015-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Adabu Za Kukidhi Haja

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

015-Adabu Za Kukidhi Haja

 

Alhidaaya.com

 

 

Mwenye kutaka kukidhi haja ndogo au kubwa, inatakikana ajihimu kwa adabu zifuatazo:

 

1.   Ajisitiri na ajiweke mbali na watu na hasa hasa uwandani. 

 

Imepokelewa na Jaabir (Radhi za Allaah ziwe juu yake), amesema: “Tulitoka na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika safari. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hafiki uwandani, isipokuwa hupotea asionekane.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (2) na Ibn Maajah (335), na tamshi ni lake].

 

 

2- Asiwe na kitu chenye utajo wa Allaah Mtukufu [Angalia Al-Majmuu (2/87), Al-Mughniy (1/227) na Al-Awswat (1/342)].

 

Ni kama pete iliyotiwa nakshi ya Jina la Allaah na vinginevyo. Hii ni kwa vile kulitukuza Jina la Allaah Mtukufu ni jambo ambalo kidini linajulikana na wote. Allaah Mtukufu Anasema:

 

ذَلِكَ وَمَنْ يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّهِ فَإِنَّهَا مِنْ تَقْوَى الْقُلُوبِ 

(( Ndivyo hivyo! Na anayetukuza alama za ‘Ibaadah za Allaah, basi hayo ni katika taqwa ya nyoyo)). [Al-Hajji (22:32)).

 

Hii ni kwa yaliyopokelewa toka kwa Anas kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiivua pete yake anapoingia msalani. [Hadiyth Dwa’iyf. Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy na Ibn Maajah. Al-Albaaniy kasema ni Dhwa’iyf.

 

 Na Hadiyth hii ni Munkar, wahafidhi wameitia dosari.

 

Na linalojulikana ni kwamba pete ya Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa imetiwa nakshi iliyoandikwa “Muhammad Rasuwlul Laah”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5872), Muslim (2092) na wengineo.]

 

Ninasema (Abuu Maalik): “Ikiwa pete hii au mfano wake imesitiriwa kwa kitu kama kuwekwa mfukoni au sehemu nyingine kama hiyo, basi itajuzu kuingia nayo. Ahmad bin Hanbal anasema: “Akitaka ataifumbata katika kiganja chake”.

 

Ikiwa atahofia kupotea kama ataiacha nje, basi itajuzu kuingia nayo kwa vile imelazimu. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

 

3- Apige BismiLlaah na ajilinde kwa Allaah wakati wa kuingia msalani

 

Atafanya hivi kama ataingia sehemu iliyojengwa (choo). Lakini kama itakuwa ni uwandani, basi atafanya hivyo wakati anapoinyanyua nguo yake. Hii ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

((ستر مابين الجن وعورات بني آدم اذا دخل أحدهم الخلاء أن يقول: بسم الله))

((Kinga iliyoko kati ya jini na tupu za wanaadamu anapoingia mmoja wao msalani, ni kusema “BismiLlaah”)).[Al-Albaaniy kasema  ni Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na At-Tirmidhiy na Ibn Maajah. Angalia “Swahiyh Al- Jaami’i” (3611)].

 

Na imepokelewa na Anas (Radhi za Allaah ziwe juu yake) akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anasema wakati anapoingia msalani:

 

اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِك  من الْخُبُثِ وَالْخَبَائِثِ 

 

((Ee Allaah! Hakika mimi ninajilinda Kwako na majini wa kiume na majini wa kike)).[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (142) na Muslim (372)].

 

4- Atangulize mguu wa kushoto wakati wa kuingia, na mguu wa kulia wakati wa kutoka

 

Abuu Maalik: “Sikupata katika hili kauli thibitishi toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lakini Ash-Shawkaaniy amesema katika “As-Saylu Al-Jarraar” (1/64): Ama kutanguliza mguu wa kushoto wakati wa kuingia na mguu wa kulia wakati wa kutoka, basi hili lina hikmah yake. Ni kuwa vitu vitukufu huanziwa kwa kulia na visivyo vitukufu huanziwa kwa kushoto. Na bila shaka yenye kuonyesha hilo yamekuja katika ujumuishi.”

 

5- Asielekee Qiblah au kukipa mgongo wakati anapokaa kukidhi haja

 

Ni kwa Hadiyth ya Abu Ayyuub Al-Answaariy (Radhi za Allaah ziwe juu yake) aliyepokea toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), amesema: 

 

(( إذا أتيتم الغائط فلا تستقبلوا القبلة ولا تستدبروها، ولكن شرقوا أو غربوا)) 

((Mnapokwenda haja kubwa, msikielekee Qiblah wala msikipe mgongo, bali elekeeni mashariki au magharibi)).

Abuu Ayyuub anasema: “Tukafika Shaam, tukakuta vyoo vimejengwa kuelekea Ka’abah, tukawa tunakiepa na kumwomba Allaah Mtukufu maghfirah”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (394), Muslim (264) na wengineo. 

 

Lakini hata hivyo, imepokelewa kwa njia sahihi toka kwa Ibn ‘Umar kwamba amesema: “Siku moja nilipanda juu ya paa la nyumba yetu, nikamwona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya matofali mawili akikidhi haja na ilhali ameelekea Baytul Maqdis”.[Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (145), Muslim (266) na wengineo.]

 

Na ikiwa ameelekea Baytul Maqdis na yeye yuko Madiynah, basi atakuwa ameipa mgongo Ka’abah!!

 

Ninasema (Abuu Maalik): “Na ili kuzifahamu Hadiyth hizi mbili, kuna kauli nne mashuhuri za Maulamaa:  [Amezitaja An Nawawiy kwenye Al-Majmuu’i (2/82), na Al-Haafidh kwenye Al-Fat-h (1/296), na ameongeza kauli tatu nyingine].

 

1- Ni kuwa katazo la kuelekea Qiblah na kukipa mgongo ni kwa hali zote sawasawa ikiwa ndani ya jengo au uwandani.

 

Haya ni madhehebu ya Abuu Haniyfah, Ahmad na Ibnu Hazm. Shaykh wa Uislamu pia ana msimamo huu. Ibnu Hazm amelinukulu hili toka kwa Abuu Hurayrah, Abuu Ayyuub, Ibn Mas’uud na Suraaqah bin Maalik. Pia amepokea toka kwa Atwa’a An-Nakh’i, Ath-Thawriy, Al-Awzaa’iy na Abuu Thawr. [Al-Muhallaa (1/194), Al-Fat-h (1/296), Al-Awswat (1/334), As Sayl Al-Jarraar (1/69) na Al-Ikhtiyaaraat Al- Fiqhiyyah (8)]. Wametoa hoja yao kwa kuitumia Hadiyth ya Abuu Ayyuub iliyotangulia.

 

Wameijibu Hadiyth ya Ibn Umar kwa mambo haya:

 

(a) Lililokatazwa linatangulizwa kabla ya lililoruhusiwa.

 

(b) Hakuna ndani ya Hadiyth hiyo kwamba hilo lilikuwa baada ya kukatazwa kuelekea Ka’abah au kuipa mgongo.

 

(c) Kitendo chake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakipingani na kauli inayouhusu umma isipokuwa kwa lile lenye dalili yenye kuashiria kwamba alitaka kumuiga katika hilo. Na kama si hivyo, basi kitendo chake kilikuwa kinamuhusu yeye mwenyewe.

 

Ninasema: “Huenda kauli yao hii ya mwisho inapata nguvu ya kuwa Ibn ‘Umar kumwona Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumeafikiana naye bila ya kukusudia. Kana kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutaka kwa hilo kubainisha hukmu mpya ya kisharia”.

 

2- Ni kuwa katazo hilo linahusiana na sehemu wazi tu lakini si ndani ya jengo.

 

Hili limesemwa na Maalik na Ash-Shaafi’iy. Kwa kauli yao hii, wao wamepitia mkondo wa kukusanya baina ya dalili mbili. Wamesema: “Kaida isemayo “Kauli hutangulizwa kabla ya kitendo”, bila shaka hutumiwa katika hali ya kuthibiti umahususi, na umahususi huo hauna dalili yoyote”.

 

3- Ni kuwa inajuzu kukipa mgongo Qiblah lakini haifai kukielekea.

 

Hili limehadithiwa toka kwa Abuu Haniyfah na Ahmad, wakiuchukulia udhahiri wa Hadiyth ya Ibn ‘Umar na Hadiyth ya Abuu Ayyuub.

 

4- Ni kuwa inajuzu kuelekea Qiblah na kukipa mgongo katika hali zote.

Hii ni kauli ya ‘Aaishah, ‘Urwah, Raby’a na Daawuud. Hoja yao wanasema kuwa Hadiyth zimegongana, na kwa hivyo suala linarejea katika asili yake ya uhalali.

 

Ninasema (Abuu Maalik): ”Huenda kauli ya kwanza ya kuharamisha kabisa hali zote mbili, ndiyo dalili yenye nguvu zaidi na yenye kinga zaidi kuitumia. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.

 

5- Ajiepushe kabisa na maneno ila kwa dharura.

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar (Radhi za Allaah ziwe juu yake) akisema kwamba mtu mmoja alimpitia Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa anakidhi haja ndogo, akamsalimia na Rasuli hakujibu. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (370), Abuu Daawuud (16), At Tirmidhiy, An Nasaaiy (1/15) na Ibn Maajah (353).

 

Kujibu maamkizi ni wajibu. Na Rasuli alipoacha kujibu, inaonyesha kuwa ni haramu kuzungumza na hasahasa kama ni kumtaja Allaah Mtukufu. Lakini ikiwa atazungumza kwa ajili ya haja isiyoepukika kama kumwongoza mtu, au kuomba maji au mfano wa hayo, basi itaruhusika kutokana na dharura. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 

6- Ajiepushe kukidhi haja njiani wanamopita watu, sehemu wanapopumzikia kupata kivuli na mfano wa sehemu hizo.

 

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 ((اتقوا اللاعنين، قالوا: وما اللاعنان يا رسول الله؟ قال: الذي يتخلى في طريق الناس أو في ظلهم))

((Waogopeni wawili waliolaaniwa)). Wakasema: Ni nani hao wawili waliolaaniwa ee Rasuli wa Allaah? Akasema: ((Ni yule anayejisaidia njiani wanamopita watu au katika kivuli chao)). [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (68) na Abuu Daawuud(25)].

 

7- Ajiepushe kukojoa mahala pa kuogea.

 

Na hasahasa kama maji yanajikusanya mahala hapo kama kwenye hodhi (bath tub) na kadhalika. Kwani Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu kukojoa mahala anapoogea. [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na An Nasaaiy (1/130) na Abuu Daawuud (28)].

 

8- Ajiepushe kukojoa katika maji yaliyotuama tuli.

 

Ni kwa Hadiyth ya Jaabir aliyesema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza watu kukojoa katika maji yaliyotuama.  [Hadiyth Swahiyh. Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (281) na An Nasaaiy (1/34).

 

09- Atafute sehemu laini wakati wa kukojoa na ajiepushe sehemu ngumu ili kujikinga najsi isimrudie.

 

10- Ashikamane na adabu za kustanji tulizotangulia kuzitaja.

 

11- Aseme wakati anapotoka: “Ghufraanak”.

 

Imepokelewa toka kwa Aaishah akisema kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anatoka msalani, alikuwa akisema: “Ghufraanak”.[Hadiyth Hasan Lighayrihi. Imefanyiwa “ikhraaj” na At Tirmidhiy (7), Abuu Daawuud (30) na Ahmad (6/155)].

 

 

 

Share