067-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Twahara: Nini Atafanya Mwenye Jeraha?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Twahara

 

067-Nini Atafanya Mwenye Jeraha?

 

Alhidaaya.com

 

 

Suala hili lina matawi juu ya asli. Ni kuwa, je, inawezekana kukusanya kati ya asili na badali, yaani baina ya wudhuu au ghusli na tayammumi?

 

Suala hili lishazungumziwa kwa uchambuzi.  [Angalia ukurasa wa 192 wa Kitabu hiki].

 

Waliopinga kukusanya kati ya viwili (asili na badali) kama Abuu Haniyfah na Maalik, nalo ndilo tulilolitilia nguvu katika mlango uliopita, wao wanaangalia kilicho kichache zaidi kwa kilicho kingi zaidi. Ina maana kuwa endapo sehemu kubwa ya mwili ina majeraha, basi mtu atatayamamu bila kuviosha viungo vizima vilivyobakia. Na ikiwa sehemu kubwa ya mwili ni nzima, atauosha mwili na ataacha sehemu yenye majeraha. [Al-Mabsuutw (1/112) na Al-Majmu’u (2/333)].

 

Ama wale waliojuzisha kukusanya kati ya ghusli na tayammumi, wanasema kuwa ataosha sehemu nzima ya mwili na yenye majeraha ataifanyia tayammumi. Ash-Shaafi’y na Ahmad wamelisema hili, na Shaykh wa Uislamu anaonekana kama amelikhitari. [Al-Mughniy (1/162), Al-Majmu’u (1/162) na Majmu’u Al-Fataawaa (21/466)].

 

Ninasema: “Inavyoonekana ni kuwa rai ya kwanza ndio sahihi zaidi kama ilivyotangulia, na hakuna katika mlango huu Hadiyth yoyote Swahiyh iliyopokelewa toka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam). Lakini pamoja na haya, kuna Hadiyth ya Jaabir iliyopokelewa. Anasema: “Tulitoka kwenda safari. Mtu mmoja kati yetu alijeruhiwa na jiwe kichwani. Alipolala aliota usingizini (akamwaga), na alipoamka aliwauliza wenzake: “Je, mwaweza kunipatia idhni ya kutayamamu? Wakasema: “Hatuwezi kukuruhusu kutayamamu nawe una uwezo wa kuyatumia maji.” Mtu yule alioga akafa. Tulipokuja kwa Rasuli (Swalla Allaahu 'Alayhi wa Aalihii wa Sallam) alijulishwa hilo naye akasema:

((Wamemwua, Awaue Allaah! Kwa nini wasiulize kama hawajui? Teguzi la asiyejua ni kuuliza. Hakika ilikuwa inamtosheleza tayammumi; akifunge kidonda chake kwa kitambaa, kisha apukuse juu yake, na sehemu iliyobaki ya mwili aioshe)). [Hadiyth Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abuu Daawuud (336), Ad-Daara Qutwniy (1/190) na Al-Bayhaqiy (1/237). Sanad yake ni Dhwa’iyf. Al-AlBaaniy ameifanya Hadiyth Hasan kwa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas iliyopo kwa Abuu Daawuud (337) na Ibn Maajah (572).  Hadiyth hii ni “Munqatwi-’i” na haifai kutolewa ushahidi].

 

Hadiyth hii ni Dhwa’iyf. Walioidhoofisha ni Al-Bayhaqiy, Ibn Hazm na wengineo ingawa Al-Albaaniy ameifanya kuwa Hasan.

 

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar, akisema: “Endapo jeraha halikufungwa, basi ataosha sehemu za pembeni yake tu, na hatoliosha jeraha lenyewe.” [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bayhaqiy].

 

Na imepokelewa kwa njia sahihi toka kwa ‘Ubayd bin ‘Umayr kuhusiana na mtu aliyepatwa na janaba akiwa na jeraha. Amesema: “Aoshe sehemu ya pembeni tu, na  maji yasikurubie jeraha lake”. [Isnadi yake ni Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na ‘Abdul Raaziq (865)].

 

Na hili liko sanjari na madhehebu ya Abuu Haniyfah na Maalik, nalo ndilo lenye nguvu. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.

 

 

Share