كتاب الزواج
Kitabu Cha Ndoa
وَلِيْمَةُ العُرْسِ
Walima Wa Harusi
Abu Maalik Kamaal Bin As-Sayyid Saalim
Imetarjumiwa na 'Abdullaah Mu'aawiyah (Abu Baasim)
Alhidaaya.com
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
وَلِيْمَةُ العُرْسِ
Walima Wa Harusi
Alhidaaya.com [3]
01: Maana Na Hukmu Yake:
Walima "الوَلْيْمَةُ" ni jina la chakula maalum cha harusi, nacho ni sunnah inayopendeza iliyokokotezwa. Hutayarishwa na mume kwa mujibu wa hali yake inavyoruhusu. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwafanyia walima wakeze na akawahimiza Maswahaba wake kufanya hivyo.
Toka kwa Anas:
"أَصْبَحَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِهَا عَرُوسًا، فَدَعَا الْقَوْمَ فَأَصَابُوا مِنَ الطَّعَامِ، ثُمَّ خَرَجُوا وَبَقِيَ رَهْطٌ مِنْهُمْ عِنْدَ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَأَطَالُوا الْمُكْثَ"
“Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipambaukiwa akiwa ameshamwoa (Zaynab bint Jahsh). Akawaalika watu wakala chakula, kisha wakatoka na wakabakia kundi dogo kati yao kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wakakaa sana”. [Al-Bukhaariy (1428), Muslim (5166), At-Tirmidhiy (3218) na An-Nasaaiy (6/136)]
‘Abdulrahmaan bin ‘Awf alipooa, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:
" أَوْلِمْ وَلَوْ بِشَاةٍ "
“Fanya walima japo kwa kondoo mmoja”. [Hadiyth iko kwa Al-Bukhaariy (5169). Angalia Fat-hul Baariy (9/237)]
Katika walima, si sharti kondoo au mnyama mwingine, bali chochote kwa mujibu wa uwezo wa mume. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitayarisha “Hays” alipomwoa Swafiyyah”. [Al-Bukhaariy (2048) na Muslim (1427)]
“Hays” ni tende zilizotolewa kokwa, zikachanganywa na samli au unga, na kuwa mlo.
Wakati Wake:
Je, ni wakati wa kufungwa ndoa, au baada yake, au wakati wa mume kukutana na mkewe, au baada yake?
Wakati mwafaka wa walima ni wakati wa mume kukutana na mkewe au baada yake, na si wakati wa kufungwa ndoa. Ni kutokana na Hadiyth iliyopita punde kuhusu ndoa ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwoa Zaynab bint Jahsh ambapo alifanya walima asubuhi baada ya kukutana na mkewe usiku.
Baadhi ya ‘Ulamaa wamesema kwamba wakati wake umeachiwa wazi kuanzia kufungwa ndoa hadi kumalizika kwa mujibu wa hali na mazingira.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
وَلِيْمَةُ العُرْسِ
Walima Wa Harusi
Alhidaaya.com [3]
02: Kualika Watu:
Inapendeza kwa mwenye kuoa awaalike watu wema, ni sawa wakiwa mafukara au matajiri kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"لاَ تُصَاحِبْ إِلاَّ مُؤْمِنًا وَلاَ يَأْكُلْ طَعَامَكَ إِلاَّ تَقِيٌّ"
“Usisuhubiane ila na Muumini tu, na asile chakula chako isipokuwa mchajimungu tu”. [Abu Daawuwd (4811) na At-Tirmidhiy (2506). Al-Albaaniy kasema ni Hasan]
Pia inapendeza zaidi akitenga sehemu maalum ya chakula hicho kwa ajili ya mafukara na masikini. Katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu), Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"شَرُّ الطَّعَامِ طَعَامُ الْوَلِيمَةِ يُدْعَى لَهَا الْأَغْنِيَاءُ وَيُتْرَكُ الْفُقَرَاءُ، وَمَنْ تَرَكَ الدَّعْوَةَ فَقَدْ عَصَى الله وَرَسُولَه"
“Chakula cha shari zaidi ni chakula cha walima. Hualikwa kuja kula matajiri na masikini wakaachwa. Na atakayesusa mwaliko, basi hakika amemuasi Allaah na Rasuli Wake”. [Al-Bukhaariy (5177) na Muslim (1432)]
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
وَلِيْمَةُ العُرْسِ
Walima Wa Harusi
Alhidaaya.com [3]
03: Kuitikia Mwaliko Wa Walima:
Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanasema kwamba kuitikia mwaliko wa walima ni lazima isipokuwa kwa udhuru. Wametoa dalili kwa haya yafuatayo:
(a) Hadiyth ya Ibn ‘Umar kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا دُعِيَ أَحَدُكُمْ إِلَى اَلْوَلِيمَةِ فَلْيَأْتِهَا"
“Akialikwa mmoja wenu walima, basi ahudhurie”. [Al-Bukhaariy (5173)]
(b) Hadiyth iliyotangulia ya Abu Hurayrah:
"وَمَنْ تَرَكَ الدَّعْوَةَ فَقَدْ عَصَى اللهَ وَرَسُولَهُ"
“Na atakayesusa mwaliko, basi hakika amemuasi Allaah na Rasuli Wake”. [Al-Bukhaariy (5177) na Muslim (1432)]
Mwanamke ni sawa na mwanaume katika hukmu hii, isipokuwa kama kutakuweko mchanganyiko wa wanawake na wanaume, au ufaragha wa haramu, hapo haitofaa kuhudhuria.
Ikiwa Mwalikwa Amefunga:
Ikiwa mtu amealikwa na yeye amefunga, ni sawa akiwa mwanamke au mwanaume, basi ni lazima aitikie mwaliko na ahudhurie mnasaba kutokana na Hadiyth zilizotangulia. Anapofika, atakuwa na chaguo kati ya mambo mawili: Ima atakula pamoja na waalikwa wengine -ikiwa swawm yake ni ya Sunnah na akataka kufungua- au atajizuia kula, na atamwombea du’aa mhusika wa walima. Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"إِذَا دُعِيَ أَحَدُكُمْ إِلَى طَعَامٍ فَلِيُجِبْ وَإِنْ شَاءَ طَعِمَ وَإِنْ شَاءَ تَرَكَ"
“Akialikwa mmoja wenu chakula basi aitikie mwaliko. Akitaka atakula, na akitaka ataacha kula”. [Muslim (1430) na Abu Daawuwd (3722)]
Na neno lake Rasuli:
"إِذَا دُعِيَ أَحَدُكُمْ إِلَى طَعَامٍ فَلْيُجِبْ فَإِنْ كَانَ صَائِمًا فَلْيُصَلِّ "
“Akialikwa mmoja wenu chakula, basi aitikie wito. Na kama amefunga, basi amwombee du’aa (mhusika)”. [Muslim (1431), Abu Daawuwd (3719) na Al-Bayhaqiy (7/263)]
Du’aa inakuwa ni katika zile zilizotajwa kwenye mlango wa adabu za chakula.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
وَلِيْمَةُ العُرْسِ
Walima Wa Harusi
Alhidaaya.com [3]
04: Nyudhuru Za Kutohudhuria Walima:
Tumesema kwamba kuhudhuria walima na kuitikia mwaliko kumefungamanishwa na kutokuwepo udhuru. Kati ya nyudhuru hizo ni:
1- Kuwepo munkari ndani ya walima wenyewe kama tembo, ulevi, muziki na kadhalika. Hali ikiwa hivi, basi haijuzu kuhudhuria ila kama atahudhuria kwa lengo la kukataza na kuwaasa wahusika kuacha munkari zilizopo. Dalili ya hili ni Hadiyth ya ‘Aliy ambaye amesema:
"صَنَعْتُ طَعَامًا فَدَعَوْتُ رَسُولَ اللهَ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَجَاءَ فَرَأَى في البَيْتِ تَصَاوِيْرَ فَرَجَعَ، فَقُلْتُ: يَا رَسُوْلَ الله، مَا أَرْجَعَكَ بِاَبِي أَنْتَ وَأُمِّي؟ قَالَ: إِنَّ في البَيْتِ سِتْرًا فِيهِ تَصَاوِيرُ، وَإِنَّ الْمَلاَئِكَةَ لاَ تَدْخُلُ بَيْتًا فِيهِ تَصَاوِيرُ"
“Nilitayarisha chakula nikamwalika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akaja, lakini aliona picha ndani ya nyumba akarudi. Nikamuuliza: Ee Rasuli wa Allaah! Kitu gani kimekurejesha, nakuapia kwa baba yangu na mama yangu. Akasema: Nyumbani kwako kuna picha, na hakika Malaika hawaingii nyumba yoyote ambayo ndanimwe kuna picha”. [Ibn Maajah (3359) na Abu Ya’alaa (436)]
2- Awe mwalikaji anawaalika matajiri tu bila masikini.
3- Awe mwalikaji hajali chanzo cha pato lake kuwa ni la haramu, au akawa anajishughulisha na kazi zenye utata.
Nyudhuru nyingine ni zile za kisharia kama udhuru unaomruhusu mtu kutokwenda kuswali Swalaah ya ijumaa kutokana na mvua nyingi, au matope, au kuhofia usalama wa mali, au kudhuriwa na adui na kadhalika.
Bi harusi Anaruhusiwa Kuwahudumia Wageni Wa Mumewe Siku Ya Harusi Yao:
Imepokelewa toka kwa Sahl bin Sa’ad (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba:
"دَعَا أَبُو أُسَيْدٍ السَّاعِدِيُّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِي عُرْسِهِ، وَكَانَتِ امْرَأَتُهُ يَوْمَئِذٍ خَادِمَهُمْ وَهِىَ الْعَرُوسُ، قَالَ سَهْلٌ: تَدْرُونَ مَا سَقَتْ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم؟ أَنْقَعَتْ لَهُ تَمَرَاتٍ مِنَ اللَّيْلِ، فَلَمَّا أَكَلَ سَقَتْهُ إِيَّاهُ"
“Abu Usayd As-Saa’idiy alimwalika Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika hafla ya harusi yake, na mkewe alikuwa ndiye anayewahudumia siku hiyo akiwa yungali bi harusi. Sahl akauliza: Mnajua ni kinywaji gani alimpa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam?). Alimloekea tende usiku, na baada ya kula, alimpa juisi anywe (ya tende hiyo iliyoloekwa)”. [Al-Bukhaariy: (5176), Muslim (2006) na Ibn Maajah (1912)]
Tunasema: Mahala pa kufanya hivi, ni kama mazingira yatakuwa mbali na fitna.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
وَلِيْمَةُ العُرْسِ
Walima Wa Harusi
Alhidaaya.com [3]
05: Pongezi Kwa Maharusi::
Katika mambo mazuri kabisa tuliyofundishwa na Uislamu, ni Muislamu kumpongeza nduguye Muislamu kwa kheri yoyote anayoipata, na kumwombea baraka, kudumu kwa neema na kuishukuru. Hivi ndivyo alivyokuwa akifanya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Alikuwa akimwombea aliyeoa baraka, umri mrefu na tawfiyq ya kudumu.
Maneno Ya Kupongeza:
"أنَّ النَّبيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ كانَ إذا رفَّأَ الإنْسَانَ إِذَا تزوَّجَ قالَ: بارَكَ اللَّهُ لَكَ، وبارَكَ علَيكَ، وَجَمعَ بَينَكُمَا فيْ خَيْرٍ"
“Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapompongeza mtu na kumwombea baada ya kuoa humwambia: Allaah Akubarikie, Akuteremshie barakah Zake, na Awatangamanishe kati yenu ndani ya kheri zote”. [Hadiyth Swahiyh. Swahiyh Abu Daawuwd (2130)]
Toka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa), amesema:
"تَزَوَّجَنِي النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَأَتَتْنِي أُمِّي فَأَدْخَلَتْنِي الدَّارَ، فَإِذَا نِسْوَةٌ مِنَ الأَنْصَارِ فِي الْبَيْتِ فَقُلْنَ عَلَى الْخَيْرِ وَالْبَرَكَةِ، وَعَلَى خَيْرِ طَائِرٍ"
“Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alinioa. Mama yangu akaja kunichukua akaniingiza nyumbani. Nikashtukizwa kuwakuta wanawake wa Kianswaar wako ndani wakinisubiri, na hapo hapo wakaniombea wakisema: Uingie kwa kheri na barakah, uingie na fali njema”. [Swahiyhul Bukhaariy (5156)]
Muislamu anatakiwa ashikamane na matamshi haya ya pongezi na aachane na mengineyo ambayo yanaweza kutoka nje ya mstari wa dini.
Kadhalika, mbali na maneno mazuri ya pongezi, inapendeza kuwapa maharusi zawadi. Na asili ya hili ni Hadiyth ya Anas aliyesema:
"لَمَّا تَزَوَّجَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ زَيْنَبَ أَهْدَتْ لَهُ أُمُّ سُلَيْمٍ حَيْسًا فِي تَوْرٍ مِنْ حِجَارَةٍ "
“Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwoa Zaynab, Ummu Sulaym alimzawadia “hays” kwenye bakuli la mawe.” [Muslim (1428)
“Hays” ni tende zilizotolewa kokwa, zikachanganywa na samli au unga.
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
وَلِيْمَةُ العُرْسِ
Walima Wa Harusi
Alhidaaya.com [3]
06: Adabu Za Usiku Wa Kukutana Mke Na Mume Baada Ya Kufunga Ndoa:
Hizi ni baadhi ya adabu ambazo inatakikana kwa maharusi kujipamba nazo usiku wa kwanza wa kukutana. Wakiingia nyumbani kwao inapendeza wafanye yafuatayo:
1- Mume amsalimie bi harusi wake. Kitendo hiki humwondoshea bi harusi hofu aliyonayo moyoni. Toka kwa Ummu Salamah kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwoa, alimtolea salamu alipotaka kumuingilia.
2- Mume amtulize bi harusi kwa kumpa kinywaji au chochote kitamu cha kula. Toka kwa Asmaa bint Yaziyd (Radhwiya Allaah ‘anhaa), amesema:
:"إِنِّيْ قَيَّنْتُ عَائِشَةَ لرَسُولِ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، ثُمَّ جِئْتُهُ فَدَعَوْتُهُ لِجَلْوَتِهَا، فَجَاءَ فَجَلَسَ إلى جَنْبِهَا، فَأَتَى بُعَسَّ فيْهِ لَبَنٌ، فَشَرِبَ ثُمَّ نَاوَلَهَا فَخَفَضَتْ رَأْسَهَا واسْتَحْيَتْ، قَالَت أَسْمَاءُ: فَانْتَهَرْتُهَا وَقُلْتُ لَهَا: خُذِيْ مِنْ يَدِ رَسُوْلِ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، فَأَخَذَتْ فَشَرِبَتْ شَيْئًا"
“Mimi nilimpamba ‘Aaishah kwa ajili ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kisha nikamwendea Rasuli nikamtaka aje amwangalie alivyopendeza. Akaja na kukaa pembeni yake, kisha akachukua gilasi ya maziwa, akanywa kisha akampa ‘Aaishah, na ‘Aaishah akainamisha kichwa chake kwa haya. Nikamtolea macho na kumwambia: Chukua gilasi hiyo, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anakupa. Akapokea, akanywa kidogo..” [Ahmad (6/453) na Sanad yake inaelekea kuhasinishwa]
3- Mume amwekee mkono kichwani bi harusi wake na amwombee:
Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
" إذا تزوَّجَ أحدُكمُ امرأةً أوِ اشْتَرَى خَادِمًا فَلِيَأْخُذْ بِنَاصِيَتِها، وَلِيُسَمِّ اللهَ عَزَّ وجَلَّ، وَلِيَدْعُ بِالبَرَكَةِ ولِيَقُلْ: اللَّهُمَّ إنِّي أَسْأَلُكَ مِنْ خَيْرِهَا َوَخَيْرِ مَا جَبَلْتَهَا عَلَيْهِ، وأَعُوْذُ بِكَ مِنْ شَرِّهَا وَشَرِّ مَا فِيْهَا وَشَرِّ مَا جَبَلْتَهَا عَلَيْهِ"
“Akioa mmoja wenu mwanamke au akanunua mtumwa (au kijakazi), basi akamate ncha ya utosi wake, alitaje Jina la Allaah ‘Azza wa Jalla, na kisha aombe barakah kwa kusema: Ee Allaah! Ninakuomba kheri zake, na kheri Ulizomuumba nazo, na najilinda Kwako na shari zake, na shari alizonazo, na shari Ulizomuumba nazo”. [Abu Daawuwd (2160), An-Nasaaiy (241-264) na Ibn Maajah (1918) kwa Sanad Hasan]
4- Apige mswaki kusafisha mdomo kabla ya kumuingilia:
Hili bila shaka liko wazi katika kunogesha tendo la jimai na mazungumzo yao kiujumla. Na hili pia kwa bi harusi bila shaka linatakiwa.
Imepokelewa toka kwa Shurayh bin Haani, amesema:
"سَأَلْتُ عائِشَةَ، قُلتُ: بأَيِّ شيءٍ كانَ يَبْدَأُ النبيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إذا دَخَلَ بَيْتَهُ؟ قالَتْ: بالسِّواك".
“Nilimuuliza ‘Aaishah: Ni jambo gani ambalo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaanza nalo anapoingia nyumbani kwake? Akasema: Ni mswaki”. [Hadiyth Swahiyh. Swahiyh Muslim (253)]
5- Kupiga “Basmalah” na kuomba du’aa wakati wa jimai:
Toka kwa Ibn ‘Abbaas, amesema: “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"أَمَا لو أنَّ أحَدَهُمْ يَقولُ حِينَ يَأْتي أهْلَهُ: باسْمِ اللَّهِ، اللَّهُمَّ جَنِّبْنِي الشَّيْطانَ، وجَنِّبِ الشَّيْطانَ ما رَزَقْتَنا، ثُمَّ قُدِّرَ بيْنَهُما في ذلكَ، أوْ قُضِيَ ولَدٌ، لَمْ يَضُرَّهُ شَيطانٌ أبَدًا"
“Naam. Lau mmoja wao atasema wakati anapoanza kumuingilia mkewe: “Bismil Laah. Ee Allaah! Niepushie shaytwaan, na mwepushie shaytwaan utakayeturuzuku”, kisha wakaandikiwa kupata mtoto kutokana na tendo hilo, basi shaytwaan hatomdhuru (mtoto) maisha yake yote”. [Al-Bukhaariy (5165) na Muslim (1434)]
6- Aswali pamoja naye rakaa mbili (hili limenukuliwa toka kwa Salaf).
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
وَلِيْمَةُ العُرْسِ
Walima Wa Harusi
Alhidaaya.com [3]
07: Adabu Na Ahkaam Za Jimai:
Ili kukamilisha faida kwenye suala hili, ingelikuwa ni vizuri kuelezea baadhi ya adabu za ahkaam za jimai ambayo ni mhimili mkuu katika maisha ya ndoa. Kati ya adabu na ahkaam zake ni:
1- Inapendeza sana mume aanze kumchezea chezea mkewe kabla ya jimai.
Ni kwa Hadiyth ya ‘Amri bin Diynaar, amesema: Nilimsikia Jaabir bin ‘Abdillaah akisema:
"قَالَ لِي رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: "هَلاَّ جَارِيَةً تُلاَعِبُهَا وَتُلاَعِبُكَ"
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia (baada ya kujua nimeoa mwanamke mkubwa): Kwa nini usioe msichana mdogo (bikra) ukamchezea chezea naye akakuchezea chezea”. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (5247) na Muslim (715)]
2- Mume anaruhusiwa kumuingilia kwa namna yoyote aipendayo kwa sharti iwe kwenye tupu ya mbele tu
Toka kwa Jaabir, amesema:
"كانتِ يَهودُ تقولُ مَنْ أَتَى امْرَأتَهُ في قُبُلِهَا مِنْ دُبُرِهَا كَانَ الْوَلدُ أَحْوَلَ، فَأَنْزَلَ اللَّهُ سبحانَهُ: نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أنَّى شِئْتُمْ"
“Mayahudi walikuwa (wanawaambia Waislamu) kwamba atakayemjimai mkewe kwa mtindo wa nyuma, basi mtoto (atakayezaliwa) atakuwa makengeza. Na hapo Allaah Ta’aalaa Akateremsha:
"نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ"
“Wake zenu ni konde kwenu. Basi ziendeeni konde zenu (panapotoka kizazi) vyovyote mpendavyo ”. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (4528), Muslim (1435), At-Tirmidhiy (2978), An-Nasaaiy (8976) na Ibn Maajah (1925)]
Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مُقْبِلَةً وَمُدْبِرَةً، ما كَانَ في الفَرْجِ"
“Ni sawa kuelekeana uso kwa uso, au kwa mgongo, lakini kwa sharti iwe kwenye tupu ya mbele”. [Asili yake ni kwenye Swahiyh mbili. Hili ni tamko la At-Twahaawiy katika Sharhul Ma’aaniy (3/41) kwa Sanad Swahiyh]
3- Mume anaruhusiwa kutembea kwenye mwili wote wa mkewe wakati wa jimai isipokuwa utupu wa nyuma.
Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) amesema:
"لا يَنْظرُ اللهُ عزَّ وجلَّ إلى رجُلٍ أتى رجُلًا أو امرأةً في دُبُرِهَا"
“Allaah ‘Azza wa Jalla Hatomwangalia Siku ya Qiyaamah mtu aliyemuingilia mwanaume au mwanamke nyuma”. [At-Tirmidhiy (1165), An-Nasaaiy (9001) na Ibn Abiy Shaybah (17070)]
Imepokelewa kwamba mtu mmoja alimuuliza Ibn Mas-‘uwd akisema:
"يَا أَبَا عَبْدِ الرَّحْمَنِ، آتِي امْرَأَتِي أَنَّى شِئْتُ؟، وحَيْثُ شِئْتُ؟، وَكَيْفَ شِئْتُ؟ قَالَ: نَعَمْ، فَنَظَرَ لهُ رَجُلٌ فَقَالَ لَهُ: إِنَّهُ يُرِيدُ الدُّبُرَ، قَالَ عَبْدُ الله: لَا، مَحَاشُّ النِّسَاءِ عَلَيْكُمْ حَرَامٌ "
“Ee Abu ‘Abdulrahmaan: Je, naweza kumuingilia mke namna yoyote nitakayo, popote nitakapo, na mtindo wowote nitakao? Akamwambia: Na’am. Mtu mwingine akamtazama na kumwambia: Anakusudia tupu ya nyuma huyu!!. Ibn Mas-‘uwd akamwambia: Tundu ya nyuma ya mwanamke ni haramu kwenu”. [Ibn Abiy Shaybah (3/530), Ad-Daarimiy (1/259) na At-Twahaawiy (3/46). Sanad yake ni Swahiyh]
Angalizo: Lililo haramu ni kujimai kwenye tupu ya nyuma (mapitio au njia ya haja kubwa). Ama kustarehe na kupapasia kwenye makalio mawili bila kuingiza dhakari nyuma, hili halina ubaya. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
4- Hairuhusiwi kumuingilia mke wakati wa hedhi:
Mwanamke anapokuwa hedhini, mwanaume anaruhusiwa kufanya naye mambo yote isipokuwa jimai tu.
5- Mwanamume akihisi hamu akataka kurudia raundi nyingine, basi atawadhe:
Ni kwa Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"إِذَا أَتَى أَحَدُكُمْ أَهْلَهُ ثُمَّ أَرَادَ أَنْ يَعُودَ فَلْيَتَوَضَّأْ"
“Akimuingilia mmoja wenu mke wake, kisha akataka tena, basi atawadhe”. [Swahiyh Muslim (308)]
6- Hakuna ukakasi wowote kama mke na mume watavua nguo zote wakati wa tendo la jimai:
Hakuna mpaka wa uchi kati ya mke na mume. Wanaweza kuangaliana sehemu zote za mwili. Hili limeelezwa kwenye mlango wa hukumu za kuangalia.
7- Haijuzu mwanamke kugomea tendo la ndoa mume wake akiwa na hamu nalo:
Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا دَعَا اَلرَّجُلُ امْرَأَتَهُ إِلَى فِرَاشِهِ فَأَبَتْ أَنْ تَجِيءَ، لَعَنَتْهَا اَلْمَلَائِكَةُ حَتَّى تُصْبِحَ "
“Mume akimwita mkewe kitandani na mke akagoma kwenda, basi Malaika watamlaani mpaka asubuhi”. [Al-Bukhaariy (5193) na Muslim (1436)]
8- Kama jicho la mwanaume litapiga kwa mwanamke mwingine akamsisimua, basi aende akamuingilie mkewe:
Imepokelewa toka kwa Jaabir bin ‘Abdullaah (Radhwiya Allaah ‘anhu):
"أنَّ رَسُولَ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ رَأَى امْرَأَةً، فأتَى امْرَأَتَهُ زَيْنَبَ وَهي تَمْعَسُ مَنِيئَةً لَهَا، فَقَضَى حَاجَتَهُ، ثُمَّ خَرَجَ إلى أَصْحَابِهِ، فَقالَ: إنَّ المَرْأَةَ تُقْبِلُ في صُورَةِ شيطَانٍ، وَتُدْبِرُ في صُورَةِ شيطَانٍ، فَإِذَا أَبْصَرَ أَحَدُكُمُ امْرَأَةً فَلْيَأْتِ أَهْلَهُ؛ فإنَّ ذلكَ يَرُدُّ ما في نَفْسِهِ"
“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona mwanamke, na hapo hapo akamwendea mkewe Zaynab ambaye alikuwa akiichakata ngozi, akamuingilia. Kisha akatoka kwa Maswahaba wake na kuwaambia: “Hakika mwanamke huwaelekea wanaume kwa picha ya shaytwaan na huwapita kwa picha ya shaytwaan. Basi yeyote akimwona mwanamke (akamsisimsha), amwendee mkewe, kwani hilo litamwondoshea moyo wake hisia aliyoipata”. [Muslim (1403), Abu Daawuwd (2151), na At-Tirmidhiy (1158), na riwaayah ni yake].
9- Yeyote katika wanandoa asieleze au kufichua siri za jimai baina yao:
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِنَّ مِنْ أَشَرِّ النَّاسِ عِنْدَ اللَّهِ مَنْزِلَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ الرَّجُلَ يُفْضِي إِلَى امْرَأَتِهِ وَتُفْضِي إِلَيْهِ ثُمَّ يَنْشُرُ سِرَّهَا ".
“Hakika mtu ambaye atakuwa na hadhi mbaya zaidi miongoni mwa watu mbele ya Allaah siku ya Qiyaamah, ni yule anayemvaa mkewe kimwili na mkewe akamvaa, kisha akaja kuelezea siri zake kwa watu”. [Muslim (1437) na Abu Daawuwd (4870)]
Lakini hili linajuzu kwa ajili ya maslaha ya kisharia kama walivyokuwa wake za Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakielezea ili kubainisha kwa watu namna Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akifanya ili tupate kumfuata. Kama yatakuwepo maslaha ya kisharia, basi hakuna ubaya. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
10-Mume anaporudi toka safari, asimshtukize mkewe, bali amjulishe siku na wakati wa kuwasili:
Ili mke apate kujitayarisha kwa ajili yake kwa usafi, kujitia manukato na kujipamba. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إذا قَدِمَ أَحَدُكُمْ لَيْلًا، فلا يأتيَنَّ أَهْلهُ طُرُوقًا، حتى تَسْتَحِدَّ المُغِيبَه، وتَمْتَشِطَ الشَّعِثَه
“Anaporudi mmoja wenu safari usiku, basi asimjie mkewe usiku huo huo, ili mkewe ambaye yeye amekuwa mbali naye, aweze kunyoa kinena, na kuzichana vizuri nywele alizokuwa hazishughulikii”. [Muslim (715)]
11- Mume anaweza kumjimai mkewe anayenyonyesha:
Toka kwa ‘Aaishah, toka kwa Judaamah bint Wahab Al-Asadiyyah kwamba alimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
"لَقَدْ هَمَمْتُ أَنْ أَنْهَى عَنِ الْغَيْلَةِ حَتَّى ذُكِّرْتُ أَنَّ الرُّومَ وَفَارِسَ يَفْعَلُونَ ذَلِكَ فَلاَ يَضُرُّ أَوْلاَدَهُمْ "
“Hakika nilidhamiria kukataza mume kumuingilia mkewe wakati ananyonyesha, kisha nikaona Warumi na Wafursi wanafanya hivyo, na watoto wao hawapati madhara yoyote”. [Muslim (1442)]
Maana ya "الغِيْلَةُ" ni mume kumuingilia mkewe wakati ananyonyesha, au kumuingilia wakati akiwa mja mzito.
12- Ni karaha mwanaume kumwaga manii nje ya tupu:
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu suala hili akasema:
" ذلِكَ الوَأْدُ الخَفِيُّ"
“Huo ni uzikaji siri wa kiumbe hai”. [Muslim (1442), Abu Daawuwd (3882), At-Tirmidhiy (2077), An-Nasaaiy (6/106) na Ibn Maajah (2011)]
Na hii ni sambamba na Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَإِذَا الْمَوْءُودَةُ سُئِلَتْ"
“Na mtoto wa kike aliyezikwa hali akiwa yuhai atakapoulizwa”. [At-Takwiyr: 08]
Jaabir (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:
"سَأَلَ رَجُلٌ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: إِنَّ عِنْدِي جَارِيَةً لِي وَأَنَا أَعْزِلُ عَنْهَا. فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: "إِنَّ ذَلِكَ لَنْ يَمْنَعَ شَيْئًا أَرَادَهُ اللَّهُ"
“Mtu mmoja alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akimwambia: Mimi nina kijakazi changu, lakini nikimuingilia, namwagia manii nje (nini hukmu yake)? Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Hilo halitozuia chochote Akitakacho Allaah.” [Muslim (1439)]
Toka kwa Jaabir (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:
"كُنَّا نَعْزِلُ عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَالْقُرْآنُ يَنْزِلُ "
“Tulikuwa enzi za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tunamwagia manii nje huku Qur-aan inateremka”. [Al-Bukhaariy (5208) na Muslim (1440)]
Matini zote hizi zinaonyesha kwamba mwanaume kumwagia nje manii wakati wa tendo la jimai na mkewe ni jambo lililokirihishwa. Na ijulikane kwamba hakuna nafsi yoyote ambayo Allaah Ameandika kwamba Ataiumba isipokuwa Atatimiza hilo, ni sawa mtu akimwagia nje au ndani. Kama Allaah Ameandika mimba ikamate, basi itakamata tu, ni sawa mtu amwagie maji ya uzazi nje, au avae kinga, au hata mwanamke atumie madawa, sindano, coil na kadhalika, itashika tu.
Links
[1] https://www.alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/284
[2] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11980&title=10G-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20%D9%83%D8%AA%D8%A7%D8%A8%20%D8%A7%D9%84%D8%B2%D9%88%D8%A7%D8%AC%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20%20%D9%88%D9%8E%D9%84%D9%90%D9%8A%D9%92%D9%85%D9%8E%D8%A9%D9%8F%20%D8%A7%D9%84%D8%B9%D9%8F%D8%B1%D9%92%D8%B3%D9%90%20Walima%20Wa%20Harusi
[3] http://www.alhidaaya.com/
[4] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11981&title=01-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Walima%20Wa%20Harusi%3A%20Maana%20Na%20Hukmu%20Yake
[5] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11982&title=02-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Walima%20Wa%20Harusi%3A%20Kualika%20Watu
[6] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11983&title=03-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Walima%20Wa%20Harusi%3A%20Kuitikia%20Mwaliko%20Wa%20Walima
[7] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11984&title=04-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Walima%20Wa%20Harusi%3A%20Nyudhuru%20Za%20Kutohudhuria%20Walima
[8] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11985&title=05-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Walima%20Wa%20Harusi%3A%20Pongezi%20Kwa%20Maharusi
[9] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11986&title=06-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Walima%20Wa%20Harusi%3A%20Adabu%20Za%20Usiku%20Wa%20Kukutana%20Mke%20Na%20Mume%20Baada%20Ya%20Kufunga%20Ndoa
[10] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11987&title=07-Swahiyh%20Fiqh%20As-Sunnah%3A%20Kitabu%20Cha%20Ndoa%3A%20Walima%20Wa%20Harusi%3A%20Adabu%20Na%20Ahkaam%20Za%20Jimai