Talaka Tatu Zimepita Lakini Bado Tunatakana

 

SWALI:

Asalamu alaykum,

Napenda kwanza kwa kumshukuru Allaah kwa neema hii alotujaalia waislam kuwa na tovuti hii ya kiislam yenye faida nyingi ndani yake na napenda kuwashukuru waislam wote waliojitolea kwa kuimarisha na kuendeleza tovuti hii ya kiislam, inshallaah m.mungu atakupeni kila la kheir hapa duniani na kesho akhera ameen.

 

Napenda kuulizia kwamba mimi ni mwanamke nilieachwa talaka tatu sasa na hizo talaka zimetokea kwa bahati mbaya tu, kutokana na sisi bado ni watoto bado, hivyo hivi sasa bado kila mmoja anamtaka mwenziwe awe nae kuishi pamoja na talaka ndo zimeisha hivyo nifanye jee ili apate kunioa na kuishi nae pamoja ili tupate kulea watoto wetu wawili naomba majibu haraka.

  


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Twakushukuru sana kwa du’aa zako na tunamuomba Allaah Atutaqabalie sisi na wewe inshaAllaah.

 

Kwa inavyoonekana hatudhani kuwa kweli huyo mume anampenda mkewe kama ulivyoashiria katika swali lako hilo. Vipi atakuwa anampenda mtu kama ulivyosema kisha akawa hana subira isipokuwa kutoa talaka mpaka zimefika tatu huku akifahamu kuwa baada ya talaka ya tatu hamtaweza kuwa pamoja tena kama mume na mke. Hili ni jambo muhali mtu kumfanyia ampendaye mapenzi ya dhati.

 

Ifahamike kuwa mke anapopewa talaka ya tatu basi mume hawezi kumrejea tena mpaka aolewe na mume mwingine kama Alivyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala):

 

Hawi halali kwake baada ya talaka ya tatu mpaka aolewe na kumuingilia mume mwingine” (2: 230).

 

Huyo mume mwingine anafaa amuoe bila kushawishiwa, kisha amuingilie kwa kufanya naye tendo la ndoa. Ikiwa hawatafanya hivyo na yule mke, kisha akaachwa hatakuwa halali kwa mume wake wa kwanza.

 

Tufahamu kuwa haifai kumpatia mume mwingine pesa ile aende amuoe mtalaka wake kwa ajili ya kumhalalishia. Hii ni ndoa iliyo batili, kwa kauli ya Ibn Mas‘uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyesema:

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemlaani mhalalishaji na mhalalishiwa” (at-Tirmidhiy, Abu Daawuud, Ibn Maajah na Ahmad).

 

Hivyo ndugu yetu huna njia nyingine ya kurudiana na mumeo mpaka wewe uolewe na mume mwingine kisha upewe talaka baada ya kufanya jimai. Na wala hairuhusiwi mume wako apange na au kukuchagulia mume wa kukuoa wewe, au apange uolewe na usiingiliwe kisha upewe talaka na yeye akuoe tena.  Mambo haya huwa yanatokea na hufanywa na watu wenye ujahili wa Dini ya, na wasio na khofu na Mola wao.

 

Mas-ala haya yanatokea katika jamii yetu kesi mbali mbali tumeshazisikia. Kutoa talaka mara tatu imekuwa ni jambo jepesi sana na la mchezo na matokeo yake ni hali kama hii mke na mume kutaka kurudiana. Kisha mke na mume wanadharau  sheria za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala). Itambulike kwamba  pindi mtakaporudiana baada ya talaka hizo tatu na bila mke kuolewa tena na mume mwingine, basi itakuwa mnaishi kiharamu kwani nyinyi sio mke na mume tena, hivyo maingiliano yenu yatakuwa ni zinaa na watoto mtakaozaa watakuwa ni watoto wa tendo la haraam na msio na haki nao kisheria kama kurithi n.k. Kwa hiyo lazima mzingaite haya na mkhofu adhabu kali  za Mola Mtukufu.  

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate manuaa zaidi:

Talaka Ziko Aina Ngapi Na Wakati Gani Zinasihi?

Amemtamkia Talaka Zaidi Ya Mara Tano Nyakati Mbali Mbali

Nimempa Talaka Mke Wa Mwanzo Lakini Bado Nampenda

Vipi Nihesabu Eda Yangu Ya Talaka

Ametamka Talaka Kwa Hamaki Kuwa Pindi Mkewe Akitoka Nje Ya Ndoa Itakuwa Talaka Yake – Anaweza Kurudisha Kauli Yake?

Talaka Ya Mara Tatu Inasihi?

Mas-ala Mbali Mbali Kuhusu Talaka

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Akupatie mume mwingine mwenye kheri nawe na mwenye Dini na maadili mema na mwenye mapenzi ya dhati inshaAllaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share