037-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Muda Wa Kupukusa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

037-Muda Wa Kupukusa

 

Alhidaaya.com

 

 

Sharia imeweka muda wa siku tatu na masiku yake kupukusa juu ya khufu mbili kwa msafiri, na siku moja na usiku wake kwa mkazi. Haya ndiyo yaliyokubaliwa na Jamhuri ya Maulamaa wa Hanafi, Hanbali, Dhwaahir na Ash-Shaafi’iy katika madhehebu mapya na Adh-Dhwaahiriyyah. [Al-Mabsuwtw (1/98), Al-Ummu (1/34), Al-Mughniy (1/209) na Al-Muhalla (2/80)].

 

Dalili ya hayo ni haya yafuatayo:

 

1- Ni Hadiyth ya ‘Aliy (Allaah Amridhie) aliyesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameweka muda wa siku tatu na masiku yake kwa msafiri, na siku moja na usiku wake kwa mkazi”.[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Muslim (276) na An-Nasaaiy (1/84)].

 

2- Ni Hadiyth ya ‘Ouf bin Maalik Al-Ashja’iy aliyesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru kupukusa juu ya khufu mbili katika Vita vya Tabuk siku tatu na masiku yake kwa msafiri, na siku moja na usiku wake kwa mkazi”.[Hadiyth Swahiyh.: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ahmad (6/27) kwa Sanad Swahiyh, nayo ina ushahidi toka Hadiyth ya Abu Bakrah iliyoko kwa Ibn Maajah (556) na wengineo].

 

3- Hadiyth ya Swafwan bin ‘Assal, amesema: “Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akituamrisha tunapokuwa safarini, tusizivue khufu zetu siku tatu na masiku yake ila kwa janaba, lakini si kwa kwenda haja kubwa, au ndogo, au kulala”. [Hadiyth Hasan: Imetajwa hivi karibuni].

 

Maalik amekwenda kinyume na haya (nayo ni kauli ya zamani ya Ash-Shaafi’iy). Yeye anaona kwamba hakuna muda wake maalumu, bali mtu anaweza kupukusa juu ya khufu zake madhali hakuzivua au kupatwa na janaba!! Na ndivyo hivi hivi alivyosema Al-Layth.  [Al-Mudawwanah (1/41) na Bidaayat Al-Mujtahid (1/24)].

 

Wao wametoa hoja kwa Hadiyth ambazo ni Dhwa’iyf. Kati ya Hadiyth hizo ni:

 

1- Iliyopokelewa toka kwa Ubayya bin ‘Ammaarah, amesema: “Nilisema: Ee Rasuli wa Allaah! Je, nipukuse juu ya khufu mbili? Akasema: Ndiyo. Nikasema: Siku moja? Akasema: Siku moja. Nikasema: Na siku mbili je? Akasema; Na siku mbili. Nikasema: Na siku tatu je? Akasema: Na siku uzitakazo”.[Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (157), At-Tirmidhiy na Ibn Maajah (553).]  

 

2- Yaliyopokelewa toka kwa Khuzaymah bin Thaabit, amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuwekea siku tatu, na lau kama tungelimtaka atuongezee, basi angetuongezea”.[Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (1/280)]. Yaani kupukusa juu ya khufu mbili kwa msafiri. Na hili lau kama lingekuwa sahihi, basi haliwezi kuwa hoja, kwani ni dhana tu ya Swahaba, na sisi tusingelichukulia.

 

3- Yaliyopokelewa toka kwa Anas bin Maalik kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((إذا توضأ أحدكم ولبس خفيه فليصل فيهما، وليمسح عليهما، ثم لا يخلعهما إن شاء إلا من جنابة))

((Anapotawadha mmoja wenu akazivaa khufu zake, basi aswali nazo na apukuse juu yake, kisha asizivue muda autakao, isipokuwa kwa janaba)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy (1/280), Atw-Twahaawiy (1/48) na Ad-Daara Qutwniy (72).

 

Hadiyth zote hizi ni dhwa’iyf na hazifai kwa ushahidi.

 

4- Ni athar iliyopokelewa toka kwa ‘Aamir akisema: “Nilitoka Sham kuelekea Madiynah. Niliondoka siku ya ijumaa na nikaingia Madiynah siku ya ijumaa. Kisha niliingia kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab akaniuliza: Ni lini uliziivaa khufu zako? Nikajibu: Siku ya ijumaa. Akauliza: Je, ulizivua? Nikajibu: Hapana. Akasema: Umefanya sawa”.

 

Hii pia ni dhwa’iyf. Al-Bayhaqiy amesema: “Tumepokea toka kwa ‘Umar kuhusu wakati. Basi inawezekana kuwa ima alirejea katika kauli hiyo wakati ilipomfikia toka kwa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au iwe kauli yake iliyowafikiana na Sunnah Swahiyh iliyo mashuhuri zaidi. Na kwa ajili hiyo, Ibn Hazm amesema katika kitabu cha Al-Muhalla (2/93): “ Haiswihi  kwa Swahaba yeyote kukhalifu muda uliowekwa isipokuwa Ibn ‘Umar peke yake”.

 

Share