Amali Za Kutenda Na Mambo Ya Kujiepusha Nayo Katika Miezi Mitukufu

'Amali Za Kutenda Na Mambo Ya Kujiepusha Nayo Katika Miezi Mitukufu

 

Alhidaaya.com

 

 

AlhamduliLLaah. Inapasa tumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Kutuendeleza uhai katika mwezi mwengine mtukufu.  Ni fursa nyingine ya kutenda mema tuchume thawabu nyingi. Mema ambayo hatuna budi kuyatenda kwa ajili ya kujenga Aakhirah yetu kabla haijafika siku ya kuaga kwetu dunia.

 

Utukufu wa miezi hiyo mitukufu imetajwa katika Qur-aan na Sunnah: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللَّـهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّـهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ ۚ فَلَا تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ ۚ وَقَاتِلُوا الْمُشْرِكِينَ كَافَّةً كَمَا يُقَاتِلُونَكُمْ كَافَّةً ۚ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ﴿٣٦﴾

Hakika idadi ya miezi mbele ya Allaah ni kumi na mbili katika hukmu ya makadirio ya Allaah, (tangu) siku Aliyoumba mbingu na ardhi. Kati ya hiyo, (iko miezi) minne mitukufu. Hivyo ndiyo Dini iliyo nyoofu. Basi msijidhulumu humo nafsi zenu (kwa kufanya maasi), na piganeni vita na washirikina wote kama wao wanavyokupigeni vita nyote. Na jueni kwamba Allaah Yu Pamoja na wenye taqwa. [At-Tawbah: 36]

 

Na miezi hiyo minne mitukufu imetajwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

عن أبي بَكْرَةَ رضي الله عنه عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أنه قَالَ:  ((إن الزَّمَانَ قَدْ اسْتَدَارَ كَهَيْئَتِهِ يَوْمَ خَلَقَ اللَّهُ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضَ السَّنَةُ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ثَلاثٌ مُتَوَالِيَاتٌ ذُو الْقَعْدَةِ وَذُو الْحِجَّةِ وَالْمُحَرَّمُ وَرَجَبُ مُضَرَ الَّذِي بَيْنَ جُمَادَى وَشَعْبَانَ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Bakr (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika mgawano wa zama umerudi katika hali yake ya asili siku Allaah Alipoumba mbingu na ardhi. Mwaka una miezi kumi na mbili; minne miongoni ya hiyo ni mitukufu, mitatu inafuatana pamoja; Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na Muharram, mwengine ni Rajab wa (kabila la) Mudhwarr ambao uko baina ya Jumaadaa na Sha'baan))  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Imaam Atw-Twabariy amesema: “Katika miezi yote kumi na mbili Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameichagua hii minne na Ameifanya kuwa ni mitukufu na kusisitiza kuitakasa, na kwamba dhambi zitakazofanyika humo ni zaidi na hali kadhalika thawabu za ‘amali njema zinakuwa maradufu na zaidi. [Atw-Twabariy 14: 238]

 

Qataadah amesema kuhusu kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

فَلَا تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ ۚ

Basi msijidhulumu humo nafsi zenu humo.

 

"Dhulma itakayotendeka katika miezi mitukufu ni mbaya na kubwa (au khatari) kuliko dhulma itakayotendeka katika miezi mingine. Hakika dhulma daima ni dhambi lakini Allaah Hufanya baadhi ya vitu kuwa ni vizito kuliko vingine vile Apendavyo. Akachagua baadhi ya viumbe Vyake na baadhi ya vitu kuwa bora zaidi kuliko vingine. Amechagua Wajumbe kutoka Malaika na kutoka wana Aadam.

Vile vile Amechagua baadhi ya kauli Zake kuwa ni bora kuliko nyingine, Misikiti kuwa bora kuliko sehemu nyingine za ardhi, Ramadhwaan na miezi mitukufu kuwa bora kuliko miezi mingine, siku ya Ijumaa kuwa ni bora kuliko siku nyingine, na usiku wa Laylatul-Qadr kuwa ni bora kuliko masiku mengine. Kwa hiyo itakase vile Alivyovitakasa Allaah, kwani kufanya hivyo ni vitendo vya watu wenye akili na wenye kufahamu" [Tafsiyr ya Ibn Kathiyr]   

 

Miongoni mwa yaliyokatazwa katika miezi mitukufu ni kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

  يَسْأَلُونَكَ عَنِ الشَّهْرِ الْحَرَامِ قِتَالٍ فِيهِ ۖ قُلْ قِتَالٌ فِيهِ كَبِيرٌ ۖ وَصَدٌّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَكُفْرٌ بِهِ وَالْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَإِخْرَاجُ أَهْلِهِ مِنْهُ أَكْبَرُ عِندَ اللَّـهِ ۚ وَالْفِتْنَةُ أَكْبَرُ مِنَ الْقَتْلِ ۗ وَلَا يَزَالُونَ يُقَاتِلُونَكُمْ حَتَّىٰ يَرُدُّوكُمْ عَن دِينِكُمْ إِنِ اسْتَطَاعُوا ۚ وَمَن يَرْتَدِدْ مِنكُمْ عَن دِينِهِ فَيَمُتْ وَهُوَ كَافِرٌ فَأُولَـٰئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۖ وَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢١٧﴾

217. Wanakuuliza kuhusu mwezi mtukufu kupigana humo. Sema: “Kupigana humo ni dhambi kubwa, lakini kuzuia (watu kufuata) njia ya Allaah na kumkufuru Yeye na (kuzuia wasiende) Al-Masjidil-Haraam na kuwatoa watu wake humo ni (dhambi) kubwa zaidi mbele ya Allaah. Na fitnah ni mbaya zaidi kuliko kuua.” Na wala hawatoacha kukupigeni vita mpaka wakutoeni katika Dini yenu wakiweza. Na atakayeritadi miongoni mwenu kutoka Dini yake, akafariki hali ya kuwa ni kafiri, basi hao zimeporomoka ‘amali zao katika dunia na Aakhirah. Na hao ni watu wa motoni, wao humo ni wenye kudumu [Al-Baqarah:  217]

 

 

Miongoni Mwa Ambayo Tunatakiwa Kujiepusha Nayo: 

  • Kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama kufanya uchawi, kuwaendea waganga, watabiri, kutufu makaburini, na mengineyo ya shirki.
  • Kuzini.
  • Kulewa.
  • Kuiba na kumdhulumu mtu haki yake.
  • Kugombana, kutukanana, kuvunjiana heshima, kudharauliana n.k.
  • Kusengenya (Ghiybah).
  • Kusema uongo, umbea, kufitinisha, na kila aina ya uovu mwengine.

 

Miongoni Mwa Ambayo Tunatakiwa Kuzidisha Kutenda: 

  • Swalaah za Sunnah (tazama maelezo chini).
  • Kufunga Swawm Jumatatu na Alkhamiys, Masiku meupe (Ayyaamul-Biydhw) (tarehe 13, 14 na 15 za Kiislamu) na Swawm ya Nabiy Daawuwd (kufunga kila baada ya siku moja).
  • Kutafuta ‘ilmu ya Dini kwa kusoma na kusikiliza mawaidha.
  • Kuomba maghfirah na kutubia (tawbah).
  • Kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa wingi kwa tasbiyh (Subhaana Allaah), tahmiyd (AlhamduliLLaah), tahliyl (laa ilaaha illa Allaah), takbiyr (Allaahu Akbar). Pia kusoma Qur-aan, kumshukuru na kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
  • Kuunga undugu, kwa kuwasiliana na ndugu, jamaa na kila anayemuhusu mtu kwa damu.
  • Kuwafanyia ihsaan wazazi wawili.
  • Kuwafanyia ihsaan majirani, marafiki na Waislamu kwa ujumla.
  • Kutoa Swadaqah.
  • Kulisha maskini.
  • Kusuluhisha waliokhasimiana.
  • Kuamrishana mema na kukatazana maovu.

‘Amali njema yoyote ile usiache kuitekeleza ee ndugu Muislamu hata iwe ndogo vipi kwa sababu hujui ‘amali ipi itakayokupatia radhi za Allaah (‘Azza wa Jalla) ikawa sababu ya kuingia kwako Jannah. Kumbuka Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

عَنْ أَبِي ذَرٍّ، قَالَ: قَالَ لِيَ النَّبِيُّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((لَا تَحْقِرَنَّ مِنَ الْمَعْرُوفِ شَيْئًا، وَلَوْ أَنْ تَلْقَى أَخَاكَ بِوَجْهٍ طَلْقٍ))

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Dharr (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Usidharau kufanya jambo jema lolote lile hata ikiwa kukutana na nduguyo kwa uso wa bashasha)) [Muslim]

 

 

Swalaah Za Sunnah Muakkadah (Zilizosisitizwa) Na Ghayr Muakkadah (Zisizosisitizwa)

 

Fadhila za Swalaah za Sunnah kwa ujumla ni nyingi, mojawapo ni Hadiyth:

 

عَنْ عبادةَ بنِ الصَّامِتِ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ أَنَّهُ سَمِعَ النَبيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((مَا مِنْ عَبْدٍ يَسْجُدُ للهِ سَجْدَةً إِلاَّ كَتَبَ اللهُ لَهُ بِهَا حَسَنَةً . وَمَحَا عَنْهُ بِهَا سَيِّئَةً ، وَرَفَعَ لَهُ بِهَا دَرَجَةً ، فَاسْتَكْثِرُوا مِنَ السُّجُودِ))

Imepokelewa kutoka ‘Ubaadah bin Swaamit (Radhwiya Allaahu 'anhu) ((Mja yeyote atakayesujudu sijda moja ataandikiwa hasanah (jema) mmoja, na atafutiwa baya moja, na atapandishwa daraja yake, kwa hiyo zidisheni kusujudu)) [Ibn Maajah]  

 

Fadhila za kuswali Swalaah za Sunnah Muakkadah (zilizosisitzwa) kabla ya Swalaah au baada ya Swalaah, jumla yake ni rakaa 12 kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:

 

(( مَا مِنْ عبْدٍ مُسْلِم يُصَلِّي للَّهِ تَعَالى كُلَّ يَوْمٍ ثِنْتَيْ عشْرةَ رَكْعَةً تَطوعاً غَيْرَ الفرِيضَةِ ، إِلاَّ بَنَى اللَّه لهُ بَيْتاً في الجَنَّةِ ، أَوْ : إِلاَّ بُنِي لَهُ  بيتٌ في الجنَّةِ  )) رواه مسلم  

((Hatoswali mja Rakaa 12 zisizo za fardhi kwa siku, ila atajengewa [na Allaah] nyumba Jannah)) [Muslim]

 

 

Alfajiri:

 

1-Muakkadah: Rakaa 2 kabla ya Swalaah

 

Suwrah za kusomwa: Suwratul-Kaafiruwn na Suwratul-ikhlaasw

 

Au Al-Baqarah 2:136 na Aal-‘Imraan 3:64 au Aal-‘Imraan 3:52.

 

Fadhila zake:

((ركْعتا الفجْرِ خيْرٌ مِنَ الدُّنيا ومَا فِيها )) رواه مسلم

((Rakaa mbili (za Sunnah) kabla ya Alfajiri ni khayr kuliko dunia na yaliyomo ndani yake) [Muslim]

 

Bonyeza kiungo kifuatacho upate faida zaidi:

 

Swalah Ya Sunnah Ya Alfajiri Inaswaliwa Vipi Na Wakati Gani? Na Surah Zipi Zisomwe?

  

 

Adhuhuri:

 

2-Muakkadah:  Rakaa 4 kabla ya Swalaah na  rakaa 2 baada ya Swalaah.

Ghayr Muakkadah:  Rakaa 2 baada ya Swalaah

 

 

Magharibi:

 

3-Muakkadah: Rakaa 2 baada ya Swalaah unasoma Suwratul-Kaafiruwn na Suwratul-Ikhlaasw.

 

Bonyeza kiungo upate faida zaidi:

 

Surah Gani Zisomwe Swalah Ya Alfajiri Na Magharibi? Inafaa Kusoma Surah Kubwa Na Ndogo?

 

Ghayr Muakkadah: Rakaa 2 kabla ya Swalaah.

 

 

‘Ishaa: 

 

4-Muakkadah:  Rakaa 2 baada ya Swalaah.

 

Ghayr Muakkadah: Rakaa 2 kabla ya Swalaah.

 

 

Swalaah Nyinginezo Zilizosisitizwa:

 

5-Swalaah ya Tahajjud:

 

Ni Swalaah bora kabisa baada ya Swalaah za fardhi kwa dalili:

 

(( أَفْضَلُ الصَّلاةِ بَعْدَ الْفَرِيضَةِ صَلاةُ اللَّيْلِ))  رواه مسلم

((Swalah iliyo bora kabisa baada ya Fardh ni Swalah ya usiku))  [Muslim]

 

Bonyeza viungo upate faida zake:

 

Wakati Wa Swalah Ya Tahajjud Na Vipi Kuswali

 

Nini Fadhila Za Swalah Ya Tahajjud?

 

 

6-Swalaah Ya Dhwuhaa:

 

Ni Swalaah inayoanza kuswaliwa baada ya kuchomoza jua vizuri mpaka karibu na Adhuhuri kabla ya kuingia kwake.

 

Idadi ya Rakaa zake kuanzia 2 hadi 8

 

Fadhila zake:

 

عـَن أبي ذَرٍّ رضي الله ُ عنه ، عن النـَبي ِّ صلـَّى الله عليه وسلم قال: ((يـُصـْبـِحُ عـَلى كـُلِّ سـُلامى مـِنْ أحـَدِكـُمْ صـَدَقةُ: فـَكُل تـَسْبـِيحـَةِ صـَدَقةٌ ،وَ كُل تـَحمِيدة صـَدَقةٌ ، وكُلُ تـَهْـليْلةٌ صـَدَقـَةٌ، وكُلُّ تـَكْبِيْرةِ صـَدقةٌ ، وأمرٌ بالمـَعرُوف صـَدقةٌ ، ونـَهىٌ عـَنِ المـُنْكرِ صـَدقةٌ ويـُجْزئ مـِنْ ذلكَ رَكـْعتـَانِ يـَركَعُهُما مـنَ الضـُّحى)) رواه مسلم

Kutoka kwa Abuu Dharr (Radhiya Allahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) amesema: ((Kila kiungo katika mwili wenu hupambaukiwa kikihitaji kutolewa sadaka, kwa hiyo kila tasbiyh (kusema ‘SubhaanaAllah’) ni sadaka na kila tahmiyd (kusema ‘AlhamduliLlaah’) ni sadaka na kila tahliyl (kusema ‘La Ilaaha Illa Allah’) ni sadaka  na kila takbiyr (kusema ‘Allahu Akbar’) ni sadaka na kuamrisha mema ni sadaka na kukataza maovu ni sadaka na itamtosheleza (Mtu) kwa Rakaa mbili za Dhuhaa)) [Muslim]

 

Na pia bonyeza kiungo upate faida zaidi:

 

Swalah Ya Dhwuhaa - Rakaa Zake, Fadhila Zake na Wakati Wake

 

 

7- Swalah Ya Witr:

 

Ni Swalaah inayoswaliwa kuanza baada ya Swalaah ya ‘Ishaa mpaka kabla ya Swalaah ya Alfajiri.

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه قَالَ: أَوْصَانِي خَلِيلِي صلى الله عليه وسلم بِثَلاثٍ: صِيَامِ ثَلاثَةِ أَيَّامٍ مِنْ كُلِّ شَهْرٍ، وَرَكْعَتَيْ الضُّحَى، وَأَنْ أُوتِرَ قَبْلَ أَنْ أَنَامَ.

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba “Ameniusia rafiki yangu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mambo  matatu; kufunga swawm siku tatu katika kila mwezi, rakaa mbili za dhwuhaa, na niswali Witr kabla ya kulala.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Bonyeza viungo kwa faida ziada:

 

Swalah Ya Witr Inaswaliwa Vipi Na Vipi Kutia Nia?

 

Surah Gani Kusoma Katika Swalah Ya Tahajjud Na Witr?

 

 

Share