Tukumbushane
Imeandaliwa Na 'Abdullaah Mu'aawiyah (Abu Baasim)
Alhidaaya.com
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
01: Khatima Mbaya:
Madhambi ni daraja la kukupeleka kwenye mwisho mbaya wakati wa kufa, kwa kuwa mwanadamu anakufa kwa mujibu wa alivyoishi. Hivyo basi, anayetaka kufa akiwa kwenye sijdah, basi akithirishe kusujudu kwa kuswali Swalah za Faradhi na za Sunnah. Na anayetaka kufa hali ya kuwa yuko kwenye swawm, basi akithirishe sana kufunga.
Lakini kiufupi, khatima njema ni mtu kufa akiwa na tawhiyd safi bila kuwa na chembe ya shirki katika moyo wake vyovyote afavyo hata akifia barabarani. Si lazima afie msikitini, au ameshika Msahafu na kadhalika. Rasuli Mbora wa viumbe alifia kitandani.
Na yeyote mnayemwona anafia kwenye maasia, basi jueni huyo alipetuka mipaka dhidi ya nafsi yake katika maisha yake, na kwa sababu hiyo akanyimwa tawfiyq ya kufa kifo chema.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
02: Mali Ni Neema:
Mali ni neema. Kwa nini? Kwa sababu Allaah ‘Azza wa Jalla Amekupa mali uliyonayo ili ununulie Pepo.
"إِنَّ اللَّـهَ اشْتَرَىٰ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُم بِأَنَّ لَهُمُ الْجَنَّةَ "
“Hakika Allaah Amenunua kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwamba watapata Jannah”. [At-Tawbah: (111)].
‘Uthmaan bin ‘Affaan alifahamu maana hii akanunua Jannah mara mbili. Mara ya kwanza alipomsikia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
"مَن جَهَّز جَيشَ العُسرةِ فلَه الجَنَّةُ"
“Atakayeliandaa jeshi la Al’Usrah (kwa wanyama na zana) basi ataipata Pepo”. [Swahiyh Al-Bukhaariy]
Hivi ni Vita vya Tabuk, na jeshi limeitwa Al-‘Usrah kutokana na hali ngumu na ya dhiki iliyokuwepo wakati huo. Hapo ‘Uthmaan akatoa mali yake yote.
Na mara ya pili ni pale alipomsikia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
"مَن حَفَر رُومةَ فَلَهُ الجَنَّةُ"
“Atakayechimba kisima cha maji, basi ataipata Jannah”. [Swahiyh Al-Bukhaariy]
‘Uthmaan akanunua kisima cha maji kilichokuwa kinamilikiwa na mtu ambaye alikuwa akiuza maji yake. Na hapa ni wakati Muhaajiruna walipokuwa wanahamia Madiynah ambapo mahitaji ya maji yangeongezeka. Akakifanya kisima hicho ni waqf kwa ajili ya Allaah.
Hivyo chochote hata kidogo utoacho kwa mujibu wa hali yako basi usikidharau. Allaah ndiye ajuaye hali yako na nia yako. Na haya ndiyo matumizi chanya ya utumiaji wa neema ya mali kwa mambo yote yenye kumridhisha Allaah.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
03: Mali Ni Niqama:
Mali mbali na kuwa ni neema toka kwa Allaah, pia inakuwa ni naqama. Inaweza kuwa ndio sababu kubwa ya kumweka mbali mtu na Allaah na kuwa kitendakazi cha nguvu cha kumsahaulisha na aakhirah kama hali ya mambo tunavyoiona hivi leo. Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam anasema:
"إِنَّ لِكُلِّ أُمَّةٍ فِتْنَةٌ وَإِنَّ فِتْنَةَ أُمَّتِي الْمَالُ"
“Hakika kila umma una mtihani wake, na hakika mtihani wa umma wangu ni mali”.
Uchu na ulafi wa mwanadamu kwa mali hauna mipaka hata akiwa na mabonde mawili ya dhahabu angelitamani awe na la tatu. Uchu huu mbaya unamsukuma kutafuta mali kwa njia yoyote ile iwayo hata ya haramu. Na ikiwa chumo litakuwa la haramu, basi tabaka za nyama za haramu zitaendelea kumea kwenye mwili, na zikifikia kumea kikamilifu, basi zitasubiriwa na moto wa Jahannam uzisafishe. Rasuli anasema:
"لَا يَدْخُلُ الْجَنَّةَ لَحْمٌ نَبَتَ مِنْ سُحْتٍ ، النَّارُ أَوْلَى بِهِ"
“Haiingii Peponi nyama iliyomea kutokana na haramu, na Moto unaistahikia zaidi”. [Imesimuliwa na Ahmad toka kwa Jaabir. Isnadi yake ni Jayyid]
Askari wa usalama barabarani wanaokusanya kila siku hongo za mamilioni toka kwa madereva, watumishi wa serikali na wengineo wengi walio kwenye nafasi zao, au waporaji wa mali za umma, hao wote miili yao inanona kwa pesa ya haramu, na wajue kuwa moto wa Jahannam utazipaparikia zaidi nyama zao. Ni furaha ya muda mfupi tu waliyonayo, lakini majuto ni marefu yasiyo na ukomo. Usiombee kuwa katika nafasi hizo, au mtoto wako, au Muislamu mwenzako.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
04: Mtoto Ni Neema:
Ni neema pale utakapomlea vyema. Kila jema atakalolifanya, basi pia linawekwa kwenye mizani za wazazi wake wawili waliomlea na kumfundisha au yeyote aliyesimamia ulezi wake. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia:
"إنَّ الرَّجلَ لتُرفَعُ درجتُه في الجنةِ فيقولُ : أنَّى هذا ؟ فيقالُ : باستغفارِ ولدِك لكَ"
“Hakika mtu atakuta daraja zake zimenyanyuliwa Peponi aseme: Zimekujaje hizi? Ataambiwa: Ni kutokana na duaa za wanao za kukuombea maghfirah”. [Hadiyth Hasan. Swahiyh Ibn Maajah]
Mtoto ni rasilimali nzuri. Iwekeze vyema ikufae duniani na aakhirah. Usijali gharama unazotoa kwa ajili ya hilo. Zote zitarudi na ziada teletele.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
05: Ulimi Ni Neema:
Ulimi ni kiungo pekee katika mwili wa mwanadamu ambacho hakichoki vyovyote kitakavyofanya kazi. Na hii ni moja kati ya Fadhila za Allaah kwetu ili tuweze kuvuna zaidi matunda ya Peponi kwa adhkaar, kusoma Qur-aan na kunena maneno mema, maneno ya haki na kadhalika. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) anasema:
"مَنْ قَالَ (سُبْحَانَ اللَّهِ الْعَظِيمِ وَبِحَمْدِهِ) غُرِسَتْ لَهُ نَخْلَةٌ فِي الْجَنَّةِ"
“Mwenye kusema: Subhaana Allaah Al-‘Adhwiym wa bihamdihi, atapandiwa mtende Peponi”. [Swahiyh At-Targhiyb. Swahiyh Lighayrih]
Ni vidole vingapi vitaumwa kwa majuto kwa mitende iliyopotezwa na watu Peponi kwa kushindwa tu kutamka maneno machache kama hayo na mengineyo mengi ya kheri kwa kushughulishwa na mambo yasiyo na faida yoyote?! Ni urahisi ulioje wa kuyatamka maneno kama haya! Hayana wakati maalum, wala sehemu maalum, wala nyenzo maalum wala masharti maalum. Ni kwa ulimi wako tu ambao hauhisi tabu yoyote vyovyote utakavyounenesha.
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema tena:
"ليسَ يتحسَّرُ أَهلُ الجنَّةِ على شيءٍ إلَّا على ساعَةٍ مرَّت بِهِم لم يذكُروا اللَّهَ عزَّ وجلَّ فيها"
“Hakuna kitu ambacho watu wa Peponi watakijutia zaidi kuliko saa moja iliyowapitia bila ya kumdhukuru Allaah ‘Azza wa Jalla ndani yake”. [Hadiyth Hasan. Al-Jaami’u As Swaghiyr]
Hawa ni watu wa Peponi. Je wa motoni majuto yao yatakuwa vipi?! Tuzindukane na wakati wetu.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
06: Ulimi Ni Maafa:
Ulimi unaweza kuwa ni maafa kwa mwanadamu kama ambavyo unaweza pia kuwa ni sababu ya kuingia Motoni kutokana na neno moja tu au tamshi moja tu. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِنَّ الرَّجُلَ لَيَتَكَلَّمُ بِالْكَلِمَةِ لاَ يَرَى بِهَا بَأْسًا يَهْوِي بِهَا سَبْعِينَ خَرِيفًا فِي النَّارِ "
“Kwa hakika mtu anaweza kutamka neno ambalo haoni madhara yoyote kwalo akaja kuporomoka nalo motoni majira 70 ya vuli (miaka 70)”. [Hadiyth Hasan Ghariyb. Imesimuliwa na Abu Hurayrah]
Linaweza kuwa neno litakalochemsha ghadhabu za Allaah na mtu akaliona halina uzito wowote. Uso wa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ulitaghayuri kwa hasira wakati Bibi ‘Aaishah alipomtia kasoro Bi Swafiyyah kwa neno linalomaanisha kuwa ni mfupi. Rasuli akamwahi hapo hapo na kumwambia:
"لقدْ قلتِ كَلِمَةً لَوْ مُزِجَتْ بماءِ البحْرِ لَمَزَجَتْهُ"
“Hakika umetamka neno ambalo lau lingechanganywa na maji ya bahari basi lingeyachafua yote (kutokana na ubaya wake)”. [Swahiyh Al-Jaami’u. Imekharijiwa na Abu Daawuwd]
Tutahadhari sana na ndimi zetu. Allaah Atusamehe madhambi yetu ya ulimi na Atujaalie tuyaepuke.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
07: Jicho Ni Neema:
Allaah Ameliumba jicho ili liwe ni moja ya macho mawili aliyoyakusudia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika neno lake:
"عَينانِ لا تمسُّهُمَا النَّارُ: عَينٌ بَكَتْ مِنْ خَشْيَةِ اللَّهِ، وعَينٌ بَاتَتْ تحرُسُ فيْ سِبِيْلِ اللَّهِ
“Macho mawili moto hautoyagusa: Jicho lililotokwa na machozi kwa kumkhofu Allaah, na jicho lililokesha usiku likichunga katika Njia ya Allaah”.
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaposema: Macho mawili hayaguswi na moto”, anamaanisha aina mbili za watu ambao hawataingia motoni. Amewaelezea kwa jicho ili kuashiria kwamba viungo vingine vya mwili vinastahiki zaidi visiadhibiwe kwa moto.
Ama jicho linalolia kwa kumkhofu Allaah, hili ni lile la mtu anayetokwa na machozi kwa sababu ya khofu na matarajio kwa Allaah ‘Azza wa Jalla wakati anapotubia, au anapomdhukuru Allaah, au anapofanya jambo jema la utiifu kwa Allaah. Na hii ni Rahma jumla kwa kila Muislamu anayesifika kwa sifa hii.
Ama jicho linalokesha katika Njia ya Allaah, hili ni lile linalowalinda Waislamu wasije kushambuliwa ghafla na maadui katika Vita vya kulinyanyua juu Neno la Allaah, au linalokesha kwa ajili ya Hajji, au kutafuta ilmu, au kusaidia wanyonge, au kuwatetea wadhulumiwa na wanyonge na mfano wa hayo katika ibada zote zinazohitajia juhudi na uzito katika kuzifanikisha.
Allaah Ta’aalaa Ameliumba jicho pia ili mtu aweze kutafakuri kwa anayoyaona katika Uumbaji wa Allaah na kuzunguka nalo katika Ufalme Mkubwa wa Allaah ili iymaan ya Muislamu izidi kukua na yaqini izidi kuimarika hadi kujikuta akisema mwenyewe:
"رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَذا بَاطِلاً سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ"
“Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu Ni Wako, basi Tukinge na adhabu ya moto”.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
08: Jicho Ni Maafa:
Jicho ni maafa wakati litakapoachiliwa kuangalia kila lile la haramu, na hapo linakuwa linafungua mlango katika milango ya Jahannam.
Ibn Al-Qayyim amesema: “Kuangalia ni mfano wa mbegu iliyotupwa kwenye udongo. Kama utaiacha bila kuifanyia chochote, basi itakauka. Na kama utainyesheleza, basi itamea. Na ndivyo hivyo kutizama ya haramu”.
Yaani ukiendekeza, basi unazidi kukoleza madhambi, na hatima inakuwa ni mbaya zaidi.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
09: Wakati:
Wakati ni neema. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatueleza:
"نِعْمَتانِ مَغْبُونٌ فِيهِما كَثِيرٌ مِنَ النَّاسِ: الصِّحَّةُ والفَراغُ"
“Neema mbili watu wengi wamekula hasara ndani yake: afya na faragha”. [Al-Bukhaariy]
Watu wengi wanapoteza afya na wakati wao wa faragha bila faida. Hawaitumii neema hiyo kwa yenye kuwafaa, wala yenye kuwakurubisha kwa Allaah, na wala yenye kuwafaa wao na wengineo kwenye dunia yao. Watu hawa wanakuwa ni wenye kujipunja wenyewe ndani ya neema hizi na kujidhulumu, na hii ni hasara kubwa.
Hadiyth hii inatuashira kwamba mtu hawezi kuwa na nafasi nzuri ya kufanya matendo mema ila atakapokuwa ana cha kumtosheleza mahitaji yake, yupo kwenye amani, na ana afya njema. Anaweza kuwa anajitosheleza lakini mgonjwa, au ana afya nzuri lakini hana cha kutosheleza mahitaji yake ya kimsingi, au kuna mengi ya kumtatiza kama kukosekana usalama, amani na kadhalika. Katika hali hii, anakuwa ni mwenye kushughulishwa na matibabu au kusaka tonge, na akili na hima yake yote inajikita katika kujinasua na hali aliyonayo, hivyo muda wa kuzingatia ibada njema unakuwa haupo.
Lakini pia kuna mtu anaweza kuwa anamiliki cha kumtosha vizuri, afya njema na usalama, pamoja na hivyo asiutumie vyema wakati wake wala afya yake. Huyu ndiye mkusudiwa wa Hadiyth hii. Atakuwa anajipunja na kujihasiri mwenyewe kwa kupoteza nafasi hiyo bure. Wakati wa kufa atakapoona hasara ya hilo, au Siku ya Qiyaamah, atajuta sana atakapoona daftari lake limesajili muda wake mwingi kuwa aliutumia kwenda viwanja vya mipira, kufuatilia ligi kuu za ndani na nje na kadhalika, wakati madaftari ya wengine yamejaa adhkaar, visomo vya Qur-aan, mahudhurio ya mihadhara ya kidini na mengineyo nufaishi na kadhalika. Muislamu asisubiri majuto hayo, bali aharakie na kuchukua hatua ya haraka ya kuupanga wakati wake vizuri katika mambo ya kheri na ya kumfaa yeye mbele ya safari ndefu na nzito huko Aakhirah.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
10: Thawabu Kubwa Kwa Huduma Ndogo:
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"مَن مَنحَ منِيحةَ لبنٍ أو وَرِقٍ أو هَدَى زِقاقًا كانَ له مثلُ عتقِ رقَبَةٍ"
“Mwenye kutoa mnyama wa kukamwa maziwa, au mkopo wa fedha, au akamwelekeza mtu njia au sehemu, basi atapata (thawabu za) mfano wa kumwacha huru mtumwa”. [Imesimuliwa na Ahmad, Al-Bukhaariy na At-Tirmidhiy]
Kuwasaidia watu na kuwapa, ni katika sifa njema ambazo Muislamu anatakikana ajipambe nazo na kujipambanua kwazo na wengineo. Na hii ni kutokana na malipo makubwa yaliyomo ndani yake.
Kadhalika, kumwelekeza mtu njia au sehemu anayotaka kwenda, thawabu zake ndio kama hizo. Jambo hilo tunaliona dogo, lakini mbele ya Allaah ni kubwa.
Hivyo, tusidharau jema lolote hata kama kwa akili zetu tutaliona ni dogo vipi.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
11: Nabiy Ibraahiym Atakataliwa Uombezi Wake Kwa Baba Yake Siku Ya Qiyaamah:
Abu Hurayrah: Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) atakutana na baba yake Aazar Siku ya Qiyaamah uso wake ukiwa umejaa vumbi umesawijika. Ibraahiym atamwambia: Je sikukwambia kwamba usikatae maneno yangu na usia wangu?! Baba yake atamjibu: Leo mimi sitokuasi. Ibraahiym atasema: Ee Rabbi wangu! Hakika Wewe Umeniahidi kuwa Hutonikhizi Siku watu watakapofufuliwa. Basi ni khizaya iliyoje baba yangu kuwa mbali kabisa (na Rahmah za Allaah)?! Allaah Ta’aalaa Atamwambia: Hakika Mimi Nimepiga marufuku Pepo kwa makafiri. Kisha patasemwa: Ee Ibraahiym! Angalia chini ya miguu yako, naye ataangalia. Hapo atashtukizwa kumwona fisi aliyetapakaa damu. Fisi atakamatwa miguu na mikono yake atupwe motoni”. [Swahiyh Al-Bukhaariy. Imesimuliwa na Abu Hurayrah]
Allaah Mtukufu Ameiharamisha Pepo kwa makafiri. Yeyote anayekufa kafiri, basi moto wa milele unamsubiri. Hii ni Ahadi ya Allaah, hakuna uombezi utakaomfaa Siku hiyo wala nasaba. Na hapa tunaona namna ambavyo Ibraahiym anajaribu kumwomba Allaah Asimkhizi kama Alivyomwahidi ili Amsamehe baba yake na Amwingize Peponi. Na kwa kuwa baba huyo alikufa kafiri baada ya kukataa hoja zote za wazi alizoletewa na mwanawe juu ya ujinga wa kuabudu masanamu yasiyosikia wala kuona, wala kunufaisha wala kudhuru, na juu ya msingi huo wa ukafiri, Atamkatalia kuingia Peponi. Na badala yake Atamgeuza kuwa fisi aliyetapakaa damu na kuwa katika picha ya kukirihisha na atupwe motoni ili Ibraahiym asiwe na hamu naye tena na ajivue naye kabisa.
Tunajifunza hapa kwamba:
1-
Mtoto Muislamu hatoweza kumsaidia mzazi wake kafiri Siku ya Qiyaamah hata kama mtoto ni Nabiy.
2-
Tujitahidi kuulinda Uislamu wetu kwa nguvu zote ili tufe nao. Kuulinda ni kujitahidi kuwajibika na yote Aliyoyaamuru Allaah, kujiepusha na yote Aliyoyakataza na kumcha Allaah wakati wote na mahala pote.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
12: Mwanaume Usivae Hariri, Utaikosa Ya Peponi:
Kujinyima na kujizuia na makatazo leo hapa duniani, ni jambo jepesi zaidi kuliko kesho Aakhirah. Nadhani ndugu yangu Muislamu umeisikia Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo:
"مَنْ لَبِسَ الْحَرِيرَ فِي الدُّنْيَا لَمْ يَلْبَسْهُ فِي الْآخِرَةِ"
“Mwenye kuvaa hariri duniani, hatoivaa akhera”.
Na ‘Abdullaah bin Az-Zubayr akaongezea kauli yake: “Na ambaye hatoivaa Aakhirah, basi ina maana haingii Peponi”.
Hivyo basi mwenye kunywa pombe ya dunia, hatokunywa ya Peponi, na mwenye kuwaangalia kwa matamanio wanawake basi kesho atanyimwa kuwaangalia wanawake wazuri wa Peponi wenye macho makubwa Mahuwr Al Ayn, na mwenye kusikiliza miziki, hatosikiliza ya huko.
Zuio hili kwa mujibu wa maneno ya ‘Abdullah bin Az-Zubayr, linamaanisha kuwa mtu haingii Peponi akayapata hayo kutokana na kujiachilia nayo hapa duniani. Na huu ni msiba mkubwa. Na hii pia inaingia ndani ya wigo wa kudharau madhambi na matokeo yake.
Lakini ‘Ulamaa wanasema kuwa ataingia Peponi kwa mujibu wa mizani yake ya matendo, lakini humo hatopata tembo la huko au kuvaa Hariri. La muhimu mtu ajiepushe na maharamisho yote kiasi awezavyo.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
13: Allaah Hufurahika Kwa Toba Yako Lakini Shetani Hununa:
Ndugu Muislamu! Jua kwamba unapotubia kikweli, basi Allaah Anafurahi, Malaika hukufurahikia na shaytwani hughadhibika mno. Isitoshe, daftari lako huwa safi bila tone ya dhambi, daraja yako hupandishwa na hadhi yako huwekwa juu. Lakini pia baraka hukuteremkia, matatizo uliyonayo huondoka, na moyo wako hupata utulivu. Hayo yote ni kwa ajili tu ya toba yako nailhali wewe ulikuwa mkosa. Na wewe ni nani hata Allaah Afurahi kwa toba yako! Ni neema iliyoje hiyo! Na kwa ajili hiyo, asiyetubu kwa Allaah, basi huyo ni katika madhalimu. Allaah Anasema:
"وَمَن لَّمْ يَتُبْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ"
“Na yeyote asiyetubu, basi hao ndio madhalimu”. [Al-Hujuraat: 11]
Mizani yako itawekwa mbele ya macho yako Siku ya Qiyaamah. Mema yako yatawekwa kwenye mkono mmoja wa mizani na mabaya kwenye mkono mwingine. Hakuna njia ya kuufanya mkono wa mema kuwa mzito isipokuwa kwa toba njema ya kufuta mabaya hayo. Usikawie hata kidogo kuacha mabaya hayo kubaki kwenye daftari lako.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
14: Faida Ya Hofu Na Huzuni Hapa Duniani:
Hofu ni hisia ya kuogopa jambo lijalo ambalo bado halijatuka, na huzuni ni hisia itokanayo na jambo lililopita. Mwanadamu hapa duniani anahofia riziki yake, anajihofia mwenyewe, anahofia watu wake, kudhulumiwa, kunyanyaswa, mauti, kifo, umasikini na kadhalika. Pamoja na haya yote, anaweza kuhuzunika kwa kufiwa na mwanaye, au kukosa ajira, kukosa mtoto na misiba mingineyo ya maisha. Haya yote ni katika misukosuko ya maisha ya hapa duniani. Na misukosuko hii haipiti bure, bali inatupandishia daraja, na inatububujishia Rahma na Baraka kochokocho toka kwa Allaah. Na hii ni kwa muumini mwenye subira tu.
Na kutokana na hofu na huzuni tunazozipata hapa duniani, tutakapoingia Peponi, hapo ndipo tutakapohisi ladha halisi ya amani na furaha ya huko. Mtu hawezi kuhisi ladha ya shibe bila kupata adha ya njaa kali. Hatuwezi kuhisi ladha ya amani na usalama bila kuonja makali ya ukosefu wa amani.
Na huko pia, hakuna mitihani wala misukosuko kwa Waumini wema, bali ni mabubujiko ya Rahma na Radhi za Allaah ambazo zitaondosha kabisa hofu kubwa itakayotanda Siku ya Qiyaamah.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
15: Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Nafsi Yako?
Yaonee haya masikio yako, macho yako na ngozi yako. Viungo hivi Allaah Amevifanya kuwa kama ni majasusi wanaokuona popote unapokwenda, na ndivyo vitakavyotoa ushahidi dhidi yako mbele ya Allaah na mbele ya kizingiti cha Jahannam.
Allaah Anasema:
"حَتَّىٰ إِذَا مَا جَاءُوهَا شَهِدَ عَلَيْهِمْ سَمْعُهُمْ وَأَبْصَارُهُمْ وَجُلُودُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ"
“Mpaka watakapoufikia, yatashuhudia dhidi yao masikio yao, na macho yao, na ngozi zao kwa yale waliyokuwa wakiyatenda”. [Fusswilat: 20]
Viungo vyako vinaona na kusajili kila tendo lako, na Siku hiyo vitatoa ushahidi dhidi yako kwa kila dogo na kubwa unalolifanya sasa. Kujua hili ni chachu ya kukufanya ujiepushe na makatazo. Hivyo basi, jionee haya mwenyewe kwa nafsi yako kumwasi Allaah, kwani viungo vyako mwenyewe vinakuona, Allaah Anakuona, na Malaika Wake wanasajili kila kitu.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
16: Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Viumbe?
Viumbe vyote vinamsabbih Allaah na wala havichoki; wanyama, mimea, majini, Malaika, bahari, milima, mabonde na kadhalika. Allaah Anatuambia:
"وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ وَلَـٰكِن لَّا تَفْقَهُونَ تَسْبِيحَهُمْ"
“Na hakuna kitu chochote (kile kiwacho) isipokuwa kinasabihi kwa Himidi Zake, lakini hamzifahamu tasbiyh zao”. [Al-Israa 44]
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam anatuambia:
"إنَّ اللهَ أذِنَ لي أن أُحدِّثَ عن ديكٍ قد مَرَقَتْ رجلاه الأرضَ، وعُنُقُه مَثْنِيَّةٌ تحت العرشِ، وهو يقول: سبحانك ما أعظَمك! فيردُّ عليه: لا يعلم ذلك من حلفَ بي كاذبًا "
“Hakika Allaah Amenipa idhini nimzungumzie jogoo ambaye miguu yake miwili imepenya kuingia ardhini, na shingo yake imeinamishwa chini ya ‘Arshi, naye anasema: Umetakasika. Ni Uadhwama na Ukubwa ulioje Wako (ee Allaah)! Allaah Humjibu: Halijui hilo mwenye kuapa kwa uongo kwa Jina Langu”. [Swahiyh Al-Jaamiu. Al-Albaaniy: Ni Swahiyh]
Huyo ni jogoo wa ukubwa huo anayemsabbih Allaah. Vipi ukubwa wa Allaah Aliyemuumba! Hilo watu wangelijua, basi wasingelithubutu kuapa kwa uongo na kuchezea Jina la Allaah Mwenye ukubwa na uadhwama usioweza kufikirika. Jogoo huyu baadhi ya Maulamaa wanasema ni katika wale Malaika wanane wabebao ‘Arshi ya Allaah, na yuko katika umbile la jogoo. Na hao Malaika wabebaji ‘Arshi, kutoka kwenye njewe ya sikio hadi bega lake ni safari ya mwendo wa miaka 700 kwa ndege kupiga mbawa zake. Jibril ‘alayhis salaam ana mbawa 600 zinazofunika mashariki yote ya uso wa dunia, naye pia pamoja na hao Malaika na wengineo, hachoki kumsabbih Allaah nyakati zote. Kwa picha hii, tunapata kujua fadhla kubwa ya kumsabbih Allaah.
Kwa nini iwe tasbiyh pekee inayotamkwa na viumbe vyote badala ya adhkaar nyingine? Hakika iko siri kubwa ndani yake.
Ikiwa viumbe hivyo vikubwa vinamsabbih Allaah bila kuchoka, mnyama unayempanda, nguo unazozivaa, kiti unachokalia, na hata udongo unaoukanyaga, au wadudu unaowadharau na kuwatweza kama nzi na kadhalika, je, huoni haya wewe kuwa nje ya duara la wanaomsabbih Allaah na kushindwa na hata viumbe wadogo kabisa!
Jitafakuri na jiweke sawa.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
17: Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Malaika?
Waonee haya Malaika wawili wanaoandamana nawe nyakati zote kwa ajili ya kuandika matendo yako yote madogo au makubwa; mema au mabaya. Matendo yako ya mchana hupandishwa kabla ya kuingia usiku, na ya usiku kabla ya kuingia siku mpya. Je, unaridhia rekodi ya matendo yako yanayopandishwa kuwa ni dhambi tupu? Hujisikii vibaya?!
Hebu jaribu kufanya kama unawaona wanavyosajili matendo yako! Fanya kama unamwona Malaika wa kuumeni anavyoandika matendo yako mema, na wa kushotoni anavyoandika kila dhambi lako. Jaribu kuwaza kwa kina, utakuwa unajisikiaje ukiona mema yako yanasajiliwa dogo lake na kubwa lake hata la uzito wa sisimizi bila ya Malaika huyo kuchelewa hata sekunde moja? Nadhani ukiikita picha hiyo kiuhalisia, hutozembea hata kidogo kujiongezea mema nyakati zote. Hali kadhalika kwa mabaya, utajikuta ukichukua hadhari kubwa kwa kila tendo unalotaka kulifanya au neno unalotaka kulitamka. Lakini huo ndio ukweli na uhalisia wa mambo.
Kwa dereva wa gari aliyepigwa tochi na askari wa usalama na kuletewa sms ya kulipa faini, huyu faini hii itamtesa sana kabla ya kulipa na hata baada ya kulipa. Hawezi kuisahau! Ni kama kidonda. Sasa hali ikoje kwa madhambi tunayoyachuma kila wakati huku tukisahau kabisa kama yanarekodiwa hapo kwa papo na kuhifadhiwa, na tutakuja kuyaona siku ya hisabu? Haya pia yatatutesa sana tutakaposimama mbele ya Allaah kwa ajili ya hisabu hiyo, isipokuwa kama tutatubia yakafutwa na kuondoshwa.
Allaah Anatuambia:
"وَوُضِعَ الْكِتَابُ فَتَرَى الْمُجْرِمِينَ مُشْفِقِينَ مِمَّا فِيهِ وَيَقُولُونَ يَا وَيْلَتَنَا مَالِ هَـٰذَا الْكِتَابِ لَا يُغَادِرُ صَغِيرَةً وَلَا كَبِيرَةً إِلَّا أَحْصَاهَا ۚ وَوَجَدُوا مَا عَمِلُوا حَاضِرًا ۗ وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا"
“Na kitawekwa Kitabu, basi utaona wakhalifu ni wenye khofu kwa yale yaliyomo ndani yake; na watasema: Ole wetu! Kitabu hiki kina nini? Hakiachi dogo wala kubwa isipokuwa kimerekodi hesabuni. Na watakuta yale waliyoyatenda yamehudhuria hapo. Na Rabb wako Hamdhulumu yeyote”. [Al-Kahf: 49]
Piga hesabu sahihi ndugu yangu kabla ya kufanya tendo lolote, na kabla ya kutamka lolote. Kama ni la kheri, basi lifanye, na kama ni la shari, basi achana nalo. Inatosha tu kujua kwamba uko na Malaika hao wawili wanakuona na kusajili, Allaah Anakuona vizuri tu, na viungo vyako vinakuona na hata ardhi pia. Jisikie haya ufaulu duniani na aakhirah.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
18: Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Mtu Mwema Katika Jamaa Zako?
Abu Sa’iyd Al-Azdiy alimwambia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) niusie. Rasuli akamwambia:
"أُوصِيكَ أَنْ تَسْتَحِيَ مِنَ اللَّهِ عَزَّ وَجَلَّ كَمَا تَسْتَحِي مِنَ الرَّجُلِ الصَّالِحِ"
“Ninakuusia umwonee haya Allaah ‘Azza wa Jalla kama unavyomwonea haya mtu mwema”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika As Swahiyhah 741]
Ndugu yangu Muislamu!
Hebu chukulia kwamba mtu mwema katika jamaa zako ameshukia nyumbani kwako kama mgeni wako, kisha akakuomba uswali naye pamoja hapo nyumbani. Je, hali yako itakuwaje ikiwa wewe huswali?! Au, acha hilo, akakutaka msome pamoja Qur-aan hali ya kuwa Msahafu wako umejaa vumbi hujaugusa tena tokea Ramadhani iliyopita! Au akakutaka umwonyeshe Msikiti wa karibu ilhali wewe daima umejitupa kwenye kochi lako, unasikia adhana na wala huendi kuswali na pengine hata Msikiti hujui ulipo. Au akataka kuswali hapo nyumbani akakutaka umwelekeze Qiblah nawe hujui kilipo! Fikiria hali yako itakuwaje au jibisho lako?! Ni fedheha tupu!!
Bila shaka katika hali hii, kwa kumwonea haya mtu huyu, kuchunga hisia zake na wewe mwenyewe kujisitiri asikujue tabia yako hiyo, kwa kutahayari, utajikuta unaswali naye hivyo hivyo. Na hapa inaingia shirki ndogo ya riyaa, na wewe mwenyewe unakuwa umejiingiza humo kwa mikono yako miwili. Na hii pia ni katika sifa za wanafiki Allaah Atulinde nayo.
Ikiwa kwa binadamu huyu unalazimika kufanya hivyo, basi iko wapi hisia yako ya haya kwa Allaah Anayejua mambo yako yote na Anakuona unavyopuuza Maamrisho Yake?!
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
19: Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Allaah ‘Azza Wa Jalla?
Inakutosha kumwogopa na kumwonea haya Allaah ukijilinganisha wewe na Ufalme na Uadhwama Wake. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
- "ما السَّماوات السّبع في الكُرسيِّ إلَّا كحلقةٍ ملقاةٍ بأرضٍ فلاةٍ ، وفضلُ العرشِ على الكُرسيِّ كفضلِ تلك الفلاةِ على تلك الحلقةِ"
“Mbingu saba kulinganisha na Kursiy si chochote isipokuwa ni kama mfano wa kijipete mviringo kilichotupwa kwenye ardhi ya jangwa kubwa, na ukubwa wa Arshi kulinganisha na Kursiy ni kama ukubwa wa jangwa hilo kulinganisha na kijipete hicho”. [Hadiyth Swahiyh Marfuw. Ibn Hibaan na Ibn Abiy Shaybah].
Sasa Allaah ‘Azza wa Jallaa Aliye Juu ya ‘Arshi hiyo Ambayo Ameielezea kama ni:
الْعَرْشِ الْكَرِيمِ
Kama Alivyosema:
"فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ"
“Basi Ametukuka Allaah kwa ‘Uluwa, Mfalme wa haki. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Rabb wa ‘Arsh Kariym”. [Al-Muuminuwn: 116]
Na:
الْعَرْشِ الْعَظِيمِ
Kama Alivyosema:
"قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ"
“Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Nani Rabb wa mbingu saba, na Rabb wa ‘Arsh ‘Adhimu?” [Al-Muuminuwn: 86]….isitoshe Yeye Ndiye Aliyekuumba, Anakuruzuku, Anakupa uhai, na Anajua nyenendo zako zote, je huoni kwamba unamvunjia hishma kwa maasia yako pamoja na Uadhwama Wake huo?
Na kwa nini unajivuna kwa maasia? Jeuri hiyo unaitoa wapi? Hujui kwamba Anaweza Akakihitilafisha kiungo chochote cha mwili wako ukajikuta umepooza? Wafalme wangapi yamewakuta hayo na hata madaktari mabingwa wameshindwa kuwaponya?!
"يَا أَيُّهَا الْإِنسَانُ مَا غَرَّكَ بِرَبِّكَ الْكَرِيمِ"
“Ee mwana Aadam! Nini kilichokughuri hata umkufuru Rabb wako Mkarimu”?
الَّذِي خَلَقَكَ فَسَوَّاكَ فَعَدَلَكَ
“Ambaye Amekuumba, Akakusawazisha (umbo sura, viungo), na Akakulinganisha sawa”.
فِي أَيِّ صُورَةٍ مَّا شَاءَ رَكَّبَكَ
“Katika sura Aliyotaka Akakutengeneza”.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
20: Je, Haujafika Tu Muda Wa Wewe Kujionea Haya Na Uteremko Wa Allaah ‘Azza Wa Jalla Kwa Ajili Yako Kila Usiku?
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"- ينزلُ اللهُ كلَّ ليلةٍ إلى السَّماءِ الدُّنْيا، حِيْنَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الآخرِ، فَيَقُولُ: مَنْ يَدْعُوْنِي فأستجيبُ له ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ ، مَنْ يَسْتَغْفِرُني فأغفرُ له"
“Allaah Anateremka kila usiku hadi mbingu ya dunia inapobakia theluthi ya mwisho ya usiku, kisha Husema: Nani aniombaye Nikamjibu? Nani anitakaye haja yake Nikampa? Nani aniombaye maghfira Nikamghufuria?”
Uteremko huu wa Allaah ni kwa ajili yetu Sisi kutokana na Rehma Zake. Ni kama vile Anatufata hadi mlangoni kutuuliza haja zetu Akiwa tayari kabisa kututatulia, lakini milango yetu inabaki tumeifunga. Hatuthamini kabisa ujio huo wa Mfalme wa wafalme!! Sisi ni nani hadi Atufanyie hivi? Je, hii haionyeshi Penzi Lake kubwa kwetu ambalo hatulithamini wala kumthamini Mwenyewe Allaah ‘Azza wa Jalla? Lakini je sisi tunahisi Takrima hii na Utukuzo huu Anaotupa? Je, tunahisi thamani yake?!
La hasha! Wakati huu kila mtu anakuwa amezama kwenye usingizi mkali mnono ila wachache tu waliotambua na kujua thamani ya Uteremko huu wa Allaah ‘Azza wa Jalla kwao. Hatuoni hata aibu tukiwa gubigubi huku Yeye Anatuita ili tumuelezee matatizo yetu yaliyosheheni ya kidunia na kiaakhirah, kisha Anaondoka bila kupata jibu, lakini kwa Rahma Zake Anateremka tena usiku unaofuata kila siku na hali kubaki hivyo hivyo. Je, hatuoni aibu?
Ndugu yangu! Hii ni nafasi ya kipekee kabisa isiyo na mfano. Pambana na usingizi wako, anza kidogo kidogo kuamka na hatimaye utazoea na kuona jambo la kawaida kabisa. Hapo itakuwa nafasi ya kumlilia matatizo yako yote ya dunia na aakhirah, Naye bila shaka Hatokuangusha kamwe na daima Atafurahika sana nawe.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
21: Kwa Nini Allaah ‘Azza Wa Jalla Anateremka Katika Theluthi Ya Mwisho Ya Usiku?
Allaah ‘Azza wa Jalla Ameihusisha theluthi ya mwisho ya usiku kuteremka ndanimwe, kwa kuwa huo ndio wakati wa faragha, mghafala na watu kuzama ndani ya usingizi mzito mtamu. Ni uteremko unaolaikiana Naye Jalla Jalaaluhu ambao hakuna ajuaye namna yake ila Yeye tu. Haufanani kabisa na wa viumbe. Na mtu kuachana na ladha ya usingizi mzito ni jambo zito sana. Hivyo mwenye kuacha usingizi wake huo, akatawadha, akaswali na kisha akamwomba Allaah ‘Azza wa Jalla, hiyo ni dalili tosha juu ya niya yake safi, utashi wake wa kweli kwa Mola Wake, na kuwa mbali kabisa na riyaa. Hapa Swalah yake inakuwa na khushuu halisi, duaa anaiomba kwa dhati na msisitizo huku akihisi ladha halisia ya kufanya ‘ibaadah katika wakati huu na kwa uhudhurio wa karibu kabisa wa Allaah.
Na kwa ajili hiyo, Allaah Huteremka kuwa karibu kabisa na watu wa aina hii. Anatuambia katika Al-Hadiyth Al-Qudsiy:
"إِذَا تَقَرَّبَ الْعَبْدُ إِلَىَّ شِبْرًا تَقَرَّبْتُ إِلَيْهِ ذِرَاعًا، وَإِذَا تَقَرَّبَ مِنِّي ذِرَاعًا تَقَرَّبْتُ مِنْهُ بَاعًا، وَإِذَا أَتَانِي مَشْيًا أَتَيْتُهُ هَرْوَلَةً"
“Mja akijikurubisha Kwangu kwa shibiri, Mimi Hujikurubisha kwake kwa dhiraa, akijikurubisha Kwangu kwa dhiraa, Mimi Hujikurubisha Kwake kwa ba-‘a, na akinijia anatembea, Mimi Humjia mwendo wa haraka”. [Swahiyh Al-Bukhaariy]
Shibiri au shubiri, ni kipimo cha urefu wa takriban sentimeta kati ya 20–25, ni umbali kati ya kidole gumba na cha mwisho kiganja kikitanuliwa. Na dhiraa ni urefu wa takriban sentimeta 50, yaani kutoka ncha ya kidole cha kati hadi kwenye kisugudi. Ama ba-’a, huo ni urefu wa mikono miwili iliyonyooshwa. Cha muhimu, hii ni mifano tu ya vipimo, vyovyote unavyojikurubisha Kwake, Yeye inakuwa ni maradufu na ziada.
Na kwa vile mtu huyu amejihimu kuacha usingizi wake ili kufanya ‘ibaadah, Naye Allaah Hufurahika zaidi Naye. Malipo yake yanakuwa kama Anavyosema Allaah:
فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَّا أُخْفِيَ لَهُم مِّن قُرَّةِ أَعْيُنٍ جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ
“Basi nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda”. [As-Sajdah: 17]
Na kabla ya aayah hii, Anawasifu Akisema:
"تَتَجَافَىٰ جُنُوبُهُمْ عَنِ الْمَضَاجِعِ يَدْعُونَ رَبَّهُمْ خَوْفًا وَطَمَعًا وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ"
“Mbavu zao zinatengana na vitanda, wanamuomba Rabb wao kwa khofu na matumaini, na katika yale Tuliyowaruzuku wanatoa”. [As-Sajdah: 16]
Tunamwomba Allaah ‘Azza wa Jalla Atujaalie tuwe kwenye kundi hili na tuwe wawajibikaji wa kikweli.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
22: لِمَنِ المُلكُ اليَوْمَ؟ Ni Wa Nani Ufalme Wa Leo?
Kila siku tunasoma Suwratul Faatihah tukimsemesha Allaah na kumwambia:
"مَالِكِ يَوْمِ الدِّينِ"
“Mfalme wa Siku ya Malipo”.
Hivi kwani leo Yeye Sio Mfalme?
Katika maisha yetu ya hapa duniani, kila mmoja ni mfalme katika uwanja wake. Allaah Amempa kila mtu nafasi ya mamlaka maalum katika mambo fulani. Kiongozi wa nchi ana mamlaka ya kuteua anaowaona kuwa wanamfaa katika shughuli za utawala ni sawa wanafaa au hawafai. IGP ana mamlaka ya kuteua maofisa anaowataka wa usalama, kuwahamisha hapa na pale na kadhalika, na kubeba dhamana ya usalama wa raia kiujumla. Hata askari au mgambo tu, wakati mwingine anaingiwa na wahaka wa kutaka kuonyesha watu misuli zake, atamsimamisha mtu, amwamuru aonyeshe kitambulisho chake, akiangalie, amwamuru achuchumae, aruke kichurachura au ampe mkong’oto wakati mtu hata hana kosa lolote achilia mbali yanayojiri ndani ya mahabusu za utesaji watu ambayo ni ya kutisha na kuogofya. Wanaotenda hayo humo wanajiona wao ni miungu watu. Humo wao ni wafalme kwa mamlaka waliyonayo ambayo wanayatumia sivyo.
Hata wabeba taka za miji, ni wafalme katika kazi yao inayodharauliwa na wengi. Siku wakigoma, itabidi hata wapigiwe magoti, kwani mji unaweza usiweze kukalika kutokana na hali mbaya ya kiafya inayoweza kujitokeza. Na hata waoshaji maiti wanaoonekana watu duni, siku wakatae kufanya kazi, itabidi kuwabembeleza na kuwalilia sana na hata ikibidi kuwaongezea malipo. Hii ni baadhi ya mifano tu ya mamlaka aliyonayo kila mmoja kati yetu ambayo anaweza kuyatumia vibaya au kuyatumia vizuri, na hisabu yake ni Siku hiyo ya Qiyaamah. Huu ndio Ufalme wetu wa hapa duniani tuliobebeshewa dhamana na Allaah, lakini Ufalme wa Allaah pia upo.
Siku hiyo ya Qiyaamah utadhihirika Ufalme wa kikweli ambao watu wengi hawaujui. Wafalme wa hapa duniani hawataonekana kabisa, kwani hawatakuwa na lolote. Ni Ufalme wa Allaah Pekee Anayetuambia:
"يَوْمَ هُم بَارِزُونَ ۖ لَا يَخْفَىٰ عَلَى اللَّـهِ مِنْهُمْ شَيْءٌ ۚ لِّمَنِ الْمُلْكُ الْيَوْمَ ۖ لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ"
“Siku watakayotokeza wao, hakitofichika kitu chochote chao kwa Allaah. Ufalme ni wa nani leo? (Allaah Mwenyewe Atajijibu): Ni wa Allaah Pekee Mmoja, Asiyepingika”. [Ghaafir: 16]
Yaani watu wataonekana dhahiri bayana, wakiwa uchi wa mnyama kama siku waliyozaliwa, wako pekupeku, na hawajatahiriwa au kukeketwa. Hakuna cha kuwasitiri wala kuwaficha, si mlima, au mti, au nyumba, au pango, kwa kuwa ardhi itakuwa nyingine, si ardhi hii tunayoishi juu yake kwa sasa, bali ni ardhi nyingine kabisa isiyo na mmea, wala bahari, wala minyanyuko wala miteremko, ni ardhi iliyo mithili ya meza. Watu kwa sasa, wanadhani kwamba wanaweza kujificha mahala fulani na Allaah ati Asiweze kuwaona wakafanya maasia. Lakini siku hiyo wataanikwa, hakuna kwamba huyu alikuwa ni mfalme au amiri jeshi mkuu, huko utofauti utakuwa kwa amali za mtu anazozichuma hapa duniani. Na hapa ndipo watu watakapojua ni Nani Mfalme wa kweli. Akiuliza: Ni wa Nani Ufalme wa leo? Hakutokuwa na jibu. Kimyaa, kimyaa kizito kabisa.
"وَخَشَعَتِ الْأَصْوَاتُ لِلرَّحْمَـٰنِ فَلَا تَسْمَعُ إِلَّا هَمْسًا"
“Siku hiyo watamfuata mwitaji hakuna kumkengeuka. Na sauti zitafifia kwa Ar-Rahmaan, basi hutosikia isipokuwa mchakato wa nyayo”.
Hapo Allaah Atajijibu Mwenyewe: “Ni wa Allaah Pekee Mmoja, Asiyepingika”.
Ndugu Muislamu! Jisalimishe na siku hii ngumu kwa kuongeza matendo mema. Haya ndiyo yatakayokuweka mahala salama ukawashinda wafalme wote wa duniani ambao siku hiyo hawatokuwa na mamlaka yoyote kama haya wanayotamba nayo hapa duniani kwa sasa.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
23: Kuamsha Watoto Kuswali:
Swalaah ni ‘ibaadah kati ya ‘ibaadah bora kabisa ambayo wengi wetu wanaifanya lakini pengine hawajui ubora wake. Kuwaamsha watoto na hususan kwa ajili ya Swalaatul Fajr na kuwazoesha Swalaah kiujumla tokea udogoni, ni moja ya ‘ibaadah bora kabisa. Kwa ‘ibaadah hii, Allaah Amemwamuru Nabiy Wake Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Akimwambia:
"وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا ۖ لَا نَسْأَلُكَ رِزْقًا ۖ نَّحْنُ نَرْزُقُكَ ۗ وَالْعَاقِبَةُ لِلتَّقْوَىٰ"
“Na amrisha ahli zako Swalaah, na dumisha uvumilivu juu ya mazito yake. Hatukukalifishi riziki, bali Sisi Ndio Tunaokuruzuku. Na khatima njema ni kwa wenye taqwa”. [Twaahaa: 132]
Na kuhusu Nabiy ‘Ismaa’iyl Amesema:
"وَكَانَ يَأْمُرُ أَهْلَهُ بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ وَكَانَ عِندَ رَبِّهِ مَرْضِيًّا"
“Na alikuwa akiwaamrisha ahli zake Swalaah na Zakaah, na alikuwa mridhiwa mbele ya Rabb wake”. [Maryam: 55]
Na wasiya wa Luqmaan kwa mwanaye:
"يَا بُنَيَّ أَقِمِ الصَّلَاةَ"
“Ee mwanangu! Simamisha Swalaah”. [Luqmaan: 17]
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
24: Usiingie Kwenye Mkumbo Huu:
Ni mara nyingi tumeshuhudia sehemu mbalimbali watu wakikimbilia kupora bidhaa za lori la mizigo lililopata ajali ya kupinduka. Kupinduka huku imekuwa ni kama kihalalisho kwao kupora bidhaa hizo ambazo mwenye mali amezinunua kwa mamilioni. Nao hukusudia hasa kuvunja na kulifungua ili kupora bidhaa zilizomo humo. Na wakati mwingine inakuwa ni lori la mafuta ambayo huyafungulia ili wayachote na kuanza kumiminika kwa kiasi kikubwa na kuwa ni hatari kwao wao na kwa wengineo wasiohusika. Maafa mengi ya kutisha yametokea kutokana na tabia hii. Wenye mali wangeweza kuja, wakalinyanyua lori na kufanya mpango wa kuhamisha mali yao kwa salama kwenye gari jingine na kuifikisha kule ilikokuwa inakwenda.
Ndugu yangu Muislamu! Usijaribe kuingia kwenye mkumbo huu. Ujue kwamba ile ni mali ya mtu. Kaa mbali nayo kabisa. Kila anayepora pale, basi atakuja na mzigo huo kama ushahidi dhidi yake Siku ya Qiyaamah. Allaah Anasema:
"ومَن يَغْلُلْ يَأْتِ بِمَا غَلَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۚ ثُمَّ تُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ"
“Na yeyote atakayekhini, atakuja na kile alichokikhini Siku ya Qiyaamah. Kisha kila nafsi italipwa kamilifu yale iliyoyachuma, nao hawatodhulumiwa”. [Aal ‘Imraan: 161]
Kila unayemwona pale akitoka na gunia begani au debe la mafuta, basi atakuja nalo hivyo hivyo Siku hiyo.
Halafu angalia, inakuwaje hali ya wale wanaofia hapo kwa mlipuko wa mafuta kwa mfano?! Wanakufa hali ya kuwa wanapora!! Inakuwaje hatima yao!!
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
25: Usiingie Kwenye Mkumbo Huu:
Ni mara nyingi tunashuhudia kibaka akipata kipigo kikali kisha kuchomwa moto. Kila anayepita hapo na kuona tukio, naye haraka hujiunga kupiga na kutafuta haraka zana za kuchomea mtu huyo kama tairi, mafuta, kiberiti na kadhalika bila kujua kama ni mwizi kweli au la?
Kila anayepiga, na kila anayesaidia kufanikisha zoezi la kumchoma sawa sawa kwa neno, au kwa kitendo, basi hao wote wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya nafsi mbele ya Allaah Siku ya Qiyaamah, na pia kesi ya kutesa na kuua kwa kutumia moto.
Kuchoma mtu au kiumbe chochote hata wadudu ni jambo lililoharamishwa. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"لا يُعَذِّبُ بالنَّارِ إلّا ربُّ النَّارِ"
“Hatesi kwa moto ila Mola wa moto”. [Hadiyth Swahiyh. Iko kwenye Al-Muhallaa (11/383)]
Na hata panya ukimkamata kwa mtego, unachotakiwa ni kumuua haraka na kwa pigo moja tu. Usimkawize baada ya kumnasa, utazidi kumtesa kisaikolojia. Muue mara moja. Mauti yanatisha hata kwa wanyama! Usimchome wala kumzamisha kwenye maji. Haya ndiyo tunayoamrishwa na Dini yetu ya kutovuka mipaka iliyowekwa na Allaah na Rasuli Wake (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hali inakuwa vipi kwa mwanadamu!
Hivyo basi, ukisadifu kukutana na tukio kama hilo, jipitie zako na njia zako. Usishiriki kwa lolote, utasalimika.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
26: Ukarimu Mkubwa Wa Allaah Kwa Wakosefu:
Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Anasema katika Al-Hadiyth Al-Qudsiy:
"قال اللهُ تعالى: يا ابنَ آدمَ! إِنَّكَ ما دَعَوْتَنِي ورَجَوْتَنِي غَفَرْتُ لكَ على ما كان فيكَ ولا أُبالِي، يا ابنَ آدمَ! لَوْ بَلَغَتْ ذُنُوبُكَ عَنانَ السَّماءِ ثُمَّ اسْتَغْفَرْتَنِي غَفَرْتُ لكَ ولا أُبالِي، يا ابنَ آدمَ! لَوْ أَتَيْتَنِي بِقُرَابِ الأرضِ خطَايا ثُمَّ لَقِيْتَني لاتُشْرِكْ بِيْ شَيْئًا لأتيْتُكَ بِقِرَابِها مَغْفِرَةً"
“Ee mwana wa Aadam! Hakika wewe madhali unaniomba na una matarajio mema Kwangu, basi Nitakusamehe madhambi yote uliyonayo, na wala Sijali. Ee mwana wa Aadam! Lau madhambi yako yatafikia kilele cha mbingu na pande zake zote, kisha ukaniomba msamaha, basi Nitakusamehe, na wala Sijali. Ee mwana wa Aadam! Lau utanijia na makosa yaliyojaa ardhi yote (baada ya kufa), halafu ukakutana Nami hali ya kuwa Hukunishirikisha na chochote, basi Nitakujia na maghfira ya ujazo wa makosa hayo yote”. [Hadiyth Hasan Lighayrih. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (3540) na Ahmad (13493)]
Allaah ‘Azza wa Jalla Ndiye Mwenye huruma kuliko wote wenye huruma. Yeye Ndiye Anayeghufiria na kufuta madhambi yote ya Mja Wake aliyemuasi vyovyote ukubwa wa madhambi utakavyokuwa, lakini kwa sharti ya mja huyu kuwa asiwe ni mshirikina, bali awe ni mwenye kumpwekesha Yeye tu. Washirikina hawana nafasi hii, na huu ndio ubaya wa ushirikina. Dhambi zote ziko chini ya Matakwa Yake Allaah; Anamsamehe Amtakaye, isipokuwa dhambi ya shirki. Dhambi hii Allaah Haisamehi ikiwa mtu atakufa nayo.
Katika Hadiyth hii ya Al-Qudsiy, tunaona ni namna gani Huruma ya Allaah ilivyo kubwa kwetu. Sisi wana wa Aadamu ni watu wa kuteleza sana kwenye madhambi mengi ya aina tofauti. Wengine hujisahau kabisa na kuogelea kwenye kona zote za madhambi makubwa na madogo na hata ya shirki. Lakini hawa wote, Allaah Anawasubiri wajirudi na warudi Kwake moja kwa moja ili Apate kuwasamehe na kuwafutia makosa yao yote bila Yeye kujali ukubwa wa makosa yao hayo, na hata bila ya kuwawekea masharti ya aina yoyote. Muhimu warejee Kwake kidhati na wawe tayari. Anatuambia:
"قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا ۚ إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ"
“Sema: Enyi Waja Wangu ambao wamepindukia mipaka juu ya nafsi zao: Msikate tamaa na Rahmah ya Allaah; hakika Allaah Anaghufuria dhambi zote. Hakika Yeye Ndiye Mwenye Kughufuria, Mwenye Kurehemu”. [Az-Zumar: 53]
Mbali na wito huu mwema wa kutubembeleza pamoja na madhambi yetu na kwamba tusikate kabisa tamaa na Rahmah Zake, na kwamba Yeye Anasamehe madhambi yote, Anaendelea kutuambia:
"وَأَنِيبُوا إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَأَسْلِمُوا لَهُ مِن قَبْلِ أَن يَأْتِيَكُمُ الْعَذَابُ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ"
“Na rudini kwa Rabb wenu (kwa tawbah na matendo mema), na jisalimisheni Kwake kabla haijakufikieni adhabu, kisha hamtonusuriwa”.
Na haya ni hapa duniani kabla ya mtu kufariki. Kama atafariki na madhambi, Allaah pia huko Aakhirah Atamsamehe madhambi yake kama hana dhambi ya shirki. Ndio hapo Anapotuambia:
"يا ابنَ آدمَ إنَّكَ لو أتيتَني بقرابِ الأرضِ خطايا ثمَّ لقيتَني لا تشرِكُ بي شيئًا لأتيتُكَ بقرابِها مغفرةً"
Ee mwana wa Aadam! Lau hata utanijia na makosa yaliyojaa ardhi yote (baada ya kufa), halafu ukakutana Nami hali ya kuwa Hukunishirikisha na chochote, basi Nitakujia na maghfirah ya ujazo wa makosa hayo yote.
Ulamaa wanasema madhambi makubwa aliyoyafanya Muumini yanahitajia kuomba tawbah, au suala la kusamehewa liko katika Mikono ya Allaah; Akitaka Atamsamehe, na Akitaka Atamwadhibu. Kadhalika, haki za watu ni lazima zirejeshwe, au Allaah Anaweza kumlipa mwenye haki kwa Fadhla Zake na kumsamehe kwa Ukarimu Wake aliyedhulumu.
Tunajifunza kutokana na Al-Hadiyth Al-Qudsiy hii:
1- Fadhla ya tawhiyd. Tawhiyd ndio sababu pekee ya Muumini kuepukana na adhabu za Allaah.
2- Shirki ni hatari mno, inabidi iepukwe kwa njia zote.
3- Ukarimu mkubwa usio na mipaka wa Allaah kwetu. Vyovyote madhambi yetu yatakavyokuwa makubwa hadi kujaza mbingu zote, Allaah Huyasamehe mja akirudi Kwake na kumwomba maghfirah.
4- Umuhimu wa kuomba duaa na kuomba maghfirah.
5- Umuhimu wa kuwa na rajua njema kwa Allaah.
6- Uharamu wa kukata tamaa na Rahma za Allaah.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
27: Siri Kubwa Ya Kumsabbih Allaah:
Ukifuatilia suala la Allaah kusabihiwa kwenye Qur-aan Tukufu, utakuta ajabu kubwa.
1- Utakuta kwamba “Tasbiyh” ina uwezo wa kuondosha Qadari ya Allaah. Katika kisa cha Nabiy Yuwnus ‘Alayhis Salaam, Allaah Anatuambia:
"فَلَوْلَا أَنَّهُ كَانَ مِنَ الْمُسَبِّحِينَ • لَلَبِثَ فِي بَطْنِهِ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ"
“Na lau kama hakuwa miongoni mwa wenye kumsabbih Allaah • Angelibakia tumboni mwake mpaka Siku watakayofufuliwa”. [Yuwnus: 143-144].
Alikuwa anasema katika kumsabbih Allaah:
"لا إِلَهَ إِلاّ أَنْتَ سُبْحَانَكَ إِنِّيْ كُنْتُ مِنَ الظَّالِمِيْنَ"
2- Utakuta kwamba “tasbiyh” ndiyo utajo ambao milima na ndege ilikuwa ikiitikia pamoja na Nabiy Daawuwd ‘Alayhis Salaam. Allaah Anatuambia:
"وَسَخَّرْنَا مَعَ دَاوُودَ الْجِبَالَ يُسَبِّحْنَ وَالطَّيْرَ"
“Na Tukatiisha milima iwe pamoja na Daawuwd ikisabihi pamoja na ndege”. [Al-Anbiyaa: 70]
3- “Tasbiyh” ni utajo wa viumbe vyote ulimwenguni; mbinguni na ardhini. Allaah Anatuambia:
"أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يُسَبِّحُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالطَّيْرُ صَافَّاتٍ ۖ كُلٌّ قَدْ عَلِمَ صَلَاتَهُ وَتَسْبِيحَهُ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِمَا يَفْعَلُونَ"
“Je, huoni kwamba wanamsabihi Allaah walioko mbinguni na ardhini, na (pia) ndege wakiwa wamekunjua mbawa zao. Kila mmoja (Allaah) Amekwishajua Swalaah yake na tasbihi yake. Na Allaah Ni Mjuzi kwa yale wayafanyao”. [An-Nuwr: 41]
4- Zakariyyaa ‘Alayhis Salaam alipotoka mihrabuni kwake, aliwaamuru watu wake walete “Tasbiyh”. Allaah Anatuambia:
"فَخَرَجَ عَلَىٰ قَوْمِهِ مِنَ الْمِحْرَابِ فَأَوْحَىٰ إِلَيْهِمْ أَن سَبِّحُوا بُكْرَةً وَعَشِيًّا"
“Basi akawatokea watu wake kutoka mihrabuni, akawaashiria: Msabihini (Allaah) asubuhi na jioni”. [Maryam: 11]
5- Nabiy Muwsaa ‘Alayhis Salaam alimwomba Allaah Amfanye nduguye Haaruwn kuwa msaidizi wake atakayemsaidia katika kumsabbih Allaah na kumtaja. Anatuambia Allaah:
"وَاجْعَل لِّي وَزِيرًا مِّنْ أَهْلِي • هَارُونَ أَخِي • اشْدُدْ بِهِ أَزْرِي • وَأَشْرِكْهُ فِي أَمْرِي • كَيْ نُسَبِّحَكَ كَثِيرًا • وَنَذْكُرَكَ كَثِيرًا"
“Na Nifanyie msaidizi kutoka ahli zangu • Haaruwn, ndugu yangu • Nitie nguvu kwaye • Ili tukusabihi kwa wingi • Na tukudhukuru kwa wingi”. [Twaahaa: 29-34]
6- “Tasbiyh” ndiyo utajo wa watu wa Peponi. Allaah Anatuambia:
"دَعْوَاهُمْ فِيهَا سُبْحَانَكَ اللَّـهُمَّ وَتَحِيَّتُهُمْ فِيهَا سَلَامٌ"
“Wito wao humo ni: Utakasifu ni Wako ee Allaah. Na maamkizi yao humo ni Salaamun!” [Yuwnus: 10]
7- “Tasbiyh” ni utajo wa Malaika. Allaah Anatuambia:
"وَالْمَلَائِكَةُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِمَن فِي الْأَرْضِ"
“Na Malaika wanasabbih na kumhimidi Rabb wao, na wanawaombea maghfirah walioko ardhini”. [Ash-Shuwraa: 05]
8- “Tasbiyh” imekuja kwa vitenzi tofauti katika Qur-aan.
(a) Cha wakati uliopita. Allaah Anasema:
"سَبَّحَ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ"
“Vimemsabbih Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na ardhi, Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote”. [Al-Hadiyd: 01].
(b) Cha wakati uliopo. Anatuambia Allaah Ta’aalaa:
"يُسَبِّحُ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ"
“Vinamsabbih Allaah Pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi, Mfalme, Ametakasika na sifa zote hasi, Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote”. [Al-Jum-‘ah: 01]
(c) Kitenzi agizi. Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
"سَبِّحِ اسْمَ رَبِّكَ الْأَعْلَى"
“Sabbih Jina la Rabb wako Mwenye ‘Uluwa Aliyetukuka kabisa kuliko vyote”. [Al-A’alaa: 01]
Vitenzi vyote hivi viko katika Aayaati za mwanzo za Suwrah. Na hapa bila shaka kuna siri kubwa.
9- “Tasbiyh” ni sababu ya kupata mambo ya kumridhisha na kumfurahisha Muislamu duniani na aakhirah. Allaah Anatuambia:
"فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا ۖ وَمِنْ آنَاءِ اللَّيْلِ فَسَبِّحْ وَأَطْرَافَ النَّهَارِ لَعَلَّكَ تَرْضَىٰ"
“Basi subiri juu ya yale wanayoyasema. Na sabihi ukimhimidi Rabb wako kabla ya kuchomoza jua, na kabla ya kuchwa kwake. Na katika nyakati za usiku pia sabbih na katikati ya mchana, lazima utapata ya kukuridhisha”. [Twaahaa: 130]
Na ili kuyapata hayo, Allaah Anatuhimiza hapa tumsabbih nyakati hizi tajwa na nyakati zingine zote.
10- “Tasbiyh” ni ponyo la dhiki ya kifua na kisaikolojia. Allaah Anasema:
"وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ • فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ"
“Na kwa yakini Tunajua kwamba kifua chako kinadhikika kwa yale wanayoyasema • Basi sabihi na mhimidi Rabb wako na uwe miongoni mwa wanaosujudu”. [Al-Hijri: 97-98]
Angalia namna Aaayah hii inavyoelekeza namna ya kuondosha dhiki ya kifua na roho kwa ‘Tasbiyh”. Ukihisi hali hiyo, basi kimbilia kumsabbih Allaah, ni dawa ya ponyo.
Haya yote yanaonyesha siri kubwa iliyoko ndani ya “Tasbiyh”. Ulimwengu wote wa juu na wa chini, av yote vilivyomo humo vinamsabbih Allaah; kila kimoja kwa namna yake Anayoijua Allaah. Muislamu usije ukajitoa ndani ya duara hilo. Usije kuwa ndani ya kundi la walioghafilika. Ni amali rahisi kabisa ya ulimi isiyohitajia zana, wala wakati maalum wala sehemu maalum. Usipoteze nafasi hii muhimu.
Kati ya “Tasbiyh” bora kabisa na zenye malipo makubwa ni:
سُبْحَانَ اللهِ وَبِحَمْدِه عَدَدَ خَلْقِهِ وَرِضَا نَفْسِهِ وَزِنَةَ عَرْشِهِ وَمِدَادَ كَلِمَاتِهِ
Alhidaaya.com [3]
28: Tuambulie Angalau Yai Zima:
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَنِ اغْتَسَلَ يَوْمَ الْجُمْعَةِ غُسْلَ الْجَنَابَةِ، ثُمَّ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الأُوْلَى فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَدَنَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّانِيَةِ، فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَقَرَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الثَّالِثَةِ، فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ كَبْشًا أَقْرَنَ، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الرَّابِعَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ دَجَاجَةً، وَمَنْ رَاحَ فِي السَّاعَةِ الْخَامِسَةِ فَكَأَنَّمَا قَرَّبَ بَيْضَةً، فَإِذَا خَرَجَ الإِمَامُ حَضَرَتِ الْمَلاَئِكَةُ يَسْتَمِعُونَ الذِّكْرَ "
“Mwenye kuoga kikamilifu siku ya Ijumaa kama anavyofanya katika ghuslu ya janaba, kisha akaenda (Msikitini) katika saa la mwanzo, basi anakuwa kama ametoa swadaqah ngamia, na mwenye kwenda saa la pili, anakuwa kama ametoa swadaqah ng’ombe, na mwenye kwenda saa la tatu, anakuwa kama ametoa swadaqah kondoo dume mwenye pembe, na mwenye kwenda saa la nne, anakuwa kama ametoa swadaqah kuku, na mwenye kwenda saa la tano, anakuwa kama ametoa swadaqah yai. Na Imamu anapotokeza (akapanda mimbari), Malaika huingia na kuketi kusikiliza utajo”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (881) na Muslim (850)]
Allaah Ta’aalaa Ametuamuru tuharakie kwenye mambo yote ya kheri. Anatuambia:
"فَاسْتَجَبْنَا لَهُ وَوَهَبْنَا لَهُ يَحْيَىٰ وَأَصْلَحْنَا لَهُ زَوْجَهُ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَيَدْعُونَنَا رَغَبًا وَرَهَبًا ۖ وَكَانُوا لَنَا خَاشِعِين"
“Basi Tukamuitikia na Tukamtunukia Yahyaa, na Tukamtengenezea mke wake. Hakika wao walikuwa wakikimbilia katika mambo ya khayr na wakituomba kwa raghba na khofu, na walikuwa wenye kutunyenyekea. [Al-Anbiyaa: 90]
Kwenda mapema kwenye Swalah ni katika jambo muhimu sana la kheri na hususan Swalah ya Ijumaa kwa wanaume. Katika Hadiyth hii, Rasuli anatueleza thawabu zinazopatikana kwa mujibu wa saa kwa saa. Anayekwenda Msikitini Siku hii ya Ijumaa katika saa la mwanzo, basi thawabu zake ni sawa na aliyetoa ngamia swadaqah, na la pili sawa na ng’ombe, la tatu sawa na kondoo, la nne sawa na kuku, na la tano na la mwisho sawa na yai.
Masaa Haya Matano Hugawanywaje Au Hupatikanaje?
Masaa haya huanza kuhesabiwa kuanzia pale jua linapochomoza mpaka adhana ya pili ya Ijumaa. Kwa mfano, kama jua linachomoza saa 06.30 a.m (kumi na mbili na nusu asubuhi), na adhana ya pili ya Ijumaa ni saa 12.30 p.m (sita na nusu mchana), hapa kutakuwa na jumla ya masaa sita yenye dakika 360 (60X6). Lakini sisi tunataka masaa matano tu kama yalivyoainishwa na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ili kuyapata, tutagawa dakika hizo 360 kwa tano (ambayo ni masaa tajwa katika Hadiyth (360÷5) na tutapata dakika 72 kwa kila saa moja. Hivyo basi, jedwali ya masaa na thawabu ya vilivyotajwa itakuwa kama ifuatavyo:
Masaa |
Kuanzia - Hadi |
Thawabu
|
La Kwanza |
6.30 a.m hadi 7.42 a.m Saa 12 na nusu asubuhi hadi saa moja na dakika 42. |
Ngamia |
La Pili |
7.42 a.m hadi 8.54 a.m Saa moja na dakika 42 hadi saa mbili na dakika 54. |
Ng’ombe |
La Tatu |
8.54 a.m hadi 10.06 a.m Saa mbili na dakika 54 hadi saa nne na dakika sita. |
Mbuzi, kondoo |
La Nne |
10.06 a.m hadi 11.18 a.m Saa nne na dakika sita hadi saa tano na dakika 18. |
Kuku |
La Tano |
11.18 a.m hadi 12.30 a.m Saa tano na dakika kumi na nane hadi saa sita na nusu. |
Yai |
Thawabu hizi pia hutofautiana ndani ya kila saa kwa mujibu wa mtu atakavyowahi. Ikiwa kwa mfano saa la kwanza ngamia wake ni wa uzito wa kilo 1000, basi anayeingia Msikitini dakika ya mwanzo kabisa ya saa kumi na mbili na nusu, basi huyo atampata huyo wa kilo 1000. Na huyu pia atasajiliwa nambari moja na Malaika wanaosimama kwenye milango ya Msikiti kuwasajili wote wanaoingia kwa ajili ya Swalah katika siku hiyo. Ni mafanikio yalioje ya kusajiliwa nambari moja! Mwingine kwa uvivu wake na mapuuza, hata nambari ya mwisho haipati. Ni wale wanaotegea hadi khatibu apande mimbari, kisha wajikongoje wafike mwisho wa khutba ya pili. Hapa Malaika wanakuwa wameshafunga madaftari yao zamani na kuingia Msikitini kusikiliza utajo wa Allaah kwenye khutbah. Ni hasara kubwa sana kwa Muislamu, kwa hakika. Anayekuja baada ya robo saa 6.45 am, basi atapata wa kilo 750 na kuendelea. Hali kadhalika katika masaa mengineyo hadi kwenye yai. Mwingine atapata la ukubwa wa mbuni, mwingine mpaka wa ndege mdogo kabisa. Je, hata hili pia litamshinda Muislamu kulipata kwa hao wanaotegea kuja saa la mwisho kabisa!
Huenda mtu akadharau kuona kwamba thawabu za yai ati ni ndogo mno! Hajui zina thamani gani mbele ya Allaah Anayezitoa. Hamfikirii pia anayepata ngamia, ni namna gani anasubiri huyu! Kukaa ndani ya Msikiti kwa masaa sita na hadi kumalizika khutba na Swalah, si jambo dogo hata kidogo, na huenda hakuna anayeweza kufanya hilo kwa sasa isipokuwa wachache mno, au hata wasipatikane kabisa. Wanaopatikana huenda ni wa ng’ombe kuanzia saa lake la mwisho. Tujitahidini ndugu Waislamu tupate angalau kuanzia kondoo, na tukishindwa sana, hata yai kamili.
Pamoja na hayo yote, thawabu zilizotajwa ni mfano tu, lakini kiuhakika ni thawabu kubwa zaidi na zaidi hata za hilo yai. Ndio maana Rasuli akasema “ni kama”. Na mwenye kuchelewa akazikosa thawabu hizo, hakosi pia fadhila za Siku hii tukufu. Hizi ni katika Fadhila za Allaah kwetu. Na katika kukamilisha malipo hayo, Muislamu asisahau kuoga vizuri mwogo maalum kwa ajili ya Siku hiyo ili kupata malipo kamili kabisa. Atumie shampoo kuosha nywele za kichwa, asugue mwili na hususan kwato mbili, baadhi hujisahau hadi kwato kutoa mipasuko, akate nywele za kinena, za kwapa na kadhalika ili kufanya malipo yawe kamili, halafu avae nguo nzuri na ajitie manukato.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
29: Lituzindushe Hili:
Tumesikia na kushuhudia tukio la kutokea tetemeko kubwa nchini Uturuki na Syria tarehe 05/02/2023. Maelfu ya watu walikufa, maelfu wengine walijeruhiwa, na maelfu wengine walioponea walipoteza kila kitu kuanzia nyumba zao na vyote vilivyomo ndani, mbali na maelfu pia waliowapoteza ndugu zao, jamaa zao na kadhalika. Bila shaka ni mtihani na msiba wa kushtua sana. Unahitaji subra ya hali ya juu kabisa kuukabili.
Tetemeko kwa kweli linatisha na kuogofya sana. Wale waliolikabili wakiwa ndani ya majengo na hasa marefu, hao ndio kiukweli wanajua maana halisi ya tetemeko. Utakuta jumba lote linayumba pamoja na uzito wake wote, sauti kali ya vyote vilivyomo ndani ya nyumba vikigongana na kucheza huku na kule pamoja na mtikisiko wa ajabu. Tetemeko hili la Uturuki na Syria, ukubwa wake ni wa nyuzi 7 na nukta kadhaa hivi kwa kipimo cha Rechter, na athari zake ndizo hizo kama zinavyoonekana kwenye vyombo vya habari. Sasa hilo la Qiyaamah litakuwaje?
Allaah Anatuambia:
"يَا أَيُّهَا النَّاسُ اتَّقُوا رَبَّكُمْ ۚ إِنَّ زَلْزَلَةَ السَّاعَةِ شَيْءٌ عَظِيمٌ • َوْمَ تَرَوْنَهَا تَذْهَلُ كُلُّ مُرْضِعَةٍ عَمَّا أَرْضَعَتْ وَتَضَعُ كُلُّ ذَاتِ حَمْلٍ حَمْلَهَا وَتَرَى النَّاسَ سُكَارَىٰ وَمَا هُم بِسُكَارَىٰ وَلَـٰكِنَّ عَذَابَ اللَّـهِ شَدِيدٌ"
“Enyi watu! Mcheni Rabb wenu, hakika zilizala la Saa (Qiyaamah) ni jambo kuu • Siku mtakapoiona, kila mnyonyeshaji atamsahau anayemnyonyesha, na kila mwenye mimba ataizaa mimba yake, na utawaona watu wamelewa, kumbe hawakulewa lakini ni Adhabu ya Allaah kali”. [Al-Hajj: 01-02]
Tukio kama hili linapotokea, hakuna mtu anashughulika na mwingine. Analoangalia wakati huo ni kujiokoa mwenyewe kwanza. Katika Hadiyth iliyohadithiwa na Mama yetu ‘Aaishah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:
"يُحْشَرُ النَّاسُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حُفَاةً عُرَاةً غُرْلاً . قُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ، النِّسَاءُ وَالرِّجَالُ جَمِيعًا يَنْظُرُ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ؟ قَالَ صلى الله عليه وسلم: "يَا عَائِشَةُ، الأَمْرُ أَشَدُّ مِنْ أَنْ يَنْظُرَ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ" .
“Watu watakusanywa Siku ya Qiyaamah wakiwa miguu peku peku, uchi wa mnyama bila nguo, hawajatahiriwa”.. Bibi ‘Aaishah alishtuka na kusema:
“Ee Rasuli wa Allaah! Na wanawake na wanaume wote watatazamana (nyuchi)! Rasuli akamwambia: Ee ‘Aaishah! Mambo yatakuwa ni magumu mno kuweza hata kuangaliana”. [Swahiyh Al-Bukhaariy (6527)]
Hawatoweza kuangaliana kutokana na kizaa zaa cha Siku hiyo, kila mtu roho juu juu akiifikiria nafsi yake tu, hata Mitume pia, isipokuwa Muhammad (Swalla Allaah ‘alyhi wa aalihi wa sallam) ambaye atakuwa anauombea umati wake badala ya nafsi yake. Tutafufuliwa bila kitu chochote, vyote tulivyokuwa navyo hapa duniani, tutakuwa tuliviacha tulipoiaga dunia, na tutarudi tena kwa Allaah kama ile siku ya mwanzo Alipotuumba.
"كَمَا بَدَأْنَا أَوَّلَ خَلْقٍ نُّعِيدُهُ ۚ وَعْدًا عَلَيْنَا ۚ إِنَّا كُنَّا فَاعِلِينَ"
“Kama Tulivyoanza umbo la awali Tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu Yetu. Hakika Sisi Ni Wenye Kufanya”. [Al-Anbiyaa: 104]
Tukio hili ni nafasi kwetu ya kuwa tunakumbushwa. Ndugu zetu waliofariki walikuwa ndani ya majumba yao wakiwa katika hali ya usalama na amani. Lakini nyumba hizo hizo zikageuka ghafla na kuwa zana ya kuwatoa uhai wao. Ghafla bila kutarajia wamejikuta washahamia kwenye maisha mengine ya barzakh kusubiri baragumu la pili la Qiyaamah. Wengi wetu tunakiona Qiyaamah kama vile kiko mbali sana. La hasha! Kiko karibu sana kuliko tunavyodhania. Mtu unapokufa, basi Qiyaamah chako kidogo kishasimama, kwa maana unakuwa umeshaingia katika duara la kwanza la Qiyaamah la maisha ya kaburini ukisubiri duara la pili la Qiyaamah kikuu cha kufufuliwa na kutoka makaburini, na kisha yanayofuatia baada ya hapo. Tujiandae vyema kwa hayo yote.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
30: Zoezi La Kila Siku:
Kila siku tunalala na kuamka. Kabla ya kulala, tunatayarisha vizuri kitanda kwa ajili ya kupata usingizi mzuri. Baada ya kupanda kitandani, huwa tunajaribu kuutafuta usingizi. Usingizi huu kama ujulikanavyo ni mauti madogo. Na mauti haya madogo, yaani usingizi wenyewe, hauji ila baada ya roho kutoka mwilini. Unastukia tu usingizi umekuchukua bila kujua umekujaje. Hapo roho inakuwa imetoka mwilini, kwani usingizi hauji ila kwa kutoka roho mwilini. Yeyote umwonaye kalala, basi ujue roho yake haipo, hapo anakuwa ndani akossa madogo. Viungo vyake vyote vya nje vinakuwa vimetulia tuli, na kinachobakia kikifanya kazi ni masikio tu. Allaah Anatuambia:
"اللَّـهُ يَتَوَفَّى الْأَنفُسَ حِينَ مَوْتِهَا وَالَّتِي لَمْ تَمُتْ فِي مَنَامِهَا ۖ فَيُمْسِكُ الَّتِي قَضَىٰ عَلَيْهَا الْمَوْتَ وَيُرْسِلُ الْأُخْرَىٰ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ"
“Allaah Huzichukua roho wakati wa kufa kwake, na zile zisizokufa katika usingizi wake, kisha Huzizuia ambazo Amezikidhia mauti, na Huzirudisha nyingine mpaka muda maalumu uliokadiriwa. Hakika katika hayo bila shaka kuna ishara kwa watu wanaotafakari”. [Az-Zumar: 42]
Ndio maana Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anaamka husema akimshukuru Allaah:
"الحَمْدُ لله الذِيْ أَحْيَانَا بَعْدَ مَا أَمَاتَنَا وَإِلَيْهِ النُّشُوْرُ"
“Himdi ni Yake Allaah Ambaye Ametuhuisha (Ametuamsha) baada ya Kutufisha (Kutupa usingizi), na Kwake ndio ufufuo”. [Al-Bukhaariy (6324)]
Hivyo basi, usingizi wetu huu ni kama zoezi la kila siku la kuandaliwa akossa makubwa ya roho kutoka na kutorejea tena mwilini. Mauti hayo ni tofauti na haya madogo. Hayo yana sakaraat, yana vishindo, yana kufunuliwa pazia la kumwona Malaika wa kutwaa roho (Malakul Mawt) na Malaika wengineo wa adhabu au wa rahmah, na mengi mengineyo yanayohusiana na zoezi hilo na yanayofuatia. Hapo tutaona yote tunayohadithiwa na Qur-aan kwa mujibu wa hali ya mtu. Allaah Anatuambia:
"لَّقَدْ كُنتَ فِي غَفْلَةٍ مِّنْ هَـٰذَا فَكَشَفْنَا عَنكَ غِطَاءَكَ فَبَصَرُكَ الْيَوْمَ حَدِيدٌ"
“(Aambiwe): Kwa yakini ulikuwa katika mghafala na haya! Basi Tumekuondoshea kifuniko chako, basi kuona kwako leo ni kukali”. [Qaaf: 22].
Ndugu Muislamu! Kama unavyotandika kitanda chako kwa shuka nzuri, mito mizuri na mablanketi mazuri ili upate usingizi mnono, basi ujue kitanda hiki pia ni kama kaburi lako dogo la mauti madogo. Na kama unavyokitayarisha hivyo, basi litayarishe pia kaburi lako kubwa baada akossa makubwa kwa kila amali njema, na kujiepusha na kila baya, madhambi, dhulma na akossa mengineyo. Hilo haliepukiki, na safari yake ni ndefu.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
31: Tuwe Tayari Kwa Majibu:
Kila kitu kinachotoka kwenye mwili wa mwanadamu kinaonekana ni kichafu kuanzia haja ndogo na kubwa, jasho la mwili, kamasi, kohozi, mate na hata manii ambayo ndio tumeumbwa nayo. Kila kimoja kati ya hivi kinatofautiana na kingine kwa mujibu wa kilivyo. Na hata matapishi ambayo ni chakula kizuri kilichoingia tumboni na kuanza kuchakatwa, kama yatatoka mtu akatapika, basi watu kuyaangalia mara mbili inakuwa ni mtihani. Matapishi haya ndiyo huja kufyonzwa na mwili na kupelekwa maeneo tofauti ikiwemo sehemu ya kutengenezewa maji ya uzazi ambayo hatimaye hutulia katika sehemu yake kusubiri yachupishwe na kutulia kwenye ukuta wa tumbo la uzazi na kuanza mchakato baada ya mchakato hadi mtu kuzaliwa. Wote tumepitia mchakato huo, hakuna wa kubisha. Na hata manii hayo pia yanaonekana ni kitu kichafu ingawa si najisi.
Mada hizi zinazotoka mwilini kama hazikuangaliwa kwa usafi stahiki, basi mtu atakuwa hakaribiki kutokana na harufu. Mtu akivaa soksi kwa siku mbili mfululizo bila kubadili, bila shaka ataudhi watu sana kwa harufu kali ya miguu. Mtu akilala, hata akapiga mswaki kabla ya kulala, akiamka atakuta kinywa kimekwishataghayuri kwa harufu. Nguo nazo inabidi kubadili takriban kila siku, la sivyo mambo yataharibika.
Hali hii ya maumbile yetu, huenda Allaah Ametuumbia nayo ili tujitathmini na kuondosha sifa ya kiburi. Ni kama tunaambiwa kuwa ukiwa hai hali yako ni hii, sasa ukifa, basi mambo yatakuwaje! Na kwa ajili hiyo, mtu akifa tunaamuriwa tumzike haraka iwezekanavyo kabla hajaanza kuharibika. Hapa hakuna tofauti kati ya tajiri wala masikini, wala kiongozi wala raia, wote ni hali moja.
Huenda pia hali hii ikatufanya tupate ladha halisi ya Pepo, kwa kuwa Peponi hakuna hali kama hizo. Mtu mwenye njaa kali, ndiye anayehisi ladha halisi ya chakula hata kwa kipande cha mkate mkavu, kama huna njaa, basi hata chakula kiwe kizuri vipi, hutoweza kuburudika nacho itakikanavyo.
Kadhalika, inawezekana kuwa Allaah Anatutakia kheri zaidi kutokana na maumbile haya. Anataka tupate thawabu zaidi wakati tukijitahidi kwa usafi ili tusiwaudhi watu kwa harufu za kinywa, harufu ya kikwapa na harufu nyinginezo. Muislamu hulipwa thawabu kwa juhudi kama hizi za usafi, na ni jambo ambalo Allaah pia Hulipenda kama Anavyosema:
"إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ"
“Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia mara kwa mara, na Anapenda wenye kujitwaharisha”. [Al-Baqarah: 222]
Kiufupi, huenda hali hii ya vinavyotoka mwilini inatukumbusha pia kwamba sisi ndio tuliokirimiwa zaidi kuliko viumbe wengine kwa upande wa vyakula, mbogamboga, matunda na vinywaji ambayo imepelekea maumbile yetu yawe hivi. Hebu jaribu kuhesabu aina za vyakula, aina za mbogamboga, aina za matunda, aina za vinywaji nk. Hesabu aina za mafuta ya kupikia, samli za aina tofauti na vinginevyo vingi. Hivi vyote tunavila na kuvinywa na kuingia ndani ya miili yetu. Ni neema kubwa kwa kweli. Wanyama wala nyama ni nyama tu basi, hawahitaji tunda wala chai, ndege walao nafaka au wadudu, ni hivyo tu walavyo basi, hawahitajii juisi wala kahawa. Lakini sisi na hasa wenye uwezo, vinavyoliwa havihesabiki. Na haya yote tutakwenda kuulizwa ni vipi tuliyatumia. Hakuna neema ya bure tu hivi.
"ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ"
“Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema”. [At-Takaathur: 08]
Tujiandae na majibu katika Siku hiyo ngumu kabisa.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
32: Ni Muda Mfupi Sana:
Mtu akilala na kuamka, ukamuuliza hapo hapo ni saa ngapi, bila shaka hawezi kukujibu. Ili kukujibu, ataitafuta saa. Ukimuuliza ni masaa mangapi kalala, pia hawezi kuwa na jibu.
Na mtu aliyepoteza fahamu pia, kwa ajali au kwa sababu nyingine yoyote, akirudisha fahamu, basi hawezi kujua muda aliopoteza fahamu mpaka aambiwe na yote yaliyojiri.
Vijana waliokimbilia pangoni, Allaah Aliwalaza kwa muda wa miaka 309. Lakini Alipowaamsha, walihisi kama wamelala kwa muda wa siku moja tu au sehemu ya siku. Hawakujua kabisa kama wamelala muda wote huo wa karne tatu. Haya yote ni kwa kuwa wakati mtu anapolala, anakuwa hana tena mahusiano na wakati. Kwa kuwa tunapokuwa macho, wakati tunauhisi kwa kufuatilia mwenendo wa jua, au kwa kutizama saa na kadhalika. Mtu kama hana saa, wala halioni jua, hawezi kabisa kujua wakati. Ni kama watu waliofungwa jela ndani ya jela.
Na wakati tutakapokufa, tutaingia katika kanuni nyingine kabisa tofauti na kanuni za maisha yetu ya dunia. Huko hakuna jua la kutujulisha wakati, au mwezi wa kutujulisha miezi au miaka. Angalia -kama inavyotueleza Qur-aan- mfano wa mtu yule aliyepita kwenye kijiji, akakikuta kimeporomoka na kubaki magofu tu. Akajiuliza vipi Allaah Ataweza kukirejesha tena kama kilivyokuwa pamoja na watu wake waliokuwa wakiishi ndani yake?! Allaah Akamfisha mtu yule kwa muda wa miaka 100. Alipomfufua, Akamuuliza -kupitia kwa Malaika Wake- muda aliokaa pale akiwa maiti. Akajibu ni siku moja au baadhi ya siku. Ni sawasawa na walivyohisi vijana wa pangoni. Allaah Akamwambia kwamba amekaa pale kwa muda wa miaka 100, na chakula chake hakikuharibika wala kinywaji chake, lakini punda wake tu aliyekufa ndiye aliyebakia mifupa. Haya yote yanaelezwa na Aayah ya 259 ya Suwrat Al-Baqarah kuonyesha Uwezo wa Allaah.
Wengi wetu tunakiona Qiyaamah kama kiko mbali sana, na kwamba kwenye makaburi tutakaa sana kukisubiri. La hasha! Kiko karibu kuliko tunavyodhania. Tutakapokufa, basi hapo kaburini kwenye maisha ya barzakh, ndio tutakuwa kwenye kituo cha kwanza cha aakhirah. Hapo hakuna saa ya kujua wakati, au jua la kuzama na kuchwa la kutujulisha siku mpya, au mwezi wa kutujulisha mwezi mpya wa hijria, huko mambo ni mengine kabisa. Watu watakuwa wanapambana na adhabu za kaburi, au wananeemeka na neema zake, huko pengine kuna nyakati za kihuko tofauti na za kidunia. Tahamaki, watashitukia baragumu la pili linapulizwa na wanatoka makaburini kukabiliana na mengineyo yanayofuatia baada ya kufufuliwa. Rabbi tunaomba Hifadhi Yako Siku hiyo ngumu kabisa. Tunaomba tuwe salama kwenye Kivuli Chako. Tunaomba Tusalimike na kitisho na kizaazaa kikubwa cha Siku hiyo.
Hapo waliokaa makaburini miaka mamilioni, na waliokaa kwa wiki, wote watajiona kama wamekaa huko siku moja au sehemu ya siku tu. Qaabiyl na Haabiyl wakifufuliwa leo, basi watajiona kama wamekaa makaburini kwao siku moja tu au sehemu ya siku.
"كَأَنَّهُمْ يَوْمَ يَرَوْنَهَا لَمْ يَلْبَثُوا إِلَّا عَشِيَّةً أَوْ ضُحَاهَا"
“Siku watakapoiona, watakuwa kama kwamba hawakubaki (duniani au makaburini) isipokuwa jioni moja au mchana wake”. [An-Naazi’aat: 46]
Na hapa ndipo tutakuja kugundua kwamba si umri wa ulimwengu, wala umri wa dunia yetu, wala umri wa maisha yetu ya duniani na ya barzakh, isipokuwa ni muda mfupi na mchache sana.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
33: Neema Ya Chakula:
Kila siku tunakula na kunywa. Tukitaamuli safari ya chakula tulichotengewa mezani au mkekani, tutakuta safari yake ni ndefu kuanzia kilipokuwa mbegu shambani, kukua hadi kukomaa, kuvunwa na kufikishwa sokoni hadi mezani mbele yako. Hii ni katika neema kubwa za Allaah ambazo wengi tunaghafilika nayo. Allaah Akituzindusha kuhusu neema hii Anatuambia:
"فَلْيَنظُرِ الْإِنسَانُ إِلَىٰ طَعَامِهِ • أَنَّا صَبَبْنَا الْمَاءَ صَبًّا • ثُمَّ شَقَقْنَا الْأَرْضَ شَقًّا • فَأَنبَتْنَا فِيهَا حَبًّا • وَعِنَبًا وَقَضْبًا • وَزَيْتُونًا وَنَخْلًا • وَحَدَائِقَ غُلْبًا • وَفَاكِهَةً وَأَبًّا • مَّتَاعًا لَّكُمْ وَلِأَنْعَامِكُمْ"
“Basi atazame mwana Aadam chakula chake • Kwamba Sisi Tumemimina maji kwa uneemefu • Kisha Tukaipasua ardhi ikafunguka (kwa mimea) • Tukaotesha humo nafaka • Na mizabibu na mimea ya mboga (ikatwayo ikamea tena) • Na mizaituni na mitende • Na mabustani yaliyositawi na kusongamana • Na matunda na majani ya malisho ya wanyama • Yakiwa ni manufaa kwenu na kwa wanyama wenu wa mifugo”. [‘Abasa: 24-32].
Kila neema tuliyopewa na Allaah, basi tujue ina thamani yake, na thamani yake ni kuitunza vyema, kuitumia vyema na kumshukuru Allaah. Kila neema tuliyonayo, iwe ndogo, iwe kubwa, basi kwa hakika, bila shaka, tutakuja kuulizwa Siku ya Qiyaamah. Allaah Anatuambia:
"ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ "
“Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema. [At-Takaathur: 08]
Miongoni mwa vipengele vya kushukuru neema ya chakula au kinywaji, ni kumhimidi Allaah baada ya kumaliza kula. Matamshi mengi ya himdi na du’aa yamethibiti toka kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumaliza kula. Kati yake ni:
1- "الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي كَفَانَا وَأَرْوَانَا، غَيْرَ مَكْفِيٍّ، وَلاَ مَكْفُورٍ"
“Himdi Anastahiki Allaah Ambaye Ametutosheleza mahitajio yetu na Akatuondoshea kiu, hazilipiki (Fadhila Zake) wala hazikanushiki”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5459)].
2- "الْحَمْـدُ للهِ حَمْـداً كَثـيراً طَيِّـباً مُبـارَكاً فِيْهِ، غَيْرَ مَكْفِيٍّ وَلا مُوَدَّعٍ وَلا مُسْتَغْـنىً عَنْـهُ رَبَّـنا"
“Himdi Anastahiki Allaah, himdi zilizo nyingi, zilizo njema na zilizojaa baraka tele ndani yake, haziwezi kulipika, wala kuachwa, wala kutohitajiwa tena, ee Rabbi wetu”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (5458), Abu Daawuwd (3849), Ibn Maajah (3284 na Ahmad (5/256)].
3- "الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِيْ أَطْعَمَ وَسَقَى وَسَوَّغَهُ وَجَعَلَ لَهُ مَخْرَجًا"
“Himdi Anastahiki Allaah Ambaye Amelisha, Amenywesha, Akakifanya (chakula) kuwa chepesi kuingia mwilini, na Akakiwekea njia ya kutoka mwilini.” [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Abu Daawuwd (3851) na Ibn As-Sunniy].
4- "اللّهُمَّ أَطْعَمْتَ وَسَقَيْتَ وَأَغْنَيْتَ وَأَقْنَيْتَ وَهَدَيْتَ وَأَحْيَيْتَ، فَلَكَ الحَمْدُ عَلَى مَا أَعْطَيْتَ"
“Ee Allaah! Umelisha, Umenywesha, Umetosheleza, Umekinaisha, Umeongoa, na Umehuisha. Basi ni Yako Himdi kwa yote Uliyotoa”. [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Ahmad katika “Al-Musnad” nambari 1600].
Duaa hizi ni sehemu ya kutusaidia maswali yanayotusubiri Siku hiyo.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
34: Vinywaji Ni Katika Neema Kubwa Kwetu:
Tukijaribu kuhesabu vinywaji vya halali tunavyotumia, bila shaka tutakuta ni vingi sana kuanzia vya moto hadi vya baridi. Tuna chai ambayo inajulikana na watu wote na imekuwa ni katika biashara kubwa zinazoongoza duniani ikifuatiwa na kahawa. Tuna maziwa, vinywaji baridi vya aina mbalimbali, juisi na kadhalika bila kusahau maji ambayo yanawashirikisha viumbe wote hai.
Vinywaji vyote hivi tunavyovitumia, ni katika neema kubwa kabisa tulizokirimiwa na Allaah Ta’aalaa kama wanadamu kulinganisha na viumbe wengine. Na kwa ajili hiyo, tunatakikana tuitumie neema hii kwa njia inayomridhisha Allaah kwa kutokufanya israfu au mengine yasiyostahiki kama Anavyotuambia:
"وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ"
“Na kuleni na kunyweni, na wala msifanye israfu, hakika Yeye (Allaah) Hapendi wanaofanya israfu”. [Al-A’araaf: 31]
Israfu ni tabia mbaya inayomchukiza Allaah. Tabia hii inahatarisha mtu kunyan’ganywa neema yoyote aliyopewa na Allaah Mtukufu. Israfu ni kutumia kitu katika halali lakini kwa ziada isiyohitajika. Mfano mdogo tu ni yale yanayoshuhudiwa kwenye mialiko ya walima na mingineyo ambapo sinia ya kuliwa na watu sita, wanawekewa watu wawili tu, na kinachobaki kinamwagwa. Tabia hii kwa kiasi kikubwa imepungua sana pengine kutokana na gharama za maisha kupanda, au watu kiasi fulani kujirekebisha na tabia hiyo.
Ili kujiepusha na israfu, kwa mfano, kama una kiu kidogo, basi weka maji kiasi tu cha kumaliza kiu chako. Usije kujaza gilasi, maji yakakushinda, kisha ukayamwaga. Hayo unayoyamwaga ni sehemu ya Neema ya Allaah ambayo utakuja kuulizwa Qiyaamah.
Tujiepushe na israfu katika vinywaji ili kuidumisha neema hiyo. Tusishangae kuona nchi mbalimbali zikikabiliwa na ukame wa muda mrefu unaoleta maafa hata kwa mifugo. Huenda ni baadhi ya matokeo ya israfu zetu.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
35: Jela Ya Buwlas:
Wote bila shaka tunaiogopa jela kutokana na madhila na hali mbaya ya kimaisha iliyomo humo. Kuna jela kwenye baadhi ya nchi zimejaa ukatili na unyama ambao umevuka mipaka yote ya kiutu. Kuna zingine mtu akiingia huko hatoki tena, na hata akitoka, basi hata jamaa zake wanashindwa kumtambua kutokana na alivyochakarishwa humo. Hii ni mbali na kukosa uhuru wa mtu aliouzoea, kwani maisha humo ni amri tupu. Wafungwa wanaweza kuamriwa kulala saa 11 jioni na kuamka saa 10 alfajiri. Lakini kutokana na hali hiyo, inabidi kuzoea tu.
Hii kwa kifupi ndio jela ya dunia. Sasa huko aakhirah, kuna jela inayojulikana kama “BUWLAS”. Jela hii ni mahususi kwa wote wenye kiburi hapa duniani. Kiburi maana yake ni kuikataa haki iliyo dhahiri yenye ushahidi kamili. Ni kama Firauni alivyokataa kumwamini Muwsaa (‘Alayhis Salaam) pamoja na muujiza aliouona ambao uliwafanya wachawi mabingwa waamini na kuporomoka kusujudu. Kiburi pia ni kuwadharau watu kutokana na hali aliyonayo mtu ya utajiri, au cheo, au mamlaka, au elimu, au utaifa, ukabila na kadhalika. Wote wenye tabia hizi, basi wanasubiriwa na jela hii ya “Buwlas”.
Jela hii ikoje? Wenye kiburi watafufuliwa vipi Siku ya Qiyaamah kabla ya kuswekwa humo? Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam) anasema:
"يُحْشَرُ الْمُتَكَبِّرُونَ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَمْثَالَ الذَّرِّ فِي صُوَرِ الرِّجَالِ، يَغْشَاهُمُ الذُّلُّ مِنْ كُلِّ مَكَانٍ، فَيُسَاقُونَ إِلَى سِجْنٍ فِي جَهَنَّمَ يُسَمَّى بُولَسَ، تَعْلُوهُمْ نَارُ الأَنْيَارِ يُسْقَوْنَ مِنْ عُصَارَةِ أَهْلِ النَّارِ طِينَةِ الْخَبَالِ ". قَالَ أَبُو عِيسَى هَذَا حَدِيثٌ حَسَنٌ.
“Wenye kiburi watakusanywa Siku ya Qiyaamah (kwenye uwanja wa mahshar) wakiwa mfano wa chembe ndogo mno iliyo katika umbo la mwanaume, na watafunikwa na udhalili kutoka kila mahali. Halafu wataswagwa kupelekwa kwenye jela iliyoko ndani ya Jahannam iitwayo “Buwlas”. Moto wa mioto utawafunika juu yao, na watanyweshwa usaha na taka mwili za watu wa motoni (ambazo ni) “Twiynatul Khabaal”. [At-Tirmidhiy: (2492)]
Watakuwa wanakanywagwa na watu hapo ikiwa ni malipo ya mfano wa kiburi walichokuwa nacho hapa duniani.
Tusisahau kwamba neema zote tulizonazo tumetunukiwa na Allaah kama majaribio. Tusije kujisahau tukaingia kwenye kundi hili tukaishilia kusekwa kwenye jela ya “Buwlas”.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
36: Walevi Nao Wanasubiriwa Na “Twiynatul Khabaal”:
Pombe inavyoonekana ni suala ambalo limekuwa la kawaida. Tumewahi kuwasikia hata baadhi ya Waislamu tena wenye umaarufu mkubwa wakikiri hadharani kwamba wanakunywa. Hawa ima nyoyo zao zishasusuwaa; hawajali tena wala kumwogopa Allaah, au pengine hawajui hatari ya hatima mbaya inayowasubiri kesho aakhirah.
Pombe yenyewe kwanza imelaaniwa pamoja na wadau wake wote akiwemo mtengenezaji, mnywaji, mnunuzi, mhudumu na kadhalika. Na laana watu wanaichukulia kama ni kitu kidogo tu. Laana maana yake ni kuwekwa mbali na Rahma ya Allaah kama ilivyomtokea Ibliys, na hatima yake ni motoni tu, na anayekunywa au kuhusika nayo kwa namna moja au nyingine, basi hatima yake ni sawa na ya Ibliys.
Isitoshe, huko ndani ya moto wa Jahannam, wanywaji pombe watanyweshwa kile alichokiita Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ni “Twiynatul Khabaal” pale aliposema:
"كُلُّ مُسْكِرٍ حَرَامٌ، إِنَّ عَلَى اللَّهِ عَهْدًا لِمَنْ يَشْرَبُ الْمُسْكِرَ أَنْ يَسْقِيَهُ مِنْ طِينَةِ الْخَبَالِ. قَالُوا: يَا رَسُولَ اللَّهِ وَمَا طِينَةُ الْخَبَالِ؟ قَالَ: عَرَقُ أَهْلِ النَّارِ أَوْ عُصَارَةُ أَهْلِ النَّار"
“Kila kinacholewesha ni haramu. Na kwa hakika Allaah Amemwekea ahadi mwenye kunywa chenye kulewesha kwamba Atamnywesha “Twiynatul Khabaal”. Wakauliza ni nini “Twiynatul Khabaal?”. Akasema: Ni jasho la watu wa motoni, au ni usaha wa watu wa motoni”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (2002), An Nasaaiy (8/327) na Ahmad (3/321)].
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
37: Tusipoteze Nafasi Hii Ya Kuombewa Maghfirah:
Kati ya Fadhila kubwa kabisa za Allaah kwetu sisi kama Waumini, ni kuwafanya Malaika Wake Watukufu watuombee maghfirah Kwake na Atukinge sisi na adhabu ya Jahiym. Malaika hawa ni wengi kuliko wanadamu kwa idadi kubwa mno ambayo hakuna aijuaye ila Allaah Mtukufu. Na kwa wingi huu, kwa hakika, Waislamu watakuwa wananufaika sana kutokana na du’aa za Malaika hawa wote ambao daima humsabbih Allaah na kumhimidi.
Wanaoongoza kwa duaa hiyo ni Malaika wabebao ‘Arshi ya Allaah ambayo ndio kiumbe kikubwa zaidi kuliko vyote, kizuri kuliko vyote na kilicho karibu zaidi kwa Allaah Ta’aalaa. ‘Arshi hii Tukufu imeenea ardhi yote, mbingu zote, pamoja na Kiti Chake. Malaika hawa kupewa kazi hii ya kubeba ‘Arshi inaonyesha kuwa ndio Malaika wakubwa zaidi na wenye nguvu zaidi kuliko viumbe wote. Na Allaah kuwachagua kubeba ‘Arshi hii, inaonyesha kuwa wao ndio Malaika bora kabisa kuliko wengineo, nao ndio walio karibu zaidi na Allaah.
Lakini, ni yepi masharti ya sisi kuweza kunufaika na tunukio hili na takrima hii kubwa kabisa ya Allaah ya kuombewa maghfira na rahmah na Malaika hao wabebao ‘Arshi na wengineo walio pembezoni mwake? Jibu la swali hili liko katika Aayah hii ya saba ya Suwrat Ghaafir:
"الَّذِينَ يَحْمِلُونَ الْعَرْشَ وَمَنْ حَوْلَهُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ وَيُؤْمِنُونَ بِهِ وَيَسْتَغْفِرُونَ لِلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا وَسِعْتَ كُلَّ شَيْءٍ رَّحْمَةً وَعِلْمًا فَاغْفِرْ لِلَّذِينَ تَابُوا وَاتَّبَعُوا سَبِيلَكَ وَقِهِمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ"
“(Malaika) ambao wanabeba ‘Arsh na walio pembezoni mwake, wanasabbih na kumhimidi Rabbi wao, na wanamwamini, na wanawaombea maghfirah wale walioamini (wakisema): Rabb wetu! Umekienea kila kitu kwa rahmah na ujuzi, basi Waghufurie wale waliotubu, na wakafuata Njia Yako, na Wakinge na adhabu ya moto uwakao vikali mno”. [Ghaafir: 07]
Masharti haya ni:
Kwanza: Kuwa na iymaan ya kikweli mbali na unafiki na shirki.
Pili: Kutubia toba ya kikweli kwa kila kosa kwa masharti yake manne yajulikanayo. Mtu atubie kila anapofanya kosa, kwani mwanadamu ni mkosaji wa mara kwa mara.
Tatu: Kufuata kikamilifu Njia ya Allaah kwa uthabiti na uimara kwa mujibu wa Qur-aan na Sunnah.
Tukitekeleza masharti haya, basi tutaingia moja kwa moja ndani ya duara hili. Hakika Mapenzi ya Allah kwa Waumini ni makubwa sana. Na tukijaaliwa kuingia, hivi kuna dhambi tutabaki nalo?
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
38: Baadhi Ya Vitendo Vinavyoingiza Ndani Ya Duara La Kuombewa Maghfirah Na Malaika:
Haya ni miongoni mwa mambo mengineyo ambayo yatakuingiza ndani ya wigo wa kuombewa maghfirah na Malaika.
1- Kusubiri swala ya jamaa msikitini na kukaa baada ya kumalizika swala. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"إِنَّ الْمَلاَئِكَةَ تُصَلِّي عَلَى أَحَدِكُمْ مَا دَامَ فِي مُصَلاَّهُ الَّذِي صَلَّى فِيهِ مَا لَمْ يُحْدِثِ : اللَّهُمَّ اغْفِرْ لَهُ، اللَّهُمَّ ارْحَمْهُ"
“Hakika Malaika wanamwombea mmoja wenu madhali amebakia sehemu yake aliyoswalia na kuwa hajatengukwa na wudhuu wake. (Wanasema): Ee Allaah, Mghufurie, ee Allaah Mrehemu”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Al-Bukhaariy (659) na Muslim (649)]
Mwanamke anaweza kuipata fadhila hii kama atakuwa na sehemu yake mahsusi ya kuswalia nyumbani kwake.
2- Kuswali safu ya kwanza.
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"إِنَّ اللَّهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى الصَّفِّ الْأَوَّلِ"
“Hakika Allaah na Malaika Wake Huwaswalia wanaoswali safu ya kwanza”. [Hadiyth Swahiyh. Swahiyh Ibn Maajah]
Kuwaswalia hapa kuna maana ya kwamba, kwa upande wa Allaah ni kuwasifu na kuwarehemu, na kwa Malaika ni kuwaombea maghfirah.
Baadhi ya Waumini utawaona wamewahi kuingia msikitini na safu ya kwanza haina watu. Badala ya kuwahi na kukaa safu hiyo ili wapate fadhila hii, hukaa safu za nyuma. Pengine hawajui fadhila hii, au wanaona safu ya kwanza ni ya watu maalum. Hili ndilo la watu kulishindania, kwani kheri zake ni kubwa.
3- Kutafuta ‘ilmu.
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"مَنْ سَلَكَ طَرِيقًا يَطْلُبُ فِيهِ عِلْمًا سَلَكَ اللَّهُ بِهِ طَرِيقًا مِنْ طُرُقِ الْجَنَّةِ وَإِنَّ الْمَلاَئِكَةَ لَتَضَعُ أَجْنِحَتَهَا رِضًا لِطَالِبِ الْعِلْمِ وَإِنَّ الْعَالِمَ لَيَسْتَغْفِرُ لَهُ مَنْ فِي السَّمَوَاتِ وَمَنْ فِي الأَرْضِ وَالْحِيتَانُ فِي جَوْفِ الْمَاء"
“Mwenye kupita njia kwa lengo la kutafuta ‘ilmu, basi Allaah Atampitisha kwayo njia katika njia za Peponi. Na kwa hakika Malaika hushusha mbawa zao kuonyesha kufurahishwa kwao na mwanafunzi mtafutaji ‘ilmu. Na kwa hakika (pia), aliyeelimika, huombewa maghfirah na walioko mbinguni na walioko ardhini, na (hata) samaki walioko ndani ya kina cha maji”. [Sunan Abu Daawuwd].
Angalia hapa, si tu kwamba anapewa hishma kubwa na Malaika ya kushushiwa mbawa zao, bali hata viumbe vyote vilivyoko mbinguni kati ya Malaika wengineo wakiwemo wale wabebao ‘Arshi ya Allaah, pamoja na viumbe vinginevyo tusivyovijua huko, mbali na viumbe vyote vilivyoko ardhini hata vile tunavyovidharau kama nzi, panya, chawa na kadhalika, isitoshe na vyote vilivyoko ardhini, -vyote hivyo kwa wingi wote huo wa idadi isiyoweza kukokotoleka- vinamwombea maghfirah mwanafunzi anayetafuta ‘ilmu. Na ‘ilmu inayolengwa hapa ni ‘ilmu ya dini, kwani hiyo ndiyo itakayomwongoza Muislamu katika ‘aqiydah safi, atajua vyema mambo yote ya ‘ibaadah kuanzia twahara, swala, zakah, funga, hijja na mengineyo yote kuhusu kusoma Qur-aan kama inavyotakikana, Hadiyth za Rasuli na kadhalika. Haya ndiyo yatakayomfanya kuishi kwa amani hapa duniani na kesho aakhirah.
Ama elimu za kidunia, hizi bila shaka mtu atazijua tu kwa mujibu wa utashi wake katika kutafuta riziki. Na hizi ndizo ambazo watu wamezipa kipaumbele zaidi kuliko za dini. Si ajabu ukamwona mhandisi mkubwa au mwanasiasa mashuhuri wa Kiislamu, lakini kwa upande wa dini yake, ni mtupu kabisa! Hii ni hasara kubwa itakayomfanya Muislamu yeyote asiyetafuta ‘ilmu ya dini, kuja kujuta sana Siku ya Qiyaamah.
4- Kufundisha watu mambo ya kheri.
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"إِنَّ اللَّهَ وَمَلاَئِكَتَهُ وَأَهْلَ السَّمَوَاتِ وَالأَرْضِ حَتَّى النَّمْلَةَ فِي جُحْرِهَا وَحَتَّى الْحُوتَ لَيُصَلُّونَ عَلَى مُعَلِّمِ النَّاسِ الْخَيْرَ"
“Hakika Allaah na Malaika Wake, pamoja na wakazi wa mbingu na ardhi, hata mdudu chungu katika shimo lake, na hata samaki, wanamwombea mwenye kuwafundisha watu mambo ya kheri”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na At-Tirmidhiy (2685) na At-Twabaraaniy (8/278)]
Mwalimu wa mambo ya kheri anayekusudiwa hapa ni Mwanachuoni, kwani yeye huwafundisha watu Maamrisho ya Allaah na kuwaonyesha Makatazo Yake ili wayaepuke, na mambo mengineyo yatakayowafaa katika dunia yao na aakhirah yao.
Ni wangapi kati yao wameshafariki zamani, lakini elimu zao hadi leo zinaendelea kuwanufaisha Waislamu. Na hii ina maana kuwa bado nao wanaendelea kuombewa na wote waliotajwa katika Hadiyth hii ingawa wako makaburini!
Lakini pia, hata yeyote anayesambaza elimu ya dini kwa njia ya mitandao kama tunavyoona vijana wetu hivi leo, basi wanaingia ndani ya duara la wigo huu, kuanzia wanaotarjumi, wanao-edit, wanaosambaza na kadhalika. Allaah Awalipe wote jazaa njema.
5- Kumswalia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam)
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَا مِنْ مُسْلِمٍ يُصَلِّي عَلَىَّ إِلاَّ صَلَّتْ عَلَيْهِ الْمَلاَئِكَةُ مَا صَلَّى عَلَىَّ فَلْيُقِلَّ الْعَبْدُ مِنْ ذَلِكَ أَوْ لِيُكْثِرْ"
“Hakuna Muislamu yeyote anayeniswalia isipokuwa Malaika nao humswalia madhali anaendelea kuniswalia. Basi na mja afanye uchache kwa hilo, au akithirishe”. [Hadiyth Hasan. Ibn Maajah]
6- Kumzuru mgonjwa
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"مَا مِنْ رَجُلٍ يَعُودُ مَرِيضًا مُمْسِيًا إِلاَّ خَرَجَ مَعَهُ سَبْعُونَ أَلْفَ مَلَكٍ يَسْتَغْفِرُونَ لَهُ حَتَّى يُصْبِحَ وَكَانَ لَهُ خَرِيفٌ فِي الْجَنَّةِ وَمَنْ أَتَاهُ مُصْبِحًا خَرَجَ مَعَهُ سَبْعُونَ أَلْفَ مَلَكٍ يَسْتَغْفِرُونَ لَهُ حَتَّى يُمْسِيَ وَكَانَ لَهُ خَرِيفٌ فِي الْجَنَّةِ"
“Hakuna mtu yeyote anayemzuru mgonjwa wakati wa jioni, isipokuwa hutoka pamoja naye Malaika elfu sabini wanaomwombea maghfira mpaka apambaukiwe asubuhi, na atapata pia bustani iliyosheheni matunda Peponi. Na atakayemwendea asubuhi, hutoka pamoja naye Malaika elfu sabini wanaomwombea maghfira mpaka jioni, na atapata bustani iliyosheheni matunda Peponi”. [Hadiyth Hasan. Swahiyh Abu Daawuwd]
7- Wanaokula daku
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"إنَّ اللهَ وَمَلائِكَتَهُ يُصَلُّوْنَ عَلَى المُتَسَحِّرِيْنَ"
“Hakika Allaah na Malaika Wake wanawaswalia wenye kula daku”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Ibn Hibaan (3467)]
Kuswaliwa na Allaah kuwasifu na kuwarehemu, na Malaika ni kuombewa maghfirah kwa Allaah.
Daku ni barakah. Si lazima kula mlo kamili wa shibe, bali inatosha hata kwa funda la maji ili kupata kusifiwa na Allaah na kuombewa maghfirah na Malaika Wake.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
39: Laiti Ningelikuwa Mkia Wa Mbwa:
Kuna baadhi ya viumbe vya Allaah ambavyo tunavichukia na hata kuvilaani kutokana na madhara yake kama nzi, mbu, kunguni, na kadhalika. Viumbe hivi Allaah Ameviumba kwa sababu na hekima maalum ambazo ni vigumu sisi kuzijua. Na hata kuna wanyama wengine ambao tunawadharau kiasi cha hata kufanywa kama ni tusi kwetu. Ni kama mtu kumwambia mtu: “Wewe punda tu”, au “Wewe mbwa tu”, au “Wewe kenge tu”. Hili ni kosa kubwa la kuwadharau viumbe hawa wa Allaah, na inakuwa ni kama kumdharau Yeye, na hii ni hatari kubwa sana.
Pamoja na kuwadharau wanyama hawa, lakini kuna siku mtu atakuja kutamani laiti yeye angelikuwa mbwa au punda au hata nguruwe. Hawa ni wale watakaojikuta Siku ya Qiyaamah wakisubiriwa na hatima mbaya ya kuishilia motoni.
Siku hii, wanyama hawa wote watafufuliwa ili walipiziwe kisasi kati yao. Kondoo mwenye pembe aliyempiga mwenzake asiye na pembe, atalipiziwa naye kwa kupigwa pembe. Aliyemparua mwenzake kwa kucha au meno, naye ataparuliwa na kadhalika. Na hii yote, ni Allaah kuonyesha uadilifu Wake uliofikia ukamilifu wa juu kabisa kwa kila kitu. Na baada ya visasi kumalizika kwa wanyama wote, hapo Allaah Atawaamuru wawe mchanga, nao watageuka kuwa mchanga. Kafiri au mtu aliyejaa madhambi, atatamani hapo laiti angeliumbwa mchanga hapa duniani, au hata wanyama hao ili yasimkute magumu yanayomsubiri mbele yake. Atatamani angelikuwa hata angalau mkia wa mbwa, au sikio la nguruwe hapa duniani, kwa kuwa angelipona Siku hiyo. Lakini wapi!!
Allaah Anatuambia:
"إِنَّا أَنذَرْنَاكُمْ عَذَابًا قَرِيبًا يَوْمَ يَنظُرُ الْمَرْءُ مَا قَدَّمَتْ يَدَاهُ وَيَقُولُ الْكَافِرُ يَا لَيْتَنِي كُنتُ تُرَابًا"
“Hakika Sisi Tumekuonyeni adhabu ya karibu. Siku mtu atakapotazama yale iliyokadimisha mikono yake, na kafiri atasema: Laiti ningelikuwa mchanga”. [An-Nabaa].
Tuheshimu sana viumbe vyote vya Allaah. Kuviheshimu ni sehemu ya kumheshimu Allaah Aliyeviumba na kuvisakharisha kwa ajili ya maslaha yetu.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
40: Je, Mamba anafaa Kwa Kitoweo?
Kuna makhitilafiano baina ya ‘Ulamaa kuhusiana na uhalali na uharamu wa kula nyama na mamba.
Kundi la wenye kuhalalisha ambao ni pamoja na Jopo la Tume Ya Fatwaa Ya ‘Ulamaa wa Saudia wanasema naam, mamba anafaa kuliwa kama anavyoliwa samaki. Na hii ni kwa Kauli Yake Ta’aalaa :
"أُحِلَّ لَكُمْ صَيْدُ الْبَحْرِ وَطَعَامُهُ مَتَاعًا لَّكُمْ وَلِلسَّيَّارَةِ"
“Mmehalalishiwa mawindo ya bahari, na chakula chake ni manufaa kwenu na kwa wasafiri”. [Al-Maaidah: 96]
Na kauli yake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"هُوَ الطَّهُورُ مَاؤُهُ الْحَلاَلُ مَيْتَتُهُ"
“(Bahari) maji yake ni twahara, na maiti yake ni halali”. [Sunan An-Nasaai (4550].
Wanyama wote wanaoishi majini ni halali kuliwa akiwemo mamba. Si lazima iwe ni bahari tu, bali kwenye mito, maziwa na kadhalika.
Ama kundi la pili la walioharamisha kula mamba, wao wanasema kwamba mamba ana meno makali ya kukamatia kiwindwa chake, na Rasuli amekataza kula nyama ya wanyama au ndege wakali wanaotumia meno au kucha kuulia viwindwa vyao kama ilivyo kwenye Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas:
"نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلًى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ عَنْ ُ َكُلِّ ذِيْ نَابٍ مِنَ السِّبَاعِ، وَعَنْ كُلِّ ذِيْ مِخْلَبٍ مِنَ الطَّيْرِ"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kila mwenye meno katika wanyama wakali, na kila mwenye kucha katika ndege”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1934), Abu Daawuwd (3785) na An Nasaaiy (7/206)].
Kadhalika, wanasema kwamba mamba yuko nusu nusu; nchi kavu na majini, hivyo hawezi kuchukuliwa kuwa ni wa majini tu ili apewe uhalali wa kuliwa.
Sheikh Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahul Laah) amewajibu kwamba ndani ya bahari kuna samaki wakubwa wenye meno ya kutisha zaidi kama nyangumi, papa na kadhalika. Lakini hao wanaopinga wamehalalisha kuliwa samaki hao. Kwa nini waharamishe mamba? Halafu, mamba si kama wanyama wakali wa nchi kavu, na kwa hivyo basi, si kila cha nchi kavu kinachoharamishwa kiharamishwe mfano wake wa kilichoko majini. Isitoshe, muda wake mwingi huwa majini kuliko nchi kavu, na wingi hutangulizwa kuliko uchache.
Hayo ndio makhitilafiano kidogo kuhusu uhalali na uharamu. Angalia mwenyewe na upime, kisha chukua uamuzi.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
41: Na Fisi Je?
Naam, fisi naye anafaa kwa kitoweo. Pengine wengi watashangaa, lakini huu ndio ukweli kwamba nyama yake ni halali kuliwa. Na hii ni kwa Hadiyth ya Jaabir bin ‘Abdullaah ambaye amesema: Nilimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu fisi. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
"هُوَ صَيْدٌ وَيُجْعَلُ فِيهِ كَبْشٌ إِذَا صَادَهُ الْمُحْرِمُ"
“Ni mnyama wa kuwindwa, na hufidiwa mahala pake beberu la kondoo kama aliyevaa ihramu atamwinda”. [Hadiyth Swahiyh. Sunan Abiy Daawuwd].
Kama asingelikuwa halali, basi Rasuli asingelimfanya kondoo kuwa fidia kwa muhrim aliyemwinda fisi, na asingeliruhusu kumwinda kwa mchezo tu kama asingelikuwa halali. Kadhalika, Hadiyth hii ni mahsusi kwa fisi ikimvua toka kundi la wanyama wenye meno na makucha makali walioharamishwa kuliwa.
Ash-Shaafi’iy (Rahimahul Laah) amesema katika “Al-Ummu” (2/273):
“Na nyama za fisi zinauzwa kwetu Makkah kati ya Swafaa na Marwa, simjui yeyote katika watu wetu ambaye amepinga uhalali wake”.
Hivyo basi, fisi ni halali nyama yake bila makhitilafiano yoyote kati ya ‘Ulamaa.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
42: Vipi Na Chura?
Chura ni haramu kumla, kwa sababu Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuua vyura. Qaaidah inasema:
“Mnyama Ambaye Allaah Au Rasuli Wamekataza Kumuua Si Halali Kuliwa”.
Ni kama sisimizi, nyuki, hud-hud, tiva (shrikes) na chura. Ni kutokana na Hadiyth hii ya Ibn ‘Abbaas ambaye amesema:
"نَهَى رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ عَنْ قَتْلِ أَرْبَعِ مِنْ اَلدَّوَابِّ : اَلنَّمْلَةُ، وَالنَّحْلَةُ، وَالْهُدْهُدُ، وَالصُّرَدُ".
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuua viumbe wanne: Sisimizi, nyuki, hud-hud na tiva (shirkes)”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na An-Nasaaiy (5/189), Ahmad (6/83) na wengineo].
Hawa wote watajwa hapa, hairuhusiwi kuwaua, hairuhusiwi kuwala.
Ama katazo la kuua chura na kuwa haramu kuliwa, ni kwa Hadiyth ya ‘Abdul Rahmaan bin ‘Uthmaan ambaye amesema:
"ذَكَرَ طَبِيبٌ عِنْدَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ دَوَاءً، وذَكَرَ الضِّفْدَعً يَجْعَلُ فِيْهِ، فَنَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ عَنْ قَتْلِ الضِّفْدَع"
“Tabibu (daktari) alitaja mbele ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) dawa, na akaeleza kwamba dawa hiyo anaitengeneza kutokana na chura. Na hapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akakataza kuua chura”. [Hadiyth Hasan. Imekharijiwa na Ahmad (15197), Ad-Daaramiy (1998) na Ibn Maajah (3223)].
Kwa msingi huu, chura haliwi wala hawindwi.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
43: Na Nyoka Je?
Nyoka ni haramu kuliwa. Na hii ni kwa sababu mbili:
Ya kwanza: Kanuni ya kifiqhi inasema:
“Mnyama Ambaye Rasuli Kaamuru Kumuua Si Halali Kuliwa”.
Na kwa msingi huu, nyoka ni haramu kuliwa kutokana na Hadiyth ya ‘Abdullaah bin Mas-‘uwd (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) ambaye amesema:
" كُنَّا مَعَ النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ فِي غَارٍ وَقَدْ أُنْزِلَتْ عَلَيْهِ : ( وَالْمُرْسَلاَتِ عُرْفًا) . فَنَحْنُ نَأْخُذُهَا مِنْ فِيهِ رَطْبَةً إِذْ خَرَجَتْ عَلَيْنَا حَيَّةٌ فَقَالَ : " اقْتُلُوهَا "، فَابْتَدَرْنَاهَا لِنَقْتُلَهَا فَسَبَقَتْنَا ، فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ : "وَقَاهَا اللَّهُ شَرَّكُمْ كَمَا وَقَاكُمْ شَرَّهَا" .
“Tulikuwa pamoja na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika pango akiwa ameshateremshiwa (Wal Mursalaat ‘Urfan). Na wakati tukiwa tunaisikiliza (suwrah) toka mdomoni mwake ikiwa bado mbichi mpya, mara ghafla akatutokezea nyoka mkubwa, na Rasuli hapo hapo akatuambia: “Muueni”. Tukakimbizana haraka tuwahi kumuua lakini akawahi kutukimbia. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam) akasema: Allaah Amemlinda na shari yenu kama Alivyowalindeni nyinyi na shari yake”. [Swahiyh Muslim (2234)]
Ya pili: Nyoka ana meno anayotumia kuulia kiwindwa chake, ni sawa kwa kumdunga sumu, au kukamatia nayo. Hivyo anaingia kwenye kundi la wanyama wenye meno kwa mujibu wa Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas:
"نَهَى رَسُولُ اللَّهِ صَلًى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلًمَ عَنْ ُ َكُلِّ ذِيْ نَابٍ مِنَ السِّبَاعِ، وَعَنْ كُلِّ ذِيْ مِخْلَبٍ مِنَ الطَّيْرِ"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kila mwenye meno katika wanyama wakali, na kila mwenye kucha katika ndege”. [Hadiyth Swahiyh. Imekharijiwa na Muslim (1934), Abu Daawuwd (3785) na An Nasaaiy (7/206)].
Hivyo nyoka si halali kuliwa; si wakubwa wala wadogo.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
44: Vipi Kuhusu Paka Na Nyani?
Wawili hawa ni haramu kuwala.
Kuhusu nyani, Al-Imaam bin Qudaamah amesema kwenye Al-Mughniy: “Kula nyani hairuhusiwi, na haijuzu pia kumuuza”.
Ibn ‘Abdul Barri pia kasema: “Hakuna mvutano wowote ujulikanao baina ya ‘Ulamaa kuhusiana na kutojuzu kula nyama ya nyani au kuiuza”.
Sababu ya kuharamishwa nyani, ni kwa kuwa ana meno makali, aliwahi kubadilishwa sura na kuwa mbaya, na ni katika wanyama wabaya.
Ama paka, yeye ni haramu kwa vile ana meno na kucha. Na kwa msingi huo, anaingia yeye pamoja na nyani kwenye kundi la wanyama wenye meno makali na ndege wenye kucha kali kwa mujibu wa Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyotajwa nyuma.
Sokwe, tumbili na mfano wao wanaingia kundi la nyani.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
45: Sote Tutabanwa Na Kaburi:
Mbano wa kaburi ni jambo la kwanza analokutana nalo maiti kwenye ulimwengu wa “Barzakh”. “Barzakh” ni hali anayoishi nayo maiti kaburini hadi siku ya kufufuliwa. Hadiyth kadhaa za Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) zimethibitisha uwepo wa kubanwa maiti na kaburi.
Kati ya Hadiyth hizo:
1- Bibi ‘Aaishah: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِنَّ لِلْقَبْرِ ضَغْطَةً وَلَوْ كَانَ أَحَدٌ نَاجِيًا مِنْهَا نَجَا مِنْهَا سَعْدُ بْنُ مُعَاذِ"
“Hakika kaburi lina mbano, na lau kama kuna ambaye angeweza kuokoka nao, basi angeliokoka nao Sa’ad bin Mu’aadh”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika “As-Silsilat As-Swahiyhah” (1695)].
2- Ibn ‘Umar: Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuhusu Sa’ad bin Mu’aadh (Radhwiya Allaah ‘anhu) wakati alipokufa:
"هَذَا الَّذِي تَحَرَّكَ لَهُ الْعَرْشُ وَفُتِحَتْ لَهُ أَبْوَابُ السَّمَاءِ وَشَهِدَهُ سَبْعُونَ أَلْفًا مِنْ الْمَلَائِكَةِ ، لَقَدْ ضُمَّ ضَمَّةً ثُمَّ فُرِّجَ عَنْهُ"
“Huyu ndiye ambaye ‘Arshi ilitikisika kwa ajili yake, milango ya mbingu ikafunguliwa kwa ajili yake, na Malaika elfu 70 walihudhuria mazishi yake, huyu (aliyefanyiwa yote haya) amebanwa akabanika, kisha akaachiliwa”. [Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika “Swahiyh An-Nasaaiy”].
Kwa muktadha huu, hakuna yeyote kati yetu atakayepona na mbano huu, ni sawa awe Muislamu, awe kafiri, awe pagani na kadhalika. Kwa hiyo kila mmoja wetu ajitayarishe kwa hilo, haliepukiki, halina budi.
Lakini kwa hali yoyote, mbano kwa Muislamu ni tofauti na mbano kwa kafiri, au pagani na kadhalika. ‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na mbano kwa Muislamu katika kauli mbili:
Ya kwanza:
Kila Muislamu atabanwa, lakini Muislamu mwema atabanwa haraka, kisha kaburi litamwachia na litatanuka, na mateso kwake hayatakuwa marefu. Ama Muislamu faasik, huyu mbano utakuwa wa nguvu kubwa, na utarefuka kwa mujibu wa madhambi yake.
Abul Qaasim As-Sa’adiy (Rahimahul Laah) amesema: “Hatonusurika na mbano wa kaburi mwema wala muovu, isipokuwa kwa Muumini mwema utakuwa ni wa haraka, kaburi litamwachia na litatanuka, na mateso hayatokuwa marefu kwake. Ama faasik, huyu mbano utakuwa mkali kwake, na kibano cha mwandani wake kitarefuka kwa mujibu wa madhambi yake na maasia yake”.
Ya pili:
Waumini wema watapatwa na mbano wa kaburi, lakini mbano wao utakuwa ni wa upole na mapenzi bila adha wala maumivu. Ama Waislamu wenye kumwasi Allaah, hao mbano utakuwa mkali kutokana na hasira za kaburi kwao, na utakuwa kwa mujibu wa madhambi yao na matendo yao mabaya.
Al-Haafidh Adh-Dhahabiy (Rahimahul Laah) amesema: “Mbano huu si chochote kwa upande wa adhabu ya kaburi, bali hilo ni jambo ambalo atalikuta Muumini kama anavyopata maumivu ya kumpoteza mwanaye au kipenzi chake duniani, na kama anavyopata maumivu ya kuugua, au maumivu ya kutoka roho yake, au maumivu ya kuulizwa maswali kaburini mwake na kujaribiwa, au maumivu ya kuathirika kutokana na kuliliwa na watu wake (vilio vya kijahili), au maumivu ya kufufuliwa toka kaburini, au maumivu ya kisimamo na kizaazaa chake, au maumivu ya kupita juu ya Jahannam na mfano wa hayo. Misukosuko yote hii mtu atakutana nayo, nayo kamwe si katika adhabu ya kaburi, wala adhabu ya Jahannam. Bali mja mwema mchaji, Allaah Atamfanyia upole katika baadhi yake au yote. Basi Sa’ad ambaye tunamjua kuwa ni katika watu wa Peponi, mbali na kuwa ni katika Shuhadaa wa daraja la juu kabisa (Radhwiya Allaah ‘anhu), naye pia hajapona na misukosuko hii. Kana kwamba wewe unadhani kuwa aliyefaulu hataguswa na misukosuko ya nyumba mbili, wala vitisho, wala maumivu, wala khofu?! Mwombe Mola wako salama na amani, na Atufufue katika kundi la Sa’ad”. [Siyar A‘alaamun Nubalaa (1/290-292].
Sheikh Ibn ‘Uthaymiyn amesema: “Mbano wa ardhi kwa Muumini ni mbano wa huruma na mapenzi, ni kama mfano wa kumbatio la mama kwa mwanaye kifuani. Ama mbano wake kwa kafiri, huo ni mbano wa adhabu na mateso”.
Nini Sababu Ya Mbano Huu?
Hakuna Aayah au Hadiyth yoyote iliyoeleza sababu. Lakini baadhi ya ‘Ulamaa wamejaribu kukisia sababu.
Al-Hakiym At-Tirmidhiy amesema: “Sababu ya mbano huu ni kwamba hakuna yeyote isipokuwa atakuwa na makosa fulani hata kama ni mtu mwema. Na mbano huu utakuwa ni malipo yake, kisha rahmah itamkumbatia”.
Wengine wamesema sababu ni maasia na uchache wa kushukuru Neema za Allaah.
Lakini pamoja na makisio ya sababu hizi, tunakuta kwamba hata watoto wasio na dhambi, nao pia hawatanusurika. Abu Ayyuwb (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema: “Mtoto alizikwa, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
"لَوْ أَفْلَتَ أَحَدٌ مِنْ ضَمَّةِ الْقَبْرِ لَأَفْلَتَ هذَا الصَّبِيُّ"
“Lau angelinusurika yeyote na mbano wa kaburi, basi angenusurika mtoto huyu”. [Imesimuliwa na At-Twabaraaniy katika Al-Mu’ujamul Kabiyr (4/121). Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh katika As-Silsilat As-Swahiyhah (2164)].
Tunamwomba Allaah Atufanyie upole wakati wa kubanwa, na mbano uchukue muda mfupi iwezekanavyo, na Atuepushe na adhabu ya kaburi na adhabu ya moto. Aamiyn.
Tukumbushane
Alhidaaya.com [3]
46: Adhabu Kwa Wasiotoa Zaka:
Toka kwa Abu Hurayrah amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Hakuna yeyote mwenye hazina ya mali ambayo haitolei Zakaah, isipokuwa atapashiwa moto kwenye moto wa Jahannam, kisha ifanywe vipande vipana [vya metali], achomwe navyo mbavu zake na kipaji chake mpaka pale Allaah Atakapohukumu kati ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini. Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni. Na hakuna yeyote mwenye kumiliki ngamia na asiwatolee Zakaah yake, isipokuwa alazwa kifudifudi mbele yao kwenye ardhi pana tambarare, wakiwa wakubwa kama walivyokuwa, watamkanyaga, kila wanapomaliza kumkanyaga wa mwisho wao, wa mwanzo wao watarejeshwa kumkanyaga tena mpaka Allaah Atakapohukumu baina ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini. Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni. Na hakuna yeyote mwenye kumiliki mbuzi na kondoo na asiwatolee Zakaah yake, isipokuwa atalazwa kifudifudi mbele yao kwenye ardhi pana tambarare, wakiwa wakubwa kama walivyokuwa, watamkanyaga kwa kwato zao, na watampiga kwa pembe zao, hakuna kati yao mwenye pembe zilizopinda wala asiye na pembe, kila wanapomaliza kumkanyaga wa mwisho wao, wa mwanzo wao watarejeshwa kumkanyaga tena mpaka Allaah Atakapohukumu kati ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini katika mnayohesabu. Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni…”. [Muslim (987) na Abu Daawuwd (1642)].
Links
[1] https://www.alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/256
[2] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11815&title=Tukumbushane
[3] http://www.alhidaaya.com/sw/
[4] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11816&title=01-Tukumbushane%3A%20Khatima%20Mbaya%20
[5] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11817&title=02-Tukumbushane%3A%20Mali%20Ni%20Neema
[6] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11818&title=03-Tukumbushane%3A%20Mali%20Ni%20Niqama
[7] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11819&title=04-Tukumbushane%3A%20Mtoto%20Ni%20Neema
[8] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11820&title=05-Tukumbushane%3A%20Ulimi%20Ni%20Neema
[9] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11821&title=06-Tukumbushane%3A%20Ulimi%20Ni%20Maafa
[10] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11822&title=07-Tukumbushane%3A%20Jicho%20Ni%20Neema
[11] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11823&title=08-Tukumbushane%3A%20Jicho%20Ni%20Maafa
[12] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11824&title=09-Tukumbushane%3A%20Wakati
[13] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11825&title=10-Tukumbushane%3A%20Thawabu%20Kubwa%20Kwa%20Huduma%20Ndogo
[14] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11826&title=11-Tukumbushane%3A%20Nabiy%20Ibraahiym%20Atakataliwa%20Uombezi%20Wake%20Kwa%20Baba%20Yake%20Siku%20Ya%20Qiyaamah
[15] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11827&title=12-Tukumbushane%3A%20Mwanaume%20Usivae%20Hariri%2C%20Utaikosa%20Ya%20Peponi
[16] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11828&title=13-Tukumbushane%3A%20Allaah%20Hufurahika%20Kwa%20Toba%20Yako%20Lakini%20Shetani%20Hununa
[17] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11829&title=14-Tukumbushane%3A%20Faida%20Ya%20Hofu%20Na%20Huzuni%20Hapa%20Duniani
[18] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11830&title=15-Tukumbushane%3A%20Je%2C%20Haujafika%20Tu%20Muda%20Wa%20Wewe%20Kujionea%20Haya%20Na%20Nafsi%20Yako%3F
[19] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11831&title=16-Tkumbushane%3A%20Je%2C%20Haujafika%20Tu%20Muda%20Wa%20Wewe%20Kujionea%20Haya%20Na%20Viumbe%3F
[20] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11832&title=17-Tukumbushane%3A%20Je%2C%20Haujafika%20Tu%20Muda%20Wa%20Wewe%20Kujionea%20Haya%20Na%20Malaika%3F
[21] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11833&title=18-Tukumbushane%3A%20Je%2C%20Haujafika%20Tu%20Muda%20Wa%20Wewe%20Kujionea%20Haya%20Na%20Mtu%20Mwema%20Katika%20Jamaa%20Zako%3F
[22] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11834&title=19-Tukumbushane%3A%20Je%2C%20Haujafika%20Tu%20Muda%20Wa%20Wewe%20Kujionea%20Haya%20Na%20Allaah%20%E2%80%98Azza%20Wa%20Jalla%3F
[23] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11835&title=20-Tukumbushane%3A%20Je%2C%20Haujafika%20Tu%20Muda%20Wa%20Wewe%20Kujionea%20Haya%20Na%20Uteremko%20Wa%20Allaah%20%E2%80%98Azza%20Wa%20Jalla%20Kwa%20Ajili%20Yako%20Kila%20Usiku%3F
[24] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11836&title=21-Tukumbushane%3A%20Kwa%20Nini%20Allaah%20%E2%80%98Azza%20Wa%20Jalla%20Anateremka%20Katika%20Theluthi%20Ya%20Mwisho%20Ya%20Usiku%3F
[25] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11837&title=22-Tukumbushane%3A%20%D9%84%D9%90%D9%85%D9%8E%D9%86%D9%90%20%D8%A7%D9%84%D9%85%D9%8F%D9%84%D9%83%D9%8F%20%D8%A7%D9%84%D9%8A%D9%8E%D9%88%D9%92%D9%85%D9%8E%D8%9F%20%20Ni%20Wa%20Nani%20Ufalme%20Wa%20Leo%3F
[26] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11838&title=23-Tukumbushane%3A%20Kuamsha%20Watoto%20Kuswali
[27] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11839&title=24-Tukumbushane%3A%20Usiingie%20Kwenye%20Mkumbo%20Huu
[28] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11840&title=25-Tukumbushane%3A%20Usiingie%20Kwenye%20Mkumbo%20Huu
[29] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11841&title=26-Tukumbushane%3A%20Ukarimu%20Mkubwa%20Wa%20Allaah%20Kwa%20Wakosefu
[30] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11842&title=27-Tukumbushane%3A%20Siri%20Kubwa%20Ya%20Kumsabbih%20Allaah
[31] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11843&title=28-Tukumbushane%3A%20Tuambulie%20Angalau%20Yai%20Zima
[32] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11844&title=29-Tukumbushane%3A%20Lituzindushe%20Hili
[33] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11845&title=30-Tukumbushane%3A%20Zoezi%20La%20Kila%20Siku
[34] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11846&title=31-Tukumbushane%3A%20Tuwe%20Tayari%20Kwa%20Majibu
[35] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11847&title=32-Tukumbushane%3A%20Ni%20Muda%20Mfupi%20Sana
[36] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11848&title=33-Tukumbushane%3A%20Neema%20Ya%20Chakula
[37] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11849&title=34-Tukumbushane%3A%20Vinywaji%20Ni%20Katika%20Neema%20Kubwa%20Kwetu
[38] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11850&title=35-Tukumbushane%3A%20Jela%20Ya%20Buwlas
[39] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11851&title=36-Tukumbushane%3A%20Walevi%20Nao%20Wanasubiriwa%20Na%20%E2%80%9CTwiynatul%20Khabaal%E2%80%9D
[40] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11852&title=37-Tukumbushane%3A%20Tusipoteze%20Nafasi%20Hii%20Ya%20Kuombewa%20Maghfirah
[41] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11853&title=38-Tukumbushane%3A%20Baadhi%20Ya%20Vitendo%20Vinavyoingiza%20Ndani%20Ya%20Duara%20La%20Kuombewa%20Maghfirah%20Na%20Malaika
[42] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11854&title=39-Tukumbushane%3A%20Laiti%20Ningelikuwa%20Mkia%20Wa%20Mbwa
[43] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11855&title=40-Tukumbushane%3A%20Je%2C%20Mamba%20anafaa%20Kwa%20Kitoweo%3F
[44] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11856&title=41-Tukumbushane%3A%20Na%20Fisi%20Je%3F
[45] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11857&title=42-Tukumbushane%3A%20Vipi%20Na%20Chura%3F%20
[46] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11858&title=43-Tukumbushane%3A%20Na%20Nyoka%20Je%3F
[47] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11859&title=44-Tukumbushane%3A%20Vipi%20Kuhusu%20Paka%20Na%20Nyani%3F
[48] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11860&title=45-Tukumbushane%3A%20Sote%20Tutabanwa%20Na%20Kaburi
[49] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11861&title=46-Tukumbushane%3A%20Adhabu%20Kwa%20Wasiotoa%20Zakaah