Kumfanyia Hajj Mama Aliyekuwa Haswali Kabisa
Al-Lajnah Ad-Daaimah
SWALI:
Je, inafaa mtoto wa kike kumfanyia Hajj na kumtolea sadaqah mama yake aliyefariki ambaye hakuwa akiswali katika uhai wake? Nini hukmu ya jambo hili ikiwa mtoto anataka kutimiza wajibu wake (wa kufawanyia wema wazazi) kama alivyopata mafunzo katika Dini yetu ya Kiislam?
JIBU:
Yeyote anayeacha Swalaah makusudi kwa sababu hadhani kuwa ni fardhi kwake, atakuwa amekufuru kutokana na rai waliyokubaliana ‘Ulamaa. Na yeyote anayeacha kuswali kwa sababu ya uvivu au kudharau, basi naye pia atakuwa amekufuru kutokana na rai za ‘Ulamaa wengi. Hii ni kwa sababu Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((إن العهد الذي بيننا و بينهم الصلاة فمن تركها فقد كفر )) أخرجه أصحاب السنن
((Mafungamano baina yetu na wao (Makafiri) ni Swalaah, atakayeiacha amekufuru)) [Abu Dawwuwd, At-Tirmidhy, An-Nasaaiy na Ibn Maajah]
Juu ya hivyo, dalili nyingine kutoka katika Qur-aan na Sunnah zimethibiti hukmu hiyo.
Kwa hiyo, haipasi kumfanyia Hajj au kumtolea sadaqah mtu mwingine aliyekufa ambaye hakuwa akiswali, kama ilivyokuwa haifai kumfanyia Hajj au kutoa sadaqah kwa ajili ya Kafiri.
Wa-BiLLaahi At-Tawfiyq wa Swalla Allaahu ‘alaa Nabiy Muhammad wa Aswhaabihi wasallam.
[Fataawa Al-Lajnatud-Daaimah lil-buhuwthil-'Ilmiyyah wal-Iftaa Mjalada 11, Uk. 113, Swali Namba 2 ya Fatwa Namba 6178 - Imejumuishwa:
Kiongozi Mkuu: Shaykh 'Abdul 'Aziyz ibn 'Abdillaah ibn Baaz
Msaidizi Kiongozi Mkuu: Shaykh ‘Abdur-Razzaaq 'Afiyfiy
Mjumbe: Shaykh 'Abdullaah Ibn Ghudayyaan
Mjumbe: Shaykh 'Abdullaah ibn Qu'uwd]
Kumfanyia Hajj Mtu Kwa Ajili Ya Kupokea Ujira
Shaykh Swaalih Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah)
SWALI:
Je, inaruhusiwa kumfanyia mtu nguzo ya Hajj ambaye anao uwezo wa kifedha na siha kutekeleza mwenyewe Hajj, kwa ajili ya kupata ujira kwake?
JIBU:
Yeyote mwenye uwezo wa kutekeleza mwenyewe nguzo ya Hajj, basi haimpasi kumuwakilisha mtu mwingine kumfanyia Hajj, na hatopata thawabu kutoka kwa Allaah kufanya hivyo.
Ama ikiwa mtu hana uwezo wa kufanya mwenyewe Hajj kutokana na hali ya kudumu inayomzuia kutekeleza fardhi hiyo, basi inaruhusiwa kumuwakilisha mtu mwingine kumfanyia Hajj.
Na hakuna ubaya kupokea ujira (kwa ajili ya kumfanyia mtu Hajj) ikiwa atautumia ujira huo kwa ajili ya Hajj na sio kwa ajili ya kutafuta uchumi wa fedha na kuzitumia katika mambo ya starehe. Tunayo hukmu ambayo baadhi ya ‘Ulamaa wametumia ambayo imetokana na dalili sahihi kwamba: “Yeyote mwenye kutia niyyah ya kufanya Hajj kwa ajili ya uchumi, basi asifanye. Na mwenye kupokea ujira kwa ajili ya kumfanyia mtu Hajj basi anaweza kufanya hivyo.”
[Majmuw' al-Fataawa Ibn Taymiyyah, Mjadala 26, Uk. 19]
Na maana ya hii ni kwamba, yeyote atakayetumia pesa kwa ajili ya kufanya Hajj (matumizi ya Hajj) basi hakuna ubaya lakini yeyote mwenye kufanya Hajj kwa ajili ya kuchuma fedha basi hairuhusiwi.
[Shaykh Swaalih ibn Fawazaan - Al-Muntaqaa min Fataawa Shaykh Swaalih al-Fawzaan – Mjalada 3, Uk. 190, Fatwa Namba 291].
Kumfanyia Hajj Aliyekuwa Kilema
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)
SWALI:
Nina mtoto kilema ambaye namfikiria kuwa akifanya Hajj mwenyewe nakhofu kuwa atataabika na kupata madhara. Hivyo je, naweza kumfanyia Hajj?
JIBU:
Ikiwa mtoto ni kilema kama unavyosema, basi inaruhusiwa kumfanyia fardhi ya Hajj ikiwa wewe mwenyewe umeshafanya fardh ya Hajj.
[Liqa-aat al-Baab al-Maftuwh – Mjalada 1, Uk. 45, Namba 67]
Kumfanyia ‘Umrah Kaka Aliyefariki
Shaykh Swaalih Al-Fawzaan (Hafidhwahu Allaah)
SWALI:
Nimetia nia kumfanyia 'Umrah kaka yangu mkubwa tokea alipofariki. Hivi sasa umefika wakati wa kuweza kumfanyia. Je, kitendo hiki kinafaa katika mafunzo ya dini kuwa thawabu zitamfikia yeye aliyefariki?
JIBU:
Ndio, kwa sababu kitendo chema cha kumfanyia 'Umrah kaka yako aliyefariki ikiwa ni 'Umrah ya fardh (inayoambatana na Hajj) au 'Umrah ya Sunnah (inayopendekezeka). Kwa hiyo hiki ni kitendo kikubwa kizuri. Lakini (kutekeleza huko hiyo 'Umrah) iwe kwa sharti kuwa kwanza wewe mwenyewe umeshatekeleza 'Umrah ya fardhi.
Na Allah Anajua zaidi
[Al-Muntaqaa min Fataawa Shaykh Swaalih Al-Fawzaan – Mjalada 5, Uk. 160, Fatwa Namba 240].
Kurudia Kufanya Umrah Baada Ya Muda Mfupi Kutoka Makkah
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah)
SWALI:
Amefanya 'Umrah, alipomaliza amekwenda Twaaif kwa kazi fulani. Kisha alipomaliza kazi zake Twaaif alitaka kufanya tena 'Umrah kwa ajili ya mtu aliyefariki. Je, inaruhusiwa?
JIBU:
Hakuna ubaya kwake kufanya hivyo. Anapofanya mtu 'Umrah kisha akaondoka Makkah kwenda Twaaif au Jeddah kwa sababu fulani, akapenda kumfanyia 'Umrah mtu aliyefariki, hakuna ubaya, hata kama akirudia tena kufanya hivyo.
Iliyokatazwa ni kubakia Makkah kisha kwenda Tan'iym (Masjid 'Aaishah, penye kutilia Ihraam) ili kurudi Makkah kufanya 'Umrah nyingine. Hii imeharamishwa.
[Liqa-aat al-Baab Al-Maftuwh – Mjalada 1, Uk. 51, Namba 86]
Links
[1] https://www.alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/265
[2] http://www.alhidaaya.com
[3] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9232&title=Fataawaa%3A%20Kumwakilisha%20Mtu%20Kufanya%20%E2%80%98Umrah%20Na%20Hajj
[4] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9233&title=01-Al-Lajnah%20Ad-Daaimah%3A%20Kumfanyia%20Hajj%20Mama%20Aliyekuwa%20Haswali%20Kabisa
[5] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9234&title=02-Shaykh%20Swaalih%20Al-Fawzaan%3A%20Kumfanyia%20Hajj%20Mtu%20Kwa%20Ajili%20Ya%20Kupokea%20Ujira
[6] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9235&title=03-Imaam%20Ibn%20%E2%80%98Uthaymiyn%3A%20Kumfanyia%20Hajj%20Aliyekuwa%20Kilema
[7] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9236&title=04-Shaykh%20Swaalih%20Al-Fawzaan%20%3A%20Kumfanyia%20%E2%80%98Umrah%20Kaka%20Aliyefariki
[8] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F9237&title=05-Imaam%20Ibn%20%E2%80%98Uthaymiyn%3A%20Kurudia%20Kufanya%20Umrah%20Baada%20Ya%20Muda%20Mfupi%20Kutoka%20Makkah