كتاب الزواج
Kitabu Cha Ndoa
الإِشْتِرَاطُ فِيْ عَقْدِ النِّكَاحِ
Kuwekeana Masharti Katika ‘Aqdi Ya Ndoa
Abu Maalik Kamaal Bin As-Sayyid Saalim
Imetarjumiwa na 'Abdullaah Mu'aawiyah (Abu Baasim)
Alhidaaya.com
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الإِشْتِرَاطُ فِيْ عَقْدِ النِّكَاحِ
Kuwekeana Masharti Katika ‘Aqdi Ya Ndoa
Alhidaaya.com [3]
01: Vigawanyo Vya Masharti: (a) Sehemu Ya Kwanza: Masharti yanayoendana na dhana ya ‘aqdi na makusudio ya kisharia.
Linalokusudiwa kiujumla ni mmoja kati ya wanandoa watarajiwa kumwekea mwenzake masharti yanayofungamanishwa na ‘aqdi ya ndoa au kabla ya kufungwa ‘aqdi.
Masharti haya yanagawanyika katika sehemu tatu:
Sehemu ya kwanza: Masharti yanayoendana na dhana ya ‘aqdi na makusudio ya kisharia.
Ni kama mke mtarajiwa kushurutisha mumewe mtarajiwa atangamane naye kwa wema, ampe matumizi, amnunulie mavazi na ampatie nyumba ya kuishi, na kama ana wake wengine, basi awatendee wote kwa usawa.
Au mume mtarajiwa ashurutishe mke asitoke nyumbani ila kwa idhini yake, au asimkatalie tendo la ndoa wakati akihitajia, au asitumie mali yake ila kwa ridhaa yake na mfano wa hayo.
Hukmu Ya Masharti Haya:
Kwa mujibu wa itifaki ya ‘Ulamaa, masharti haya yanakubalika kisharia, yako sahihi, na ni lazima yatekelezwe.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الإِشْتِرَاطُ فِيْ عَقْدِ النِّكَاحِ
Kuwekeana Masharti Katika ‘Aqdi Ya Ndoa
Alhidaaya.com [3]
02: Vigawanyo Vya Masharti: (b) Sehemu Ya Pili: Masharti yasiyoendana na dhana ya ‘aqdi, au yenye kukiuka Maagizo ya Allaah na Sharia Zake (masharti mabovu).
Ni kama mke mtarajiwa kushurutisha asimtii mumewe, au atoke bila idhini yake, au asiwape zamu wakewenza wake wala matumizi, au asimpe tendo la ndoa. Au ashurutishe asipewe mahari na mfano wa hayo. Haya yote ni masharti yanayokwenda kinyume na sharia.
Hukmu Ya Masharti Haya:
Kwa mujibu wa itifaki ya ‘Ulamaa, masharti kama haya hayafai, kwa kuwa ndanimwe kuna kuamuru Aliyoyakataza Allaah, au kukataza Aliyoyaamuru, au kuharamisha Aliyohalalisha, au kuharamisha Aliyohalalisha. Na hii ndio maana ya kauli yake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"مَنِ اشْتَرَطَ شَرْطًا لَيْسَ فِي كِتَابِ اللَّهِ فَهُوَ بَاطِلٌ، وَإِنِ اشْتَرَطَ مِائَةَ شَرْطٍ، شَرْطُ اللَّهِ أَحَقُّ وَأَوْثَقُ"
“Mwenye kushurutisha sharti lolote ambalo haliko katika Sharia za Allaah basi ni batili, hata akishurutisha masharti mia moja. Sharti la Allaah ndilo lenye haki kuliko yote na ndilo madhubuti zaidi”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (2155) na Muslim (1504)]
Lakini, Nini Hukmu Ya ‘Aqdi Yenye Masharti Batili Kama Haya?
Baada ya kujua kwamba masharti haya mabovu hayatakikani yawepo na yasitekelezwe, tunakuta kwa upande mwingine ‘Ulamaa wakikhitilafiana kuhusiana na hukmu ya ‘aqdi iliyowekewa masharti kama haya katika kauli tatu:
Kauli ya kwanza: ‘Aqdi haibatiliki kwa masharti mabovu, isipokuwa sharti la ndoa ya muda maalum (ndoa ya mut’a), sharti hili linabatilisha ‘aqdi.
Haya ni madhehebu ya Mahanafiy. Wanasema kwamba ndoa zilizokatazwa kama ndoa ya shighaar au ndoa ya kumhalalishia mke mtu aliyeacha talaka tatu, hizi zinaswihi ikiwa hazitokuwa na masharti mabovu isipokuwa ndoa ya mut’a, hii haiswihi, kwa kuwa sharti la muda maalum lipo ndani yake.
Kauli ya pili: Kuna ‘aqdi ambazo zinabatilika kwa kuwepo sharti bovu na kuna zingine ambazo hazibatiliki.
Haya ni madhehebu ya Mashaafi’iy na Mahanbali. Kidhibiti cha sharti ambalo linabatilisha ‘aqdi kwa mujibu wa mwono wao, ni sharti kuwa linafisidi dhana ya ndoa, kama vile mume kushurutisha amtaliki mke, au asimjimai, au ndoa iwe ya muda maalum.
Ama kidhibiti cha sharti ambalo halifisidi ndoa kwa mujibu wa mwono wao, ni kuwa sharti lisiwe linafisidi dhana ya ndoa. Ni kama mke kushurutisha awe na uhuru wa kutoka nyumbani wakati wowote atakao, au mume amtaliki mkemwenza wake na mfano wa hayo.
Kauli ya tatu: ‘Aqdi ambayo ndanimwe kuna sharti bovu ni batili.
Haya ni madhehebu ya kundi la ‘Ulamaa. Pia ni chaguo la Ibn Taymiyah. Hoja zao ni:
1- Katazo lililopo ndani ya masharti haya linatosha kubatilisha ‘aqdi mbali na kuwepo uharibifu ndani yake. Ni kama ndoa ya shighaar, ndoa ya mhalalishaji, au ndoa ya mut’a.
2- Maswahaba walitengua ndoa za aina hii kwa kumwachisha mke na mume katika ndoa ya shighaar, wakaifanya ndoa ya mhalalishaji kwa aliyemwacha mkewe talaka tatu kuwa ni zinaa, na wakatoa onyo kali kwa mhalalishaji kuwa atapigwa mawe hadi kufa.
3- Kuzifanya ndoa kama hizi kuwa ni sahihi sambamba na ubatilifu wa masharti mabovu, kunapelekea kulazimisha ndoa bila ya ridhaa za wanandoa wawili au mmoja wao. Kwa sababu, kusema kwamba ‘aqdi ni sahihi, ni ima iambatane na sharti haramu lisilofaa au iambatane na kulibatilisha sharti. Ikiwa hivi: (a) Tukisema ‘aqdi ni sahihi pamoja na uwepo wa sharti haramu ndani yake, hii itakuwa ni kinyume na Qur-aan na itifaki ya ‘Ulamaa. (b) Tukisema ‘aqdi ni sahihi pamoja na kuibatilisha sharti, hiyo itakuwa ni kumlazimisha mhusika kuingia kwenye ‘aqdi ambayo yeye hajaridhika nayo wala Allaah Hakumlazimisha. Na mikataba au makubaliano hayawi wajibishi ila ile tu ambayo Allaah Ameamuru iwe lazima mtu kuwajibika nayo. Hivyo basi, hiyo inakuwa ni kumlazimisha jambo ambalo Allaah na Rasuli Wake Hawajalilazimisha. Na hii haijuzu.
Ninasema: “Madhehebu haya ya mwisho ndiyo yenye nguvu zaidi isipokuwa yanatiwa dosari (kwa mujibu wa mwono wangu) na Hadiyth ya ‘Aaishah ambayo ndiyo mhimili katika mlango huu. Bi ‘Aaishah alipotaka kumnunua kijakazi (aitwaye Bariyrah) ili amkomboe na utumwa, watu wake walikataa kumuuza isipokuwa kwa sharti kwamba “Walaa” wa Bariyrah ubakie kwao wao. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
"اشْتَرِيهَا وَأَعْتِقِيهَا، فَإِنَّمَا الْوَلاَءُ لِمَنْ أَعْتَقَ، ثُمَّ قَامَ فَخَطَبَ: مَا بَال ُرِجَالٍ يَشْتَرِطُوْنَ شُرُوْطًا لَيْسَتْ في كِتَابِ اللهِ"
“Mnunue kisha mwache huru, kwani, hakika si jinginelo, “Walaa” ni kwa mwenye kuacha huru”. Kisha Rasuli akasimama na kukhutubu akisema: Inakuwaje watu wanashurutisha masharti ambayo hayako katika Hukumu za Allaah?! [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma]
"الوَلَاءُ"](Walaa) ni fungamano linalobakia kati ya mwenye kumkomboa mtumwa na mtumwa mwenyewe, yaani, ikiwa mtumwa huyu atakufa, na hana watu wake wa kumrithi, basi aliyemkomboa ndiye anamrithi kwa “Walaa”. “Walaa” ni kama nasaba].
Dalili hapa ni kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimruhusu aingie mkataba pamoja na uwepo ndanimwe sharti lisilofaa.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الإِشْتِرَاطُ فِيْ عَقْدِ النِّكَاحِ
Kuwekeana Masharti Katika ‘Aqdi Ya Ndoa
Alhidaaya.com [3]
03: Vigawanyo Vya Masharti: (c) Sehemu Ya Tatu: Masharti ambayo Allaah Hakuyaamuru wala Hakuyakataza, na ambayo kama yatashurutishwa yatakuwa na maslaha kwa mmoja wa wanandoa.
Ni kama mke kumshurutishia mume kwamba asimtoe toka nyumbani kwao au nchini kwake, au asisafiri pamoja naye, au asioe mke mwingine zaidi yake, au amwache aendelee na masomo yake au kazi yake na mfano wa hayo.
Hukmu yake: ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na kuswihi kwa masharti kama haya katika kufunga ‘aqdi katika kauli mbili:
Kauli ya kwanza: Masharti haya si halali, ni batili, lakini ‘aqdi ni sahihi. Ni madhehebu ya Jumhuwr ya ‘Ulamaa. Dalili zao ni:
1- Kwamba kiasili, mikataba na masharti ni marufuku isipokuwa ile tu ambayo sharia imehalalisha (kwa mwono wao).
2- Ni kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"مَا بَال ُرِجَالٍ يَشْتَرِطُوْنَ شُرُوْطًا لَيْسَتْ في كِتَابِ اللهِ؟ مَنِ اشْتَرَطَ شَرْطًا لَيْسَ فِي كِتَابِ اللَّهِ فَهْوَ بَاطِلٌ، شَرْطُ اللَّهِ أَحَقُّ وَأَوْثَقُ "
“Inakuwaje watu wanashurutisha masharti ambayo hayako katika Hukumu za Allaah?!. Mwenye kushurutisha sharti lolote ambalo haliko katika Sharia za Allaah basi ni batili. Sharti la Allaah ndilo lenye haki kuliko yote na ndilo madhubuti zaidi”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (2155) na Muslim (1504)]
Wamesema: “Katika Kitabu cha Allaah” ina maana ya Hukmu ya Allaah na Rasuli Wake, au katika yale yaliyoashiriwa na Qur-aan na Sunnah. Hivyo, hakuna sharti inayozingatiwa isipokuwa ile tu iliyopo ndani ya Viwili hivi.
3- Kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"الْمُسْلِمُونَ عَلَى شُرُوطِهِمْ إِلَّا شَرْطًا حَرَّمَ حَلَالًا أَوْ أَحَلَّ حَرَامًا"
“Waislamu ni lazima wachunge masharti waliyowekeana isipokuwa sharti lenye kuharamisha halali au lenye kuhalalisha haramu”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy na Muslim (59)]
Wamesema: Masharti haya yanakwenda kinyume na dhana ya mkataba wa ndoa. Kuyabadilisha ni sawa na kuyabadilisha Aliyoyawajibisha Allaah. Ni sawa na kuibadilisha ibada yoyote katika ibada za Kiislamu. Hivyo basi, kuoa kwake mke mwingine, kusafiri na mfano wa hayo -mambo ambayo ni halali- kunakuwa ni haramu kwa mujibu wa mkataba, na hii inakuwa ni kukiuka Mipaka ya Allaah na kuongeza jambo ambalo haliko kwenye dini.
Kauli ya pili: Masharti ni halali, si lazima kuyatekeleza, na mwanamke anaweza kuvunja ndoa mume asipoyatekeleza.
Ni madhehebu ya Al-Imaam Ahmad, Al-Awzaaiy, Is-Haaq, Abu Thawr, ni kauli iliyopokelewa toka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab, Sa-‘ad bin Abiy Waqqaasw, Mu’aawiyah na ‘Amri bin Al’Aaswiy (Radhwiya Allaah ‘anhum). Pia ni chaguo la Shaykhul Islaam. Hoja yao ni haya yafuatayo:
1- Asili ya mikataba na masharti ni jambo linaloruhusiwa kwa sababu ni katika mambo ya kawaida.
2- Ujumuishi wa Aayah na Hadiyth zenye kuamuru kutekeleza ahadi, masharti na mikataba. Kati yake ni:
(a) Kauli Yake Ta’aalaa:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَوْفُوا بِالْعُقُودِ"
“Enyi walioamini! Timizeni mikataba”. [Al-Maaidah: 01]
(b) Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَأَوْفُوا بِالْعَهْدِ ۖ إِنَّ الْعَهْدَ كَانَ مَسْئُولًا"
“Na timizeni ahadi, hakika ahadi itakuwa ni yenye kuulizwa”. [Al-Israa: 34]
(c) Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ"
“Na ambao amana zao na ahadi zao wanazichunga”. [Al-Muuminuwna: 08]
(d) Kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu alama tatu za mnafiki ambayo mojawapo ni kuwa akiahidi hatekelezi ahadi.
Hivyo basi, ikiwa kutekeleza na kuchunga ahadi ni jambo lililoamuriwa, itajulikana moja kwa moja kwamba asili ni kuswihi kwa mikataba na masharti husika. Kwa kuwa, hakuna maana ya kuhalalisha kitu bila kuwepo athari na makusudio yake, na makusudio ya mkataba, ni kuutekeleza.
3- Maana ya kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"كُلُّ شَرْطٍ لَيْسَ فِي كِتَابِ اللَّهِ فَهُوَ بَاطِلٌ وَإِنْ كَانَ مِائَةَ شَرْطٍ"
“Sharti lolote ambalo haliko ndani ya Kitabu cha Allaah, basi hilo ni batili hata kama ni masharti mia moja”… ni kwamba chochote kilichokanushwa, au kuharamishwa, au kubatilishwa ndani ya Kitabu cha Allaah, basi hicho ni batili, na kama hakuna kinachoashiria haya matatu, basi ni halali.
Au maana nyingine ya kuwepo ndani ya Kitabu cha Allaah, ni kile ambacho Allaah Ta’aalaa Amekihalalisha. Ikiwa kilichoshurutishwa ni kitendo au hukumu halali (kinafaa kufanywa au kuachwa), basi itajuzu kukishurutisha na ni wajibu pia kukitekeleza. Na kama Allaah Hakukihalalisha, basi haijuzu kukishurutisha.
4- Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"أَحَقُّ الشُّرُوطِ أَنْ تُوفُوا بِهِ مَا اسْتَحْلَلْتُمْ بِهِ الْفُرُوْجَ"
“Masharti yenye haki zaidi ya nyinyi kuyatekeleza, ni yale ambayo mmehalalishia kwayo tupu (kustarehe na mke)”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (2721) na Muslim (1418)]
Hadiyth inaonyesha kwamba kutekeleza masharti katika nikaah ni muhimu zaidi kuliko kwenye mikataba mingineyo. [Fat-hul Baariy (9/218)]
5- Hadiyth ya Al-Miswar bin Makhramah ambaye amesema:
"إنَّ عَلِيًّا خَطَبَ بنْتَ أبِي جَهْلٍ، فَسَمِعَتْ بذلكَ فاطِمَةُ، فأتَتْ رَسولَ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وسلَّمَ، فقالَتْ: يَزْعُمُ قَوْمُكَ أنَّكَ لا تَغْضَبُ لِبَناتِكَ، وهذا عَلِيٌّ ناكِحٌ بنْتَ أبِي جَهْلٍ! فَقامَ رَسولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عليه وسَلَّمَ، فَسَمِعْتُهُ حِينَ تَشَهَّدَ يقولُ: أمَّا بَعْدُ؛ أنْكَحْتُ أبا العاصِ بنَ الرَّبِيعِ، فَحدَّثَني وصَدَقَنِي، وإنَّ فاطِمَةَ بَضْعَةٌ مِنِّي، وإنِّي أكْرَهُ أنْ يَسُوءَها، واللَّهِ لا تَجْتَمِعُ بنْتُ رَسولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّمَ وبِنْتُ عَدُوِّ اللَّهِ عِنْدَ رَجُلٍ واحِدٍ، فَتَرَكَ عَلِيٌّ الخِطْبَةَ"
“ ‘Aliy alimchumbia binti ya Abu Jahl, na Faatwimah akasikia habari hiyo. (Faatwimah) akamwendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Watu wako wanazungumza wakidai kwamba wewe hukasiriki kwa adha inayowapata mabanati zako. Sasa huyo ‘Aliy anakwenda kumwoa bint ya Abu Jahl. Hapo hapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasimama, nami (Al-Miswar) nikamsikia baada ya kutashahadia akisema: Amma ba-‘adu: Nilimwozesha Abul ‘Aaswiy bin Ar-Rabiy’ah (binti yangu Zaynab), naye amekuwa mkweli kwa kila aliloniambia, na Faatwimah ni kipande kitokacho kwangu, na mimi nachukia yeyote kumfanyia lolote la kumuudhi. Naapa kwa Allaah! Binti ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na binti ya adui wa Allaah mustahili wawe wake wa mume mmoja. Na hapo ‘Aliy akaivunja posa”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (3729) na Muslim (2449)]
Al-Haafidh (7/86) amesema: “Huenda yeye (yaani Abul ‘Aaswiy), alikuwa amejiwekea mwenyewe sharti la kwamba hatomwolea Zaynab mke mwenza, na ‘Aliy kadhalika (kwa Faatwimah). Na kama si hivyo, basi uko uwezekano kwamba ima ‘Aliy alisahau sharti hilo akaenda kumposa (binti huyo wa Abu Jahl), au hakukuweko sharti lolote juu yake kwa kuwa hajaligusia au kulisema. Lakini pamoja na yote, ilikuwa anapaswa kuchunga hadhi, na kwa sababu hiyo, Rasuli akamlaumu”.
[Kadhalika, hakuna uharamu wa ‘Aliy kumwoa binti ya Abu Lahab. Rasuli anasema:
"وإنِّي لَسْتُ أُحرِّمُ حَلالًا، وِلَا أُحِلُّ حَرامًا"
“Na mimi kwa hakika siwezi kuharamisha la halali, au kuhalalisha la haramu”.
Tatizo hapa ni kuzuia kumuudhi Rasuli wa Allaah kutokana na adha itakayompata Faatwimah kama ndoa hiyo ingepita. Maudhi yanayompata Faatwimah, yanampata pia Rasuli wa Allaah hata kwa jambo la halali kama hilo la ndoa, ni sawa kwa wivu ambalo ni jambo la kimaumbile kwa wanawake, au hata hisia ya uadui wa Abu Lahab aliokuwa nao dhidi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam]
6- Toka kwa ‘Abdulrahmaan bin Ghanam, amesema: “Nilikuwa nimekaa kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab goti langu likiwa linagusana na goti lake. Mtu mmoja akamwambia ‘Umar: Nimemwoa huyu, lakini ameshurutisha abakie kwao nyumbani, na mimi nimeamua kuhamia mji mwingine. Akamwambia: Ana haki atimiziwe sharti lake. Mtu yule akasema: Kwa hali hii, wanaume wameangamia. Mwanamke akitaka kuvunja ndoa wakati wowote, anaivunja! ‘Umar akamwambia:
"المُسْلِمُونَ عَلَى شَرْطِهِمْ عِنْدَ مَقَاطِعِ حُقُوْقِهِمْ"
“Waislamu ni lazima wawajibishwe sharti walilowekeana mbele ya sehemu ya kuchanganua haki zao (mimbari au ofisi ya kadhi kama watazozana)”. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy amesema ni Mu’allaq (9/323), Sa’iyd bin Mansuwr amesema ni Mawsuwl (663), ‘Abdulrazzaaq (10608), Ibn Abiy Shaybah (4/199) na Al-Bayhaqiy (7/249]
7- Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"الْمُسْلِمُونَ عَلَى شُرُوطِهِمْ إِلَّا شَرْطًا حَرَّمَ حَلَالًا أَوْ أَحَلَّ حَرَامًا"
“Waislamu ni lazima wachunge masharti waliyowekeana isipokuwa sharti lenye kuharamisha halali au lenye kuhalalisha haramu”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy na Muslim (59)]
Kiufupi, ikiwa mwanamke atamshurutishia mumewe kwamba asioe mke mwingine zaidi yake, kwa mujibu wa sharti hili, ikiwa mwanaume huyu ataoa mwingine, basi si haramu kwake. Na akioa kweli, basi mwanamke ana haki ya kuvunja ndoa.
Ninasema: “Kauli iliyo na nguvu zaidi ni kuwa kuweka sharti kwa jambo ambalo ni la halali kisharia (yaani ambalo inafaa kulifanya au kuliacha) na ambalo sharia haijalikataza, kunajuzu katika ndoa kwa mujibu wa dalili zilizotangulia, na pia watu wanaweza kuhitajia hilo katika baadhi ya nyakati. Na ikiwa mmoja wa wana ndoa atakiuka masharti, basi mwingine atakuwa na haki ya kuvunja ndoa. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الإِشْتِرَاطُ فِيْ عَقْدِ النِّكَاحِ
Kuwekeana Masharti Katika ‘Aqdi Ya Ndoa
Alhidaaya.com [3]
04: Nini Hukmu Ya Ndoa Ya Misyaar المِسْيَارُ?
“Ndoa ya “Misyaar” ni katika aina za ndoa zilizojitokeza katika miaka ya hivi mwishoni katika baadhi ya nchi. Ndoa hii inakuwa kwa mwanaume kufunga ndoa halali ya kisharia na mwanamke ikitimiza masharti yote na nguzo zote, isipokuwa tu mwanamke anaachilia kwa ridhaa yake mwenyewe baadhi ya haki zake stahiki za ndoa kama makazi ya kuishi, pesa za matumizi, mume kulala kwake, zamu ya kulala kama mwanaume ana wake wengine na mfano wa hayo.
Miongoni mwa sababu kubwa zilizopelekea kujitokeza kwa aina hii ya ndoa na kuenea kwenye baadhi ya nchi, kwa upande wa wanawake, ni kuwepo idadi kubwa ya wanawake waliofikia umri wa kuolewa na umri wao ukasonga mbele bila ya kuolewa, au kuwa waliolewa kisha wakafarikiana na waume zao kwa sababu ya kifo au talaka, kutafuta shibisho halali la hamu ya tendo la ndoa, na mwanamke kuhitajia tu kuwa na mwanaume pembeni yake.
Ama kwa upande wa wanaume, baadhi yao wanaweza kusukumwa kwenye ndoa hii kutokana na matamanio makali ya kujimai, kutotosheka na mke mmoja, kutokuwa na uwezo wa kubeba gharama za kuoa mke mwingine kuanzia mahari, matumizi, nyumba na kadhalika, kuwa na tamaa ya kutwaa mali za mwanamke hususan akiwa tajiri na sababu nyinginezo.
Hukmu Ya Ndoa Hii:
Inabainika kutokana na taarifu kwamba, ndoa ya “Misyaar” ni ndoa yenye sharti la kudondosha baadhi ya haki za mke zinazomlazimu mume. Kwa picha hii, Fuqahaa wa enzi yetu ya leo wamekhitilafiana kuhusiana na kuswihi kwa ndoa hii katika kauli tatu:
Kauli ya kwanza:
Ni halali pamoja na ukaraha. Ni halali kwa sababu imetosheleza nguzo na masharti ya kisharia, na pia haikufanywa kuwa njia ya kwenda kwenye haramu kama ndoa ya mhalalishaji au ya muda maalum (mut’a). Mhimili mkuu hapa ni kuwa wote wawili wamekubaliana kwa ridhaa yao kwamba mke hana haki ya mume kulala kwake, au kupata zamu sawa na wake wengine, au kupewa pesa za matumizi na kadhalika.
Imethibiti kwamba Mama wa Waumini Sawdah binti Zum-‘atah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) alipozeeka, aliitoa siku yake ya Rasuli kulala kwake kwa mke mwenza wake ‘Aaishah. Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawa anagawa siku mbili kwa ‘Aaishah; siku yake na siku ya Sawdah. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5212) na Muslim (1463)]
Tunafahamu kutokana na Hadiyth hii kwamba mwanamke ana haki ya kudondosha baadhi ya haki zake alizodhaminiwa na sharia kama pesa za matumizi au mume kulala kwake na kadhalika.
Halafu, ndoa ni shibisho la hisia za kimaumbile za mwanamke za jimai, lakini pia ndoa inamzuia asifanye machafu, isitoshe, anaweza kwa ndoa hiyo kupata mtoto.
Ama siri ya ndoa hii kuwa na ukaraha, ni kuwa -pamoja na uhalali wake- lakini inakosa ufanikishaji wa dhana ya kisharia ya ndoa kama nyumba ya utulivu, mume kuwa karibu na mkewe na watoto, uangalizi wa karibu wa familia, malezi bora na kadhalika.
Kauli ya pili:
Ni haramu. Kwa sababu:
(a) Inakwenda kinyume na makusudio ya ndoa kwa upande wa kijamii, kisaikolojia na kisharia kati ya mapenzi, huruma, makazi tulivu, na kusimamia haki na mawajibiko yanayozalikana kutokana na ‘aqdi ya ndoa ya kisharia. Mazingatio katika mikataba ni dhana na maana, na si matamshi.
(b) Inakwenda kinyume na mfumo wa ndoa ulioletwa na sharia, na Waislamu hawakuwa wakijua aina hii ya ndoa huko nyuma.
(c) Ndanimwe kuna baadhi ya masharti yanayokiuka makusudio na dhana ya ‘aqdi.
(d) Ni njia ya kuleta uharibifu. Ndoa haitoi uzito wa kukadiria mahari, mume habebi jukumu la familia, na inaweza pia kuwa ni siri au bila ya walii.
Kauli ya tatu:
Kunyamazia na kuivutia subra hukmu yake. Ni maneno yaliyonukuliwa toka kwa Al’Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahul Laah).
Ninasema: “Kipambanuzi cha mvutano ni uoanishaji wa sharti la kudondosha matumizi na kulala na upeo wa athari yake kwa upande wa kuswihi kwa ‘aqdi ya ndoa. Nasi tumeshasema nyuma kwamba masharti yanayohusiana na ‘aqdi ya ndoa ni ya aina tatu: Kwanza: Masharti yanayoendana na dhana ya ‘aqdi na dhana ya kisharia. Pili: Masharti yasiyoendana na dhana ya ‘aqdi, au yenye kwenda kinyume na Hukmu ya Allaah na Sharia Yake (masharti mabovu). Tatu: Masharti ambayo Allaah Hakuyaamuru wala Hakuyakataza, na ambayo kama yatashurutishwa yatakuwa na maslaha kwa mmoja wa wanandoa.
Ninaloliona mimi kuwa lina nguvu ni kwamba kushurutisha kudondosha matumizi, kulala na mfano wa hayo katika mambo ambayo ni ya wajibu kisharia kwa mume, ni katika masharti mabovu. Hivyo basi nasema kiufupi kwamba ‘aqdi ni sahihi, na ndoa ni sahihi, lakini masharti ndio mabovu. Na ndoa hii itabeba athari zote za kisharia ikiwa ni pamoja na uhalali wa kimwingilia mke, kuthibiti nasaba kwa watoto watakaozaliwa, wajibu wa kutoa matumizi na zamu ya kulala kwake. Kadhalika, ni haki ya mwanamke kuzidai haki hizo. Lakini, ikiwa mwenyewe ataridhia kuziachia, basi hakuna ubaya, kwa kuwa ni haki yake.
Juu ya yote haya, ni lazima tukumbuke kwamba aina hii ya ndoa haisalimiki na kuwemo ndani yake ukaraha. Kadhalika, wigo wake usiachiwe ukatanuka kiholela. Na huenda picha hii imewafanya baadhi ya ‘Ulamaa kunyamazia kuhusu hukmu yake. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi usahihi wake”.
Links
[1] https://www.alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/284
[2] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11936&title=10D-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20%D9%83%D8%AA%D8%A7%D8%A8%20%D8%A7%D9%84%D8%B2%D9%88%D8%A7%D8%AC%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20%D8%A7%D9%84%D8%A5%D9%90%D8%B4%D9%92%D8%AA%D9%90%D8%B1%D9%8E%D8%A7%D8%B7%D9%8F%20%D9%81%D9%90%D9%8A%D9%92%20%D8%B9%D9%8E%D9%82%D9%92%D8%AF%D9%90%20%D8%A7%D9%84%D9%86%D9%91%D9%90%D9%83%D9%8E%D8%A7%D8%AD%D9%90%20Kuwekeana%20Masharti%20Katika%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%20
[3] http://www.alhidaaya.com/
[4] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11937&title=01-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kuwekeana%20Masharti%20Katika%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20%28a%29%20Vigawanyo%20Vya%20Masharti
[5] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11938&title=02-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kuwekeana%20Masharti%20Katika%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20%28b%29%20Vigawanyo%20Vya%20Masharti%20
[6] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11939&title=03-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kuwekeana%20Masharti%20Katika%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20%28c%29%20Vigawanyo%20Vya%20Masharti%20
[7] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11940&title=04-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Kuwekeana%20Masharti%20Katika%20%E2%80%98Aqdi%20Ya%20Ndoa%3A%20Nini%20Hukmu%20Ya%20Ndoa%20Ya%20Misyaar%20%D8%A7%D9%84%D9%85%D9%90%D8%B3%D9%92%D9%8A%D9%8E%D8%A7%D8%B1%D9%8F%3F