07-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Allaah Na Malaika Wanamswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Na Amri Kwa Waumini Wamswalie

Fadhila Za  Nabiy  (صلى الله عليه وآله وسلم)

07-Allaah Na Malaika Wanamswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

Na Amri Kwa Waumini Wamswalie

 

www.alhidaaya.com

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾

Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini mswalieni na msalimieni kwa maamkizi ya amani na kwa tasliymaa.  [Al-Ahzaab 33: 56]

 

Maana ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Ni kumsifia kwa Malaika, kumteremshia rahmah na baraka, fadhila n.k.

 

Maana ya Malaika Wake kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kumuombea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  du’aa Amghufurie na Amteremshie baraka.  

 

Maana ya Waumini kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kumuombea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) du’aa na amani. Juu ya hivyo Waumini kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inawarudia wenyewe thawabu tele kutokana na fadhila zilizotajwa katika Hadiyth kadhaa za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), miongoni mwazo ni:

 

عنْ عبد اللَّه بن عمرو بن العاص رضي اللَّه عنْهُمَا أنَّهُ سمِع رسُول اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم يقُولُ: ((مَنْ صَلَّى عَلَيَّ صَلاَةً، صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ بِهَا عشْراً))  رواهُ مسلم

Imetoka kwa 'Abdullaah bin 'Amru bin Al'-Aasw (رضي الله عنهما)  kwamba kamsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Atakayeniswalia mara moja, Allaah Atamswalia mara kumi)) [Muslim]

 

Na pia:

 

عن ابن مسْعُودٍ رضي اللَّه عنْهُ أنَّ رسُول اللَّهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم قال: ((أَوْلى النَّاسِ بي يوْمَ الْقِيامةِ أَكْثَرُهُم عَليَّ صلاةً)) رواه الترمذي وقال: حديثٌ حسنٌ

Imetoka kwa Ibn Mas'uwd (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watu wa mwanzo kwangu (watakaokuwa karibu yangu) siku ya Qiyaamah ni wale wanaoniswalia sana))  [At-Tirmidhy na kasema ni Hadiyth Hasan]

 

 

Na pia:

 

عنْ أبي هُريْرةَ رضي اللَّه عنهُ أنَّ رسُولَ اللَّه صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم قال: ((ما مِنْ أحد يُسلِّمُ علَيَّ إلاَّ ردَّ اللَّه علَيَّ رُوحي حَتَّى أرُدَّ عَليهِ السَّلامَ)) رواهُ أبو داود بإسناد صحيحٍ

Imetoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hapana yeyote atakayeniswalia ila Allaah Hurudishia mimi roho yangu hadi nimrudishie salaam (huyo aliyenisalimia))) [Abuu Daawuwd kwa IsnaadHasan]

 

 

Share