أحاديث عَنْ رَمَضان وَصِيام وعبرة
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Pamoja Mafunzo Yake
Zimekusanywa Na: Abuu Baasim
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
01-Ikhlaasw Katika Swawm
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: (( مَنْ صَامَ رَمَضَانَ إِيمَانًا وَاحْتِسَابًا غُفِرَ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ))
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) akisema: Amesema Rasuli wa Allaah Swalla Allaahu Alayhi wa Sallam: ((Mwenye kufunga Ramadhwaan kwa iymaan na kutaraji malipo, hughufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Imesimuliwa na Al Bukhaariy 38 na Muslim]
Hadiyth hii ni dalili wazi juu ya fadhila ya mwezi mtukufu wa Ramadhwaan. Mwezi huu ni sababu ya Muislamu kughufuriwa madhambi yake na kufutiwa makosa yake. Lakini hilo halifanyiki isipokuwa kwa masharti matatu kama Hadiyth inavyoeleza:
La kwanza: Ni kuwa na iymaan kamili kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Aliyeifaradhisha Swawm na Yeye Ndiye Atakayewalipa wafungaji malipo makubwa kwa kutii amri Yake.
La pili: Kufunga kwa ajili ya kumtakasia niyyah Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Peke Yake. Swawm anayofunga mtu kwa ajili ya riyaa tu, au kufuata desturi au mkumbo tu, basi haina malipo.
La tatu: Mwenye swawm kujiepusha na madhambi makubwa. Madhambi haya ni yale yote yaliyowekewa adhabu hapa duniani, au kutolewa laana, au makamio makali na adhabu za Aakhirah kama shirki, kula ribaa, kula mali ya yatima, kuzini, kufanya uchawi, kuwaasi wazazi wawili, madhambi saba yanayoangamiza na kadhalika. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatuambia:
إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا ﴿٣١﴾
Mkijiepusha na madhambi makubwa mnayokatazwa Tutakufutieni madhambi yenu madogo na Tutakuingizeni katika mahali patukufu. [An-Nisaa (4:31)]
Hivyo mja akifunga Swawm yake ya Ramadhwaan kama inavyotakikana, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atamghufuria madhambi yake madogo na makosa aliyoyafanya kama atajilinda na madhambi hayo makubwa.
Hivyo basi, Muislamu anatakikana katika mwezi huu aharakie kufanya tawbah kwa madhambi yake yote makubwa na madogo ili awe na uhakika zaidi wa kupata maghfirah.
Na yeyote atakayechafua maisha yake kwa maasia na madhambi, basi amejipotezea mwenyewe nafasi ya kujitakasa na kusamehewa. Huyo hastahiki kupata maghfirah yaliyoahidiwa, bali huenda yakampata maapizo ya du’aa ya Jibriyl ('Alayhis-Salaam) iliyoitikiwa “aamiyn” na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama anavyoeleza Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipanda mimbari akasema: “Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn”. Mtu mmoja akamwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Umepanda mimbari ukasema: “Aamiyn, Aamiyn, Aamiyn”. Akasema: ((Hakika Jibriyl ('Alayhis-Salaam) alinijia akaniambia: Aliyeupata mwezi wa Ramadhwaan, naye asighufiriwe, na akaingia motoni, basi Allaah Amtupilie mbali, akasema: Aamiyn, nami nikasema Aamiyn)) [‘Allaamah Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh]
Muislamu mwenye swawm anatakikana awe na shime ya kuzitafuta nyenzo zote za kupatia maghfirah na Radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kuilinda Swaum yake na kuwajibika ipasavyo na mawajibiko yote, na ajiweke mbali kabisa na visababishi vyote vya kumkosesha Radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
Kati ya nyenzo hizo kama alivyokuwa akifanya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ni kukithirisha aina mbalimbali za ‘ibaadah, kutoa swadaqah kwa wingi, kufanya ihsaan, kusoma Qur-aan, kufanya I’tikaf na kadhalika.
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
02-Milango Ya Jannah Hufunguliwa Milango Ya Moto Hufungwa
عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: (( إِذَا دَخَلَ رَمَضَانُ فُتِّحَتْ أَبْوَابُ الجَنَّةِ ، وَغُلِّقَتْ أَبْوَابُ جَهَنَّمَ ، وَسُلْسِلَتِ الشَّيَاطِينُ )
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ikiingia Ramadhwaan, milango ya Jannah hufunguliwa, milango ya Moto hufungwa, na mashaytwaan hutiwa minyonyoro)) [Al Bukhaariy (3277) na Muslim (1079)]
Mafunzo:
Hadiyth hii inatakikana ichukuliwe kwa ufahamu huu ulioelezewa kwa uhalisia wake kwamba milango ya Jannah hufunguliwa na kuachwa wazi, milango ya moto hufungwa, na mashaytwaan hutiwa minyonyoro wasiweze kufurukuta. Asili ni kuchukuliwa kwa mwonekano huu mpaka ije dalili ya kupindua maana kusudiwa.
Imaam Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahu Allaah) aliulizwa swali lisemalo: “Hadiyth hii ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inasema mashaytwaan hufungwa pingu na kutiwa minyororo katika mwezi huu lakini pamoja na hayo tunawaona watu wakipandwa na mashaytwaan na pia wakimwasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) mchana wa mwezi huu? Vipi mashaytwaan watiwe minyororo na baadhi ya watu waendelee kupandwa na mashaytwaan na kuasi?”
Sheikh alijibu akisema: “Yaliyotajwa katika Hadiyth hii ni mambo ya ghaibu. Wajibu wetu sisi ni kuyasadiki, kuyakubali na kutojaribu kuzungumzia yaliyo nyuma yake. Hivi kunakuwa ni salama zaidi kwa Dini ya mtu na salama zaidi kwa hatima yake”.
‘Ulamaa wengine wanasema kuwa jawabu la swali kama hilo linakuwa kama ifuatavyo:
Kwanza: Hufungwa kwa wafungaji swawm iliyo kidhi vigezo na masharti, si swawm tu mradi swawm. Mfungaji wa swawm kama hii hana kinga dhidi ya shaytwaan.
Pili: Kuna sababu nyinginezo nyingi za kufanyika maasia na shari. Si shaytwaan tu ndiye chanzo cha shari zote bali nafsi khabithi, desturi mbaya na mashaytwaan wa kibinaadamu ni sababu pia za maasia.
Tatu: Wanaofungiwa ni mashaytwaan sugu wabaya. Ama mashaytwaan wa kawaida wasio na athari kubwa kwa watu, hao hawafungwi. Na hii ndio sababu ya kupungua sana maasia katika mwezi wa Ramadhwaan kulinganisha na miezi mingineyo.
‘Ulamaa wengine wanasema kuwa kutiwa pingu mashaytwan kuna maanisha kushindwa kwao kuwarubuni wafungaji swawm na kuwazainia matamanio.
Wengine wanasema kuwa shaytwaan aliyefungwa anaweza pia kusababisha adha, lakini adha yake si kama ya yule aliye huru.
Ama hikma ya kufunguliwa milango ya Jannah na kufungwa milango ya moto, ‘Ulamaa wanasema ni kuwa katika mwezi huu wa Ramadhwaan, nyoyo za Waumini huchangamkia kheri na matendo mema yanayokuwa sababu ya kufunguliwa milango hiyo, na hujizuia na maasia na madhambi ambako kunakuwa ni sababu ya kufungwa milango ya moto. Na hii ni ishara kubwa juu ya utukufu na fadhila za mwezi huu wa Ramadhwaan.
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
03-Umahasusi Wa Swawm Kwa Allaah ‘Azza wa Jalla
عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((قال الله عزوجل: كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ لَهُ إِلَّا الصِّيَامَ فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ))
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah ‘Azza wa Jalla Kasema: Kila ‘amali ya mwana Aadam inamhusu Yeye isipokuwa Swiyaam kwani hakika hiyo inanihusu Mimi, Nami Ndiye Ninayeilipia)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Mafunzo:
Hadiyth hii adhimu imethibiti toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), inaonyesha fadhila na hadhi kubwa ya ‘amali ya Swawm kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kulinganisha na ‘amali nyinginezo za mja pale Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alipotujulisha kwamba ‘amali hii Ameinasibishia Kwake Pekee kimalipo.
‘Ulamaa wamejaribu kufafanua maana ya Neno Lake:
إِلَّا الصِّيَامَ فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ
((Isipokuwa Swiyaam kwani hakika hiyo inanihusu Mimi, Nami Ndiye Ninayeilipia))
Wakisema: “’Amali zote anazozifanya mja hapa duniani, basi thawabu za ‘amali zake zitatumika Siku ya Qiyaamah kulipiwa makosa na haki za watu alizodhulumu hapa duniani. Aliowadhulumu watalipwa mema yake yatokanayo na ‘amali zake njema zitokanazo na Swalaah, Zakaah, swadaqah, na kadhalika kama anavyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((أَتَدْرُونَ مَا الْمُفْلِسُ؟)) قَالُوا: الْمُفْلِسُ فِينَا مَنْ لاَ دِرْهَمَ لَهُ وَلاَ مَتَاعَ . فَقَالَ: ((إِنَّ الْمُفْلِسَ مِنْ أُمَّتِي يَأْتِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ بِصَلاَةٍ وَصِيَامٍ وَزَكَاةٍ وَيَأْتِي قَدْ شَتَمَ هَذَا وَقَذَفَ هَذَا وَأَكَلَ مَالَ هَذَا وَسَفَكَ دَمَ هَذَا وَضَرَبَ هَذَا فَيُعْطَى هَذَا مِنْ حَسَنَاتِهِ وَهَذَا مِنْ حَسَنَاتِهِ فَإِنْ فَنِيَتْ حَسَنَاتُهُ قَبْلَ أَنْ يُقْضَى مَا عَلَيْهِ أُخِذَ مِنْ خَطَايَاهُمْ فَطُرِحَتْ عَلَيْهِ ثُمَّ طُرِحَ فِي النَّارِ)) مسلم
((Je, Mnamjua muflis?)) Wakasema [watu]: “Muflis kwetu sisi ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na dirhamu [pesa] wala vyenye kumnufaisha yeye hapa duniani”. Akasema (صلى الله عليه وآله وسلم): ((Hakika muflis katika Ummah wangu ni yule atakayekuja Siku ya Qiyaamah na Swalaah, Swiyaam, na Zakaah, lakini amemtusi huyu, kumsingizia huyu mwingine kuwa amezini, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya mwingine na kumpiga mwengine. Thawabu zake zitapatiwa huyu na yule mpaka zimalizike. Na zinapokwisha basi madhambi ya hao [aliowadhulumu] atabandikwa nayo, hivyo kuingizwa Motoni))]. [Muslim]
Lakini Swawm yake haitoguswa kabisa, bali Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atamhifadhia na kumbakishia.
Maneno haya yanathibitishwa na Hadiyth nyingine isemayo:
(( كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ لَهُ كَفَّارَة إِلَّا الصّوْم فَإِنَّهُ لِي وَأَنَا أَجْزِي بِهِ))
((Kila ‘amali ya mwana Aadam ina kafara isipokuwa Swawm, kwani hakika Swawm kwani hakika hiyo inanihusu Mimi, Nami Ndiye Ninayeilipia)) [Musnad Ahmad]
Wengine wakasema:
“Maana yake ni kuwa Swawm ni ‘amali ya kindani isiyoonekana, na kwa hivyo hakuna ajuaye undani wake isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Peke Yake. Ni niyyah ya kimoyo kinyume na ‘amali nyinginezo zinazoonekana na watu. Lakini Swawm, ni ‘amali ya siri kati ya mja na Mola wake. Na kwa ajili hiyo, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
((انه ترك شهوته وطعامه وشرابه من اجلي))
((Ameacha matamanio yake, chakula chake na kinywaji chake kwa ajili Yangu)).
Swadaqah, Swalaah, Zakaah, Hijjah ni ‘amali za kuonekana, lakini Swawm hakuna aionaye”.
‘Ulamaa wengine wanasema: “Swawm haiingiliwi na shirki kabisa kinyume na ‘amali nyinginezo. Wapagani na washirikina tunawaona wakitoa kafara kwa viabudiwa vyao kama wanyama na kadhalika. Wanasujudia masanamu yao na kuyabusu. Lakini hakuna mshirikina yeyote au mpagani yeyote anayefunga Swawm kwa ajili ya masanamu hayo. Hivyo, Swawm inakuwa kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Peke Yake pasina mwengine. Na hii ndio maana ya Neno Lake:
(( الصوم لي وانا اجزبي به))
((Swawm ni kwa ajili Yangu, Nami Ndiye Ninayeilipia))
Hadiyth nyengineyo kuhusu fadhila za Swawm:
عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: قال رسول اللَّه صلى الله عليه وسلم: (( قالَ اللَّهُ: كُلُّ عَمَلِ ابْنِ آدَمَ لَهُ إِلاَّ الصِّيَامَ، فَإِنَّهُ لِي، وَأَنَا أَجْزِي بِهِ. وَالصِّيَامُ جُنَّةٌ، وَإِذَا كَانَ يَوْمُ صَوْمِ أَحَدِكُمْ، فَلاَ يَرْفُثْ وَلاَ يَصْخَبْ، فَإِنْ سَابَّهُ أَحَدٌ، أَوْ قَاتَلَهُ فَلْيَقُلْ إِنِّي امْرُؤٌ صَائِمٌ. وَالَّذِي نَفْسُ مُحَمَّدٍ بِيَدِهِ لَخُلُوفُ فَمِ الصَّائِمِ أَطْيَبُ عِنْدَ اللَّهِ مِنْ رِيحِ الْمِسْكِ، لِلصَّائِمِ فَرْحَتَانِ يَفْرَحُهُمَا إِذَا أَفْطَرَ فَرِحَ، وَإِذَا لَقِيَ رَبَّهُ فَرِحَ بِصَوْمِهِ )) رواه البخاري.
Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Allaah ‘Azza wa Jalla Amesema: “Kila ‘amali ya bin Aadam inamhusu yeye isipokuwa Swiyaam, kwani hakika hiyo inanihusu Mimi, Nami Ndiye Ninayeilipia. Na Swawm ni ngao, na itakapokuwa siku ya Swawm ya mmoja wenu, basi asitamke maneno yasiyolaiki, wala asifanye maasia, wala asipayuke ovyo. Ikiwa mtu atamvuta watukanane au wapigane, basi aseme: “Hakika mimi nimefunga”. Naapa kwa Ambaye Nafsi ya Muhammad iko Mkononi Mwake, hakika kutaghayari harufu ya kinywa cha mwenye Swawm kunanukia mbele ya Allaah kuliko harufu ya miski. Mwenye Swawm ana furaha mbili anazozifurahikia; anapofungua hufurahika kwa Swawm yake, na atakapokutana na Mola wake atafurahi kwa Swawm yake)) [Al-Bukhaariy]
Swawm ni nguzo ya nne kati ya nguzo za Uislamu. Mwislamu huupokea mwezi wa Ramadhwaan kwa kifua kilichofunguka, nafsi nzuri na moyo uliotulia kwa kuwa anajua fika kwamba huu ni mwezi wa kheri na barkah zisizopatikana katika mwezi mwingine.
Mwislamu kama huyu, utamwona anafanya hima ya juu ya kujichunga na kila lile ambalo linaweza kuivuruga Swawm yake, na anakuwa na shime ya kweli ya kufanya kila tendo jema ili apate jaza iliyoahidiwa na Allaah (‘Azza wa Jalla) isiyokuwa na mipaka maalumu.
Swawm hii ni ngao na kinga kwa Mwislamu wa kweli, kwani humzuia na mambo yote yatakayomghadhibisha Allaah (‘Azza wa Jalla) hapa dunaini, na Aakhirah itakuwa kinga dhidi ya moto.
Hadiyth hii tukufu imetupa mwongozo kamili juu ya namna ya kuitumia kinga hii:
Kwanza, mwenye Swawm anatakiwa auzuie ulimi wake usije kutamka mambo ya ovyo yasiyolaikiana na mwezi huu. Ni kama kutaja mambo ya ngono ambayo yanaweza kuchemsha matamanio ya mtu.
Pili, asifanye vitendo vyovyote vya maasia na ufasiki, kwani haviendani kabisa na uadhama wa mwezi huu.
Tatu, asinyanyue sauti yake kama inavyofanyika kwenye mazingira ya sokoni. Upazaji huu unamkosesha mtu haiba yake na hasa kama kinachopaziwa sauti ni kitu kisicho na maana.
Nne, ikiwa mtu atajaribu kumtukana au kumporomoshea maneno ya kumuudhi, basi asirudishe wala kujibu, bali ajiondokee zake taratibu bila kumjibisha wala kumjali. Madereva wengi sana huwa na tabia ya kutukana kwa kosa dogo la barabarani. Hawa inabidi kuwapuuza, na Mwislamu inabidi ajiweke mbali kabisa na tabia hii. Hali kadhalika, ikiwa yeyote atamkabili na kumkunja shati, basi apoe na kuondokana naye kwa amani na salama ila kama atashambuliwa, basi hapo itabidi kujitetea kwa mujibu wa hali.
Kisha Hadiyth inatugusia kuwa harufu mbaya ya kutaghayari kinywa cha mfungaji kutokana na kutokula, inanukia kuliko mafuta ya miski mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Na haya ni makarimio makubwa ya Allaah (‘Azza wa Jalla) kwa mwenye Swawm na nafasi kubwa aliyonayo mwenye Swawm mbele ya Mola wake kutokana na kuitii amri Yake na kutekeleza ili kuzipata Radhi Zake.
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
04-Swawm Ni Taqwa
عَنْ ابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : (( بُنِيَ الإِسْلامُ عَلَى خَمْسٍ شَهَادَةِ أَنْ لا إِلَهَ إِلا اللَّهُ وَأَنَّ مُحَمَّدًا رَسُولُ اللَّهِ وَإِقَامِ الصَّلاةِ وَإِيتَاءِ الزَّكَاةِ وَالْحَجِّ وَصَوْمِ رَمَضَانَ)) "
Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Uislamu umejengwa juu ya matano: Kushuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki illa Allaah na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, kusimamisha Swalaah, kutoa Zakaah, kuhiji na Swawm ya Ramadhwaan)) [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy (8) na Muslim (16)]
Mafunzo:
Hadiyth hii inatujulisha kuwa kufunga mwezi wa Ramadhwaan ni wajibu kwa kila Mwislamu asiye na udhuru, na kwamba Swawm ni moja kati ya nguzo tano za Uislamu ambayo Allaah (‘Azza wa Jalla) Ameifaradhisha kwa Waja Wake kwa hikma adhimu, na siri kubwa ambayo ameijua aliyeijua na amejingikiwa aliyejingikiwa.
Makusudio makuu ya Swawm ni kuizuia nafsi na matamanio, kuiweka mbali na mambo iliyoyazoea, na kuzidhibiti nguvu zake za kimatamanio ili Mwislamu aweze kulifikia lengo halisi la Swawm ambalo ni taqwa.
Allaah (‘Azza wa Jalla) Anatuambia:
أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٨٣﴾
Enyi walioamini! Mmefaridhishwa Swiyaam kama ilivyofaridhishwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa. [Al-Baqarah: 183]
Aayah hii inaelezea wazi sababu ya kufaradhishiwa sisi Swawm kama Waislamu wenzetu waliotutangulia katika umma zilizopita. Swawm inakuwa ni kama zoezi la kumwandaa Mwislamu kuwa na uwezo wa kujizuia na makatazo kwa kuacha matamanio yake halali ya kimaumbile kwa ajili tu ya kutekeleza agizo la Allaah (‘Azza wa Jalla) na kutarajia malipo Yake. Irada yake inaleleka kutokana na Swawm hii kuwa na uwezo wa kuacha matamanio na kujipamba kwa subra ambayo malipo yake yanakuwa hayana hisabu au mpaka maalum, na hakuna ajuaye malipo yake isipokuwa Allaah (‘Azza wa Jalla) Peke Yake.
Swawm ina athari ya ajabu katika kuvilinda na kuvihifadhi viungo vya nje na nguvu za ndani ya mwili. Mfungaji Swawm wa kweli, hujikuta moyo wake ukichukia kila lile lenye kumkasirisha Allaah (‘Azza wa Jalla) na kulipenda kila lile lenye kumfurahisha huku akitaraji malipo makubwa kabisa toka kwa Allaah (‘Azza wa Jalla) kutokana na subra anayoifanya ya kufuata amri Yake na kujizuia na matamanio yote ya mwili.
Imaam As-Sa’diy katika Tafsiyr yake amenukuu yafuatayo kuhusu maana ya taqwa katika Aayah ya Swawm. Akasema kuwa Swawm ni sababu kuu ya taqwa (kumcha Allaah) kwa kuwa ni kutekeleza amri za Allaah na kujiepusha na yaliyokatazwa.
Kwa hiyo katika Swawm yanapatikana:
1. Taqwa ya asw-swaaim (anayefunga swawm) huacha yote Aliyoyakataza Allaah; kula, kunywa, kujimai na kama hayo, na yote yanayoelemea nafsi yake kuyatamani; hapo basi hujikurubisha kwa Allaah kwayo akitaraji thawabu kwa kujiepusha nayo. Haya yote ni kutokana na taqwa.
2. Na Swawm pia inamfunza mtu kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) basi hujiepusha na hawaa ya nafsi yake, kwa (kutegemea) Uwezo Wake (Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kuwa anatambua kwamba Allaah Anamuona (ayatendayo yote).
3. Swawm pia inamzuia mtu na shaytwaan, kwani hakika shaytwaan anatembea katika mwili wa binaadam kamba damu inavyotembea katika mishipa. Kwa hiyo Swawm inamvunja nguvu shaytwaan (na uchochezi wake), hivyo madhambi hupunguka.
4. Swawm pia aghalbu humfanya mtu azidishe utiifu na utiifu ni katika sifa za taqwa.
5. Swawm pia inamfanya tajiri anaposhikwa na njaa inayombidi imshike (kwa kuwa ni fardhi kwake, huwafikiria na) huwahurumia masikini na mafuqara na hii ni miongoni mwa sifa za taqwa.
Hali kadhaalika taqwa ni kuacha kila aina ya maovu na khasa kuzuia ulimi kutokunena maovu kama kusema uongo, uzushi, kushuhudia uongo, ghiybah (kusengenya), namiymah (kufitinisha au kuchongesha baina ya watu), kutukana, kumfanyia mtu kejeli na kadhaalika kwa kuwa maovu katika Swawm humaharibia mtu Swawm yake kwa dalili zifuatazo:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: (( مَنْ لَمْ يَدَعْ قَوْلَ الزُّورِ وَالْعَمَلَ بِهِ فَلَيْسَ لِلَّهِ حَاجَةٌ فِي أَنْ يَدَعَ طَعَامَهُ وَشَرَابَهُ))
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Asiyeacha kusema uongo (kutoa ushahidi wa uongo, na maasi yote ya ulimi) na vitendo vibaya basi ajue kuwa Allaah hana haja na Swawm yake katika kuacha chakula chake na kinywaji chake)) [Al-Bukhaariy]
Kwa maana: Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hataikubali Swawm yake.
Bila shaka Swawm ina faida nyinginezo mbali ya hilo la kufikia kilele cha taqwa. Hadiyth kadhaa zimetufahamisha kuwa mwenye kutekeleza ya wajibu na ya faradhi, na akaacha maharamisho, basi huyo ni katika watu watakaofuzu na kuingia Peponi:
عَنْ طَلْحَةَ بْنَ عُبَيْدِ اللَّهِ، يَقُولُ جَاءَ رَجُلٌ إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَإِذَا هُوَ يَسْأَلُهُ عَنِ الإِسْلاَمِ، فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((خَمْسُ صَلَوَاتٍ فِي الْيَوْمِ وَاللَّيْلَةِ)) فَقَالَ: هَلْ عَلَىَّ غَيْرُهَا؟ قَالَ: ((لاَ، إِلاَّ أَنْ تَطَّوَّعَ)) فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((وَصِيَامُ رَمَضَانَ)) قَالَ: هَلْ عَلَىَّ غَيْرُهُ ؟ قَالَ: ((لاَ، إِلاَّ أَنْ تَطَّوَّعَ)) قَالَ: وَذَكَرَ لَهُ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم الزَّكَاةَ. قَالَ: هَلْ عَلَىَّ غَيْرُهَا؟ قَالَ: ((لاَ، إِلاَّ أَنْ تَطَّوَّعَ)) فَأَدْبَرَ الرَّجُلُ وَهْوَ يَقُولُ: "وَاللَّهِ لاَ أَزِيدُ عَلَى هَذَا وَلاَ أَنْقُصُ". قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((أَفْلَحَ إِنْ صَدَقَ))
Imepokelewa kutoka kwa Twalhah bin ‘Ubaydillaah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba: Mtu mmoja alimwendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuanza kumuuliza kuhusu Uislamu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Swalaah tano usiku na mchana)). Akauliza: “Je, liko jingine zaidi ya hilo linalonipasa?” Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema ((Hakuna, ila kama utafanya lililosuniwa)). Halafu Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamkamilishia na kumwambia: ((Na Swawm ya Ramadhwaan)). Akauliza: “Je, liko jingine zaidi ya hilo linalonipasa?” Akasema: ((Hakuna, ila kama utafanya lililosuniwa)). Akasema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamtajia kuhusu Zakkaah. Akauliza: “Je, liko jingine zaidi ya hilo linalonipasa?” Akasema: ((Hakuna, ila kama utafanya lililosuniwa)) Hapo yule mtu akaondoka zake huku akisema: “Wa-Allaahi sitozidisha juu hayo wala sitoyapunguza.” Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Ikiwa kasema ukweli basi atafuzu)) [Al-Bukhaariy]
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
05-Swawm Ni Ngao
عن عثمان بن عفان رضي الله عنه، قال: سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول: الصِّيامُ جُنَّةٌ من النَّارِ ، كَجُنَّةِ أحدِكمْ من القِتالِ))
Imepokelewa toka kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) akisema: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Swiyaam ni ngao dhidi ya moto, kama ngao ya mmoja wenu katika mapigano)) [Ibn Maajah, amiesahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Ibn Maajah (1336), Swahiyh Al-Jaami’ (3879)]
Mafunzo:
Bila shaka makusudio makuu ya wenye akili ni kufuzu kwa kuingia Jannah (Peponi) na kuepushwa na moto wa Jahannam. Allaah (‘Azza wa Jalla) Anatuambia:
فَمَنْ زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ
Basi atakayewekwa mbali na moto na akaingizwa Jannah kwa yakini amefuzu. [Aal-‘Imraan: 185]
Na Anatuambia tena:
قُلْ إِنَّ الْخَاسِرِينَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَأَهْلِيهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ أَلَا ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ ﴿١٥﴾
Sema: “Hakika waliokhasirika ni wale waliokhasiri nafsi zao na ahli zao Siku ya Qiyaamah. Tanabahi! Hiyo ndio khasara bayana.” [Az-Zumar: 15]
Hakuna mafanikio makubwa zaidi kuliko mtu kuingia Jannah (Peponi), na hakuna khasara kubwa zaidi kama mtu kuishilia motoni. Na haya ndiyo wanayoyaendea mbio watu wenye akili; kulipapia kila lile litakalowafikisha Jannah, na kujiepusha kwa nguvu zao zote na kila lile linalopelekea motoni.
Na swawm ni ‘ibaadah ambayo Allaah (‘Azza wa Jalla) Ameifanya kuwa ni kinga na ngao kwa mwenye Swawm. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia katika Hadiyth:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رضي الله عنه قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ صَامَ يَوْماً فِي سَبِيلِ اللَّهِ بَعَّدَ اللَّهُ وَجْهَهُ عَنْ النَّارِ سَبْعِينَ خَرِيفًا )) مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayefunga Swawm siku moja kwa ajili ya Allaah, Allaah Atamweka mbali uso wake na moto masafa ya miaka sabini)) [Muslim 2/208]
Na hii ni siku moja tu. Vipi ikiwa Mwislamu atafunga siku 100 kwa mfano wa siku kama hiyo katika maisha yake?! Mwislamu anaweza kuisikia Hadiyth kama hii lakini asiitie akilini au kuipa uzito. Lakini Mwislamu mwerevu na mjanja, kwa vile amejua kwamba akifunga siku kama hiyo atabaidishwa mbali na moto kwa urefu huo, basi mara moja huichangamkia na kuifunga siku kama hiyo hata angalau mara moja katika umri wake wote.
Na siku ya Qiyaamah, Waislamu wengi watajuta na kuhuzunika kutokana na kuiachilia nafasi kama hii na zinginezo ambazo zilikuwa ni kochokocho hapa duniani wakati watakapoona malipo makubwa yakitolewa kwa Waislamu wenzao werevu walioitumia kila nafasi ya kujichumia mambo ya kheri.
Hivyo basi ndugu yangu Mwislamu, wakati bado tunao wa kuweza kujichumia mengi ya kutufaa huko Aakhirah kuliko kupoteza umri wetu katika mambo yasiyo na faida.
Ngao hii ya swawm dhidi ya moto kwa mfungaji, ni lazima iwe ni ngao ya kumzuia mfungaji huyo na maasia hapa duniani, ili iweze kuwa ni ngao kwake dhidi ya moto Siku ya Qiyaamah. Ikiwa haitomkinga na maasia hapa duniani, basi haiwezi kumkinga na moto siku hiyo. Ni lazima imkinge hapa duniani na maneno machafu, matusi, masengenyo na matendo yote mabaya.
Baadhi ya watangu wema wamesema: “Masengenyo huitoboa Swawm, na istighfaar huikarabati, na mwenye kuweza miongoni mwenu asije na Swawm yenye kuvuja, basi afanye.”
Hakika mwenye Swawm amefungamanishwa na malipo na fadhla kutoka kwa Mola wake (‘Azza wa Jalla). Hivyo basi, awe na pupa ya kuzipata thawabu hizi kwa kutimiza masharti yake na kujiepusha na vizuizi vyake ili apate mradi tarajiwa wa kuepushwa na moto wa Jahannam.
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
06-Malipo Ya Swawm Siku Moja Kwa Ajili Ya Allaah
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رضي الله عنه قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: مَنْ صَامَ يَوْماً فِي سَبِيلِ اللَّهِ بَعَّدَ اللَّهُ وَجْهَهُ عَنْ النَّارِ سَبْعِينَ خَرِيفًا .
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayefunga (Swawm) siku moja kwa ajili ya Allaah, Allaah Ataubaidisha uso wake na moto masafa ya miaka sabini)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Mafunzo:
‘Ulamaa wametofautiana kuhusiana na maana ya “Fiy SabiyliLLaah.”
Kauli ya kwanza inasema kuwa kinachofahamika kwa hisia ya kwanza katika Hadiyth hii tukufu, ni kuwa kinachokusudiwa hapa ni kufunga Swawm wakati wa vita ambapo mfungaji anakusanya ‘ibaadah ya Swawm, ‘ibaadah ya jihaad katika Njia ya Allaah, na ‘ibaadah ya kufanya subra wakati anapokuwa amekabiliana na mazito na mashaka na hususan katika taharuki ya vita ambapo mtu huhofia nafsi yake kuuawa au kujeruhiwa, na huhofia watoto wake na nduguze Waislamu kiujumla.
Kauli ya pili, ni kwamba makusudio ya “Fiy SabiyliLlaah” ni Dini ya Allaah ('Azza wa Jalla) na Shariy’ah Yake. Hivyo itakuwa na maana ya mwenye kufunga kwa ajili ya Radhi za Allaah ('Azza wa Jalla) tu, na kuzitafuta thawabu Zake, na si vinginevyo. Kwa maana hii, anatoka nje ya wigo hapa mwenye kufunga kwa ajili ya riyaa na umashuhuri, au kutaka kusifiwa kutokana na Swawm yake au kwa lengo jingine lolote la maslaha yake binafsi.
Hivyo basi, kwa mujibu wa kauli hii, yeyote mwenye kufunga kwa ajili ya Allaah ('Azza wa Jalla) tu akiwa mjini kwake, au akiwa safarini, basi huyo anaingia katika wigo wa “Fiy SabiyliLLaah” na hivyo kustahiki malipo haya makubwa ya kuwekwa mbali na moto wa Jahannam umbali wa miaka 70. Hii ni kwa vile SabiyliLLaah inajumuisha kila tendo analolifanya Mwislamu kwa ajili ya kuitumikia Dini yake, na kuwatumikia Waislamu kwa ajili ya kuiweka juu Dini ya Allaah ('Azza wa Jalla).
Kujenga madrasa kwa ajili ya kuhifadhisha watoto Qur-aan na kuwafundisha ilmu ya Dini, kuwalipia ada na karo za shule, kuwanunulia wagonjwa madawa na kuwalipia matibabu, hayo yote yanaingia ndani ya wigo wa Fiy SabiyliLlaah.
Ama kuwekwa mbali na moto huo kama wanavyosema ‘Ulamaa, ni kwamba mfungaji huyu atabaidishwa umbali wa mwendo wa miaka 70 asiweze kusikia mngurumo wake wala sauti yake, na hivyo pia atakuwa ameepushwa nao, na hatoweza kuingia humo. Wameeleza maana ya neno “khariyf” kama ni miaka ingawa maana yake hasa ni msimu kati ya misimu ya mwaka ambao ni “autumn”. Msimu huu huja mara moja kila mwaka, na hivyo ukija mara sabini ni sawa na miaka 70. Miaka hii sabini si sawa na miaka ya hapa duniani, bali ni kwa vipimo Vyake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), kwani siku moja Kwake ni kama miaka 1000 ya hapa duniani kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالْعَذَابِ وَلَن يُخْلِفَ اللَّـهُ وَعْدَهُ ۚ وَإِنَّ يَوْمًا عِندَ رَبِّكَ كَأَلْفِ سَنَةٍ مِّمَّا تَعُدُّونَ ﴿٤٧﴾
Na wanakuhimiza kwa adhabu, na Allaah Hakhalifu ahadi Yake. Na hakika siku moja kwa Rabb wako ni kama miaka elfu katika yale mnayoihesabu. [Al-Hajj: 47]
Tunarudi tukisema kwamba kwa mujibu wa tafsiyr ya kwanza ya ‘Ulamaa kuhusu “Fiy SabiyliLLaah” ni kuwa hapo Swawm itakuwa na sifa mbili muhimu. Sifa ya wakati na sifa ya mahala.
Sifa ya wakati ni kuwa wakati wa mapambano na vita, ni wakati wa kujibiwa zaidi du’aa. Ama sifa ya mahala, ni kuwa eneo panapopiganiwa vita na Mwislamu, linakuwa ni eneo lililo karibu zaidi na Jannah yake, kwani akiuawa tu kishahidi, basi huingia moja kwa moja Jannah. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((وَاعْلَمُوا أَنَّ الْجَنَّةَ تَحْتَ ظِلاَلِ السُّيُوفِ))
((Jueni kwamba Janna iko chini ya vivuli vya panga)) [Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Awfaa imesimuliwa na Al-Bukhaariy]
Na hii ni kwa ajili ya kuwahamasisha na kuwaraghibisha kuipigania Dini ya Allaah ('Azza wa Jalla) kwa nguvu zao zote. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتًا ۚ بَلْ أَحْيَاءٌ عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ ﴿١٦٩﴾
Na wala usiwadhanie kabisa wale waliouawa katika njia ya Allaah ni wafu, bali wahai, kwa Rabb wao wanaruzukiwa. [Al-Baqarah: 169]
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
07-Mlango Wa Rayyan Peponi Wataingia Wenye Swawm
عَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ رضى الله عنه عَنِ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم قَالَ: (( فِي الْجَنَّةِ ثَمَانِيَةُ أَبْوَابٍ، فِيهَا باب يُسَمَّى الرَّيَّانَ لاَ يَدْخُلُهُ إِلاَّ الصَّائِمُونَ )) البخاري
Imepokelewa toka kwa Sahl bin Sa’d (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Peponi kuna milango minane. Humo kuna mlango uitwao Rayyaan, hawauingii isipokuwa Asw-Swaaimuwn (wafungaji)) [Al-Bukhaariy]
Mafunzo:
Mlango huu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameuweka maalumu kwa ajili ya wafungaji (Swawm) tu. Wafungaji peke yao ndio watakaopita kwenye mlango huu. Umeitwa Rayyaan kutokana na wingi wa mito inayopita kuelekea kwake pamoja na maua na matunda mazuri yenye kuuzunguka.
Pia umeitwa hivyo kwa kuwa mwenye kuufikia, kitamwondokea kiu kikali cha Siku ya Qiyaamah, na kisha atadumu milele na hali ya kutohisi kiu.
Aidha, umeitwa hivi kwa kuwa ni jazaa kwa wafungaji kutokana na kiu na njaa iliyokuwa ikiwakabili wakati wa swawm yao, nao wakasubiri na kuitii amri ya Mola wao mpaka wakati wa kufungua Swawm, na hususan kwa wale wenye kuishi kwenye nchi za joto kali.
Na hapa Hadiyth imegusia tu kiu kutokana na neno "ري" linalonyambuka toka “Ar Rayyaan” kwa kuwa mara nyingi kiu kinakuwa kikimsumbua zaidi mfungaji kuliko njaa, na mwana Aadam anaweza kusota kwa muda mrefu bila ya kula lakini hawezi kusota na kiu kwa zaidi ya wiki moja.
Kutokana na hali hiyo, mlango huu umewekwa spesheli na Allaah ('Azza wa Jalla) kwa wafungaji kwa ajili ya kuwakirimu kutokana na Swawm yao waliyoifanya hapa duniani na tabu ya kiu iliyowasumbua.
Lakini je wahusishwa hapa ni wale wenye kufunga Swiyaam za Ramadhwaan pekee?
‘Ulamaa wanatuambia kwamba wahusishwa hapa ni wale waliofunga Ramadhwaan pamoja na kushikamana na Swawm za Sunnah kama za Jumatatu na Alkhamisi, Ayyamul-biydwh (Masiku meupe) na kadhalika.
Lakini pia kuna mushkel mwingine wa kuunganisha kati ya Hadiyth hiyo na Hadiyth ifuatayo:
عَنْ عُمَرَ رضى الله عنه قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صلى الله عليه وسلم { مَا مِنْكُمْ مِنْ أَحَدٍ يَتَوَضَّأُ، فَيُسْبِغُ اَلْوُضُوءَ، ثُمَّ يَقُولُ: أَشْهَدُ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا اَللَّهُ وَحْدَهُ لَا شَرِيكَ لَهُ، وَأَشْهَدُ أَنَّ مُحَمَّدًا عَبْدُهُ وَرَسُولُهُ، إِلَّا فُتِحَتْ لَهُ أَبْوَابُ اَلْجَنَّةِ" } أَخْرَجَهُ مُسْلِم
Kutoka kwa ‘Umar (رَضِيَ اللهُ عَنْهُ) amesema: Rasuli wa Allaah (صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ) amesema: “Hakuna yeyote miongoni mwenu anayetawadha vizuri, kisha akasema: “Ash-hadu an laa ilaaha illa Allaah Wahdahu laa shariyka Lahu, wa ash-hadu anna Muhammad ‘Abduhuu wa Rasuwluhu” (Nashuhudia kuwa hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah, Peke Yake, hana mshirika, na ninashuhudia kuwa Muhammad ni mja Wake na Rasuli Wake) ila atafunguliwa milango minane ya Jannah.” [Imetolewa na Muslim na At-Tirmidhiy]
Hapa swali linakuja:
“Je, kiwa mtu huyu si katika wafungaji (Swawm), vipi aachiliwe milango yote minane ukiwemo mlango wa “Rayyaan” wakati mlango huu ni kwa wafungaji tu?”
Jibu linasema:
“Ni kweli atakuwa na uhuru kamili wa kuingia mlango wowote autakao. Lakini mlango wa “Rayyaan” hatouchagua, bali atachagua mwingine wowote. Kwa kuwa hapo, wataitwa wafungaji, wakishajitokeza wataambiwa waingie kwenye mlango huo kisha utafungwa. Hii ni kwa Hadiyth nyingine ifuatayo:
عَنْ سَهْلٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((إِنَّ فِي الْجَنَّةِ بَابًا يُقَالُ لَهُ الرَّيَّانُ يَدْخُلُ مِنْهُ الصَّائِمُونَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ لَا يَدْخُلُ مِنْهُ أَحَدٌ غَيْرُهُمْ يُقَالُ أَيْنَ الصَّائِمُونَ فَيَقُومُونَ لَا يَدْخُلُ مِنْهُ أَحَدٌ غَيْرُهُمْ فَإِذَا دَخَلُوا أُغْلِقَ فَلَمْ يَدْخُلْ مِنْهُ أَحَدٌ ))
Imepokelewa kutoka kwa Sahl (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika katika Jannah kuna mlango unaitwa Rayyaan, wataingia humo siku ya Qiyaamah wenye kufunga (Swawm), hatoingia yeyote mwingine. Itasemwa: “Wako wapi waliokuwa wakifunga? Watasimama kuingia hatoingia yeyote mwengine, watakapoingia, utafungwa, basi hatoingia mwengine)) [Al-Bukhaariy 1763, Muslim 1947]
Kadhalika, milango mingine inayobaki pia ina watu wake. Kila mtu ataitwa kwa mujibu wa ubobezi wake kwenye ‘amali fulani. Haya yanathibitishwa na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
عن أَبِي هُرَيْرَةَ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((مَنْ أَنْفَقَ زَوْجَيْنِ فِي سَبِيلِ اللَّهِ نُودِيَ فِي الْجَنَّةِ: يَا عَبْدَ اللَّهِ هَذَا خَيْرٌ فَمَنْ كَانَ مِنْ أَهْلِ الصَّلاَةِ دُعِيَ مِنْ بَابِ الصَّلاَةِ وَمَنْ كَانَ مِنْ أَهْلِ الْجِهَادِ دُعِيَ مِنْ بَابِ الْجِهَادِ وَمَنْ كَانَ مِنْ أَهْلِ الصَّدَقَةِ دُعِيَ مِنْ بَابِ الصَّدَقَةِ وَمَنْ كَانَ مِنْ أَهْلِ الصِّيَامِ دُعِيَ مِنْ بَابِ الرَّيَّانِ)) . فَقَالَ أَبُو بَكْرٍ الصِّدِّيقُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ مَا عَلَى مَنْ يُدْعَى مِنْ هَذِهِ الأَبْوَابِ مِنْ ضَرُورَةٍ فَهَلْ يُدْعَى أَحَدٌ مِنْ هَذِهِ الأَبْوَابِ كُلِّهَا؟ قَالَ: نَعَمْ وَأَرْجُو أَنْ تَكُونَ مِنْهُمْ ))
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kutoa dinari mbili fiy SabiyliLLah (katika njia ya Allaah) basi ataitwa: “Ee mja wa Allaah! Hii ni kheri.” Atakayekuwa ni katika watu wa Swalaah, basi ataitwa toka mlango wa Swalaah, na atakayekuwa ni katika watu wa Jihaad, ataitwa toka mlango wa Jihaad, na atakayekuwa ni katika watu wa Swadaqah, ataitwa toka mlango wa Swadaqah, na atakayekuwa ni katika watu wa Swiyaam, ataitwa toka mlango wa Ar-Rayyaan)) Abu Bakr Asw-Swiddiyq akasema: “Ee Rasuli wa Allaah! Hivi ni lazima mtu aitwe katika mlango mmojawapo tu kati ya milango hii? Je, hivi mtu anaweza kuitwa aingie milango yote?” Akasema: ((Naam! Na nataraji uwe miongoni mwao)) [Muwatwah bin Maalik Kitaab Al-Jihaad]
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
08-Swawm Hufuta Madhambi Yatokanayo Na Mtu Kufitinika Na Mkewe Na Mali Yake
سأل عمر رضي الله عنه قال: من يحفظ حديثًا عن النبي صلى الله عليه وسلم في الفتنة؟ قال حذيفة: أنا سمعته يقول: ((فِتْنَةُ الرَّجُلِ فِي أَهْلِهِ وَمَالِهِ وَجَارِهِ تُكَفِّرُهَا الصَّلَاةُ وَالصِّيَامُ وَالصَّدَقَةُ)).
‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliuliza: “Nani anahifadhi Hadiyth toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu fitnah?” Hudhayfah akasema: Mimi nimemsikia akisema: ((Kufitinika mtu kutokana na mke wake, mali yake na jirani yake, (dhambi yake) hufutwa na Swalaah na Swawm na swadaqah..)) [Al-Bukhaariy]
Mafunzo:
Maana ya fitnah hapa ni makosa anayoyafanya mtu kutokana na mkewe na watoto kwa kujaribu kuwafurahisha kwa linalomkasirisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), au kuitumia mali yake visivyo akaipeleka kwenye sehemu isipo pake, au akakiuka haki za ujirani mwema kwa kumuudhi jirani yake kimatendo au kimaneno na kadhalika.
Asili ya neno “fitnah” ni الابتلاء na الاختبار. Kwa maana kuwa hayo yote yanakuwa ni mtihani kwa mtu, na anaposhindwa mtihani huo, basi anakuwa amefitinika “maftuwn”. Allaah ('Azza wa Jalla) Anatuambia:
أَلَا فِي الْفِتْنَةِ سَقَطُوا ۗ
Tanabahi! Wamekwishaanguka katika fitnah. [At-Tawbah: 49]
Hivyo basi, mtu anapata mtihani kwa mtoto wake, mke wake, mali yake, jirani yake na wengineo. Kwenye mtihani huu ima afaulu au afeli. Na hii inatupa picha ni namna gani kila mtu anavyokabiliwa na mtihani kama huu ambao bila shaka ni mgumu kwa kila mmoja wetu.
Na kwa vile kufeli ni jambo lisiloepukika kwenye mtihani huu, Allaah ('Azza wa Jalla) kwa Rahmah Zake Ameifanya Swalaah, Swawm na Swadaqah, kuwa ni visafisho vya makosa anayoyafanya mtu na kuanguka kwenye mtihani huo.
Swalaah tano anazoziswali Mwislamu kila siku, na Swalaah za Ijumaa anazoziswali wiki baada ya wiki, na Ramadhwaan anayoifunga hadi Ramadhwaan nyingine, hizi zote humtakasa kutokana na makosa hayo ya kuteleza na makosa mengineyo madogo madogo, lakini kwa sharti ya kujiepusha na madhambi makubwa yaliyokemewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na yale saba yanayoangamiza yaliyotajwa kwenye Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
Sharti jingine ni kutofungamana makosa hayo na haki za watu. Ikiwa zitafungamana, basi haki hizo ni lazima awarejeshee wenyewe hapa duniani, na kama hakufanya hivyo, basi atawarejeshea Siku ya Qiyaamah. Hatari ya hili ni kuwa ikiwa haki hizo ni nyingi, basi zinaweza kumaliza mema yake yote, na hatimaye atabebeshwa makosa na madhambi ya walalamikaji, na kisha atatupwa motoni. Na huyo ndio muflis wa kweli kama inavyoeleza Hadiyth iliyopokelewa na Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu):
((أَتَدْرُونَ مَنِ الْمُفْلِسُ؟)) قالوا: المفلس فينا من لا درهمَ له ولا دِينار. قال: ((الْمُفْلِسُ مَنْ يَأْتِي يَوْمَ الْقِيَامَةِ بِصَلَاةٍ وَصَدَقَةٍ وَصَوْمٍ، وَيَأْتِي وَقَدْ ضَرَبَ هَذَا، وَشَتَمَ هَذَا، وَقَذَفَ هَذَا، وَأَخَذَ مَالَ هَذَا، فَيُؤْخَذُ مِنْ حَسَنَاتِهِ لِهَذَا، ولم يبقَ له حسنة، حَتَّى إِذَا فَنِيَتْ حَسَنَاتُهُ أُخِذَ مِنْ سَيِّئَاتِهِ فَوُضِعَتْ عَلَيْهِ))
Mtume Swalla Allaahu Alayhi wa Sallam aliwauliza: ((Je, mnamjua ni nani muflis?)). Wakasema: “Muflis tunayemjua sisi ni mtu asiye na dirham wala dinari”. Akasema: ((Muflis ni yule atakayekuja Siku ya Qiyaamah na Swalaah, Swadaqah na Swawm. Anakuja akiwa amempiga huyu, amemtusi huyu, amemzushia huyu na amedhulumu mali ya huyu. Fungu la mema yake litachukuliwa apewe huyu, mpaka yanapomalizika mema yake (yaani thawabu za Swalaah zake, Swaum zake na Swadaqah zake), na hakubakiwa na chochote - yatachukuliwa mabaya yake abebeshwe yeye)) [Muslim]
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
09-Swawm Na Qur-aan Zitamuombea Mja Ash-Shafaa’ah Siku Ya Qiyaamah
وعَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ : ((الصِّيَامُ وَالْقُرْآنُ يَشْفَعَانِ لِلْعَبْدِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ يَقُولُ الصِّيَامُ أَيْ رَبِّ مَنَعْتُهُ الطَّعَامَ وَالشَّهَوَاتِ بِالنَّهَارِ فَشَفِّعْنِي فِيهِ وَيَقُولُ الْقُرْآنُ مَنَعْتُهُ النَّوْمَ بِاللَّيْلِ فَشَفِّعْنِي فِيهِ قَالَ فَيُشَفَّعَانِ))
Imepokelewa toka kwa Abdullaah bin ‘Amr (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Swiyaam na Qur-aan zitamwombea shafaa’ah (uombezi) mja Siku ya Qiyaamah. Swawm itasema: “Nilimzuia chakula na matamanio yake mchana, basi Niwezeshe nimwombee shafaa’ah. Na Qur-aan itasema: Nilimzuia usingizi usiku, basi Niwezeshe nimwombee shafaa’ah. Akasema, basi vitaomba shafaa’ah)) [Ahmad ni Hadiyth Swahiyh taz Swahiyh Al-Jaami’ (3882)]
Mafunzo:
Mwenye Swawm anatakiwa akithirishe kusoma Qur-aan Tukufu katika masiku haya ya barakah na hususan usiku kwa mujibu wa Hadiyth hii tukufu ambapo Qur-aan wakati inalilia shafaa’ah (uombezi) toka kwa Allaah ('Azza wa Jalla) inaeleza: “Nilikuwa nikimzuia asilale usingizi usiku. Alikuwa halali kwa ajili ya kunisoma mimi.” Na hii ni pengine kwa kuwa Qur-aan yenyewe iliteremshwa wakati wa usiku, usiku wa Laylatul-Qadr ambao ‘amali zake ni bora kuliko za miezi 1000. Mtu anaposoma Qur-aan usiku, tadaburi yake inakuwa ni kubwa zaidi, na moyo unakuwa umetulia kwa kuwa akili yake haishughulishwi na jambo lolote kinyume na mchana wakati wa pilikapilika nyingi za kutafuta riziki.
Imethibiti kwamba Jibriyl ('Alayhis-Salaam) alikuwa akikutana na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kila usiku wa Ramadhwaan na kumsomesha Qur-aan Tukufu.
عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ قَالَ كَانَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَجْوَدَ النَّاسِ وَكَانَ أَجْوَدُ مَا يَكُونُ فِي رَمَضَانَ حِينَ يَلْقَاهُ جِبْرِيلُ وَكَانَ يَلْقَاهُ فِي كُلِّ لَيْلَةٍ مِنْ رَمَضَانَ فَيُدَارِسُهُ الْقُرْآنَ
Imepokelewa kutoka kwa Ibn ‘Abaaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mbora (mwenye matendo mema) wa watu, lakini alikuwa mbora zaidi katika Ramadhwaan kwa sababu Jibriyl alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhwaan akimfundisha Qur-aan)) [Al-Bukhaariy]
Na tukio hili linatufidisha kuwa inapendeza kusoma zaidi Qur-aan, kuifasiri na kuisomesha kama inavyofanyika kwenye Misikiti yetu mingi.
Ash-Shafaa’ah ni nini?
Shafaa’ah ni mtu kumwombea mtu mwingine apatiwe manufaa au aondoshewe adhabu.
Na shafaa’ah iliyothibiti inagawanyika vigawanyo viwili:
Ya kwanza ni Shafaa’ah jumuishi, na hii ni ile ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atawapa idhini baadhi ya waja Wake wema Awatakao kuwaombea wengine. Shafaa’ah hii watapewa Manabii, Wasadikishaji, Mashuhadaa na watu wema. Hawa watawaombea shafaa’ah Waislamu walioko motoni ili watolewe toka humo.
Ya pili ni shafaa’ah mahsusi kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Shafaa’ah hii ijulikanayo kama الشفاعة العظمى ni ile ambayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ataiomba ili mambo yafunguke kutokana na hali ngumu kabisa ya kisimamo cha Siku ya Qiyaamah. Na hii ni baada ya watu kwenda kwa Manabii Aadam, Nuwh, Ibraahiym, Muwsaa na Iysas (‘Alayhimus-salaam) ili wamwombe Allaah ('Azza wa Jalla) mambo yafunguke, na wote hao wakatoa nyudhuru. Kisha wataelekea kwa kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye atasujudu, na atamwomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) mambo yafunguke, nayo yatafunguka. Hadiyth kama ilivyokuja ni ifuatayo:
عَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: يَجْتَمِعُ الْمُؤْمِنُونَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَيَقُولُونَ: لَوْ اسْتَشْفَعْنَا إِلَى رَبِّنَا، فَيَأْتُونَ آدَمَ فَيَقُولُونَ: أَنْتَ أَبُو النَّاسِ خَلَقَكَ اللَّهُ بِيَدِهِ وَأَسْجَدَ لَكَ مَلَائِكَتَهُ وَعَلَّمَكَ أَسْمَاءَ كُلِّ شَيْءٍ فَاشْفَعْ لَنَا عِنْدَ رَبِّكَ حَتَّى يُرِيحَنَا مِنْ مَكَانِنَا هَذَا. فَيَقُولُ: لَسْتُ هُنَاكُمْ وَيَذْكُرُ ذَنْبَهُ فَيَسْتَحِي ، ائْتُوا نُوحًا فَإِنَّهُ أَوَّلُ رَسُولٍ بَعَثَهُ اللَّهُ إِلَى أَهْلِ الْأَرْضِ، فَيَأْتُونَهُ فَيَقُولُ لَسْتُ هُنَاكُمْ وَيَذْكُرُ سُؤَالَهُ رَبَّهُ مَا لَيْسَ لَهُ بِهِ عِلْمٌ. فَيَسْتَحِي فَيَقُولُ: ائْتُوا خَلِيلَ الرَّحْمَنِ فَيَأْتُونَهُ فَيَقُولُ: لَسْتُ هُنَاكُمْ، ائْتُوا مُوسَى عَبْدًا كَلَّمَهُ اللَّهُ وَأَعْطَاهُ التَّوْرَاةَ. فَيَأْتُونَهُ فَيَقُولُ: لَسْتُ هُنَاكُمْ وَيَذْكُرُ قَتْلَ النَّفْسِ بِغَيْرِ نَفْسٍ فَيَسْتَحِي مِنْ رَبِّهِ فَيَقُولُ: ائْتُوا عِيسَى عَبْدَ اللَّهِ وَرَسُولَهُ وَكَلِمَةَ اللَّهِ وَرُوحَهُ فَيَقُولُ: لَسْتُ هُنَاكُمْ ، ائْتُوا مُحَمَّدًا صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَبْدًا غَفَرَ اللَّهُ لَهُ مَا تَقَدَّمَ مِنْ ذَنْبِهِ وَمَا تَأَخَّرَ، فَيَأْتُونِي، فَأَنْطَلِقُ حَتَّى أَسْتَأْذِنَ عَلَى رَبِّي فَيُؤْذَنَ لِي ، فَإِذَا رَأَيْتُ رَبِّي وَقَعْتُ سَاجِدًا فَيَدَعُنِي مَا شَاءَ اللَّهُ ثُمَّ يُقَالُ: ارْفَعْ رَأْسَكَ وَسَلْ تُعْطَهْ، وَقُلْ يُسْمَعْ وَاشْفَعْ تُشَفَّعْ، فَأَرْفَعُ رَأْسِي فَأَحْمَدُهُ بِتَحْمِيدٍ يُعَلِّمُنِيهِ ثُمَّ أَشْفَعُ فَيَحُدُّ لِي حَدًّا فَأُدْخِلُهُمْ الْجَنَّةَ. ثُمَّ أَعُودُ إِلَيْهِ فَإِذَا رَأَيْتُ رَبِّي مِثْلَهُ ثُمَّ أَشْفَعُ فَيَحُدُّ لِي حَدًّا فَأُدْخِلُهُمْ الْجَنَّةَ. ثُمَّ أَعُودُ الرَّابِعَةَ فَأَقُولُ: مَا بَقِيَ فِي النَّارِ إِلَّا مَنْ حَبَسَهُ الْقُرْآنُ وَوَجَبَ عَلَيْهِ الْخُلُودُ)) البخاري، مسلم، مالك، الترمذي وابن ماجه
Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Watakusanyika Waumini Siku ya Qiyaamah na Watasema: Lau tungetafuta kuombewa shafaa’ah kwa Rabb wetu! Watakwenda kwa Aadam na watasema: Wewe ndio baba wa watu, Amekuumba Allaah kwa Mkono Wake na Akaamrisha Malaika wakusujudie, na Akakufundisha majina ya vitu vyote, basi tuombee kwa Rabb wako ili Atupe faraja kutokana na sehemu yetu hii? Atasema: Mimi siwezi kufanya mnaloomba! Na atakumbuka makosa yake na ataona hayaa, atasema: Mfuateni Nuwh, hakika yeye ndiye Rasuli wa kwanza Aliyemtuma Allaah kwa watu ardhini. Watamfuata. Naye atasema: Siwezi kufanya mnaloomba! Na atakumbuka kumuomba kwake Allaah kwa jambo asilokuwa na ujuzi nalo. Naye ataona hayaa na atasema: Nendeni kwa Khaliylur-Rahmaan. Watakwenda kwa Ibraahiym. Naye atawaambia: Siwezi kufanya mnaloomba! Nendeni kwa Muwsaa mja ambaye Allaah Alizungumza naye na Akampa Tawraat. Muwsaa atasema: Siwezi kufanya mnaloomba! Atakumbuka kuwa aliwahi kumuua mtu bila ya haki na ataona hayaa kwa Rabb wake. Atasema: Nendeni kwa ‘Iysaa kwani ni mja wa Allaah na Rasuli Wake na neno Lake na Roho Yake. Naye atasema: Siwezi kufanya mnaloomba! Nendeni kwa Muhammad, ni mja aliyefutiwa makosa yaliyotangulia na yajayo. Watakuja kwangu na nitakwenda kwa Rabb wangu kumuomba idhini (ya maombi), nitapewa idhini. Nitakapomuona Rabb wangu nitasujudu na Ataniacha hivyo hivyo mpaka Atakavyo. Kisha itasemwa: Inua kichwa chako na omba utapewa! Na sema yatasikilizwa (uyasemayo)! Na omba shafaa‘ah utapewa! Nitainua kichwa changu na nitamhimidi kwa Himdi Zake Atakazonifundisha, kisha nitaomba na Atanikubalia idadi kubwa ya watu, nitawaingiza Jannah. Kisha nitarudi tena Kwake. Nitakapomuona Rabb wangu, nitafanya kama mara ya kwanza, kisha nitaomba na Atanikubalia idadi kubwa ya watu nitawaingiza Jannah. Kisha nitarejea mara ya tatu, kisha nitarudi mara ya nne kisha nitasema: Hakuna watu waliobakia motoni isipokuwa Qur-aan imewazuia na watawajibika kubakia humo.” [Al-Bukhaariy, Muslim, Maalik, At-Tirmidhiy na Ibn Maajah]
Na hii ndio ijulikanayo kama المقام المحمود ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amemwahidi Aliposema:
وَمِنَ اللَّيْلِ فَتَهَجَّدْ بِهِ نَافِلَةً لَّكَ عَسَىٰ أَن يَبْعَثَكَ رَبُّكَ مَقَامًا مَّحْمُودًا ﴿٧٩﴾
Na katika usiku, amka uswali (tahajjud) kuisoma (Qur-aan); ni ziada ya Sunnah kwako Asaa Rabb wako Akakuinua cheo kinachosifika. [Al-Israa: 79]
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
10-Du’aa Ya Mwenye Swawm Hairejeshwi
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ قَالَ قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((ثَلاثَةٌ لا تُرَدُّ دَعْوَتُهُمْ الإِمَامُ الْعَادِلُ وَالصَّائِمُ حِينَ يُفْطِرُ وَدَعْوَةُ الْمَظْلُومِ ))
Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) akisema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watatu du’aa zao hazirejeshwi: Imaam (kiongozi) mtenda haki, mwenye Swawm wakati anapofungua, na du’aa ya aliyedhulumiwa)) [Imesimuliwa na At-Tirmidhiy Hadiyth nambari (2525), na Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahihy At-Tirmidhiy Hadiyth nambari (2050)]
Mafunzo:
Hadiyth hii tukufu ni dalili ya kuwa mwenye Swawm anatakiwa akitumie kitambo cha wakati wa kufungua Swawm yake kwa kuomba du’aa ya kheri, kwani wakati huo du’aa hujibiwa.
Bora zaidi cha kusema wakati huo ni yale yaliyopokelewa na ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) aliyesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapofungua Swawm alikuwa Anasema:
(( ذَهَبَ الظَّمَأُ وَابْتَلَّتْ الْعُرُوقُ وَثَبَتَ الأَجْرُ إِنْ شَاءَ اللَّهُ ))
((Kiu kimeondoka, mishipa imelowana, na ujira umethibiti In Shaa Allaah)). [Imesimuliwa na Abuu Daawuwd (2357). Al-Albaaniy kasema ni Hadiyth Hasan katika Swahiyh Abiy Daawuwd (2066)]
Hivyo basi, mwenye Swawm anapoomba wakati huu, anatakikana ahudhurishe moyo wake na awe na yakini kwamba Allaah ('Azza wa Jalla) Atamwitikia du’aa yake hiyo, kwani huo ni wakati wa udhalili na unyenyekevu mkubwa Kwake Subhaanahu wa Ta’aalaa. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth nyingine:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ ، قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وسلم: ((إِنَّ لِلَّهِ تَبَارَكَ وَتَعَالَى عُتَقَاءَ فِي كُلِّ يَوْمٍ وَلَيْلَةٍ)) يَعْنِي: فِي َمَضَانَ وَإِنَّ لِكُلِّ مُسْلِمٍ فِي كُلِّ يَوْمٍ وَلَيْلَةٍ دَعْوَةً مُسْتَجَابَةً))
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Ana watu wa kuwaacha huru na moto kila siku na usiku, na kila mja kati yao ana dua inayojibiwa)) [Imesimuliwa na Ahmad (7401). Na Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika Swahihy Al-Jaami’i (2169), Swahiyh At-Targhiyb Wat-Tarhiyb (1002)]
Na kwa vile hilo la kuachwa huru limethibitishwa na Hadiyth hii, inakuwa ni vizuri zaidi pia mfungaji Swawm aombe kuachwa huru na moto, kwani hakuna mafanikio makubwa kama mtu kuwekwa mbali na moto wa Jahannam.
Hivyo basi, atakayemwomba Mola wake wakati huo wa kufungua swawm yake kwa moyo safi na maombi halali ya ki-Shariy’ah, na wala kisiwepo kizuizi cha kukubaliwa du’aa kama mlo wa haramu na kadhalika, mbali na kuwa ni mwenye kuwajibika kwa maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake, basi Allaah ('Azza wa Jalla) Huijibu du’aa yake moja kwa moja.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametaja kuhusu kuomba ‘duaa mubashara baada ya Aayah za kuhusu Ramadhwaan na Swiyaam, kwamba Anamtaqabalia mja Wake pindi anapomuomba du’aa ikiwa atamwamini Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyosema:
وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ ۖ فَلْيَسْتَجِيبُوا لِي وَلْيُؤْمِنُوا بِي لَعَلَّهُمْ يَرْشُدُونَ ﴿١٨٦﴾
Na watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni Niko karibu (kwa ujuzi); Naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba. Basi waniitikie Mimi na waniamini Mimi, wapate kuongoka. [Al-Baqarah: 186]
Kingine anachotakiwa mfungaji wa Swawm kushikamana nacho wakati wa swawm yake, ni kukithirisha kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika kipindi chote cha mchana, kwani swawm humfanya awe karibu zaidi na Allaah ('Azza wa Jalla) na wakati anapokuja kumwomba wakati wa kufungua Swawm, Allaah (‘Azza wa Jalla) Anakuwa Ashajikurubisha zaidi naye.
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
11-Fadhila Za Suhuwr (Daku)
عن انس بن مالك رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((تَسَحَّرُوا فَإِنَّ فِي السَّحُورِ بَرَكَةً))
Imepokelewa toka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Kuleni suhuwr (daku), kwani kuna barakah katika daku)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Mafunzo:
‘Ulamaa wanasema kwamba barakah katika suhuwr (daku) inapatikana kwa njia tofauti.
Kwanza: Barakah hupatikana kwa kuifuata Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Pili: Barakah inapatikana kwa kukhalifiana na Ahlul-Kitaab.
Tatu: Barakah inapatikana kwa kumpatia Mwislamu nguvu ya kufunga Swawm na kufanya kazi zake nyinginezo mchana.
Nne: Barakah inapatikana kwa kumfanya mwenye Swawm kuwa mbali na hali ya hamaki hamaki itokanayo na njaa.
Tano: Barakah inapatikana kwa sababu ya kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuomba du’aa wakati huo ambapo inakuwa yakini kujibiwa kabla ya mwisho wa usiku ambapo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anateremka katika wingu wa dunia.
Aidha, barka hiyo inaweza kuambatana na mambo ya Aakhirah, kwani kusimamisha Sunnah, humpatisha Muumini malipo ya Aakhirah.
Na kubwa zaidi ya hayo, ni kuwa Allaah ‘Azza wa Jalla) pamoja na Malaika Wake, Huwatakia rahmah wote wenye kula daku. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
عَنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ : ((السُّحُورُ أَكْلَةٌ بَرَكَةٌ فَلا تَدَعُوهُ وَلَوْ أَنْ يَجْرَعَ أَحَدُكُمْ جَرْعَةً مِنْ مَاءٍ فَإِنَّ اللَّهَ وَمَلائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى الْمُتَسَحِّرِينَ)) رواه أحمد (11003) وحسنه الألباني في صحيح الجامع (3683) .
Imepokelewa toka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Suhuwr (Daku) chakula chake ni barakah, basi msikiache hata kumeza mmoja wenu funda la maji. Kwani Allaah na Malaika Wake, wanawatakia rahmah wenye kula daku)) [Ahmad (11003) na ameipa daraja la Hasan Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (3683)]
Na kwa ajili ya kufaidika zaidi na barakah hizo, inakuwa vyema kwa walaji daku wautumie vyema muda huo kwa kutawadha na kuswali angalau rakaa mbili, kukithirisha du’aa, kusoma Qur-aan Tukufu na kuleta nyiradi. Pia kuwakirimu majirani kwa kuwapelekea daku na hata kwa wasiojiweza.
Tunarudi tukisema: “Je, amri hii ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwetu “تسحروا” (kuleni daku), ni amri ya wajibu?
‘Ulamaa wanasema kuwa si amri ya wajibu, bali ni amri ya Sunnah au Mustahabb (inapendekezwa). Na dalili ni kuwa yeye Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya الوصال pamoja na Maswahaba. الوصال ni kufunga Swawm siku mbili mfululizo bila kufuturu au kula daku.
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
12-Fadhila Za Kuchelewesha Suhuwr (Daku)
عَنْ أَنَسٍ، عَنْ زَيْدِ بْنِ ثَابِتٍ ـ رضى الله عنه ـ قَالَ تَسَحَّرْنَا مَعَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم ثُمَّ قَامَ إِلَى الصَّلاَةِ. قُلْتُ : كَمْ كَانَ بَيْنَ الأَذَانِ وَالسَّحُورِ؟ قَالَ: قَدْرُ خَمْسِينَ آيَةً .
Imepokelewa toka kwa Anas aliyepokea toka kwa Zayd bin Thaabit (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa alisema: “Tulikula daku pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kisha akanyanyuka kwenda katika Swalaah. Nikauliza: Kulikuwa na muda gani baina ya iqaamah na suhuwr (daku)? Akasema: “Kama Aayah khamsini hivi” [Al-Bukhaariy]
Mafunzo:
Hadiyth hii ni dalili ya kuwa imesuniwa kuchelewesha kula suhuwr (daku) hadi muda kidogo kabla ya Swalatul Fajr, kwani kitambo cha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Zayd kumaliza kula daku na kuingia katika Swalaa kilikuwa ni kiasi cha kusoma mtu Aayah khamsini (50) za Qur-aan Tukufu kwa kisomo cha wastani; si cha haraka wala cha kuvuta sana. Na hii inaonyesha kwamba wakati wa Swalaah uko karibu na wakati wa kuanza siku mpya ya Swawm.
Lakini pamoja na hivyo, inajuzu kula suhuwr (daku) katikati ya usiku kama saa sita au saba, au hata kabla ya hapo kwa mujibu wa hali ya kila mmoja ingawa ni kinyume na Sunnah.
Mwislamu akila daku mapema, anaweza kulala na kupitwa na Swalaah ya Alfajiri pamoja na mengi ya kheri yanayopatikana nyakati za mwisho za usiku Alizoziita Allaah (‘Azza wa Jalla) katika Qur-aan الاسحار, neno ambalo السحور (daku) limenyambulika toka hapo.
Mla suhuwr (daku) anatakikana ale kidogo kiasi cha kushiba. Asijaze tumbo, kwani kutamletea uvivu na uzito utakaosababisha kushindwa kufanya mengi ya kheri. Hata tembe chache tu za tende zinatosha kwa daku.
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
(( سحور المؤمن التمر))
((Suhuwr (Daku) ya Muumini ni tamr (tende))). [Abuu Daawuwd, na isnadi yake imenyooka]
Hadiyth hii pia inaonyesha kuwa imesuniwa suhuwr (daku) kuwa tende, au mlo pamoja na tende.
Sunnah hii wengi wameghafilika nayo wakidhani kuwa tende ni wakati wa kufungulia Swawm pekee.
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
13-Fadhila Za Kuwahi Kufuturu
عَنْ سَهْلِ بْنِ سَعْدٍ، أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ : ((لاَ يَزَالُ النَّاسُ بِخَيْرٍ مَا عَجَّلُوا الْفِطْرَ)) متفق عليه
Imepokelewa toka kwa Sahl bin Sa’d As Saa’idiy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watu wataendelea kudumu kwenye kheri, madhali wanaharakia kufungua Swawm)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Mafunzo:
Hadiyth hii ina mambo kadhaa ndani yake:
Kwanza: Ni Sunnah mtu asicheleweshe kufungua Swawm yake, bali afungue mara tu baada ya kuhakikisha kuwa jua lishazama. Na hii ni Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), na madhali Waislamu wataishikilia Sunnah hii, basi wataendelea kuwa ndani ya kheri.
Pili: Ni Sunnah mwenye Swawm afungue kwa “rutwab” na kama hatopata, basi kwa “tamr”, na kama hakupata, basi afungue kwa maji. Hili limesuniwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth yake nyingine.
“Rutwab” na “tamr” vinameng’enyeka haraka tumboni kutokana na mada zake za kisukari.
Rutwab = Tende freshi, mpya safi ziloiva ambazo zimajimaji.
Tamr = Tende zinazobadilika hali baada ya hatua ya rutwb kwa kuanikwa juani, hivyo huwa ni kavu kiasi fulani.
Tatu: Uharakiaji kufungua Swawm unabeba hukmu zifuatazo:
(a) Kuharakia huko ni kulitii Agizo la Allaah (‘Azza wa Jalla) kama Muumini alivyoitikia agizo la kufunga Swawm.
(b) Ni kuwa mbali na uchupaji mipaka “ghuluwwi” na kujiingiza katika jambo ambalo halikuamrishwa.
(c) Mwislamu anaitumia vyema rukhsa aliyopewa inayoingia ndani ya wigo wa kuwepesishiwa na kusahilishiwa maarisho ya Dini.
(d) Kutojishabihisha na Ahlul- Kitaab. Hao huchelewesha kufungua Swawm kama alivyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((لا يَزَالُ الدِّينُ ظَاهِرًا مَا عَجَّلَ النَّاسُ الْفِطْرَ لأَنَّ الْيَهُودَ وَالنَّصَارَى يُؤَخِّرُونَ ))
((Dini itaendelea kuwa shindi na juu madhali watu wataharakia kufungua Swawm, kwa kuwa Mayahudi na Manaswara huchelewesha)) [Sunan Abiy Daawuwd (2353) na Al-Albaaniy ameipa daraja ya Hasan]
(e) Mfungaji hupata nguvu ya kuendelea na ‘ibaada zingine kama Swalaah za faradhi na za Sunnah zinazofuatia baada ya kufungua Swawm.
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
14-Thawabu Za Kumfuturisha Mwenye Swawm
عن زيد بن خالد رضي الله عنه قال: قال رسول صلى الله عليه وسلم: ((مَنْ فَطَّرَ صَائِمًا كَانَ لَهُ مِثْلُ أَجْرِهِ غَيْرَ أَنَّهُ لَا يَنْقُصُ مِنْ أَجْرِ الصَّائِمِ شَيْئًا )) أخرجه أحمد والنسائي وصححه الألبان
Imepokelewa kutoka kwa Zayd bin Khaalid (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallaam) amesema: ((Atakayemfuturisha aliyefunga atapata ujira (wa Swawm) kama ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga)) [Ahmad, An-Nasaaiy – Ameipa daraja ya Swahiyh Shaykh Al-Albaaniy]
Mafunzo:
Hadiyth hii inatuonyesha fadhila ya kumfuturisha mwenye Swawm na ujira mkubwa unaopatikana ambao ni sawa na mfungaji anayefuturishwa. Jambo hili waliLlaahil-Hamd linafanywa na Waislamu wengi wenye uwezo. Kuna baadhi yao huleta vyakula vya futari Misikitini ikiwa ni pamoja na mlo kamili kwa ajili ya wenye kuswali. Kuna wengine huleta na kugawa tende kwa wafungaji, na kuna wengine hata maji tu, kila mtu kwa mujibu wa uwezo wake na hali yake.
Isitoshe, kuna ada nzuri iliyotanda kwenye baadhi ya nchi zetu. Majirani hupelekeana futari kila mtu kwa mujibu wa kile alichokiandaa angalau kidogo. Kwa ada hii, utakuta majirani hupata futari za aina tofauti tofauti, na hili bila shaka linazidisha mapenzi na roho ya ushirikiano zaidi kati ya majirani. Na hapa kila mmoja hujipatia fungu lake la thawabu bila kumpunguzia thawabu mwingine.
Kufuturisha kunakuwa pia vile vile kwa njia ya kutoa pesa, au kuwagaiwa wafungaji vifurushi vya unga, sukari, mafuta, tambi na kadhalika kama inavyofanyika katika baadhi ya nchi. Katika baadhi ya nchi pia, utakuta watu wanazunguka na magari yao wakati wa kabla ya adhana ya Swalaah ya Magharib, wakiwatafuta walio majiani ambao wamechelewa kufika majumbani mwao, na kuwagaiwa milo ya futari iliyofungwa vizuri.
Katika nchi nyingine, kuna matajiri ambao huweka mahema ya kuwafuturisha wafungaji kwa muda wa mwezi mzima, na futari huwa ni ya hali ya juu inayomfanya aliyefuturishwa kutoka hapo akiwa ameridhika kabisa. Hili ni jambo la kushukuriwa na kuombewa du’aa.
Haya yote yanaingia ndani ya wigo huu wa kheri ambao Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ndio mtoaji zaidi kuliko miezi mingine yote.
Na huenda kinachowapa chachu Waislamu kuwa na pupa ya kuwafuturisha nduguzo Waislamu, ni pale wanapoikumbuka neema ya Allaah ('Azza wa Jalla) kwao ya kumiliki hicho wanachokitoa kwa nduguzo katika mwezi huu wa kheri na Baraka, na kuwezeshwa kufunga.
Kukutana Swawm na kulisha masikini kunakuwa na msukumo zaidi kwa Mwislamu kufutiwa makosa yake na kulindwa na moto wa Jahannam likiongezewa hili na Qiyaamul-Layl (kisimamo cha usiku kuswali). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Mu’aadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'anhu):
أَلَا أَدُلُّكَ عَلَى أَبْوَابِ الْخَيْرِ ؟ الصَّوْمُ جُنَّةٌ، وَالصَّدَقَةُ تُطْفِئُ الْخَطِيئَةَ كَمَا يُطْفِئُ الْمَاءُ النَّارَ، وَصَلَاةُ الرَّجُلِ فِي جَوْفِ اللَّيْلِ، ثُمَّ تَلَا: ((تَتَجَافَى جُنُوبُهُمْ عَنْ الْمَضَاجِعِ...)) حَتَّى بَلَغَ ((يَعْمَلُونَ))
((Je, nikuonyeshe milango ya kheri? Swawm ni kinga, Swadaqah inazima makosa kama maji yanavyozima moto, na Swalaah ya mtu usiku mpevu)). Kisha akasoma:
تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ
Mbavu zao zinatengana na vitanda …. Mpaka akafikia:
يَعْمَلُونَ
wakiyatenda. [Imesimuliwa na At Tirmidhiy. Amesema ni Hadiyth Hasan – Aayah ni Suwrah As-Sajdah: 16-17]
Cha muhimu zaidi kuchunga katika ‘amali hii ya kheri ya kuwafuturisha wafungaji, ni kujiepusha na ufujaji, israfu na riyaa. Chakula kipikwe kwa mujibu wa idadi ya watu, na ikiwa kitabaki basi kihifadhiwe na kitumike siku inayofuatia. Allaah ('Azza wa Jalla) Anatuambia:
وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ ﴿٣١﴾
Na kuleni na kunyweni; na wala msifanye israfu. Hakika Yeye (Allaah) Hapendi wanaofanya israfu [Al-A’raaf: 31]
Anatuambia tena:
إِنَّ الْمُبَذِّرِينَ كَانُوا إِخْوَانَ الشَّيَاطِينِ ۖ وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِرَبِّهِ كَفُورًا ﴿٢٧﴾
Hakika wabadhirifu wamekuwa ni ndugu wa mashaytwaan, na shaytwaan amekuwa ni mwingi wa kumkufuru Rabb wake. [Al-Israa: 27]
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
15-Fadhila Za Swalaah Ya Taraawiyh
عَنْ أَبِي سَلَمَةَ بْنِ عَبْدِ الرَّحْمَنِ ، أَنَّهُ سَأَلَ عَائِشَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهَا : كَيْفَ كَانَتْ صَلاَةُ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي رَمَضَانَ ؟ قَالَتْ : " مَا كَانَ يَزِيدُ فِي رَمَضَانَ وَلاَ فِي غَيْرِهِ عَلَى إِحْدَى عَشْرَةَ رَكْعَةً ، يُصَلِّي أَرْبَعَ رَكَعَاتٍ ، فَلاَ تَسْأَلْ عَنْ حُسْنِهِنَّ وَطُولِهِنَّ ، ثُمَّ يُصَلِّي أَرْبَعًا ، فَلاَ تَسْأَلْ عَنْ حُسْنِهِنَّ وَطُولِهِنَّ ، ثُمَّ يُصَلِّي ثَلاَثًا ، فَقُلْتُ : يَا رَسُولَ اللَّهِ تَنَامُ قَبْلَ أَنْ تُوتِرَ؟ قَالَ : ( تَنَامُ عَيْنِي وَلاَ يَنَامُ قَلْبِي ) .
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Salamah bin ‘Abdir-Rahmaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba kamuuliza ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa): Vipi ilikuwa Swalaah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Ramadhwaan? Akasema: “Hakuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akizidisha katika Ramadhwaan wala katika miezi mingineyo zaidi ya rakaa kumi na moja. Anaswali nne, usiulize umakinifu na urefu wa rakaa hizo. Kisha anaswali nne, usiulize umakinifu na urefu wa rakaa hizo, halafu anaswali tatu)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Mafunzo:
Swalaah ya Taraawiyh ni Swalaah inayoswaliwa kwa jamaa katika mwezi wa Ramadhwaan. Inaweza pia kuswaliwa na mtu peke kama hakupata nafasi ya kuswali jamaa na wenzake.
Imeitwa kwa jina hili la Taraawiyh kutokana na neno ترويحة ambalo wingi wake ni تراويح , kwa kuwa Maswahaba walikuwa wakipumzika kidogo kati ya kila tasliym mbili, yaani kila baada ya rakaa nne.
Na kwa mujibu wa Hadiyth hii ya Mama wa Waumini‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa), ni kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali rakaa kumi na moja tu. Lakini kitendo hiki cha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakidulishi kuwa ni lazima ziwe rakaa hizo hizo kumi na moja, bali zinaweza kupungua chini ya hapo kwa mujibu wa hali ya mtu, au zikazidi kwa mujibu wa nguvu na utashi wa mwenye kuiswali. Anaweza kuswali rakaa 36 kama ilivyo kwa dhehebu la Imaam Maalik.
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Taraawiyh jamaa na Maswahaba wake kwa muda wa siku tatu tu. Haya yanaelezwa na Mama wa Wuamini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) aliposema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliswali Msikitini. Watu wengi wakaswali pamoja naye. Kisha akaswali usiku uliofuata, na watu wakazidi kuwa wengi zaidi. Kisha usiku wa tatu walijumuika, lakini yeye hakutoka kuswali nao. Asubuhi ilipopambazuka aliwaambia: ((Niliona mlichokifanya. Hakuna kilichonizuia kutoka niwajieni isipokuwa nilichelea kufaradhiwa juu yenu)) [Al-Bukhaariy]
Na baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kufariki, ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliifufua Sunnah hii.
Imepokelewa toka kwa Abdur-Rahmaan bin Abdil-Qaariy akisema: “Nilitoka pamoja na ‘Umar bin Al–Khattwaab usiku mmoja wa Ramadhwaan kwenda Msikitini. Tukakuta watu wamezagaa wakiswali. Mwingine anaswali peke yake, na mwingine anaswali na watu kidogo. Umar akasema: “Naona ingelikuwa bora zaidi kama ningeliwakusanya hawa wakaswalishwa na Imaam mmoja.” Halafu akaazimia na akawakusanya waswalishwe na Ubayya bin Ka’ab. Kisha nikatoka naye usiku mwingine, na watu wanaswalishwa na Imaam mmoja. Umar akasema: “Bid‘ah njema hii.”
Makusudio ya bid‘ah hapa kwa mujibu wa kauli ya ‘Umar, ni bid‘ah ya kilugha na si bid‘ah ya kiistilahi. Ni Sunnah aliyoiasisi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kisha ‘Umar akaifufua. Anatuambia:
عَلَيْكُمْ بِسُنَّتِي وَسُنَّةِ الْخُلَفَاءِ الرَّاشِدِينَ الْمَهْدِيِّينَ عَضُّوا عَلَيْهَا بِالنَّوَاجِذِ وَإِيَّاكُمْ وَمُحْدَثَاتِ الأُمُورِ فَإِنَّ كُلَّ بِدْعَةٌ ضَلاَلَةٌ)) رواه أبو داوود والترمذي وقال حديث حسن صحيح
(Shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa waongofu, waliohidika zishikilieni kwa magego [mambo yao]. Na tahadharini na mambo yenye kuzushwa, kwani kila uzushi ni upotovu)) [Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy, na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh].
Swalaah hii ya Taraawiyh Waislamu wengi hufanya pupa ya kuiswali. Lakini baadhi yao, huiswali kwa spidi ya hali ya juu bila khushuw’ (utulivu, unyenyekevu) wala khudhwu’ (utiifu, kujisalimisha kikamilifu kiakili na moyo) almuradi kumaliza. Hawa wana hatari ya kukosa thawabu kubwa na kukosa mafanikio Aliyoyagusia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) yatokanayo na khushuw’ na khudhuw’ ndani ya Swalaah. Anatuambia:
قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾
Kwa yakini wamefaulu Waumini.
الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾
Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea. [Al-Muuminuwn: 1-2]
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
16-Fadhila Za I’tikaaf
عَنْ عَائِشَةَ رضى الله عنها قَالَتْ: "كَانَ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم يَعْتَكِفُ فِي الْعَشْرِ الأَوَاخِرِ مِنْ رَمَضَانَ، فَكُنْتُ أَضْرِبُ لَهُ خِبَاءً فَيُصَلِّي الصُّبْحَ ثُمَّ يَدْخُلُهُ"
Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) akisema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikaa I’tikaaf katika kumi la mwisho la Ramadhwaan. Nilikuwa nikimtengenezea kijihema, akaswali Alfajiri, kisha akaingia humo)) [Al-Bukhaariy (4/346)]
Mafunzo:
Maana ya I’tikaaf ki Shariy’ah ni kukaa Msikitini kwa lengo la kufanya ‘ibaadah kwa ajili ya Allaah (‘Azza wa Jalla) Peke Yake. ‘Ibaadah hii tukufu imesuniwa kwa wanaume na wanawake kutokana na yaliyothibiti toka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alikuwa akikaa I’tikaaf katika kumi la mwisho pamoja na baadhi ya wakeze, na wake zake hao waliendelea kukaa I’tikaaf baada ya yeye kufariki.
Mahala pa kufanyia I’tikaaf hii ni kwenye Msikiti unaoswaliwa jamaa, na ikiwa I’tikaaf itapitiwa na Ijumaa, basi inakuwa ni bora zaidi.
I’tikaaf haina muda maalumu kwa mujibu wa kauli sahihi zaidi za ‘Ulamaa, na pia haina sharti kuwa lazima mtu awe amefunga (Swawm), lakini akiwa amefunga inakuwa bora zaidi.
Muda mzuri zaidi wa kukaa I’tikaaf ni katika kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhwaan kwa kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikuwa akikaa I’tikaaf katika kumi hili na kutoka moja kwa moja baada ya kumalizika. Alikuwa akiianza Alfajiri ya tarehe 21 ya Ramadhwaan hadi mwisho.
Mwenye kukaa I’tikaaf anaruhusiwa kutenga kijieneo chake ndani ya Msikiti ili aweze kupumzika na kulala wakati anapohitajia kufanya hivyo. Na wakati ‘ibaadah yake inaendelea, anatakikana akithirishe kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kusoma Qur-aan, kuomba maghfirah, na kuomba du’aa badala ya kujishughulisha na mambo ya kidunia ambayo aslani ameyasusa kwa ajili ya I’tikaaf yake.
Hakuna ubaya kutembelewa na watu kama watahitaji kufanya hivyo na kuzungumza naye. Wakeze Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wakimtembelea na kuzungumza naye. Mara moja mkewe Swafiyyah alimtembelea, akazungumza naye, na wakati alipoondoka, alikwenda naye mpaka kwenye mlango wa Msikiti. Na hili linaonyesha kuwa hakuna ubaya kufanya hivyo.
Masharti ya I’tikaaf:
1- Kuwa Mwislamu.
2- Kuwa na akili.
3- Kuweka niyya ya kujikurubisha kwa Allaah (‘Azza wa Jalla) kama zilivyo amali nyinginezo.
4- Wakati wa I’tikaaf uwe muda ambapo Swawm inasihi. Haijuzu kukaa I’tikaaf siku ya ‘Iyd Al-Fitwr au ‘Iyd Al-Adhw-haa kwa kuwa ni haramu kuwa katika Swawm.
5- Ifanyike ndani ya Msikiti mkubwa ambapo watu huswalia jamaa. Kwa maana hiyo, haifai I’tikaaf kwenye Msikiti mdogo wa zawiya au nyumbani. Hii ni kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَلَا تُبَاشِرُوهُنَّ وَأَنتُمْ عَاكِفُونَ فِي الْمَسَاجِدِ ۗ
Na wala msiwaingilie hali ya kuwa nyinyi wenye kukaa i’tikaaf Misikitini. [Al-Baqarah: 186]
6- Msikiti uwe ni mmoja tu. Haifai kufanyia I’tikaaf moja kwenye Misikiti miwili kwa kukaa kwenye Msikiti mmoja baadhi ya siku na kumalizia zingine kwenye Msikiti mwingine.
7- Asitoke Msikitini ila kwa dharura tu.
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
17-Fadhila Za Laylatul-Qadr
عن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: ((مَن قام ليلةَ القدر إيمانًا واحتسابًا، غُفر له ما تقدَّم من ذنبه)) متفق عليه.
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mwenye kusimama Usiku wa Laylatul-Qadr kwa iymaan na kutaraji malipo, hughufiriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Mafunzo:
Hadiyth hii ina faida kadhaa:
1-Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameutunuku umma wetu huu usiku huu wa barka wenye sifa hizi mahsusi:
2-Ni usiku uliobarikiwa kwa kheri zake nyingi, fadhila na thawabu kochokocho. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ﴿٣﴾
Hakika Sisi Tumeiteremsha (Qur-aan) katika usiku uliobarikiwa [Ad-Dukhaan: 3]
3-Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameteremsha ndani yake Qur-aan Tukufu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)
إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ ﴿١﴾
Hakika Sisi Tumeiteremsha Qur-aan katika Laylatil-Qadr (usiku wa Qadar). [Al-Qadr: 1]
4-Amali anayoifanya mja ndani ya usiku huu, malipo yake ni zaidi ya amali iliyofanywa katika miezi 1000 ambayo ni zaidi ya miaka 84 kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍ ﴿٣﴾
Laylatul-Qadr ni mbora kuliko miezi elfu. [Al-Qadr: 3]
5-Malaika huteremka ardhini wakibubujisha kheri, barkah na rahmah. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatuambia:
تَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم
Wanateremka humo Malaika na Ar-Ruwh (Jibriyl) kwa idhini ya Rabb wao [Al-Qadr: 4]
6-Ni usiku wa amani na usalama kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ ﴿٥﴾
Amani mpaka kuchomoza Alfajiri. [Al-Qadr: 5]
7-Mwenye kuswali usiku huo kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) basi hughufuriwa dhambi zake zote.
Maana Ya Al-Qadr:
‘Ulamaa wametofautiana kuhusu maana ya neno la القدر . Kuna kauli tatu mashuhuri.
Kauli ya kwanza inasema kuwa maana ya Al-Qadri ni التقدير yaani makadirio (ukadirishaji). Na hapa ina maana kwamba katika usiku huu, makadirio ya mwaka ya viumbe vyote hupitishwa na kukadiriwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ﴿٤﴾
Katika (usiku) huo hupambanuliwa kila jambo la hikmah. [Ad-Dukhaan: 4]
Kauli ya pili inasema: Maana ya القدر ni utukufu na uluwa wa cheo. Hii ina maana kwamba usiku huu una utukufu maalumu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
Kauli ya tatu inasema kwamba القدر ni kwa maana ya ufinyu au mbanano. Kwa maana kwamba kutokana na wingi wa Malaika wanaoteremka siku hiyo, ardhi inakuwa finyu.
Tafsiyr zote hizi tatu zinaonyesha ni namna gani usiku huu ulivyo na uzito kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa Malaika Wake na kwa Waumini.
Mwislamu anatakiwa afanye hima na juhudi zake zote katika mwezi mzima wa Ramadhwaan kwa jili ya kuusaka usiku huu.
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
18-Du’aa Usiku Wa Laylatul-Qadr
عَن عَائِشَةَ، قالَتْ: قُلْتُ: يا رَسُولَ اللهِ، أرَأيْتَ إنْ عَلِمْتُ أيُّ لَيْلَةٍ لَيْلَةُ الْقَدْرِ، مَا أقُولُ فِيها؟ قَالَ: ((قُولي: اللَّهُمَّ إنَّكَ عَفُوٌّ كَرِيمٌ تُحِبُّ العَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي)).
Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba amesema: “Ee Rasuli wa Allaah! Nieleze ikiwa nitajua usiku fulani ndio wa Laylatul-Qadr, niseme nini?” Akasema: ((Sema: Allaahumma Innaka 'Afuwwun Kariymun Tuhibbul-'Afwa fa'fu 'anniy (Ee Allaah Hakika Wewe ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa Ukarimu Unapenda kusamehe basi Nisamehe mimi)) [At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy fiy Sunan Al-Kubraa (7712) Ibn Maajah (3850), Ahmad (25384) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (3513)
Mafunzo:
العفو (Al-‘Afw) Ni Jina kati ya Majina Matukufu ya Allaah ('Azza wa Jalla) yenye kuonyesha upana wa kusamehe Kwake madhambi ya Waja Wake vyovyote yawavyo kama watatubia na kurejea.
Na العفو “Al-Afw” asili yake ni kufuta na kuondosha kabisa athari ya kitu. Na hii ina maana kuwa Allaah ('Azza wa Jalla) Huyafuta kabisa madhambi ya mja Wake bila kubakisha chembe ya athari.
Ama “Al Kariym”, hili pia ni Jina katika Majina ya Allaah ('Azza wa Jalla) linaloonyesha wingi wa kuwapururia kheri waja Wake.
Katika Hadiyth hii Tukufu, Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anamfundisha Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu anhaa) du’aa mwafaka ya kuomba kama atabahatika kuutambua usiku fulani kuwa ni usiku wa Laylatul-Qadr. Hakumtaka aombe mali, au cheo, taqwa au kingine chochote isipokuwa msamaha wa kufutiwa kabisa madhambi yote. Kwa kuwa mambo mengine anaweza kuyaomba katika nyakati nyingine zozote ambazo humpitia mtu kila siku. Lakini usiku huu ambao ni nadra kuupata, na unakuja mara moja tu kila mwaka, du’aa hii inakuwa mwafaka zaidi kuliko du’aa nyingine yoyote.
Msamaha huu wa Allaah ('Azza wa Jalla) kama mja ataupata, basi moja kwa moja mja huyo ataingia Peponi kwa kuwa hakuna tena kizuizi cha kufika huko.
Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anayapenda Majina Yake na Sifa Zake, na Anapenda waja Wake wamwabudie kwayo, na wayafanyie kazi kwa muktadha wake na maana zake.
Madhambi na maasia ni moja kati ya sababu kubwa za kuteremka misukosuko kwetu, mitihani na naqama nyinginezo hapa duniani, na pia kuondoshewa neema ambazo Allaah ('Azza wa Jalla) Amewaneemesha waja Wake. Ama huko Aakhirah, mja kama hana madhambi basi bila shaka ataingia Peponi moja kwa moja.
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
19-Sifa Za Laylatul-Qadr
عَنْ أَبِي هُرَيْرَة رَضِيَ اللَّه عَنْهُ قَالَ : لَمَّا حَضَرَ رَمَضَان قَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ((قَدْ جَاءَكُمْ شَهْرُ رَمَضَان شَهْرٌ مُبَارَكٌ اِفْتَرَضَ اللَّهُ عَلَيْكُمْ صِيَامَهُ تُفْتَح فِيهِ أَبْوَاب الْجَنَّة وَتُغْلَق فِيهِ أَبْوَابُ الْجَحِيم وَتُغَلُّ فِيهِ الشَّيَاطِين فِيهِ لَيْلَة خَيْرٌ مِنْ أَلْف شَهْر مَنْ حَرُمَ خَيْرهَا فَقَدْ حُرِمَ)) وَرَوَاهُ النَّسَائِيّ
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Huraryah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba ilipofika Ramadhwaan, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Umekujieni mwezi wa Ramadhwaan, ni mwezi wa Baraka. Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni fardhi, milango ya Jannah hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na mashaytwaan hufungwa. Katika mwezi huu, kuna usiku ulio bora kuliko miezi elfu. Atakayenyimwa kheri zake, basi hakika amenyimwa!)) [An-Nasaaiy]
Mafunzo:
Ni vipi Mwislamu ataujua usiku huo? Kuna baadhi ya alama zilizothibitishwa na Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kati ya hizo ni:
1-Mwezi kuwa na umbo la nusu sinia kutokana na Hadiyth:
عَنْ أَبِي حَازِمٍ، عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ، رضى الله عنه قَالَ تَذَاكَرْنَا لَيْلَةَ الْقَدْرِ عِنْدَ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ: ((أَيُّكُمْ يَذْكُرُ حِينَ طَلَعَ الْقَمَرُ وَهُوَ مِثْلُ شِقِّ جَفْنَةٍ)) مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Haazim, kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyesema: “Tulitajiana Laylatul-Qadr kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye akasema: ((Yupi kati yenu ana kumbuka wakati ulipochomoza mwezi ukiwa mithili ya nusu sinia?)) [Muslim]
Na hapa kuna ishara kuwa usiku wa Laylatul Qadr unakuwa katika kumi la mwisho, kwa kuwa mwezi hauwi katika picha hiyo, isipokuwa katika kumi la mwisho la mwezi wa Hijriyyah.
2-Ni usiku wake kuwa na nuru, na utulivu, na hali ya hewa ya wastani. Ni kwa Hadiyth isemayo:
وَهِيَ لَيْلَةٌ طَلْقَةٌ بَلْجَةٌ لَا حَارَّةٌ وَلَا بَارِدَةٌ ،
((Nao ni usiku mwangavu, uliotulia, usio na joto wala baridi)) [Hadiyth Marfuw’ kutoka kwa Jaabir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Ibn Khuzaymah (2190)]
Zingine ni kama Mwislamu kujisikia hali nzuri ya kisaikolojia, uchangamfu wa mwili, khushuu ya moyo na kadhalika.
La muhimu kwa Mwislamu ili aweze kuupata usiku huo, ni kujitahidi kuanzia mwanzo wa mwezi hadi mwisho kufanya ‘ibaadah kwa nguvu zake zote, na ahakikishe kuwa hakuna usiku wowote wa Ramadhwaan unaompitia bila kufanya ‘ibaadah ila kwa udhuru.
Hadiyth Kuhusu Ramadhwaan Na Swiyaam Na Mafunzo
20- Zakaatul-Fitwr Hikma Yake Kiwango Chake Na Kuwajibika Kwake
عَن ْابْنِ عُمَرَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: " فَرَضَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَكَاةَ الْفِطْرِ صَاعًا مِنْتَمْرٍ أَوْ صَاعًا مِنْ شَعِيرٍ عَلَى الْعَبْدِ وَالْحُرِّ وَالذَّكَرِ وَالأنْثَى وَالصَّغِيرِ وَالْكَبِيرِ مِنْ الْمُسْلِمِينَ". البخاري
Kutoka kwa bin 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhuma): "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameifanya Zakaatul-Fitwr ni fardhi kwa mtumwa na aliye huru, mwanamume na mwanamke, mdogo na mkubwa miongoni mwa Waislamu kwa kutoa swaa' moja ya tende kavu au swaa’ moja ya shayiri." [Al-Bukhaariy]
Mafunzo:
Kuwajibika kwa Zakaatul-Fitwr:
Hadiyth hiyo tukufu ni dalili kuwa Zakaatul-Fitwr ni fardhi kwa Waislamu. Na pia katika Hadiyth nyengine ifuatayo:
عنْ أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ رضى الله عنه قَالَ: "كُنَّا نُخْرِجُ فِي عَهْدِ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَوْمَ الْفِطْرِ صَاعًا مِنْ طَعَامٍ". وَقَالَ أَبُو سَعِيدٍ "وَكَانَ طَعَامَنَا الشَّعِيرُ وَالزَّبِيبُ وَالأَقِطُ وَالتَّمْرُ".
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) akisema: “Tulikuwa tukitoa zama za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Siku ya ‘Iydul-Fitwr pishi ya chakula.” Na Akasema Abuu Sa’iyd: “Na chakula chetu kilikuwa ni shayiri zabibu, jibini na tende”. [Al-Bukhaariy]
Zakaatul-Fitwr ni wajibu kwa kila Mwislamu mwenye chakula cha kutosha na ziada kwake yeye na wale wote ambao anawalisha kwa usiku wa kuamkia ‘Iyd na mchana wake. Zakaatul-Fitwr hii imewekwa kwa hikmah iliyoelezewa kwenye Hadiyth hii tukufu kuwa ni kitwaharisho kwa mfungaji Swawm kutokana na matelezo madogo madogo ambayo anaweza kuwa aliyafanya wakati wa Swawm yake, au makosa mengineyo ambayo pengine yalitia madoa kwenye Swawm yake kama kauli chafu, kukebehi na kadhalika. Zakaatul-Fitwr hii inasafisha madoa doa hayo na kukarabati popote pale palipoharibika katika Swawm ya mtu.
Ni wajibu kuwatolea watoto wadogo na wakubwa, mke, mtumishi na kila yule ambaye mtu anamkimu kimaisha. Ama mtoto ambaye bado hajazaliwa yumo tumboni mwa mama yake, basi hawajibiki kutolewa Zakaatul-Fitwr, lakini kama mtoto kazaliwa baada ya kuzama jua usiku wa mwisho wa Ramadhwaan basi inapendekezeka kumtolea kwa sababu Swahaba Mtukufu ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) alifanya hivyo japokuwa si fardhi.
Aina ya chakula:
Wengi katika ya ‘Ulamaa wanasema kuwa chakula kinachokusudiwa kwenye Hadiyth hii ni “burri” yaani ngano. Lakini ‘Ulamaa wengine wanaona kuwa chakula chochote kinacholiwa zaidi na wenyeji wa mji wowote vyovyote kiwavyo ikiwa ni ngano, mahindi, mtama na kadhalika basi chafaa kutolewa Zakaatul-Fitwr.
Lengo na hikma yake:
Hadiyth imetaja hikma yake.
عَن ابنِ عَبَّاسٍ رضي الله عنهما قَالَ: "فَرَضَ رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم زَكَاةَ الفِطرِ طُهرَةً لِلصَّائِمِ مِنَ اللَّغوِ وَالرَّفَثِ، وَطُعمَةً لِلمَسَاكِينِ، مَنْ أدَّاهَا قَبلَ الصَّلَاةِ فَهِيَ زَكَاةٌ مَقبُولَةٌ، وَمَن أدَّاهَا بَعدَ الصَّلَاةِ فَهِيَ صَدَقَةٌ مِنَ الصَّدَقَاتِ"
Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) akisema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amefaradhisha Zakaatul-Fitwr kwa ajili ya kumtwaharisha mfungaji (Swawm) kutokana na maneno yasiyolaikiana, na kauli au matendo machafu, na kwa ajili ya chakula kwa masikini. Mwenye kuitoa kabla ya Swalaah, basi hiyo ni Zakaa yenye kukubaliwa. Ama mwenye kuitoa baada ya Swalaah, basi hiyo ni swadaqah katika swadaqah nyinginezo.” [Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Abiy Daawuwd (1609), Swahiyh Ibn Maajah (1492), Swahiyh Al-Jaami’ (3570)]
Na pia hikmah nyingine ni kuwawezesha masikini kupata mlo katika siku hiyo ya furaha ambapo chakula kinakuwa ni sehemu muhimu ya kukamilisha furaha hiyo. Kuwapatia chakula, kunakuwa ni kinga kwao na sitara ya kunyoosha mikono ya ombaomba, na hivyo kuifanya furaha ienee kwa Waislam wote matajiri na masikini.
Chakula gani kutoa:
Zakatul-Fitwr ni kutoa chakula kinachopendwa zaidi na nchi nyingi za Kiislamu kama mchele na hususan kwenye nchi za ghuba. Hivyo hakuna ubaya kutoa mchele kama Zakaatul-Fitwr kuliko kutoa ngano ingawa pia inatumika sana lakini si kulinganisha na mchele. Lakini ikiwa mtu hakupata mchele, anaweza kutoa mtama, shayiri na kadhalika ikiwa vyakula hivyo vinatumika zaidi sehemu alipo.
Kiasi cha kutoa Zakaatul-Fitwr:
Ni kama ilivyotajwa katika Hadiyth zilizotangulia kwamba ni swaa' ya chakula.
swaa’: Ni kiasi cha chakula cha ujazo kamili wa viganja viwili vya mikono vya ukubwa wa wastani.. Hiyo ndio tafsiyr ya صاع kwa mujibu wa kamusi. Na ujazo huo ni sawa na takriban kilo mbili na nusu.
Wakati wa kutoa Zakaatul-Fitwr:
La wajibu jingine, ni kutoa Zakaatul-Fitwr kabla ya kwenda kuswali Swalaah ya ‘Iyd, na haijuzu kuichelewesha baada ya Swalaah, kwani itahesabiwa kuwa ni swadaqah ya kawaida, na si Zakaatul-Fitwr. Baadhi ya ‘Ulamaa wanasema kuwa inajuzu kuitoa kabla ya ‘Iyd kwa siku moja au mbili kwa kuwa Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa wakiitoa kabla ya ‘Iyd kwa siku moja au mbili.
Wanaopewa Zakaatul-Fitwr
Wanaostahiki kupewa Zakaatul-Fitwr ni masikini na mafukara, kwani hao ndio walengwa wakuu.
Je, Zakaatul-Fitwr inafaa kutolewa mali badala ya chakula?
Kwa mujibu wa Jamhuri ya ‘Ulamaa, haifai kutoa Zakaatul-Fitwr kwa thamani ya pesa, bali la wajibu ni kutoa chakula kama alivyoamuru Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambapo yeye mwenyewe alifanya hivyo na Maswahaba wake pia wakafanya hivyo. Mwenye kutoa thamani ya chakula, basi kaenda kinyume na alivyofanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Jamhuri ya ‘Ulamaa wanasema kuwa haijuzu kabisa kutoa fedha badala ya chakula. Kwa kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amefaradhisha kitolewe chakula na kuainisha aina ya vyakula hivyo, na Maswahaba wake walitoa pia vile vile chakula huku wakiwa pia na fedha. Na sisi bila shaka ni lazima tuwafuate.
Halafu utoaji Zakaatul-Fitwr wa chakula, kipimo chake kisha ainishwa cha pishi moja. Lakini kwa fedha kipimo hiki hakidhibitiki ingawa baadhi ya ‘Ulamaa wamesema kinaweza kwa thamani ya kilo mbili na nusu ya chakula kinachotolewa ambazo ni sawa na pishi moja.
Na mtu anaweza kusema: “Pesa zinamfaa zaidi masikini kwa kuwa anaweza kununulia kitu kingine chochote anachokihitajia kwa mapishi kama chumvi, mafuta na kadhalika.”
Lakini tunasema: “Kuna vyanzo vingine vya maduhuli ya pesa kwa masikini kama Zakaatul-Maal (Zakaah ya mali) swadaqah nyinginezo kiujumla, tunukio na kadhalika. Hivyo basi, haifai kutoa pesa kama Zakaatul-Fitwr kwa masikini, bali chakula kama alivyoamuru Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kulifanya hilo Maswahaba wake (Radhwiya Allaahu ‘anhum).