025-Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-HAKAM

 

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Swifa Zake

 

Alhidaaya.com

 

 

الْحَكَمْ

 

AL-HAKAM

  

 

 

 

 

Al-Hakam: Hakimu/Mwamuzi: Ni Ambaye ana hukumu baina ya viumbe Wake kwa uadilifu, hamdhulumu yeyote kati yao. Naye Ndiye Aliyeleta kitabu Chake kitukufu ili kiwe hakimu baina ya watu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

أَفَغَيْرَ اللَّـهِ أَبْتَغِي حَكَمًا وَهُوَ الَّذِي أَنزَلَ إِلَيْكُمُ الْكِتَابَ مُفَصَّلًا ۚ  

 (Sema): “Je, nitafute hakimu ghairi ya Allaah na hali Yeye Ndiye Ambaye Aliyekuteremshieni Kitabu kilichofasiliwa waziwazi?”  [Al-An’aam: 114]

 

Wala hambebeshi mwingine mzigo wa mwingine, wala hamlipi mja kwa zaidi ya dhambi zake, na hufikisha haki kwa wanaostahiki, haachi kumpa mwenye haki ila atakuwa amemfikishia haki yake. [Al-Asnaa 1/437]

 

Hukumu Zake ni za aina mbili:

 

a-Hukumu za ki-Ulimwengu:

 

Ni hukmu Anazozihukumu katika uumbaji Wake mbali mbali wa vitu na uendeshaji Wake mfano mzunguko wa dunia, mabadiliko ya usiku na mchana, kuchomoza na kukuchwa jua, mwezi kuanza upya na kumalizikia idadi ya siku zake,  kama Anavyosema:

 

وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَّهَا ۚ ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ ﴿٣٨﴾

Na jua linatembea hadi matulio yake. Hiyo ni takdiri ya Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mjuzi wa yote.

 

وَالْقَمَرَ قَدَّرْنَاهُ مَنَازِلَ حَتَّىٰ عَادَ كَالْعُرْجُونِ الْقَدِيمِ ﴿٣٩﴾

Na mwezi Tumeukadiria vituo mpaka ukarudi (mwembamba) kama kwamba karara la shina la mtende lililopinda la zamani.

 

 

لَا الشَّمْسُ يَنبَغِي لَهَا أَن تُدْرِكَ الْقَمَرَ وَلَا اللَّيْلُ سَابِقُ النَّهَارِ ۚ وَكُلٌّ فِي فَلَكٍ يَسْبَحُونَ ﴿٤٠﴾

Halipasi jua kuudiriki mwezi, na wala usiku kuutangulia mchana; na vyote viko katika falaki vinaogelea. [Yaasiyn: 38-40]

 

Nayo ni hali halisi ambayo haikwepeki, nayo inahusiana na matakwa Yake Allaah ('Azza wa Jalla) ambayo hayawi ila kwa maana ya kilimwengu; Anayotaka ndio yanakuwa, na Asichotaka hakiwi.  Hukmu Yake hairejeshwi wala hapana baada ya hukumu Yake na hakuna mwenye kushinda jambo lake Anapolihukumu.

 

 

b-Hukumu ya ki-Shariy’ah

 

Shariy'ah zilizowekwa kwa ajili ya wana Aadam kuzifuata zinazohusiana na maamrisho na makatazo Yake, na Shariy'ah zinazohusiana na utendaje wa 'ibaadah.  Hizi ni hukumu za kimajukumu ya ki-Shariy’ah, ambazo ni hukumu zilizokuwa nzuri zaidi, ambayo ni mambo mema na ukamilifu wake, wala Dini yao haiongoki isipokuwa kwa kufuata hukumu hizi, ambazo Amezifanya kuwa ni Shariy’ah katika ndimi za Manabii. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

وَمَنْ أَحْسَنُ مِنَ اللَّـهِ حُكْمًا لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ ﴿٥٠﴾

Na nani mbora zaidi kuliko Allaah katika kuhukumu kwa watu wenye yakini. [Al-Maaiidah: 50]

 

Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

  ((إِنَّ اللَّهَ هُوَ الْحَكَمُ وَإِلَيْهِ الْحُكْمُ))  

 Hakika Allaah ndiye Hakimu na Kwake kuna hukmu zote))   [Abuu Daawuwd na wengineo].

 

Hukmu hii ndio ambayo mtu atalipwa kwayo thawabu au adhabu, katika Siku ya hesabu.

 

Na aina mbili za hukmu hizo zinaingia kwa mja. Hukmu ya kilimwengu inapita kwake, naye anadhalilishwa kwayo atake au asitake. Na hukumu za kilimwengu haiwezikani kwenda kinyume chake.  Ama hukmu za ki-Shariy’ah mja anaweza kwenda kinyume nazo, na hukmu Zake zote hizi ni kwa hekima, na uadilifu, nayo ni hukumu ya uadilifu ambayo maneno Yake yametimia kwa ukweli katika habari, na uadilifu katika maamrisho, na makatazo.  Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) aliyetekeleza hukmu Zake kwa waja Wake na Akafanya uadilifu baina yao katika hukumu zao, na kuwaenea kwa rahmah Zake Allaah ('Azza wa Jalla) na Akawaweka katika matakwa Yake.  

 

Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah; Al-Hakam:

 

1-Jina na Sifa ya Al-Hakam imethibiti kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Pekee kama vile ambavyo hakuna mshirika pamoja naye katika kumwabudu, basi pia hakuna wa kushiriki Naye katika Hukmu Zake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

  وَلَا يُشْرِكُ فِي حُكْمِهِ أَحَدًا ﴿٢٦﴾

na wala Hamshirikishi katika hukumu Zake yeyote. [Al-Kahf: 26]

 

2-Muumini anapaswa kuelemea na kukubali  hukmu za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٦٥﴾

Basi Naapa kwa Rabb wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasipate katika nyoyo zao karaha katika yale uliyohukumu na wajisalimishe, kwa kujisalimisha kikamilifu. [An-Nisaa: 65] 

 

Na Sababu ya kuteremshwa Aayah hiyo na kama ilivyothibiti  ifuatavyo:

 

Az-Zubayr bin Al-‘Awwaam (رضي الله عنه)  na bwana mmoja katika Answaar, pale walipokhitilafiana kuhusu mfereji wa kupitisha maji ya mvua waliokuwa wakitumia maji yake. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akatoa hukmu baina yao kwamba Az-Zubayr amwagilie maji ardhini mwake kisha ayaache yatiririke kwa Answaar. Akakasirika Answaar huyo na kumwambia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): “Umempendelea yeye kwa kuwa ni mtoto wa ‘ammat yako! Hapo Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) akabadilika uso rangi kwa hasira akamwambia tena Az-Zubayr amwagie maji kwanza kisha yatiririke kwa jirani yake huyo kwa kuwa hukumu hiyo ilikuwa kwa manufaa ya wote wawili. Hivyo akampatia Az-Zubayr haki yake. Ikateremka Aayah hii: “Basi Naapa kwa Rabb wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao… (4: 67). [Amehadithia Az-Zubayr (رضي الله عنه) ameipokea Al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

 

3-Unapokuwa ni hakimu wa watu unapaswa uhukmu bila ya kupendelea. Allaah (‘Azza wa Jalla) Anasema:

 

وَإِذَا حَكَمْتُم بَيْنَ النَّاسِ أَن تَحْكُمُوا بِالْعَدْلِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ نِعِمَّا يَعِظُكُم بِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ سَمِيعًا بَصِيرًا ﴿٥٨﴾

Na mtakapohukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Hakika uzuri ulioje Anayokuwaidhini nayo Allaah; hakika Allaah daima ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote. [An-Nisaa: 58]

 

Na pindi ukidhulumiwa vuta subira na muombe Al-Hakam Akuhukumie dhulma uliyotendwa kwani Yeye Ndiye Mbora wa mahakimu. Anasema Allaah (‘Azza wa Jalla):

 

  وَاصْبِرْ حَتَّىٰ يَحْكُمَ اللَّـهُ ۚ وَهُوَ خَيْرُ الْحَاكِمِينَ﴿١٠٩﴾

na subiri mpaka Allaah Ahukumu. Naye ni Mbora wa wanaohukumu.  [Yuwnus: 109]

 

Na Anasema pia (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

أَلَيْسَ اللَّـهُ بِأَحْكَمِ الْحَاكِمِينَ ﴿٨﴾

Je, kwani Allaah Si Mwadilifu zaidi wa wanaohukumu kuliko mahakimu wote?   [At-Tiyn: 8]

 

 

 

 

4-Omba du’aa ya Sunnah ifuatayo unapopatwa huzuni:

 

اللّهُـمَّ إِنِّي عَبْـدُكَ، ابْنُ عَبْـدِكَ، ابْنُ أَمَتِـكَ نَاصِيَتِي بِيَـدِكَ، مَاضٍ فِيَّ حُكْمُكَ، عَدْلٌ فِيَّ قَضَاؤكَ، أَسْأَلُـكَ بِكُلِّ اسْمٍ هُوَ لَكَ، سَمَّـيْتَ بِهِ نَفْسَكَ، أِوْ أَنْزَلْتَـهُ فِي كِتَابِكَ، أَوْ عَلَّمْـتَهُ أَحَداً مِنْ خَلْقِـكَ، أَوِ اسْتَـأْثَرْتَ بِهِ فِي عِلْمِ الغَيْـبِ عِنْـدَكَ، أَنْ تَجْـعَلَ القُرْآنَ رَبِيـعَ قَلْبِـي، وَنورَ صَـدْرِي، وجَلَاءَ حُـزْنِي، وذَهَابَ هَمِّـي 

Ee Allaah hakika mimi ni mtumwa Wako, mtoto wa mtumwa Wako, mtoto wa kijakazi Chako, utosi wangu uko Mikononi Mwako, yaliyopita kwangu yako katika hukumu Yako, ni usawa kwangu kunihukumu Kwako, nakuomba kwa kila Jina ambalo ni Lako Ulilojiita Kwako Mwenyewe au Uliloliteremsha katika Kitabu Chako, au Ulilomfundisha yoyote yule kati ya viumbe Vyako, au Ulilolihifadhi Wewe mwenyewe (na kujihusisha kulijuwa) katika ilimu ya ghaibu Kwako, nakuomba Ujaalie Qur-aan kuwa ni rabiy' (uhuisho, raha, furaha na ustawisho) wa moyo wangu na nuru ya kifua changu, na ufumbuzi wa  huzuni yangu [Hadiyth ya ‘Abdullaahi bin Mas-‘uwd (رضي الله عنه) - Ahmad (1/391) [452], Al-Haakim (1/509) na ameisahihisha Al-Albaaniy (رحمه الله) katika Al-Kalimi Atw-Twayyib [124].

 

 

 

Share