Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
01: "الإِسْتِعَاذَةُ" Al-Isti’aadhah (A’uwdhu Bil Laahi Minash-Shaytwaan Ar Rajiym)
"الإِسْتِعَاذَةُ" (Al-Isti’aadhah), ni kuomba kinga kutokana na Neno Lake Taalaa: "أَعُوْذُ بِاللهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيْمِ".
Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Ametuwekea neno hili ili liwe ni njia kwa mwanadamu kuweza kujilinda na shetani na kumweka mbali naye ili asiweze kusababisha aina yoyote ya madhara kwake.
Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Anatuambia:
"وَقُل رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ ● وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُونِ"
“Na sema: Rabb wangu! Najikinga Kwako kutokana na udokezi wa mashaytwaan • Na najikinga Kwako Rabb wasinihudhurie”. [Al-Muuminuwna: 97-98]
Na Anatuambia tena:
"فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ"
“Unaposoma Qur-aan basi (kwanza) omba kinga kwa Allaah dhidi ya shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa”. [An Naml: 98].
Kuna aya nyingi zinazozungumzia suala hili na zote zinaonyesha juu ya umuhimu wa kujilinda na shari za kiumbe huyu ambaye ni adui mkubwa wa watu wote.
Hivyo basi, maana ya (Isti’aadhah) ni kujilinda au kukimbilia kwa mwenye kutoa hifadhi kutokana na jambo lenye kuogopewa. Mfano wa maana hiyo ni Kauli Yake Ta’alaa:
"وَقَالَ مُوسَىٰ إِنِّي عُذْتُ بِرَبِّي وَرَبِّكُم مِّن كُلِّ مُتَكَبِّرٍ لَّا يُؤْمِنُ بِيَوْمِ الْحِسَابِ"
“Na Muwsaa akasema: Hakika mimi najikinga kwa Rabb wangu na Rabb wenu, kutokana na kila mwenye kutakabari asiyeamini Siku ya Hesabu”. [Ghaafir: 27]
Miundo Ya Isti’aadhah:
Tamshi hili la isti’aadhah lina miundo kadhaa, nayo ni kama ifuatavyo:
1- أعُوْذُ بِاللهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيْمِ
“Najilinda kwa Allaah kutokana na shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa”.
Ni kutokana na Kauli Yake Ta’alaa:
"فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ"
“Unaposoma Qur-aan, basi (kwanza) omba kinga kwa Allaah dhidi ya shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa”. [An-Nahl: 97].
2- أَعُوْذُ بِاللهِ السَّمِيْعِ العَلِيْمِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيْمِ
“Najilinda kwa Allaah Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote kutokana na shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa”.
Ni kutokana na Kauli Yake Ta’alaa:
"وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ ۚ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ"
“Na pindi utakapokuchochea uchochezi kutokana na shaytwaan, basi omba kinga kwa Allaah. Hakika Yeye Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote”. [Al-A’araaf: 200]
3- أَعُوْذُ بِاللهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيْمِ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيْعُ العَلِيْمُ"
“Najlinda kwa Allaah kutokana na shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa, hakika Yeye (Allaah) Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote”.
Tamko hili limechanganya aya mbili zilizotangulia.
4- أَعُوْذُ بِاللهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيْمِ مِنْ نَفْخِهِ، وَنَفْثِهِ، وَهَمْزِهِ
“Najilinda kwa Allaah na shetani aliyewekwa mbali na rehma za Allaah kutokana na kiburi chake, mashairi yake, na wasiwasi wake”.
Kwa maana, najilinda kwa Allaah shetani asinipulizie sifa ya kuwa na kibri, wala kunikoroga nikatunga mashairi potoshi, wala kunishawishi akanitia kwenye upotovu.
Matamshi haya yote yanafaa kisheria kutokana na kuthibiti kwake kwenye Qur-aan na Sunnah.
Isti’aadhah inatubainishia uhakika wa mwanadamu kwamba ni kiumbe mhitaji, kiumbe dhaifu, na kiumbe mwenye uwezo mdogo kabisa. Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Anaujua udhaifu huu wa mwanadamu na Anajua kwamba shetani ndiye adui wake mkubwa anayemwandama kwa ushawishi, na kumuingiza kwenye maasia, machafu na madhara mengineyo katika kipindi cha masaa 24. Na mwanadamu kutokana na udhaifu wake huu, ni vigumu mno kukabiliana na ushawishi huu wa shetani usiokoma. Na hapa ndipo unapokuja umuhimu wa isti’aadha kwa Mwislamu ambapo anakimbilia kwa Allaah Mtukufu ili Amlinde kutokana na uadui huu, na ili aweze kushikamana ipasavyo na Njia ya Allaah Mtukufu iliyonyooka. Yeye Pekee Ndiye Mweza wa kumshinda shetani na kumwepushia Mwislamu shari zake na adha zake.
Bila shaka kumshinda shetani kunakuwa kwa kumtii Allaah, kumdhukuru na kunyooka sawasawa. Mwislamu anawajibika kupambana na shetani kwa njia zote ambazo Allaah Ameziweka, kwa kuwa shetani ni adui mbaya zaidi kuliko adui wa kibinadamu anayeonekana. Adui anayeonekana ni rahisi kukabiliana naye hata kama ana nguvu. Ama asiyeonekana, bila shaka inakuwa ni vigumu mno kukabiliana naye. Adui wa kibinadamu anawezekana kufanya naye mazungumzo ya suluhu, anaweza kukabiliwa kwa mujibu wa nguvu zake kwa mikakati tofauti na pia uadui wake unaweza kumalizwa kwa njia ya kidiplomasia. Allaah Anatuambia:
"وَلَا تَسْتَوِي الْحَسَنَةُ وَلَا السَّيِّئَةُ ۚ ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِي بَيْنَكَ وَبَيْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِيٌّ حَمِيمٌ"
“Na wala haulingani sawa wema na uovu. Zuia (uovu) kwa ambalo ni zuri zaidi. Hapo utamkuta yule ambaye baina yako na baina yake kuna uadui, kama ni rafiki mwandani”. [Fusswilat: 34]
Hivyo basi, ni wajibu kwa Mwislamu ajilinde daima kwa Allaah kutokana na shari za kiumbe huyu akichukua kwa hilo kigezo chema toka kwa Manabii wa Allaah pamoja na watu wema ambao kutokana na kujilinda kwao huku, Allaah Aliwaepushia shari za shetani na kuwafanikishia mambo yao mema waliyokuwa wakiyatarajia. Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Akituelezea kuhusu Nabii Nuhu ‘Alayhis Salaam Anatuambia:
"قَالَ رَبِّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ أَنْ أَسْأَلَكَ مَا لَيْسَ لِي بِهِ عِلْمٌ ۖ وَإِلَّا تَغْفِرْ لِي وَتَرْحَمْنِي أَكُن مِّنَ الْخَاسِرِينَ"
“Akasema: Ee Rabb wangu! Hakika mimi najikinga Kwako kukuomba yale nisiyo na elimu nayo. Na Usiponighufuria na Ukanirehemu, nitakuwa miongoni mwa waliokhasirika”. [Hud: 47]
Na hapo Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Alimpa mambo mawili ambayo ni amani na Baraka kama linavyoelezea Neno Lake Ta’alaa:
"قِيلَ يَا نُوحُ اهْبِطْ بِسَلَامٍ مِّنَّا وَبَرَكَاتٍ عَلَيْكَ وَعَلَىٰ أُمَمٍ مِّمَّن مَّعَكَ ۚ وَأُمَمٌ سَنُمَتِّعُهُمْ ثُمَّ يَمَسُّهُم مِّنَّا عَذَابٌ أَلِيمٌ"
“Pakasemwa: Ee Nuwh! Teremka (jahazini) kwa salama kutoka Kwetu na baraka nyingi juu yako, na juu za umati zilizo pamoja na wewe. Na umati Tutakazozistarehesha, kisha zitawagusa kutoka Kwetu adhabu iumizayo”. [Hud: 48]
Naye mama wa Maryam aliposema kama inavyotuelezea Quraan Tukufu:
"وَإِنِّي أُعِيذُهَا بِكَ وَذُرِّيَّتَهَا مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ"
“Nami namkinga Kwako na dhuria wake kutokana na shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa”. [Aaal ‘Imraan: 36]
Allaah Mtukufu Akamkirimu kama Anavyotuambia:
"فَتَقَبَّلَهَا رَبُّهَا بِقَبُولٍ حَسَنٍ وَأَنبَتَهَا نَبَاتًا حَسَنًا وَكَفَّلَهَا زَكَرِيَّا"
“Basi Rabb wake Akampokea kwa kabuli njema, na Akamkuza mkuzo mwema, na Akamfanya Zakariyyaa kuwa mlezi wake”. [Aaal ‘Imraan: 37]
Kadhalika, Bi Maryam ‘Alayhas Salaam wakati alipomwona Jibriyl katika sura ya mwanamume akimjia naye yuko peke yake mbali kabisa na watu alisema kama inavyotuhadithia Quraan:
"قَالَتْ إِنِّي أَعُوذُ بِالرَّحْمَـٰنِ مِنكَ إِن كُنتَ تَقِيًّا"
“(Maryam) akasema: Najikinga kwa Ar-Rahmaan usinidhuru, ukiwa ni mwenye taqwa”. [Maryam: 18]
Na hapo bi huyo akapata neema mbili; mtoto bila ya baba na utakaso toka kwa Allaah kupitia ulimi wa kitoto chake kichanga baada ya kutuhumiwa kwamba amezini.
Ama tukija kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), tunakuta kwamba Allaah Subhaanahu wa Taalaa Amemwelekeza faida ya neno hili mbali na kumwamuru kushikamana nalo katika mwenendo mzima wa maisha yake. Allaah Anamwambia:
"وَقُل رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ ● وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُونِ"
“Na sema: Rabb wangu! Najikinga Kwako kutokana na udokezi wa mashaytwaan ● Na najikinga Kwako Rabb wasinihudhurie”. [Al-Muuminuwna: 97-98]
Na Anamwambia tena:
"وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ"
“Na utakapokuchochea uchochezi kutoka kwa shaytwaan, basi omba kinga kwa Allaah. Hakika Yeye Ndiye Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote”. [Fusswilat: 36]
Na imepokelewa toka kwa Khawlah binti Hakiym kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَنْ نَزَلَ مَنْزِلًا فَقَالَ: أَعُوْذُ بِكَلِمَاتِ اللهِ التَّامَّاتِ مِنْ شَرِّ مَا خَلَقَ، لَمْ يَضُرَّهُ شَيءٌ حَتَى يَرْتَحِلَ مِنْ مَنْزِلِه"
“Mwenye kufikia kwenye nyumba yoyote kisha akasema: Najilinda kwa Maneno ya Allaah yaliyotimia kutokana na shari ya Alivyoviumba, basi hakitomdhuru chochote mpaka aondoke kwenye nyumba hiyo”. [Hadiyth hii iko kwenye Fat-hul Baariy kwa Sharh ya Swahiyh Al Bukhaariy].
Kadhalika, imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu Anhumaa) akisema:
" انَ رسولُ اللَّهِ صلى اللَّهُ عليهِ وسلَّمَ كَانَ يعوِّذُ الحسنَ والحسينَ ، يقولُ : أعيذُكُما بِكلماتِ اللَّهِ التَّامَّةِ ، مِن كلِّ شيطانٍ وَهامَّةٍ ومن كلِّ عينٍ لامَّةٍ"
“Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwaombea kinga Al-Hasan na Al-Husayn akisema: Nawalindeni kwa usaidizi wa Maneno ya Allaah yaliyotimia kutokana na mashetani wa aina zote na wanyama wenye sumu, na kutokana na kila jicho lenye kudhuru”. [Hadiyth Swahiyh. Swahiyhul Bukhaariy (3371)]
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
02: Basmalah:
"البَسْمَلَةُ" (Basmalah), ni kifupisho cha neno "بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ" (Bismil Laah Ar Rahmaan Ar Rahiym. Kwa ‘ijmaa ya Maulamaa, “Basmalah” ni sehemu ya aya ya Qur-aan kwenye Suwrat An Naml Anaposema Allaah Mtukufu:
"إِنَّهُ مِن سُلَيْمَانَ وَإِنَّهُ بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ"
“Hakika inatoka kwa Sulaymaan, na hakika (imeanza) Kwa Jina la Allaah, Ar-Rahmaan, Mwenye Kurehemu”. [An Naml: 30
Na mtu anaposema neno hili wakati wa kuanza jambo lake lolote, ni kana kwamba anasema: “Naanza kumtaja Allaah Mtukufu, na ninataka msaada na tawfiyq kwa Jina Lake Tukufu katika jambo langu hili, kwani Yeye Ndiye Mweza wa kila kitu, Mwenye Fadhila duniani na akhera, na Mwenye Kuwaneemesha viumbe wote”. Na Mwislamu anatakiwa wakati wote aianze kazi yake kwa kulitamka neno hili kwa ulimi wake na kulihudhurisha ndani ya moyo wake. Ikiwa atalitamka kwa nia safi na ya kweli, basi shetani atajiweka mbali naye, baraka ya kazi yake itaongezeka, na tawfiyq na utekelezaji mwema wa kazi utakuwa pamoja naye.
Uhakika wa neno hili unamaanisha kwamba Muislamu amejisalimisha na kuingia ndani ya kumbatio la Kimola, anafanya kazi yake kwa ajili ya Allaah Peke Yake, anatarajia msaada Wake Yeye Peke Yake, ametawakali Kwake Yeye Pekee na anatarajia kuzipata Rehma Zake za kudumu. Anakuwa kana kwamba anasema: “Hakika mimi ninafanya kazi yangu hii nikijivua kwamba inafanyika kwa jina langu mimi, bali kwa Jina la Allaah Mtukufu, kwa kuwa mimi ninapata nguvu na usaidizi kutoka Kwake Yeye tu. Nazitaraji ihsani Zake na Msaada Wake, kwani bila Yeye, mimi siwezi lolote wala chochote”.
Inatosha kwa Muislamu kuwa “Basmalah” inampa liwaziko kwamba yu pamoja na Allaah, na kwamba yeye anajipamba kwa lile Analolipenda Allaah, na kwamba madhali usaidizi wa Allaah u pamoja naye, basi amali yake na kazi yake haitokwenda arijojo.
Maulamaa wote wanakubaliana kwamba “Basmalah” ni muhimu mno katika kila kitendo na kila neno. Aidha, wamekubaliana kwamba Maswahaba walioandika Msahafu katika enzi ya ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu Anhum), waliandika “Basmalah” mwanzoni mwa kila sura, kwa kuwa “Basmalah”, ni aya ya Qur-aani Tukufu inayonasibiana na ufunguzi wa kila sura.
Lakini pamoja na hivyo, Maulamaa hawa wamekhitalifiana katika suala la kuizingatia “Basmalah” kwamba ni aya ya Quraan kwenye Sura nyinginezo ikiwemo Surat Al-Faatihah. Rai zao ziko kwenye mielekeo mitatu:
Mwelekeo wa kwanza:
“Basmalah” mwanzoni mwa sura si aya ya Qur-aan Tukufu, si katika Surat Al-Faatiha wala sura nyingineyo yoyote, bali imeandikwa mwanzoni mwa kila sura kwa ajili ya kutenganisha kati ya sura na nyingineyo. Wenye rai hii wametoa dalili za nukuu na dalili za kiakili.
Dalili Za Nukuu:
Dalili ya kwanza:
Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyopokelewa na Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"قسَّمْتُ الصَّلاةَ بَيْنِي وَبَيْنَ عَبْدِيْ نِصْفَيْنِ، فَنِصْفُهَا لي وَنِصْفُهَا لِعَبْدِيْ، وَلِعَبْدِيْ مَا سَألَ ، فَإِذَا قَالَ : الحمدُ للهِ ربِّ العالمين، فَأَقُوْلُ: حمَدَنِي عَبْدِيْ...."
“Allaah Anasema: Nimeigawanya Al-Faatihah nusu mbili, kati Yangu na Mja Wangu. Nusu yake ni Yangu, na nusu nyingine ni ya Mja Wangu. Na Mja Wangu Nitampa analoliomba. Mja Wangu akisema: “Al-Hamdu Lillaahi Rabbil ‘Aalamiyna”, basi na Mimi Nasema: Mja Wangu Kanihimidi…..”. [Hadiyth Swahiyh. Imepokelewa na Abu Hurayrah]
Wanasema kwamba makusudio ya swalah hapa قَسَّمْتُ الصَّلَاة, ni kusoma Al-Faatihah katika swalah, kwani kila mwenye kuswali anaposoma aya ya sura hii, Allaah Humjibu mpaka mwisho wa sura kama ilivyobainisha Al Hadiyth Al-Qudsiy hii ambayo hatukuimalizia. Na katika Hadiyth hii, Rasuli Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuitaja “Basmalah”, na wala hakuizingatia kwamba ni sehemu ya Al-Faatihah.
Dalili ya pili:
Ubayya bin Ka’ab amesema: Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniuliza:
"ما تقرأُ في الصَّلاةِ؟ فقرأتُ عليه أمَّ القرآنِ، فقال: والَّذي نفسي بيدِه ما أُنزِل في التَّوراةِ ولا في الإنجيلِ ولا في الزَّبورِ ولا في الفرقانِ مثلُها، إنَّها السَّبعُ المثاني، والقرآنُ العظيمُ الَّذي أُعطيتُه"
“Vipi unasoma unapoifungua swalah yako?” Nikamsomea Ummul Qur-aan. Akaniambia: Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko Mkononi Mwake, haikuteremshwa si katika Tauraat, wala katika Injiyl, wala katika Zaburi, wala katika Furqaan mfano wake. Hakika hiyo ni As-Sab-’u Al-Mathaaniy (Aya saba zenye kukaririwa mara kwa mara), na Al-Qur-aan Al-‘Adhwiym ambayo nimepewa”. [Imechakatwa na At-Tirmidhiy (2875), An-Nasaaiy katika As-Sunan Al-Kubraa (11205) na Ahmad (9345)]
Hii ni dalili kwamba Basmalah si katika Al-Faatihah, kwa kuwa Ubayya hakuisoma pamoja na aya nyingine za Surat Al-Faatihah. Na Rasuli akamkubalia hilo, na wala hakumweleza kwamba ni lazima asome Basmalah.
Dalili Za Kiakili:
Dalili ya kwanza:
Lau kama Basmalah ingelikuwa ni sehemu ya Qur-aan, basi ingelithibitishwa kwa njia ya masimulizi jumuiya ya kizazi hadi kingine “Tawaatur”, na hili halikutokea. Na lau kama lingetokea, basi lingejulikana kwa lazima.
Dalili ya pili:
Inatutosha sisi kujua kwamba Basmalah imekhitalifiwa kati ya Maulamaa, na Qur-aan haikhitilafiwi.
Dalili ya tatu:
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameibainisha Qur-aan Tukufu ubainisho mmoja ulio sawa. Hakudhihirisha baadhi ya mambo na kuyaficha mengine, bali yote kayadhihirisha kwa usawa mmoja.
Mwelekeo Wa Pili:
Hawa wanasema kwamba Basmalah ni aya kamili ya Qur-aan Tukufu iliyoteremka kwa ajili ya kutenganisha kati ya sura. Dalili zao ni:
Dalili ya kwanza:
Kuandikwa Basmalah kwenye Msahafu, ni dalili kwamba ni Qur-aan, lakini haionyeshi kwamba ni aya katika Surat Al-Faatihah au kwenye sura nyingineyo yoyote ile.
Mwelekeo Wa Tatu:
Wanasema kwamba Basmalah ni aya katika Surat Al-Faatihah na katika kila sura ya Qur-aan Tukufu. Dalili zao ni hizi zifuatazo:
Dalili ya kwanza:
Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إذَا قَرَأْتُم الحَمْدُ فَاقْرَؤُوْا بِسْمِ اللهِ الرّحْمَنِ الرّحِيمِ، إِنَّهَا أُمُّ القُرْآنِ وَأُمُّ الكِتَابِ والسَّبْعُ المَثَانِي وبِسْمِ اللهِ الرّحْمَنِ الرّحِيمِ إحدى آياتها"
“Mnaposoma Alhamdu, basi someni: Bismillaahi Ar Rahmaan Ar Rahiym, kwani hakika Al-Hamdu ni mama wa Qur-aan, mama wa Kitabu, na aya saba zenye kurudiwa mara kwa mara, na Bismil Laahir Rahmaanir Rahiym ni moja ya aya zake ”. [Imechakatwa na Ad-Daaraqutwniy (1/312) na Al-Bayhaqiy (2486)]
Dalili ya pili:
"سُئِلَ أنَسٌ: كيفَ كَانَتْ قِرَاءَةُ النَّبيِّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم؟ فَقالَ: كَانَتْ مَدًّا، ثُمَّ قَرَأَ: بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ [الفاتحة: 1]؛ يَمُدُّ بـ{بِسْمِ اللَّهِ}، ويَمُدُّ بـ{الرَّحْمَنِ}، ويَمُدُّ بـ{الرَّحِيمِ}"
“Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliulizwa namna Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa anaisoma Qur-aan akasema: “Alikuwa anavuta “madd” (herufi za kuvutwa kwa mujibu wa taaluma ya tajwiyd). Kisha akasoma: "بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ" hadi kuimaliza suwratil Faatihah yote. Akasema: Anavuta "بِسْمِ اللَّـهِ" , anavuta "الرَّحْمَـٰنِ", na anavuta "الرَّحِيمِ".” [Hadiyth Swahiyh. Swahiyhul Bukhaariy (5046)]
Hapa Anas ameanza kwa "بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ"
Dalili ya nne:
Hadiyth ya Anas Radhwiya Allaahu ‘Anhu:
"بَيْنَا رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم ذَاتَ يَوْمٍ بَيْنَ أَظْهُرِنَا، إِذْ أَغْفَىٰ إِغْفَاءَةً. ثُمَّ رَفَعَ رَأْسَهُ مُتَبَسِّماً. فَقُلْنَا: مَا أَضْحَكَكَ يَا رَسُولَ اللّهِ؟ قَالَ: أُنْزِلَتْ عَلَيَّ آنِفاً سُورَةٌ. فَقَرَأَ: بِسْمِ الله الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ ● إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ ● فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ● إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الأَبْتَرُ ، ثُمَّ قَالَ: أَتَدْرُونَ مَا الْكَوْثَرُ؟ فَقُلْنَا: الله وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ. قَالَ: فَإِنَّهُ نَهْرٌ وَعَدَنِيهِ رَبِّي عَزَّ وَجَلَّ، ...."
“ Siku moja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa nasi, alisinzia kidogo, kisha akanyanyua kichwa chake akitabasamu. Tukamuuliza: “Nini kimekuchekesha ewe Rasuli wa Allaah?!” Akasema: “Imenishukia sasa hivi Surah”. Kisha akasoma:
بِسْمِ الله الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ ● إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ ● فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ● إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الأَبْتَرُ
Kisha akauliza: “Mnajua ni nini Al-Kawthar?” Tukajibu: “Hapana”. Akasema: “Ni mto ambao Allaah Ameniahidi Peponi….”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Muslim (400)]
Wenye rai hii wanasema kwamba Hadiyth hii inaonyesha kwamba Basmalah ni aya ya katika kila Surah ya Qur-aan Tukufu kwa dalili kwamba Rasuli kaisoma mwanzoni mwa Surat Al-Kawthar.
Dalili ya tano:
Hii ni dalili ya kiakili wakisema kwamba Msahafu wa Al Imaam uliandikwa ndani yake Basmalah mwanzoni mwa Surat Al-Faatihah, na kila mwanzoni mwa Sura zote za Quraan tukufu isipokuwa Surah moja tu ambayo ni Baraa’. Na hili limekuwa kwa njia ya “tawaatur” kati ya Waislamu huku tukijua kwamba wao hawakuwa wakiandika kwenye Qur-aan kile ambacho si katika Qur-aan Tukufu.
Kutokana na dalili zote hizi zilizotiliwa nguvu kwa dalili hizi za kunukuliwa na dalili za kiakili toka kwa Maulamaa wetu hao wenye hima na shime kubwa ya kukilinda Kitabu chetu hiki, tunasema kwamba Basmalah ni aya ya Qur-aan ambayo imekariri mwanzoni mwa kila Sura kwa ajili ya kutabaruku.
Mwahala Ambapo Basmalah Imekokotezwa Kuitamka:
1- Wakati wa kuanza kusoma Qur-aan Tukufu.
2- Wakati wa kuanza khutba ya swalah ya ijumaa, khutba ya eid mbili na kadhalika.
3- Wakati wa kuingia chooni.
4- Wakati mtu anapoanza kutawadha.
.
5- Wakati wa kuanza kula.
.
6- Wakati wa kuchinja mnyama na katika kila shughuli yoyote ya kheri anayoifanya Muislamu.
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
03: Suwrat Al-Faatihah
Suwrat Al Faatihah, ni mama wa Qur-aan Tukufu, nayo ndiyo sura ya mwanzo kabisa kuandikwa kwenye Msahafu wa ‘Uthmaan. Aya zake ni saba.
Sura hii ina majina mbalimbali. Kati ya majina hayo ni:
1- Faatihatul Kitaab "فَاتِحَةُ الكِتَابِ"(Kifungua Kitabu(. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"لاَ صَلاَةَ لِمَنْ لَمْ يَقْرَأْ بِفَاتِحَةِ الْكِتَابِ"
“Swalah haiswihi kwa asiyesoma Faatihatul Kitaab”. [Swahiyh Muslim (394)]
2- Ummul Qur-aan na Ummul Kitaab "أُمُّ القُرْآنِ وَأُمُّ الكِتَابِ" (Mama wa Qur-aan na Mama wa Kitabu).
Ni kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam:
"كُلُّ صَلاَةٍ لاَ يُقْرَأُ فِيهَا بِأُمِّ الْكِتَابِ فَهِيَ خِدَاجٌ "
“Swalah yoyote ambayo haikusomwa ndani yake Ummul Kitaab, basi ni pungufu”. [Sunan Ibn Maajah: 840]
3- As Sab-‘u Al-Mathaaniy "السَّبْعُ المَثَانِيْ"
Hii ni kwa vile aya zake ni saba ambazo hukaririwa kwenye swalah moja. Baadhi ya Mufassiruuna wanasema kwamba sababu ya kuitwa hivyo ni kwa vile ilishuka mara moja Makkah na ikashuka mara nyingine Madiynah.
4- Al-Qur-aan Al-‘Adhwiym "القُرْآنُ العَظِيْمُ"
Ni kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam:
"(الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ) هِيَ السَّبْعُ الْمَثَانِي وَالْقُرْآنُ الْعَظِيمُ الَّذِي أُوتِيتهُ"
“Al-Hamdu Lillaahi Rabbi Al-‘Aalamiyna, ni As Sab-‘ul Mathaaniy, na Al-Qur-aan Al-Adhwiym niliyopewa”. [Hadiyth Swahiyh. Swahiyhul Bukhaariy (5006)]
Haya ndiyo majina yake mashuhuri zaidi. Ina majina mengineyo kama:
الْحَمْدُ، الصَّلاةُ، الشِّفَاءُ، الرُّقْيَةُ، أَسَاسُ القُرْآنِ، الوَاقِيَةُ، الكَافِيَةُ، الوَافِيَةُ
Himdi, du’aa, ponyo, zinguo. msingi wa Qur-aan, kinga, toshelezi, yenye kukidhi.
Na majina yote haya bila shaka yanaonyesha nguvu ya sura hii na yale yaliyomo ndani yake.
Fadhila Yake:
Kuna Hadiyth nyingi zinazozungumzia kuhusiana na fadhila za sura hii. Kati ya hizo ni:
(a) Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd bin Al-Mu’allaa Radhwiya Allaahu ‘anhu, amesema:
" كُنْتُ أُصَلِّي فِي الْمَسْجِدِ، فَدَعَانِي النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم فَلمْ أُجِبْهُ حَتَّى صَلَّيْتُ ثُمَّ أَتَيْتُهُ. فَقُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ: إِنِّي كنت أُصَلِّي، فَقَالَ: أَلَمْ يَقُلِ اللَّهُ: اسْتَجِيبُوا لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دعَاكُمْ، ثمَّ قَالَ لي: أَلَا أُعَلِّمُكَ أَعْظَمَ سُورَةٍ فِي الْقُرْآنِ قَبْلَ أَنْ تَخْرُجَ مِنَ الْمَسْجِدِ. فَأَخَذَ بِيَدِي، فَلَمَّا أَرَادَ أَنْ يَخْرُجَ قُلْتُ لَهُ: أَلَمْ تَقُلْ لَأُعَلِّمَنَّكَ سُورَةً هِيَ أَعْظَمُ سُورَة مِنَ الْقُرْآنِ، قَالَ: الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ، هِيَ السَّبْعُ الْمَثَانِي وَالْقُرْآنُ الْعَظِيمُ الَّذِي أُوتِيتهُ "
“Nilikuwa nikiswali Msikitini, kisha Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniita, nami sikumwitikia. Nikamaliza kuswali kisha nikamwendea na kumwambia: Ee Rasuli wa Allaah! Nilikuwa naswali”. Akaniambia: Je, Hakusema Allaah: Mwitikieni Allaah na Rasuli Anapokuiteni?!” Kisha akaniambia: Je, nikufundishe sura iliyo adhimu zaidi ndani ya Qur-aan Tukufu kabla hujatoka Msikitini?. Kisha akaukamata mkono wangu. Na wakati alipotaka kutoka nilimwambia: Si umeniambia kwamba utanifundisha sura adhimu zaidi katika Qur-aan! Akasema: Al-Hamdu Lillaahi Rabbil ‘Aalamiyna, ndiyo As Sab-‘ul Mathaaniy na Al-Qur-aan Al-‘Adhwiym niliyopewa”. Hadiyth Swahiyh. Swahiyhul Bukhaariy (5006)]
(b) Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema:
"بَيْنَمَا جِبْرِيلُ قَاعِدٌ عِنْدَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم سَمِعَ نَقِيضًا مِنْ فَوْقِهِ فَرَفَعَ رَأْسَهُ فَقَالَ: هَذَا بَابٌ مِنَ السَّمَاءِ فُتِحَ الْيَوْمَ لَمْ يُفْتَحْ قَطُّ إِلاَّ الْيَوْمَ، فَنَزَلَ مِنْهُ مَلَكٌ فَقَالَ: هَذَا مَلَكٌ نَزَلَ إِلَى الأَرْضِ لَمْ يَنْزِلْ قَطُّ إِلاَّ الْيَوْمَ فَسَلَّمَ وَقَالَ: أَبْشِرْ بِنُورَيْنِ أُوتِيتَهُمَا لَمْ يُؤْتَهُمَا نَبِيٌّ قَبْلَكَ: فَاتِحَةُ الْكِتَابِ وَخَوَاتِيمُ سُورَةِ الْبَقَرَةِ، لَنْ تَقْرَأَ بِحَرْفٍ مِنْهُمَا إِلاَّ أُعْطِيتَهُ"
“Wakati Jibriyl alipokuwa amekaa kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), mara alisikia sauti toka juu yake. Akanyanyua kichwa chake akamwambia: “Huu ni mlango wa mbinguni, umefunguliwa leo. Haujawahi kamwe kufunguliwa isipokuwa leo. Malaika akateremka kupitia mlango huo na Jibriyl akamwambia Rasuli: Huyu Malaika ameteremka ardhini, kamwe hakuwahi kuteremka isipokuwa leo. Malaika akamtolea salaam (Nabiy) na kumwambia: Furahia nuru hizi mbili ulizopewa, hakupewa Nabiy yeyote kabla yako: Faatihatul Kitaab na aya (mbili) za mwishoni mwa Suwrat Al-Baqarah. Hutasoma herufi yeyote toka humo isipokuwa utapewa (nuru zake na kujibiwa du’aa zilizomo humo)”. [Hadiyth Swahiyh. Swahiyh Muslim (806)]
Maana Ya Kiujumla Ya Suwrat Al Faatihah:
Katika sura hii, Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Anawaelezea Waja Wake kwamba Yeye Pekee Ndiye Anayestahiki himdi yote, na kwamba himdi hii ni lazima iendelee wakati wote, kwani Yeye Ndiye Mfalme Anayeuendesha ulimwengu huu wote ukiwa ndani ya rehma kamili, ya kudumu na jumuishi. Kama ambavyo Yeye Subhaanahu wa Ta’alaa, Ndiye Mwenye mamlaka ya mwisho huko akhera ambapo Atawafanyia viumbe vyote hisabu kutokana na matendo yao waliyoyafanya hapa duniani, mema yatalipwa kwa mema na ziada, na mabaya yatalipwa mabaya mithili yake. Siku hiyo hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kufurukuta kama ilivyo hapa duniani ambapo viongozi wenye madaraka makubwa, ndio wanaojiona kwamba wao ndio wao. Siku hiyo wote watanywea na Uadhama wa kweli wa Allaah utadhihiri mbele ya viumbe vyote kuanzia Malaika, majini, wanadamu na vinginevyo.
Kisha sura hii inabainisha njia ya kuokoka, nayo ni kumfanyia Allaah ibada Yeye tu na kumtakasia nia, na kumtaka msaada Yeye tu pasina mwingine. Na hapo ndipo unapodhihiri utwana wa viumbe mbele ya Mwabudiwa Mtukufu Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Ambaye Hafai kushirikishwa na kiumbe chochote katika ibada. Na wakati mja anapoishi katika hali ya utumwa, hapo anahisi daima kumhitajia Mola wake, kumtaka msaada na kumwomba wakati wote. Hapo ndipo inapobubujika Nuru ya Allaah kwenye nafsi yake na akili yake, na anakuwa na furaha ya kufuata njia ya kweli iliyo sahihi ambayo Allaah Ta’aalaa Amemwamuru Rasuli kuifuata. Njia hii ni ile waliyoifuata Manabii, wasadikishaji na mashahidi ambao Allaah Ta’aalaa Amewaneemesha. Na wakati huo huo, mja huyu anajiepusha na njia ya upotovu na anajiepusha kwa akili yake na wasiwasi wa shetani na anaishi ndani ya Radhi za Allaah Mtukufu.
Hakika kilele cha kuomba msaada kwa Allaah Mtukufu kiko katika dua ambayo kwayo Mwislamu kwa nia safi kabisa na kwa ikhlasi ya mwisho, anaelekea kwa Mola wake akimwomba Amwepushe na njia ya wenye kutangatanga waliopotea ambao Allaah Amewaghadhibikia kwa kupotoka kwao na kwenda njia nyingine, huku ukweli wakiujua na kuukataa kwa kiburi, inda na hasadi. Na hao wanaongozwa na Ahlul Kitaab.
Kuisoma Suwratul Faatihah katika Swalah.
Mafuqahaa wamekhitalifiana kuhusiana na suala la kusoma Al-Faatiha katika swalah katika rai mbili:
Rai Ya Kwanza:
Wenye rai hii wanasema kwamba kusoma Al-Faatihah katika swalah ni sharti ya kusihi kwa swalah na mwenye kuiacha pamoja na kuwa na uwezo wa kuisoma, basi swalah yake hubatilika. Dalili yao ni Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"لاَ صَلاَةَ لِمَنْ لَمْ يَقْرَأْ بِفَاتِحَةِ الْكِتَابِ"
“Swalah haiswihi kwa asiyesoma Faatihatul Kitaab”. [Swahiyh Muslim (394)]
Rai Ya Pili:
Hawa wanasena kwamba Al-Faatihah si sharti ya kusihi swalah. Mwenye kuaicha na akasoma sura nyingine, basi swalah yake ni sahihi. Dalili yao ni Kauli Yake Ta’alaa:
"إِنَّ رَبَّكَ يَعْلَمُ أَنَّكَ تَقُومُ أَدْنَىٰ مِن ثُلُثَيِ اللَّيْلِ وَنِصْفَهُ وَثُلُثَهُ وَطَائِفَةٌ مِّنَ الَّذِينَ مَعَكَ ۚ وَاللَّـهُ يُقَدِّرُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ ۚ عَلِمَ أَن لَّن تُحْصُوهُ فَتَابَ عَلَيْكُمْ ۖ فَاقْرَءُوا مَا تَيَسَّرَ مِنَ الْقُرْآنِ"
“Hakika Rabb wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Anajua kwamba unasimama (kuswali) karibu na thuluthi mbili za usiku au nusu yake, au thuluthi yake, na pia kundi miongoni mwa wale walio pamoja nawe. Na Allaah Anakadiria usiku na mchana. Anajua kwamba hamuwezi kuukadiria wakati wake na kusimama kuswali, hivyo basi Amepokea tawbah yenu. Basi someni kile kilicho chepesi katika Qur-aan”. [Al-Muzzammil: 20]
.
Mufassiruna wote wanakubaliana kwamba aya hii iliteremka kuhusiana na swalah ya usiku isipokuwa wenye rai hii wanasema kwamba inahusiana na swalah za usiku na swalah nyinginezo kiujumla.
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
04: Ulinganio Wa Tawhiyd:
Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
"يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ● الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ"
“Enyi watu! Mwabuduni Rabb wenu Ambaye Amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kuwa na taqwa. Ambaye Amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa ni paa, na Akateremsha kutoka mbinguni maji, Akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu. Basi msimfanyie Allaah waliolingana naye na hali ya kuwa nyinyi mnajua”. [Al-Baqarah: 21-22]
Aya hizi mbili tukufu zinaelekezwa kwa watu wote juu ya kutofautiana akida zao na mapote yao, na juu ya kupita na kutanuka zama mpaka Siku ya Qiyaamah. Aya hizi zinawazindua juu ya ulazima wa kumpwekesha Allaah Mtukufu na kumtakasia ibada Yeye Peke Yake, kwani Yeye Ndiye Anayestahiki kwa hilo. Imekuwa ni katika Neema Zake Allaah Mtukufu kuwajulisha watu mambo ambayo yanaonyesha juu ya Upweke wa Allaah Aliyeuumba ulimwengu wote huu na kuweka ndani yake yale yote wanayoyahitajia viumbe Vyake katika maisha yao. Amewakumbusha hapa kwamba Yeye Ndiye Aliyewapatisha baada ya kuwa hawapo, Akawaumba, Akawaweka sawa, Akawapa akili na nguvu na Akawafadhilisha wanadamu kuliko viumbe vinginevyo Alivyoviumba.
Yeye Ndiye Aliyewaumba wanadamu waliopita, waliopo hivi sasa na watakaokuja baadaye. Na hii si kwa wanadamu tu, bali hata kwa viumbe vinginevyo hai na visivyo hai. Viko vilivyoanza vikaondoka, na viko vinavyokuja na kufuatiliwa na vinginevyo mpaka mwisho wa ulimwengu wetu huu. Na huu ndio Ukamilifu wa Qudra na Uwezo wa Allaah Mtukufu. Ukweli huu unawathibitishia wanadamu na viumbe vinginevyo vyote ya kuwa wakati wao wa kuondoka hapa duniani unapofika, basi wataondoka na kurejea kwa Rabi wao. Na wanadamu kwa kuwa ndio waliobeba jukumu la amana ya taklifu kwa vitendo vyao, Allaah Atawafanyia hisabu kwa matendo yao waliyoyachuma hapa duniani, mema kwa mema na mabaya kwa mabaya. Shani yao katika hilo ni shani ya wale waliowatangulia, hakuna yeyote atakayesazwa au kusahauliwa. Watu wote watasimamishwa mbele ya Mola wao Siku ya hisabu ili kila mmoja apate jaza yake. Na hili ndilo linalomwogopesha Mwislamu daima na kujikuta akijitahidi kufanya mambo mema na kujiepusha na mambo machafu ili aweze kuipata Jannah. Allaah Anatuambia:
"فَأَمَّا مَن طَغَىٰ ● وَآثَرَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ● فَإِنَّ الْجَحِيمَ هِيَ الْمَأْوَىٰ ● وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ ● وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَىٰ ● فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَىٰ"
“Basi yule aliyepindukia mipaka kuasi • Na akahiari uhai wa dunia ● Basi hakika moto uwakao vikali mno ndio makaazi yake ● Ama yule aliyekhofu kisimamo mbele ya Rabb wake, na akaikataza nafsi yake na hawaa ● Basi hakika Jannah ndio makaazi yake”. [An-Nazi’aat: 38-41]
Na kati ya dalili za Uwezo Wake Allaah Mtukufu na ujumuishi wa Fadhila Zake kwa Viumbe Vyake, ni kuwakunjulia ardhi na kuifanya kama tandiko la kupumzikia na kuweza kuendesha maisha yao bila ya matatizo yoyote. Ardhi yetu ingawa ni ya mviringo au umbo la yai, lakini hata hivyo popote anapokuwa mtu, basi hujikuta yuko kwenye ardhi iliyonyooka kabisa mbele yake inayomwezesha kugura huku na kule kwa usahali na wepesi kabisa bila ya kikwazo chochote. Ardhi hii pia imewekewa nguvu ya mvutano ili kuvikita imara vilivyoko juu yake.
Mbali ya ardhi hii, Allaah Ameikita milima na majabali ardhini ili yawe kama ni vigingi vya kuizuia ardhi isipate kuyumbayumba na kuyafanya maisha yasiwezekane, mbali na manufaa mengi yanayopatikana kutokana na milima na majabali.
Aidha, kuna bahari kubwa (oceans) na ndogo (sea) zenye manufaa makubwa kabisa kwetu kuanzia harakati za usafiri, samaki freshi, chumvi, vito vya thamani, kuwa chanzo cha mvua na mengineyo mengi tunayoyapata kutokana na bahari. Zaidi ya asilimia 75 ya uso wa ardhi imefunikwa na maji chumvi ya bahari wakati ambapo maji tamu yanayopatikana kwenye maziwa, mito, chemchemu na kadhalika, kiwango chake hakizidi zaidi ya asilimia 2.2.
Mbali ya hayo, Allaah Ameiteremsha mvua toka kwenye mawingu yaliyo juu kwa ajili ya kuotesha mimea yenye kuzalisha mazao ya aina mbalimbali kuanzia nafaka, matunda na mbogamboga, mbali na maji hayo kuwa ndio chanzo kikuu cha uhai kwa viumbe hai. Neema hii ya chakula ni moja kati ya neema kubwa kabisa ambayo inabidi tuizingatie na tuitaamuli. Yote haya yanaonyesha uwezo wa Allaah katika mchakato mzima wa kupatikana chakula hicho ambacho mtu hukitenga mezani na kukila bila kurudi nyuma na kutaamuli namna kilivyoanzia mpaka kumfikia mezani au jamvini. Allaah Anatuambia:
"فَلْيَنظُرِ الْإِنسَانُ إِلَىٰ طَعَامِهِ ● أَنَّا صَبَبْنَا الْمَاءَ صَبًّا ● ثُمَّ شَقَقْنَا الْأَرْضَ شَقًّا ● فَأَنبَتْنَا فِيهَا حَبًّا ● وَعِنَبًا وَقَضْبًا ● وَزَيْتُونًا وَنَخْلًا ● وَحَدَائِقَ غُلْبًا ● وَفَاكِهَةً وَأَبًّا ● مَّتَاعًا لَّكُمْ وَلِأَنْعَامِكُمْ"
“Basi atazame mwana Aadam chakula chake ● Kwamba Sisi Tumemimina maji kwa uneemefu ● Kisha Tukaipasua ardhi ikafunguka (kwa mimea) ● Tukaotesha humo nafaka ● Na mizabibu na mimea ya mboga (ikatwayo ikamea tena) ● Na mizaituni na mitende ● Na mabustani yaliyositawi na kusongamana ● Kwa ajili ya manufaa kwenu na kwa wanyama wenu wa mifugo.”. [‘Abasa: 25-32]
Haya yote ili Tawhiyd izame na ijikite zaidi ndani ya nyoyo zetu. Tumtakasie Yeye tu katika ibada zetu zote na tujiweke mbali kabisa na aina yoyote ya shirki ya dhahiri au ya iliyofichikana. Na kwa ajili hiyo, Allaah Anatuambia:
"فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ"
“Basi msimfanyie Allaah waliolingana naye na hali ya kuwa nyinyi mnajua”. [Al-Baqara: 22]
Kwa maana kwamba tusimfanyie Allaah mfano Wake nailhali sisi tunajua kwamba hakuna kinachofanana Naye ambacho kinastahiki kuabudiwa kama Anavyoabudiwa Yeye.
Ni lazima tujue kwamba Tawhid ndiyo msingi wa Uislamu uliyolinganiwa na Mitume wote. Wote hao wametumwa kwa ajili ya kuitangaza na kuilingania Tawhiyd. Allaah Mtukufu Anatuambia:
"وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ"
“Na Hatukutuma kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Rasuli yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: Hakika hapana mwabudiwa wa haki ila Mimi; basi Niabuduni”. [Al-Anbiyaa: 25]
Tawhiyd na ibada kwa ajili ya Allaah Peke Yake ni nyuso mbili za sarafu moja. Na kutokana na umuhimu wa Tawhiyd, tunamwona Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiilingania huko MakkaH kwa muda wa miaka 13 na wala hakuingia kwa kina kwenye masuala mengineyo isipokuwa baada ya kupata uhakika kwamba Tawhiyd ishajikita katika nyoyo za waliomwamini.
Tawhiyd ya kweli, ni ile iliyowaunganisha Waislamu wote kuwa ni wamoja kutokea Nabiy wa mwanzo hadi Nabiy wa mwisho Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Al-Imaam Ash-Shaaf’iy aliulizwa na watu: “Nini dalili ya kuwepo Muumbaji?”
Akajibu: “Ni majani ya mforosadi. Je, ladha yake, rangi yake, na harufu yake ni moja?” Wakajibu: “Ndio”. Akasema: “Majani yake huliwa na nondo akatoa hariri, huliwa na nyuki akatoa asali, huliwa na mbuzi akatoa kinyesi chake, na huliwa na digidigi akatoa miski. Je, ni nani aliyeyafanya mambo yote haya pamoja na kwamba mti ni huo huo mmoja?!” Waulizaji wakageuka mabubu na wakasilimu. Walikuwa ni watu 27.
Naye bedui mmoja aliulizwa kuhusu dalili ya kuwepo kwa Allaah Mtukufu akasema: “Kinyesi cha ngamia huonyesha kwamba kuna ngamia, kinyesi cha punda huonyesha kwamba kuna punda, na athari ya unyayo huonyesha mwendo. Basi mbingu zenye minara, ardhi zenye njia na bahari zenye mawimbi, je hayo yote hayaonyeshi kwamba kuna Muumbaji, Aliye Mjuzi, Mwenye uwezo?!”
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
05: Kuthibitisha Ujumbe Wa Rasuli Na Malipo Kwa Wenye Kuamini Na Makafiri:
Allaah Ta’alaa Anatuambia:
" وَإِن كُنتُمْ فِي رَيْبٍ مِّمَّا نَزَّلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِّن مِّثْلِهِ وَادْعُوا شُهَدَاءَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ● فَإِن لَّمْ تَفْعَلُوا وَلَن تَفْعَلُوا فَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ۖ أُعِدَّتْ لِلْكَافِرِينَ"
“Na ikiwa mko katika shaka kutokana na Tuliyoyateremsha juu ya Mja Wetu (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi leteni Suwrah mfano wake, na waiteni mashahidi wenu pasipo na Allaah mkiwa ni wakweli ● Msipofanya, na wala hamtoweza kufanya, basi ogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe, umeandaliwa kwa makafiri”. [Al-Baqarah: 23-24]
Qur-aan Tukufu ni Maneno ya Allaah Aliyoyateremsha kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kidogo kidogo kwa ajili ya kuwalingania watu, kuwafundisha Uislamu na kuwaongoza katika Njia iliyonyooka. Na kwa vile makafiri wameukanusha ukweli wa risala ya Uislamu aliyokuja nayo Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na wakadai kwamba Qur-aan hii imetungwa na mwanadamu, na kwamba Muhammad amenukulu kutoka kwa watu tena wasio Waarabu, kutokana na madai haya, Allaah Amewachalenji Akiwataka watunge wao mfano wa sura fupi zaidi iliyopo kwenye Qur-aan Tukufu. Wametakiwa hivyo, kwa kuwa herufi za Qur-aan ni herufi zao, nao ni watu mafasaha wa lugha yao kwa balagha na kwa bayaan, na wao ni mashuhuri kwa utunzi wa mashairi na uandishi wa nathari. Lakini pamoja na yote hayo, walishindwa kutunga angalau kijisura kimoja kilicho mfano wa Qur-aan Tukufu. Kushindwa huko, pamoja na uweledi wao na ubingwa wao wa kuichezea lugha yao wenyewe, kumethibitisha wazi kabisa kwamba Qur-aan si maneno ya binadamu, bali ni Maneno ya Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Aliyoyateremsha kwa Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuyafanya ni muujiza wenye kuthibitisha na kushuhudia ukweli wake. Na chalenji hiyo haikukomea kwao tu, bali imeelekezwa kwa wakanushaji wote, wasaidizi wao, wanaowaunga mkono na walio mithili yao mpaka Siku ya Qiyaamah.
Na Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Ametueleza kwamba hawatoweza kamwe kuleta mfano wa Qur-aan Tukufu, na kwa ajili hiyo, Amewataka wauogope moto na waiamini risala ya Uislamu, kwa vile moto umeandaliwa kwa kila mpingaji wa ukweli na mkanushaji wa jambo lisilokanushika. Na hao ndio makafiri katika zama zote.
فَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ۖ أُعِدَّتْ لِلْكَافِرِينَ"
“Basi ogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe, umeandaliwa kwa makafiri.”
Na hii ndio sifa ya moto ambao Allaah Anawaonya kwao makafiri hao. Moto huu unawaunguza watu na mawe, na watu ndio mafuta yake. Hali hii inabainisha ukali wa moto huo na makali ya uchungu wa adhabu yake. Ni moto wenye kuhisika machungu yake mpaka ndani ya nyoyo, wenye harufu mbaya mno ya kuchukiza, wenye moshi mzito, wenye joto kali la ajabu, na wenye kuambata miili ya waliomo humo.
Na ikiwa itaulizwa: “Watu watachomwa kwa ajili ya kulipwa matendo yao ya kuukanusha wahyi na kumpinga Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi nini hikma ya kuchomwa mawe?”.
Jawabu linasema kwamba muradi wa mawe ni masanamu yao waliyokuwa wakiyachonga na kisha kuyaabudu. Na hili linathibitishwa na Kauli Yake Ta’alaa:
"إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ"
“Hakika nyinyi na yale mnayoyaabudu badala ya Allaah ni vichochezi vya moto wa Jahannam, nyinyi mtauingia”. [Al-Anbiyaa: 98]
Moto huu uko tayari na umeshaumbwa ukiwasubiri watu wake.
Kisha baada ya Allaah Mtukufu kutuelezea kuhusu hatima ya watu hao wanaopinga risala, moja kwa moja Ameingia kutoa bishara na hatima njema kwa WachajiMungu. Anatuambia:
"وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ كُلَّمَا رُزِقُوا مِنْهَا مِن ثَمَرَةٍ رِّزْقًا ۙ قَالُوا هَـٰذَا الَّذِي رُزِقْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَأُتُوا بِهِ مُتَشَابِهًا ۖ وَلَهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ ۖ وَهُمْ فِيهَا خَالِدُونَ"
“Na wabashirie wale walioamini na wakatenda mema kwamba watapata Jannaat (bustani) zipitazo chini yake mito, kila watakaporuzukiwa humo katika matunda kuwa ni riziki husema: Haya ndiyo yale tuliyoruzukiwa kabla. Na wataletewa hali ya kuwa yanashabihiana, na watapata humo wake waliotakaswa, nao humo ni wenye kudumu”. [Al-Baqarah: 25]
Bishara maana yake ni kutoa habari ya furaha. Na katika aya hii tukufu, Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Anamwamuru Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awabashirie Waumini Jannah yenye sifa kemkem zilizotajwa. Kati ya sifa hizo ni kuwa Jannah hii inapita chini yake mito isiyokauka. Mito hii kama ilivyoelezewa kwenye aya nyingine ni ya maji safi tamu, asali safi iliyosafishwa, maziwa tamu yasiyochachuka na pombe yenye ladha tamu kabisa. Ladha ya vinywaji hivyo haina mfano, na huko vitakuwa vimetakaswa kabisa na aina yoyote ya madhara. Aidha, kuna matunda ya aina tofauti na ya kila aina yasiyokatika kwa msimu maalumu au kwa sababu maalumu, bali yako daima dom.
Mbali ya hayo, wataozeshwa mahurl ‘ayn waliotakasika na kasoro zozote walizonazo wanawake wa hapa duniani. Utwaharifu wao hapa haujaainishwa, bali unahusiana na kila utwaharifu unaohitajika kuwepo kwao. Wametwaharika kimwenendo, wametwaharika kisura, wametwaharika kimatamshi, na wametwaharika kiuoni na kimwono. Isitoshe, ni wanawake waliohirimu moja na waume zao, wenye kupendeza kwa waume zao kwa akhlaki bora kabisa, matendo bora kabisa ya kuridhiwa, ukomo wa mwisho wa hishma na adabu katika mazungumzo yao, na utwaharifu wa kutokana na hedhi, nifasi, manii, kwenda haja ndogo na kubwa, kutokwa makamasi, kutokwa mate, au kuwa na harufu mbaya. Wanawake hao hawana kasoro yoyote, bali ni wake wema wazuri kabisa wenye kuinamisha macho yao kwa waume zao tu. Wake hao si kwa ajili ya kuzaa nao, bali ni kustarehe nao milele na milele.
Haiwezekani kwa akili zetu za kibinadamu kuyajengea taswira yaliyomo humo isipokuwa kwa yale ambayo tunayo hapa duniani na Allaah Akatueleza kwamba yako mfano wake huko kama asali, matunda, mahurul ‘ayn na kadhalika. Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatueleza katika Al-Hadiyth Al-Qudsiy:
"أَعْدَدْتُ لِعِبَادِيَ الصَّالِحِينَ مَا لَا عَيْنٌ رَأَتْ وَلَا أُذُنٌ سَمِعَتْ وَلَا خَطَرَ عَلَى قَلْبِ بشر. واقرؤوا إِنْ شِئْتُمْ: (فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَا أُخْفِيَ لَهُمْ مِنْ قُرَّة أَعين"
“Nimewaandalia Waja Wangu wema mambo ambayo hakuna jicho lolote lililopata kuyaona, wala jicho lolote kupata kuyasikia, wala hata kupitikiwa kwenye moyo (akili) wa mwanadamu yeyote. Na someni mkitaka: Basi nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (4779) na Muslim (2824)]
Ni mambo ambayo pamoja na sisi kujiona kwamba tumefikia kwenye kilele cha teknolojia cha kutuwezesha kuwa na vyombo vya aina tofauti, lakini hivyo na vinginevyo vitakavyogunduliwa baadaye, haviko huko Peponi, bali kuna mengine ambayo hatuwezi kuyaelewa wala kuyafahamu.
Haya yote yanawasubiri Waumini wachaMungu, na hayo pia yanawasubiri wake zao wachaMungu. Watakutanishwa wote huko Peponi na kuwa pamoja wastarehe humo milele.
Bishara hii aliyoamriwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuitoa, inamhusu kila yule aliyetekeleza ipasavyo yale yote aliyokalifishwa nayo hapa duniani. Na hii ni ili watu wajue kwamba matendo yao husajiliwa, na kwamba ni wajibu kwao wamwamini Allaah kikweli kweli, na wakusanye kati ya kuyasadikisha aliyokuja nayo Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na matendo mema anayotakiwa mja kuyafanya. Imani ni lazima iambatane na matendo bora. Ikiwa viwili hivi vitapatikana, basi mja atastahiki kuipata Jannah hiyo yenye sifa hizi kidogo zilizogusiwa na aya hii tukufu.
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
06: Neema Za Allaah Kwa Watu: (a) Neema Ya Kwanza: Allaah Amewaleta Ulimwenguni Baada Ya Kuwa Hawapo:
Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
"كَيْفَ تَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَكُنتُمْ أَمْوَاتًا فَأَحْيَاكُمْ ۖ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ
“Vipi mnamkufuru Allaah na hali mlikuwa wafu Akakuhuisheni, kisha Atakufisheni, kisha Atakuhuisheni, kisha Kwake mtarejeshwa? [Al-Baqarah: 28]
Katika aya hii tukufu, Allaah Anauliza swali la kimshangao kuhusiana na msimamo wa makafiri kwa upande wa Tawhiyd. Swali hili linaistaajabia hali ya makafiri hawa wanaouona mbele yao ukweli na kisha kuukataa. Je, kuna yeyote aliyewahi kudai kwamba yeye kayafanya haya Aliyoyaelezea Allaah Mtukufu katika aya hii? Je, kuna yeyote mwenye uwezo wa kufanya angalau chembe tu ya haya yaliyoelezewa katika aya hii? Si haya tu, bali makafiri hawa wanaompinga Allaah, wanaishi katika neema zote ambazo Allaah Anawapa na kuwaruzuku kuanzia vyakula wanavyokula, vinywaji na mengineyo mengi ambayo wao wamekuja hapa duniani na kuyakuta yako tayari kwa ajili yao na kwa ajili ya wengineo. Je, hawafikirii haya!?
Makafiri hawa wanaomkanusha na kumkataa Allaah, walikuwa hawako katika maisha wanayoishi hivi sasa. Kisha Allaah Akawatoa hai toka matumboni mwa mama zao. Je, kwanza hawaangalii tu muujiza wa mchakato wa mlolongo wa kuumbiwa tumboni kuanzia tone la manii hadi kuwa binadamu kamili?! Ni nani awezaye kufanya haya kama si Allaah Mweza wa kila jambo?! Kisha baada ya kutoka matumboni, wakakuta maziwa ya mama yako tayari kabisa, nayo hayapatikani kama mama hana mtoto? Nani Aliyeyaweka maziwa haya tayari yakiwa na elementi zote muhimu za kumfaa mtoto mchanga? Kisha wakakua na kupata akili ya kuweza kupambanua mambo kwa akili waliyopewa na Allaah, na hatimaye wanaona kila siku watu wakifa bila ya yeyote kuweza kuyaepa mauti hayo na kuishi milele. Je, ni nani Anayeyaendesha haya yote?!
Na hakuna shaka yoyote kwamba Huyu Allaah Aliyeyafanya yote haya, Ana uwezo wa kuwarejesha tena kwenye uhai mpya Siku ya Qiyaamah ambapo wanadamu wote watasimamishwa mbele Yake kwa ajili ya kuhesabiwa matendo yao yote waliyoyafanya katika kipindi chote cha maisha yao ya hapa duniani ambapo watalipwa mema kwa mema, na mabaya kwa adhabu.
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
07: Neema Za Allaah Kwa Watu: (b) Neema Ya Pili: Allaah Amewasakharishia Vyote Vilivyoko Ardhini Ili Viwanufaishe Katika Maisha Yao:
Allaah Anatuambia:
"هُوَ الَّذِي خَلَقَ لَكُم مَّا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا"
“Yeye Ndiye Ambaye Amekuumbieni vyote vilivyomo ardhini.” [Al-Baqarah: 29]
Aya hii inatueleza ikisema enyi watu, jueni kwamba Allaah Amekukirimuni nyinyi zaidi kuliko viumbe vingine vyote, kwani Yeye Amewasakharishieni vyote vilivyoko ardhini ikiwa ni pamoja na maji, mimea, wanyama, ndege na kila kitu. Haya yote ni kwa ajili ya kutuwezesha kuishi maisha bora ya kuweza kuiamirisha ardhi na kumwabudu Allaah kwa usahali, na hatimaye kuweza kufuzu na kuipata Jannah.
Allaah Anatuambia:
"يَا أَيُّهَا النَّاسُ اذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ ۚ هَلْ مِنْ خَالِقٍ غَيْرُ اللَّـهِ يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ"
“Enyi watu! Kumbukeni Neema za Allaah kwenu. Je, kuna muumbaji yeyote badala ya Allaah Anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye. Basi wapi mnapogeuzwa?” [Faatwir: 03]
Mwanadamu akijiangalia kulinganisha na viumbe vingine, atajikuta kuwa yeye ndiye mwenye neema zaidi zisizo na hisabu. Akianzia upande wa lishe, atajikuta kwamba Allaah Amemruzuku aina tofauti tofauti za vyakula vinavyopikwa kwa miundo tofauti na visivyopikwa. Halafu vinywaji navyo, havina idadi, kati ya moto na baridi. Kisha mavazi ya malighafi tofauti, ya kazi tofauti, minasaba tofauti na kadhalika. Hali kadhalika kwa makazi yake, vipando na vyote vinavyohusiana na maisha yake. Lakini viumbe wengine kama wanyama, zaidi hula aina moja tu ya chakula kama majani au nyama na hawana kingine zaidi ya hayo.
Haya yote ni neema kubwa kwa mwanadamu zisizo na hisabu. Na kila mtu anatakikana azitumie neema hizi kwa namna inayomridhisha Allaah, kwani kila mtu bila shaka, atakuja kuulizwa kuhusiana na neema hizi Siku ya Qiyaamah. Allaah Anatuambia:
"ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ"
“Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema”. [At-Takaathur: 08]
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
08: Neema Za Allaah Kwa Watu: (c) Neema Ya Tatu:Allaah Amempa Mwanadamu Uwezo Wa Kujifunza:
Allaah Anatuambia:
"وَعَلَّمَ آدَمَ الْأَسْمَاءَ كُلَّهَا ثُمَّ عَرَضَهُمْ عَلَى الْمَلَائِكَةِ فَقَالَ أَنبِئُونِي بِأَسْمَاءِ هَـٰؤُلَاءِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ● قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ"
“Na Akamfunza Aadam majina yote (ya kila kitu), kisha Akavionesha mbele ya Malaika Akisema: Niambieni majina ya hivi mkiwa ni wakweli ● Wakasema: Utakasifu ni Wako, hatuna elimu isipokuwa Uliyotufunza, hakika Wewe Ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote”. [Al-Baqarah: 31-32]
Maudhui ya aya hizi inazungukia kuhusu uwezo alionao mwanadamu katika kujifunza, kufahamu na kudiriki mambo. Zinabainisha sifa za mwanadamu katika nyanja ya elimu ambazo Malaika hawanazo.
Tunakuta kwamba viumbe viko vya aina mbalimbali na aina nyingi, lakini vyenye akili za kuweza kuamrishwa kutenda na kutotenda ni viumbe vitatu: Malaika, majini na wanadamu. Mwanadamu ndiye aliyekirimiwa zaidi kwa kupewa uwezo mkubwa zaidi wa kufahamu, kujifunza, kutafiti, kubuni, kutengeneza, kuboresha na kadhalika. Mwanadamu umbo lake ni dogo kulinganisha na baadhi ya viumbe wengineo ambao ni wakubwa na wenye nguvu zaidi kuliko yeye. Lakini pamoja na udhaifu wake huo, Allaah Amemkirimu na kumfadhilisha kwa elimu juu ya viumbe wengineo.
Uwezo mkubwa wa mwanadamu umeonekana katika ulimwengu wetu huu. Tunashuhudia maajabu ya ujuzi na utaalamu wake katika kuyatoa madini mbalimbali toka ardhini na kuyatumia katika matumizi mbalimbali yaliyoleta mapinduzi makubwa ya kiteknolojia. Kwa utaalamu wake na ujuzi wake, ameweza hata kwenda anga za juu na kugundua yaliyokuwa hayajulikani, amezamia kwenye vina virefu vya bahari na kugundua siri za baharini na mengi mengineyo yasiyoweza kufanywa na viumbe wengineo. Na hapa mwanadamu anatakikana asisahau kwamba uwezo huu alionao, ni takrima tu toka kwa Allaah Mtukufu. Ni lazima awajibike na ile mipaka Aliyowekewa na Allaah Ta’aalaa na aendelee kujiweka chini ya utumwa wa Allaah Mtukufu Aliyemfanya yeye kuwa ni khalifa wa kuiamirisha na kuijenga ardhi hii. Na hili ndilo lililofanikishwa na mwanadamu. Ameweza kufanya mapinduzi katika nyanja zote kuanzia majenzi, kilimo, tiba, uhandisi, uchumi na kadhalika, mbali na mawasiliano ambayo kwa leo yameshuhudia mapinduzi yanayofanana na muujiza.
Malaika pamoja na utukufu wao na utwaharifu wao wa kutomwasi kwao Allaah, walivyoambiwa wamweleze Allaah majina aliyofundishwa Aadam ambayo wao walikuwa hawayajui, walijibu moja kwa moja kwamba hawajui kwa kutanguliza neno la kumtakasa Allaah wakisema: “Subhaanak”. Na hii ni kwa ajili ya kubainisha kwamba wao wana yakini ya kuwa Vitendo vya Allaah vimesimamia juu ya hikma ya juu kabisa, na kwamba wao wanakiri kwamba hawawezi kutaja majina ya vitu hivyo kwa kuwa wao hawajui isipokuwa yale tu Aliyowafundisha Allaah Mtukufu. Hapo walijua kwamba maumbile ya mwanadamu yako tayari kupokea elimu ya majina hayo na elimu nyinginezo wakati ambapo maumbile yao yako mbali kabisa na hayo. Na kwa ajili hiyo, walihitimisha kauli yao kwa kusema:
"إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ"
Kwa maana kwamba Wewe Pekee Ndiye Mjuzi kwa yaliyotuka, yenye kutuka na yatakayotuka mpaka Siku ya Qiyaamah, na Mwenye hekima kwa kila jambo.
Na hizi zilizotajwa ni baadhi ya Neema chache tu za Allaah kwetu. Neema Zake hazihesabiki wala kukokotoleka.
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
09: Kuanza Mapambano Kati Ya Aadam (‘Alayhis Salaam) Na Ibliys:
Allaah Ta’alaa Anatuambia:
"وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ وَاسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ"
“Na pale Tulipowaambia Malaika: Msujudieni Aadam. Wakasujudu isipokuwa Ibliys, alikataa na akatakabari, na akawa miongoni mwa makafiri. [Al-Baqarah: 34]
Baada ya Aadam (‘alayhis Salaam) kuweza kuyataja majina ya vitu ambavyo Allaah Ta’aalaa Alimfundisha na Malaika kushindwa kuvijua, Allaah Ta’aalaa Aliwaamrisha wamsujudie Aadam. Makusudio ya sijdah hapa ni kumpa heshima na taadhima na wala si kumsujudia sijdah ya ibada, kwa kuwa kusujudiwa kwa ibada hakuwi isipokuwa kwa Allaah Peke Yake.
Kumsujudia Allaah kumegawanyika mafungu mawili. Fungu la kwanza ni sijdah inayofanywa na wanadamu na majini waliokalifishwa. Hii inahusiana na sijdah za aina zote tunazozifanya katika swalah zetu za faradhi na za sunnah, au hata sijdah za kumshukuru Allaah kwa neema Alizotuneemesha.
Fungu la pili ni sijdah inayofanywa na viumbe vyote kwa Allaah Mtukufu. Allaah Anatuambia:
"وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَظِلَالُهُم بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ" ۩
“Na waliomo mbinguni na ardhini humsujudia Allaah Pekee wakipenda wasipende na vivuli vyao pia (vinamsujudia) asubuhi na jioni”. [Ar-Ra’ad: 15]
Na Anasema tena:
"وَالنَّجْمُ وَالشَّجَرُ يَسْجُدَانِ"
“Na nyota na miti vinasujudu”. [Ar-Rahmaan: 06]
Maulamaa wanasema kwamba Ibliys aliyetajwa hapa hayuko katika kundi la Malaika, bali ni katika majini. Wametolea dalili kwa haya yafuatayo:
(a) Ni kutokana na Neno Lake Ta’alaa:
"وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ"
“Na pindi Tulipowaambia Malaika: Msujudieni Aadam. Wakasujudu isipokuwa Ibliys, alikuwa miongoni mwa majini”. [Al-Kahf: 50]
(b) Ibliys aliasi amri ya Allaah, na Malaika hawaasi kabisa Amri ya Allaah. Allaah Anatuambia:
"لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ"
“Hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa”. [At-Tahriym: 06]
(c) Ibliys alitakabari, na Malaika hawatakaburi.
(d) Malaika wameumbwa kutokana na nuru wakati Ibliys ameumbwa kutokana na moto. Na hili linabainishwa na Kauli Yake Ta’alaa:
"قَالَ مَا مَنَعَكَ أَلَّا تَسْجُدَ إِذْ أَمَرْتُكَ ۖ قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ"
“(Allaah) Akasema: Nini kilichokuzuia usisujudu Nilipokuamrisha? Akasema (Ibliys): Mimi ni mbora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, na yeye Umemuumba kwa udongo”. [Al-A’araaf: 12]
Lakini Maulamaa wengine wanaona kwamba Ibliys ni katika Malaika kwa kuwa Allaah Alipowaamuru kumsujudia Aadam, Alielekeza amri kwa wote Akiwaambia: Msujudieni Aadam. Wanasema kwamba hakuna dalili ya nguvu ya kutofautisha kati ya Malaika na majini. Linaloonekana ni kwamba majini ni katika jamii ya Malaika, na mashetani ni katika jamii ya majini. Allaah Mtukufu Amelitumia jina la "الْجِنَّةُ"(majini) kwa maana ya Malaika katika Kauli Yake Aliposema:
"وَجَعَلُوا بَيْنَهُ وَبَيْنَ الْجِنَّةِ نَسَبًا ۚ وَلَقَدْ عَلِمَتِ الْجِنَّةُ إِنَّهُمْ لَمُحْضَرُونَ"
“Na wakafanya baina Yake (Allaah) na baina ya Malaika unasaba. Na hali Malaika wamekwishajua kwamba wao (washirikina) bila shaka watahudhurishwa (kuadhibiwa)”. [As-Swaaffaat: 158]
Aidha, Amelitumia jina "الْجِنَّةُ"(majini) Akikusudia mashetani katika Suwrat An Naas Aliposema:
"مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ"
“Miongoni mwa (mashetani) majini na watu”. [An-Naas: 06]
Kiujumla, tunasema kwamba hayo yote ni majina. Majina haya yako katika ulimwengu wa ghaibu ambao sisi hatuujui ukweli wake wowote. Ni vizuri tutosheke na yaliyoelezewa bila kupekua kitu ambacho hatuwezi kukifikia undani wake.
Kiufupi, tunasema kwamba kwa kukataa amri hii ya Allaah, na Ibliys kujiona kwamba yeye ni bora kuliko Aadam kwa kuwa ameumbwa kwa moto na Aadam kaumbwa na udongo, Allaah Alimlaani na Akamweka mbali na Rehma Zake na akawa ni katika makafiri. Na hapo ndipo uadui ukaanza kutokota ndani ya nafsi yake, lakini Alimwomba Allaah Mtukufu Ampe umri wa kuweza kuishi mpaka Siku ya Qiyaamah ili aweze kuwapoteza wana wa Aadam, na Allaah Akamkubalia. Na hapa mtu anaweza kusema kwa nini Allaah Alimkubalia aje atupoteze na kutushawishi kufanya maasia?
Jibu ni kwamba kila jambo lina hikma yake. Na hikma ya hilo ni kwamba hakuna mafanikio yanayopatikana bila ya taabu. Wanadamu tumeumbiwa matamanio ya mambo mbalimbali. Kila mwanadamu inabidi ayadhibiti matamanio yake ili aweze kufanikisha malengo yake. Mfungaji kwa mfano, ili aweze kuikamilisha saumu yake, inabidi awe na subira ya mwisho kabisa ya kuacha matamanio yake yote kwa ajili ya kuitii amri ya Allaah Mtukufu.
Hivyo basi, ikiwa Mwislamu ataweza kupambana na ushawishi wa shetani, akakabiliana na uchochezi wake wa kumpambia maasi, basi bila shaka huyo atakuwa amefaulu mafanikio makubwa. Pepo kama tunavyojua ina mambo ambayo hakuna jicho lililoyaona, wala sikio lililoyasikia wala hata pia kumpitikia mwanadamu katika akili yake. Hayo yaliyomo humo hayawezi kupatikana kwa usahali, bali ni lazima yakabiliwe na kila aina ya ugumu. Na ugumu huo uko katika mikono ya shetani na Ibliys.
Dunia yetu kama tunavyoiona, inazidi kusonga mbele kutokana na matatizo yanayotukabili tukayatafutia ufumbuzi na kutokana na changamoto tunazopambana nazo tukazishinda. Bila kuwepo matatizo, hakutakuweko maendeleo, na bila kuwepo changamoto, ladha ya maisha itakosekana.
Hivyo basi, kuwepo kwa Ibliys wa kutushawishi, na sisi kuweza kukabiliana naye, kutatuwezesha kuwa na mafanikio makubwa kabisa huko akhera.
Mapambano kati ya mwanadamu na shetani yalianzia Peponi wakati alipokataa shetani kuitii amri ya Mola wake ya kumsujudia Aadam. Allaah Akamfukuza toka peponi na Akamlaani. Na hapo Akaapa mbele ya Allaah kwamba atampoteza Aadam pamoja na wanawe kwa nguvu na mbinu zake zote. Allaah Mtukufu Anatuambia:
"قَالَ فَبِعِزَّتِكَ لَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ"
“(Ibliys) akasema: Naapa kwa Utukufu Wako, bila shaka nitawapotosha wote ● Isipokuwa waja Wako miongoni mwao waliokhitariwa kwa ikhlasi zao”. [Swaad: 82-83]
Raundi ya kwanza ya upotezaji huo ilikuwa ni kwa wazazi wetu wawili. Shetani alifanikiwa kuwapoteza na hivyo kusababisha kutolewa Peponi na kuteremshwa hapa ardhini ili Aadam pamoja na wanawe waendelee kukabiliana na njama za shetani za kuwapotosha. Shetani huyu ana silaha mbalimbali za kufanikisha vita vyake na mwanadamu. Kati ya silaha hizo ni pamoja na:
1- Uwezo wa kumpambia mwanadamu maasia mpaka akajisahau na kujikuta ameshatumbukia kwenye shimo la maasia. Allaah Anasema:
"قَالَ رَبِّ بِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأُزَيِّنَنَّ لَهُمْ فِي الْأَرْضِ وَلَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ"
“(Ibliys) akasema: Rabb wangu! Kwa vile Umenihukumia kupotoka, basi bila shaka nitawapambia (maasi) katika ardhi na nitawapotoa wote”. [Al-Hijri: 39]
Anasema tena:
"تَاللَّـهِ لَقَدْ أَرْسَلْنَا إِلَىٰ أُمَمٍ مِّن قَبْلِكَ فَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَهُوَ وَلِيُّهُمُ الْيَوْمَ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ"
“Ta-Allaahi, kwa yakini Tulipeleka (Rusuli) kwa nyumati za kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), na shaytwaan akawapambia vitendo vyao. Na yeye leo ni rafiki mwandani wao, nao watapata adhabu iumizayo”. [An-Nahl: 63]
2- Uwongo na hadaa. Uwongo huu ulionekana pale alipoweza kuwashawishi Aadam na Hawaa kula mti waliokatazwa. Aliwahadaa na kuwaambia kwamba ikiwa wataula mti huo, basi watakuwa ni malaika wawili au watakuwa ni katika watu watakaoishi milele. Mbali ya hivyo, aliwaapia ya kwamba anayoyasema ni kweli tupu. Allaah Anatuambia:
"فَوَسْوَسَ لَهُمَا الشَّيْطَانُ لِيُبْدِيَ لَهُمَا مَا وُورِيَ عَنْهُمَا مِن سَوْآتِهِمَا وَقَالَ مَا نَهَاكُمَا رَبُّكُمَا عَنْ هَـٰذِهِ الشَّجَرَةِ إِلَّا أَن تَكُونَا مَلَكَيْنِ أَوْ تَكُونَا مِنَ الْخَالِدِينَ ● وَقَاسَمَهُمَا إِنِّي لَكُمَا لَمِنَ النَّاصِحِينَ"
“Basi shaytwaan (naye ni Ibliys) akawatia wasiwasi ili awafichulie sehemu zao za siri zilizositiriwa. Na akasema: Rabb wenu Hakukukatazeni huu mti isipokuwa msije kuwa Malaika wawili au kuwa miongoni mwa wenye kudumu milele ● Naye akawaapia: Hakika mimi ni katika wenye kukunasihini kidhati. [Al-A’araaf: 20-21]
Na Anasema tena Allaah Mtukufu:
" الشَّيْطَانُ يَعِدُكُمُ الْفَقْرَ وَيَأْمُرُكُم بِالْفَحْشَاءِ"
“Shaytwaan anakutishieni ufukara na anakuamrisheni machafu.” [Al-Baqarah: 268]
3- Yeye anatuona wakati sisi hatumwoni, naye tunaye miilini mwetu ndani ya damu zetu. Allaah Anatuambia:
"إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ"
“Hakika yeye (Ibliys) anakuoneni, yeye na kabila lake (la mashaytwaan) na hali ya kuwa nyinyi hamuwaoni”. [Al-A’araaf: 27]
Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"إِنَّ الشَّيْطَانَ يَجْرِي مِنِ ابْنِ آدَمَ مَجْرَى الدَّمِ ".
“Hakika shetani anatembea ndani ya (mwili) wa mwanadamu kama inavyotembea damu yake”. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (2038) na Muslim (2175)]
Kwa maana anaweza kucheza na akili ya binadamu, moyo wake na hisia zake kumpeleka kwenye mabaya kwa wepesi mno mtu akijiachaia ovyo.
Na lengo kuu la mwisho la shetani kwa mwanadamu, ni kuwafikisha wote kwenye moto wa Jahannamu. Allaah Anatuambia:
"وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُضِلَّهُمْ ضَلَالًا بَعِيدًا"
“Na shaytwaan anataka awapoteze upotofu wa mbali”. [An-Nisaa: 60]
Na Anatuambia tena:
"إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمْ عَدُوٌّ فَاتَّخِذُوهُ عَدُوًّا ۚ إِنَّمَا يَدْعُو حِزْبَهُ لِيَكُونُوا مِنْ أَصْحَابِ السَّعِيرِ"
“ Hakika shaytwaan kwenu ni adui, basi mfanyeni kuwa ni adui. Hakika anaitia kikosi chake ili wawe miongoni mwa watu wa moto uliowashwa vikali mno”. [Faatwir: 06]
Na ikiwa shetani hakufanikiwa katika lengo lake la kuwapoteza watu au kuwakufurisha, basi hakati tamaa, bali huendelea hivyo hivyo tu hata kama anaona hakuna matunda ya kazi yake.
Katika maisha yote ya mwanadamu, shetani humganda mwanadamu katika hali zake zote huku akiwa na mbinu mbalimbali za kumpotosha. Humjilia katika kila kitu chake kinachomuhusu. Humjia katika swalah yake ili amshawishi asiweze kufanya khushuu. Wakati mwingine mtu hujikuta amemaliza swalah yake na wala hajui ni rakaa ngapi kaswali au ni sura zipi kazisoma. Shetani pia hula pamoja naye kama hakusema Bismillaah, na hata wakati wa tendo la ndoa huwepo, na anaweza kushiriki ikiwa Mwislamu hakumdhukuru Allaah kabla ya kuanza. Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametutaka tuwalinde watoto wetu wanaotarajiwa kutokana na tendo la ndoa kwa kusoma baadhi ya nyiradi ili watoto wetu waweze kusalimika na vitimbi vya shetani huyu. Na hata kabla ya kulala, imesuniwa kusoma nyiradi maalumu alizotufundisha Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya kujilinda na shari kiumbe huyu na balaa zingine.
Mgando wa shetani kwa mwanadamu huendelea hata katika dakika za mwisho za mwanadamu za kuondoka hapa duniani. Na kwa ajili hiyo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha dua ya kujikinga naye katika dakika hizo ngumu za kutoka roho. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaomba kinga kwa Allaah akisema:
"وَأَعُوذُ بِكَ أَنْ يَتَخَبَّطَنِي الشَّيْطَانُ عِنْدَ الْمَوْتِ"
“Na najilinda Kwako shetani asije kunizuga zuga wakati wa kufa”. [An-Nasaaiy 5531) na Abu Daawuwd (1552)]
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
10: Kukubaliwa Toba Ya Aadam (‘Alayhis Salaam):
Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
" فَتَلَقَّىٰ آدَمُ مِن رَّبِّهِ كَلِمَاتٍ فَتَابَ عَلَيْهِ ۚ إِنَّهُ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ "
“Kisha Aadam akapokea maneno kutoka kwa Rabb wake; na (Rabb wake) Akapokea tawbah yake. Hakika Yeye Ndiye Mwingi wa Kupokea tawbah, Mwenye Kurehemu. [Al-Baqarah: 37]
Aadam (‘Alayhis Salaam) baada ya kughilibiwa na shetani na kumwasi Mola wake na kisha kuamuriwa wote wateremke ardhini, Aadam (‘Alayhis Salaam) alipokea maneno toka kwa Mola wake, na hapo hapo moja kwa moja akaomba toba na msamaha kwa Mola wake, Naye moja kwa moja Akaikubali. Na kwa vile kufanya makosa ni jambo lisiloepukika kutokana na shetani kumwandama mwanadamu katika hali zake zote, Allaah Ametuwekea wazi milango ya toba ili tuweze kutubia wakati wowote tutakapoteleza na kufanya madhambi. Na fursa hii ndiyo aliyoitumia Aadam (‘Alayhis Salaam) mara moja bila kuchelewa, na hili ni somo muhimu sana kwetu kwamba tunapoteleza na kufanya madhambi, basi tutubie hapo hapo bila kuchelewa.
Mufassiruuna wamekhitalifiana kuhusiana na maneno hayo ambayo Aadam (‘Alayhis Salaam) aliyapokea toka kwa Mola wake. Baadhi wanasema ni yale ambayo Allaah Alimfunulia kwa njia ya wahyi na Akamfundisha kwayo njia ya kutubia na kurejea Kwake. Na maneno haya kwa mujibu wa ilivyo mashuhuri kwa yaliyopokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas ni Kauli Yake Ta’alaa:
"قَالَا رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ "
“Wakasema: Rabb wetu! Tumedhulumu nafsi zetu, na basi Usipotughufuria na Ukaturehemu, bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika”. [Al-A’araaf: 23]
Ama Mujaahid, yeye anasema kwamba maneno hayo ni:
"سُـبْحانَكَ اللّهُـمَّ، لا إِلهَ إِلَّا أَنْتَ، إِنّيْ ظَلَـمْتُ نَفْسِيْ فَاغْـفِرْ لِي، فَإِنَّهُ لا يَغْفِـرُ الذُّنوبَ إِلاّ أَنْـتَ"
“Nakutakasa (na kila sifa ya upungufu) Ewe Allaah! Hakuna apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Wewe tu. Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu, basi Nighufirie, kwani hakika hakuna aghufiriaye madhambi isipokuwa Wewe tu”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2602) na tamshi ni lake, At-Tiemidhiy (3446) na Ahmad (753)]
Wengine wanasema kwamba makusudio ya maneno ni kulia na kutokwa machozi, kuhisi haya, kujuta, kuomba du’aa, kuomba maghfira, kuhuzunika na kadhalika, kwani haya yote yanakusanya maneno.
Baadhi ya Masalaf waliulizwa linalotakiwa kwa mtendaji dhambi aseme wakajibu kwamba atasema yale waliyoyasema wazazi wetu wawili (Aadam na Hawwaa):
(a)
"رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ "
“Rabb wetu! Tumedhulumu nafsi zetu, na basi Usipotughufuria na Ukaturehemu, bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika”. [Al-A’araaf: 23]
(b) Yale aliyoyasema Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam):
"قَالَ رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي"
“Akasema: Rabb wangu! Hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu”. [Al-Qaswas: 16]
(c) Yale aliyoyasema Nabiy Yuwnus (‘Alayhis Salaam):
"لا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ"
“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Subhaanak! Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu”. [Al-Anbiyaa: 87]
(d) Ni kusema:
"سُبحانَك اللَّهُمَّ وبحَمْدِك أشهَدُ أنْ لا إلهَ إلَّا أنت، أستَغفِرُك وأتوبُ إليك، عَمِلتُ سُوءًا وظلَمْتُ نفسي، فاغفِرْ لي؛ إنَّه لا يَغفِرُ الذُّنوبَ إلَّا أنت"
“Ninakutakasa (na kila upungufu) Ewe Allaah pamoja na kukuhimidi. Hapana wa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Wewe tu. Ninakuomba maghfirah na ninatubia Kwako. Nimefanya mabaya na nimeidhulumu nafsi yangu, basi Nighufurie, kwani hakika hakuna yeyote mwenye kusamehe madhambi isipokuwa Wewe tu”. [Imechakatwa na An-Nasaaiy (10188), Al-Haakim (1972) na At-Twabaraaniy (4/278)]
Na kama tujuavyo, toba ni kwanza kulijua dhambi alilolitenda mtu na madhara yake, kisha kujuta kwa kulifanya, halafu kuweka nia ya kweli ya kutolirudia, na mwisho kujiweka mbali na visababisho vyake. Na kama kuna haki ya mtu inabidi irejeshwe.
Na bila shaka tutalahidhi kwamba katika aya tukufu, Allaah Anamalizia kwa kusema kwamba Yeye Ni Mwingi wa Kupokea toba na Mwingi wa rehma. Hapa bila shaka kunakusudiwa maana nyingi:
1- Kutilia nguvu matumaini na matarajio ya wafanyao dhambi, na kuiunga mioyo ya wakosefu kwa kuwathibitishia kwamba Allaah Yuko tayari kuwapokea kama watarejea Kwake wakati wowote ule.
2- Kwamba hata kama makosa yatakariri na kuwa mengi, Allaah Yu tayari kuikubali toba hata kama mja atakariri kosa mara kwa mara. Muhimu ni mtu aweke nia ya kweli ya kutorejea kosa.
3- Kwamba Allaah Huzikubali toba za watubiaji vyovyote iwavyo idadi yao.
4- Kwamba fadhila za Allaah wigo wake ni mpana mno kwa kuzikubali toba za waja na kuwa Mrehemevu kwao.
Kwa haya yote, tunasema kwamba aya hii tukufu inaashiria juu ya kima muhimu ambacho Waislamu wote wanakihitajia, nacho ni toba na kurejea kwa Allaah Mtukufu. Binadamu kama tujuavyo ni dhaifu na wakati mwingi hulemewa na matamanio na hawaa ya nafsi mbali na kushawishiwa na shetani. Na kwa ajili hiyo, Allaah Amemwekea njia ya kurejea Kwake ambayo ni toba.
Kwa kuwepo toba, matumaini hujadidika na mwanadamu huwa na uwezo wa kujitakasa na makosa yoyote aliyoyafanya. Toba huudhaminia umma mkondo sahihi wa kupita, kwa kuwa toba huliweka bayana kosa na humrejesha mkosaji kwenye mwelekeo sahihi, mbali na kudhamini haki za watu. Na hii yote huwafanya watu kuishi kwa furaha chini ya kivuli cha Uislamu.
Na cha muhimu zaidi kwa Waislamu ni kuusiana kufanya mema na kuomba toba mara tu baada ya kufanya kosa bila kuchelewa chelewa, na kujiweka mbali na kukata tamaa na kupoteza matumaini. Ni lazima tujue kwamba Allaah Hufurahia toba zenu na Hutupenda kwa kutubia na kurejea Kwake. Anatuambia:
"إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ"
“Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha.” [Al-Baqarah: 222]
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
11: Maumbile Ya Mwanadamu:
Kutokana na kisa cha baba yetu Aadam kama kilivyoelezewa na Qur-aan Tukufu ni kuwa mwanadamu kiasili ameumbwa kutokana na udongo na mpulizo uliotokana na Roho ya Allaah. Hivyo basi, mwanadamu ni mzaliwa wa ardhi, mlelekaji katika ardhi, mkaazi wa ardhi na mwenye kuishi juu ya ardhi. Anafanya kazi na shughuli zake zote juu ya ardhi, anahangaika huku na kule, anazitumia rasilmali za ardhi kwa ajili ya maslaha yake ya kuiamirisha ardhi na amepewa uwezo wa kuvitawala viumbe vinginevyo.
Mwanadamu huyu sura yake ilifinyangwa kwa udongo na Malaika, kisha ukaja mpulizo toka kwa Allaah, na udongo huo ukawa ni mtu mwenye uwezo wa kufikiri, kuzungumza, kujifunza, kutafiti, kuutaamuli ulimwengu na kuujenga hatua kwa hatua.
Huyu ndiye mwanadamu mwenye kiwiliwili cha udongo, akili ya kiroho, mwenye utambuzi, mwenye nishati na nguvu za mwili, na mwenye khiyari ya kujichagulia mambo. Na kwa ajili hiyo, amekuwa ni “Mukallaf”, kwa maana amebebeshwa na Allaah maamrisho ya kuyafuata na makatazo ya kuyaepuka kupitia kwa Mitume Wake Aliowatuma kuwafikishai watu Ujumbe Wake.
Mwanadamu huyu amekirimiwa na Mola wake kwa kuumbwa kutokana na elementi zile zile za ardhi anayoishi, akawekewa sheria zinazoendana na maumbile yake, na akakatazwa yale yote yatakayomweka mbali na kheri na usalama. Na lau kama mwanadamu angeliumbwa kwa udongo wa kutoka sehemu nyingine, basi asingeliweza kuishi katika ardhi hii na kutulia au kunufaika na rasilmali zake zilizopo. Kuumbwa kwa udongo hakumaanishi kumtweza mwanadamu au kumshusha thamani, bali udongo huu ni tunu ya kipekee isiyo na mfano wake. Kutokana na udongo huu, vimeundika vito na madini za thamani kubwa kati ya lulu, marijani, dhahabu, silva na mengineyo. Na vyote alivyoviunda mtu na kuvitengeneza, vimetoka kwenye udongo. Hata mazao ya vyakula, maji anayokunywa, moto anaoutumia ukitokana na gesi au mkaa au mada nyingine yoyote, vyote hivyo vimetoka ardhini.
Mbali ya hayo, mwanadamu huyu amepewa uwezo wa kujiweka mwenyewe pale atakapo. Akitaka anaweza kuwa ni kito cha thamani kubwa, na kama atataka, atakuwa ni udongo wa tope uliovunda, au jiwe gumu. Allaah Subhaanahuu wa Ta’aalaa Anatuambia:
"لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ ● ثُمَّ رَدَدْنَاهُ أَسْفَلَ سَافِلِينَ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَلَهُمْ أَجْرٌ غَيْرُ مَمْنُونٍ"
“Kwa yakini Tumemuumba mwana-Aadam katika umbile bora kabisa ● Kisha Tukamrudisha chini kabisa ya walio chini ● Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema; hao watapata ujira usiokatika”. [At-Tiyn: 4-6]
Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"تَجِدُونَ النَّاسَ مَعَادِنَ، خِيَارُهُمْ فِي الْجَاهِلِيَّةِ خِيَارُهُمْ فِي الإِسْلاَمِ إِذَا فَقِهُوا"
“Mtawakuta watu wana asili tofauti (kama yalivyo madini). Waliokuwa wema wao enzi ya kabla ya Uislamu, wanakuwa ni wema wao baada ya kuingia kwenye Uislamu kama watafahamu vyema (Uislamu)”. [Imechakatwa na Al-Bukhaariy (3493) na Muslim (2526)]
Hadiyth hii ina maana kwamba watu wanatofautiana katika “silica” (ghariza) na maumbile yao kama yanavyotofautiana madini yaliyoko ardhini, na kwamba kujikita makhitalifiano ndani ya nafsi, ni kama kujikita mizizi ya madini ndani ya ardhi. Kama ilivyo kwa madini kuwa yapo ambayo sifa zake hazibadiliki, ni hivyo hivyo kwamba sifa ya utukufu wa mtu haibadiliki katika dhati yake. Anayekuwa mtukufu kwenye ujahili kisha akasilimu na kuingia kwenye Uislamu, basi utukufu na wema wake utaendelea katika Uislamu zaidi na zaidi.
Na tokea dakika za mwanzo, Allaah Subhaanahuu wa Ta’alaa kabla ya kumuumba Aadam (‘Alayhis Salaam), Aliwaambia Malaika ya kwamba Yeye Atamweka katika ardhi mwandamizi (Khalifa) kwa ajili ya kuja kuiamirisha ardhi hii, kuijenga na kuistawisha. Na kwa hilo, yakadhihiri majaliwa ya Allaah katika kumkirimu mwanadamu kwa kumpa ukhalifa huo, au kumwakilisha katika kufichua majaliwa ya Muumbaji katika kubuni vitu, kutengeneza, kuchanganua, kupandikiza, kuhamisha "modulation", kugeuza na kufichua yaliyomo juu na ndani ya ardhi kati ya nishati, hazina, malighafi, na mengineyo. bNa hii yote ni kwa ajili ya kuweza kutekeleza kazi kubwa aliyonayo mwanadamu juu ya uso huu wa ardhi.
Hakika nafasi au roli ya mwanadamu kama Alivyomkadiria Allaah Mtukufu, ndio roli ya kwanza. Yeye ndiye mwenye kugeuza na kubadili maumbo ya ardhi kwa shughuli zake za kilimo, majenzi, miundo mbinu na kadhalika. Mtizamo wa Qur-aan unamfanya mwanadamu huyu kwa ukhalifa wake ardhini, kuwa ni kitenda kazi muhimu katika mfumo wa ulimwengu huu. Ukhalifa wake unahusiana na mafungamano mbalimbali na mbingu, upepo, mvua, nyota na sayari mbalimbali. Na ili mwanadamu aweze kuendeshana na yote yenye kumzunguka kwa ajili ya kufanikisha lengo la kuweza kuishi kama inavyotakikana, Allaah Amempa uwezo wa kujifunza na kufahamu siri ya mambo mbalimbali yaliyopo juu ya ardhi, ndani ya ardhi, kwenye vina vya bahari na hata kwenye anga za juu. Baba yetu Aadam alijifundisha majina ya vitu vyote, na Allaah aliidhihirisha sifa hii ya kujifunza mbele ya Malaika ili wahakikishe Hikma ya Allaah katika mapendeleo Yake na Uwezo Wake, na ili hilo liwe pia ni jaribio la kiutendaji kwa wana wa Adamu walibebe baada yake katika maisha yao huku wakiwa wamejivika silaha ya elimu, ufahamu, udadisi, utafiti na upekuzi katika nyanja zote za maisha. Na hili bila shaka linaonekana wazi kabisa katika ardhi yetu hii. Hakuna kiumbe chochote kinachoishi katika ardhi hii kilichofanya hata asilimia moja tu ya aliyoyafanya mwanadamu.
Na kwa ajili ya kuweza kuishi maisha shwari na tulivu ya kumwezesha kuisimamia roli yake na nafasi yake kwa mujibu wa akili na nguvu alizopewa mwanadamu, Allaah Amemwekea mwanadamu huyu mipaka ambayo inabidi aishi ndani yake. Ikiwa mwanadamu huyu atajiona kwamba ana uwezo kuliko ule aliopewa na Allaah, au nguvu za juu zaidi kuliko zile alizoumbiwa nazo, basi bila shaka atagongana na kitu asichoweza kukikabili.
Mwanadamu huyu ameumbwa akiwa na uwezo wa kufikiri, kuangalia na kuchagua. Ni kiumbe aliyepewa uhuru wa kujichagulia yale anayoyaona yananasibiana naye kwa fikra zake na kwa akili yake. Ana uhuru wa kufanya ibada au kutofanya ibada lakini baada ya Allaah kumtumia Mitume wa kumwonyesha njia ya haki na njia isiyo ya haki kisha uhuru akaachiliwa yeye mwenyewe ajichagulie alitakalo. Anapondokea kulielekea la kheri kwa dhati yake, au hulitamani la shari kwa irada yake, na yote mawili yana tija yake. Aadam na mkewe walilipa thamani ya matashi yao yaliyowapelekea kuula mti, wakatolewa Peponi na kuteremshwa ardhini. Hivyo basi, maasia ya kwanza ya mwanadamu yalikuwa ni ya kitendo cha uhuru wa kujichagulia. Na kwa ajili hiyo, Allaah Mtukufu Aliikubali toba ya Aadam na Akamghufiria kama ilivyotueleza Qur-aan Tukufu.
Mbali ya yote hayo, mwanadamu ameumbwa akiwa na maadui kadhaa mbele yake ili apate changamoto ya kuweza kujiimarisha na kujiwekea kinga dhidi ya maadui hao. Kuwepo kwa changamoto katika maisha ya mwanadamu, kumemfanya afanikishe maendeleo yote tunayoyashuhudia kwa hivi sasa na kwa siku za usoni.
Adui yake wa mwanzo ni nafsi yake mwenyewe yenye kumwamrisha mabaya. Nafsi hii ndiyo iliyomwezesha Ibliys kumpoteza na kumpotoa Aadam na Hawwaa, wakaula mti kwa ajili ya kupata ufalme na umilele kama walivyolaghaiwa na Ibliys.
Adui yake wa pili ni marafiki na masahibu wabaya. Hawa hawampelekei isipokuwa kwenye madhara na machafu.
Adui wa tatu ni Ibliys na askari wake. Huyu ndiye adui hatari zaidi kwa kuwa anaishi pamoja na mawazo yanayompitikia mwanadamu katika nafsi yake, anapita ndani ya damu ya mwanadamu, anajiingiza kwenye mahangaiko ya ndani na ghariza za kimatamanio, na huyapa nguvu matumaini yake ambayo aghalabu huwa ni matumaini hewa.
Allaah kwa Rehma Zake, Amemjulisha mwanadamu kinga zote za kujihami na maadui hao kupitia Mitume na Vitabu walivyokuja navyo. Kinga hizi ni pamoja na kujiepusha na maadui hao, kuchagua marafiki wema, kuamiliana na ndugu wa kheri, kusuhubiana na watu wema wachaMungu na kuomba hifadhi kwa Allaah kutokana na shetani aliyewekwa mbali na rehma za Allaah.
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
12: Mwanadamu Alipitikiwa Na Kitambo Bila Kuwa Anajulikana:
Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
"هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورًا ● إِنَّا خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن نُّطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَّبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعًا بَصِيرًا"
“Kwa hakika kilimpitia mwana-Aadam kipindi fulani katika dahari, hakuwa kitu kinachotajwa • Hakika Sisi Tumemuumba mwana-Aadam kutokana na tone la manii iliyochanganyika ili Tumjaribu, Tukamfanya mwenye kusikia na mwenye kuona”. [Al-Insaan: 1-2]
Hebu rudi nyuma kupitia tarehe yako au siku yako au mwaka wako wa kuzaliwa, halafu jiulize: Je ulikuwepo? Je, ulikuwa unatajika? Je, kulikuweko yeyote anayekujua? Je, kulikuweko yeyote anayekufikiria? Bila shaka jibu litakuwa hapana, kwa maana kwamba wewe ni kiumbe mpya; hukuwepo kabla, uwepo wako haukuwepo, utajo wako haukuwepo, jina lako halikuwepo, hukuwa ukifikiriwa na yeyote, hakuna akujuaye, wala yeyote akutajaye na wala hakukuwepo na yeyote ajuaye kuja kwako isipokuwa Allaah Mtukufu. Halafu jiulize, Huyu Aliyekupatisha ukapatikana baada ya kuwa hujulikani, Hawezi kukurejesha tena kwenye uhai baada ya kufa na kutowekea mchangani?
Na hapa inabidi kila mtu akumbuke kwamba kuna maagano aliyoyakiri mbele ya Allaah hapo kabla akiwa katika ulimwengu wa kiroho.
Katika Hadiyth iliyopokelewa na Ibn ‘Abbaas na kufanyiwa ikhraaj na Ahmad, An-Nasaaiy, Ibn Jariyj na Al-Haakim, Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"إنَّ اللَّهَ تعالى أخذَ الميثاقَ من ظَهرِ آدمَ عليهِ السَّلامُ بنعمانَ يومَ عرفةَ فأخرجَ من صلبِه كلَّ ذرِّيَّةٍ ذرأَها فنثرَها بينَ يديه ثمَّ كلَّمَهم قُبُلًا قال تعالى: أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ؟ قَالُوا بَلَى شَهِدْنَا أَنْ تَقُولُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَذَا غَافِلِينَ أَوْ تَقُولُوا إِنَّمَا أَشْرَكَ آبَاؤُنَا مِنْ قَبْلُ وَكُنَّا ذُرِّيَّةً، أَفَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ الْمُبْطِلُونَ "
“Hakika Allaah Alichukua maagano katika mgongo wa Aadam huko Nu’umaan Siku ya Arafah. Akatoa toka mgongoni mwake watoto wote Aliowaumba, kisha Akawatawanya mbele Yake. Halafu Akazungumza nao moja kwa moja mbele yao Akiwauliza: Je, Mimi Si Rabbi wenu? Wakasema: Kwani! Tumeshuhudia. Msije mkasema Siku ya Kiyama sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo. Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walio shirikisha kabla yetu, na sisi ni dhuriya zao tu baada yao. Basi Utatuangamiza kwa sababu ya waliyo yafanya wapotovu?!” [Imechakatwa na Ahmad (2455), An-Nasaaiy (11191) na Al-Haakim (75)]
Hadiyth hii inatiliwa nguvu na Kauli Yake Ta'alaa:
"وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ ۖ قَالُوا بَلَىٰ ۛ شَهِدْنَا ۛ أَن تَقُولُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَـٰذَا غَافِلِينَ • أَوْ تَقُولُوا إِنَّمَا أَشْرَكَ آبَاؤُنَا مِن قَبْلُ وَكُنَّا ذُرِّيَّةً مِّن بَعْدِهِمْ ۖ أَفَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ الْمُبْطِلُونَ"
“Na pindi Rabb wako Alipowaleta wana wa Aadam kutoka migongoni mwao kizazi chao, Akawashuhudisha juu ya nafsi zao (Akiwauliza): Je, Mimi Siye Rabb wenu? Wakasema: Ndio bila shaka, tumeshuhudia! (Allaah Akawaambia): Msije kusema Siku ya Qiyaamah: Hakika sisi tulikuwa tumeghafilika nayo haya • Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walioshirikisha kabla, nasi tulikuwa kizazi baada yao. Basi Utatuangamiza kwa yale waliyoyafanya wabatilifu? [Al-A’araaf: 172-173]
Pia inatiliwa nguvu na Hadiyth hii nyingine iliyopokelewa na Anas bin Maalik ambapo Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"يقالُ للرجلِ من أهلِ النارِ يومَ القيامَةِ: أرأَيْتَ لو كان لكَ ما على الأرضِ من شيءٍ أكنتَ مفتديًا بِه؟ فيقولُ: نعم؟ فيقولُ اللهُ: كذبْتَ قدْ أردْتُّ منكَ أهونَ من ذلِكَ، قد أخذتُ عليكَ في ظهرِ آدمَ أن لَّا تُشرِكَ بي شيئًا فأبيتَ إلَّا أنْ تُشْرِكَ"
“Mtu katika watu wa motoni ataambiwa Siku ya Qiyaamah: Unasemaje kama ungelikuwa na chochote katika vilivyoko juu ya ardhi, je ungeliweza kukitolea fidia? Atasema: Ndio. Na Allaah Azza wa Jalla Atamwambia: Umesema uongo. Mimi Nilikutaka jambo dogo kuliko hilo. Nilichukua ahadi kwako katika mgongo wa Aadam kwamba usinishirikishe Mimi na chochote, nawe ukakataa, ukashikilia ushirikina”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (3334) na Muslim (2805)]
Hadiyth hii tukufu inaonyesha kwamba watoto wote wa Aadam, (yaani sisi wanadamu), wote walikuwa katika mgongo wake wakati ule wa kuumbwa yeye kati ya mabilioni ya wanadamu walioishi na wakafa, na sisi tulio hai kwa sasa tunaojaza pembe zote za dunia kwa zaidi ya watu bilioni saba, na kwa wale ambao bado hawajazaliwa na ambao wanazaliwa kila sekunde mpaka siku ya Qiyaamah. Wote hawa, (mimi na wewe), tulikuwa kwenye mgongo wa baba yetu Aadam wakati ule alipoumbwa. Kisha Allaah Mtukufu Alitutoa toka kwenye mgongo wa Aadam, halafu Akatushuhudilisha kwamba Yeye Ndiye Allaah, Muumbaji wa kila kitu, Mmoja Aliye Mpweke, Mwenye kulisimamia kila jambo, Asiye na mshirika katika Ufalme Wake, wala mpinzani katika Madaraka Yake, Asiye na mshabaha na chochote katika viumbe Vyake, na Asiye hitajia mke au mtoto, kwa kuwa hayo ni katika sifa za viumbe Vyake.
Na baada ya wanadamu wote kukiri hayo yote wakiwa katika ulimwengu wa roho, Malaika walisema: "Sisi Tumeshuhudia hayo, msije mkasema Siku ya Qiyaamah sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo. Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walio shirikisha kabla yetu, na sisi ni dhuriya zao tu baada yao, basi Utatuangamiza kwa sababu ya waliyo yafanya wapotovu!?"
Anayejua ukweli na uhakika wa Uungu, bila shaka anajua kwamba Allaah Mtukufu ni Mweza wa kila kitu na Anapolitaka jambo lolote, basi Huliambia kuwa, nalo huwa hapo hapo.
Hivyo basi, haya yote yalitimu huko nyuma katika ulimwengu wa kiroho, kisha wanadamu wakaanza kuzaliwa kwa mujibu wa utaratibu Alioupanga Allaah wa kudhihiri kila mmoja katika ulimwengu wetu huu. Tuko sisi tunaoishi katika enzi hii ya teknolojia, wako walioishi kabla yetu na kuna wengineo mabilioni kwa mabilioni ambao wako njiani kuja kuishi baada yetu sisi. Sisi Tulikuwa hatujulikani na sasa tumejulikana na hata watoto tunaowatarajia kuwazaa mpaka sasa pia bado hawajulikani, na sisi hatuwajui. Mababu zetu hawakujua lolote kuhusiana nasi, nasi hatujui lolote kuhusiana na vizazi vijavyo. Ndio hapa Allaah Anapotuambia katika aya ya mada yetu ya leo:
"هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورً
“Kwa hakika kilimpitia mwana-Aadam kipindi fulani katika dahari, hakuwa kitu kinachotajwa”. [Al-Insaan: 01]
Kila mmoja kati yetu ana tarehe yake ya kuzaliwa, na baadhi yetu husherehekea kila mwaka sikukuu ya kuzaliwa. Lakini kabla ya tarehe hii, hakuwa mtu ni mwenye kutajika, hakuna amjuaye, hakuna amdhukuruye, hana uwepo wowote, hana utajo, hana jina, hana utambulisho na hana chochote kijulikanacho kuhusu yeye. Kisha baada ya hapo, mtu huzaliwa akatoka ndani ya tumbo la mama yake, akaanza kunyonyeshwa maziwa ya mama, akiogeshwa na kuvalishwa nepi, huku akiwa hajui chochote katika ulimwengu unaomzunguka. Kisha kidogo kidogo anaanza kuvaana na mazingira yanayomzunguka akili yake ikiendelea kukua pamoja na mwili wake hadi anapokuwa kijana anayeweza kujitegemea kwa mambo yake yote.
Kisha baada ya hapo, anakuwa ni mtu mwenye shani kubwa katika jamii. Anaweza kuwa na shahada ya uzamivu au ya uzamili. Anaweza kuwa na cheo kikubwa kabisa katika jamii akawa Mfalme, rais, waziri, daktari, mhandisi na kadhalika. Haya yote anayafikia huku akisahau kwamba yeye alipitikiwa na kitambo cha zama nailhali hakuwa ni mtu mwenye kujulikana au kutajika kabisa.
Watu wakubwa duniani, walikuwa ni watoto wadogo, na wakati walipokuwa wadogo, hakukuwepo yeyote anayewajali au kuwatia akilini. Walikuwa wakinyonya maziwa ya mama zao, wakibebwa, wakilishwa, wakilalishwa, wakichungwa wasije kudhurika na vitu wasivyovijua hatari yake, wakijiendea haja wenyewe, wakisafishwa na kuvalishwa.
Lakini hawa wote, baada ya kufikia hapo walipo; wakiwa na madaraka makubwa, wakiwa na utajiri mkubwa, na wakiwa na ushawishi mkubwa, wameisahau kabisa safari yao yote ya utotoni na kuwakalia juu Waja wanyonge wa Allaah. Watu hawa utakuta wakiwanyanyasa watu, wakiwanyonya nguvu zao, wakiwabeza, wakiwadhulumu na mengi mengineyo mabaya. Baadhi yao hujenga ngome za utukufu wao kwa jasho la wengine, wengine hujenga utajiri wao kwa kuwadhulumu watu, na wengine hujichumia utajiri kwa kuwaua watu. Na haya bila shaka yako wazi kabisa kwetu sote. Na hii si tu kuwa iko kwa wakubwa, bali hata kwa wadogo pindi wanapopata nafasi ya kuwaumiza wengine kwa ajili ya maslaha yao.
Huyu ndiye mwanadamu ambaye hakuwa hapo kabla ni mwenye kujulikana. Amemsahau Allaah Aliyemuumba, amemsahau Allaah Aliyemtia sura Aliyeitaka Yeye akiwa tumboni mwa mama yake, amemsahau Allaah Aliyemtoa kwa usahali kabisa toka ndani ya tumbo hilo wakati wa kuzaliwa.
"ثُمَّ السَّبِيلَ يَسَّرَهُ"
“Kisha Akamuwepesishia njia”. [‘Abasa: 20]
Halafu anamsahau Allaah Aliyempa ilhamu ya kunyonya maziwa ya mama hata bila ya kuyaona akiwa kitoto kichanga ambacho hata macho hakijaweza kufungua. Hata baada ya kufungua macho, hata katika kiza kinene, mtoto hulijua titi la mama yake. Mtoto huyu hakufundishwa na yeyote namna ya kunyonya, na wala hakusoma kitabu chochote cha kumpa maelekezo. Utamwona akiweka midomo yake miwili kwenye titi la mama, halafu huikaza vizuri midomo yake, kisha huvuta hewa na kupata maziwa freshi. Hii ni neema kubwa ya Allaah Aliyetupumzisha na kazi ya kuwafunza watoto namna ya kunyonya maziwa ya mama.
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
13: Dhana Ya Kusimamisha Swalah:
Allaah Ta’aalaa Anasema:
"وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ"
“Na simamisheni Swalaah”. [Al-Baqarah: 43]
Kusimamisha swalah maana yake ni kuitekeleza katika wakati wake maalumu pamoja na kuhifadhi nguzo zake, wajibu zake, masharti yake pamoja na unyenyekevu na khushuu ndani yake. Khushuu pamoja na haya tuliyoyataja, ni sababu ya kumfanya Mwislamu afanikiwe katika maisha yake ya hapa duniani na huko akhera. Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
"قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ • الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ"
“Kwa yakini wamefaulu Waumini ● Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea”. [Al-Muuminuwna: 1-2]
Maulamaa wamejaribu kuelezea njia kadhaa za kufanikisha suala la khushuu katika swalah. Njia hizo zimefikia takriban 33, nasi tutajaribu kuzitaja baadhi yake tu hapa ili Mwislamu aweze kuzizingatia na kupata mafanikio hayo yaliyoelezewa na Allaah Mtukufu katika aayah hii. Njia hizi ni:
1- Kujiandaa na swalah na kujiweka tayari nayo. Huku kunaanzia tokea pale Mwislamu anapomjibisha mwadhini adhana na kisha kuomba du’aa ya baada ya adhana. Kabla ya adhana inakuwa pia ni vizuri zaidi kuanza maandalizi ili kudhamini kuipata safu ya kwanza yenye fadhila nyingi sana. Kisha baada ya hapo kuchukua wudhuu wake kama inavyotakikana kisheria. Halafu kuvaa kivazi kizuri kabisa ili kuonyesha heshima kwa Allaah, kwani Mwislamu anakuwa kana kwamba anakwenda kumtembelea Allaah katika Nyumba Yake. Halafu hatimaye kuelekea Masjid katika hali ya utulivu na utuvu, kwani katika hatua zote hizi, Mwislamu anazingatiwa kwamba ashaingia ndani ya wigo wa swalah.
2- Mwenye kuswali kujua na kutambua kwamba Allaah Anamjibisha katika swalah wakati anaposoma Suwrat Al-Faatihah.
Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Al-Hadiyth Al-Qudsiy:
"إنَّ اللهَ تعالى يقولُ: قَسَّمْتُ الصَّلاةَ بَيْني وَبَيْنَ عَبْدِي نِصْفَيْنِ ، نِصْفُهَا لِيْ وَنِصْفُها لِعَبْدِيْ ولِعَبْدِيْ ما سألَ ، فَإذا قَالَ : الحَمْدُ للهِ ربِّ العَالمين، قالَ اللهُ : حمِدني عَبْدِي ، وإذا قالَ : الرَّحمنِ الرَّحيمِ ، قالَ اللهُ : أَثْنَى عَلَيَّ عَبْدِيْ ، وإذَا قَالَ : مَالِكِ يومِ الدِّينِ، قال اللهُ عَزَّ وَجَلَّ : مجَّدَنِي عَبْدِي، وإذا قالَ : إياكَ نعبدُ وإياكَ نستعينُ، قال : فَهذِهَ الآيةُ بَيْنِي وَبَيْن عبْدِي نِصْفَيْنِ وَلِعَبْدِي مَا سَألَ ، فإذا قالَ : اهدنا الصراطَ المستقيمَ صراطَ الذين أنعمتَ عليهم غيرِ المغضوبِ عليهم ولا الضالينَ، قال : فهؤلاءِ لعبدي ولعبدي ما سألَ"
“Hakika Allaah Ta’aalaa Anasema: Nimeigawanya Suwrat Al-Faatihah kati Yangu na Mja Wangu nusu mbili, nusu moja ni Yangu na nusu ya pili ni ya Mja Wangu, na Mja Wangu Nitampa analoliomba.
(Mja) anaposema: “Al-Hamdulil Laahi Rabbil 'aalamiyna”, Allaah Husema: Mja Wangu Amenihimidi. Anaposema: “Ar Rahmaanir Rahiym”, Allaah Husema: Mja Wangu Amenisifu. Anaposema: “Maaliki yawmid Diyn”, Allaah ‘Azza wa Jalla Husema: Mja Wangu Amenitukuza utukuzo mkubwa. Anaposema: “Iyyaaka na-'abudu wa iyyaaka nasta'iyn”, Allaah Husema: Aayah hii ni nusu mbili kati Yangu na Mja Wangu, na Mja Wangu Nitamjibu atakaloliomba. Anaposema: “Ihdinas swiraatwal mustaqiym, swiraatwal ladhiyna An'amta 'alayhim ghayril maghdhwuubi 'alayhim waladh dhwaalliyna”, Allaah Husema: Haya ni ya Mja Wangu (aliyoyaomba), na Mja Wangu atajibiwa aliyoyaomba”. [Hadiyth Swahiyh. Chanzo: Majmuw’ul Fataawaa (7/14)]
Ni nafasi pekee anayoipata Muislamu ya kujibishwa na Mola wake kila siku mara 17 kwenye swalaah za faradhi na nyinginezo za sunnah.
Ni nafasi pekee ya kumsifu Allaah, kumtukuza na kumwomba mubashara Atuthibitishe katika Njia Yake iliyonyooka ya wale Aliyowaneemesha kati ya Manabii, Swalihina, Waliosadikisha Imani yao kikweli. Tukijua hili, basi swalah itakuwa daima ndio kimbilio letu la kufarijika mbele ya Allaah. Ndio maana Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam alikuwa akimwambia Bilaal:
"يا بلالُ، أَقِمِ الصَّلاةَ، أَرِحْنا بها"
“Ee Bilaal! Kimu swalah, tupe faraja za nyoyo kwayo”.
3- Utulivu wa viungo na moyo katika swalah. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati alipokuwa anaswali, alikuwa akitulia mpaka kila kiungo kinarejea mahala pake. Baadhi ya wenye kuswali utawalahidhi kwamba hawatulii kabisa baada ya kuingia kwenye swalaah; mara kajikuna kichwa, mara kakamata ndevu, mara kanyoosha nguo yake huku macho yake yakizunguka hapa na pale. Hii si tabia nzuri kabisa.
4- Kukumbuka mauti wakati wa swalah kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:
"اذْكُرِ المَوْتَ في صَلاتِكَ، فإنَّ الرَّجُلَ إذَا ذَكَرَ المَوْتَ في صَلاتِهِ لحَرَيٌّ أَنْ يُحْسِنَ صَلاتَه، وَصَلِّ صَلاةَ رَجُلٍ لا يَظُنُّ أَنْ يُصلِّيَ صلاةً غيرَها، وَإِيَّاك وكلُّ أمرٍ يُعتذرُ منه"
“Yakumbuke mauti katika swalah yako, kwani ikiwa mtu atayakumbuka mauti katika swalah yake, basi ni hakika kwamba ataiswali vyema swalah yake. Swali swalah ya mtu ambaye hana uhakika ya kwamba ataswali swalah nyingine tena. Na jiepushe na kila jambo utakalokuja kuomba usamehewe”. [Imesimuliwa na Anas bin Maalik na iko kwenye As-Silsilat As-Swahiyhah (2839). Isnaad yake ni Hasan. Imechakatwa na Al-Bayhaqiy katika Az-Zuhdul Kabiyr (527) na Ad-Daylamiy katika Al-Firdaws (1755)].
5- Kuzizingatia aya zinazosomwa na adhkari nyinginezo za swalah na kuchangamkiana nazo. Mazingatio ya aya hayaji ila kwa kuelewa maana yake, na hili ni kwa wale wenye kufahamu lugha ya Kiarabu. Ama kwa wale wasio fahamu lugha ya Kiarabu, hawa itawatosha kumsikiliza imamu kisomo chake kwa umakini, kwani usikilizaji huo utawafanya Qur-aan iwaathiri na kuwapa msisimko.
6- Kusoma Qur-aan kwa tartiyl na kwa sauti nzuri. Allaah Mtukufu Anatuambia:
"وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا"
“Na soma Qur-aan kwa tartiyl; kisomo cha utaratibu upasao, kuitamka vizuri na kutaamali”. [Al-Muzzammil: 04]
Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"زيِّنوا القرآنَ بِأصْواتِكم، فإنَّ الصَّوتَ الحَسَنَ يزيدُ القرآنَ حُسنًا"
“Ipambeni Qur-aan kwa sauti zenu, kwani sauti nzuri huizidishia Qur-aan uzuri”. [Imechakatwa na Al-Bukhaariy (7544), Abu Daawuwd (1468), An-Nasaaiy (1015), Ibn Maajah (1342), Ahmad (18517) na Al-Haakim (2125)]
7- Kutuliza jicho mahala pa kusujudia bila kugeuka huku wala kule. Hii husaidia kwa kiasi kikubwa katika kuleta khushuu katika swalah.
8- Kusoma "Isti’aadhah" (أعوذ بالله من الشيطان الرجيم) kwa ajili ya kumweka mbali shetani na swalah. Kama tujuavyo, shetani ndiye adui wetu mkubwa. Shetani hujaribu kwa njia zote kumshawishi Mwislamu asiende kwenye swalah. Anaposhindwa hilo, basi humwandama ndani ya swalah yake kwa kumshawishi hadi kumtoa nje kabisa ya khushuu na khudhuu, Mwislamu akatoka kwenye swalah na maksi ndogo kabisa.
9- Kujitahidi kuomba du’aa na hususan wakati wa kusujudu. Wakati huu mja anakuwa karibu zaidi na Allaah kuliko kipindi kingine chochote. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia:
"أَقْرَبُ مَا يَكُونُ الْعَبْدُ مِنْ رَبِّهِ وَهُوَ سَاجِدٌ فَأَكثِرُوا الدُّعَاءَ"
“Wakati ambao mja anakuwa karibu zaidi na Mola wake, ni pale anapokuwa amesujudu. Basi kithirisheni dua”. [Hadiyth Swahiyh. Swahiyh Muslim (482)]
Haya ndiyo muhimu yanayosaidia kumfanya mtu aswali kwa khushuu. Mengineyo ya haraka haraka ni pamoja na kutoswali na nguo yenye madoido ya kuvutia, kutoswali wakati chakula kiko tayari mezani, kutoswali wakati mtu amebanwa na haja ndogo au kubwa, kutonyanyua macho juu, kutotema mate mbele bali pembeni, kutoswali nyuma ya mtu aliyelala au anayezungumza na kutogeukageuka katika swalah.
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
14: Dhana Ya Zaka:
Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
"وَآتُوا الزَّكَاةَ ۚ"
“Na toeni zaka”. [Al-Baqarah: 110]
Zaka kama tujuavyo ndiyo anwani ya kijamii kwa imani ya mtu, ni madh-hari ya kumshukuru Allaah kwa neema Zake, na ni kiunganishi muhimu kati ya watu.
Agizo la kutoa zaka limekuja likikutanishwa na agizo la kusimamisha swalah kwa ajili ya kuzisafisha nafusi, kuzitakasa mali na kumtwaharisha mwanadamu, kwa kuwa kila kimoja kinakikamilisha kingine, na kukiacha kimoja, hukidhoofisha kingine.
Yeyote mwenye kuisimamisha swalah kama inavyotakikana, hapo ataikuta nafsi yake inasafika, anajikuta akiukumbuka wajibu wa kutoa zaka na kusaidia katika njia za kheri na kutoa msaada wowote unaohitajika kwa wahitajio.
Hivyo basi, ikiwa Waislamu wote watasimamisha swalah tano kama inavyotakikana, na wakatoa zaka kwa mpangilio mzuri, basi bila shaka wataishi maisha bora kabisa, wakijawa na utukuko wa kumwabudu Allaah, wakiwa wanyoofu katika matendo yao yote, wakijenga maadili bora kabisa ya Kiislamu, wakiunyanyua umma na kuwa ni wenye furaha hapa duniani na huko akhera.
Hakika Mwislamu mwenye kuishi katika hali ya kumwabudu Allaah wakati wote, anajijua kwamba yeye hakuumbwa kwa ajili ya nafsi yake pekee, bali ameumbwa ili awe ni kiungo hai nufaishi katika jamii itakayowageuza watu kuwa ni umma wenye kuishi ndani ya msafara mmoja wa haki, na wenye kumtii Allaah Ta’aalaa wakati wote.
Zaka bila shaka ni utakaso wa kinafsi na kisaikolojia. Tajiri hali yake ya kisaikolojia inakuwa katika hali nzuri mno anapohisi kwamba yeye ni sababu ya furaha ya maelfu ya familia. Ni wakati ule anapoiona mali yake imekuwa ni furaha kwenye nyuso za watu, anapoona mali yake imevisha watu na kusitiri miili yao, anapoona mali yake imeyashibisha matumbo yenye njaa, anapoona mali yake imekuwa ni nyumba za kuwahifadhi wanafunzi wanaosoma Qur-aan Tukufu, anapoona mali yake imesomesha vijana wahitimu wa fani mbalimbali za kusukuma mbele gurudumu la maendeleo na kusukuma mbele Uislamu na dunia kiujumla na kadhalika. Hii ndio amali bora zaidi ya kuingiza furaha kwenye moyo wa mwanadamu. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"أحَبُّ النَّاسِ إلى اللهِ أنْفَعُهُمْ لِلنَّاسِ، وَأَحَبُّ الأعْمَالِ إلى اللهِ عزَّ وجلَّ سُرُورٌ يدْخِلُهُ عَلَى مُسْلِمٍ"
“Mtu anayependeka zaidi kwa Allaah ni yule mwenye kuwanufaisha zaidi watu, na amali inayopendwa zaidi kwa Allaah ‘Azza wa Jalla ni furaha anayoiingiza mtu kwa Muislamu”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na At-Twabaraaniy (6026). Iko katika Silsilat As-Swahiyhah (906)]
Hivyo basi, Mwislamu anatakiwa asije kufanya ubakhili wa mali yake akashindwa kuja kutoa zakatul maali au kutoa sadaka. Allaah Ametoa onyo kali kwa wale wote wenye kufanya ubakhili hata kufikia kushindwa kutoa zaka. Anatuambia:
"وَلَا تَحْسَبَنَّ اللَّـهَ غَافِلًا عَمَّا يَعْمَلُ الظَّالِمُونَ ۚ إِنَّمَا يُؤَخِّرُهُمْ لِيَوْمٍ تَشْخَصُ فِيهِ الْأَبْصَارُ"
“Na wala usidhanie kabisa kwamba Allaah Ameghafilika na yale wanayoyatenda madhalimu. Hakika Anawaakhirisha kwa ajili ya Siku ambayo macho yatakodoka (kwa kiwewe)”. [Ibraahiym: 42]
Maana ya aya hii tukufu ni kwamba Allaah ‘Azza wa Jalla Ndiye Ampaye Amtakaye, na Ndiye Amnyimae Amtakaye, na hii yote ni kwa Hikma Yake ya juu kabisa. Basi yule ambaye Allaah Atampa mali hapa duniani ambayo mali hiyo ni katika Fadhila Zake Allaah, basi asifanye ubakhili na choyo akaizuia na kuwanyima wengineo. Ubakhili uliokusudiwa katika aya hii tukufu ni kutoitoa zaka stahiki kwa wenye kustahiki kwa mujibu wa walivyotajwa kwenye Qur-aan Tukufu. Ubakhili huu wa kuzuia zaka, si kheri kwa mzuiaji kama anavyodhani mwenyewe, bali ni shari kwake, kwa kuwa Allaah Ta’aalaa Amekufanya kuyatoa mali kwa ajili Yake kuwa ndiyo sababu ya kuzidi mali na kuongezeka kinyume na ubakhili ambao hatima yake ni kuteketea mali na kuangamia hapa duniani, na huko akhera kuna adhabu chungu inayomsubiri. Adhabu hiyo kama ilivyoelezewa na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ni mali yake kugeuka na kuwa joka kubwa lenye upara na ndimi mbili kali litakalomwadhibu Siku ya Qiyaamah. Aidha, mali za wasio toa zaka, zitageuka na kuwa moto utakaozichoma nyuso zao, mbavu zao na migongo yao. Hayo yote ni kutokana na ubakhili wa kutoa zaka ya mali ambayo mtu hakuichuma kwa akili yake wala kwa jasho lake, bali kwa tawfiyq kutoka kwa Allaah Mtukufu.
Toka kwa Abu Hurayrah kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَنْ آتَاهُ اللَّهُ مَالاً فَلَمْ يُؤَدِّ زَكَاتَهُ، مُثِّلَ لَهُ يوم القيامة شُجَاعًا أَقْرَعَ، لَهُ زَبِيبَتَانِ يُطَوَّقُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، ثم يَأْخُذُ بِلِهْزِمَتَيْهِ ـ يَعْنِي شِدْقَيْهِ ـ ثم يَقُولُ أَنَا كنزك أنا مَالُكَ . ثُمَّ تَلاَ هَذِهِ الآيَةَ : وَلاَ يَحْسِبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّهُ مِنْ فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُم ۖ ... بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ"
“Mtu ambaye Allaah Amempa mali naye asiitolee Zakaah yake, basi ataundiwa kwa mali hiyo Siku ya Qiyaamah mfano wa joka lenye kichwa cheupe (upara), lina mabaka meusi juu ya macho yake, litamviringa Siku ya Qiyaamah. Kisha litambana kwa taya zake mbili liseme: Mimi ni hazina ya mali yako, mimi mali yako. Kisha akasoma Aayah hii:
"وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُم ۖ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ ۖ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُوا بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ وَلِلَّـهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ"
“Wala wasidhani kabisa wale wanaofanya ubakhili kwa yale Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kwamba hayo ni khayr kwao, bali ni shari kwao. Watafungwa kongwa yale waliyoyafanyia ubakhili Siku ya Qiyaamah. Na ni Wake Allaah Pekee urithi wa mbingu na ardhi. Na Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika”. [Al-Bukhaariy (1403)]
“Toka kwa Abu Hurayrah amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Hakuna yeyote mwenye hazina ya mali ambayo haitolei Zakaah, isipokuwa atapashiwa moto kwenye moto wa Jahannam, kisha ifanywe vipande vipana [vya metali], achomwe navyo mbavu zake na kipaji chake mpaka pale Allaah Atakapohukumu kati ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini. Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni. Na hakuna yeyote mwenye kumiliki ngamia na asiwatolee Zakaah yake, isipokuwa atatandazwa kifudifudi mbele yao kwenye ardhi pana tambarare, wakiwa wakubwa kama walivyokuwa, watamkanyaga, kila wanapomaliza kumkanyaga wa mwisho wao, wa mwanzo wao watarejeshwa kumkanyaga tena mpaka Allaah Atakapohukumu baina ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini. Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni. Na hakuna yeyote mwenye kumiliki mbuzi na kondoo na asiwatolee Zakaah yake, isipokuwa atatandazwa kifudifudi mbele yao kwenye ardhi pana tambarare, wakiwa wakubwa kama walivyokuwa, watamkanyaga kwa kwato zao, na watampiga kwa pembe zao, hakuna kati yao mwenye pembe zilizopinda wala asiye na pembe, kila wanapomaliza kumkanyaga wa mwisho wao, wa mwanzo wao watarejeshwa kumkanyaga tena mpaka Allaah Atakapohukumu kati ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini katika mnayohesabu. Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni…”. [Muslim (987) na Abu Daawuwd (1642)]
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
15: Dhana Ya Hijja: (a) Mwitiko Wa Nguvu Wa Waumini Na Shauku Kubwa Ya Kufanikisha ‘Amali Hii:
Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Ameifanya Nyumba Takatifu ya Makkah kuwa ni mahala pa kujikurubisha Kwake. Ameifanya Nyumba hii kuwa ni mahala pa kumwabudu Yeye na mtu kujipa nafasi na wasaa wa kumwabudu Yeye tu. Na kwa ajili hiyo, imekuwa ni katika hikma ya amali ya hijja kwamba Allaah Mtukufu Amewaamuru Waumini waiendee Nyumba hiyo wakiacha nyuma yao nyumba zao, wake zao, watoto wao, mali zao, kazi zao, starehe zao, burudani zao na kila kile kinachowashughulisha katika dunia yao, ili dunia hii isiwe ni kikwazo kati ya mja na Mola wake.
Allaah Mtukufu Amewaamuru watu wamwendee Yeye na wajiweke mbali na dunia yao. Na wanapofika kwenye Ardhi Takatifu na kuanza amali za hiJja, hapo Anawaharamishia baadhi ya mambo ambayo kwa kawaida ni halali kwao kama kuvaa nguo iliyoshonwa kwa wanaume. Shuka mbili wanazovaa wanaume, huwasahaulisha mavazi yao mazuri ya mitindo tofauti wanayovaa, viatu vyao vya aina tofauti na mapambo mengineyo huku mkusanyiko wao wa pamoja toka pande zote za dunia, ukiwakumbusha saa ya kufufuliwa na saa ya kukusanywa viumbe vyote vya kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Katika amali hii ya hijja, Allaah Amewaamuru Waislamu wafunge safari toka makwao hadi Makka na waache kila kitu chao. Na hapa bila shaka Anataka kuwakumbusha kwamba kuna kitu kiitwacho kuiacha dunia kupitia mauti. Hijja hii inakuwa ni kama ukumbusho wa siku ya mwisho inayomsubiri kila mwanadamu ambapo ataondoka hapa duniani na kuelekea akhera kwa Mola wake Mtukufu. Na hili halina shaka kwa yeyote.
Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Ameifanya Nyumba Hii kuwa ni mahala patakatifu na Akaiita "Haram" kwa kuwa ni haramu kufanya katika Nyumba hii jambo lolote lenye kumuudhi kiumbe. Kuna Miezi Mitakatifu ambapo inakuwa ni kosa kubwa sana kutenda madhambi katika miezi hiyo, kama ambavyo imekatazwa kupigana ndani ya Msikiti Mtakatifu wa Makka, kulipiza kisasi, kufanya uadui au kuua kiwindwa jambo ambalo sehemu nyingine ni halali. Yeyote mwenye kuingia kwenye Nyumba hii basi huyo yuko salama hata kama inabidi auawe. Na hii yote inaonyesha utukufu wa sehemu hiyo. Hapo ni mahala pa ibada tu, mahala pa kutaabudia, mahala pa kuitakasa nafsi, mahala pa kujiweka mbali na dunia, migogoro yake, matatizo yake na mivutano yake. Ni mahala pa kuwakumbusha watu Siku ya Mwisho, na kuwakumbusha kwamba watahamia na kugura kwa Mola wao. Na kwa ajili hiyo, inabidi kila mwenye kuweko kwenye Nyumba hiyo, autumie wakati wake wote kwa ajili ya kulifanya kila lile litakalomkurubisha kwa Allaah Mtukufu.
Na Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa kutokana na hekima Zake, Ameijaalia Al-Ka’aba kuwa katika bonde lisilo na mmea wowote, wala mvua wala hali nzuri ya hewa. Amefanya hivi ili asiikusudie sehemu hiyo isipokuwa mwenye nia ya kuhiji tu. Na lau kama ingelikuwa kwenye bonde lenye mimea, hali nzuri ya hewa, maziwa, milima ya kijani, mito inayobubujika na kadhalika, basi wangeliiendea Mahujaji na watalii. Lakini kwa mujibu wa hali yake hiyo, haiendewi isipokuwa na mwenye kuhiji pekee ingawa joto la Makka ni kali pamoja na msongamano mkubwa wa Mahujaji toka pande zote za dunia. Na la kushangaza, pamoja na joto kali au msongamano mkubwa au tabu nyinginezo wanazokabiliana nazo mahujaji, utawasikia baadhi yao wakisema: "Sikuonja katika maisha yangu neema na furaha kama ya hijja hii". Kana kwamba kuna mmetuko wa utwaharifu kwa Mahujaji hawa toka kwa Allaah Mtukufu, kwani Mahujaji hawa ni Wageni Wake. Mwislamu anapoingia kwenye msikiti wowote kwa ajili ya ibada katika nchi yake, hawezi kupata hisia na furaha kama hii ingawa Allaah Humkirimu mwisho wa kumkirimu anapokuwa ndani ya msikiti.
Ikiwa mambo yenyewe yako hivi ikiwa utaingia kwenye msikiti wowote nchini kwako kwa ajili ya kufanya ibada, basi hali itakuwaje ikiwa utatafuta pesa za halali, kisha ukafunga safari hadi Makkah ukiacha mambo yako yote nyuma kwa ajili ya kuitikia wito wa Mola wako wa kutekeleza faradhi ya hijja?!! Kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema katika Hadiyth yake tukufu:
"لَا تُشَدُّ اَلرِّحَالُ إِلَّا إِلَى ثَلَاثَةِ مَسَاجِدَ: اَلْمَسْجِدِ اَلْحَرَامِ، وَمَسْجِدِي هَذَا، وَالْمَسْجِدِ اَلْأَقْصَى "
“Mtu asifunge safari isipokuwa kuiendea Misikiti Mitatu: Al-Masjidul Haraam (Makkah), Masjid yangu hii (Madiynah), na Al-Masjidul Al-Aqswaa (Palestina) ”. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (1197) na Muslim (2/975)]
Misikiti hii Mitatu ina hadhi yake maalumu mbele ya Allaah Mtukufu.
Bila shaka haiingii akilini Allaah kukuita wewe toka nchini mwako ufunge safari yako yote toka popote pale ulipo hapa duniani ukaacha mambo yako yote, kisha ukaenda halafu Allaah Asikukikirmu inavyopasa kukirimiwa. Hili bila shaka ni katika mambo yasiyowezekanika. Na kwa ajili hiyo, Allaah Anatuambia:
"لِيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ""
“Ili washuhudie manufaa yao”.
Maulamaa katika kuifasiri aya hii wanasema kwamba kuna manufaa ya kiroho na kuna manufaa ya kidunia. Hijja pamoja na kuwa kwake ibada tukufu, vile vile huwafanya Waislamu kukutana toka pande zote za dunia wakiwa na lugha tofauti, rangi tofauti, desturi tofauti, uraia tofauti na kadhalika, lakini wote wanajikuta kwamba wao ni umma mmoja wakiunganishwa na Uislamu pamoja na tofauti zao hizo. Hilo bila shaka huwazidishia imani zaidi, mahaba zaidi, mshikamano zaidi na mapenzi zaidi kati yao. Na hapa ndipo linapothibitika neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"تَرَى المُؤْمِنِينَ في تَراحُمِهِمْ وتَوادِّهِمْ وتَعاطُفِهِمْ، كَمَثَلِ الجَسَدِ، إذا اشْتَكَى عُضْوًا تَداعَى له سائِرُ جَسَدِهِ بالسَّهَرِ والحُمَّى"
“Utawaona Waumini katika kuoneana kwao huruma, kupendana kwao, na kufanyiana kwao upole, ni kama kiwiliwili kimoja. Ikiwa kiungo chochote kitashtakia (adha), basi mwili mzima utaitana kwa ajili ya homa na kukesha”. [Hadiyth Swahiyh. Muslim (2586) na Al-Bayhaqiy (91)]
Mwislamu kwa ibada hii, huondoka na hisia na kumbukumbu ambayo itakuwa ni vigumu mno kufutika katika akili yake mpaka siku yake ya mwisho ya kuondoka hapa duniani. Mbali na manufaa hayo, wafanyabiashara pia hutumia nafasi hii kukaguakagua bei za vitu na aina ya biashara ambayo wanaweza kuchukua na faida nyinginezo kemkem zinazopatikana kwa amali hii ya hijja.
Mwislamu aliyehiji hija ya kisawasawa, utamwona anatamani ahiji kila mwaka kutokana na athari njema iliyomganda katika nafsi yake. Anatamani lau kama masiku ya umri wake wote yangelikuwa ni hija. Huyu ndiye yule aliyeutumia wakati wake wote vyema wakati akiwa katika pilikapilika za hijja kama Anavyosema Allaah:
"لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ"
“Ili wahudhurie kupata manufaa yao, na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu”. [Al-Hajji 28]
Mwenye kuhiji katika masiku haya machache ya kufanya amali za hija hujaribu kwa nguvu zake zote kumdhukuru Allaah Mtukufu wakati wote anapokuwa katika pilikapilika za amali za hijja. Anapolala na kuamka, hujikuta akimdhukuru Allaah, akikutana na wenzake hujikuta akimdhukuru Allaah.
Hijja yote kwake inakuwa ni dhikri, hijja yote kwake ni dua, hija yote kwake ni swalah na maombi, na hijja yote ni mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Allaah na Waja Wake.
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
16: Dhana Ya Hijja: (b) Manufaa Makuu Ya Hijja:
Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anatuambia:
"لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ ۖ فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ"
“Ili wahudhurie kupata manufaa yao, na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu kupitia yale Aliyowaruzuku kati ya wanyama wenye miguu minne wa mifugo. Basi kuleni sehemu yake, na lisheni mwenye shida fakiri”. [Al-Hajj: 28]
Hapa Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anawaasa Waislamu wamdhukuru kwa wingi sana Yeye katika masiku maalumu kutokana na neema kubwa Aliyowapa kutoka kwa wanyama wa kufugwa; ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo. Wanyama hawa kwetu ni neema kubwa sana ambayo Allaah Ametupa. Allaah Ametuwezesha kupata manufaa kutoka kwa wanyama hawa kama nyama, maziwa, ngozi na kadhalika, kutokana na kuwapa hulka na tabia ya sisi kuweza kuwadhibiti bila ya matatizo yoyote. Ngamia pamoja na ukubwa wake na nguvu zake, utamkuta akiongozwa na mtoto mdogo kabisa bila ya matatizo yoyote, lakini nyoka hata awe ni mdogo vipi, utakuta watu wote wanamwogopa na hakuna yeyote awezaye kumdhibiti. Hivyo basi, lau kama Allaah Angelipandikiza kwa wanyama hawa tunaowafuga hulka ya wanyama wakali kama fisi, simba, chui na kadhalika, basi bila shaka tusingeliweza kufaidika nao kabisa.
Hivyo basi, Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anawaambia mahujaji kwamba wale sehemu ya nyama ya wanyama hawa waliowachinja na wawalishe nyama hiyo wenye shida waliyo mafakiri. Na kwa ajili hiyo, wanachuoni wamejuzisha mwenye kuhiji ale sehemu ya nyama. Na kama tunavyojua, mwenye kuhiji anaweza kufanya “Ifraad”, anaweza kufanya “Tamattui”, na anaweza kufanya “Qiraan”. Mwenye kufanya “Ifraad”, huyu halazimiki kuchinja. Ama mwenye kufanya “Tamattui” au “Qiraan”, huyu ni lazima kuchinja. Kuchinja kwa mwenye kufanya “Tamattui”, kunakuwa ni kwa kuunga (jabr), na mwenye kufanya “Qiraan” inakuwa ni kama zawadi ya shukrani, kwa kuwa Allaah Amemsaidia na kumwezesha kufanya ‘umrah pamoja na hijja. Na kwa ajili hiyo, ni juu yake kuchinja mnyama wa shukrani. Ama mwenye kufanya “Tamattui”, huyu atachinja mnyama wa kuunga, kwa kuwa yeye amefanya ‘umrah, kisha akafanya tahalluli, halafu akaja tena kuhirimia toka Makkah muda mdogo kabla ya kuanza hijja. Huyu inakuwa juu yake kuchinja mnyama wa kuunga.
Maulamaa wamejuzisha mwenye kuhiji ale sehemu ya nyama aliyochinja ima kwa njia ya sunna, au kwa njia ya wajibu, au kwa njia ya mubaha. Atakula sehemu ndogo tu, kisha sehemu iliyobaki atawalisha masikini asiyeomba na masikini aombaye. Mnyama aliyechinjwa kama kafara ya kosa alilolifanya mwenye kuhiji, au kwa ajili ya kutekeleza nadhiri, basi hapo mwenye kuhiji anatakikana asile chochote katika nyama ya mnyama aliyemchinja.
Kisha Allaah Anaendelea kutuambia:
"ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُمْ وَلْيُوفُوا نُذُورَهُمْ وَلْيَطَّوَّفُوا بِالْبَيْتِ الْعَتِيقِ "
“Kisha wajisafishe taka zao, na watimize nadhiri zao, na watufu kwenye Nyumba ya Kale (Al-Ka’bah)”. [Al-Hajji: 29]
Mwanadamu wakati anapokata kucha zake anakuwa anaondosha uchafu wa mwili wake. Anaponyoa nywele za kichwa na hata za kinenani, anaondosha uchafu. Anapooga na kuondosha jasho la mwili, anakuwa akiondosha uchafu wa mwili wake. Mwenye kuhiji baada ya kuhirimia tarehe nane mfungo tatu (Siku ya At-Tarwiyah), au kwa mwenye kufanya “Tamattui” ambapo huhirimia umra na kuendelea na hijja, hao wote huendelea kuwepo ndani ya ihramu yao kwa siku kadhaa bila kuoga, bila kugusa manukato, bila kunyoa na bila ya kuvaa nguo ya kushonwa huku wakikabiliana na mikikimikiki ya amali za hijja ya kupanda na kushuka, wakitokwa jasho, wakiparazana na mahujaji wenzao na hasa katika kipindi cha joto kali, na hata wakati mwingine wakikabiliana na vumbi ikiwa ni siku ya upepo. Yote haya huifanya miili yao kuwa katika hali ya uchafu. Baada ya yote haya, unapokuja wakati wa kufanya tahalluli, Allaah Anawaambia:
“Kisha wajisafishe taka zao, na watimize nadhiri zao, na watufu kwenye Nyumba ya Kale (Al-Ka’bah)”.
Mahujaji baada ya kutupia Jamaratul Aqabah, na baada ya kuchinja, kunyoa na kuoga, wanakuwa wamefanya tahalluli ya kwanza. Hapa wanaweza kufanya kila lile lililokuwa haramu kulifanya isipokuwa tendo la ndoa. Na wanapotufu Twawafur Rukni, yaani Twawaaful Ifaadhwah, hapo kila kitu kilichokuwa marufuku kitakuwa ni halali kwao ikiwemo kuwaingilia wake zao.
Na Allaah Anapotuambia:
وَلْيَطَّوَّفُوا بِالْبَيْتِ الْعَتِيقِ "
“Na watufu kwenye Nyumba ya Kale (Al-Ka’bah)”. [Al-Hajji: 29]
Maulamaa wa lugha wanatueleza kwamba kitenzi "طَوَّفَ" (Twawwafa) hapa kiko katika uzani wa "فَعَّلَ" (shadda juu ya ‘ayn), na uzani huu wa "فَعَّلَ" unakuja mara zote kwa ajili ya kuonyesha wingi au ukaririfu wa kitenzi au kitendo. Wanasema kwa mfano kitenzi "كَسَّرَ"(Kassara) si sawa na "كَسَرَ" (Kasara). "كَسَّرَ" inakuwa na maana amevunjavunja vipande vipande wakati "كَسَرَ" ina maana amevunja ima kidogo tu au vipande viwili.
Hivyo basi, Allaah Ta’aalaa Anaposema hapa وَلْيَطَّوَّفُواkwa kutumia kitenzi "طَوَّفَ" katika uzani wa "فَعَّلَ" , basi hapa kwa mujibu wa Maulamaa hawa mabingwa wa Lugha, ina maana kwamba watu wakithirishe kuitufu Al-Ka’aba. Na hili ndilo alilolifahamu Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Uchache wa mizunguko (ashwatw) katika Al-Ka’aba ni minne tu, na huu ndio wajibu, lakini sunnah ni mizunguko saba. Yeyote mwenye kuzunguka mizunguko minne kisha akapoteza fahamu au akashindwa kukamilisha kwa sababu yoyote ile, basi huyo anakuwa ashatekeleza faradhi yake.
Na Al-Ka’aba hii wanayoizunguka mahujaji, imeitwa kongwe kwa kuwa ndiyo nyumba kongwe zaidi katika uso wa dunia, au kwa kuwa kwake iko huru haijaguswa na mikono yoyote ya wavamizi au watawala madikteta. Neno "العَتِيْقُ" lina maana ya kongwe au iliyo huru. Vita vyote vilivyoshuhudiwa na ulimwengu wa Kiislamu, hakuna vita vyovyote vilivyofanikiwa kuingia kwenye Al-Ka’aba Tukufu na Al-Ka’aba kuwa chini ya utawala wa kiongozi dikteta.
Maana nyingine ni kuwa kila mwenye kuingia ndani ya Nyumba hii huku akiwa ni mwenye kumtakasia Allaah ibada, basi Allaah Humwacha huru na moto. Na hii pia inawahusu mahujaji ambao Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia katika Hadiyth yake:
"مَنْ حَجَّ فَلَمْ يَرْفُثْ وَلَمْ يَفْسُقْ رَجَعَ كَيَوْمِ وَلَدَتْهُ أمُّهُ"
“Mwenye kuhji, halafu asiingilie au kufanya tendo lolote baya, basi hurejea kama siku aliyozaliwa na mama yake”. [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na kwa ajili hiyo, Maulamaa wanatuambia kwamba mwenye kumiminika toka ‘Arafaat na wala dhana yake haikulemea ya kwamba Allaah Amemsamehe makosa yake, basi huyo hana hijja. Ni kwa nini? Ni kwa kuwa mtu huyo ametoka mbali maelfu ya kilometa kwa mujibu wa eneo lake kijiografia, akalipa gharama zote za safari, akaacha shughuli zake zote na kuwaacha watu wake wote, kisha akaja Makkah kwa ajili ya hijja. Kwa nini amekuja? Je, si kwa ajili ya kutafuta na kutaka maghfira ya Mola wake? Basi ni kwa nini baada ya yote hayo asihisi kwamba ameghufiriwa madhambi yake? Huyu inabidi ajitafiti vizuri kuanzia chumo lake na matendo yake yote mengineyo. Huenda chumo lake ni la haramu, huenda ana haki za watu ambazo hataki kuzirejesha na kadhalika. Na Allaah Hatokubali kwa hali yoyote amali kama hii iliyofanywa kutokana na chumo la haramu. Na hata du’aa ya mtu mwenye kula vya haramu, Allaah Haikubali kamwe sembuse ibada zinginezo zote.
Allaah Ta’aalaa Anaendelea kutuambia:
"ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ"
“Hayo ndio hivyo. Na yeyote anayeadhimisha Ishara za Allaah, basi hayo ni katika taqwa ya nyoyo”. [Al-Hajj: 32]
"شَعَائِرُ" ni wingi wa "شَعِيْرَةُ" , na maana yake ni alama au ishara yenye kutaarifu amali ya hijja au ibada yoyote ile. Al-Ka’aba ni katika Alama za Allaah, Al-Baytul Haraam ni katika Alama za Allaah, Al-Haram ya Makka pamoja na mipaka yake yote ni katika Alama za Allaah, Msahafu ni katika Alama za Allaah, Msikiti wowote ni katika Alama za Allaah, Muumini ni katika Alama za Allaah, mwenye kutafuta ‘ilmu ya dini anakuwa ni katika Alama za Allaah na kadhalika. Alama zote hizi ni lazima ziheshimiwe na kutukuzwa. Na hata ngamia na wanyama wengineo wanaopelekwa Makkah kwa ajili ya kuchinjwa wanakuwa ni katika Alama za Allaah. Allaah Anatuambia:
"وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّـهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ ۖ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ"
“Na ngamia na ng’ombe Tumekufanyieni kuwa ni miongoni mwa Ishara za Allaah; kwa hao mnapata khayr nyingi. Basi tajeni Jina la Allaah juu yao wanapopangwa safu (kuchinjwa)”. [Al-Hajji: 36]
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
17: Dhana Ya Hijja: (c) Matunda Mema Ya Baada Ya Kuhiji
Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
"قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ● لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ"
“Sema: Hakika Swalaah yangu, na ‘ibaadah yangu ya kuchinja, na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu. ● Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza (katika ummah huu)”. [Al-An’aam: 162-163]
Hivi ndivyo Waislamu wote duniani tunavyowashuhudia wenzetu waliopewa khatua ya kutekeleza nguzo ya tano ya Uislamu Hijja wakirejea makwao baada ya kuimaliza safari ya kiimani iliyojaa Baraka na kuwajumuisha Waislamu toka pembe zote za dunia. Hawa wote pamoja na tofauti zao za kilugha, kiutaifa, kitamaduni na mengineyo, walijumuishwa pamoja na wito wa Allaah Ta’aalaa wa kuitekeleza nguzo hiyo kupitia kwa Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) tokea miaka maelfu iliyopita. Mjumuiko wao huu ukawathibitishia kwamba wao ni umma mmoja na Mola wao ni Mmoja na hakuna ubora kati ya Mwarabu juu ya asiye Mwarabu, wala mweupe juu ya mweusi isipokuwa kwa uchaMungu. Hao wote tuna matarajio makubwa kabisa kwamba wanarejea makwao hali ya kuwa wamesamehewa madhambi yao yote kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asemaye:
"مَنْ حَجَّ لِلَّهِ فَلَمْ يَرْفُثْ وَلَمْ يَفْسُقْ، رَجَعَ كَيَوْمِ وَلَدَتْهُ أُمُّهُ"
“Atakayehiji, kisha asifanye jimai na vitangulizi vyake (au maneno ya ovyo), au lolote la kumtoa nje ya mstari wa utiifu kwa Allaah, basi hurudi na kuwa kama siku aliyozaliwa na mama yake”. [Hadiyth Swahiyh. Bukhaariy (1521) na Muslim (1350)]
Miongoni mwa siri kubwa za hijja ni kuwa hijja inatuunganisha na kiongozi wetu mkuu Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyetuambia:
"خُذُوا عَنِّيْ مَنَاسِكَكُمْ"
“Jifunzeni kutoa kwangu amali zenu za Hijja”. [Abu Daawuwd (2877), Ahmad (15041) na Ibn Khuzaymah]
Hivyo basi, aliyefanya amali zake zote za hijja kwa mujibu wa maelekezo ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi huyo bila shaka, atakuwa akijitahidi kuishi maisha yake yote juu ya uongofu wa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kazi zake, shughuli zake, ibada zake na kila hatua zake zote za kimaisha mpaka siku yake ya mwisho ya kuondoka hapa duniani. Wakati wote anakuwa akilikumbuka Neno Lake Ta’aalaa kama tulivyoanza mwanzoni:
"قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ● لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ"
“Sema: Hakika Swalaah yangu, na ‘ibaadah yangu ya kuchinja, na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu. ● Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza (katika ummah huu)”. [Al-An’aam: 162-163]
Maisha yote ya mwanadamu bali hata umauti wake, ni lazima uwe kwa mujibu wa njia na uongofu wa Allaah Ta’aalaa na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akiswali aswali kwa mujibu wa alivyoelekeza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akifunga ni lazima afunge kama alivyoelekeza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akifanya lolote lile ni lazima liwe juu ya msingi wa methodolojia ya Allaah na Rasuli Wake, na kinyume na hivyo, mtu ataangamia.
Na kati ya siri nyingine ya hajji na manufaa yake, ni kuzilea nafsi juu ya utwaharifu na adabu ya hali ya juu kabisa. Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
"الْحَجُّ أَشْهُرٌ مَّعْلُومَاتٌ ۚ فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلَا رَفَثَ وَلَا فُسُوقَ وَلَا جِدَالَ فِي الْحَجِّ ۗ وَمَا تَفْعَلُوا مِنْ خَيْرٍ يَعْلَمْهُ اللَّـهُ ۗ وَتَزَوَّدُوا فَإِنَّ خَيْرَ الزَّادِ التَّقْوَىٰ ۚ وَاتَّقُونِ يَا أُولِي الْأَلْبَابِ"
“Hajj ni miezi maalumu. Na atakayekusudia kuhiji ndani ya miezi hiyo (akahirimia), basi asifanye tendo la ndoa wala ufasiki wala mabishano katika Hajj. Na lolote la khayr mlifanyalo basi Allaah Analijua. Na chukueni masurufu, kwani hakika bora ya masurufu ni taqwa. Na nicheni Mimi enyi wenye akili! [Al-Baqarah: 197]
Tukirudi kiuchambuzi kwenye aya hizi tukufu, tunasema: Kwanza kabisa, sababu ya kushushwa kwake kwa mujibu wa wanavyosema Mufassiruna ni kuwa washirikina walikuwa wakiyaabudu masanamu na wakichinja wanyama kwa ajili yake. Na hapo Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Akamwamuru Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Waumini waende kinyume na hayo wanayoyafanya washirikina hao kwa kuyaelekeza makusudio yao, hima zao na yote wanayoyafanya kwa ajili Yake Allaah Ta’aalaa Peke Yake.
Pili, tukijaribu kuchanganua neno moja baada ya jingine tunasema, Allaah Ta’aalaa Anaposema "صَلَاتتِيْ" , Mufassiruna wanasema makusudio yanaweza kuwa kwa maana ya swalah kijumuishi yaani dua yangu, unyenyekevu wangu na ibada yangu. Au inaweza kuwa kwa maana ya swalah za faradhi na za sunnah ambazo mimi ninaziswali kwa ajili ya Allaah Ta’aalaa Peke Yake bila ya kumshirikisha na chochote. Na hapo ikiwa kwa maana ya swalah za faradhi ambazo ni tano, tutakuta kwamba hiyo ni nguzo kuu ya pili kati ya nguzo za Kiislamu ambayo haipomoki kwa Mwislamu vyovyote hali yake itakavyokuwa. Ni lazima kila Mwislamu atekeleze swalah tano kwa hali yoyote ya uzima na ugonjwa na hata katika wakati wa vita. Shahada moja inamtosha Mwislamu kuthibitisha Uislamu wake, swaumu inaweza kupomoka kwa Mwislamu kama hawezi kufunga, hajji kama mtu hana uwezo wa kimali na kiafya hawajibikiwi, lakini swalah ni wajibu katika hali zote. Kama mtu hawezi kusimama ataswali kwa kukaa, kama hawezi kwa kukaa, ataswali kwa kulala kwa ubavu, au chali na kadhalika isipokuwa tu kama amepoteza fahamu. Lakini fahamu zinapomrejea ni lazima ailipe swalah iliyompita.
Hivyo basi, Allaah Ta’aalaa Anapomwambia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aseme hapa "Hakika swalah yangu", Anataka kutukumbusha sisi kwamba swalah ndiyo nguzo kuu ya Uislamu ambayo inabidi tuishikilie kwa magego yetu na kwa nguvu na hali zetu zote..
· Hadhi Ya Swalaah Katika Uislamu:
1- Swalah ndiyo faradhi iliyosisitiziwa na iliyo bora zaidi baada ya shahada mbili na ni moja kati ya nguzo za Kiislamu.
Imepokelewa na Ibn 'Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"بُنِيَ الإسْلَامُ علَى خَمْسٍ: شَهَادَةِ أنْ لا إلَهَ إلَّا اللَّهُ وأنَّ مُحَمَّدًا رَسولُ اللَّهِ، وإقَامِ الصَّلَاةِ، وإيتَاءِ الزَّكَاةِ، والحَجِّ، وصَوْمِ رَمَضَانَ"
“Uislamu umejengewa juu ya (nguzo) tano: Kushuhudia kwamba hapana mungu mwingine isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zaka, kuhiji na kufunga Ramadhani”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (08) na Muslim (16)]
2- Allaah Ta’aalaa Ametoa onyo kali kwa mwenye kuacha swalah kufikia mpaka Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumnasibisha mtu huyo na ukafiri na ushirikina, akasema:
"إنَّ بيْنَ الرَّجُلِ وبيْنَ الشِّرْكِ والْكُفْرِ تَرْكَ الصَّلاةِ"
“Hakika baina ya mtu na (kuingia kwenye) shirki na ukafiri ni kuacha swalah”. [Hadiyth Swahiyh. Muslim (82)]
‘Abdullah bin Shuqayq ambaye ni Taabi’iy amesema: “Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa hawaoni amali ambayo kuiacha kwake ni ukafiri isipokuwa swalah”.
3- Swalah ndio nguzo ya dini, na dini haisimami ila kwa nguzo hii. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"رأسُ الأمرِ الإسلام، وعمودُه الصَّلاةُ، وذِروةُ سَنامِهِ الجِهادُ"
“Kichwa cha mambo yote ni Uislamu, nguzo yake kuu ni swalah, na kilele chake cha juu kabisa ni kufanya Jihadi”. [Hadiyth Hasan. Imechakatwa na At-Tirmidhiy (2616), An Nasaaiy katika Al-Kubraa (11330) na Ibn Maajah (3973)]
4- Ni jambo la kwanza atakalohisabiwa mja Siku ya Qiyaamah. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِنَّ أَوَّلَ مَا يُحَاسَبُ بِهِ الْعَبْدُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مِنْ عَمَلِهِ صَلَاتُهُ. فَإِنْ صَلُحَتْ فَقَدْ أَفْلَحَ وَأَنْجَحَ، وَإِنْ فَسَدَتْ فَقَدْ خَابَ وَخَسِرَ"
“Hakika jambo la kwanza atakalohisabiwa kwalo mja siku ya Qiyaamah katika matendo yake ni swalah zake. Zikikutwa ziko sahihi, basi atakuwa amefaulu na kufuzu. Na kama zitakuwa mbovu, basi atakuwa amepita utupu na amekula hasara”. [Hadiyth Hasan Ghariyb. Sunan At-Tirmidhiy (413)]
5- Swalah ilikuwa ndio kitulizo cha jicho kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika maisha yake. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"حُبِّبَ إِلَىَّ النِّسَاءُ وَالطِّيبُ وَجُعِلَتْ قُرَّةُ عَيْنِي فِي الصَّلاَةِ "
“Nimefanywa kuwapenda wanawake na mafuta mazuri, na kitulizo cha jicho langu kimewekwa ndani ya swalah”. [An-Nasaaiy (3939) na Ahmad (13079)]
6- Swalah ilikuwa ndio wasiya wa mwisho wa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa umati wake wakati wa kufariki kwake. Amesema:
"الصَّلاةَ وما ملَكَت أيمانُكم، الصَّلاةَ وما مَلَكت أيمانُكم"
“Chungeni swalah, na walio na vilivyo chini ya mamlaka yenu. Chungeni swalah, na walio na vilivyo chini ya mamlaka yenu”. [Hadiyth Swahiyh. Al-Jaami’u As-Swaghiyr (5154)]
7- Ni ibada pekee isiyombanduka aliyebaleghe. Humganda maisha yake yote na wala hasameheki nayo vyovyote hali iwavyo.
8- Swalah ina sifa za kipekee kulinganisha na ibada nyinginezo. Kati ya sifa hizo:
(a) Allaah Mtukufu Aliifaradhisha Yeye Mwenyewe kwa kuzungumza moja kwa moja na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku wa Miiraji.
(b) Ni faradhi iliyotajwa zaidi katika Qur-aan Tukufu.
(c) Ni ibada ya kwanza Aliyoifaradhisha Allaah Mtukufu kwa Waja Wake.
(d) Imefaradhishwa mara tano mchana na usiku kinyume na ibada na nguzo nyinginezo.
Ama Neno Lake Ta’aalaa "وَنُسُكِيْ", Mufassiruna wanasema "النُّسُكُ" maana yake ni ibada. Nusuk vile vile ni wingi wa "نَسِيْكَة", nayo ina maana ya mnyama wa kuchinjwa. Pia neno hili humaanisha matendo maalumu yanayofanyika katika amali ya hijja kama kutufu, kusai, kusimama Arafah, kutupia viguzo na kadhalika. Matendo yote haya huitwa "نُسُك"
Ibn Kathiyr anasema kwamba An Nusuk maana yake ni wanyama wanaochinjwa kwa ajili ya hijja au umra. Na hii ni kwa vile Waarabu walikuwa wakifanya vitendo vya ushirikina huku wakidai kwamba wao wako katika Dini ya Ibraahiym. Na hapo ndipo Allaah Ta’aalaa Alipomwamuru Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awabainishie ya kwamba Ibraahiym alikuwa ni mnyoofu, anayemwabudu Allaah Ta’aalaa Peke Yake bila ya kumshirikisha na yeyote au chochote.
Hivyo basi, inatakikana Mwislamu anapomchinja mnyama wakati wa sikukuu ya eid au kwenye amali za hijja, amchinje kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah Ta’aalaa Pekee na si kwa ajili ya malengo ya kidunia ya kusifiwa na kadhalika.
Ama Neno Lake Ta’aalaa "مَحْيَاي وَمَمَاتِيْ", Mufassiruna wanasema kwamba "المَحْيَا" na "المَمَات" zina maana ya amali za wakati wa uhai na amali za wakati wa kufa. Amali zote za uhai huungana na kipindi cha wakati mtu anapokufa. Ikiwa matendo ya katika uhai wa mtu yalikuwa ni mazuri, basi mtu huyu bila shaka atafia katika hali njema na mwisho mwema. Na ikiwa matendo yake ni mabaya, basi mauti yake yatamkuta akiwa katika ubaya na mwisho wake utakuwa ni mbaya.
Nuru Ya Qur-aan
Alhidaaya.com [2]
18: (a) Baadhi Ya Neema Za Allaah Kwa Bani Israaiyl :
Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anatuambia:
"يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ وَأَنِّي فَضَّلْتُكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ ● وَاتَّقُوا يَوْمًا لَّا تَجْزِي نَفْسٌ عَن نَّفْسٍ شَيْئًا وَلَا يُقْبَلُ مِنْهَا شَفَاعَةٌ وَلَا يُؤْخَذُ مِنْهَا عَدْلٌ وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ"
“Enyi wana wa Israaiyl! Kumbukeni Neema Zangu Nilizokuneemesheni, na hakika Mimi Nimekufadhilisheni juu ya walimwengu wote. ● Na iogopeni Siku ambayo nafsi haitoifaa nafsi nyingine kwa kitu chochote kile, na wala hautokubaliwa kutoka kwake uombezi wowote, na wala hakitochukuliwa kutoka kwake kikomboleo, na wala hawatonusuriwa”. [Al-Baqarah: 47-48]
Aya hizi zinawakumbusha Bani Israaiyl juu ya neema ambazo Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Aliwafadhili kwazo juu ya walimwengu au watu waliokuwa wakiishi katika zama zao, na Akawaamuru wawajibike na kufanya matendo mema ili wapate malipo mema katika siku ya mwisho ambapo kila mmoja atalipwa mema yake na mabaya yake hata kama yatakuwa na uzito wa atom.
Mara nyingi tunaona katika aya mbalimbali, Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Akiwaita Bani Israaiyl kwa jina la baba yao Israaiyl ambaye ni Ya’aquuwb (Alayhis Salaam) ambaye wao kwao ni asili ya fahari yao na kujitukuza kwao. Kuwaita hivi ni dalili juu ya kubobea kwao katika maasi na uasi na kutojibisha kwao Wito wa Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa. Na kwa ajili hiyo, Anawakumbusha baba yao na kwa picha ya ukaririfu ili wapate kurejea Kwake mbali na neema na fadhila nyingi Alizowapa.
Makusudio ya walimwengu hapa ni watu wale waliokuwa wakiishi katika enzi yao tu na si watu wote, kwa kuwa umati wa Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni bora kuliko wao kutokana na Neno Lake Ta’aalaa:
"كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ ۗ وَلَوْ آمَنَ أَهْلُ الْكِتَابِ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُم ۚ مِّنْهُمُ الْمُؤْمِنُونَ وَأَكْثَرُهُمُ الْفَاسِقُونَ"
“Mmekuwa Ummah bora kabisa uliotolewa (mfano) kwa watu; mnaamrisha mema na mnakataza munkari na mnamwamini Allaah. Na lau wangeliamini Ahlul-Kitaabi basi ingelikuwa ni bora kwao. Wako miongoni mwao wanaoamini lakini wengi wao ni mafasiki”. [Aal ‘Imraan: 110]
Hivyo kutokana na neema zote walizoneemeshwa, Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anawakumbusha kwamba ni lazima waiogope siku ya mwisho ambayo ni tofauti kabisa na masiku ya hapa duniani. Siku hiyo ni kwa ajili ya malipo tu, na kwa hivyo basi, ni lazima wajitayarishe nayo kwa kufanya matendo mema. Siku hiyo ina sifa tatu za kipekee:
Kwanza:
Mtu hatoweza kumfaa mwingine kwa lolote. Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anatuambia:
"وَاتَّقُوا يَوْمًا لَّا تَجْزِي نَفْسٌ عَن نَّفْسٍ شَيْئًا"
“Na iogopeni Siku ambayo nafsi haitoifaa nafsi nyingine kwa kitu chochote kile”. [Al-Baqarah: 48]
Kama tujuavyo, nafsi za wanadamu ziko aina mbili. Kuna nafsi ya Muumini iliyo huru, na kuna nafsi ya kafiri iliyojifunga. Mtu yeyote mwenye kwenda kinyume na Maamrisho ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa na kutoka nje ya Njia Yake, basi huyo anajitendea ubaya mwenyewe, na anajifunga mwenyewe. Ndio pale Allaah Ta’aalaa Anapotuambia:
"كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ رَهِينَةٌ ● إِلَّا أَصْحَابَ الْيَمِينِ"
“Kila nafsi iko katika rehani kwa yale iliyoyachuma ● . Isipokuwa watu wa kuliani”. [Al-Muddath-Thir: 38-39]
Binadamu hapa duniani ikiwa anaishi kwenye jamii iliyojipangia sheria zake na mawajibiko yake, inabidi mtu huyo azitii na kuzifuata sheria hizo na kuwajibika na yote ambayo inampasa awajibike nayo. Ikiwa atakwenda kinyume, basi bila shaka atakamatwa, atawekwa mahabusu, atasomewa mashtaka na anaweza kufungwa. Na hapa bila shaka anakuwa amelipa thamani ya uhalifu na makosa yake. Huko jela atakuwa chini ya ulinzi, atakuwa hana uhuru wa kufanya mambo yake na kadhalika. Na hii ni hali yetu sisi wanadamu. Je, hali itakuwa vipi mbele ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa?
Hivyo, ubaya au maasia yoyote aliyoyafanya mtu, atafungika nayo na hatoweza kusonga mbele kupata Rehma za Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa isipokuwa kama Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Atapenda. Na hata kama atalipata hilo, lakini hata hivyo, atakuwa amepitia misukosuko mikubwa ya Siku ya Qiyaamah.
Na kwa ajili hiyo, Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anatuambia tena:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ"
“Enyi walioamini! Mcheni Allaah, na nafsi itazame imetanguliza nini kwa ajili ya kesho, na mcheni Allaah. Hakika Allaah Ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale myatendayo”. [Al-Hashr: 18]
Ichungue kwa makini amali yako. Iangalie kwa makini kazi yako. Je, chumo lake unalolipata ni la halali safi isiyo na pumba yoyote ya ghushi, utegeaji, uzembe na kadhalika. Jiangalie, je unajenga utukufu wako juu ya migongo ya wengine? Je, wewe unashiba na wenzako wanalala njaa? Je, wewe unapata uhai na wengine wanakufa?
‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:
"حاسِبوا أنفسَكم قبل أن تُحاسَبوا، وزِنوا أنفسَكم قبل أن تُوزنوا"
“Jitathminini wenyewe kabla hamjasailiwa, jipimeni wenyewe kabla amali zenu hazijakuja kupimwa”.
Kwa hiyo yeyote mwenye kujitathmini mwenyewe hapa duniani kama inavyotakikana, akajirekebisha kwa kasoro anazoziona na akalingamana sawasawa katika kufuata maamrisho na kuacha makatazo, basi huyo hisabu yake mbele ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa itakuwa ni nyepesi mno.
Pili:
Mtu hatokubaliwa uombezi wake. Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anatuambia:
"وَلَا يُقْبَلُ مِنْهَا شَفَاعَةٌ"
“Na wala hautokubaliwa kutoka kwake uombezi wowote”. [Al-Baqarah: 48]
"شَفَاعَةٌ"maana yake kilugha ni ombi. Ama kiistilahi kama alivyoeleza Al-Imaam As Saalimiy, ni ombi la kuharakiziwa kuingizwa Peponi, au kuongezewa daraja humo toka kwa Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa kwa ajili ya Waja Wake Waumini.
Kutokana na taarifu hii, inatubainikia kwamba Shafa’ah maana yake imejizinga katika ombi la kuharakishiwa kuingizwa Peponi na kunyanyuliwa daraja ya Waumini huko.
Maulamaa wanatuambia kwamba kuna watu maalumu ambao Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Atawapa nafasi ya kufanya uombezi kwa wengineo. Na hawa ni Waumini wenye kumpwekesha Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa na ambao hawakutenda madhambi makubwa. Na juu ya msingi huu, inawabidi Waumini wote wajiweke sawa kwa kufuata yote aliyokuja nayo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kutenda mema ili angalau pia waweze kupatiwa nafasi hiyo ya kufanya Shafaa’ah kwa wengineo, na kama hawatafanya hivyo, basi bila shaka mambo yatawawia magumu sana Siku ya Qiyaamah.
Tatu:
Hakitachukuliwa kikomboleo toka kwa yeyote ili aepushwe na adhabu. Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anatuambia:
"وَلَا يُؤْخَذُ مِنْهَا عَدْلٌ"
“Na wala hakitochukuliwa kutoka kwake kikomboleo”. [Al-Baqarah: 48]
Siku hiyo ya Qiyaamah, kila mtu aliyetenda madhambi na makosa hapa duniani, atatamani lau kama ataweza kutoa vyote alivyokuwa anavimiliki hapa duniani kwa ajili ya kuepushwa na adhabu ya Siku hiyo. Atatamani hata watoto wake na jamaa zake awatoe ili yeye aepukane na yote yanayomsubiri. Lakini hayo yote hayatakuwa, hata kama mali yake yote itakuwa na thamani ya vyote vilivyomo duniani na mara mbili yake.
Hapa duniani mtu akiwa na mkubwa fulani, basi mambo yake yote yanakuwa sahali. Lakini huko mbele ya Allaah hayo hakuna, ni hapa duniani tu.
"يُحْشَرُ النَّاسُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حُفَاةً عُرَاةً غُرْلًا. قُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ الرِّجَالُ وَالنِّسَاءُ جَمِيعًا يَنْظُرُ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ؟ فَقَالَ: يَا عَائِشَةُ الْأَمْرُ أَشَدُّ مِنْ أَنْ يَنْظُرَ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ"
Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) amesema: “Nilimsikia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: Watu watakusanywa Siku ya Qiyaamah wakiwa pekupeku, bila nguo, wakiwa hawajatahiriwa. Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Wake kwa waume wote wataangaliana?! Akasema: Ee ‘Aaishah! Mambo ni mazito mno hata kuweza kuwashughulisha kuangaliana”. [Al-Bukhaariy na Muslim]
Hii ni picha ndogo tu anayotupa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na siku hiyo ngumu kabisa ambayo inabidi kila mtu ajiandae nayo kwa amali njema. Watu wa familia moja watakimbiana. Hivyo inabidi Banu Israaiyl na Waislamu wote walikumbuke hili vyema kabisa kabla wakati haujapita.
Nne:
Waovu, madhalimu na waasi hawatapata wa kuwanusuru kama walivyokuwa wakisaidiana hapa duniani. Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
"وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ"
“Na wala hawatonusuriwa”. [Al-Baqarah: 48]
Ama kwa upande wa neema walizoneemeshwa Bani Israaiyl na Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa ni neema nyingi mno. Kati ya neema hizo ni:
Kwanza: Allaah Ta’aalaa Aliwaokoa kutokana na udhalimu wa Firauni. Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anasema:
"وَإِذْ نَجَّيْنَاكُم مِّنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَسُومُونَكُمْ سُوءَ الْعَذَابِ يُذَبِّحُونَ أَبْنَاءَكُمْ وَيَسْتَحْيُونَ نِسَاءَكُمْ ۚ وَفِي ذَٰلِكُم بَلَاءٌ مِّن رَّبِّكُمْ عَظِيمٌ "
“ Na pindi Tulipokuokoeni kutoka kwa watu wa Fir’awn walipokusibuni adhabu mbaya, wakiwachinja watoto wenu wa kiume na wakiacha hai wanawake wenu, na katika hayo kwenu ulikuwa ni mtihani mkuu kutoka kwa Rabb wenu”. [Al-Baqarah: 49]
Hizi ndizo adhabu ambazo Firauni alikuwa akiwapa Bani Israaiyl. Akiwanyanyasa kwa kuwafanyisha kazi ngumu na kazi duni, akiwakalifisha kwa wasiyoyaweza, akiwachinja watoto wao wa kiume pamoja na vitendo vinginevyo vyote vibaya. Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Akawaokoa toka kwenye mateso haya.
Pili: Allaah Ta’aalaa Alimwangamiza adui yao Firauni kwa kumgharakisha pamoja na askari wake. Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anasema:
"وَإِذْ فَرَقْنَا بِكُمُ الْبَحْرَ فَأَنجَيْنَاكُمْ وَأَغْرَقْنَا آلَ فِرْعَوْنَ وَأَنتُمْ تَنظُرُونَ"
“Na pale Tulipoitenganisha bahari kwa ajili yenu, Tukakuokoeni na Tukawagharikisha watu wa Fir’awn na huku nyinyi mnatazama”. [Al-Baqarah: 50]
Katika uokozi huu, Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Aliwapa Bani Israaiyl neema nyinginezo juu ya neema hii. Kwanza, Aliwafungulia njia baharini wakaweza kupita jambo ambalo hakuna wanadamu wengineo waliolishuhudia. Pili, Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Aliwazamisha Firauni na askari wake huku wao wakitizama namna maadui wao wanavyoangamia. Al-Imaam Al-Fakhru Ar Raaziy anatuambia:
“Jua kwamba tukio la kupasuka bahari, limekusanya neema nyingi kwa Banu Israaiyl. Kwanza: Ni kwamba wao walipoikurubia bahari na wakawa katika hali ngumu huku Firauni na askari wake wakiwajia kwa nyuma, hapo faraja iliwajia baada ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa kuwapasulia bahari iliyokuwa mbele yao. Pili: Ni kwamba Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Amewakhusu kwa neema hii kuu na muujiza huu wa kushangaza kwa ajili ya kuwakirimu na kuwatunza. Tatu: Ni kuwa kwa kuangamia Firauni, wanakuwa wameshamalizana na mateso yaliyokuwa yakiwakabili na nyoyo zao zikajaa utulivu na ushwari. Nne: Watu wa Musa waliposhuhudia muujiza ule wa kushangaza, iliondoka kwenye nyoyo zao shaka na utata kuhusiana na ukweli wa Nabii Musa ‘Alayhis Salaam. Tano: Kwa kuyaona hayo, imani yao ilizidi, wakazidi kuthibiti juu ya haki na kuyafuata maamrisho. Sita: Walipata kujua kwamba mambo yote yako Mkononi mwa Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa, na kwamba hakuna utukufu zaidi ya aliokuwa nao Firauni hapa duniani, na hakuna udhalili uliokuwa mbaya zaidi kuliko ule waliokuwa nao Bani Israaiyl. Kisha Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa kufumba na kufumbua, Akamfanya mnyonge kuwa mtukufu, na mtukufu kuwa mnyonge, mwenye nguvu kuwa dhaifu na dhaifu kuwa mwenye nguvu.
Lakini pamoja na yote hayo, Banu Israaiyl baada ya kuokolewa, waliyasahau haya yote na wakaanza kumtaka Musa awafanyie sanamu walifanye kuwa mungu waliabudu! Ni ukengeukaje wa aina gani huu?!
Links
[1] https://www.alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/237
[2] http://www.alhidaaya.com/
[3] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11990&title=Nuru%20Ya%20Qur-aan
[4] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11991&title=01-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Al-Isti%E2%80%99aadhah
[5] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11992&title=02-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Basmalah
[6] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11993&title=03-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Suwrat%20Al-Faatihah
[7] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11994&title=04-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Ulinganio%20Wa%20Tawhiyd
[8] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11995&title=05-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Kuthibitisha%20Ujumbe%20Wa%20Rasuli%20Na%20Malipo%20Kwa%20Wenye%20Kuamini%20Na%20Makafiri
[9] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11996&title=06-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Neema%20Za%20Allaah%20Kwa%20Watu%3A%20%28a%29%20Neema%20Ya%20Kwanza%3A%20Allaah%20Amewaleta%20Ulimwenguni%20Baada%20Ya%20Kuwa%20Hawapo
[10] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11997&title=07-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Neema%20Za%20Allaah%20Kwa%20Watu%3A%20%28b%29%20Neema%20Ya%20Pili%3A%20Allaah%20Amewasakharishia%20Vyote%20Vilivyoko%20Ardhini%20Ili%20Viwanufaishe%20Katika%20Maisha%20Yao
[11] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11998&title=08-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Neema%20Za%20Allaah%20Kwa%20Watu%3A%20%28c%29%20Neema%20Ya%20Tatu%3AAllaah%20Amempa%20Mwanadamu%20Uwezo%20Wa%20Kujifunza
[12] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F11999&title=09-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Kuanza%20Mapambano%20Kati%20Ya%20Aadam%20%28%E2%80%98Alayhis%20Salaam%29%20Na%20Ibliys
[13] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F12000&title=10-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Kukubaliwa%20Toba%20Ya%20Aadam%20%28%E2%80%98Alayhis%20Salaam%29%3A
[14] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F12001&title=11-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Maumbile%20Ya%20Mwanadamu
[15] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F12002&title=12-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Mwanadamu%20Alipitikiwa%20Na%20Kitambo%20Bila%20Kuwa%20Anajulikana
[16] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F12003&title=13-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Dhana%20Ya%20Kusimamisha%20Swalah
[17] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F12004&title=14-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Dhana%20Ya%20Zaka
[18] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F12005&title=15-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Dhana%20Ya%20Hijja%3A%20%28a%29%20Mwitiko%20Wa%20Nguvu%20Wa%20Waumini%20Na%20Shauku%20Kubwa%20Ya%20Kufanikisha%20%E2%80%98Amali%20Hii
[19] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F12006&title=16-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Dhana%20Ya%20Hijja%3A%20%28b%29%20Manufaa%20Makuu%20Ya%20Hijja
[20] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F12007&title=17-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20Dhana%20Ya%20Hijja%3A%20%28c%29%20Matunda%20Mema%20Ya%20Baada%20Ya%20Kuhiji
[21] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F12008&title=18-Nuru%20Ya%20Qur-aan%3A%20%28a%29%20Baadhi%20Ya%20Neema%20Za%20Allaah%20Kwa%20Bani%20Israaiyl%20