كتاب الزواج
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Abu Maalik Kamaal Bin As-Sayyid Saalim
Imetarjumiwa na 'Abdullaah Mu'aawiyah (Abu Baasim)
Alhidaaya.com
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
01: Taarifu Yake Na Hukmu Yake:
"الصَّدَاقُ" katika istilahi, ina maana ya badali inayotolewa kwa ajili ya ndoa au mfano wake, ni sawa kwa kupangwa na mtawala, au kwa kuridhiana kati ya mke na mume. Inaitwa pia "مَهْرٌ" , "أَجْرٌ" na "فَرِيْضَةٌ" na kadhalika.
Sababu ya kuitwa "الصَّدَاقُ" , ni neno lenyewe kuhisisha ukweli wa utashi wa mwanaume kumwoa mwanamke.
Mahari hii ni wajibu kwa mwanaume kwa sababu ya kuoa au kumuingilia mwanamke kwa mujibu wa ‘Ijmaa ya Ulamaa wa Kiislamu. Uimara wa ‘Ijmaa hii hautiwi doa na Mahanafiy na Mashaafi’iy ambao wao wamejuzisha kutokuwepo mahari kwenye ndoa kama ilivyoelezwa nyuma.
Na nyuma ishaelezwa kwamba mahari ni sharti kwa ajili ya kuswihi kwa ‘aqdi ya ndoa, ni sawa mahari iliyobainishwa ikatajwa au ambayo haikubainishwa. Mwanamke atapewa mahari mfano wake kwa mujibu wa kauli mbili za ‘Ulamaa zilizo sahihi zaidi.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
02: Kinachofaa Kutolewa Kama Mahari:
1- Ni kila kinachofaa kuwa thamani katika mauzo au manunuzi.
Kinachotolewa ni sharti kiwe kinabeba thamani, kiwe twahara, kiwe halali, kiwezekanike kupatiwa manufaa, au kiwe chenye kuweza kukabidhika kama fedha, vitu na kadhalika. Allaah Ta’aalaa Amesema:
"وَأُحِلَّ لَكُم مَّا وَرَاءَ ذَٰلِكُمْ أَن تَبْتَغُوا بِأَمْوَالِكُم مُّحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ"
“Na mmehalalishiwa wengineo wasiokuwa hao, mtafute (kuwaoa) kwa mali zenu mkijistahi pasi na kuzini”. [An-Nisaa: 24]
2- Kazi ya kuweza kulipwa:
Kazi kama hii inafaa kuwa mahari. Ni kama kufundisha Qur-aan, kutengeneza bidhaa, kutoa huduma na kadhalika. Ni madhehebu ya Shaafi’iy na Ahmad, Abuu Haniyfah amelikataa hili, na Maalik kalikirihisha.
Lililo sahihi ni kujuzu. Allaah Ta’aalaa Ametuhadithia katika Qur-aan kisa cha mzee mwema aliyemwozesha Muwsaa (‘alayhis salaam) mmoja ya binti zake wawili, na akaifanya kazi ya kumtumikia kwa muda wa miaka minane iwe ndiyo mahari ya binti. Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
"قَالَ إِنِّي أُرِيدُ أَنْ أُنكِحَكَ إِحْدَى ابْنَتَيَّ هَاتَيْنِ عَلَىٰ أَن تَأْجُرَنِي ثَمَانِيَ حِجَجٍ ۖ فَإِنْ أَتْمَمْتَ عَشْرًا فَمِنْ عِندِكَ"
“Akasema: Mimi nataka nikuozeshe mmojawapo wa binti zangu hawa wawili kwa sharti kuwa unitumikie miaka minane; ukitimiza kumi, basi ni uamuzi wako”. [Al-Qaswas: 27]
Na hii ni kwa mujibu wa ‘Ulamaa waliosema kwamba sharia za waliopita kabla yetu ni sharia ambazo zinatuhusu pia sisi mpaka iwepo dalili ya kuonyesha kwamba hazituhusu.
Na nyuma tumeielezea Hadiyth kuhusiana na mwanamke aliyejinadi mwenyewe kwa Rasuli ili amwoe bure bila mahari, lakini Rasuli hakumjibu kitu, kisha akajitokeza mtu kutaka kumwoa badala yake, na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
"اذْهَبْ، فَقَدْ زَوَّجْتُكَهَا بِمَا مَعَكَ مِنَ الْقُرْآنِ"
“Nenda, nishakuozesha yeye kwa Qur-aan uliyoihifadhi”, lakini kwa taawili ya kwamba makusudio ni amfundishe suwrah moja ya Qur-aan au zaidi.
3- Kumwacha huru kijakazi:
Toka kwa Anas, amesema:
"أَعْتَقَ رَسُولُ اللَّهِ صلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ صَفِيَّةَ وَجَعَلَ عِتْقَهَا صَدَاقَهَا"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwacha huru Swafiyyah na akakufanya kumwacha huru huko kuwa ndiyo mahari yake”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy na Muslim]
Ash-Shaafi’iy, Ahmad na Daawuwd, hawa ndio waliojuzisha kuachwa huru kuweza kuwa mahari. Lakini Fuqahaaul Amswaar (Fuqahaa saba wa Madiynah wa enzi hizo) wamelipinga hili kwa kuwa linapingana na usuwl. Wanasema sababu ni kwamba kuacha huru ni kuvua umiliki, na kuvua huku hakujumuishi kupatiwa manufaa kwa jambo jingine lolote, kwani, kijakazi huyo akiachwa huru, hapo hapo anajimiliki mwenyewe, sasa vipi alazimikiwe kuolewa kwa hilo? Ama kwa Hadiyth, wamesema kwamba la Rasuli na Swafiyyah, hilo ni jambo mahsusi kwake na si kwa wengine, kwani kuna mengi yahusuyo ndoa ambayo ni mahsusi kwake tu.
Ninasema: “Inavyoonekana kwa picha ya nguvu ni kwamba kuachwa huru kunajuzu kuwa mahari kutokana na Hadiyth iliyotangulia. Na asili ya matendo ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni yawe kiigizo na kielelezo kwetu isipokuwa kwa yale ambayo yana dalili ya umahususi kwake kama kumwoa mwanamke aliyejitolea kwake mwenyewe bila mahari au kuoa zaidi ya wanawake wanne. Na hayo waliyoyaelezea ya kupingana na uswuwl hayakinzaniwi kwayo Hadiyth hii. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.
4- Kusilimu Mume
Anas amesema:
"تَزَوَّجَ أَبُو طَلْحَةَ أُمَّ سُلَيْمٍ، فَكَانَ صَدَاقُ مَا بَيْنَهُمَا الْإِسْلَامَ، أَسْلَمَتْ أُمُّ سُلَيْمٍ قَبْلَ أَبِي طَلْحَةَ فَخَطَبَهَا فَقَالَتْ: إِنِّي قَدْ أَسْلَمْتُ فَإِنْ أَسْلَمْتَ نَكَحْتُكَ فَأَسْلَمَ فَكَانَ صدَاقَ مَا بَينهمَا"
“Abu Twalha alimwoa Ummu Sulaym, na mahari kati yao ilikuwa ni kusilimu. Ummu Sulaym alisilimu kabla ya Abu Twalha. Abu Twalha akamposa, lakini akamwambia: Mimi nimesilimu, na kama na wewe utasilimu, basi nitakubali unioe. Akasilimu, na kukawa ndio mahari kati yao”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na An-Nasaaiy (6/114)]
Hadiyth hii ni hoja kwa waliojuzisha kusilimu mwanaume kuwa mahari yake. Lakini Muhammad bin Hazm amepinga kuitolea Hadiyth hii dalili kwa mambo mawili:
La kwanza: Hilo lilikuwa kabla ya kuhamia Madiynah kwa muda, na Abu Twalha alikuwa amesilimu kitambo. Yeye ni katika watu wa mwanzo wa Madiynah kusilimu, na wala halikuwa bado limeshuka wajibisho la kuwapa wanawake mahari.
La pili: Hakuna katika taarifa hii lolote linalojulisha kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ana habari nalo.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
03: Kiwango Cha Juu Zaidi Na Cha Chini Zaidi Cha Mahari :
1- Hakuna mpaka wa kiwango cha juu zaidi cha mahari. ‘Ulamaa wote -bila ya kupinga hata mmoja wao- wamekubaliana kwamba mahari anayolipa mwanamume kwa mkewe hayana mpaka wa kiwango cha juu.
Sheikh wa Uislamu amesema: “Mwenye uwezo na mwenyewe akapenda kumpa mkewe mahari mengi, basi hakuna ubaya. Ni kama Alivyosema Allaah Ta’aalaa:
"وَآتَيْتُمْ إِحْدَاهُنَّ قِنطَارًا فَلَا تَأْخُذُوا مِنْهُ شَيْئًا"
“Na mmempa mmoja wao mirundi ya mali, basi msichukue kutoka humo chochote”. [An-Nisaa: 20]
2- Na pia hakuna mpaka wa kiwango cha chini zaidi cha mahari kwa kauli yenye nguvu. Mahari yanafaa kwa kila kile ambacho kinaweza kuitwa mali, au kinachotiwa thamani kwa mali madhali tu yapo maridhiano kati ya mke na mume. Haya ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-haaq, Abu Thawr, Al-Awzaaiy, Al-Layth, Ibn Al-Musayyib na wengineo. Na Ibn Hazm kafikia kujuzisha kila kile chenye nusu hata punje ya shayiri. Dalili zinazotilia nguvu rai hii ya kutokuwepo mpaka wa kiwango cha chini kabisa cha mahari ni hizi zifuatazo:
(a) Ujumuishi wa Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَأُحِلَّ لَكُم مَّا وَرَاءَ ذَٰلِكُمْ أَن تَبْتَغُوا بِأَمْوَالِكُم مُّحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ"
“Na mmehalalishiwa wengineo wasiokuwa hao, mtafute (kuwaoa) kwa mali zenu mkijistahi pasi na kuzini”. [An-Nisaa: 24]
Na hii ni kwa mali nyingi au kidogo.
(b) Kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa yule aliyetaka kumwoa mwanamke aliyejitolea aolewe na yeye bila mahari:
"اذْهَبْ فَاطْلُبْ وَلَوْ خَاتَمًا مِنْ حَدِيدٍ"
“Nenda ulete hata pete ya chuma”. [Imetajwa nyuma]
Hadiyth inaonyesha kwamba mahari yanafaa kwa kila kile kinachoitwa mali.
Bali mahari yanafaa kwa kila kile chenye thamani ya kugusika au isiyo ya kugusika. Na hili ndilo ambalo dalili zinakutana kwalo na kukubaliana na maana sahihi ya uhalali wa mahari, kwani makusudio ya mahari si kutolewa mali tu, bali mahari ni alama ya utashi na nia ya kweli ya mwanaume ya kumwoa mwanamke. Na mahari hii hutolewa zaidi ikiwa mali, na pia kwa kila kile chenye thamani isiyogusika madhali mke yuko radhi nayo (kama kufundishwa Qur-aan na kadhalika).
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwozesha mtu kwa Qur-aan aliyoihifadhi, mahari ya Abu Twalha kumwoa Ummu Sulaym ikawa ni yeye kusilimu, na Rasuli akakufanya kumwacha huru Swafiyyah ndio mahari yake. Kunufaika kwa Qur-aan, elimu na kusilimu mume, na Bi Swafiyyah kunufaika kwa kupata uhuru wa kujimiliki mwenyewe, yote hayo yamekuwa ni mahari. Na hii yote ikiwa mwanamke mwenyewe ataridhia, kwani kiasili, mahari ni haki yake.
Kupandisha Kiwango Cha Mahari Kupita Kiasi:
Si katika Uislamu tabia hii iliyotawala kwenye vichwa vya baadhi ya watu ya kutoza mahari ya juu kupita kiasi mpaka kufikia watu mara wanapotoka kwenye mnasaba wa ndoa, kuwa hawana jingine wanalolizungumzia isipokuwa mahari ya juu waliyoisikia. Wanakuwa kama vile wametoka kwenye mnada wa kuuza bidhaa.
Mwanamke siyo bidhaa kwenye soko la ndoa mpaka watu wagandamane na tabia hii ya uchu wa mali ambayo matokeo yake yanakuwa ni mabaya kama tunavyoona katika picha hizi zifuatazo:
1- Inawafanya vijana wengi kukimbia ndoa na wasichana wengi pia kubakia bila kuolewa.
2- Mmomonyoko wa tabia huwakumba wasichana na wavulana wakati wanapokata tamaa ya ndoa, na hivyo kutafuta mbadala wa hilo.
3- Magonjwa ya kisaikolojia huwapata wavulana na wasichana kutokana na mkwamo na matumaini yao kugonga mwamba.
4- Watoto wengi huacha kuwasikiliza wazazi wao na wanaziasi desturi na tabia njema za vizazi na vizazi.
5- Mwanaume akilipishwa mahari ya kumzidi uwezo wake, huzalikana uadui na uhasama kwenye moyo wake dhidi ya mkewe na watu wake.
Yanayotakiwa Kuhusiana Na Suala Hili:
1- Ni kupunguza na kutopandisha.
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"خَيْرُ الصَّدَاقِ أَيْسَرُهُ"
“Mahari yenye kheri zaidi ni yale yaliyo kidogo zaidi.” [Mustadrak Al-Haakim (2/182)]
Ibn Al-Qayyim amesema: “Kuweka mahari ya bei ya juu mno ni makruhu katika ndoa, hupunguza baraka ya ndoa na huleta ugumu”.
‘Umar bin Al-Khattwaab amesema:
" أَلَا لَا تُغْلُوا صُدُقَ النِّسَاءِ أَلَا لَا تُغْلُوا صُدُقَ النِّسَاءِ فَإِنَّهَا لَوْ كَانَتْ مَكْرُمَةً فِي الدُّنْيَا أَوْ تَقْوَى عِنْدَ اللَّهِ كَانَ أَوْلَاكُمْ بِهَا النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مَا أَصْدَقَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ امْرَأَةً مِنْ نِسَائِهِ وَلَا أُصْدِقَتْ امْرَأَةٌ مِنْ بَنَاتِهِ أَكْثَرَ مِنْ ثِنْتَيْ عَشْرَةَ أُوقِيَّةً وَإِنَّ الرَّجُلَ لَيُبْتَلَى بِصَدُقَةِ امْرَأَتِهِ وَقَالَ مَرَّةً وَإِنَّ الرَّجُلَ لَيُغْلِي بِصَدُقَةِ امْرَأَتِهِ حَتَّى تَكُونَ لَهَا عَدَاوَةٌ فِي نَفْسِهِ وَحَتَّى يَقُولَ كَلِفْتُ إِلَيْكِ عَلَقَ الْقِرْبَةِ "
“Zindukeni! Msipandishe juu mahari za wanawake. Zindukeni! Msipandishe juu mahari za wanawake. Kwani, lau kama lingelikuwa ni jambo lenye kumletea mtu utukuzo duniani, au kuwa ndio uchamungu mbele ya Allaah, basi Rasuli angelikuwa ndiye anastahiki zaidi kulifanya hilo kuliko nyinyi. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakulipa mahari za wake zake, wala hakuna yeyote katika mabinti zake aliyelipiwa mahari ya zaidi ya uqiya 12 (dirham 480). Na kwa hakika mtu anaweza kuingia kwenye matatizo makubwa kutokana na mahari ya mkewe. Na akasema mara nyingine: Mtu kwa hakika atamlipa mke wake mahari nyingi kisha hilo likazalisha uadui ndani ya nafsi yake na kujikuta akijiambia mwenyewe: Umenifilisi kila kitu mpaka kamba ya kutundikia kiriba changu”. [Ni Swahiyh. Abu Daawuwd (2106), At-Tirmidhiy (1114), An-Nasaaiy (6/117), na Ibn Maajah (1887)]
Bibi ‘Aaishah alipoulizwa kuhusu kiasi cha mahari ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alijibu:
"كَانَ صَدَاقُهُ لأَزْوَاجِهِ ثِنْتَىْ عَشْرَةَ أُوقِيَّةً وَنَشًّا. قَالَتْ أَتَدْرِي مَا النَّشُّ؟ قَالَ قُلْتُ لاَ. قَالَتْ نِصْفُ أُوقِيَّةٍ. فَتِلْكَ خَمْسُمِائَةِ دِرْهَمٍ، فَهَذَا صَدَاقُ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم لأَزْوَاجِهِ."
“Mahari ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa wakeze yalikuwa ni uqiya 12 na nash. Akauliza: Unajua nash ni kiasi gani? Nikasema: Sijui. Akasema: Ni nusu uqiya, kwa hivyo hizo ni dirhamu 500. Na haya ndiyo mahari ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa wakeze”. [Muslim (1426), An-Nasaaiy (6/116) na Ibn Maajah (1886)]
Sheikh wa Uislamu amesema: “Na yule ambaye nafsi yake itamghilibu kuzidisha mahari ya binti yake zaidi ya mahari ya mabinti wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambao wao ndio viumbe walio bora zaidi wa Allaah juu ya wanawake wa walimwengu katika kila sifa, au kuliko mahari za Mama za Waumini, basi mtu huyo ni jaahil na mpumbavu. Na hii ni pamoja na uwezo na wasaa. Ama aliye masikini na mfano wake, huyo hatakiwi kumpa mwanamke kile ambacho hana uwezo wa kukilipa na kujibebesha mwenyewe mazito”.
2- Ikiwa kupandisha juu sana mahari ni uzito na taklifu kwa mume, basi hilo linakuwa ni lenye kulaumiwa.
Katika Hadiyth ya Abu Hurayrah, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuuliza mtu ambaye amekusudia kumwoa mwanamke wa Kianswaar:
"عَلَى كَمْ تَزَوّجْتَهَا؟ قَالَ: عَلَى أَرْبَعِ أَوَاقٍ، فَقَالَ لَهُ النَّبِيُّ صلى الله عليه وسلم: عَلَى أَرْبَعِ أَوَاقٍ؟ كَأَنّمَا تَنْحِتُونَ الفِضَّةَ مِنْ عُرْضِ هذَا الجَبَلِ"
“Utamwoa kwa mahari kiasi gani? Akasema: Kwa uqiya nne. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Kwa uqiya nne (mbona nyingi sana)?! Kana kwamba mnachimba fedha toka kwenye kina cha mlima huu“. [Muslim (1424) na An-Nasaaiy (6/69)]
Toka kwa Abu Hadrad Al-Aslamiy, amesema:
" أتَيتُ رسولَ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّمَ أَسْأَلُهُ في صَدِاقٍ، فَقَالَ: كَمْ أَصْدَقْتَ؟ قُلْتُ: مِئَتَيْ دِرهَمٍ، قَالَ: لَوْ كُنْتُمْ تَغرِفونَ مِن بُطحانَ، لمَا زادَ"
“Nilimwendea Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwomba anisaidie mahari. Akaniuliza: Umepanga kutoa kiasi gani? Nikamjibu: Dirhamu 200. Akasema: Hata mngelikuwa mnachota (dirham) toka kwenye bonde (kama maji), isingelipendeza kuzidi zaidi ya hizo”. [Ahmad (3/448) na Al-Bayhaqiy (7/235) kwa Sanad swahiyh]
Katika Hadiyth hizi mbili, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anapinga na kushangaa wanaume hawa kutozeshwa mahari kubwa wakati hali zao za kifedha ni ngumu. Lakini yeye kama ilivyoelezwa hapo nyuma, aliwaozesha mabanati zake na kulipa kwa wake zake mahari zaidi ya hizo, na hii ni kwa mujibu wa uwezo wake yeye na wale waliowaoa mabanati zake.
3- Ikiwa mtu ni tajiri mwenye uwezo, basi anaweza kutoa mahari nyingi awezayo kwa mkewe.
"فَقَدْ زَوَّجَ النَّجَاشِيُّ أُمَّ حَبِيْبَةَ لِرَسُوْلِ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَأَمْهَرَهَا عَنهُ أَرْبَعَة آلَاف وَبَعَثَ بِهَا إِلَى رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ مَعَ شُرَحْبِيل بن حَسَنَة"
“Negus (An-Najaashiy, Mfalme wa Uhabeshi) alimwozesha Ummu Habiybah kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akamlipia mahari ya dirhamu elfu nne [mahari za wakeze Rasuli zilikuwa ni dirhamu mia nne tu], kisha akampeleka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiandamana na Shurahbiyl bin Hasanah”. [Hadiyth Swahiyh. Abu Daawuwd (2107), Ahmad (6/427) na An-Nasaaiy (6/119)]
Toka kwa Ash-Sha’abiy amesema: “ ‘Umar bin Al-Khattwaab aliwahutubia watu. Akaanza kwa kumhimidi Allaah na kumsifu, kisha akasema: Zindukeni! Msipandishe juu mahari za wanawake, kwani hainifikii mimi habari kuhusu yeyote aliyetoza mahari zaidi ya mahari aliyotoza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au aliyoletewa, isipokuwa ninaichukua ziada na kuiingiza kwenye Baytul Maal. Kisha akateremka, lakini hapo hapo mwanamke mmoja wa Kiquraysh alimpinga na kumwambia: Ee Amiri wa Waumini! Je, Kitabu cha Allaah ‘Azza wa Jalla kina haki zaidi kufuatwa au maneno yako? Akasema: Bali ni Kitabu cha Allaah ‘Azza wa Jalla. Kwani kuna shida gani? Akamwambia: Wewe sasa hivi umewakataza watu kupandisha juu sana mahari ya wanawake nailhali Allaah ‘Azza wa Jalla Amesema katika Kitabu Chake:
"وَآتَيْتُمْ إِحْدَاهُنَّ قِنطَارًا فَلَا تَأْخُذُوا مِنْهُ شَيْئًا"
“Na mmempa mmoja wao mirundi ya mali, basi msichukue humo chochote”, ‘Umar akamwambia: Kila mmoja ni mjuzi zaidi kuliko ‘Umar -mara mbili au tatu- Kisha akapanda tena mimbari na kuwaambia watu: Hakika nilikuwa nimewakataza kupandisha sana mahari ya wanawake. Basi na afanye mtu katika mali yake analoliona sawa”. [Sunan Sa’iyd bin Mansuwr (598), na toka kwake Al-Bayhaqiy (7/233). Ni Hadiyth Hasan Lighayrihi, na ina Hadiyth wenza kama ilivyobainishwa kwenye Kitabu cha Jaami’u Ahkaamin Nisaa (3/301)].
Kiufupi: Ni kwamba watu wanatofautiana katika utajiri na umasikini. Hivyo basi ni lazima kuchunga hali ya mwoaji. Asitakwe asichokuwa na uwezo nacho hadi kulazimika kwenda kukopa na mfano wa hivyo. Lakini kama ana uwezo, basi si vibaya akizidisha, isipokuwa tu hilo lisikutanishwe na niya ya kujifaharisha na mfano wa hivyo, hapo itakuwa ni jambo baya.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
04: Mahari Ni Haki Ya Mwanamke Na Si Mawalii Wake:
Ni kwa Neno Lake Ta’aalaa:
"وَآتُوا النِّسَاءَ صَدُقَاتِهِنَّ نِحْلَةً"
“Na wapeni wanawake mahari zao kwa maridhawa.” [An-Nisaa: 04]
Na Kauli Yake:
"فَمَا اسْتَمْتَعْتُم بِهِ مِنْهُنَّ فَآتُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ فَرِيضَةً"
“Basi mliostarehe nao, wapeni mahari yao kuwa ni waajib”. [An-Nisaa: 24]
Pamoja na Aayaat nyinginezo zinazoonyesha kwamba mahari ni haki ya mwanamke. Hivyo si halali kwa baba yake wala mwingine yeyote kuchukua chochote katika mahari yake bila idhini yake. Na kwa ajili hiyo, Mashaafi’iy na Mahanbali wanasema kwamba haijuzu kwa mume kulipa mahari kwa asiye mke au mwakilishi wake au yeyote aliyeidhinisha apokee.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
05: Aina Za Mahari: (a) Mahari Yaliyobainishwa:
Kwa kuzingatia makubaliano kuhusu thamani yake, mahari yanagawanyika katika yaliyobainishwa na yasiyobainishwa.
Ama kwa kuzingatia muda wa kulipwa kwake, yanagawanyika katika yanayolipwa kwa wakati na yanayolipwa baadaye.
Ama kwa kuzingatia kiasi ambacho mwanamke anastahiki kulipwa, yanagawanyika katika mahari kamili, nusu mahari na kiliwazo.
Mahari Yaliyobainishwa:
1- Inapendeza kwa wafungao ndoa kupanga mahari, kuyabainisha na kuyaainisha ili kuepusha mizozo na migogoro. Baada ya kupatana, mahari iliyokubaliwa inakuwa juu ya dhima ya mume ambaye ni lazima ailipe.
2- Inajuzu kufunga ‘aqdi bila kutaja mahari kama linavyoashiria Neno Lake Ta’aala:
"لَّا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِنْ طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ مَا لَمْ تَمَسُّوهُنَّ أَوْ تَفْرِضُوا لَهُنَّ فَرِيضَةً"
“Hakuna dhambi kwenu mkiwataliki wanawake ambao hamkuwagusa au kuwabainishia mahari yao”. [Al-Baqarah: 236]
Hii inaitwa “Nikaahut-Tafwiydh”, nayo inajuzu kwa ‘Ijmaa ya ‘Ulamaa. Katika hali hii, mwanamke ni lazima apewe mahari ya mfano wake. Mahari ya mfano wake ni kiasi ambacho wanawake mfano wake katika jamaa zake toka upande wa baba yake kama madada na mashangazi wamelipwa, lakini si kutoka upande wa mama yake. Kwa kuwa mama anaweza kutoka kwenye familia ambayo desturi zake zinapishana na desturi za familia ya baba yake. Na kama hawatapatikana mfano wake toka kwa baba yake, basi ni wanawake wa mfano wake katika mji wake.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
06: Aina Za Mahari: (b) Mahari Inayolipwa Kwa Wakati Bila Kucheleweshwa:
Kiasili, mahari hukabidhiwa mara moja kwa mwanamke kabla ya mumewe kumuingilia, na mwanamke huyu ana haki ya kukataa kuingiliwa na mumewe mpaka apokee mahari yake. Allaah Ta’aalaa Amesema:
"وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ أَنْ تَنكِحُوهُنَّ إِذَا آتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ" ۚ
“Na wala si dhambi kufunga nao nikaah mkiwapa mahari yao”. [Al-Mumtahinah: 10]
Imepokelewa toka kwa ‘Aliy (Radhwiya Allaah ‘anhu) akisema:
تزوَّجْتُ فَاطِمَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهَا، فَقُلْتُ: يَا رَسُوْلَ اللهِ، ابْنِ بي، قَالَ: أَعْطِهَا شَيْئًا، قُلْتُ: مَا عِنْدِيْ مِنْ شَيْءٍ، قَالَ: فَأَيْنَ دِرْعُكَ الحُطَمِيَّةُ؟ قُلْتُ: هِيَ عِنْدِي، قَالَ: فَأَعْطِهَا إيَّاهُ"
“Nilimwoa Faatwimah (Radhwiya Allaah ‘anhaa). Kisha nikamwambia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Naomba niruhusu nimuingilie. Akaniambia: Mpe chochote. Nikasema: Sina kitu. Akaniambia: Liko wapi deraya lako la kihutwamiyya? Nikamwambia: Ninalo. Akaniambia: Basi mpe (hilo hilo)”. [Hasan Swahiyh. Swahiyh An-Nasaaiy (3375)]
Na hili limekwishafanywa na watangu wema.
Lakini pamoja na hivyo, inajuzu kuchelewesha mahari au sehemu yake, au hata kuilipa kidogo kidogo kama hali ya mume hairuhusu au kuwepo sababu nyingine yeyote lakini kwa sharti mume na mke wakubaliane kucheleweshwa huko baada ya mke kuingiliwa na mumewe. Kwa kuwa mahari ni deni kama yalivyo madeni mengineyo, hivyo basi inajuzu kulipwa baadaye ingawa inapendeza zaidi ikilipwa haraka.
Lakini Je, Ni Sharti Kuainishwa Muda Wa Kulipa Ikiwa Mahari Yatacheleshwa?
1- Ikiwa yatacheleweshwa muda usiojulikana, kama mume kusema: “Nimekuoa kwa mahari ya milioni moja kwa sharti niwe na uwezo wa kuyalipa, au nitayalipa wakati wa kuvuma upepo, au kuwasili fulani na mfano wa hayo”, basi haitofaa kucheleweshwa.
2- Mahari yakicheleweshwa yote au baadhi yake bila kutajwa au kuainishwa muda wa kulipwa, hapa kuna mvutano baina ya Fuqahaa:
(a) Mahanafiy na Mahanbali wamesema: Uhalali wa mahari utabakia pale pale kwa mwanamke na haki ya kupewa pia itabaki atakapotalikiwa au mumewe akifariki kama ilivyo ada na desturi kwenye nchi za Kiislamu!!
(b) Mashaafi’iy wamesema: Uhalali wa mahari unakuwa haupo tena, na badala yake atapewa mahari ya mfano.
(c) Wamaalik wamesema: Ikiwa muda wa kulipwa haujulikani, kama kucheleweshwa hadi mume kufa au kuachana, basi ‘aqdi itakuwa ni lazima ivunjwe isipokuwa kama mume atamuingilia mke, hapo italazimu mahari ya mfano.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
07: Mahari Anayostahiki Mwanamke Na Hali Zake: Hali Zinazolazimu Apewe Mahari Kamili (a) Akiingiliwa Na Mume Jimai Halisia:
‘Ulamaa wamekubaliana wote kwamba mwanamke anastahiki kupewa mahari kamili kama mume atamuingilia kutokana na Neno Lake Ta’alaa:
"وَإِنْ أَرَدتُّمُ اسْتِبْدَالَ زَوْجٍ مَّكَانَ زَوْجٍ وَآتَيْتُمْ إِحْدَاهُنَّ قِنطَارًا فَلَا تَأْخُذُوا مِنْهُ شَيْئًا ۚ أَتَأْخُذُونَهُ بُهْتَانًا وَإِثْمًا مُّبِينًا ● وَكَيْفَ تَأْخُذُونَهُ وَقَدْ أَفْضَىٰ بَعْضُكُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ وَأَخَذْنَ مِنكُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا"
“Na mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke, na mmempa mmoja wao mirundi ya mali, basi msichukue humo chochote. Je, mnaichukua kwa dhulma na dhambi iliyo bayana? • Na mtachukuaje na hali nyinyi kwa nyinyi mmeingiliana (kimwili na kustarehe), na wao wanawake wamechukua toka kwenu fungamano thabiti?”. [An-Nisaa: 20-21]
Hapa Allaah Ta’aalaa Amemkataza mume kuchukua chochote katika mahari aliyompa mkewe kama atamtaliki, na Amekuzingatia kuchukua huko kama ni dhulma na dhambi bayana kabisa. Na hii ni kwa vile mahari hayo yalikuwa kwa mkabala wa kumuingilia, na mume ashajishibisha haki yake ya kujimai. Hivyo ni haki ya mwanamke kuchukua mahari yote.
Na pia kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"أَيُّمَا امْرَأَةٍ نَكَحَتْ بِغَيْرِ إِذْنِ وَلَيِّهَا فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ فَنِكَاحُهَا بَاطِلٌ، فَإِنْ دَخَلَ بِهَا فَلَهَا الْمَهْرُ بِمَا اسْتَحَلَّ مِنْ فَرْجِهَا"
“Mwanamke yeyote atakayeolewa bila ya idhini ya walii wake, basi ndoa yake ni batili, ndoa yake ni batili, ndoa yake ni batili. Na ikiwa mume atamuingilia, basi mahari ni haki yake kwa uhalali alioupata wa kustarehe na utupu wake”. [Hadiyth Swahiyh. Imetajwa nyuma]
Ikiwa mahari kamili ni wajibu kuyalipa kwa kumuingilia mwanamke katika ndoa iliyo batili, basi ulazima wa kuyalipa katika ndoa sahihi ni mkubwa zaidi.
Faida:
Mwanamke ni lazima apewe mahari yake yote kwa kuingiliwa hata kama kwa mtindo ulio haramu kama kumuingilia kinyume na maumbile, au katika hali ya hedhi, au nifasi, au akiwa amehirimia, au amefunga swawm, au yuko kwenye itikafu na mfano wa hayo.
Ikiwa Ndoa Ni Sahihi Na Mmoja Wa Wanandoa Akafariki Kabla Ya Kufanyika Tendo La Jimai Kati Yao, Nini Kifanyike?:
Hapa kuna hali mbili:
Hali ya kwanza:
Ikiwa mahari imebainishwa katika ‘aqdi na mmoja wa wanandoa akafariki kabla ya tendo la jimai, basi mwanamke atastahiki mahari kamili kwa mujibu wa itifaki ya ‘Ulamaa. ‘Ijmaa ya Maswahaba (Radhwiya Allaah ‘anhum) pia iko kwenye rai hii. Hii ni kwa sababu ‘aqdi haivunjiki kwa kifo, bali inamalizika kwa kifo hicho ambacho ndio umri wa mtu, na hukumu zake zinabakia pale pale kwa kumalizika kwake yakiwemo mahari.
Hali ya pili:
Ikiwa mahari haikubainishwa katika ‘aqdi (Nikaahu Tafwiydh), na mmoja wa wanandoa akafariki, ‘Ulamaa kwa hili wamekhitilafiana katika kauli mbili:
Kauli ya kwanza: Mwanamke anastahiki mahari ya mfano. Ni madhehebu ya Mahanafiy na Mahanbali, na ni kauli ya Ash-Shaafi’iy. Na hoja zao ni hizi zifuatazo:
1- Hadiyth ya ‘Alqamah aliyesema:
"أُتِيَ عَبْدُ الله بنُ مَسْعُوْدٍ فِي امْرَأَةٍ تَزَوَّجّهَا رَجُلٌ ثُمَّ مَاتَ عَنْهَا، وَلَمْ يَفْرِضْ لَهَا صَدَاقًا وَلَمْ يَكُنْ دَخَلَ بِهَا، فَاخْتَلَفُوْا إليْهِ فَقَالَ: أَرَى لَهَا مِثْلَ صَدَاقِ نِسَائِهَا، وَلَهَا المِيْرَاثُ وَعَلَيْهَا العِدَّةُ، فَشَهِدَ مَعْقِلُ بنُ سِنَانِ الأَشْجَعِيُّ: أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم قَضَى فِي بَرْوَعَ ابنةِ وَاشِقٍ بِمِثْلِ مَا قَضَى"
“Abdullaah bin Mas-‘uwd aliendewa mara kadhaa na watu wakimuuliza kuhusiana na hukmu ya mwanamke aliyeolewa na mwanamume, kisha mume akafariki na hakuwa amemtajia mahari yake wala kuwahi kumuingilia. Akawaambia: Naona anastahiki apewe mahari mfano wa wanawake wenzake, pia ana haki ya mirathi, na lazima akae eda. Mi-‘qal bin Sinaan Al-Ashja’iyy akalitolea hilo ushahidi akisema: Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alihukumu kwa Bar-wa’a bint Waashiq sawa na alivyohukumu”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2114), At-Tirmidhiy (1145), An-Nasaaiy (6/121), Ibn Maajah (1891) na Ahmad (3/480)]
2- Ndoa ni mkataba, na muda wa kudumu kwake ni umri. Na kwa kufa mmoja wao, mkataba unaisha lakini malipo yake yanabaki pale pale.
Kauli ya pili: Hapewi chochote. Ni madhehebu ya Maalik na kauli nyingine ya Ash-Shaafi’iy.
Faragha Inayokubalika Kisharia Kwamba Ni Faragha Kati Ya Mke Na Mume Hata Bila Ya Jimai:
Kidhibiti cha faragha sahihi inayozingatiwa, ni kukutana mke na mume baada ya ‘aqdi sahihi mahala asipoweza mtu yeyote kuwaingilia na ambapo wanaweza kustarehe kwa raha zao na kujifaragua watakavyo.
Faragha hii ikifanyika baada ya ‘aqdi, ‘Ulamaa wamekhitalifiana kuhusiana na kiasi cha mahari anachostahiki mwanamke kama mume atamtaliki katika kauli mbili:
Ya kwanza: Anastahiki kupewa mahari kamili hata kama jimai haikufanyika. Ni madhehebu ya Abu Haniyfah na Ash-Shaafi’iy (msimamo wa kale). Ni madhehebu mashuhuri pia ya Ahmad, Is-Haaq na Al-Awzaaiy. Kadhalika, ni kauli iliyohadithiwa toka kwa Makhalifa Wanne Waongofu pamoja na Ibn ‘Umar na Zayd bin Thaabit. Hoja ya kauli hii ni:
1- Toka kwa Zuraaratu bin Awfaa, amesema:
"قَضَى الْخُلَفَاءُ الرَّاشِدُونَ الْمَهْدِيُّونَ أَنَّ مَنْ أَغْلَقَ بَابًا أَوْ أَرْخَى سِتْرًا فَقَدْ وَجَبَ الصَّدَاقُ وَالْعِدَّةُ"
“Makhalifa Werevu Waongofu wamehukumu kwamba mwenye kufunga mlango, au akateremsha pazia, basi mahari na eda zimelazimu”. [Isnaad yake imekatika. Imechakatwa na Al-Bayhaqiy (7/255) na Ibn Hazm]
2- Toka kwa Sa’iyd bin Al-Musayyib kwamba ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaah ‘anhu):
"قَضَى فِي الْمَرْأَةِ إذَا تَزَوَّجَهَا الرَّجُلُ، أَنَّهُ إِذَا أُرْخِيَتِ السُّتُوْرُ، فَقَدْ وَجَبَ الصَّدَاقُ وَالعِدَّةُ".
“Alihukumu kuhusu mwanamke kwamba akiolewa na mtu, na mtu huyo akateremsha pazia, basi mahari imelazimu”. [Isnaad yake ni swahiyh. Imechakatwa na Maalik katika Al-Muwattwa (2/528) na Al-Bayhaqiy (7/255)]
3- Toka kwa ‘Aliy amesema:
"إِذَا أُرْخِيَتِ السُّتُوْرُ، فَقَدْ وَجَبَ الصَّدَاقُ"
“Pazia zikiteremshwa, basi mahari ni wajibu”. [Isnaad yake ni swahiyh. Imechakatwa na Sa’iyd bin Manswuwr (1/201) na Al-Bayhaqiy (7/255)]
4- Neno Lake Ta’aalaa:
"وَكَيْفَ تَأْخُذُونَهُ وَقَدْ أَفْضَىٰ بَعْضُكُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ"
“Na mtachukuaje na hali nyinyi kwa nyinyi mmeingiliana (kimwili na kustarehe)?”. [An-Nisaa: 21]
Wamesema "الإفْضَاءُ" ni "الخلْوَة" yaani faragha, kwa kuwa "الإفْضَاءُ" inatokana na neno "الفَضَاءُ" lenye maana ya "الخَلَاءُ" yaani sehemu tupu, kana kwamba Allaah Amesema: “Na hali nyinyi kwa nyinyi mmekaa faraghani bila mwingine”.
5- Wamelichukulia neno kugusa katika Neno Lake Ta’aalaa:
"وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ"
“Na mkiwataliki kabla ya kuwagusa na mkawa mmeshawabainishia mahari yao, basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha”. [Al-Baqarah: 237]
6- Kwa kuwa matokeo ya faragha kwa asilimia kubwa ni kuchezeana na kujimaiana. Na mume akiwa faragha na mkewe (na hasa baada ya ndoa), utashi wa nguvu unachemka wa kufanyika hilo.
Kauli ya pili: Hastahiki mahari kamili isipokuwa kwa kuingiliwa tu. Ni madhehebu ya Maalik, Ash-Shaafi’iy na riwaayah nyingine toka kwa Ahmad na Ibn Hazm. Pia imesimuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas na Ibn Mas-‘uwd (Radhwiya Allaah ‘anhumaa). Hoja zao ni:
1- Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ"
“Na mkiwataliki kabla ya kuwagusa na mkawa mmeshawabainishia mahari yao, basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha”. [Al-Baqarah: 237]
Wamesema kwamba makusudio ya kugusa katika aayah ni jimai.
2- Wamefasiri "الإفْضَاءُ" katika Neno Lake Ta’alaa:
"وَكَيْفَ تَأْخُذُونَهُ وَقَدْ أَفْضَىٰ بَعْضُكُمْ إِلَىٰ بَعْضٍ"
“Na mtachukuaje na hali nyinyi kwa nyinyi mmeingiliana (kimwili na kustarehe)?”… kwa maana ya kujimai.
3- Imeripotiwa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba alikuwa anasema kuhusu mwanamume ambaye amekabidhiwa mkewe kisha akamtaliki, halafu akadai kwamba hajamgusa:
"عَلَيْهِ نِصْفُ الصًّدَاقِ"
“Ni lazima alipe nusu mahari”. [Isnaad yake ni dhwa’iyf. Imechakatwa na Sa’iyd bin Mansuwr (772)]
4- Toka kwa Ibn Mas-‘uwd, amesema:
"لَهَا نِصْفُ الصَّدَاقِ، وَإِنْ جَلَسَ بَيْنَ رِجْلَيْهَا"
“Ni haki yake nusu mahari, hata kama mume atakaa kati ya miguu miwili ya mkewe”. [Isnaad yake imekatika. Ibn Hazm (9/484)]
Ninasema: “Lau riwaayah hizi zilizonukuliwa toka kwa Ibn ‘Abbaas na Ibn Mas-‘uwd (ambazo moja Isnaad yake ni dhwa’iyf na nyingine imekatika) zingethibiti, basi zingekabilishwa na riwaayah zilizothibiti kunukuliwa toka kwa ‘Umar na ‘Aliy (ambazo zote Isnaad zake ni swahiyh), na mpingaji asingelikuwa na hoja yoyote, bali mvutano ungelibakia katika kuawilisha maana ya kugusa "المَسُّ" na kuingiliana "الإِفْضَاءُ" katika aayah mbili tukufu (237 Al-Baqarah na 21 An-Nisaa). Na kwa mujibu wa ninavyojua, hakuna riwaayah kama hizo zilizopokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas au Ibn Mas-‘uwd. Kauli za ‘Umar na ‘Aliy na Maswahaba wengineo ndizo ninazozikubali. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.
Lakini mtu anaweza kujiuliza aseme: Imekubalika kwamba mume atalipa mahari kamili kwa kukaa faragha na mkewe, kwa kuwa faragha ni chachu ya kumuingilia. Na lau itathibiti kwamba mke hajaingiliwa kwa kukiri yeye mwenyewe, au ikathibiti kwa njia ya vipimo vya kisasa, je, hapo atapewa nusu mahari? Jibu la hili litafitiwe na ‘Ulamaa na wajitahidi kulipembua kupata jawabu mwafaka.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
08: Mahari Anayostahiki Mwanamke Na Hali Zake: Hali Zinazolazimu Apewe Mahari Kamili (b) Mke Akikaa Mwaka Mzima Kwenye Nyumba Ya Mumewe Hata Bila Ya Kuingiliwa:
Kwa mujibu wa kauli ya Wamaalik, ikiwa mtu ameoa mke, na mke akapelekwa kwake, halafu akakaa kwake mwaka mzima bila kumuingilia, basi ni lazima atoe mahari kamili kwa mujibu wa Wamaalik.
Ninasema: “Sioni dalili yoyote kuhusiana na wao kuainisha kipindi cha mwaka mmoja. Lau mwanamke atapelekwa kwa mumewe, na akakaa bila kumuingilia, hili litarejeshwa kwenye hali iliyotangulia kuelezwa (faragha sahihi inayozingatiwa). Yaliyoelezwa huko ndiyo yatakayosemwa kuhusiana na hili”.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
09: Mahari Anayostahiki Mwanamke Na Hali Zake: Hali Zinazolazimu Apewe Mahari Kamili (c) Talaka Ya Kukimbia (Mke Asirithi) Katika Maradhi Ya Umauti Kabla Ya Kumuingilia:
Kwa mujibu wa Mahanbali, ikiwa mume atamtaliki mkewe ambaye hakuwahi kumuingilia katika ugonjwa ambao hatima yake kwa asilimia kubwa ni umauti ili mke asiambulie mirathi, na mume akafariki kweli, basi ni lazima apewe mahari kamili (kwa mujibu wa Mahanbali), kwa sababu ni lazima mke akae eda katika hali hii madhali hajaolewa au kuritadi.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
10: Mahari Anayostahiki Mwanamke Na Hali Zake: Hali Inayolazimu Apewe Mahari Nusu: Ni Kutalikiwa Mwanamke Kabla Hajaingiliwa, Na Mahari Ikawa Imebainishwa Kwenye ‘Aqdi:
Mwanaume akimtaliki mkewe kabla hajamuingilia (na pia kabla hajakaa naye faraghani) na mahari ikawa ilibainishwa kwenye ‘aqdi, basi mwanamke atastahiki nusu ya mahari kwa itifaki ya ‘Ulamaa. Na hii ni kwa Neno Lake Ta’alaa:
"وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ"
“Na mkiwataliki kabla ya kuwagusa na mkawa mmeshawabainishia mahari yao, basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha”. [Al-Baqarah: 237]
Kadhalika, hali inakuwa hivi hivi, pakitokea mtengano bila talaka (ikiwa ni kutoka upande wa mume) kama mume kufanya "إِيْلَاءُ" (Iylaau) au "لِعَانُ" (Li’aan), au mume kuritadi, au akakataa kusilimu baada ya mkewe kusilimu na mfano wa hayo. Haya ni madhehebu ya Mashaafi’iy na Mahanbali.
"إِيْلَاءُ"] (Iylaau), ni mume kumwapia mkewe kwa Allaah kwamba hatomjimai kwa zaidi ya miezi minne kwa lengo la kumdhuru. Ama "لِعَانُ" (Li’aan), ni mume kumtuhumu mkewe kufanya zinaa bila kuwa na mashahidi, na badala yake ataapa viapo vinne kwamba yeye ni mkweli kwa madai yake dhidi ya mkewe, na kiapo cha tano atajiapiza kwamba laana ya Allaah imshukie kama ni mwongo. Mke kama anakanusha tuhuma, na yeye pia ataapa viapo vinne kwamba anasingiziwa, na kwamba yeye ni mkweli kwa anayoyasema, na kiapo cha tano atajiapiza ghadhabu za Allaah zimshukie kama madai ya mume wake ni ya kweli]
Kama mahari ilikuwa haijabainishwa, na mume akamtaliki kabla hajamuingilia (au kukaa naye faragha), katika hili, ‘Ulamaa wamekhitilafiana katika kauli tatu kuhusu kiasi cha mahari anachostahiki mwanamke:
Ya kwanza:
Hapewi kitoka nyumba (kiliwazo). Ni madhehebu ya Abu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Is-haaq, Ath-Thawriy, Abu ‘Ubayd na wengineo. Hoja zao ni:
1- Neno Lake Ta’aalaa:
"لَّا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ مَا لَمْ تَمَسُّوهُنَّ أَوْ تَفْرِضُوا لَهُنَّ فَرِيضَةً ۚ وَمَتِّعُوهُنَّ عَلَى الْمُوسِعِ قَدَرُهُ وَعَلَى الْمُقْتِرِ قَدَرُهُ مَتَاعًا بِالْمَعْرُوفِ ۖ حَقًّا عَلَى الْمُحْسِنِينَ"
“Hakuna dhambi kwenu mkiwataliki wanawake ambao hamkuwagusa au kuwabainishia mahari yao. Wapeni kiliwazo, kwa mwenye wasaa kadiri ya uwezo wake na mwenye dhiki kadiri ya uwezo wake. Maliwaza kwa mujibu wa ada, ni haki kwa wafanya ihsaan”. [Al-Baqarah: 236]
2- Kauli Yake Ta’alaa:
"وَلِلْمُطَلَّقَاتِ مَتَاعٌ بِالْمَعْرُوفِ ۖ حَقًّا عَلَى الْمُتَّقِينَ"
“Na wanawake waliotalikiwa wapewe kiliwazo (kitoka nyumba) kwa mujibu wa shariy’ah, ni haki juu ya wenye taqwa”. [Al-Baqarah: 241]
3- Kauli Yake Ta’alaa:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ فَمَا لَكُمْ عَلَيْهِنَّ مِنْ عِدَّةٍ تَعْتَدُّونَهَا ۖ فَمَتِّعُوهُنَّ وَسَرِّحُوهُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا"
“Enyi walioamini! Mnapofunga nikaah na Waumini wa kike, kisha mkawataliki kabla ya kujimai nao, basi hamna juu yao eda yoyote mtakayohesabu. Basi wapeni kitoka nyumba na waacheni huru, kwa mwachano mzuri”. [Al-Ahzaab: 49]
Kauli ya pili:
Hapewi chochote, lakini inapendeza kama atapewa kiliwazo. Ni madhehebu ya Maalik na Al-Layth. Dalili yao ni Neno Lake Ta’aalaa:
"مَتَاعًا بِالْمَعْرُوفِ ۖ حَقًّا عَلَى الْمُحْسِنِينَ"
“Maliwaza kwa mujibu wa ada, ni haki kwa wafanya ihsaan”. [Al-Baqarah: 236]
Wanasema kwamba aayah hapa inaonyesha kwamba kiliwazo ni kwa njia ya ihsaan na kufanya wema tu, lakini si wajibu. Na kama ni wajibu, basi hilo lisingehusishwa na wafanya ihsaan.
Hoja yao imejibiwa kwamba kutenda wajibu ni katika ihsaan.
Kauli ya tatu:
Anastahiki kupewa mahari ya mfano. Ni madhehebu ya Ahmad, na hoja yake anasema kwamba hiyo ni nikaah sahihi inayowajibisha mahari ya mfano wake baada ya kumuingilia, hivyo inawajibisha nusu ya mahari kwa kumtaliki kabla ya kumuingilia.
Ninasema: “Kauli sahihi ni ya kwanza kutokana na uwazi wa aayah tukufu zilizotolewa dalili. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”
Faida: Imeshakubalika na kupitishwa kwamba ikiwa mahari yamepangwa na kubainishwa kiasi chake katika ‘aqdi, kisha mume akamtaliki mkewe kabla ya kumuingilia, basi mke atapewa nusu. Lakini, endapo kama mahari hayakutajwa au kubainishwa katika ‘aqdi bali yakaja kupangwa baada yake kwa maridhiano au kwa hukumu, je, mwanamke atastahiki kupata nusu ya mahari yaliyobainishwa baada ya ‘aqdi au la?
‘Ulamaa wa Kihanafi wamesema: Mahari iliyopangwa baada ya ‘aqdi haikatwi tena nusu. Inayokatwa nusu ni ile iliyobainishwa wakati wa ‘aqdi kama ilivyobainishwa na Qur-aan Tukufu. Hapa mwanamke atapewa kiliwazo tu na si vinginevyo.
Lakini Jumhuwr ya ‘Ulamaa wana rai nyingine. Wanasema kwamba mahari iliyopangwa baada ya ‘aqdi inagawika nusu kama ile iliyotajwa wakati wa kufunga ‘aqdi. Na hili ni sahihi, kwa kuwa Neno Lake Ta’alaa:
"فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ"
“Basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha”, ni tamshi jumuishi kwa mahari yote katika ndoa sahihi, ni sawa mwenye kuoa akawa ameipanga katika ‘aqdi au baada ya ‘aqdi. Na Allaah ‘Azza wa Jalla Hakusema: Basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha kabla au wakati wa kufunga ‘aqdi”. Na kama Angelitaka hilo, basi Angelibainisha.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
11: Yanayopelekea Kudondoka Mahari Yote:
1- Kutokea utengano -kwa matakwa ya mke- kabla ya kumuingilia.
Ni kama mke kusilimu -na mumewe kubaki kafiri-, au mume kuvunja ndoa kutokana na kasoro aliyonayo mke, au mke kuritadi, au kugundulika kwamba mke aliwahi kumnyonyesha mume aliyemwoa, au mke kuvunja ndoa kutokana na kasoro aliyonayo mume, au mume kuwa masikini kupindukia na mfano wa hayo. Hapo mahari iliyobainishwa na mahari ya mfano itadondoka. Ni madhehebu ya Mashaafi’iy, Mahanbali, Mahanafiy na Wamaalik. Lakini wao hawajatofautisha kati ya kuwa mtengano unatokana na mume au mke.
2- Khulu’u (Mwanamke kudai talaka kwa kumlipa mume kitu au kumrejeshea mahari yake): Ikiwa mume atakubali kuachana na mkewe kwa kuachia mahari yake, hapo mahari yote itadondoka. Na kama mke bado hajapokea, basi mume hatotoa, na ikiwa amemkabidhi, basi mke atarejesha.
3- Kusamehe mahari yote kabla ya kuingiliwa au baada ya kuingiliwa.
Mwanamke akisamehe mahari yake iliyobainishwa, na mahari hiyo ilikuwa ni deni katika shingo ya mume, basi mahari hiyo hudondoka, lakini kwa sharti mke awe na vigezo vya kusamehe na kutoa anachomiliki.
4- Mwanamke kutunuku mahari yake yote kwa mume:
Madhali mke ana vigezo vya kutoa anachomiliki, na mume akakubali kutunukiwa mahari kwenye baraza ya kufunga ‘aqdi, ni sawa tunu hiyo ikawa kabla ya kukabidhi mahari au baada yake, basi mahari itadondoka.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
12: Kusamehe Mwanamke Mahari Au Yule Ambaye Fungamano La Ndoa Liko Mikononi Mwake:
Allaah Mtukufu Amesema:
"وَإِن طَلَّقْتُمُوهُنَّ مِن قَبْلِ أَن تَمَسُّوهُنَّ وَقَدْ فَرَضْتُمْ لَهُنَّ فَرِيضَةً فَنِصْفُ مَا فَرَضْتُمْ إِلَّا أَن يَعْفُونَ أَوْ يَعْفُوَ الَّذِي بِيَدِهِ عُقْدَةُ النِّكَاحِ ۚ وَأَن تَعْفُوا أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ۚ وَلَا تَنسَوُا الْفَضْلَ بَيْنَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ"
“Na mkiwataliki kabla ya kuwagusa na mkawa mmeshawabainishia mahari yao, basi (wapeni) nusu ya hayo mliyobainisha isipokuwa wakisamehe au asamehe yule ambaye fungamano la ndoa liko mikononi mwake. Na kusamehe kuko karibu zaidi na taqwa. Na wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Allaah Ni Mwenye Kuona yote myatendayo”. [Al-Baqarah: 237]
Maana ya aayah hii tukufu ni kwamba mwanamke akitalikiwa na mumewe kabla hajamuingilia, na mume akawa amembainishia kiasi cha mahari yake, naye akawa ameridhia kiasi hicho, basi ni haki yake apewe nusu ya mahari hiyo, isipokuwa kama mwenyewe atasamehe nusu hiyo na kumwachia mwanamume, au asamehe yule ambaye fungamano la ndoa liko mkononi mwake.
‘Ulamaa wamekhitilafiana katika kauli mbili kuhusu maana ya mtu ambaye fungamano la ndoa liko mkononi mwake.
Kauli ya kwanza:
Ni walii wa mwanamke. Walii anaweza kusamehe nusu ya mahari aliyostahiki mwanamke.
Kauli ya pili:
Ni mume mwenyewe. Hapa maana inakuwa: Au mume mwenyewe asamehe na akampa mwanamke mahari kamili.
Mwelekeo wa taawili hii ni imara zaidi. Kwa sababu mahari ni haki ya mwanamke kama ilivyoelezwa nyuma, haijuzu kwa yeyote kutia mkono wake kuigusa ila kwa idhini yake. Ni haki yake kabla ya talaka na baada ya talaka.
Basi yeyote kati ya wawili atakayesamehe haki yake, basi anakuwa karibu zaidi na taqwa, na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
13: Ikiwa Zitatajwa Mahari Mbili:
Ikiwa watu wa mke watamtaka mume ataje mahari mbili; moja kwa ajili ya ‘aqdi, na nyingine kwa ajili ya kutangazwa hadhirani kwa lengo la kujifaharishia kwa watu na si kwamba ndio inayomlazimu kutoa, hapa Jumhuwr ya ‘Ulamaa -kinyume na Mahanbali- wanasema kwamba atatoa iliyobainishwa kwenye ‘aqdi, na si ile iliyotangazwa mbele za watu. Ni chaguo pia la Sheikh wa Uislamu.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
14: Kinachotolewa Zaidi Ya Mahari "الحِبَاءُ"
"الحِبَاءُ", ni mtu kuchukua mahari ya binti yake kwa faida yake binafsi, ni sawa kwa kupewa, au kwa kumshurutisha mume kiasi fulani cha pesa nje ya mahari.
‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na hukmu ya hili katika kauli tatu:
Ya kwanza:
Inafaa kwa baba tu. Ni madhehebu ya Mahanafiy, Mahanbali na baadhi ya Mashaafi’iy. Hoja yao ni:
1- Kauli Yake Ta’aalaa:
"قَالَ إِنِّي أُرِيدُ أَنْ أُنكِحَكَ إِحْدَى ابْنَتَيَّ هَاتَيْنِ عَلَىٰ أَن تَأْجُرَنِي ثَمَانِيَ حِجَجٍ ۖ فَإِنْ أَتْمَمْتَ عَشْرًا فَمِنْ عِندِكَ ۖ وَمَا أُرِيدُ أَنْ أَشُقَّ عَلَيْكَ ۚ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ مِنَ الصَّالِحِينَ"
“Akasema: Mimi nataka nikuozeshe mmojawapo wa binti zangu hawa wawili kwa sharti kuwa unitumikie miaka minane, na ukitimiza kumi, basi ni uamuzi wako. Na wala sitaki kukutia mashakani, utanikuta In Shaa Allaah miongoni mwa Swalihina”. [Al-Qaswas: 27]
Wamesema: Mzee huyo aliyafanya mahari kuwa ni kumtumikisha Muwsaa amchungie wanyama wake.
2- Kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"أَنْتَ وَمَالُكَ لأَبِيكَ "
“Wewe na unavyomiliki, vyote ni mali ya baba yako”. [Sunan Ibn Maajah 2291]
Kauli ya pili:
Ikiwa hilo litashurutishwa wakati wa kufunga ndoa, basi ni haki ya mwanamke, na ikiwa ni baada, basi ni haki ya baba. Ni madhehebu ya Maalik, na ni kauli ya ‘Umar bin ‘Abdul Aziyz, Ath-Thawriy na Abu ‘Ubayd. Kwa sababu kushurutisha wakati huo inakuwa ni kama tuhuma ya kwamba mahari ni pungufu, lakini baada ya ‘aqdi tuhuma inakuwa mbali kabisa.
Wametoa dalili kwa Hadiyth ya ‘Amri bin Shu’ayb, toka kwa baba yake, toka kwa babu yake kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"أَيُّمَا اِمْرَأَةٍ نَكَحَتْ عَلَى صَدَاقٍ، أَوْ حِبَاءٍ، أَوْ عِدَةٍ قَبْلَ عِصْمَةِ اَلنِّكَاحِ فَهُوَ لَهَا، وَمَا كَانَ بَعْدَ عِصْمَةِ اَلنِّكَاحِ فَهُوَ لِمَنْ أُعْطِيَهُ، وَأَحَقُّ مَا أُكْرِمَ اَلرَّجُلُ عَلَيْهِ اِبْنَتُهُ أَوْ أُخْتُهُ "
“Mwanamke yeyote atakayeolewa kwa mahari, au zawadi, au kuahidiwa kitu kabla ya fungamano la ndoa, basi ni haki yake, na kinachokuja baada ya fungamano la ndoa, basi ni cha mwenye kupewa. Na cha haki zaidi anachokirimiwa kwacho mwanaume, ni binti yake au dada yake”. [Hadiyth Hasan. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2129), An-Nasaaiy (6/120), Ibn Maajah (1955) na Ahmad (2/182)]
Kauli ya tatu:
Haijuzu kabisa, inaharibu mahari, na mwanamke atapewa mahari mithili. Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy.
Ninasema: “Kauli yenye nguvu ni kwamba mwanamke atastahiki kile kilichotajwa kabla ya kufungwa ‘aqdi, ni sawa ikiwa ni mahari au zawadi, hata kama zawadi hiyo itakuwa imeainishiwa mtu mwingine kama baba yake na kadhalika. Ama kinachotajwa baada ya ‘aqdi, basi hicho ni kwa yule aliyeainishiwa, ni sawa akiwa walii wake au mtu mwingine, na hii ni kutokana na Hadiyth iliyotangulia. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
Alhidaaya.com [3]
15: Vyombo Vya Biharusi Ni Jukumu La Nani?:
Hivi ni vyombo ambavyo bi harusi hupelekwa navyo kwa mumewe kama fenicha, vyombo vya jikoni, matandiko na kadhalika.
Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanasema kwamba si wajibu kwa mwanamke kutumia mahari yake au pesa nyingine kununulia vyombo, bali hilo ni jukumu la mume. Mume ni lazima amtayarishie mkewe nyumba iliyokamilika kwa vyombo vyote vinavyohitajika kwa mujibu wa uwezo wake na mazingira yalivyo, ili nyumba iwe ni makazi ya kuwatuliza wote wawili. Allaah Ta’alaa Amesema:
"أَسْكِنُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ سَكَنتُم مِّن وُجْدِكُمْ"
“Wawekeni wanawake kwenye majumba mnayokaa nyinyi kwa kadiri ya kipato chenu”. [At-Twalaaq: 06]
Mahari iliyolipwa si kwa ajili ya kununulia vyombo, bali ni tunu kwa mwanamke kama Alivyosema Allaah Mtukufu:
"وَآتُوا النِّسَاءَ صَدُقَاتِهِنَّ نِحْلَةً"
“Na wapeni wanawake mahari zao kwa maridhawa.” [An-Nisaa: 04]
Kadhalika, mahari ni kwa mkabala wa kuhalalikiwa mume kustarehe na mkewe kama ilivyotangulia, na kitu kimoja hakikabiliwi na badali mbili. Na hii ni hata kama mume atalipa mahari mara mbili ya ile iliyobainishwa kwa matarajio ya mke kununulia vyombo vya thamani ya juu. Kama anataka hivyo, basi mahari iwe kando na pesa za vyombo ziwe kando. Akifanya hivyo, hapo itakuwa ni wajibu kwa mwanamke kununua vyombo kwa pesa hiyo.
Na ikiwa mwanamke atanunua vyombo vyake mwenyewe, au akanunuliwa na jamaa zake, basi vyombo vitabaki mali yake.
Faida:
Ikiwa mke au jamaa zake watanunua vyombo vyovyote kwa ridhaa yao bila kulazimishwa, basi hilo ni jambo jema. Toka kwa ‘Aliy, amesema:
"جَهَّزَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَاطِمَةَ فِي خَمِيلٍ وَقِرْبَةٍ وَوِسَادَةِ أَدَمٍ حَشْوُهَا لِيفُ الْإِذْخِرِ"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtayarishia Faatwimah mavazi ya mahameli, kiriba cha maji, na mto uliojazwa nyuzi za idhkhir”. [Hadiyth Hasan. Imechakatwa na An-Nasaaiy (6/135) na Ibn Maajah (4152)]
“Idhkhir” ni aina ya mmea wenye harufu nzuri.
Links
[1] https://www.alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/284
[2] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11959&title=10E-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20%D9%83%D8%AA%D8%A7%D8%A8%20%D8%A7%D9%84%D8%B2%D9%88%D8%A7%D8%AC%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20%D8%A7%D9%84%D8%B5%D9%91%D9%8E%D8%AF%D9%8E%D8%A7%D9%82%D9%8F%3A%20Mahari
[3] http://www.alhidaaya.com/
[4] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11960&title=01-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Taarifu%20Yake%20Na%20Hukmu%20Yake
[5] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11961&title=02-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Kinachofaa%20Kutolewa%20Kama%20Mahari
[6] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11962&title=03-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Kiwango%20%20Cha%20Juu%20Zaidi%20Na%20Cha%20Chini%20Zaidi%20Cha%20Mahari%20
[7] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11963&title=04-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Mahari%20Ni%20Haki%20Ya%20Mwanamke%20Na%20Si%20Mawalii%20Wake
[8] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11964&title=05-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Aina%20Za%20Mahari%3A%20%28a%29%20%20Mahari%20Yaliyobainishwa
[9] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11965&title=06-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Aina%20Za%20Mahari%3A%20%28b%29%20%20Mahari%20Inayolipwa%20Kwa%20Wakati%20Bila%20Kucheleweshwa
[10] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11966&title=07-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Mahari%20Anayostahiki%20Mwanamke%20Na%20Hali%20Zake%3A%20%20Hali%20Zinazolazimu%20Apewe%20Mahari%20Kamili%20%20%28a%29%20%20Akiingiliwa%20Na%20Mume%20Jimai%20Halisia
[11] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11967&title=08-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Mahari%20Anayostahiki%20Mwanamke%20Na%20Hali%20Zake%3A%20Hali%20Zinazolazimu%20Apewe%20Mahari%20Kamili%20%28b%29%20Mke%20Akikaa%20Mwaka%20Mzima%20Kwenye%20Nyumba%20Ya%20Mumewe%20Hata%20Bila%20Ya%20Kuingiliwa
[12] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11968&title=09-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Mahari%20Anayostahiki%20Mwanamke%20Na%20Hali%20Zake%3A%20%20Hali%20Zinazolazimu%20Apewe%20Mahari%20Kamili%20%20%28c%29%20%20Talaka%20Ya%20Kukimbia%20%28Mke%20Asirithi%29%20Katika%20Maradhi%20Ya%20Umauti%20Kabla%20Ya%20Kumuingilia
[13] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11969&title=10-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Mahari%20Anayostahiki%20Mwanamke%20Na%20Hali%20Zake%3A%20%20Hali%20Inayolazimu%20Apewe%20Mahari%20Nusu%3A%20%20Ni%20Kutalikiwa%20Mwanamke%20Kabla%20Hajaingiliwa%2C%20Na%20Mahari%20Ikawa%20Imebainishwa%20Kwenye%20%E2%80%98Aqdi
[14] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11970&title=11-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Yanayopelekea%20Kudondoka%20Mahari%20Yote
[15] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11971&title=12-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Kusamehe%20Mwanamke%20Mahari%20Au%20Yule%20Ambaye%20Fungamano%20La%20Ndoa%20Liko%20Mikononi%20Mwake
[16] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11972&title=13-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Ikiwa%20Zitatajwa%20Mahari%20Mbili
[17] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11973&title=14-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Kinachotolewa%20Zaidi%20Ya%20Mahari%20%22%D8%A7%D9%84%D8%AD%D9%90%D8%A8%D9%8E%D8%A7%D8%A1%D9%8F%22
[18] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11974&title=15-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Mahari%3A%20Vyombo%20Vya%20Biharusi%20Ni%20Jukumu%20La%20Nani%3F%3A