كتاب الزواج
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Abu Maalik Kamaal Bin As-Sayyid Saalim
Imetarjumiwa na 'Abdullaah Mu'aawiyah (Abu Baasim)
Alhidaaya.com
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
01: Kufunga Ndoa:
Fungamano la ndoa ni sawa na mikataba mingineyo ambayo makubaliano yake yanakuwa juu ya msingi wa utashi wa watu wawili wanaoingia mkataba kwa ridhaa yao. Ridhaa na utashi ni vitu vya ndani ya moyo ambavyo hakuna binadamu anayeweza kuviona au kuvijua, na kwa ajili hiyo, imekuwa ni lazima kitoke kwa wawili wanaoingia mkataba chenye kuonyesha kukubali kwao mkataba na kuuwafiki.
Kwa upande wa wanandoa, kinachoonyesha kukubali na kuwafiki kwao ni matamshi yanayojulikana kama "الإِيْجَابُ" (Al-Iyjaab) na "القَبُوْلُ" (Al-Qabuwl). Matamshi haya ndio nguzo mbili za kufungika ndoa.
Al-Iyjaab "الإيجاب" , ni tamshi toka kwa walii wa mwanamke au mwakilishi wake ambapo humwambia mwenye kuoa: “Nimekuozesha binti yangu fulani”.
Ama Al-Qabuwl "القَبُوْلُ", hili ni tamshi toka kwa anayeoa au anayemwakilisha ambapo humjibu walii kwa kusema: “Nimekubali”.
Matamshi haya mawili ndiyo ambayo kwayo ndoa inafungika.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
02: Masharti Ya Kufungika ‘Aqdi Ya Ndoa: Masharti Ya Tamko La ‘Aqdi:
Sharti la kwanza:
Tamko la “Iyjaab” na “Qabuwl” ni lazima libebe maana ya ndoa kama vile
"أَنْكَحْتُ" au"زَوَّجْتُ" au "مَلَّكْتُ" au "وَهَبْتُ" na mfano wa hivyo, na hili ni kwa mujibu wa ada. Na si sharti muundo uwe kwa tamko la kuozesha, kwa kuwa linalozingatiwa ni makusudio na maana, na si tamko. Na hii ndio kauli iliyo sahihi zaidi ya ‘Ulamaa, na pia ni madhehebu ya Abu Haniyfah, na Maalik, na chaguo pia la Ibn Taymiyah.
Linalotilia nguvu hili ni lile lililothibiti kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwozesha mtu fulani mwanamke akamwambia:
"فَقَدْ مَلَّكْتُكَهَا بِمَا مَعَكَ مِنَ الْقُرْآنِ"
“Basi nimekumilikisha (nimekuozesha) kwa kiasi ulichohifadhi katika Qur-aan”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (1425) na Muslim (5871)]
Ama ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy na Kihanbali, wao wanaona kwamba ndoa haiswihi isipokuwa kwa tamko lililonyambulika kutokana na kuozesha "التَّزْوِيْجُ" au"الإِنْكَاحُ" , kwa kuwa hakuna tamshi jingine lolote lililokuja ndani ya Qur-aan zaidi ya haya mawili. Hivyo ni lazima kuyatumia ki‘ibada, kwani nikaah ni ‘ibada, na matamshi au adhkaar huwa yanachukuliwa toka ndani ya shariy’ah, na si vinginevyo.
Kufunga Ndoa Kwa Lugha Nyingine Isiyo Kiarabu:
Ikiwa wafungao ndoa au mmoja wao hafahamu Kiarabu, basi itajuzu kufunga kwa lugha inayofahamika. Na ikiwa wanaifahamu vizuri lugha ya Kiarabu na wanaweza kufungishiwa kwayo ndoa, basi hapo haitojuzu kufungwa ndoa kwa lugha nyingineyo. Hii ni kauli ya ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy na Kihanbali.
Lakini lililo sahihi, ni kwamba inajuzu. Sheikh wa Uislamu amesema: “Kulazimisha tamko la Kiarabu katika kufungisha ndoa kuko mbali kabisa na misingi ya kisharia, kwa kuwa ndoa inaswihi kwa Muislamu na kwa kafiri. Ndoa ni sawa na kuacha huru mtumwa au kutoa sadaka. Na kama ilivyo au ilivyozoeleka, mkataba wowote hauna lazima ya kuwa na tamshi, si kwa Kiarabu au kwa lugha nyingine yoyote. Vile vile sadaka, au waqfu, au tunu, haya yote hayana lazima kutamkiwa kwa Kiarabu kwa mujibu wa Ijmaa ya ‘Ulamaa. Isitoshe, ikiwa asiye Mwarabu atajifundisha papo kwa hapo Kiarabu, anaweza asifahamu makusudio ya tamshi hilo kama anavyolifahamu katika lugha yake anayoijua.
Ndoa Haifungiki Kwa Ishara Isipokuwa Kwa Bubu Tu:
Jumhuwr ya ‘Ulamaa kinyume na ‘Ulamaa wa Kimaalik, wamekubaliana kwamba mwenye uwezo wa kutamka na badala yake akatumia ishara, basi ishara yake hiyo haizingatiwi katika kufunga ‘aqdi ya ndoa. Ama kwa bubu, ishara yake iliyozoeleka na kufahamika inakubalika kisharia. Lakini hapo hapo wamekhitilafiana katika swali lisemalo: Je, utumiaji wa ishara ni sharti uende sambamba na kutoweza bubu kuandika? Ilivyo sahihi ni kwamba ni sharti, kwa maana ikiwa anaweza kuandika, basi ishara haitozingatiwa.
Sharti la pili:
Muundo wa tamshi ni lazima ubebe maana ya upapo kwa hapo. Ikiwa utabeba maana ya wakati ujao au wakati maalum, basi ‘aqdi ya ndoa haifungiki. Ni kama kusema: “Ikifika tarehe mosi ya mwezi, basi nitakuwa nimekuozesha”, au “Nimekuozesha binti yangu wakati atakapokuwa amefaulu mtihani”, kwa kuwa hili linakuwa limefungamanishwa na sharti ambalo halipo kwa wakati uliopo. Lakini kama atafungamanisha na sharti ambalo limeshapatikana, basi ndoa itafungika.
Sharti la tatu:
“Qabuwl” na “Iyjaab” zikubaliane kwa pande zote. Hili ndilo ambalo ‘Ulamaa wa Fiqh wameafikiana. Hivyo basi, ikiwa qabuwl itatofautiana na iyjaab kwa jambo, basi ndoa haitoswihi. Ikiwa walii atasema kwa mfano: “Nimekuozesha binti yangu Fatmah kwa mahari ya shilingi laki moja”, na mwoaji akasema: “Nimekubali kumwoa binti yako ‘Aaishah kwa mahari ya shilingi elfu 50”, basi ndoa haitoswihi”.
Sharti la nne:
Qabuwl na Iyjaab ziungane. Kwa maana kwamba kikao cha kufungisha ndoa ni lazima kiwe kimoja, na qabuwl na iyjaab zitamkwe kwa pamoja ndani ya kikao hicho kimoja.
Lakini pamoja na hivyo, si sharti kutamkwa qabuwl moja kwa moja baada ya iyjaab. Muda kupita hakuna neno madhali qabuwl itatamkwa ndani ya kikao kimoja. Upapo kwa hapo haukushurutishwa na Jumhuwr ya ‘Ulamaa. [Al-Badaai’u (5/137), Mawaahibul Jaliyl (4/241) na Kash-shaaful Qinaa (3/147)]
Faida:
Fuqahaa walishurutisha siku za nyuma kikao kuwa kimoja kutokana na uduni wa njia za mawasiliano. Ama enzi yetu ya leo, bila shaka teknolojia ya mawasiliano imepiga hatua kubwa. Tuna simu za viganjani na mfano wake ambazo zinaweza kutuletea tukio lolote, toka popote lilipo, na kwa wakati huo huo. Watu wote wanaweza kulishuhudia toka kona yoyote ya dunia. Hivyo basi, hakuna kizuizi kufunga ndoa hata kama vikao viko sehemu mbili tofauti, muhimu ni upapo kwa papo uwepo wa “qabuwl” na “iyjaab”. Isitoshe, ni lazima kila mmoja wa wafungaji ndoa ahakikishe utambulisho wa mwingine na usiwepo udanganyifu.
Sharti la tano:
Mtamkaji wa “iyjaab” asilirejeshe tamko lake kabla ya upande wa pili wa “qabuwl” kukubali. Jumhuwr kinyume na Maalik wanasema kwamba “iyjaab” si lazima ipite, na mtamkaji wake anaweza kulirejesha tamko lake kabla ya upande wa pili kukubali. Akilirejea tamko lake, basi ndoa haifungiki.
Kadhalika, ikiwa mmoja wa wafungao ndoa (walii au mwoaji) atakufa baada ya “iyjaab” na kabla ya “qabuwl” kutamkwa, basi ndoa inakuwa haijafungika.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
03: Masharti Yanayowahusu Walii Na Mwoaji:
La kwanza:
Ni lazima kila mmoja wao awe na vigezo vya kumwezesha kufanikisha ‘aqd ya ndoa.
Vigezo vyenyewe ni awe amebaleghe, mwenye akili na mtambuzi. Ama mtoto mdogo ambaye bado hajabaleghe lakini mtambuzi, kama walii wake atamruhusu, basi ndoa yake itaswihi.
La pili:
Wawe na haki na mamlaka wao wenyewe ya kuzindua ‘aqd:
Hii ni kwa aliyebaleghe, mwenye akili na anayejitambua, huyu ana haki na mamlaka ya kufunga ndoa mwenyewe au kumwakilisha mwingine amfungie. Kadhalika walii, yeye kapewa haki na sharia ya kusimamia ndoa. Ama mtu kando aliyejiingiza bila idhini yake, huyo ‘aqd yake haishwihi.
La tatu:
Wote waridhie kwa hiari yao.
Kama ndoa itafungwa bila ya ridhaa yao au kwa ridhaa ya mmoja wao tu, basi haitoswihi.
La nne:
Kila mmoja wao ayasikie maneno ya mwingine na ayafahamu.
La tano:
Kila mmoja kati ya wanandoa watarajiwa (bwana harusi na bibi harusi) ajulikane na atambulike. Ikiwa walii ana binti zaidi ya mmoja na akasema: “Nimekuozesha mmoja ya binti zangu” bila kumtaja jina, hapo ndoa haitoswihi.
La sita:
Kusiwepo kati ya wanandoa watarajiwa sababu ya kuharamisha kuoana. Katika milango ya nyuma, wanawake walioharamishwa kuwaoa wametajwa.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
04: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (a) Idhini ya walii wa mwanamke:
Haya ni masharti ambayo kuswihi ‘aqdi ya ndoa kunasimamia juu yake pamoja na athari zake, na inabatilika kwa kukosekana moja katika masharti haya. La kwanza ni idhini ya walii wa mwanamke.
Walii ni msimamizi wa mwanamke katika zoezi la kufunga ndoa. Jumhuwr ya ‘Ulamaa wakiwemo ‘Umar, ‘Aliy, Ibn Mas-‘uwd, Abu Hurayrah, ‘Aaishah, Maalik, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-Haaq, Abu ‘Ubayd, Ath-Thawr na Ahlu Adh-Dhwaahir, wanasema kwamba walii ni sharti ya kuswihi kwa ‘aqdi. Ikiwa mwanamke atajiozesha mwenyewe, basi ndoa yake ni batili. Dalili zao ni hizi zifuatazo:
(a) Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَأَنكِحُوا الْأَيَامَىٰ مِنكُمْ"
“Na waozesheni wajane miongoni mwenu”. [An-Nuwr: 32]
Hapa Allaah Ta’aalaa Ameelekeza agizo la kuozesha wajane kwa wanaume. Lau kama amri ya kuozesha inawahusu wanawake, basi Allaah Asingeliwaamuru wanaume.
(b) Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَلَا تُنكِحُوا الْمُشْرِكِينَ حَتَّىٰ يُؤْمِنُوا"
“Na wala msiwaozeshe (wanawake wa Kiislamu) wanaume washirikina mpaka waamini”. [Al-Baqarah: 221)]
(c) Mzee kikongwe alimwambia Muwsaa (‘alayhis salaam):
"إِنِّي أُرِيدُ أَنْ أُنكِحَكَ إِحْدَى ابْنَتَيَّ هَاتَيْنِ"
“Mimi nataka nikuozeshe mmojawapo wa binti zangu hawa wawili”. [Al-Qaswas: 27]
(d) Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا تَعْضُلُوهُنَّ أَن يَنكِحْنَ أَزْوَاجَهُنَّ إِذَا تَرَاضَوْا بَيْنَهُم بِالْمَعْرُوفِ"
“Na mtakapowataliki wanawake wakafikia muda wa kumaliza eda yao, basi msiwazuie kuolewa na waume zao (wa awali) ikiwa wameridhiana baina yao kwa mujibu wa ada”. [Al-Baqarah: 232]
Hapa Allaah Ta’aalaa Amewakataza Mawalii wasiwazuie wanawake kurudi kwa waume zao. Na hii ni dalili tosha ya kumzingatia walii, na kama si hivyo, basi kuambiwa asimzuie kusingelikuwa na maana yoyote. Isitoshe, kama angelikuwa na haki ya kujiozesha mwenyewe, basi asingelimhitajia walii wake.
(e) Kauli Yake Ta’aalaa:
"فَانكِحُوهُنَّ بِإِذْنِ أَهْلِهِنَّ"
“Basi waoeni kwa idhini ya watu wao”. [An-Nisaa: 25]
Hapa imeshurutishwa idhini ya walii wa msichana ili ndoa iswihi, na inaonesha kwamba hawezi kujiozesha mwenyewe.
(f) Kauli Yake Ta’aalaa:
"الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ"
“Wanaume ndio wasimamizi wa wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine.” [An-Nisaa: 34]
(g) Bibi ‘Aaishah akiizungumzia Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَمَا يُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فِي الْكِتَابِ فِي يَتَامَى النِّسَاءِ اللَّاتِي لَا تُؤْتُونَهُنَّ مَا كُتِبَ لَهُنَّ وَتَرْغَبُونَ أَن تَنكِحُوهُنَّ"
“Na (hukmu ya) yale mnayosomewa katika Kitabu kuhusu mayatima wanawake ambao hamuwapi (mahari) waliyoandikiwa nanyi mna raghba ya kuwaoa”. [An-Nisaa: (127)]
…anasema:
“Hili linahusiana na binti yatima anayelelewa na mwanaume. Binti huyu anaweza kuwa na mali akaichanganya na ya mwanaume huyo na kuwa mshirika wake kiubia. Na yeye (kwa kuwa ni mlezi wake) anastahiki zaidi kuwa na ubia huo na binti. Lakini ikaja kutokea asimpende penzi la kumwoa na hapo akamzuia kuolewa na mtu mwingine kwa ajili ya mali yake kwa kuhofia kwamba mtu huyo atafaidika na mali ya binti”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5128)]
Ama kipande cha aayah kinachosema:
"وَتَرْغَبُونَ أَن تَنكِحُوهُنَّ"
“nanyi mna raghba ya kuwaoa”, hiki kinahusiana na aayah ya tatu ya Suwrat An-Nisaa ambapo Allaah Ta’aalaa Amesema:
"وَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا تُقْسِطُوا فِي الْيَتَامَىٰ فَانكِحُوا مَا طَابَ لَكُم مِّنَ النِّسَاءِ مَثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ"
“Na mkikhofu kuwa hamtoweza kufanya uadilifu kwa mayatima; basi oeni waliokupendezeni katika wanawake wengine; wawili au watatu au wanne”.
Ni kwamba ‘Taabi’iy ‘Urwah bin Az-Zubayr alimuuliza khalati yake Mama wa Waumini Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) kuhusiana na aayah hii, naye akamwambia: “Ee mtoto wa dada yangu, aayah hii iliteremka kuhusiana na binti yatima anayelelewa na mtu, na mali (yake na ya mlezi wake) ikawa ya ushirika baina yao, na mlezi huyo akaifanyia biashara. Halafu ikatokea akavutiwa na mali yake na uzuri wake na akataka amuoe, lakini kwa mahari chache kulinganisha na wanawake wengine. Na hapo ndipo walipokatazwa kuwaoa ila kama watawapa mahari wanayostahiki kama wanavyostahiki wanawake wengine wote. Na kama hawataki hilo, basi waoe wanawake wengineo; wa pili, wa tatu na wanne, kwa hao bila shaka watalipa mahari kamili, na wawaache mabinti hao mayatima (lakini pia wasiwazuie kuolewa na wengineo)”.
Na dalili zilizo wazi zaidi kuliko zote zilizotangulia, ni hizi zifuatazo:
(a) Hadiyth ya Abu Muwsaa kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لَا نِكَاحَ إِلَّا بِوَلِيٍّ"
“Hakuna ndoa bila walii”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2085), At-Tirmidhiy (1101), Ibn Maajah (1879), Ahmad (4/394) na wengineo. Angalia Al-Irwaa (6/234)]
(b) Hadiyth ya ‘Aaishah kwamba Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"أَيُّمَا امْرَأَةٍ نَكَحَتْ بِغَيْرِ إِذْنِ موَالِيْهَا فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ وَلَهَا ْمَهْرُهَا بِمَا أَصَابَ مِنْهَا، فَإِنِ اشْتَجَرُوا فَالسُّلْطَانُ وَلِيُّ من لَا ولي لَهُ ".
“Mwanamke yeyote ambaye ataolewa bila idhini ya mawalii wake, basi ndoa yake ni batili, ndoa yake ni batili, ndoa yake ni batili. Na mahari yake atapewa kama mume atakuwa amemuingilia. Na kama mawalii watazozana, basi kiongozi (Kadhi) ni walii kwa asiyekuwa na walii”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2083), At-Tirmidhiy (1101), Ibn Maajah (1879) na Ahmad (6/156)]
(c) Maana hii imethibiti kutokana na kauli za ‘Umar bin Al-Khattwwaab, ’Aliy bin Abiy Twaalib na Ibn ‘Abbaas. [Angalia Jaami’u Ahkaamin Nisaa (3/327-328)]
(e) Toka kwa Abu Hurayrah, amesema:
"لا تُنْكِحُ الْمَرْأَةُ نَفْسَهَا، فَإِنَّ الزَّانِيَةَ تُنْكِحُ نَفْسَهَا"
“Mwanamke hajiozeshi mwenyewe, bali mzinifu ndiye anayejiozesha mwenyewe”. [Isnadi yake ni swahiyh. Imechakatwa na Abdul Razzaaq (6/200) na Ibn Abiy Shaybah (4/135)]
Wakati huo huo, kinyume na hayo, Abu Haniyfah anasema kwamba mwanamke aliye huru, mwenye akili zake timamu na aliyebaleghe, hashurutishiwi kuwepo walii wake ili ndoa yake iswihi, anayeshurutishiwa hilo ni msichana mdogo tu!! Na hoja yake ni haya yafuatayo:
1- Kauli Yake Ta’aalaa:
" فَإِن طَلَّقَهَا فَلَا تَحِلُّ لَهُ مِن بَعْدُ حَتَّىٰ تَنكِحَ زَوْجًا غَيْرَهُ"
“Na akimtaliki (mara ya tatu), basi hatokuwa halali kwake baada ya hapo mpaka aolewe na mume mwengine”. [Al-Baqarah: (230)]
Amesema: “Ndoa imetegemezewa kwao, na kwa hivyo basi, ni dalili kwamba ndoa inaswihi kwa matamshi yao bila sharti ya walii”.
2- Kauli Yake Ta’aalaa:
" وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا تَعْضُلُوهُنَّ أَن يَنكِحْنَ أَزْوَاجَهُنَّ"
“Na mtakapowataliki wanawake wakafikia muda wa kumaliza eda yao, basi msiwazuie kuolewa na waume zao (wa awali)”. [Al-Baqarah: (232)]
Amesema: “Utohoaji dalili kwa aayah hii ni kwa njia mbili:
1- Allaah Ametegemeza ndoa kwao wanawake.
2- Inawezekana katazo la kuwazuia kuolewa kwenye aayah linawahusu waume. Aayah imewakataza wasiwazuie wake zao waliowataliki kuolewa na mwanaume yeyote wamtakaye baada ya kumalizika eda zao.
Ninasema: “Sababu ya kuteremka aayah hii imeshaelezwa nyuma, na sababu hiyo inaradd taawiyl hii”.
3- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“Mwanamke asiye na mume (ayyim) ana haki zaidi ya kujiamulia kuliko walii wake, na msichana bikra hutakwa idhini kwa nafsi yake mwenyewe, na idhini yake ni kunyamaza.”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Muslim]
"الأَيِّمُ"] kiasili, ni mwanamke asiye na mume, ni sawa akiwa bikra au bila bikra, ametalikiwa, au amefiwa na mumewe.
"الأَيِّمُ" pia ina maana ya mwanaume asiye na mke. Inasemwa: "رَجُلٌ أَيِّمٌ" mwanaume asiye na mke, na kwa mwanamke inasemwa: "امْرَأَةٌ أَيِّمَةٌ" mwanamke asiye na mume. Na Allaah Anaposema:
"وَأَنكِحُوا الْأَيَامَىٰ مِنكُمْ "
“Na waozesheni wajane miongoni mwenu”, hapa inakusudiwa wanaume wasio na wake na wanawake wasio na waume.]
Faida:
1- Kama ilivyotangulia, Abu Haniyfah amejuzisha mwanamke kujiozesha mwenyewe, lakini pamoja na hivyo, amempa haki walii kuvunja ndoa kama mume haendani kwa kiwango na mwanamke!!
2- Mwanamke hamwozeshi mwanamke mwenzake, na wala ndoa haifungiki kwa matamshi yake. Kwa kuwa kiasili, mwanamke hafai kujiozesha mwenyewe, na kwa hivyo kumwozesha mwenzake ndio haifai kabisa.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
05: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (b) Walii Hana Haki Ya Kumlazimisha Mwanamke Aliyebaleghe Kuolewa:
(a) Kumlazimisha aliyewahi kuolewa (au asiye bikra “thayyib”):
Haijuzu kumwozesha “thayyib” na aliye baleghe na bila idhini yake, hana ruhusa baba yake wala mwingine yeyote. Na hii ni kwa itifaki ya Waislamu wote. Zifuatazo ni dalili za kuthibitisha hili:
1- Hadiyth ya Khansaa bint Khidhaam Al-Answaariyyah:
"أنَّ أبَاهَا زَوَّجَهَا وهْيَ ثَيِّبٌ، فَكَرِهَتْ ذلكَ، فأتَتْ رَسولَ اللَّهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم، فَرَدَّ نِكَاحَهَا"
“Kwamba baba yake alimwozesha baada ya kuwa aliwahi kuolewa (thayyib), naye hakufurahishwa na hilo, akaenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) (kumshtakia), na Rasuli akaivunja ndoa”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5138), Abu Daawuwd (2101), An-Nasaaiy (6/86) na Ibn Maajah (1873)].
2- Abu Hurayrah: “Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لَا تُنْكَحُ الْأَيِّمُ حَتَّى تُسْتَأْمَرَ، وَلَا تُنْكَحُ الْبِكْرُ حَتَّى تُسْتَأْذَنَ . قَالُوا: يَا رَسُول الله، وَكَيف إِذْنهَا؟ قَالَ: أَنْ تَسْكُتَ"
“Mwanamke asiye na mume (ayyim) haolewi mpaka atakwe shauri lake, na bikra haolewi mpaka atakwe idhini yake. Wakauliza: Idhini yake inakuwaje? Akasema: Akinyamaza”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5136) na Muslim (1419)]
3- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas: “Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لَيْسَ لِلْوَلِيِّ مَعَ الثَّيِّبِ أَمْرٌ وَالْيَتِيمَةُ تُسْتَأْمَرُ فَصَمْتُهَا إِقْرَارُهَا"
“Walii hana lake jambo kwa aliyewahi kuolewa (thayyib), na yatima hutakwa shauri lake, na akinyamaza ndio kakubali”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2100) na wengineo]
Faida Mbili:
Ya kwanza: Msichana ambaye ubikira wake umeondoka kutokana na zinaa, anakuwa katika ndoa ni sawa na mwanamke aliyekwishawahi kuolewa (thayyib). Haitojuzu kwa walii wake kumlazimisha kuolewa. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Maswahibu wawili wa Abu Haniyfah. Ama Abu Haniyfah mwenyewe pamoja na Maalik, wao wanasema kwamba mwanamke huyo ni sawa na bikra.
Na kama ubikira wake utaondoka bila kuingiliwa (kama kwa kuruka, au kwa kidole, au kwa kubakwa, au mfano wa hayo), basi atazingatiwa bikra kwa mujibu wa Maimamu wanne. [Majmuw’ul Fataawaa (32/29). Angalia pia Fat-hul Qadiyr (3/270), Rawdhwat At-Twaalibiyna (7/54), na Al-Mughniy (6)]
Ya pili: Kama walii atamwozesha aliyewahi kuolewa bila ya idhini yake, kisha yeye mwenyewe mwanamke akapasisha fungisho la ndoa hiyo, basi ndoa ni sahihi, haihitajii kufungwa tena upya. Hii ni rai ya ‘Ulamaa walio wengi akiwemo Abu Haniyfah, Maalik na riwaayah toka kwa Ahmad.
Lakini ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy wanaona kwamba ndoa iliyofungwa ni batili, na ni lazima ifungwe tena upya. [Majmuw’u Fataawaa Shaykhil Islaam (32/29)]
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
06: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (c) Kumlazimisha Bikra Aliye Baleghe:
‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na bikra aliye baleghe. Je, walii wake anaweza kumlazimisha kuolewa? Wamekhitilafiana hili katika kauli mbili. Kauli iliyo sahihi zaidi ni kuwa haijuzu kwa walii wake kumlazimisha. Ni kauli ya Abu Haniyfah, riwaayah toka kwa Ahmad, Al-Awzaa’iy, Ath-Thawriy, Abu ‘Ubayd, Abu Thawr, na Ibnul Mundhir. Sheikh wa Uislamu ameikhitari. Dalili zao ni:
1- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas:
"إِنَّ جَارِيَةً بِكْرًا أَتَتْ رَسُولَ اللَّهِ َصَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَذَكَرَتْ لَهُ أَنَّ أَبَاهَا زَوَّجهَا وَهِي كَارِهًة، فَخَيَّرَهَا النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم"
“Kwamba msichana bikra alimjia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akamweleza kwamba baba yake amemwozesha bila ridhaa yake, na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamchaguza (kati ya kuivunja ndoa au kuendelea nayo)”. [Hadiyth Hasan Lishawaahidih. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2099) na Ibn Maajah (1875)]
2- Neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"وَلَا تُنْكَحُ الْبِكْرُ حَتَّى تُسْتَأْذَنَ"
“Na bikra haolewi mpaka atakwe idhini yake”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5136) na Muslim (1419)]
3- Kwa vile walii kujiamulia aonavyo yeye kuhusiana na ndoa ya binti yake, ni sawa na kujiamulia aonavyo katika mali ya binti huyo. Sasa ikiwa walii huyu haruhusiwi kuamua aonavyo katika mali ya binti yake ambaye ni mwelewa na mtambuzi isipokuwa kwa idhini yake, basi vipi itajuzu kumwamulia ndoa ambayo ni jambo zito bila ridhaa yake ilhali binti anajitambua? [Majmuw’ul Fataawaa (32/39)]
4- Kumwozesha bila ridhaa yake ni kinyume na misingi ya kishariy’ah na kiakili. Allaah Ta’aalaa Hajamruhusu walii wake kumlazimisha kuuza au kukodisha kwa mfano ila kwa idhini yake, au hata chakula asichokipenda, au kinywaji au kivazi, basi vipi atamlazimisha kuolewa, halafu kuingiliwa na kuishi pamoja na mtu asiyemtaka au kumpenda? Allaah Ta’aalaa Amejenga mapenzi na huruma kati ya wanandoa wawili, basi vipi hilo litapatikana ikiwa binti hayuko tayari kuishi na mwanaume asiyemtaka?! [As-Saabiq: (32/25)]
5- Mwanamke kama amemchukia mume, basi ameruhusiwa na sharia kuachana naye. Sasa vipi itajuzu kwa walii kumwozesha mtu ambaye kabla ya ndoa ashamchukia?
Faida:
Suala hili ni kama walii atakuwa ni baba au babu. Na ikiwa si hawa wawili kama kaka yake au ami yake, Sheikh wa Uislamu amenukuu Ijma’a ya Waislamu kwamba bikra aliyebaleghe hakuna mwenye ruksa ya kumwozesha bila idhini yake isipokuwa baba yake au babu yake tu (wengine hawana mamlaka hayo).
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
07: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (d) Kumlazimisha Binti Mdogo:
‘Ulamaa wamekubaliana wote -isipokuwa wachache mno- kwamba binti bikra mdogo ambaye bado hajabaleghe, inajuzu kwa baba yake kumwozesha bila ya idhini yake. Kwa kuwa hakuna maana ya kumtaka idhini binti kama huyu ambaye hajui nini maana ya idhini yake, na ambaye pia kunyamaza kwake na kununa kwake ni sawa.
Dalili yao wanasema kwamba Abu Bakr (Radhwiya Allaah ‘anhu) alimwozesha ‘Aaishah akiwa binti mdogo ambaye bado hajabaleghe. Kadhalika, wamelichukulia neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"وَلَا تُنْكَحُ الْبِكْرُ حَتَّى تُسْتَأْذَنَ"
“Na bikra haolewi mpaka atakwe idhini yake”….kwamba muradi wa bikra ambaye anatakwa idhini ni yule ambaye amebaleghe (na siye ambaye bado hajavunja ungo).
Lakini, ikiwa binti huyo mdogo anajitambua na anajua nini ndoa, na anaweza kumtathmini aliyekusudia kumwoa, basi hapa ni wazi kwamba atatakwa idhini yake. Ni kwa kuwa pia anaingia ndani ya wigo wa ujumuishi wa mabikra; haijalishi ni mdogo au mkubwa, pamoja na kuzingatia maslaha ya kumtaka mwenyewe idhini. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
Faida:
Je, Asiye Baba Anaweza Kumlazimisha Binti Mdogo?
Sheikh wa Uislamu ameeleza kwamba kwa mujibu wa itifaki ya ‘Ulamaa, sharia haimpi kibali mtu mwingine yeyote asiye baba au babu kumlazimisha binti mdogo. [Majmuw’ul Fataawaa (32/57)]
Ninasema: “Huenda (Sheikh wa Uislamu) anawakusudia Maimamu watatu (katika itifaki hiyo). Kwani Abu Haniyfah na Al-Awzaa’iy wamesema kuhusiana na “thayyib” mdogo (binti mdogo aliyeshawahi kuolewa): “Atamwozesha msimamizi wake yeyote, lakini akibaleghe, basi haki ya kujichagulia mwenyewe itathibiti”. [Fat-hul Baariy (9/98) na Bidaayatul Mujtahid (2/29)]
Jumhuwr ya ‘Ulamaa wametolea dalili Hadiyth ya Abu Hurayrah: “Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"تُسْتَأْمَرُ الْيَتِيمَةُ فِي نَفْسِهَا، فَإِنْ صَمَتَتْ فَهُوَ إِذْنُهَا، وَإِنْ أَبَتْ فَلَا جَوَازَ عَلَيْهَا"
“Yatima ni lazima atakwe ushauri kuhusiana na nafsi yake mwenyewe. Kama atanyamaza, basi hiyo ndiyo idhini yake, na kama atakataa, basi hakuna ndoa kwake”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2093), At-Tirmidhiy (1190), An-Nasaaiy (3270) na Ahmad (7519)]
Yatima anayekusudiwa hapa ni msichana mdogo aliyefiwa na baba yake na ambaye pia bado
hajavunja ungo. Akivunja, si yatima tena.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
08: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (e) Walii Kuzuia Ndoa:
Tumeshasema nyuma kwamba walii haruhusiwi kumlazimisha mwanamke kuolewa na mtu asiyemtaka, kama ambavyo haruhusiwi pia kumzuia kuolewa na mtu aliyemridhia ikiwa mtu huyo ana vigezo vinavyokubalika.
Allaah Ta’aalaa Amesema:
"وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَلَا تَعْضُلُوهُنَّ أَن يَنكِحْنَ أَزْوَاجَهُنَّ إِذَا تَرَاضَوْا بَيْنَهُم بِالْمَعْرُوفِ"
“Na mtakapowataliki wanawake wakafikia muda wa kumaliza eda yao, basi msiwazuie kuolewa na waume zao (wa awali) ikiwa wameridhiana baina yao kwa mujibu wa ada”. [Al-Baqarah: (232)]
Ikiwa walii atamzuia binti yake, basi uwalii wake utahamishiwa kwa mwengine. Ash-Shaafi’iy amesema kwamba walii akizuia, basi uwalii wake utahamishiwa kwa kadhi. Ama Abu Haniyfah, yeye amesema utahamishiwa kwa walii wa ngazi ya mbali zaidi, lakini kwa sharti awe na vigezo vinavyokubalika. Na ikiwa mawalii wote watakataa kumwozesha na wakamzuia, basi uwalii utahamishiwa kwa kadhi moja kwa moja. [Majmuw’ul Fataawaa: (32/37)]
Ninasema: “Kauli iliyo karibu zaidi ni ya Abu Haniyfah kutokana na Hadiyth Marfuw’u ya ‘Aaishah:
"فَإِنِ اشْتَجَرُوا فَالسُّلْطَانُ وَلِيُّ من لَا ولي لَهُ "
“Na kama watazozana, basi Sultani ndiye walii kwa asiye na walii”. [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma]
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
09: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (f) Ni Nani Mawalii?
Mawalii wa mwanamke ambao wana haki ya kumwozesha ni (العَصَبَةُ)“Al-‘Aswabah”, nao ni akaribu zake wanaume kwa upande wa baba yake na si kwa upande wa mama yake. Haya ndiyo madhehebu ya Jumhuwr kinyume na Abu Haniyfah ambaye anasema kwamba hata jamaa wa mama yake pia ni mawalii.
‘Ulamaa wamekhitilafiana katika suala la nani mwenye haki zaidi ya kutangulizwa na vipi unakuwa mpangilio.
- Mahanafiy: Kwanza watoto wa kiume wa mwanamke, kisha watoto wao, halafu baba kisha babu, halafu makaka kisha watoto wao, halafu maami, na mwisho watoto wao.
- Wamaalik: Kwanza watoto wa kiume, kisha watoto wao, halafu baba, kisha makaka halafu watoto wao, na mwisho babu.
- Mashaafi’iy: Kwanza baba, halafu babu, kisha makaka halafu watoto wao, halafu maami na hatimaye watoto wao.
- Mahanbali: Kwanza baba, halafu babu, kisha watoto halafu watoto wao, kisha makaka halafu watoto wao, kisha maami na mwisho watoto wao.
Ninasema: “Kidhibiti kwa walii ni ukaraba, kuwa na pupa na maslaha ya mwanamke, na kumsimamia. Na baba kiuhalisia, ndiye walii aliye karibu zaidi, na ndiye mwenye penzi na huruma zaidi. Katika hili, anafuatiwa na babu, yeye ni kama baba, na anaweza kuwa na huruma na mapenzi zaidi kwa mabanati wa mwanaye.
Wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), baba (kama yuko) alikuwa ndiye anayefunga ndoa ya binti yake. Abu Bakr na ‘Umar waliwaozesha ‘Aaishah na Hafswah kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hali ilikuwa hivyo hivyo kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipowaozesha mabinti zake. Kadhalika, Maswahaba pia. Na kama baba au babu hawako, basi jamaa wa karibu zaidi kisha anayefuatia atasimamia hilo. Mimi ninavyoona, kauli yenye nguvu zaidi ni ya Mashaafi’iy kisha Mahanbali (Rahimahumul Laah) kutokana na yaliyotangulia, na kwa vile mtoto anaweza kugoma kumwozesha mama yake kinyume na kaka na ami. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi”.
Mawalii Walio Ngazi Moja Wakivutana, Nini Kifanyike?
Ni kama ndugu wawili kuzozana, kila mmoja wao ana mtu anayetaka kumwozesha dada yao, au mama yao kwa mfano. Ikiwa mwanamke atamkubali yeyote katika hao wanaume wawili bila kuainisha, na ndugu zake wakawa kila mmoja ameozesha, basi ndoa iliyofungwa mwanzo ndio itakayozingatiwa. Na hii ni kwa Hadiyth ya Samurah kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"أَيُّمَا امْرَأَةٍ زَوَّجَهَا وَلِيَّانِ، فَهِيَ لِلْأَوَّلِ مِنْهُمَا"
“Mwanamke yeyote ambaye ameozeshwa na mawalii wawili (mmoja kamwozesha mume na mwingine mume mwingine), basi ni mke wa mume wa kwanza (kwa walii wa kwanza)”. [Imesimuliwa na Ahmad. At-Tirmidhiy kasema ni Hasan]
Hii ni kwa vile ndoa ya mume wa pili, inakuwa ni kumwozesha mwanamke ambaye ameshaolewa, na hili halifai.
Ama ikiwa mwanamke atamkataa mmoja wao, basi ndoa ya mkataliwa haiswihi, kwa kuwa ridhaa yake mwanamke ni sharti ya kuswihi ndoa yake.
Ikiwa mvutano utaendelea kati ya mawalii, basi mwanamke atakuwa na haki ya kuwasilisha shauri lake kwa kadhi, na kadhi atakuwa na haki ya kumwozesha wakati huo kutokana na kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"فَإِنِ اشْتَجَرُوا فَالسُّلْطَانُ وَلِيُّ من لَا وَليَّ لَهُ ".
“Na kama watavutana, basi kiongozi (kadhi) ndiye walii kwa asiyekuwa na walii”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2083), At-Tirmidhiy (1101), Ibn Maajah (1879) na Ahmad (6/156)]
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
10: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (g) Kuozesha Walii Wa Mbali Kama Wa Karibu Hayuko:
Kiasili, haijuzu walii wa mbali kuozesha ikiwa wa karibu yuko. Ikiwa wa karibu hayuko, na kumsubiri hadi awepo kutapoteza maslaha ya mwanamke, basi hapo uwalii utahamia kwa wa mbali. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Ahmad na Maalik. Kadhalika, ikiwa walii wa karibu atamzuia asiolewe na mtu mwenye vigezo, basi hapo uwalii utahamia kwa wa mbali.
Na ikiwa walii wa mbali ataruhusu na mwanamke akaolewa, basi baada ya hapo, walii wa karibu hatokuwa na haki ya kupinga ndoa hiyo au kutaka ivunjwe.
Je, Inajuzu Kwa Walii Kumwakilisha Mtu Mwingine Au Kutoa Wasiya Wa Kuozesha?
Inajuzu kwa walii kumwakilisha mtu kumwozesha mwanamke ambaye yeye anasimamia mambo yake. Mwakilishi huyo atabeba yote yanayomuhusu walii.
Ama wasiya wa kuozesha baada ya yeye kufa, kauli sahihi zaidi ya ‘Ulamaa inasema kwamba hilo halijuzu. Uwalii haupatiwi manufaa kwa wasiya, kwa kuwa uwalii wa muusiaji unakatika kwa kifo chake mbali na kwamba penzi na huruma vinavyomfanya walii kuwa walii, vinakuwa haviko tena.
Haya ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy, riwaayah toka kwa Ahmad, Ath-Thawriy, An Nakh’iy, Ibn Al-Mundhir, Ibn Hazm na Ash-Shawkaaniy.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
11: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (h) Masharti Ya Walii:
(a) Awe Muislamu. Kafiri hana uwalii kwa mwanamke wa Kiislamu. Allaah ‘Azza wa Jalla Amesema:
"وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ"
"Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni marafiki wandani wao kwa wao", [At-Tawbah: 71]
Anasema tena:
"وَالَّذِينَ كَفَرُوا بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ"
“Na wale waliokufuru ni marafiki wandani wao kwa wao”. [Al-Anfaal: 73]
Na Anasema tena:
"وَلَن يَجْعَلَ اللَّـهُ لِلْكَافِرِينَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ سَبِيلًا"
“Na Allaah Hatojaalia kwa makafiri njia ya kuwashinda Waumini”. [An-Nisaa: 141]
Hii ni kauli ya ‘Ulamaa wote. Ibn Al-Mundhir amesema: “Wote tunaowajua vyema, wamelikubali hili”.
(b) Awe mwanaume: Ni sharti lililopata itifaki ya wote.
(c) Awe na akili timamu: Asiye na akili hawezi kusimamia maslaha yake, vipi ataweza kusimamia maslaha ya mwingine!
(d) Awe amebaleghe: Ni sharti kwa ‘Ulamaa walio wengi.
(e) Awe huru: Ni sharti kwa ‘Ulamaa walio wengi. Mtumwa hana uwezo wa kujisimamia mwenyewe, hivyo hawezi kumsimamia mwingine.
Ash-Shaafi’iy ameshurutisha jingine ambalo ni uadilifu. Ni lazima walii awe mwadilifu, akiwa kinyume chake, basi haaminiki kumchagulia mwanamke mtu afaaye. Lakini Jumhuwr wanasema kwamba uadilifu si sharti kwa walii, kwa sababu hali ambayo walii anamchagulia binti yake mtu mwenye vigezo, inakuwa ni hali ya kimaumbile, nayo ni kumtakia lenye kheri kwake, na uadilifu hapo unakuwa hauna nafasi, ni sawa awe mwadilifu au asiwe mwadilifu, yote ni sawa.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
12: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti la Kwanza: (i) Je, Walii Anaweza Kujiozesha Mwenyewe Mwanamke Ambaye Yeye Anasimamia Mambo Yake?
Jumhuwr ya ‘Ulamaa akiwemo Al-Awzaa’iy, Ath-Thawriy, Abu Haniyfah, Maalik, Al-Layth, Ibn Hazm na wengineo wanasema kwamba yeyote mwenye kusimamia jambo la mwanamke -na hakuwa katika maharimu zake- basi inajuzu kwake kujiozeshea yeye mwenyewe kama mwanamke ataridhia hilo, na mwanaume huyu hahitajii mwanaume mwingine ili amwozeshe. Dalili zao ni haya yafuatayo:
1- Neno Lake Ta’aalaa:
"وَأَنكِحُوا الْأَيَامَىٰ مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُمْ"
“Na waozesheni wajane miongoni mwenu na walio Swalihina kati ya watumwa wenu wanaume na wajakazi wenu”. [An-Nuwr: 32]
Basi yeyote atakayejiozesha mwenyewe mjane kwa ridhaa yake, basi anakuwa amefanya Aliloamrishwa na Allaah Ambaye Hakumzuia mwozeshaji wa mjane kuwa huyo huyo ndiye mwenye kumwoa.
2- Hadiyth ya Anas bin Maalik kwamba:
"أَنَّ رَسُوْلَ اللهِ َصَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَعْتَقَ صَفِيَّةَ، وَجَعَلَ عِتْقَهَا صَدَاقَهَا"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwacha huru Swafiyyah, na akaufanya uhuru huo kuwa ndio mahari yake”. [Imechakatwa na Al-Bukhaariy (4200) na Muslim (1365)]
Hapa tunaona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amejiozesha mwenyewe kijakazi wake.
3- Bibi ‘Aaishah akiizungumzia aayah hii:
"وَيَسْتَفْتُونَكَ فِي النِّسَاءِ ۖ قُلِ اللَّـهُ يُفْتِيكُمْ "
“Na wanakuuliza wewe hukmu ya kishariy’ah (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu wanawake. Sema: Allaah Anakubainishieni hukmu ya kishariy’ah kuhusu wao”, anasema kwamba inahusiana na binti yatima anayelelewa na mwanaume, na yatima akawa na mali ambayo mwanaume huyo akaichanganya na mali yake. Halafu ikatokea kwamba mwanaume asipende kumwoa yatima huyu, na pia akahofia kumwozesha kwa mwanaume mwingine asije kufaidika na mali yake na hivyo akamfunga asiolewe. Na hapo ndipo Allaah Alipowakataza jambo hilo”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (4200) na Muslim (1365)]
4- Toka kwa Sa’iyd bin Khaalid kwamba Ummu Hakiym bint Qaaridh alimwambia ‘Abdul Rahmaan bin ‘Awf:
"إِنَّه قَدْ خَطَبَنِي غَيْرُ وَاحِدٍ، فَزَوِّجْني أَيَّهُم رَأَيْتَ، قَالَ: أَتَجْعَلِيْنَ أَمْرَكِ إِلَيَّ ؟ قالت: نَعَمْ، فَقَالَ: قَدْ تَزَوْجُتِكِ"
“Mimi nimeposwa na zaidi ya mtu mmoja, basi niozeshe yeyote unayemwona ananifaa. Akasema: Je, utaniachia mimi hilo (la kukuoa)? Akasema: Na’am. Akasema: “Basi nimekuoa”. [Al-Bukhaariy ameizingatia mu’allaq (9/94)]
Ash-Shaafi’iy na Daawuwd wamesema kwamba haijuzu kujiozesha mwenyewe mwanamke ambaye mtu ana madaraka juu yake bali mtu mwingine ndiye atamwozesha. Sababu waliyotoa ni:
1- Asili ya Rasuli katika kujiozesha ni kwamba hilo ni jambo mahsusi kwake mpaka ipatikane dalili ya kuwahusisha Waislamu wote. Hivyo haiwezekani kutolea dalili kwa Hadiyth ya Swafiyyah.
2- Haijuzu mwoaji kuwa mwozeshaji. Ni kama kutowezekana hakimu kuwa shahidi kwa wakati mmoja.
Ninasema: “Kauli inayosema kwamba inajuzu ndiyo yenye nguvu zaidi kwa vile hakuna dalili yoyote yenye kuzuia. Ama ndoa ya Swafiyyah, tukichukulia kwamba ndoa za Rasuli zina umahususi- na hili halina shaka- basi mbali ya hili, tunaona kwamba kuna Hadiyth nyingi tu sana zinazohimizia kumwoa kijakazi baada ya kumfundisha maadili mema na kumwacha huru. Na hili linawahusu wote.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
13: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti La Pili: Ridhaa Ya Mwanamke Kabla Ya Kuolewa:
Nyuma tushasema kwamba walii hana mamlaka ya kumlazimisha mwanamke kuolewa na mtu asiyemtaka, na ikiwa atamlazimisha, basi mwanamke ana haki ya kuwasilisha mashtaka yake kwa kadhi ili kuivunja ndoa.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
14: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti La Tatu: Mahari, Ni Sawa Yakatajwa Au Yasitajwe:
Ikiwa mke na mume watakubaliana kuoana bila mahari, basi ndoa hiyo inakuwa imeharibika, kwani mahari ni lazima, ni sawa yawe yametajwa au hayakutajwa.
Kushurutisha mahari katika ndoa ni madhehebu ya Maalik, moja ya riwaayah mbili toka kwa Ahmad, na ni chaguo la Sheikh wa Uislamu. Dalili ya wayasemayo ni:
1- Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَآتُوا النِّسَاءَ صَدُقَاتِهِنَّ نِحْلَةً"
“Na wapeni wanawake mahari zao kwa maridhawa”. [An-Nisaa: 04]
Wamesema kwamba maana ya نِحْلَةً ni kwa “Wajibu na lazima”, nayo ndio kauli ya Mufassiruna wengi. [Angalia Al-Qurtubiy na Ibn Kathiyr Suwrat An-Nisaa 04]
2- Kauli Yake Ta’aalaa:
"فَمَا اسْتَمْتَعْتُم بِهِ مِنْهُنَّ فَآتُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ فَرِيضَةً"
“Basi mliostarehe nao, wapeni mahari yao kuwa ni waajib.” [An-Nisaa: 24]
3- Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ أَن تَنكِحُوهُنَّ إِذَا آتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ"
“Na wala si dhambi kwenu kufunga nao nikaah mkiwapa mahari yao”. [Al-Mumtahinah: 10]
4- Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَامْرَأَةً مُّؤْمِنَةً إِن وَهَبَتْ نَفْسَهَا لِلنَّبِيِّ إِنْ أَرَادَ النَّبِيُّ أَن يَسْتَنكِحَهَا "
“Na mwanamke Muumini akijitunuku mwenyewe kwa Nabiy, ikiwa Nabiy anataka kumuoa”. [Al-Ahzaab: 50]
Hapa kuoa bila mahari ni mahsusi kwa Nabiy tu na si kwa mwingine yeyote.
5- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas:
" لَمَّا تَزَوَّجَ عَلِيٌّ فَاطِمَةَ عَلَيْهِمَا اَلسَّلَامُ قَالَ لَهُ رَسُولُ اَللَّهِ َصلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: أَعْطِهَا شَيْئًا، قَالَ: مَا عِنْدِي شَيْءٌ . قَالَ: فَأَيْنَ دِرْعُكَ الحُطَمِيَّةُ "
“ ‘Aliy alipomwoa Faatwimah (‘Alayhimas Salaam), Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia: Mpe chochote. Akasema: Sina kitu. Akamwambia: Liko wapi deraya lako la Kihutwami?” [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Abu Daawuwd (3125) na An-Nasaaiy (6/129)]
6- Hadiyth ya Sahl bin Sa’ad -kuhusiana na mwanamke aliyejipeleka mwenyewe kwa Rasuli kumwambia kuwa yuko tayari kuolewa naye bila mahari, na Rasuli hakuonyesha yuko tayari kwa hilo- ambapo sehemu ya Hadiyth inasema:
"فَقَامَ رَجُلٌ فَقَالَ: يا رَسُولَ الله، زَوِّجْنِيهَا إِنْ لَمْ يكُنْ لَكَ بِهَا حَاجَةٌ. فَقَالَ رَسُولُ الله صلى الله عليه وسلم: "هَلْ عِنْدَكَ مِنْ شيء تُصَدِقُهَا إِيَّاهُ؟ ". قَالَ مَا عِنْدِي.... فَقَالَ صلى الله عليه وسلم: "الْتَمِسْ وَلَوْ خَاتَمًا مِنْ حَدِيدِ "....[ثُمَّ قَالَ فِي آخِرِهِ] : زَوَّجْتُكَهَا بِمَا مَعَكَ مِنَ الْقُرْآنِ ".
“Mtu mmoja akasimama na kusema: Ee Rasuli wa Allaah! Niozeshe mimi ikiwa wewe humtaki. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: Je, una chochote ukampa kwacho mahari yake? Akasema: Sina. Rasuli akamwambia: Basi angalia hata pete ya chuma. [Kisha mwishowe akamwambia: Basi nimekuozesha kwa kiasi ulichohifadhi katika Qur-aan”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5149) na Muslim (1425)]
7- Yaliyosimuliwa toka kwa ‘Aaishah, amesema:
"أَمَرَنِي رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ لا أُدْخِلَ امْرَأَةً على زَوْجِهَا قَبْلَ أَنْ يُعْطِيَهَا شَيْئًا"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameniamuru nisimwingize mwanamke yeyote kwa mumewe kabla hajampa chochote”. [Hadiyth hii ni dhaifu. Imechakatwa na Abu Daawuwd kwa njia ya Khaythamah bin ‘Abdulrahmaan toka kwa ‘Aaishah]
Mwonekano wa Hadiyth na aayaat zote hizi, unaonyesha kwamba kutajwa mahari na kukabidhiwa ni sharti ya kuswihi kwa ndoa. Lakini, Allaah Aliposema:
"لَّا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ مَا لَمْ تَمَسُّوهُنَّ أَوْ تَفْرِضُوا لَهُنَّ فَرِيضَةً"
“Hakuna dhambi kwenu mkiwataliki wanawake ambao hamkuwagusa au kuwabainishia mahari yao”, aayah hii inaonyesha kwamba ndoa inaswihi bila ya kutaja mahari na kabla ya kuyakabidhi, na hii ndiyo itifaki ya ‘Ulamaa.
Lakini lenye uimara zaidi ni kauli ya kwanza. Sheikh wa Uislamu amesema (29/344): “Mwenye kusema kwamba mahari siyo yenye kukusudiwa, basi hiyo ni kauli isiyo na mashiko. Mahari ni nguzo ya nikaah, na kama itashurutishwa, inakuwa na uhakika zaidi kutokana na kauli yake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"إِنَّ أَحَقَّ الشُّرُوطِ أَنْ تُوفُوا بِهِ مَا اسْتَحْلَلْتُمْ بِهِ الْفُرُوجَ "
“Hakika sharti lenye haki zaidi ya nyinyi kulitekeleza, ni lile la kuhalalisha tupu”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5151) na Muslim (1418)]
Mali huhalalishwa kwa mbadala wake, na tupu hazihalalishwi ila kwa mahari. Na hakika si jinginelo, ndoa inafungika bila kutaja mahari au kuyakadiria, lakini hayakanushwi, lazima yawepo mahari tajwa au yaliyonyamaziwa”.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
Alhidaaya.com [3]
15: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti La Nne: Uwepo Wa Mashahidi (Kuishuhudishia) Au Kuitangazia Ndoa:
Kwa sharti hili, ndoa inajipambanua na uchafu wa zinaa. ‘Ulamaa wamekhitilafiana katika chenye kushurutishwa hapa, je, ni uwepo wa mashahidi au kuitangazia? Je, ni yote mawili, au kimojawapo? Au hakuna chochote katika hayo mawili? Wamekhitilafiana katika kauli tano:
Ya kwanza:
Uwepo wa mashahidi ni sharti, lakini kuitangaza ni jambo linalopendeza. Haya ni madhehebu ya Jumhuwr, ni kauli pia ya An-Nakh’iy, Ath-Thawriy na Al-Awzaaiy, na pia imepasishwa na waliokuja hivi mwishoni. Hoja zao ni:
1- Ziada ya “mashahidi wawili” iliyopo kwenye Hadiyth:
"لَا نِكَاحَ إِلَّا بِوَلِيٍّ [وَشَاهِدَيْ عَدْلِ]"
“Hakuna ndoa bila walii [na mashahidi wawili]”. Lakini ziada hii ina udhaifu kwa njia zote ingawa baadhi ya ‘Ulamaa wameipa usahihi.
Ash-Shaafi’iy amesema: “Na hii ijapokuwa imekatika (mpokezi mmoja amedondoka), lakini hata hivyo ‘Ulamaa wengi wanaizingatia, na wanasema: Tofauti kati ya ndoa na zinaa ni mashahidi”.
Naye At-Tirmidhiy amesema kuandamizia Hadiyth hii: “Hili (la uwepo wa mashahidi) ndilo lililofanywa na ‘Ulamaa katika Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na waliokuja baada yao kati ya Taabi’iyna na wengineo. Wote wamesema: “Hakuna ndoa ila kwa mashahidi”. Hakuna yeyote aliyekwenda kinyume na hilo katika wao, isipokuwa ‘Ulamaa waliokuja hivi mwishoni”.
2- Yaliyosimuliwa moja kwa moja toka kwa ‘Aaishah:
"كُلُّ نِكَاحٍ لَمْ يَحْضُرْهُ أَرْبَعَةٌ فَهُوَ سَفَاحُ: خَاطِبٌ، وَوَلِيُ، وَشَاهِدَانِ"
“Ndoa yoyote ambayo haijahudhuriwa na wanne, basi ni zinaa: Mposaji, walii na mashahidi wawili”. Hadiyth hii ni munkar, haizingatiwi.
3- Yaliyosimuliwa moja kwa moja toka kwa Ibn ‘Abbaas:
"الْبَغَايَا اللَّاتِي يُنْكِحْنَ أَنْفُسَهُنَّ بِغَيْرِ بَيِّنَةٍ"
“Wanawake wazinifu ni wale wanaojiozesha wenyewe bila ushahidi”. [Imechakatwa na Ad-Daaraqutwniy (3/224). Kuna mpokezi asiyejulikana katika mlolongo wa wapokezi wake]
4- Kauli ya Ibn ‘Abbaas:
"لا نِكَاحَ إِلاَّ بِشَاهِدَيْ عَدْلٍ وَوَلِيٍّ مُرْشِدٍ"
“Hakuna ndoa isipokuwa kwa mashahidi wawili waadilifu na walii mwenye busara”. [Angalia Al-Irwaa (6/235, 251)]
Ya pili:
Kuitangazia ni sharti lakini kuishuhudishia ni jambo linalopendeza. Na hili ndilo lililo sahihi. Wenye kauli hii ni Maalik, Ahmad na baadhi ya ‘Ulamaa wa Kihanafiy. Vile vile, ni chaguo la Sheikh wa Uislamu bin Taymiyah .
Wamesema: “Lau walii atamwozesha mwanamke bila kuwepo mashuhuda, kisha akaja kuitangaza ndoa na habari ikatangaa kati ya watu, basi ndoa ni sahihi na makusudio yanakuwa yamepatikana”.
Hoja zao ni:
1- Lililoamuriwa ni kutangazwa ndoa kama alivyosema Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"أَعْلِنُوا هذَا النِّكَاحَ واضْرِبُوا عَليْهِ بالغِرْبَالِ"
“Itangazieni nikaah hii, na ipigieni dufu”. [Swahiyh Ibn Maajah. Imechakatwa na Ibn Maajah (1895) na Al-Bayhaqiy (15094)]
Linalolengwa katika nikaah ni kudhihirishwa na kutangazwa ili ijipambanue na siri ambayo ni zinaa. Kutangazwa huku kunatangaa zaidi kuliko kushuhudiliwa na mashahidi, na kutangazwa kukitimia, basi hata uwepo wa mashuhuda unakuwa hahuhitajiki. Na kama ikishindikana kutangazwa, basi uwepo wa mashuhuda unakuwa ni waajib, kwa kuwa inakuwa ni sehemu ya tangazo.
2- Wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), watu walikuwa wakiwaozesha wanawake, na Rasuli hakuwa akiwaamuru washuhudishie ndoa. Kadhalika, hakuna Hadiyth iliyothibiti yenye kushurutisha uwepo wa mashahidi katika nikaah.
3- Ni jambo lisilowezekanika kuwa jambo hili ambalo Waislamu wamekuwa wakilifanya siku zote liwe na masharti ambayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuyabainisha. Ikiwa hivi, basi litakuwa ni tatizo kubwa mno. Na lau kama uwepo wa mashahidi ungekuwa ni sharti, basi Rasuli kutaja sharti hilis ingelikuwa muhimu zaidi kuliko kutaja mahari na mengineyo.
4- Mashuhuda wanaweza kufa, au hali zao zikabadilika.
5- Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwacha huru Swafiyyah kisha akamwoa bila mashuhuda. Toka kwa Anas:
"اشْتَرَى رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ جَارِيَةً بِسَبْعَةِ أَرْؤُسٍ، فَقَاَل النَّاس: مَا نَدْرِيْ أَتَزَوَّجَهَا رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَمْ جَعَلَهَا أُمَّ وَلَدٍ؟ فَلَمَّا أَنْ أَرَادَ أَنْ يَرْكَبَ حَجَبَهَا، فَعَلِمُوْا أَنَّهُ تَزَوَّجَهَا"
“ Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimnunua kijakazi (Swafiyyah) kwa (malipo ya) watumwa saba. Watu wakasema: Hatujui kama Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemwoa au amemfanya kijakazi wake wa kumzalia. Na alipotaka kupanda naye ngamia, alimfunika, na hapo wakajua kwamba amemwoa”.
Wa kundi la awali wameijibu hoja hii wakisema kwamba kuoa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bila mashuhuda ni jambo mahsusi kwake. Allaah Amemruhusu kumwoa mwanamke anayejitunukisha kwake bila mahari, na kwa hivyo kuoa bila mashahidi kunakubalika zaidi.
6- Mauziano ambayo Allaah Ta’aalaa Ameamuru uwepo ushuhuda ndani yake, zipo dalili zinazothibitisha kwamba ushuhuda huo si katika mambo ya lazima katika mauziano. Hivyo basi, ndoa ambayo Allaah Ta’alaa Hakutaja ndani yake ushuhuda, inastahiki zaidi ushuhuda usiwe katika shuruti zake.
Kauli ya tatu:
Ni sharti kutangazwa na uwepo wa mashahidi. Hii ni riwaayah ya tatu toka kwa Ahmad.
Kauli ya tano:
Si sharti kutangazwa wala kuwepo mashahidi. Ni kauli iliyokwenda kinyume na ‘Ulamaa wote (shaadh), nayo imenukuliwa toka kwa Ibn Abiy Laylaa na wengineo.
Ninasema: “Kwa yaliyotangulia, tunasema kwa muhtasari:
1- ‘Ulamaa wamekubaliana kwamba ndoa inayofungwa bila mashahidi wala kutangazwa ni batili.
2- Wamekubaliana kwamba ndoa inayoshuhudiwa na wanaume wawili au zaidi ya hapo na ikatangazwa, inakuwa ni sahihi.
3- Wamekhitilafiana kuhusiana na kuswihi ndoa ambayo imeshuhudiwa na mashahidi lakini haikutangazwa kwa watu, na ile iliyotangazwa lakini mashahidi hawakuwepo kama ilivyoelezwa hapo nyuma. Lililo karibu zaidi na usahihi hapa ni kwamba sharti ni kutangazwa ndoa kama mashahidi hawakuhudhuria, lakini uwepo wa mashahidi una akiba zaidi ya kuchunga na kuhifadhi haki za mke na watoto ambao baba yao anaweza kuwakana na nasaba kupotea”.
Faida Mbili:
Ya kwanza: Ikiwa mke na mume, walii na mashahidi wawili watakubaliana ndoa wasiitangaze, je, ndoa itaswihi?
Suala hili tunaweza kusema kwamba ni matunda ya mvutano wa suala lililopita. Anayeona kwamba mashahidi ni sharti, basi atasema ndoa ni sahihi, kwa kuwa mashahidi wawili wapo. Ama anayeona kutangazwa ni sharti, atasema ndoa ni batili kwa kuwa sharti la kutangazwa halipo.
Ya pili: Ni yapi masharti kwa mashahidi (kwa wanaosema ni sharti wawepo)?
1, 2- Akili na kubaleghe. Hili limekubaliwa na wote Ndoa haifungiki kwa asiyekuwa na viwili hivi.
3- Uislamu. Hili halina mvutano wowote ikiwa wanaofunga ndoa ni Waislamu. Ama ikiwa mke ni “dhimmiyyah” (si Muislamu na anaishi chini ya himaya ya Dola ya Kiislamu), kwa huyu, Abu Haniyfah na Abu Yuwsuf wamejuzisha mwanaume “dhimmiy” kuwa shahidi, lakini wengine wamekataa.
4- Wawe wanaume. ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy na Kihanbali wameshurutisha mashahidi wawili wawe ni wanaume, na wamekataa ushahidi wa wanawake. Ama ‘Ulamaa wa Kihanafiy, wao wamejuzisha ushahidi wa mwanaume mmoja na wanawake wawili. Ibn Hazm amesema hivyo hivyo na ameongezea juu ya hilo kwamba wanawake wanne wanatosha kuwa mashahidi.
5- Wawe waadilifu: Hili ni sharti kwa ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy na Kihanbali. Wanachokusudia kwa uadilifu kama inavyoonekana ni kuwa mashahidi hao wawe wamesitirika, yaani hawana dalili yoyote ya utendaji maovu. Ama ‘Ulamaa wa Kihanafiy, wao wamesema ndoa ni sahihi hata kama mashahidi ni watenda maovu.
6- Wawe ni wenye kusikia matamshi ya Iyjaab na Qabuwl na kufahamu pia makusudio yake.
Links
[1] https://www.alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/284
[2] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11911&title=10C-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20%D9%83%D8%AA%D8%A7%D8%A8%20%D8%A7%D9%84%D8%B2%D9%88%D8%A7%D8%AC%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20%D8%B9%D9%8E%D9%82%D9%92%D8%AF%D9%8F%20%D8%A7%D9%84%D8%B2%D9%91%D9%8E%D9%88%D9%8E%D8%A7%D8%AC%D9%90%20Kufunga%20Ndoa
[3] http://www.alhidaaya.com/
[4] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11912&title=01-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%20
[5] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11913&title=02-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%3A%20Masharti%20Ya%20Kufungika%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20%20Masharti%20Ya%20Tamko%20La%20%E2%80%98Aqdi
[6] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11914&title=03-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%3A%20Masharti%20Yanayowahusu%20Walii%20Na%20Mwoaji
[7] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11915&title=04-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%3AMasharti%20Ya%20Kuswihi%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20Sharti%20La%20Kwanza%3A%20%28a%29%20Idhini%20Ya%20Walii%20Wa%20Mwanamke
[8] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11916&title=05-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%3A%20Masharti%20Ya%20Kuswihi%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20Sharti%20la%20Kwanza%3A%20%20%28b%29%20Walii%20Hana%20Haki%20Ya%20Kumlazimisha%20Mwanamke%20Aliyebaleghe%20Kuolewa
[9] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11917&title=06-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%3AMasharti%20Ya%20Kuswihi%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20Sharti%20la%20Kwanza%3A%20%28c%29%20Kumlazimisha%20Bikra%20Aliye%20Baleghe
[10] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11918&title=07-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%3A%20Masharti%20Ya%20Kuswihi%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20Sharti%20la%20Kwanza%3A%20%28d%29%20Kumlazimisha%20Binti%20Mdogo
[11] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11919&title=08-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%3A%20Masharti%20Ya%20Kuswihi%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20Sharti%20la%20Kwanza%3A%20%28e%29%20Walii%20Kuzuia%20Ndoa
[12] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11920&title=09-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%3A%20Masharti%20Ya%20Kuswihi%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20Sharti%20la%20Kwanza%3A%20%28f%29%20Ni%20Nani%20Mawalii%3F
[13] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11921&title=10-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%3A%20Masharti%20Ya%20Kuswihi%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20Sharti%20la%20Kwanza%3A%20%28g%29%20Kuozesha%20Walii%20Wa%20Mbali%20Kama%20Wa%20Karibu%20Hayuko
[14] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11922&title=11-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%3A%20Masharti%20Ya%20Kuswihi%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20Sharti%20la%20Kwanza%3A%20%28h%29%20Masharti%20Ya%20Walii%3A
[15] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11923&title=12-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%3A%20Masharti%20Ya%20Kuswihi%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20Sharti%20la%20Kwanza%3A%20%28i%29%20Je%2C%20Walii%20Anaweza%20Kujiozesha%20Mwenyewe%20Mwanamke%20Ambaye%20Yeye%20Anasimamia%20Mambo%20Yake%3F
[16] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11924&title=13-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%3A%20Masharti%20Ya%20Kuswihi%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20Sharti%20La%20Pili%3A%20Ridhaa%20Ya%20Mwanamke%20Kabla%20Ya%20Kuolewa
[17] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11925&title=14-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%3A%20%20Masharti%20Ya%20Kuswihi%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20Sharti%20La%20Tatu%3A%20Mahari%2C%20Ni%20Sawa%20Yakatajwa%20Au%20Yasitajwe
[18] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11926&title=15-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kufunga%20Ndoa%3A%20%20Masharti%20Ya%20Kuswihi%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20Sharti%20La%20Nne%3A%20Uwepo%20Wa%20Mashahidi%20%28Kuishuhudishia%29%20Au%20Kuitangazia%20Ndoa