011-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Mlango Wa Janaazah: Kuwapa Pole Wafiwa (Ta-‘aziyah)

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

Mlango Wa Janaazah

 

011-Kuwapa Pole Wafiwa (Ta-‘aziyah)

 

Alhidaaya.com

 

 

Inajuzu kisharia kwa watu – wanaume na wanawake- kuwapa ta-’aziyah (kuwafariji) jamaa wa maiti kwa maneno ya kuwaliwaza na kuwaondoshea huzuni, na kuwafanya waridhie na wasubiri kutokana na yale yaliyothibiti toka kwa Rasuli  (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na hii ikiwa watawaendea. Na kama hawakuwaendea, basi watawaazi kwa namna yoyote itakayofanikisha hilo bila kwenda kinyume na sharia. Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kumfariji nduguye Muumini katika msiba wake, Allaah Atamvika kipambo cha kijani afurahishwe kwacho Siku ya Qiyaamah)). Ikasemwa: Ee Rasuli wa Allaah! Nini maana ya kufurahishwa? Akasema: ((Watu watalitamania hilo)). [Al-Albaaniy kasema ni Hasan: Angalia Al-Irwaa (764)].

 

Kati ya yaliyothibiti ya kusemwa katika kumfariji mfiwa (kutoa pole) ni:

(( لله ما أخذ وله ما أعطى، وكل شيء عنده بأجل مسمى، فلتصبر وتحتسب ))

[Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (1224) na Muslim (923)].

 

· Zindusho

 

Ni karaha kukusanyika sehemu maalumu kwa ajili ya kutaazia (kufanya matanga). [Al-Ummu cha Ash-Shaafi’iy (1/248) na Fiqhu As-Sunnah Lin Nisaai (uk. 202)].

 

Hii ni kwa vile kufanya hivyo hujadidisha huzuni na hugharimu. Imesimuliwa katika Hadiyth ya Jariyr bin ‘Abdillaah (Radhwiya Allaahu Anhu) akisema: “ Tulikuwa tunaona kukusanyika kwa jamaa wa maiti na kupikwa chakula, ni katika maombolezo mabaya”. [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Abu Daawuud (3132), At-Tirmidhiy (998) na Ibn Maajah (1610). Inatiliwa nguvu na yanayofuatia].

 

Hivyo mtu asikubali kwenda kwenye mjumuiko huu, bali atoe pole kwa mujibu wa itakavyowepesika kwake.

 

Ama vinavyoitwa khamiys na arubaini zinazofanywa kila mwaka na mfano wake, ni katika bid-’a zilizozushwa zenye kupingana na Dini ya Allaah Mtukufu.

 

· Kuwatayarishia Chakula Wafiwa

 

Ni Sunnah kwa jamaa wa maiti na majirani zake kuwatayarishia chakula wafiwa. Imeripotiwa toka kwa ‘Abdullah bin Ja’afar akisema: “ Rasuli wa Allaah amesema: (( Waandalieni watu wa Ja’afar chakula, kwani limewajilia wao jambo la kuwashughulisha)). [Isnadi yake ni Dhwa’iyf: Imefanyiwa “ikhraaj” na Ibn Maajah (1612) na Ahmad (2/204)].

 

Hadiyth hii ni Dhwa’iyf, lakini inatiliwa nguvu na Hadiyth ya ‘Aaishah ya kwamba yeye alikuwa wakati anapokufa jamaa yake: “Huamuru liletwe jungu la “talbinah” ikapikwa, kisha uji wa shayiri ukatayarishwa, halafu “talbinah” ikamiminwa humo. Halafu husema: Kuleni, kwani mimi nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Talbinah hufariji moyo wa mgonjwa, na huondosha sehemu ya huzuni)). [Hadiyth Swahiyh: Imefanyiwa “ikhraaj” na Al-Bukhaariy (5417) na Muslim (2216)].

 

“Talbinah”, ni chakula kinachopikwa kwa unga, na pia huweza kuongezewa asali.

 

· Zindusho:

 

Ama waliyoyazoea watu kinyume na Sunnah hii, na waliofiwa kuwatayarishia chakula watoaji pole, haya ni makruhu kwa kuwa yanapishana na Sunnah, na kwa Hadiyth iliyotangulia ya Jariyr.

 

 

Share