Tawbah Hukmu Na Fadhila Zake
01-Maana ya Tawbah
Maana ya tawbah ni kurejea. Na tawbah inaanza pale mtu anapokumbuka madhambi yake, akaingiwa na khofu ya kughadhibikiwa na Rabb wake, ikampelekea kurejea kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kumuomba Amghufurie madhambi yake.
Tawbah ni aina ya ‘ibaadah, haghafiliki nayo Muumini. Hata Manabii walikuwa wakiomba tawbah na wakiwaamrisha watu wao pia waombe maghfirah na tawbah:
Nabiy Shu’ayb ('Alayhis-Salaam) aliwaamrisha watu wake:
وَاسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ ۚ إِنَّ رَبِّي رَحِيمٌ وَدُودٌ﴿٩٠﴾
“Na ombeni maghfirah kwa Rabb wenu, kisha tubieni Kwake. Hakika Rabb wangu ni Mwenye kurehemu, Mwenye upendo khalisi.” [Huwd: 90]
Tawbah ni sababu mojawapo ya kufaulu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾
Na tubuni kwa Allaah nyote, enyi Waumini mpate kufaulu. [An-Nuwr: 31]
Kuomba tawbah kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) isiwe kwa ajili ya madhambi makubwa pekee, bali mtu anahitaji kuomba tawbah usiku na mchana kwani madhambi mangapi madogo madogo mtu anayafanya mengine bila ya kujijua. Atakuja kuyakuta katika daftari lake ikiwa ataipuuza tawbah.
Muislam anapofanya maasi ni muhimu kurudi kwa Allaah ('Azza wa Jalla) aombe maghfirah na tawbah ili airudishe nafsi yake katika kutakasika. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) yuko tayari kabisa kupokea tawbah zetu na kutughufuria madhambi yetu. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَهُوَ الَّذِي يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَعْفُو عَنِ السَّيِّئَاتِ
Naye Ndiye Ambaye Anapokea tawbah kutoka kwa waja Wake, na Anasamehe maovu [Ash-Shuwraa: 25]
Nani aliyejidhulumu nafsi yake akawa hana raha kutokana na madhambi aliyoyatenda? Basi tambua ee ndugu Muislamu kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Mwingi wa kughufuria na Mwenye kurehemu kama Anavyosema:
وَمَن يَعْمَلْ سُوءًا أَوْ يَظْلِمْ نَفْسَهُ ثُمَّ يَسْتَغْفِرِ اللَّـهَ يَجِدِ اللَّـهَ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿١١٠﴾
Na atakayetenda ovu au akajidhulumu nafsi yake; kisha akamwomba Allaah maghfirah; atamkuta Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu [An-Nisaa: 110]
Na kwa Rahmah Yake Allaah ('Azza wa Jalla) Ametuamrisha pia kukimbilia Kwake kuomba tawbah. Anasema (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَسَارِعُوا إِلَىٰ مَغْفِرَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ
Na kimbilieni maghfirah kutoka kwa Rabb wenu [Aal-'Imraan: 133]
Tawbah Hukmu Na Fadhila Zake
02-Vipi Kuomba Maghfirah Na Tawbah?
1-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Mara Sabiini Au Mara Mia Kwa Siku:
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alibashiriwa kufutiwa madhambi yake yaliyotangulia na yaliyo mbele yake. Juu hivyo alikuwa akiomba kila siku maghfirah na tawbah mara sabiini au mara mia. Kwa hiyo inatupasa sisi tuombe zaidi yake, au angalau mara mia kwa siku. Hadiyth ya Abuu Hurayrah ifuatayo:
عن أبي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه : سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ : ((وَاللَّهِ إِنِّي لاَسْتَغْفِرُ اللَّهَ وَأَتُوبُ إِلَيْهِ فِي الْيَوْمِ أَكْثَرَ مِنْ سَبْعِينَ مَرَّةً)) رواه البخاري (6307)
Imetoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Wa-Allaahi mimi naomba maghfirah kwa Allaah na kutubia Kwake zaidi ya mara sabiini kwa siku)) [Al-Bukhaariy]
Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaamrisha watu kuomba maghfirah na kutubia kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) mara mia kwa siku aliposema:
((يَا أَيُّهَا النَّاسُ تُوبُوا إِلَى اللَّهِ وَاسْتَغْفِرُوهُ، فَإِنِّي أَتُوبُ إِلَى اللَّهِ، وَأَسْتَغْفِرُهُ فِي كُلِّ يَوْمٍ مِائَةَ مَرَّةٍ))) مسلم
((Enyi Watu tubieni kwa Allaah na muombe maghfirah kwani mimi natubia kwa Allaah na namuomba maghfirah mara mia kwa siku)) [Muslim]
2-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kwa Kuswali Rakaa Mbili:
Akaamrisha pia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuswali rakaa mbili kwa ajili ya kuomba maghfirah na kutubia kwa Allaah ('Azza wa Jalla):
عن أبي بكر الصديق رضي الله عنه قال: سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول: ((ما من رجل يُذْنِبُ ذَنباً، ثمَّ يَقومُ فَيتَطَهَّرُ ويصلي، ثُمَّ يَستَغْفِر اللهَ إِلا غُفِرَ لهُ)) ثم قرأ: ((وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنْفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَنْ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَى مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ)) رواه ابو داود و الترمذى والنسائي - وصححه الألباني في صحيح الترميذي وصحيح الترغيب
Kutoka kwa Abuu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Yeyote atakayefanya dhambi kisha akachukua wudhuu, kisha akaswali, kisha akaomba maghfirah basi ataghufuriwa)) Kisha akasoma: ((Na wale ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao (kwa maasi), humdhukuru Allaah wakaomba maghfirah kwa madhambi yao. Na nani anayeghufuria madhambi isipokuwa Allaah. Na hawaendelei katika waliyoyafanya na wao wanajua)) [Aal-‘Imraan: 135 – Ameipokea Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy, na Imesahihishwa na Shaykh Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (406) na Swahiyh At-Targhiyb (680)]
3-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kwa Sayyid Al-Istighfaar (Du’aa Adhimu Kabisa Ya Kuomba Maghfirah)
وعن شداد بن أوس رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم أنه قال: ((سيد الاستغفار أن يقول العبد: اللّهـمَّ أَنْتَ رَبِّـي لا إلهَ إلاّ أَنْتَ، خَلَقْتَنـي وَأَنا عَبْـدُك، وَأَنا عَلـى عَهْـدِكَ وَوَعْـدِكَ ما اسْتَـطَعْـت، أَعـوذُبِكَ مِنْ شَـرِّ ما صَنَـعْت، أَبـوءُ لَـكَ بِنِعْـمَتِـكَ عَلَـيَّ وَأَبـوءُ بِذَنْـبي فَاغْفـِرْ لي فَإِنَّـهُ لا يَغْـفِرُ الذُّنـوبَ إِلاّ أَنْتَ)) رواه البخاري في صحيحه
Imetoka kwa Shaddaad Bin 'Aws (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Du’aa adhimu kabisa ya kuomba maghfirah ni kusema:
Allaahumma Anta Rabbiy laa ilaaha illaa Anta Khalaqtaniy wa ana ‘abduka wa anaa ‘alaa ‘ah-dika wawa’-dika mastatwa’-tu, a’uwdhu bika min sharri maa swana’-tu, abuw-u Laka bini’-matika ‘alayya wa abuw-u bidhanbiy, faghfir-liy fainnahu laa yaghfirudh dhunuwba illaa Anta
((Ee Allaah, Wewe ni Rabb wangu, hapana muabudiwa wa haki ila Wewe, umeniumba mimi na mimi ni mja Wako, nami niko juu ya ahadi Yako, na agano Lako, kiasi cha uwezo wangu, najikinga Kwako kutokana na shari ya nilichokifanya, nakiri Kwako kwa kunineemesha, na nakiri kwa madhambi yangu, basi nakuomba unighufurie kwani hakuna wa kughufuria madhambi ila Wewe.)) [Al-Bukhaariy]
4-Kuomba Maghfirah Na Tawbah kwa Du’aa Ya Nabiy Yuwnus (‘Alayhis-salaam) alipokuwa tumboni mwa samaki:
لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٨٧﴾
“Hapana Muabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Subhaanak! (Utakasifu ni Wako), hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu.” [Al-Anbiyaa: 87]
5-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kwa Kumsabbih Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
قَالَ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((مَنْ قَالَ: سُبْحَانَ اللهِ وَبِحَمْدِهِ فِي يَوْمٍ مائَةَ مَرَّةٍ، حُطَّتْ خَطَاياهُ وَلَوْ كانَتْ مِثْلَ زَبَدِ الْبَحْرِ))
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallaam amesema: ((Mwenye kusema:Subhaana-Allaahi wa Bihamdihi (Utakasifu ni wa Allaah na Himdi ni Zake) mara mia kwa siku, atafutiwa madhambi yake hata kama yalikuwa mfano wa povu la bahari)) [Hadiyth ya Abu Huraryah (Radhwiya Allaah ‘anhu) - Al-Bukhaariy (7/168) [6405], Muslim (4/2071)]
6-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kila Baada Ya Swalaah Za Fardhi:
قال النبي صلى الله عليه وسلم: ((من سبَّحَ اللَّهَ في دُبُرِ كلِّ صلاةٍ ثلاثًا وثلاثينَ وحمدَ اللَّهَ ثلاثًا وثلاثينَ وكبَّرَ اللَّهَ ثلاثًا وثلاثينَ فتلكَ تسعةٌ وتسعونَ وقالَ تمامَ المائةِ لا إلهَ إلَّا اللَّهُ وحدَهُ لا شريكَ لهُ لهُ الملكُ ولهُ الحمدُ وهوَ على كلِّ شيءٍ قديرٌ غُفِرت خطاياهُ وإن كانت مثلَ زَبَدِ البحرِ)) مسلم
Amesema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((Atakaye sabbih (Subnaaha Allaah) kila baada ya Swalaah mara thelathini na tatu, akaleta takbiyrah (Allaahu Akbar) mara thelathini na tatu, akaleta tahmiyd (AlhamduliLlaah) mara thelathini na tatu akamalizia kwa “Laa ilaaha illa-Allaahu Wahdahu laa shariyka Lah, Lahul-Mulku wa Lahul-Hamdu wa-Huwa ’alaa kulli shay-in Qadiyr - ataghufuriwa makosa yake japokuwa ni mfano wa povu la bahari)) [Hadiyth ya Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) katika Muslim (1/418) [597]
7-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kwa Kutaja Majina Matukufu Kabisa Ya Allaah (‘Azza wa Jalla):
قَالَ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((مَنْ قَالَ أَسْتَغْفِرُ اللَّهَ الَّذِى لاَ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ الْحَىُّ الْقَيُّومُ وَأَتُوبُ إِلَيْهِ؛ غُفِرَ لَهُ وَإِنْ كَانَ فَرَّ مِنَ الزَّحْفِ))
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayesema: Astaghfiru-Allaahal-‘Adhwiyma Alladhiy laa ilaaha illaa Huwal-Hayyul-Qayyuwmu wa atuwbu Ilayhi
Namuomba maghfira kwa Allaah Mtukufu Ambaye Hapana muabudiwa wa haki ila Yeye, Aliyehai daima, Msimamizi wa kila kitu, na ninarejea kutubuia Kwake, Allaah Atamghufuria kama ana makosa hata kama ya kukimbia vitani)) [Hadiyth ya ibn Mas-‘uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) - Abu Daawuwd (2/85) [1517], At-Tirmidhiy (5/569) [3577], ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (3/182)]
Tawbah Hukmu Na Fadhila Zake
03-Tawbah Ya Naswuwhaa Kweli Na Masharti Yake
Kuomba maghfirah na tawbah, kunampasa Muumini awe na yaqini kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atamghufuria madhambi madhambi yake pindi yakitimizwa masharti yake. Na kufanya hivyo ndio inapohakiki Tawbah ya Naswuwhaa (Tawbah ya kikwelikweli). Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametuamrisha tuiombe tawbah hiyo Anaposema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا
Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya nasuha (kwelikweli) [At-Tahriym: 8]
Tawbah Ya Naswuwhaa (Tawbah ya kwelikweli) ni kutubia kikweli kwa kuijiepusha na maasi yote, na kujirekebisha kwa kutokurudia hayo maasi aliyokuwa akiyatenda Muislamu na badili yake mtu azidishe kufanya mema. Na anapoomba mtu Tawbah ya kweli bila shaka Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atamghufuria madhambi yake zote. Anasema Allaah:
وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ ﴿٨٢﴾
Na hakika Mimi bila shaka ni Mwingi mno wa kughufuria kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema kisha akaendelea kuongoka. [Twaahaa: 82]
Masharti Ya Tawbah Ya Naswuwhaa:
Zifuatazo ni shuruti za Tawbah Ya Naswuwhaa:
1. Kuomba maghfirah
2. Kuacha hayo maasi
3. Kujuta
4. Kuweka niyyah (azimio) kutokurudia tena maasi hayo.
5. Kama kaidhulumu haki ya mtu basi ni kuirudisha hiyo haki.
Tawbah Hukmu Na Fadhila Zake
04-Nyakati Bora Za Kuomba Tawbah
1-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Wakati Wowote Ule:
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hupokea tawbah zetu wakati wowote kama alivyotuelezea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth ifuatayo:
عَنْ أَبِي مُوسَى عَبْدِ الله بنِ قَبَسٍ الأَشْعَرِيِّ (رضي الله عنه) عن النَّبيّ (صلى الله عليه و آله وسلم) قال: ((إِنَّ اللَّهَ تَعَالَى يَبْسُطُ يَدَهُ بِاللَّيْلِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ النَّهَارِ وَيَبْسُطُ يَدَهُ بِالنَّهَارِ لِيَتُوبَ مُسِيءُ اللَّيْلِ حَتَّى تَطْلُعَ الشَّمْسُ مِنْ مَغْرِبِهَا)) رواه مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abu Muwsaa ‘Abdillaah bin Qays Al-Ash‘ariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallamamesema: ((Hakika Allaah Anakunjua Mkono Wake usiku ili Apokee tawbah ya mkoseaji mchana. Na Anakunjua Mkono Wake mchana ili Apokee tawbah ya mkoseaji usiku mpaka jua lichomoze Magharibi [mahali linapokuchwa])) [Muslim]
2-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kabla Ya Alfajiri:
Lakini wakati mzuri kabisa wa kuomba maghfirah na tawbah ni nyakati za kabla ya Alfajiri kama Anavyowasifu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) waja wema wafanyao hivo; Anasema (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
الصَّابِرِينَ وَالصَّادِقِينَ وَالْقَانِتِينَ وَالْمُنفِقِينَ وَالْمُسْتَغْفِرِينَ بِالْأَسْحَارِ﴿١٧﴾
Wenye kusubiri na wasemao kweli, na watiifu, na watoaji mali katika njia ya Allaah na waombao maghfirah kabla ya Alfajiri. [Aal-‘Imraan: 17]
Vilevile Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewasifu waje Wake Waumini wanao omba maghfirah kabla ya Alfajiri. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ﴿١٨﴾
Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfirah. [Adh-Dhaariyaat: 18]
3- Kuomba Maghfirah Na Tawbah Usiku Wa Manane:
Kuamka usiku na kufanya 'Ibaadah kama hii ya kuomba maghfirah na tawbah kunapatikana ndani yake fadhila adhimu kabisa, mojawapo ni mja kukaribiana na Rabb wake. Hadiyth ifuatayo imetuthibitikia kuteremka Kwake usiku kuja katika mbingu ya kwanza kupokea tawbah:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم
Imetoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia (mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani Ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Hii ni neema kubwa kwetu kuwa Allaah ('Azza wa Jalla) Anateremka katika mbingu ya kwanza kutupokelea haja zetu na kutughufiria. Basi nani ambaye ataacha neema hii impitie ilhali binaadamu anaingia madhambini kila siku?
Faida: Swala hili la 'Aqiydah ni muhimu kulijua kuhusu kuteremka Kwake Allaah ('Azza wa Jalla) kwamba: Kuteremka Kwake kunalingana na Utukufu Wake na sisi hatujui ni vipi uteremkaji huo unakuwa, wala hatupaswi kuhoji.
Tawbah Hukmu Na Fadhila Zake
05-Hatari Ya Kuchelewa Kuomba Maghfirah Na Tawbah
Muislam anapofanya maasi ni muhimu kwake atubie haraka iwezekanavyo ili apate kughufuriwa madhambi yake na ipokelewe tawbah yake kwa kufuata amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaposema:
إِنَّمَا التَّوْبَةُ عَلَى اللَّـهِ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ يَتُوبُونَ مِن قَرِيبٍ فَأُولَـٰئِكَ يَتُوبُ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ عَلِيمًا حَكِيمًا ﴿١٧﴾
Hakika tawbah inayokubaliwa na Allaah ni ya wale wanaofanya uovu kwa ujahili kisha wakatubia haraka, basi hao Allaah Anapokea tawbah yao. Na Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote. [An-Nisaa: 17]
Kuchelewa kuomba tawbah huenda kusifae tena. Huenda mtu akaendelea kufanya madhambi hadi akafika wakati wa kukata tamaa ya kuishi na mauti yakamfikia ndipo akatambua umuhimu wa kuomba tawbah kwa Rabb wake, hapo tena atakuwa kachelewa kabisa na hapo tawbah yake itakuwa haina faida tena kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anaonya:
وَلَيْسَتِ التَّوْبَةُ لِلَّذِينَ يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ حَتَّىٰ إِذَا حَضَرَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ إِنِّي تُبْتُ الْآنَ وَلَا الَّذِينَ يَمُوتُونَ وَهُمْ كُفَّارٌ ۚ أُولَـٰئِكَ أَعْتَدْنَا لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿١٨﴾
Lakini tawbah si kwa wale wanaofanya maovu mpaka mauti yanapohudhuria kwa mmoja wao husema: “Hakika mimi sasa nimetubu.” Na wala wale wanaokufa na hali wao ni makafiri. Hao Tumewaandalia adhabu iumizayo. [An-Nisaa: 18]
Mfano wake kama ni mfano wa Fir'awn alivyofanya wakati anazama baharini hapo akaona hana hila ila aombe tawbah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَجَاوَزْنَا بِبَنِي إِسْرَائِيلَ الْبَحْرَ فَأَتْبَعَهُمْ فِرْعَوْنُ وَجُنُودُهُ بَغْيًا وَعَدْوًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا أَدْرَكَهُ الْغَرَقُ قَالَ آمَنتُ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا الَّذِي آمَنَتْ بِهِ بَنُو إِسْرَائِيلَ وَأَنَا مِنَ الْمُسْلِمِينَ﴿٩٠﴾
Na Tukawavukisha wana wa Israaiyl bahari, basi Fir’awn akawafuata na jeshi lake kwa ukandamizaji na uadui; mpaka ilipomfikia (Fir’awn) gharka akasema: “Nimeamini kwamba hapana muabudiwa wa haki, isipokuwa Yule waliyemwamini wana wa Israaiyl, na mimi ni miongoni mwa Waislamu.” [Yuwnus: 90]
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akamuuliza Fir'awn wakati anatapatapa katika mauti huku akiomba na kudai kuwa kaamini:
آلْآنَ وَقَدْ عَصَيْتَ قَبْلُ وَكُنتَ مِنَ الْمُفْسِدِينَ﴿٩١﴾
“Sasa (ndio unaamini) na ihali umeasi kabla, na ulikuwa miongoni mwa mafisadi!?” [Yuwnus: 91]
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akaikataa Tawbah yake katika hali hii, Akasema:
فَالْيَوْمَ نُنَجِّيكَ بِبَدَنِكَ لِتَكُونَ لِمَنْ خَلْفَكَ آيَةً ۚ وَإِنَّ كَثِيرًا مِّنَ النَّاسِ عَنْ آيَاتِنَا لَغَافِلُونَ﴿٩٢﴾
Basi leo Tunakuokoa kwa (kuuweka) mwili wako ili uwe Aayah (zingatio, ishara) kwa watakaokuja nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika na Aayaat Zetu. [Yuunus: 92]
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) vile vile hakuaacha kutufahamisha hatari ya kuchelewa kuomba tawbah katika Hadiyth zifuatazo :
1- Kuomba Maghfirah Na Tawbah kabla ya Sakaraatul-Mawt:
قال صلى الله عليه وسلم: ((إِنَّ الله عزَّ وجَلَّ يقْبَلُ توْبة العبْدِ مَالَم يُغرْغرِ)) رواه أحمد والترمذي وصححه النووي
((Hakika Allaah ‘Azza wa Jalla Huikubali tawbah ya mja Wake kabla ya roho kufika kwenye mkoromo wa mauti)) [Imesimuliwa na Ahmad na At-Tirmidhiy na kusahishwa na An-Nawawiy]
2-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kabla ya kuchomoza jua upande wa Magharibi:
عن أبي هريرة رضي الله عنه أن النبي صل قال : ((مَنْ تَابَ قَبْلَ أَنْ تَطْلُعَ الشَّمْسُ مِنْ مَغْرِبِهَا، تَابَ اللَّهُ عَلَيْهِ)) رواه مسلم
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Atakayetubu kabla ya kuchomoza jua upande wa Magharibi, Allaah Atamkubalia tawbah yake)) [Muslim]
3-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kabla ya moyo kupofuka wote:
Hatari nyingine ni kuwa huenda mtu ukapofoka moyo wake akawa hajali tena kufanya maovu na hata ikawa shida tena mtu huyo kupata hidaaya kwa kuwa huwa haoni wala hasikii, bali ametumbukia katika maasi. Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ifuatayo inaelezea hali kama hiyo:
عن أبي هُرَيرة، قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((إنَّ العبدَ إذا أخطأَ خطيئةً نُكِتت في قلبِهِ نُكْتةٌ سوداءُ، فإذا هوَ نزعَ واستَغفرَ وتابَ سُقِلَ قلبُهُ، وإن عادَ زيدَ فيها حتَّى تعلوَ قلبَهُ، وَهوَ الرَّانُ الَّذي ذَكَرَ اللَّه عز وجل ((كَلاَّ بَلْ رَانَ عَلَى قُلُوبِهِم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ)) رواه أحمد والترمذي وحسنه الألباني
Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mja anapofanya dhambi, doa jeusi (kutu) huwekwa katika moyo wake. Akiacha dhambi hiyo, na kuomba maghfirah na kutubu, moyo wake husafishwa ukawa msafi, lakini akirudia kufanya dhambi, doa (kutu) huzidi kuenea mpaka kufunika moyo wote na hiyo ndio 'Raan' (kutu) aliyosema Allaah ‘Azza wa Jalla: ((Laa hasha! Bali imefanya kutu juu ya nyoyo zao yale waliyokuwa wakiyachuma] [Al-Mutwaffifiyn: 14] [Imesimuliwa na Ahmad, At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy amesema ni Hasan.
Inasikitisha kwamba baadhi ya Waislamu huchelewa kuomba Tawbah. Kuna ambao hawatilii umuhimu wake, na wengine wakijiona kuwa ni vijana bado, hivyo hutegemea kutubia wakifika uzeeni ambako hakuna uhakika wake wa kuishi mpaka huko. Huo ni uchochezi wa Ibliys anayempambia binaadamu kwa kumpa matumaini ya maisha marefu. Basi inapasa kumwepuka Ibliys na kukimbilia kutubu Tawbah ya kweli kabla ya majuto.
Tawbah Hukmu Na Fadhila Zake
06-Allaah Anampenda Mja Anayeomba Tawbah
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ ﴿٢٢٢﴾
Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha. [Al-Baqarah: 222]
Tusome Kisa hiki kidogo kilichoelezewa katika Hadiyth Swahiyh:
عن أَنَسُ بْنُ مَالِكٍ قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم: ((الَلَّهُ أَشَدُّ فَرَحًا بِتَوْبَةِ عَبْدِهِ حِينَ يَتُوبُ إِلَيْهِ مِنْ أَحَدِكُمْ كَانَ عَلَى رَاحِلَتِهِ بِأَرْضِ فَلاَةٍ فَانْفَلَتَتْ مِنْهُ وَعَلَيْهَا طَعَامُهُ وَشَرَابُهُ فَأَيِسَ مِنْهَا فَأَتَى شَجَرَةً فَاضْطَجَعَ فِي ظِلِّهَا قَدْ أَيِسَ مِنْ رَاحِلَتِهِ فَبَيْنَا هُوَ كَذَلِكَ إِذَا هُوَ بِهَا قَائِمَةً عِنْدَهُ فَأَخَذَ بِخِطَامِهَا ثُمَّ قَالَ مِنْ شِدَّةِ الْفَرَحِ: "اللَّهُمَّ أَنْتَ عَبْدِي وَأَنَا رَبُّكَ" أَخْطَأَ مِنْ شِدَّةِ الْفَرَحِ)) مسلم
Amesimulia Anas (رضي الله عنه): Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: Allaah Hufurahikiwa mno na tawbah ya mja Wake wakati anapotubia Kwake kuliko furaha ya mmoja wenu aliyekuwa amempanda mnyama wake kwenye jangwa (la joto kali hakuna mtu), kisha mnyama huyo aliyebeba chakula chake na maji yake akampotea, na akakata tamaa kabisa ya kumpata tena. Akaenda kwenye mti, akalala chini ya kivuli chake huku akiwa amekata tamaa kabisa ya kumpata tena mnyama wake. Akiwa katika hali hiyo (ya kutojua nini la kufanya), mara anashtuka kumwona huyo amesimama mbele yake, akaikamata hatamu yake, na kwa ile furaha akasema: "Ee Allaah, Wewe ni mja wangu na mimi ni Rabb wako.” Alikosea (kumshukuru Rabb wake) kwa wingi wa furaha aliyokuwa nayo.” [Muslim]
Vile vile Hadiyth Al-Qudsiy ifuatayo inatuonyesha vipi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alivyo Mpole na Mwenye Rahmah nyingi kiasi cha kwamba yuko tayari kupokea tawbah zetu hata dhambi zikiwa na ukubwa gani.
عن أَنَسُ بْنُ مَالِكٍ قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ: ((قَالَ اللَّهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى يَا ابْنَ آدَمَ، إِنَّكَ مَا دَعَوْتَنِي وَرَجَوْتَنِي غَفَرْتُ لَكَ عَلَى مَا كَانَ فِيكَ وَلَا أُبَالِي، يَا ابْنَ آدَمَ لَوْ بَلَغَتْ ذُنُوبُكَ عَنَانَ السَّمَاءِ ثُمَّ اسْتَغْفَرْتَنِي غَفَرْتُ لَكَ وَلَا أُبَالِي، يَا ابْنَ آدَمَ إِنَّكَ لَوْ أَتَيْتَنِي بِقُرَابِ الْأَرْضِ خَطَايَا ثُمَّ لَقِيتَنِي لَا تُشْرِكُ بِي شَيْئًا لَأَتَيْتُكَ بِقُرَابِهَا مَغْفِرَةً)) أخرجه الترمذي وحسنه الألباني في الصحيحة
Anas (Radhwiya Allaahu 'anhu) amehadithia kwamba: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Amesema: Ee bin-Aadam! Hakika ukiniomba na ukanitaraji (kwa malipo) Nitakughufuria yale yote uliyonayo na wala Sijali, Ee bin-Aadam! Lau zingefikia dhambi zako ukubwa wa mbingu, kisha ukaniomba maghfirah, Ningekughufuria bila ya kujali (kiasi cha madhambi uliyoyafanya). Ee bin-Aadam! Hakika ungenijia na madhambi yakaribiayo ukubwa wa ardhi, kisha ukakutana nami na hali hukunishirikisha chochote, basi Nami Nitakujia na maghfirah yanayolinga nayo.” [At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy kaipa daraja ya Hasan]
Na Hadiyth ifuatayo pia inazidi kutuonyesha uvumilvu na upole wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwamba hata kama mja anarudia kufanya dhambi, madamu tu anarudi kwa Rabb wake kila mara kutubia, basi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Humghufuria:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فِيمَا يَحْكِي عَنْ رَبِّهِ عَزَّ وَجَلَّ قَالَ: ((أَذْنَبَ عَبْدٌ ذَنْبًا فَقَالَ: اللَّهُمَّ اغْفِرْ لِي ذَنْبِي، فَقَالَ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: أَذْنَبَ عَبْدِي ذَنْبًا فَعَلِمَ أَنَّ لَهُ رَبًّا يَغْفِرُ الذَّنْبَ وَيَأْخُذُ بِالذَّنْبِ ثُمَّ عَادَ فَأَذْنَبَ فَقَالَ: أَيْ رَبِّ اغْفِرْ لِي ذَنْبِي، فَقَالَ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: عَبْدِي أَذْنَبَ ذَنْبًا فَعَلِمَ أَنَّ لَهُ رَبًّا يَغْفِرُ الذَّنْبَ وَيَأْخُذُ بِالذَّنْبِ ثُمَّ عَادَ فَأَذْنَبَ فَقَالَ: أَيْ رَبِّ اغْفِرْ لِي ذَنْبِي، فَقَالَ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: أَذْنَبَ عَبْدِي ذَنْبًا فَعَلِمَ أَنَّ لَهُ رَبًّا يَغْفِرُ الذَّنْبَ وَيَأْخُذُ بِالذَّنْبِ. اعْمَلْ مَا شِئْتَ فَقَدْ غَفَرْتُ لَكَ)) البخاري و مسلم
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuhusu mambo aliyohadithia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka kwa Rabb Wake (‘Azza wa Jalla) kwamba ((Mja wa Allaah alifanya dhambi na akasema: Ee Rabb nighufurie dhambi zangu. Na yeye Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa) Akasema: Mja wangu kafanya dhambi kisha kajua kwamba anaye Rabb Ambaye Anaghufuria dhambi na Anayeadhibu kwa kufanya dhambi. Kisha akarudi tena kufanya dhambi akasema: Ee Rabb nighufurie dhambi zangu. Na yeye Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa) Akasema: Mja wangu kafanya dhambi kisha kajua kwamba anaye Rabb Ambaye Anaghufuria dhambi na Anayeadhibu kwa kufanya dhambi. Kisha akarudia tena dhambi na akasema: Ee Rabb nighufurie dhambi zangu. Na yeye Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa) Akasema: Mja wangu kafanya dhambi kisha kajua kwamba anaye Rabb Ambaye Anaghufuria dhambi na Anayeadhibu kwa kufanya dhambi. (Allaah Akasema): Fanya utakavyo, kwani Nimekughufuria)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Tawbah Hukmu Na Fadhila Zake
07-Fadhila Za Kuomba Tawbah
Kuomba Tawbah haimaanishi kuwa inamtosheleza mtu kuwa hana dhambi tena, bali juu yake, kuna Fadhili nyingi ambazo faida zake zinamrudia mwenye kutubia. Miongoni mwa fadhila na faida hizo ni:
1-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kunasababisha Kujaaliwa Starehe Na Maisha Mazuri:
Ameamrishwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) awaambie watu wake:
وَأَنِ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ يُمَتِّعْكُم مَّتَاعًا حَسَنًا إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى وَيُؤْتِ كُلَّ ذِي فَضْلٍ فَضْلَهُ ۖ وَإِن تَوَلَّوْا فَإِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ كَبِيرٍ﴿٣﴾
Na kwamba: “Mwombeni Rabb wenu maghfirah kisha tubuni Kwake, Atakustarehesheni starehe nzuri mpaka muda maalumu uliokadiriwa; na Atampa kila mwenye fadhila, fadhila Zake. Na mkikengeuka, basi hakika mimi nakukhofieni adhabu ya Siku kubwa.” [Huwd: 3]
2-Kuomba Maghfirah Na Tawbah Kunasabisha Kuletewa neema ya mvua na kuzidishiwa nguvu:
Nabiy Huwd ('Alayhis-Salaam) aliwaambia watu wake:
وَيَا قَوْمِ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَارًا وَيَزِدْكُمْ قُوَّةً إِلَىٰ قُوَّتِكُمْ وَلَا تَتَوَلَّوْامُجْرِمِينَ﴿٥٢﴾
“Na enyi kaumu yangu! Mwombeni maghfirah Rabb wenu, kisha tubieni Kwake, Atakuleteeni mbingu zenye kunyesha mvua tele ya kumiminika na Atakuzidishieni nguvu juu ya nguvu zenu, na wala msikengeuke mkawa wahalifu.” [Huwd: 52]
3-Kuomba Maghfirah Na Tawbah kunasababisha kumiminiwa mvua tele, mali na watoto, na kupewa kila aina ya neema:
Nabiy Nuwh ('Alayhis-Salaam) alipowalingania watu wake miaka ili awatoe katika shirki, aliwanasihi waombe maghfirah na tawbah na akawatajia fadhila na faida zake:
فَقُلْتُ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ إِنَّهُ كَانَ غَفَّارًا﴿١٠﴾
Nikasema: “Ombeni maghfirah kwa Rabb wenu; hakika Yeye ni Mwingi mno wa kughufuria.
يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَارًا﴿١١﴾
“Atakutumieni mvua tele ya kuendelea.”
وَيُمْدِدْكُم بِأَمْوَالٍ وَبَنِينَ وَيَجْعَل لَّكُمْ جَنَّاتٍ وَيَجْعَل لَّكُمْ أَنْهَارًا﴿١٢﴾
“Na Atakuongezeeni mali na wana, na Atakupeni mabustani na Atakupeni mito.” [Nuwh: 10-12]
4-Kuomba Maghfirah Na Tawbah kunasababisha Kuingizwa Jannah:
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَالَّذِينَ إِذَا فَعَلُوا فَاحِشَةً أَوْ ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ ذَكَرُوا اللَّـهَ فَاسْتَغْفَرُوا لِذُنُوبِهِمْ وَمَن يَغْفِرُ الذُّنُوبَ إِلَّا اللَّـهُ وَلَمْ يُصِرُّوا عَلَىٰ مَا فَعَلُوا وَهُمْ يَعْلَمُونَ ﴿١٣٥﴾
Na wale ambao wanapofanya machafu au wakajidhulumu nafsi zao (kwa maasi), humdhukuru Allaah wakaomba maghfirah kwa madhambi yao. Na nani anayeghufuria madhambi isipokuwa Allaah. Na hawaendelei katika waliyoyafanya na wao wanajua.
أُولَـٰئِكَ جَزَاؤُهُم مَّغْفِرَةٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَجَنَّاتٌ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ وَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ ﴿١٣٦﴾
Hao jazaa yao ni maghfirah kutoka kwa Rabb wao na Jannaat zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo. Na uzuri ulioje ujira wa watendaji (wema). [Aal-‘Imraan: 135-136]
5-Kuomba Maghfirah Na Tawbah kunasababisha Kuwekewa Nuru katika Swiraatw Siku ya Qiyaamah ambayo itammulika mtu atakapokuwa akiivuka hiyo njia:
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّـهِ تَوْبَةً نَّصُوحًا عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يُكَفِّرَ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيُدْخِلَكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ يَوْمَ لَا يُخْزِي اللَّـهُ النَّبِيَّ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ ۖ نُورُهُمْ يَسْعَىٰ بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَبِأَيْمَانِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا أَتْمِمْ لَنَا نُورَنَا وَاغْفِرْ لَنَا ۖ إِنَّكَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٨﴾
Enyi walioamini! Tubieni kwa Allaah tawbah ya nasuha (kwelikweli); asaa Rabb wenu Akakufutieni maovu yenu, na Akakuingizeni Jannaat zipitazo chini yake mito. Siku ambayo Allaah Hatomfedhehesha Nabiy (Muhammad Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wale walioamini pamoja naye. Nuru yao itatembea mbele yao na kuliani mwao, watasema: “Rabb wetu! Tutimizie Nuru yetu, na Tughufurie, hakika Wewe juu ya kila kitu ni Muweza. [At-Tahriym: 8]
7-Kuomba Maghfirah Na Tawbah ni mojawapo wa Sifa Za Waja Wa Rahmaan na kunasababisha kubadilishiwa maovu ya mtu na badala yake kugezwa kuwa mema:
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) katika kutaja sifa za ‘Ibaadur-Rahmaah (Waja wa Rahmaan):
وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا ﴿٦٨﴾
Na wale ambao hawaombi pamoja na Allaah mwabudiwa mwengine na wala hawaui nafsi ambayo Allaah Ameiharamisha isipokuwa kwa haki, na wala hawazini. Na atakayefanya hivyo atakutana na adhabu.
يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا ﴿٦٩﴾
Ataongezewa adhabu maradufu Siku ya Qiyaamah, na mwenye kudumu humo akiwa amedhalilika.
إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾
Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akatenda ‘amali njema; basi hao Allaah Atawabadilishia maovu yao kuwa mema. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.
وَمَن تَابَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَإِنَّهُ يَتُوبُ إِلَى اللَّـهِ مَتَابًا ﴿٧١﴾
Na atakayetubu na akatenda mema, basi hakika yeye anatubia kwa Allaah tawbah ya kweli. [Al-Furqaan: 68-71]
8-Kuomba Maghfirah Na Tawbah kabla ya Alfajiri ni ‘amali mojawapo za watakaoingia Jannah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ﴿١٥﴾
Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu.
آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ ۚ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَٰلِكَ مُحْسِنِينَ﴿١٦﴾
Wakichukua yale Atakayowapa Rabb wao. Hakika wao walikuwa kabla ya hapo ni wahisani.
كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ﴿١٧﴾
Walikuwa kidogo tu katika usiku wakilala kwa raha.
وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ﴿١٨﴾
Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfirah.
[Adh-Dhaariyaat: 15-18]
Tunataraji kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwamba makala hizi za kuomba maghfirah na tawbah ziwazidishie iymaan Waislamu wakimbilie kutubia kwa Allaah ('Azza wa Jalla) na wajaaliwa kuzipata fadhila zake adhimu.
Links
[1] https://www.alhidaaya.com/sw/taxonomy/term/257
[2] http://www.alhidaaya.com
[3] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F6857&title=Tawbah%3A%20Hukmu%20Na%20Fadhila%20Zake%20%20
[4] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F6886&title=01-Tawbah%20Hukmu%20Na%20Fadhila%20Zake%3A%20Maana%20Ya%20Tawbah%20%20
[5] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F6887&title=02-Tawbah%20Hukmu%20Na%20Fadhila%20Zake%3A%20Vipi%20Kuomba%20Maghfirah%20Na%20Tawbah%3F
[6] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F6888&title=03-Tawbah%20Hukmu%20Na%20Fadhila%20Zake%3A%20Tawbah%20Ya%20Naswuwhaa%20%28Ya%20Kwelikweli%29%20Na%20Masharti%20Yake
[7] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F6889&title=04-Tawbah%20Hukmu%20Na%20Fadhila%20Zake%3A%20Nyakati%20Bora%20Za%20Kuomba%20Tawbah
[8] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F6890&title=05-Tawbah%20Hukmu%20Na%20Fadhila%20Zake%3A%20Hatari%20Ya%20Kuchelewa%20Kuomba%20Maghfirah%20Na%20Tawbah
[9] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F6891&title=06-Tawbah%20Hukmu%20Na%20Fadhila%20Zake%3A%20Allaah%20Anampenda%20Mja%20Anayeomba%20Tawbah
[10] https://www.addtoany.com/share#url=https%3A%2F%2Fwww.alhidaaya.com%2Fsw%2Fnode%2F6892&title=07-Tawbah%20Hukmu%20Na%20Fadhila%20Zake%3A%20Fadhila%20Za%20Kuomba%20Tawbah