم إلى الغائط فليستطب بثلاثة احجار فإنها تجزيء عنه))

((Anapokwenda mmoja wenu haja kubwa, basi astanji kwa vijiwe vitatu, kwani vinamtosheleza)). [Hadiyth Hasan. Kuna Hadiyth kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (40), An-Nasaaiy (1/18), Ahmad (6/108 – 133) kwa Sanad Dhwa’iyf. Kuna Hadiyth nyingine kama hii iliyopokelewa na Swahaba mwingine yenye kuitilia nguvu. Angalia Al-Irwaa (44)].

 

Na hii ni amri, nayo ni amri ya wajibu. Kisha neno lake:

 

((فإنها تجزيء))

 

((kwani humtosheleza))…

 

 

…na neno kutosheleza hutumika katika wajibu. Na Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

((لا يستنجى أحدكم بدون ثلاثة أحجار))

 

((Asistanji mmoja wenu kwa chini ya vijiwe vitatu)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (262), An-Nasaaiy (1/16), At-Tirmidhiy (16) na Abuu Daawuud].

 

Na katazo la kupunguza chini ya vijiwe vitatu, kunahukumia uharamu. Na itakapokuwa ni haramu kuacha baadhi ya najsi, basi kuiacha yote ni vibaya zaidi.

 

 

Share